Katika miaka ya hivi karibuni Marekani imekuwa ikitekeleza kile inachokiita kurudi Afrika, sera ambayo hapo awali ilitajwa kuwa ni kurekebisha makosa ya kisera na kutambua umuhimu wa kimkakati wa bara la Afrika, sio tu kwa siasa za ndani za Marekani, bali pia kwa uchumi wa Marekani na nafasi yake kwenye siasa za kijiografia duniani. Wakati Marekani imeendelea na jaribio la kutekeleza azma hiyo kwa kusuasua, kuna kila dalili kuwa ni jaribio halina mwelekeo.
Kelele ambazo zimekuwa zinapigwa na baadhi ya nchi za magharibi kukosoa uwepo wa China barani Afrika kwa visingizio mbalimbali, zimejibiwa vizuri mara kwa mara na wanasiasa na wanasera wa nchi za Afrika, kwamba bara la Afrika ni kubwa na lina nafasi kwa kila mwenye nia njema ya kufanya ushirikiano. Hata hivyo nchi za magharibi, hasa Marekani, ambazo ndio walalamikaji wakubwa wa uwepo wa China barani Afrika, bado zinaonekana kuendelea kukosoa zaidi kuliko kuingia wenyewe barani Afrika.
Uwepo wa China barani Afrika unaozungumziwa hapa, ni ule wa kuwa tayari kufanya uwekezaji wa moja kwa moja, kutoa soko la bidhaa kwa nchi za Afrika, kutoa misaada na mikopo na hata kutekeleza kandarasi za ujenzi, iwe ni miundombinu ya usafiri, au majengo ya makazi, biashara na ya huduma za kijamii kama vile shule, hospitali, viwanja vya michezo au hata ofisi za serikali. Marekani inaona kuwa mambo hayo yanayofanywa na China ndio yanafanywa China ipendwe. Ni kweli.
Msingi wa ushirikiano wa China na nchi za Afrika ni kuwa kila nchi ina nafasi yake kwa China bila kujali iwe ni nchi kubwa, au ndogo. Nchi nyingi za magharibi zina mawasiliano ya karibu kiuchumi na nchi chache sana za Afrika, na muundo wake wa ushirikiano ni ule mwenye mwelekeo wa vyombo vya fedha vya kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha duniani IMF. Muundo huo umeonesha dosari kubwa kwa kuwa umekaa kimtindo wa kuzinyonya, na sio kuziendeleza nchi za Afrika.
Mwaka jana, tumesikia mara nyingi kuwa Marekani inafanya juhudi kubwa kuwekeza kwenye ujenzi wa reli ya ushoroba wa Lobito ya Angola, ikiwa ni hatua yake ya kurudi Afrika, na kukabiliana na uwepo wa China barani Afrika. Imetajwa kabisa kuwa lengo la Marekani katika ujenzi huo, sio kulenga kuwasaidia watu wa Angola, lakini ni kufika kwenye chanzo cha madini muhimu katika kipindi hiki, hasa yale yanayotumika kwenye utengenezaji wa betri za magari.
Pamoja na ukweli kwamba nia ya Marekani haina tofauti na nia ya nchi yoyote kwenye kutafuta nafasi yake kwenye ushindani, ni wazi kuwa njia hiyo haiwezi kuifanya Angola au watu wa Angola waiweke Marekani moyoni.
Tukiangalia jinsi China inavyoendesha ushirikiano wake na nchi za Afrika, tunaweza kuona tofauti kubwa na Marekani. Licha ya kuwa ipo kwenye ushindani na nchi nyingine kwenye sekta ya madini, lakini tunaona pia kuwa China inajitokeza sana kwenye sekta nyingi zinazohusu maslahi ya kijamii na maendeleo ya watu wa nchi za Afrika. Miradi mingine inayoonekana, kimsingi ni miradi ya hisani ya China, wala haina msalahi ya kiuchumi (kama vile shule, hospitali, majengo ya bunge, viwanja vya michezo), na ni miradi kama hiyo inayofanya watu waone kuwa China iko mioyoni mwao.
Miradi mikubwa kama mradi wa reli ya Lobito, bila shaka ni mradi unaokaribishwa, lakini mradi kama huo peke yake au hata miradi kama hiyo miwili haiwezi kubadilisha ghafla sura ya Marekani na kuonekana kuwa nchi inayopendwa na watu wa Afrika. Marekani bado ina safari ndefu kufika hatua hiyo.