SIKU MOJA NA SHEIKH PONDA MAHAKAMANI MOROGORO
Miaka saba iliyopita siku kama ya leo.
Siku nyingi zilikuwa zimepita sijamuona Sheikh Ponda si kwa kuwa alikuwa kifungoni mahabusi bali nilikuwa nje ya Dar es Salaam kwa muda mrefu.
Nikaamua kwenda kumuona mahakamani Morogoro kesi yake ilipokuwa inasikilizwa.
Nikapanda basi la kwanza ili niwahi mahakamani Morogoro.
Kufikia mahakamani nikakuta ulinzi mkali kupita kawaida na kisa ni kuwa kabla sijafika Waislam walikuwa wametiana misukosuko na polisi nje ya jengo la mahakama.
Kwa ajili hii polisi wakawa wamewazuia Waislam kuingia mahakamani.
Baadhi ya watu wanaonifahamu kuniona nimefika pale wakanifuata kunisalimia na kunifahamisha yaliyotokea pale punde wakisikitika kuwa nimekuja kutoka mbali lakini sitaweza kusalimiana na Sheikh Ponda.
Hata hivyo wakanishauri kwenda pale getini nizungumze na askari huenda akaniruhusu kuingia mahakamani kusikiliza kesi na kupata nafasi ya kuonana na Sheikh Ponda.
Baada ya kunisaili yule askari akaniruhusu kupita akiniambia kuwa amefanya staha ya umri wangu na kuwa ni ndugu yake sheikh na nimekuja kutoka mbali.
Mahakamani nilimkuta Mzee Bilal Rehani Waikela katoka Tabora kaja Morogoro kusikiliza kesi ya Sheikh Ponda.
Ilikuwa hapo Morogoro miaka mitatun iliyopita asubuhi najitayarisha kwenda studio za Radio Imaan kufanya kipindi ndipo niliposikia katika taarifa ya habari kuwa Sheikh Ponda amekwenda kwenye kiwanja cha iliyokuwa EAMWS kiwanja palipokusudiwa kujengwa Chuo Kikuu Cha Waislam mwaka wa 1968 na amechukua sehemu ndogo kurejesha kwa Waislam na patajengwa msikiti utakaoitwa Masjid Sheikh Hassan bin Ameir.
Yaliyomfika Sheikh Ponda yanafahamika.
Kumuona Mzee Waikela ndani ya mahakama na Sheikh Ponda kasimama kizimbani machozi yalinilengalenga.
Machozi yalinitoka kwa kuwa nilikuwa naijua nafasi ya Mzee Waikela na Sheikh Hassan bin Ameir katika historia ya Tanganyika.
Miaka mingi imepita toka watu hawa walipokuwa pamoja kama viongozi wa Waislam katika EAMWS.
Lakini niliingiwa na simanzi na kumuonea wivu Sheikh Ponda kuwa leo jina lake linatajwa pamoja na jina la Sheikh Hassan bin Ameir na mwanafunzi wa Sheikh Hassan bin Ameir, Mzee Waikela yuko mahakamani kusikiliza kesi yake.
Sheikh Ponda aliposhinda kesi zote alinialika kwenye shule ambayo yeye ni kiongozi, Ilala Islamic nimzungumze na vijana kuhusu mchango wa Sheikh Hassan bin Ameir katika elimu na kupigania uhuru wa Tanganyika.
Sheikh Ponda ana historia kubwa sana
Naamini iko siku In Shaa Allah atanyanyua kalamu kuiandika.
View attachment 2069458
Kulia ni Wakili Msomi Juma Nassor na Sheikh Ponda Mahakamani Morogoro
View attachment 2069462
Kushoto wa kwanza ni Mzee Bilal Rehani Waikela akiwa mahakamani Morogoro