Phiri apanga kutumia chipukizi kesho
Send to a friend Friday, 15 October 2010 08:20 0diggsdigg
Patrick Phiri
Jackson Odoyo, Mwanza
KOCHA wa Simba, Partick Phiri amesema kuongezeka kwa majeruhi kwenye kikosi chake amepanga kuwatumia chipukizi wengi zaidi kwenye mchezo wake wa kesho dhidi ya Yanga.
Akizungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya mazoezi jana asubuhi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Phiri alisema wachezaji wake wengi nyota ni majeruhi na wengi wamebaki Dar es Salaam.
"Wachezaji wengi wakongwe ni majeruhi, lakini hii itakuwa nafasi pekee kwangu kuanza kuwatumia chipukizi wangu ambao naamini wana uwezo wa kutosha kuziba mapengo yote.
Majeruhi wa timu hiyo ni pamoja na Nico Nyagawa, Uhuru Selemani, Salum Kanoni waliobaki Dar es Salaam kuendelea na matibabu.
Kiungo Mohamed Banka aliyecheza kwa dakika 15, kwenye kikosi cha taifa Taifa Stars dhidi ya Morocco na kuonyesha kiwango cha juu uwezo anasumbuliwa na tumbo. "Tutamwangali hadi kesho (leo) kuona anaendelea vipi," alisema Phiri.
Naye Mussa Hassan Mgosi aliyejiengua kwenye kikosi cha Stars kwa matatizo ya mguu bado ni majeruhi, lakini anaweza kucheza Jumamosi, japokuwa alishindwa kufanya mazoezi na wenzake asubuhi.
"Sina shaka na hali hiyo kwa kuwa nina vijana wengi wenye uwezo mkubwa wa kuziba mapengo hayo kama Rashid Gumbo, Haruna Shamte, Humuod na Shija Mkina wote wapo kwenye kiwango cha juu kwa sasa."
Katika mazoezi hayo Phiri alimtumia zaidi Gumbo kucheza winga ya kulia na kupiga faulo nyingi alipoulizwa kwanini ameamua kumtumia kiungo huyo wa zamani wa African Lyon alisema: "Gumbo ni mwepesi na mwenye uwezo mzuri wa kuchezesha timu kutoka pande zote anaweza kuziba pengo la Nyagawa.
Phiri alisema mechi itakuwa ngumu kwake kwa sababu ya kuwakosa wazoefu, lakini bado ana imani kubwa kwa chipukizi wake.
"Mchezaji yoyote akiaminiwa anaweza kufanya vizuri hivyo naamini kwamba vijana wangu hawataniangusha kwenye mchezo huo, sina hofu."
Katika hatua nyingine kocha huyo mwenye tabia ya upole na ucheshi wakati wote alisema ingawa timu yake itakuwa na mabadiliko makubwa ila ana amini kuwa bado itaonyesha ushindani mkubwa zaidi katika mechi hiyo.
Hata hivyo alipoulizwa kuhusu imani ya mashabiki wake juu ya mechi hiyo alisema "Nina imani kuwa mashabiki wa Simba wanahitaji ushindi na si wao tu bali hata mimi mwenyewe ninahitaji ushindi katika mechi hii," alisema Phiri na kuongeza:
"Na ninaingiza chipukizi wangu nikiwa na kumbukumbu ya kufungwa katika mechi ya ngao ya hisani hivyo niingependa kupoteza tena mechi ili kurudisha hata imani ya mashabiki."
Habari zilizopatikana mjini hapa zinasema kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wa ngazi za juu wa Yanga wameingia kimya kimya kwa mafungu na wengine wanatarajia kuwasili leo asubuhi tayari kwa mchezo huo.
Yanga wanaofanya safari yao kuwa siri, imepanga kuondoka leo asubuhi kwa ndege ya Prescision ikiwa kamili baada ya Nsa Job aliyekuwa anasumbuliwa na tumbo kupona.
Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani alisema mchezaji huyo amepona na anaweza kuchea lakini itategemea na maamuzi ya kocha.
Naye kocha wa timu hiyo, Kosta Papic aliyejihakikishia ushindi wa mabao 3-0, alisema anaipeleka Yanga Mwanza kuchukua pointi tatu muhimu.
Naye Sweetbert Lukonge anaripoti kuwa wakati homa ya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga ikizidi kushika kasi uongozi wa Chama cha Soka mkoani Mwanza, MZFA, umejipanga kuhakikisha mchezo huo unamalizika kwa amani na utilivu.
Mwenyekiti wa MZFA, Jackson Songora alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, ili kukabiliana unaganyifu kutoka kwa pande zote zinazohusika na mchezo huo.
Mwenyekiti wa MZFA, Jackson Songora alisema: "Mchezo wowote ule unaozikutanisha timu hizi mbili huwa na mambo mengi ambayo kama tusipokuwa makini yaweza kutokea matatizo na mvurugano mkubwa. Sisi kama wenyeji tumejipanga kuhakikisha mambo yote yanakwenda vizuri."
source :mwananchi