Kikwete kushinda kwa kishindo 2010
Gloria Tesha
Daily News; Thursday, January 08, 2009 @21:15
Mtabiri maarufu nchini, Shehe Yahya Hussein, amemtabiria ushindi wa kishindo Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu mwakani na kwamba Serikali yake itakuwa ya Muungano wa Vyama vya Siasa.
Shehe Yahya amesema pia kuwa ushindi wa Kikwete utatokana na mwendelezo wake wa kufichua mafisadi na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila woga na kwamba katika uchaguzi huo, hakutakuwa na wizi wa kura, bali watu watashughulikia kutafuta fedha na mtandao wa mafuta.
Mtabiri huyo alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa ya utabiri wake kwa mwaka huu kwa waandishi wa habari. Kuhusu ushindi wa Kikwete na hali ya kisiasa kuelekea mwaka wa uchaguzi, alisema utabiri wa mwaka huu uliopewa baraka zote na Umoja wa Mataifa, kuwa mwaka wa kuongozwa na nyota duniani, unaonyesha kuwa kiongozi mwenye jina lenye herufi J na K nchini, ndiye anayeongoza nchi.
Pamoja na kuwa na herufi hizo, pia mwenye bahati kuwa katika uongozi wa awamu ya pili, ya tatu na sasa ya nne, awe mwenye kichwa cha bapa, uso wa meza na rangi ya maji ya kunde
mwenye nyota hiyo ni Kikwete na hivyo namtabiria kuendelea kuongoza nchi 2010, alisema Shehe Yahya.
Alisema pamoja na kuwa na nyota hiyo inayoonyesha ushindi, endapo ataacha kuwatetea wanyonge kwa kupingana na baadhi ya matakwa ya watu wa chama chake, atashindwa vibaya katika uchaguzi na akakionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kiburi na kutambua kuwa hakitaongoza nchi peke yake mwaka huo.
Akifafanua kuhusu Serikali ya Muungano wa Vyama, alisema dalili zilizopo zinaonyesha Serikali ya Mseto na kuzitaja dalili hizo kuwa ni kampeni za kinyanganyiro cha ubunge Mbeya Vijijini, ambako vyama vya upinzani vinaangushana na kuiunga mkono CCM.
Hata hivyo, alisisitiza hakutakuwa na wizi wa kura katika uchaguzi ujao na badala yake itaundwa Serikali ya Mseto na kwamba viongozi wakiwamo wabunge walioko madarakani watakaoendelea kufanya ufisadi na kutotenda haki kwa wanyonge, watashindwa vibaya katika uchaguzi huo.
Mwaka huu vifo vya watu mashuhuri vitaongezeka sana na kutakuwa na kukwama kwa viongozi wapenda rushwa na wale watakaosema ukweli bungeni bila kuficha kitu, watachanua katika uongozi na maisha kifedha, alisema.
Shehe huyo alimzungumzia pia Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, kuwa atajiunga na siasa mwakani na pia mgogoro wake na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, hauwezi kuendelea kwa kuwa herufi za majina yao ya pili ni M zikifuatiwa na herufi E na A ambazo kinajimu ni ndugu wa baba mmoja. Pia mnajimu huyo alimtabiria Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa kati ya sasa na Aprili mwaka huu, atapata kazi kubwa duniani ambayo itaiacha Dunia ikishangaa, hasa Watanzania.