Simba, Mazembe waongoza vitani Afrika
Send to a friend Thursday, 31 March 2011 21:11 0diggsdigg
Clara Alphonce na mashiriki ya habari
BAADA ya mchaka mchaka wa mwishoni mwa wiki wa kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012, macho ya mashabiki wiki hii yanaelekea kwenye mechi kumi na sita za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Mabingwa watetezi TP Mazembe watakuwa makini kuepuka matokeo ya kushangaza jijini Dar es Salaam watakapoikabili Simba SC. Bao la penati la mshambuliaji Emmanuel Okwi liliipa matumaini timu hiyo ya Tanzania iliyolala mabao 3-1, kuweza kupata nafasi ya kutengeneza rekodi ya kuwaondoa mabingwa hao watetezi.
Hata hivyo, Mazembe wanajivunia timu yao bora iliyojaa nyota wengi wenye vipaji kama Kabangu, Kaluyituka Dioko, Singuluma na kipa bora Kidiaba. Lakini wapinzani wao bado wana nafasi ya kusonga mbele, ingawa TP Mazembe pia wanaonekana watashinda mchezo huo.
Mwanzoni mwa wiki hii uongozi wa TP Mazembe waliwatumia taarifa Simba kuwa watawasili nchini Ijumaa kwa ajili ya mchezo huu, lakini mpaka jana mchana walikuwa hawajatuma taarifa ni saa ngapi watawasiri nchini.
Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alisema kuwa mpaka jana wao kama Simba hawajatumiwa taarifa yoyote kutoka kwa wapinzani pamoja na kuwa wameshawaandalia sehemu ya kufikia.
Alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na watawasubiri wageni wao na tiketi za mchezo huu tayari zimeanza kuuzwa katika vituo mbali mbali.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alipoulizwa kama kuna taarifa yoyote walitumiwa na Shirikisho la Soka la Congo juu ya ujio wa mabingwa hao.
''Bado hawajanitumia taarifa yoyote ila mimi nimewatumia barua pepe kwa shirikisho lao ya kuwauliza timu hiyo itakuja lini, lakini hawajanijibu kama watatoa taarifa mapema tutawajulisha,'' alisema Wambura.
Michezo mingine wiki hii ni Esperance na Zesco United watakuwa ugenini huko Cotonou na Mbabane zote zikiwa mbele kwa mabao matano, El Hilal na Diaraf ya Dakar wapo kwenye mazingira hayo pia baada ya kupata ushindi mabao 3-0 dhidi ya Recreativo Caala na Djoliba.
Timu nyingine inayopewa nafasi kubwa ya kusonga mbele ni Dynamos ya Harare iliyojiweka kwenye mazingira hayo baada ya kuichakaza Mouloudia ya Algiers 4-1.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa klabu hiyo ya Algeria kuruka kihunzi hicho, wanatakiwa kufunga mabao si chini ya matatu na kutoruhusu bao. Cotonsport ya Garoua pia ipo kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya ushindi wake wa bao 1-0 ugenini dhidi ya AS Vita Club.
Mabingwa wa zamani klabu mbili kongwe za Misri, Al Ahly na Zamalek watakuwa kwenye kibarua kizito wiki hii, Al Ahly watakuwa wageni wa SuperSport United kwenye Uwanja wa Mokaba mjini Polokwane, ambapo ni moja ya viwanja vilivyotumika kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2010.
Zamalek miamba mingine ya Misri itaikaribisha Club Africain ya Tunisia iliyoshinda kwa mabao 4-2. Timu zote zinakutana zikiwa hazipo kwenye kiwango kizuri baada ya kusimamishwa kwa ligi zao kufutia vurugu za kisiasa zilizotokea katika nchi zao hivi karibuni.
Raja Casablanca watakuwa wenyeji wa Stade Malien huku wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-1 walichokipata jijini Bamako. Vigogo wengine wa Morocco, WAC wakiwa mbele kwa mabao 2-0 kabla ya safari yao ya Nigeria kuivaa Kano Pillars, Matokeo hayo yanawapa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye mchezo huo wa ugenini.