Simba yaibipu Yanga, yainywa Mtibwa 4-1
Send to a friend Sunday, 27 February 2011 21:23 0diggsdigg
Kocha wa timu ya Simba,Patrick Phiri
Clara Alphonce
MABAO matatu (hat-trick) ya Mbwana Samatta, yakiwamo mawili ya kipindi cha pili na jingine la Amri Kiemba yameipa Simba ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na kuirejesha kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 37.
Katika mchezo huo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Samatta ambaye alifungua milango kwa kupachika bao la dakika ya 13 ya kipindi cha kwanza baada ya krosi ya Kiemba alirejea tena nyavuni dakika ya 65 na 89 kwa mabao mawili zaidi yaliyokamilisha siku nzuri kwake.
Kiemba, ambaye alianzishwa katika mchezo huo aliiandikia timu yake bao la pili, dakika ya 46 ya mchezo huo uliokuwa wenye ushndani kutokana na kona ya Rashid Gumbo.
Nao Mtibwa waliandika bao la dakika ya 55 kupitia kwake Hussein Javu baada ya pasi ya Machaku ambaye aling'ara katika mchezo huo.
Mapema, katika mchezo huo Mtibwa ambao walimkosa kipa wao namba moja, Shaaban Kado anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mechi ya karibuni walipata pigo baada ya kipa wao, Omary Ally kuumia dakika ya nane ya mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Soud Slim.
Kipa huyo alikimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi baada ya hali yake kuwa mbaya.
Kwa sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, sehemu ya kiungo ya Simba ilipwaya na kuwapa nafasi Mtibwa kuchezea mpira, ingawa safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi iliwapa wakati mgumu mabeki wa wakata miwa hao wa Manungu.
Kama katika kipindi cha kwanza, Machaku Salum alikosa nafasi nzuri ya kuipa bao timu yake dakika ya 53 ya mchezo kwa kushindwa kumalizia pasi ya Issa Rashid.
Samatta angeweza kupata mabao matatu (hat-trick) yake mapema, lakini alikosa nafasi nzuri ya kufanya hivyo dakika ya 75 ya mchezo kwa kushindwa kutumia pasi nzuri ya Mussa Hassan Mgosi aliyekuwa ameingia uwanjani kuchukua nafasi ya Nico Nyagawa.
Mtibwa nao walikosa nafasi ya kupunguza idadi ya mabao baada ya mkongwe Yona Ndabila kushindwa kutumia pasi ya Issa Rashid, dakika ya 84 ya mchezo huo.
Kocha Tom Olaba wa Mtibwa alisema nafasi ya kipa ndiyo iliyomwangusha katika mchezo huo kiasi cha kuwapa urahisi washambuliaji wa Simba kupachika mabao kirahisi.
Naye Patrick Phiri wa Simba alimsifu Samatta kwa uchezaji mzuri licha ya umri wake mdogo na kueleza kuwa ushindi huo ni faraja kubwa kwao kabla ya mechi dhidi ya Yanga mwisho wa wik