Simba kusaka tiketi ya Brazil leo
Send to a friend Wednesday, 19 January 2011 21:27
Clara Alphonce
SIMBA inashuka dimbani leo kucheza mchezo wa kirafiki na Atletico Paranaense ya Brazil, mchezio utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa huku ikimjaribu mchezaji wake raia wa Cameroon, Eke Cosmas.
Mchezaji huyo ambaye ni kiungo amekuja katika klabu hiyo kwa ajili ya kujaribiwa na katika mechi ya leo atakuwa ni mmoja wa wachezaji wanaotaraji kuongoza Simba kwenye mchezo huo.
Afisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema jana kuwa mchezaji huyo yuko katika majaribio kwani alitua nchini wiki iliyopita na endapo atafaulu majaribio hayo watabaki naye mpaka kwenye usajili wa msimu ujao.
Endapo Cosmas atafuzu majaribio yake, atawaweka mashakani wachezaji viungo wawili wa kimataifa ambao ni Hilal Echessa, Jerry Santo pamoja na mkongwe, Mohamed Banka.
Simba inaingia dimbani leo ikiwa na mawazo ya kwenda Brazil kwa ajili ya kuweka kambi baada ya Mkurungezi wa timu ya African Lyon, Rahma Kharoos ambaye ndio aliyeileta timu hiyo kutoka Brazil kuiahidi Simba kuipeleka nchini humo lakini endapo tu, itashinda mchezo wa leo.
Hata hivyo, mechi ya leo itakuwa na hamasa kubwa baada ya mkurugenzi huyo kuruhusu mashabiki kuingie bure baada ya kuona viti vikiwa tupu katika mchezo dhidi ya Yanga juzi kutokana viingilio walivyoweka kuwa vikubwa.
Meneja wa Simba, Innocent Njovu alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na mpaka sasa wachezaji majeruhi katika timu ya Simba ni Uhuru Seleman na Emmanuel Okwi.
Alisema huenda kocha wao Patrick Phiri akawatumia wachezaji waliokuwepo katika timu ya taifa nchini Misri waliojiunga na wenzao jana au asiwatumie na kuwachezesha wale waliokuwepo.
Katika hatua nyingine, klabu ya Yanga imelalamikia maamuzi ya mratibu wa ziara ya Wabrazil hao, Rahma kuwa haikuwatendea haki kwa kuruhusu mashabiki kuingia bure kwenye mechi ya Simba wakati wao walicheza viti vikiwa wazi.
Yanga ilipambana na Wabrazil hao na kufungwa mabao 3-2 kwenye uwanja huo, katika mechi iliyokuwa na mashabiki kiduchu kabla ya mratibu huyo kutoa ofa kwa Simba kwa mashabiki wake kuingia bure na endapo itashinda, Simba itakwenda Brazil.
source:mwananchi