SAWA MKUU,
Nijuze mafanikio ya mweneyekiti wa simba kwenye michezo,
Fitina zipi zimeleta mafanikio.?
MWENYEKITI mpya wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage alifanya mambo kadhaa saa nane tu baada ya kuingia madarakani Jumapili usiku.
Hatua ya kwanza Jumatatu asubuhi alifanya ziara kwa mara ya kwanza makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi na akakagua jengo la zamani.
Katika ukaguzi huo aligundua kuwa jengo la zamani limechakaa na mfumo wa umeme umeharibika muda mrefu.
Hatua ya pili Rage alikwenda Tanesco kulipia bili ya umeme uliokatwa yapata miaka 15 iliyopita kutokana na kudaiwa Sh 3.7 milioni.
Hatua ya tatu aliwasiliana kwa simu na mwanachama wa klabu hiyo Michael Richard Wambura na kumsihi afute kesi alizofungua mahakama ya Kisutu akitaka uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Jumapili uzuiwe.
Wambura ndiye alimwondoa Rage katika uchaguzi mkuu nafasi ya katibu mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) Desemba 31, 2001 na leo Wambura anafurukuta bila mafanikio kuzuia uchaguzi ambao Rage ameshinda.
Hatua ya nne aliwaita waandishi wa habari akasema pamoja na mambo mengine, uongozi wake upimwe kwa utendaji wake baada ya siku 100 tu.
Halafu alifanya kikao kwa siri akazungumza na watu aliowataja kuwa ni Friends of Simba, wakamkabidhi fedha za kuanza kazi mara moja.
Mbali na wanachama wa rika tofauti, waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, Rage alionekana mwingi wa bashasha, hali iliyoonyesha aliihitaji nafasi hiyo kwa udi na uvumba.
Lakini huenda ni kutokana na kumshinda kwenye nafasi hiyo mfuasi wa kundi la Friends of Simba, Hassan Othman ‘Hassanol' katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili ya Mei 9, kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi, Dar es Salaam.
"This is day one-hii ni siku ya kwanza," alisema Rage alipofika juu ya jengo hilo lililoachwa liharibike bila kufanyiwa ukarabati licha ya watu kupigana vikumbo kutaka kuongoza klabu hiyo kongwe.
Staili ya Rage kuingia kwenye klabu hiyo haitofautiani sana na watangulizi wake katika nafasi mbalimbali. Wambura alipokuwa kaimu mwenyekiti wa klabu hiyo alidai angefuatilia mikataba ya pango la jengo jipya la klabu, lakini hadi anaondoka hakufanya kitu.
Hassan Dalali na katibu mkuu wake, Mwina Kaduguda walidai wangeifanyia makubwa klabu hiyo, lakini hadi wanaondoka wameacha jengo limeoza.
Rage ameingia kwenye klabu hiyo iliyokatika mapande mawili; moja likimuunga Wambura ambaye amefungua kesi ya kupinga kufanyika uchaguzi huo uliomwingiza Rage na wenzake madarakani.
Je, atamudu kuyashona makundi hayo likiwemo la Friends of Simba ambalo hubalika kadri kiongozi anapokwenda kinyume na matakwa yao?
Je, ataimudu klabu hiyo aliyowahi kuiongoza siku za nyuma na akaipeleka timu ya soka Brazil ilikorudi na staili ya uchezaji ya samba na diagonal?
Rage mwenyewe ameonekana mgeni, kwani hali ya klabu imekuwa ikitia kinyaa siku nyingi; mfumo wa maji umeharibika, vyoo vimeziba na masinki machafu, kuta zimekakama, baadhi ya vyumba havina milango na vyenye milango ina hali mbaya.
Kwa hiyo, tatizo si umeme pekee bali jengo zima na kwamba vyumba ambavyo vilikuwa vinafaa kwa malazi ya wachezaji na wageni havifai. Bado wadau au wanachama au wapenzi wamekuwa wakidai ni walinzi wa mali za klabu.
Rage, kwa mbwembwe kabisa, alizunguka jengo hilo akiwa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Cliford Ndimbo ambaye alimpandisha hadi ghorofa ya nne kukagua jengo hilo. Alikuwa kama mgeni.
Ziara hiyo ilikuwa kama filamu fulani, kwani baada ya kutamka ‘This is day one' aligeuka upande wa pili, akasema: "Hali mnayoiona hapa inasikitisha. Kwa kuwa nimesema kwamba ahadi yangu si ya miaka minne tuanze na siku 100, naanza leo."
Staili hii haina tofauti na alipokuwa mwenyekiti wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) na hata alipokuwa katibu mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT)-mbashasha nyingi.
Rage pia ndiye mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Tabora kwa hiyo waliomchagua hakuwafanya patapotea, wanamjua uwezo wake.
Bahati mbaya wengi hawamjui Rage kama mjenzi bali Rage kama mjuzi wa fitina za soka. Hata watani wao wa jadi, Yanga wametikisika kusikia mwanachama huyo wa Saigon ameukwaa uenyekiti wa Simba.
"Rage ni mtu sahihi na muhimu Simba," alisema kiongozi mmoja wa zamani wa Yanga.
"Kama hatukupata mtu imara, atatusumbua sana," alisema bosi huyo.
"Hebu mwangalie Rage alipoongoza DRFA (Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam), chama kilionekana kweli kweli, hebu angalie alivyotua FAT, Simba imelamba dume.
"Hawa Friends of Simba wamwangalie sana Rage, hataki mchezo tena," alisisitiza bosi huyo.
Hata hivyo, Rage atakonga nyoyo za wapenzi wa klabu hiyo ikiwa hayo aliyoanza kuyashughulikia atafanya hivyo, apate ukweli kuhusu mikataba ya jengo jipya, akarabati jengo la zamani liweze kutumika kama watani wao Yanga, awaunganishe wanachama.
Mbali ya siasa za klabuni, asimamie Simba iweze kusimama kwa miguu yake, ijenge kikosi imara cha ushindi si katika Ligi Kuu ya Bara tu bali michuano ya kimataifa.
Atafanikiwa ikiwa kwanza atajenga mshikamano na viongozi wenzake, makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu' na wajumbe wa kamati ya utendaji; Joseph Kinesi, Ibrahimu Masoud ‘Maestro', Swedi Mkwabi, Damian Manembe, Said Pamba na Francis Waya.
Kila kiongozi apangiwe majukumu yake, ajue mipaka na wasiopaswa kuwa wasemaji wajizuie kusema ovyo hasa kwa masuala yasiyowahusu.
Halafu afanye hivyo kwa wanachama wote, awape darasa kuhusu katiba mpya na wajibu wao kuchangia mafanikio ya klabu.
Ushauri wa bure kwa Rage ni kwamba japokuwa yeye ni msemaji mkuu wa klabu, ajizuie kutoa matamko mazito bila kuwasiliana na wenzake.
Source: Mwanahalisi