Wajipa matumaini kwa Simba kuitoa TP Mazembe
Send to a friend Monday, 21 March 2011 20:24 0diggsdigg
Kocha wa Simba Patrick Phiri
Waandishi Wetu
BAO la mkwaju wa penalti lililofungwa na mshambuliaji Emmanuel Okwi limewapa matumaini wadau wa soka nchini kiasi cha kuanza kuamini Simba inaweza kuwafungasha virago mabingwa wa Afrika, TP Mazembe kwenye mchezo wa marudiano mwezi ujao.
Mabingwa hao wa Afrika walipata ushindi wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa mjini Lubumbashi DR Congo juzi.
Wakizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana wadau hao walieleza hisia na ushauri wao kwa Simba kama inataka kutimiza azma hiyo.
Beki wa zamani wa Yanga, Willy Martin 'Gari Kubwa' amemtaka kocha Patrick Phiri kuifanyia marekebisho safu yake ya ulinzi kabla ya mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo.
"Sababu kubwa iliyofanya Simba kufungwa mabao 3-1 kwenye mchezo huo ni safu yake ya ulinzi kujisahau na kutoa mwanya kwa wapinzani wao kupata mabao mawili ya haraka.
"Kukosa umakini na kuzubaa kwa safu ya ulinzi ya Simba ndiko kulikosababisha timu hiyo kufungwa mabao ya haraka," alisema Martin.
"Nafikiri kwa sasa inamlazimu mwalimu (Phiri) kuifanyia marekebisho safu hiyo kabla ya mchezo wa marudiano kwa siku hizi chache zilizosalia," aliongeza.
Mshambuliaji na nahodha msaidizi wa Simba, Mussa Hassan Mgosi aliwatoa hofu wapenzi wa soka nchini na kusema kuwa Mazembe ni timu rahisi tofauti na walivyowachukulia awali.
Alikiambia kituo kimoja cha redio jana kuwa uwezo wa kuwafunga mabao Mazembe mabao 2-0 kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili upo."Hatimaye tumewaona Mazembe ni wa kawaida sana tofauti na nilivyowachukulia mwanzo kabla ya kukuatana nao, uwezo wa kuwafunga hata mabao 2-0 tunao," alisema Mgosi.
"Mwanzoni ni sisi tulijichanganya kwenye ulinzi, lakini nawahakikishia Watanzania kwamba mchezo wa marudiano lazima waondoke na mabao si chini ya mawili," alisisitiza Mgosi ambaye alikuwa nahodha katika mchezo huo.
Naye Okwi aliyefunga bao hilo la kufutia machozi alisema kufungwa kwao kulitokana na wapinzani wao kuwazidi uzoefu pamoja na kutumia vyema nafasi walizopata.
Alisema wapinzani wao walitumia nafasi walizopata na kufunga mabao na ndio sababu walipata idadi hiyo ya magoli na kuongeza kuwa pia uzoefu wa kucheza miche zo mingi ya kimataifa imechangia ushindi huo.
Alisema kiujumla mchezo huo ulikuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa kufuatia wapinzani wao kuwa nyumbani, lakini akaongeza kuwa Mazembe ni timu ya kawaida na yenye kucheza mpira wa kawaida.
"Ukweli wenzetu walijipanga zaidi na walitumia nafasi ndogo walizopata katika kuhakikisha wanashinda,tulijitahidi kadri ya uwezo wetu kwani tulifahamu fika tunacheza na timu gani, wao wana uzoefu mkubwa wa kucheza mechi nyingi za kimataifa kitu ambacho kimechangia ushindi huo,"alisema Okwi.
Aidha, Okwi alisema bado wana nafasi nzuri ya kusonga mbele endapo watatumia vyema uwanja wao wa nyumbani na kuhakikisha wanashikamana na kushinda na kuahidi kuwa watajipanga kitimu zaidi ili kushinda mchezo wa marudiano.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ambaye aliongoza msafara wa kwenda Lubumbashi alisema Mazembe si timu ya kutisha sana kama inavyopewa sifa na wameikuta tofauti na sifa zinazotajwa.
Alisema kuwa timu yake (Simba) ina uwezo mkubwa wa kushinda kwa mabao tena zaidi ya mawili katika mchezo wa marudiano.
Alisema kuwa wamefungwa mchezo wa awali kutokana na makosa ambayo wachezaji waliyafanya hasa upande wa mabeki zaidi katika kipindi cha kwanza.Mechi haikuwa ngumu sana na hata matokeo hayafanani na jinsi tulivyocheza, tunaamini kuwa mchezo wa pili ambao tutautumia uwanja wa nyumbani, tutafanya vyema,î alisema Rage.
ìHata wao wameshangaa na hasa mchezo wa kipindi cha pili, tuliwabana sana na kupata bao muhimu kwetu, tunaamini tutafanya vyema, alisema.Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesingwa alisema jana kuwa Simba ni klabu ya Tanzania hivyo matokeo mabaya ni ya Watanzania wote.
"Tumesikitishwa na kipigo cha watani zetu hasa ukizingatia kule walikuwa wanawakilisha taifa, ushauri wangu ni kwamba wajiande mapema kwa mechi ya marudiano.
"Jambo la kushukuru ni kwamba walipata bao moja ugenini, hivyo kitu muhimu ni wafanye maandalizi ya uhakika tena mapema badala ya kujisahau na kuona nyumbani itakuwa mechi rahisi halafu matokeo yake wakafungwa tena,"alisema Mwesingwa.
Alisema kuwa kiuhalisia TP ni timu bora, lakini mbinu inayoweza kuisaidia Simba na hatimaye kushinda mchezo wa marudio ni wachezaji kujituma kwa nguvu, akili zao zote.
*Calvin Kiwia, Sosthenes Nyoni,Jessca Nangawe na Majuto Omary, Lubumbashi