Sheikh ametoa onyo kwa Waislam kuhusu maandamano ya Desemba 25, akisisitiza kuwa jamii inapaswa kutazama matokeo ya mwisho ya hatua yoyote badala ya kushawishika na mipango au kauli zinazotolewa mitandaoni.
Akizungumza katika somo la siku, shekhe huyo amesema kuwa baada ya maandamano ya tarehe 9 kufeli, kumekuwa na hasira kubwa, hususan kutoka kwa watu walioko nje ya nchi.
“Tukio la tarehe 25 Desemba ambalo sasa hivi, ukiingia kwenye mitandao, watu wanalipanga; bado sisi kama Waislam tunatazama mwisho wa jambo. Sisi kama Waislam tunatazama mwisho wa jambo hili utakuaje, si kwa sababu ya mtu fulani amesema.”
“Baada ya kufeli lile la tarehe 9, watu wengi sana wamekasirika, na hasa wale walioko nje ya nchi — wale maadui wetu wa nje. Inaonekana walikuwa na mipango yao, na ile mipango baada ya kufeli, ndiyo mwisho wa siku wanasema Waislam wamefelisha maandamano.”
Sheikh huyo alihoji nia halisi ya waliokuwa wanapanga maandamano hayo, akisema: “Lengo lao lilikuwa Waislam waingie barabarani wakafe? Au wangeharibu nchi? Au wangechafua amani? Au wangechoma miundombinu?”
“Lengo lao lilikuwa ni nini mpaka waseme Waislam wamefelisha? Kwani nchi hii ni ya Waislam pekee yake? Si wapo na dini nyingine?”