SIMBA BINGWA LIGI KUU YA VODA TANZANIA BARA !!!!!
* Ni baada ya kuilamba Azam 2-0
SIMBA Bingwa 2009-2010, hivyo ndivyo ilivyo baada ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Azam FC katika mchezo uliofanyika jana katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mike Barasa ndiye aliyeipatia Simba ubingwa baada ya kuifungia timu hiyo mabao yote mawili, na kuamsha shamrashamra na nderemo kwa mamia ya mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.
Kutokana na matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote hata kama itafungwa michezo yake miwili iliyobaki dhidi ya Yanga na Mtibwa Sugar. Ushindi huo umeipatia tiketi ya kucheza michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, mwakani.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, timu zote zilianza mchezo kwa kasi huku Simba ikisaka ushindi wa mapema.
Ndivyo ilivyokuwa, kwani dakika ya nane tu, Mike Barasa aliwanyanyua vitini mamia ya mashabiki wa Simba baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza, akiunganisha pasi iliyopigwa na Hilary Echeza.
Baada ya bao hilo, Simba ilizidisha mashambulizi na kutawala sehemu kubwa ya mchezo, huku wachezaji wa Azam wakionekana kupoteana na kuwaachia wachezaji wa Simba kutamba kwa kupeana pasi fupi fupi.
Azam nao walijaribu kutafuta mpira na kufanya mashambulizi ya kushtukiza langoni kwa wapinzani wao, lakini umaliziaji mbovu uliifanya timu hiyo kuambulia patupu.
Simba iliendelea kufanya mashambulizi makali langoni kwa wapinzani wao na dakika ya 32 nusura Barasa aipatie timu yake bao lingine, lakini shuti kali alilopiga lilipaa juu ya goli na kutoka nje.
Dakika tano baadae, Azam ilijibu shambulizi hilo baada ya mabeki wa Simba kufanya makosa na kumpa nafasi, lakini John Boco alishindwa kumalizia mpira huo na uliotoka nje.
Kipindi cha pili kilipoanza, timu zote zilifanya mabadiliko. Simba iliwatoa Ramdhani Chombo, Ulimboka Mwakingwe na Mike Barasa, nafasi zao waliingia Uhuru Selemani, Mohamed Kijuso na Jerry Santo.
Azam iliwatoa Malika Ndeule, Danny Wagaluka na Said Sued na kuwaingiza Mau Bafio, Ally Manzi na Suleyman Kassim.
Baada ya mabadiliko hayo timu zote ziliendelea kucheza kwa kasi huku zikishambuliana kwa zamu na dakika ya 57 nusura Simba ipate bao la tatu, kupitia kwa Echeza aliyepiga mpira wa faulo uliogonga mwamba na kurudi uwanjani.
Laiti kama Boco na Shaaban Kisiga wangetumia vyema nafasi walizopata, wangeweza kuifungia timu yao mabao, lakini walishindwa kutumia nafasi hizo na kuwaacha wapinzani wao kuondosha hatari zote.
Baada ya mchezo kumalizika, wachezaji wa Simba walimbeba juu kocha wao huku wakimpongeza, hali iliyoamsha shangwe uwanjani hapo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba. Patrick Phiri, alisema amefurahi kuona timu yake ikipata ubingwa ambao alikuwa akiuota.
Phiri alisema ligi hiyo ilikuwa ngumu, lakini kwa uwezo wa Mungu ameweza kufanikiwa kushinda na kusema ushirikiano ndani ya timu yake ndio uliofanikisha kutwaa ubingwa huo huku ikiwa ina mechi mbili mkononi.
Simba iliwachezesha Juma Kaseja, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyoso, Kevin Yondan, Mohamed Banka, Hilary Echesa, Ramadhan Chombo/Jerry Santo, Mussa Hassan 'Mgosi', Mike Barasa/Mohamed Kijuso na Ulimboka Mwakingwe/Uhuru Seleman.
Azam: Vladmir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule/Mau Bofu, Tumba Swed, Salum Sued, Himid Mao, Danny Wagaluka/Ally Manzi, Salum Aboubakar, John Boco, Shaban Kisiga na Said Sued/Suleyman Kassim.