Hii nadharia inayozungumzwa ya Ruto na Uhuru kutengeneza "uadui" kati yao ili wamzime Raila, binafsi naiona ngumu kutekelezeka japo kweli inawezekana ilitokea.
Nakumbuka kuna wakati Ruto alimuomba samahani Uhuru kwa hicho kinachoitwa ugomvi wao, japo Uhuru alionekana kupuuza hakuwa msikivu sana kwa Ruto wala kumjibu chochote cha maana.
Binafsi nikitaka kuuzungumzia huu uchaguzi wa Kenya, zaidi nitaangalia mambo matatu; Uchaguzi ulivyofanyika, Ushindi wa Ruto, na malalamiko ya Raila.
- Uchaguzi wa Kenya, huu ulionekana kufanyika kwa uhuru na uwazi mpaka kura zilipomaliza kupigwa, hapakuwa na mawakala kusumbuliwa vituoni, karatasi za kupigia kura kuchelewa kufika vituoni, vituo kuchelewa kufunguliwa n.k kama ambavyo tumezoea kwenye chaguzi zetu Tanzania.
Hapo nawapa wakenya na tume yao 95% nikiamini kwamba kama palikuwepo na irregularities, basi zilikuwa kwa kiwango kidogo ambacho hakiwezi kuharibu taswira nzima ya uchaguzi wao mkuu waliofanya.
- Ushindi wa Ruto; binafsi nikiri, mwanzo sikutegemea kabisa kuona Ruto akiibuka na kutoa ushindani mkali kiasi kile, na mwishowe akatangazwa mshindi.
Kilichokuja kunifanya nijue wapi Ruto alipata nguvu zake nikajua ni kwenye kampeni zake, hapa naungana na mwandishi Ngurumo alipozungumzia maeneo kama kuwashawishi na kuaminiwa na vijana hasa kuhusu ukosefu wa ajira, hawa walijitokeza kwa wingi kupiga kura.
Tukaona picha wengine wakiwa na taulo viunoni, wengine miswaki mdomoni kuonesha vile walivyojitoa kumpigia kura waliyemuamini, pia chimbuko la Ruto ametokea tabaka la chini [hustler] ni sababu nyingine ya kuaminiwa na kuchaguliwa kwake, na hicho kinachoitwa ugomvi wake na Uhuru [sijui kama ni wa kweli, au uongo].
Hapo kwa tathmini yangu naamini Ruto ameshinda kihalali, alikuwa na hoja nzito alizofanikiwa kuwashawishi wapiga kura wakamchagua.
- Malalamiko ya Raila, hapa nimekuja kugundua kumbe wale makamishna wanne kati ya saba waliogoma kukubali matokeo ya ushindi wa Ruto waliteuliwa na Uhuru, hivyo kwa akili za kawaida watu wanaona kwamba inawezekana hii ndio sababu yao kumkataa Ruto wakimtaka "mgombea wao" nikimaanisha aliyewekwa na mtu wao ndie ashinde.
Lakini tatizo linakuja kwamba, kama tukienda na mentality hiyo ya kusema hao walioteuliwa na Uhuru walimtaka Raila ashinde, basi nami naweza kusema pia, inawezekana na huyo Chebukati ambaye hakuteuliwa na Uhuru, akawa kipenzi cha Ruto ndio maana akampa ushindi.
Hivyo kama picha itaenda kwa mtindo huo, basi naona madai ya Raila na hao makamishna wanne kuamini kwamba matokeo yaliyotangazwa na IEBC yalikuwa na tatizo, ni VALID, kwasababu inaonekana hiyo tume ilikuwa na pande mbili zenye wagombea wao tofauti, hapa tume kwa mtazamo wangu inapoteza uhalali wake.
Kwa hali hiyo, inavyoonekana kwa nje, hakuna wa kumuamini kati ya Chebukati na makamishna wake watatu wa IEBC, au Makamu wake na makamishna wake wanne, naona tuiachie Supreme Court yao ije kutupa majibu ya mwisho, mpaka hapa Urais wa Ruto ni 50% anything can happen mahakamani.