Siku yangu na Alquam Kiobya mjukuu wa Saadan Abdu Kandoro

Siku yangu na Alquam Kiobya mjukuu wa Saadan Abdu Kandoro

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
SIKU YANGU NA ALQUAM KIOBYA MJUKUU WA SAADAN ABDU KANDORO

Alquam Kiobya ni kijana mdogo kama mnavyomuona.

Huyu ni mjukuu wa Saadan Abdu Kandoro mmoja kati ya wazalendo 17 waliounda chama cha TANU mwaka wa 1954.

Katika timu ya waasisi hawa alikuwapo kwa kuwataja wachache babu yake Alquam Saadan Abdu Kandoro, Abdul Sykes na nduguye Ally Sykes, John Rupia, Dossa Aziz, Germano Pacha na Julius Nyerere.

TANU ndicho chama kilichopigania uhuru wa Tanganyika hadi ukapatikana mwaka wa 1961.

Alquam ameletwa nyumbani kwangu na mtoto wa mmoja katika waasisi wa TANU ambao baba yake alikuwa rafiki kipenzi wa Julius Nyerere wakati wa kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.

Bahati mbaya sana Alquam hakumfaidi babu yake kwa kuwa alikuwa mdogo na hakupata kusoma kitabu alichoandika babu yake, ‘’Wito wa Uhuru,’’ kilichochapwa mwaka wa 1961 kabla ya Tanganyika kupata uhuru wake.

Alquam aliponifahamisha kuwa hajapata kukiona kitabu hicho cha babu yake nilinyanyuka hadi Maktaba nikamtolea nakala kumuonyesha.

Uso wake ulijaa tabasamu alipokuwa akikifungua kitabu na kuangalia picha ndani ya kitabu ya babu yake akiwa kijana sana wastani wa umri wa miaka 30.

Kama alivyokuwa babu yake bingwa wa lugha ya Kiswahili na mtunzi mahiri wa mashairi, mjukuu Alquam Mashaallah ana ulimi mkali wa lugha ya Kiingereza kiasi utapenda kumsikiliza akikimwaga kimombo.

Tulizungumza kiasi nikajaribu kumueleza kwa muhtasari ninavyomfahamu babu yake kwa kumsoma na kumuona.

Naamini alishangaa nilipomwambia kuwa babu yake na viongozi wenzake wa TAA Western Province, Tabora walitaka kuunda TANU mapema kabisa mwanzoni mwa miaka ya 1950.

Nikamfahamisha kuwa mara ya mwisho mimi kumuona babu yake ilikuwa Salender Bridge tumepishana sote tuko dani ya gari katika mwendo wa taratibu kiasi cha mimi kuweza kumwangalia vizuri Mzee Kandoro.

Aikuwa kavaa kanzu nyeupe na kofia nyeupe pia; na lile umbo lake kubwa la Kimanyema hakuwanalo katika utu uzima.

Siku zake za mwisho Mzee Kandoro alikua na umbo jembamba kama la kijana kumfanya zile nguo alizovaa zimkae vyema.

Alquam amenitia hamu ya kufanya rejea katika kitabu cha Abdul Sykes kumsoma Saadan Abdu Kandoro na nakuwekeeni hapo chini vipande nilivomtaja mpigania uhuru huyu ambae si wengi wanaijua historia yake au hata kama alikuwa Mtanganyika wa kwanza kuandika historia ya TANU:

''Katika majimbo ya ziwa katika miaka ya 1950 tawi la TAA lililokuwa na nguvu lilikuwa tawi la Mwanza.

Viongozi wake, Saadan Abdu Kandoro, Mmanyema na mtunga mashairi, na Bhoke Munanka walikuwa wakitupiwa macho na serikali.

Kandoro na Munanka walikuwa wakijaribu kumuunga mkono Ali Migeyo ambaye peke yake alikuwa akijaribu kufungua matawi ya TAA sehemu za Bukoba.

Pale Bukoba mwanasiasa mkongwe Migeyo, akiwa na umri wa miaka hamsini na tatu alikuwa akihangaika kufungua matawi katika jimbo la Ziwa Magharibi.

Akiwa Kamachumu katika kampeni hii, Migeyo alishambuliwa na mabomu ya kutoa machozi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.

Migeyo alikuwa na kipawa cha kuzungumza na hotuba zake zilikuwa za kusisimua kiasi kwamba ilikuwa rahisi sana kwake kuwapandisha watu ghadhabu.

Siku ile ya mkasa wa mabomu alikuwa akiwaandaa wananchi kuipokea TANU.
Alipokuwa akihutubu askari walikuja kuwatawanya watu kutoka kwa viwanja vya mkutano.

Mabomu ya machozi yalitupwa na Migeyo akatiwa mbaroni.

Wakoloni kwa ujanja wakamshtaki Migeyo peke yake bila ya kumuunganisha na TAA, chama alichokuwa akikitumikia."

Naendelea na historia ya Saadan Abdu Kandoro na juhudi zake kukabiliana na Mgogoro wa Ardhi ya Wamweru:

''Tawi la chama cha TAA la Tabora lilichukua changamoto hiyo kwa kupitia juhudi za Kandoro aliyeuona mgogoro wa ardhi ya Wameru kama jukumu lake binafsi.

Kandoro aliitisha mkutano wa matawi ya TAA ya Mwanza, Kigoma na Tabora kujadili suala hilo. Mwanza iliwakilishwa na Bhoke Munanka, Mzee Mkama Mlaji na Mohamed Kihaka Kitenge; kutoka Kigoma mjumbe aliyekuja alikuwa Jumanne Mawimbi na Tabora iliwakilishwa na Sheikh Kinana, Kandoro na George Magembe kama rais wa TAA tawi la Tabora.

Mkutano wa Tabora uliahidi mshikamano wa pamoja na watu wa Meru katika mapambano dhidi ya walowezi.''

''Uongozi wa TAA Makao Makuu ulianza kampeni ya nchi nzima kuueleza umma matokeo ya safari ya Kirilo kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa ardhi ya Wameru na vilevile kuchangisha fedha za kupeleka msafara mwingine katika Umoja wa Mataifa kuueleza umoja huo kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya udhamini na Watanganyika walikuwa sasa na haki ya kudai uhuru wao.

Kamati ya TAA ya watu watatu iliyowajumuisha Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes iliundwa kwa ajili hiyo.

Ally Sykes akiwa mweka hazina msaidizi wa TAA aliombwa ampelekee Kirilo hawala ya posta Usa River kama nauli ya kumwezesha kusafiri hadi Dodoma kujiunga na ile kamati ya Abdu Kandoro.

Kulikuwa hakuna huduma ya fedha katika posta ya Usa River na fedha zile zilikaa hapo kwa muda bila ya kuchukuliwa hadi hapo zilipopelekwa posta ya Arusha mjini ambako Kirilo alizichukua.

Kuanzia tarehe 26 Septemba, 1953 kwa takriban mwezi mmoja ile kamati ilitembelea na kuhutubia mikutano ya hadhara, ikikusanya fedha Dodoma, Mwanza, Bukoba, Ukerewe, Tarime, Musoma na Shinyanga.

Rais wa chama cha TAA, kanda ya ziwa, Paul Bomani aliipokea ile kamati ya watu watatu na kuhutubia mikutano pamoja nao katika jimbo lote.''

''... kiongozi mashuhuri kutoka Jimbo la Ziwa, Abdu Kandoro, Chifu Patrick Kunambi kutoka Morogoro, Jimbo la Mashariki, Japhet Kirilo, Joseph Kimalando, John Rupia na Julius Nyerere, walikutana katika Government House kujadili ile sekula ya serikali na Gavana Edward Twining.''

(Hii ilikuwa Government Secular No. 5 ya 1953 iliyowakataza wafanyakazi wa serikali Waafrika kujihusisha na siasa).

''TANU ilihitaji takriban shilingi elfu kumi na mbili kumwezesha Nyerere kusafiri kwenda Umoja wa Mataifa, New York.

''Kamati ya Abdu Kandoro, Japhet Kirilo na Abbas Sykes ilikuwa imekusanya kiasi cha fedha kutoka majimboni ambacho kilitumika katika ile safari ya Ally na Phombeah kwenda kwenye Pan African Congress mjini Lusaka.

Kilichosalia hakikutosha kumpeleka Rais wa TANU, Nyerere Amerika. Ilibidi fedha za ziada zitafutwe kutoka kwa wananchi ili kumwezesha Nyerere kufanya safari hiyo.

John Rupia alichangia zaidi ya theluthi moja ya fedha zilizotakikana.

Wanachama wengine walichangia kwa uwezo wao wote lakini TANU katika siku zile ikiwa bado changa ilikuwa maskini, kiasi hicho kilikuwa bado kiko nje ya uwezo wake.

Ikitambua ule upungufu wa fedha za safari ya Nyerere, Idd Faiz aliombwa na uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya kutoa fedha katika mfuko wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganika) na kuzitia katika hazina ya TANU kukiwezesha chama kumpeleka Nyerere UNO, New York.''

Bado nipo na Saadan Abdu kandoro:

''Miaka mitano ilikuwa imeshapita tangu kuasisiwa kwa TANU.

Nyerere alikuwa amekwenda Umoja wa Mataifa mara tatu na alikuwa ametembelea takriban sehemu zote za Tanganyika isipokuwa Mpanda na Sumbawanga.

Makao makuu ya TANU iliona kuwa wakati ulikuwa umewadia kwa Nyerere kuzitembelea sehemu hizo na kukutana na wananchi kabla TANU haijapata serikali ya ndani.

Machi, 1959 TANU Youth League Tabora iliombwa na makao makuu ya TANU kupanga safari ya Nyerere na kushughulikia mambo ya usalama wa rais wa TANU atakapokuwa katika ziara ya sehemu hizo.

Saadan Abdu Kandoro, Katibu wa TANU Tabora na Rajabu Tambwe, Mwenyekiti waliwataka Kassongo na kikundi chake kuchukuwa dhima ya mipango ya usalama wa Nyerere.''

Picha: Alquam akiangalia kitabu alichoandika babu yake, "Mwito wa Uhuru," na picha ya pili akiangalia kitabu cha Abdul Sykes.

Picha ya mwisho ni Saadan Abdu Kandoro wakati wa ujana wake.

ALQUAM KIOBYA.jpg


1624681291882.png


1624681381600.png


1624681448613.png
 
Aisee, alfu kumi na mbili ilitosha kumpeleka Nyerere US mwaka 1953

Ahsante kwa uzi mujarab kabisa Shekh na mzee wetu Mohamed (japo kuna wakati katika kusoma nilikua napotea maana umegusia mambo tofauti tofauti)
 
Back
Top Bottom