Simulizi: Ajira Toka Kuzimu

Simulizi: Ajira Toka Kuzimu

SEHEMU YA 86



Yule mganga ambaye alionekana kuwa amekufa tayari alinyanyuka kutoka katika ile sahani kubwa, mwili wake ukiwa unachuruzika damu.
“Brenda we Brenda wewe…” mganga akamuita Brenda huku akijiweka sawa katika ile sahani.
Brenda akaanza kurudi kinyumenyume mara ajikwae aanguke anasimama tena. Wengineo walikuwa wanagugumia tu kwa hofu ya maajabu yake.
Mwili ule ukashuka na kuanza kutambaa ukimfuata Brenda.
Mamamia akaiona hatari ya mdogo wake kufa ilikuwa karibu sana.
Akaangaza huku na kule akaokota jiwe ili aweze kumbamiza nalo yule kiumbe.
“Mamamiaaaa tupa tupa hichooo…” Tembo akapiga mayowe Mamamia akaduwaa, na kutazama alichokuwa amebeba.
Kilikuwa kichwa cha mtu!! Kilichofuata hapo ulikuwa mtafutano kila mmoja anakimbia kuelekea anapojua.
Mwishowe wakajikuta mbele ya Asia Digitali.
“Huo ni mwanzo nilikuwa nawafanyia pashapasha…. Kumbe kukimbia mnajua vizuri kabisa…….”
Malipo ya kumtumikia shetani ni makali na yanaumiza kuliko zile faraja anazokupatia wakati unamtumikia*

ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 87


“Huo ni mwanzo nilikuwa nawafanyia pashapasha…. Kumbe kukimbia mnajua vizuri kabisa…….”
******
Asia alitoweka akiwaacha akina Tembo katika sintofahamu ya hali ya juu.
Alikuwa ni Mamamia aliyeunyanyua mdomo wake na kuanza kumlaumu Tembo moja kwa moja, kisha Brenda na Beatrice wakaungana katika kulaumu.
Tembo alitamani sana kuwaeleza kuwa hakuna alilokuwa nafahamu hadi wakati ule lakini wote walikuwa na hasira kali katu asingeweza kuwabadili.
Ile hali ya wenzake kuwa na hasira ilimsababisha Tembo awe kama ametengwa kila mmoja akimuona kuwa ni adui yao. Na wengine wakafikia hatua ya kusema huenda yeye na tuntu lao ni moja katika mpango huo.
Hali ile ya kutengwa ikampelekea Tembo kujikuta akiunda urafiki na kiumbe aliyejiita Maziku. Huyu ndioye kiumbe peke waliyemkuta huko walipoaminishwa kuwa ni kuzimu na mtu aliyeitwa Tuntufye Kanyenye.
Hali hii ilizidisha chuki kwa wenzake ambao walizidi kuamini kuwa Tembo hayupo katika suluba ya nafsi kama wanayoipata wao.
LAKINI ni Maziku huyu huyu ambaye badala ya kuwaacha wageni hawa wa kuzimu wapigwe njaa na kubaki na uchaguzi mmoja tu wa kula nyama ya watu na damu. Aliwasaidia kupata majani majani japo yalikuwa machungu sana walilazimika kula hivyohovyo kuliko nyama za watu.
 
SEHEMU YA 88

“Mwenyekiti atawaua mmoja baada ya mwingine” Maziku ambaye hakuwa amewahi kuzungumza hata siku moja alimweleza Tembo.
Tembo akashtushwa na kauli ya Maziku na ajabu zaidi ule uwezo wake wa kuzungumza ambao hakuwa akiujua.
“Unashangaa kuwa nazungumza… mimi sikukatwa ulimi mdogo wangu!! Nilikuwa mtiifu sana baada ya kugundua sina la kufanya.”
“Nini sasa kilikuleta huku…”
“Tamaa, hata nyie najua ni tamaa tu imewasukumia huku hakuna jingine…” Maziku alijibu.
“Kwa hiyo sisi tunakufa!!” Tembo alihoji na kabla Maziku hajajibu aliuliza tena, “Na hapa ni wapi tulipo…”
“Hapa ni kuzimu…. Hapa hamtoki nd’o mmeshafika.” Maziku alijibu kwa utulivu, kisha akamalizia, “Jamaa ana hasira sana na wewe… ujue siku anakuchagua kukupa kazi tulikuwa wote… akakuamini sana lakini umemwangusha sana… atakuua yule..”
Tembo alipagawa mno kusikia kuna habari za kukatwa ulimi na kuuwawa. Na mbaya zaidi hapakuwa na namna yoyote ya kutoka kule kuzimu.
:Maziku… niombee msamaha.”
“Ukithubutu kumwomba msamaha nd’o umempa ruhusa ya kukuua, Tuntu akusamehe. Jambo la msingi Tembo….” Akasita Maziku akamsogelea Tembo sikioni, “Unatakiwa kupambana naye, anakuogopa sasa hivi maana ulimzika wewe na ilibaki kidogo utukomboe wote, Tembo wewe ni shujaa sana. Pambana utukomboe…’
Tembo alifadhaika baada ya mtu aliyetegemea kuwa atamsaidia na yeye akadai kuwa Tembo nd’o mtu wa kuwasaidia wote.
“Hata jamaa zako wanaokuchukia wote watakupenda ukitukomboa…” alizidisha makali ya motisha ile. Tembo akabaki kujishangaa, ataanza vipi kupambana na mtu mwenye uwezo mkubwa kama Tuntu, ataanza vipi kufanya ukombozi.
 
SEHEMU YA 89



Ni kama Maziku alijua ni kitu gani Tembo anawaza. Akaongezea kauli nyingine iliyoamsha akili ya Tembo.
“Sikia Tembo wenzako sisi hapa ni kama misukule tu, wewe mwenzetu unazo nguvu. Ukifanya mapenzi tu na mwanamke unakuwa na nguvu kama yeye japo kwa muda.”
Tembo akainama chini akakumbuka namna alivyofanikiwa kurejea katika hali yake japo kwa muda mfupi baada ya kuingiliana na Asia.
“Lakini kama alivyokuonya hakuna kurudia kumwingilia msichana mmoja mara mbili….. na hii utaifanya mchana kama huu maana nd’o muda ambao anakuwa ameenda kuzurura duniani kusaka watu wake.” Maziku alimaliza kisha akatoweka akimuacvhya Tembo katika mtihani wa namna yake.
Kuingiliana na msichana kimapenzi halikuwa tatizo, shida ilikuwa kurudia mara mbili. Yaani kwa kuwa aliwahi kulala na Brenda na Mamamia, atakiwi tena kugusa hapo. Hivyo waliobaki ni yule mama mtu mzima aliyekatwa mkono ama yule mwanadada mcharuko naliyedundwa na Mamamia.
Namuanzaje sasa!!! Tembo alijiuliza huku akivutavuta majani yaliyokuwa miguuni kwake.
“Ingekuwa usiku mi ningemlazimisha kwani nini?” akajiuliza kwa sauti ya juu kidogo.
“Kaka!” sauti ya kike ikamtoa katika mawazo mazito aliyokuwanayo. Akageuka kutazama akakutanisha macho na huyu mwanamke mcharuko asili ya uzaramoni aliyedundwa na Mamamia walipokuwa ulimwenguni.
Tembo akabaki kuduwaa, yule binti akaketi jirani naye.
“Yule mkaka anayetupatia chakula amesema unaniita…”
Maziku, Maziku keshaanza wakati sijajiandaa!!! Tembo alilalamika huku akijiweka vyema na kujivika uanaume wake tena akiamua kuamini maneno ya maziku kuwa ni sahihi na hii ilikuwa nafasi ya dhahabu.
“Mi namweleza kama ilivyo aaargh!!” akaghafirika Tembo kisha akaanza kumweleza yule mwanamke juu ya harakati zao za kujikomboa. Akamweleza zaidi hadi kufikia suala la yeye kutafuta nguvu za kukabiliana na yule Tuntu wa Kanyenye.
“Kama haupo tayari basi tungoje atuue kwa mateso ya kutukata kiungo kimoja kimoja hadi tunakata roho.. si umeona alivyomkata yule mama pale…” Tembo alikazia baada ya yule mwanamke kuonekana akipinga kabisa ile hali.
Kusikia juu ya kifo cha mateso yule dada akauliza swali, “Sasa tunafanyia wapi…. Mchana huu…..” swali hilo likamfanya Tembo apepese macho kisha akaenda mahali alipokuwa Maziku. Akamuuliza juu ya hilo.
 
SEHEMU YA 90

Maziku kwa shangwe kuu akamchukua Tembo na yule dada asiyemjua hata jina hadi katika kipori kidogo akawaacha huko.
Upesi upesi na kwa tahadhari kubwa Tembo akataka kumvamia yule dada… na hapo likatokea tukio lililomfadhaisha Tembo kupindukia.
Tembo alikuwa hajiwezi tena, hakupata hamu ya tendon a hata maungo yake hayakuweza kufanya kazi.
Tembo akabaki kulia kama mtoto mdogo.
Yule dada akalazimika kuvaa nguo zake na kumwacha Tembo kichakani, Maziku akaenda akiwa na furaha akiamini Tembo amefanya mambo tayari. Akamkuta akiwa analia.
“Maziku…. Siwezi kufanya lolote tena…..” akataka kuzungumza zaidi upepo mkali ukavuma.
“Mwenyekiti amekuja aisee…..” Tuntu akamkurupua Tembo….. lakini9 kabla hawajapiga hatua yoyote Tuntu ndani ya mwili wa Asia digitali alikuwa mbele yao.
Kama kawaida alikuwa anatabasamu.
“Nilivyokuacha uongee nadhani unaongea hadi yasiyokuhusu sasa…. Haya sema mengine ya mwisho, mwambie upesi maana unaungana na wenzako katika ulimwengu mbaya wa wasiooongea… na wewe Tembo usidhani kuwa nitakukata ulimi wewe. Utajikata mwenyewe kwa meno yako.
“Tembo.. nipiganie naenda kukatwa ulimi…. Nisaidie Tembo.” Maziku huku akiwa anatetemeka kabisa na macho ameyakodoa alimweleza Tembo.
Tuntu alipiga hatua nne kubwa akamfikia Maziku na kumnyanyua juu juu. Kisha akachomoa kisu kidogo na kikali katika upande wa nguo yake.
Tembo akafadhaika na kutaka kujizuia kushuhudia mwanadamu akikatwa ulimi.
“naanza na huyu halafu ni wewe utakayefuata…. Nakukata masikio yako yote mawili na ninakuahidi Tembo kuwa mimi ni jeuri zaidi yako. Utakula sikio lako moja baada ya jingine!!” Tuntu alifoka.
Ubaridi ukapenya katika mwili wa Tembo akasisimka masikio!!!
Maziku akanyanyuliwa juu na kisu kikawekwa tayari!!!
ITAENDELEA KESHOKUTWA!!!.....
 
SEHEMU YA 91

Kwa mara ya kwanza tangu afike eneo hilo asilolijua na akiaminishwa kuwa ni kuzimu Tembo akakumbuka kuwa hajawahi kuomba msaada wowote ule kwa mtu asiyeonekana bali kila siku huwategemea wanadamu na kama ilivyoandikwa basi hujikuta wanamwangusha.
Tembo akafumba macho kwa sekundfe kadhaa.
“Allah! Mbele zako hakuna mchafu wala msafi linapokuja suala la dua. Nimekukosea sana bila kujua kwa kipindi kirefu. Nigeuze shujaa sasa na nipate kuusimulia ulimwengu.” Alipomaliza hapo bila kungoja muujiza wa macho kwa macho alisimama wima.
Akaenda kwa kasi na kumvamia Tuntu ambaye alikuwa ameufungua mdomo wa Maziku kwa ajili ya kuukata ulimi wake.
Akamzaba kibao kimoja bila uoga. Tuntu akamwachia Maziku huku akipigwa na butwaa.
Tembo akamuangalia Tuntu kama anayeangaliana na msichana mwingine tu. Akamuona kuwa ni Asia na hana uwezo wa kumfanya lolote jambo, japo alimzidi urefu.
Mara Tuntu akauchomoa upanga mkubwa, Tembo akaanza kutetemeka lakini akajiaminisha kuwa ni heri kufa akiwa amejaribu kumtegemea Mungu kuliko fedheha waliyotarajia kuipata ikiambatana na mateso makali. Kabla Asia hajamfikia Tembo, Maziku naye alijirusha akamkwaa miguuu yake akatua chini kama gunia la mahindi.
Tembo akamsogelea na kumpa amri moja kuu iliyomstaajabisha. Wala Tembo hakujua ametoa wapi ujasiri wa kuitamka.
“Una machaguo mawili, aidha kutuacha huru tuondoke ama Mungu wetu atakuangamiza kwa mateso makali….”
Tuntu hakujibu lolote alibaki ametulia tuli pale pale.
Tembo alianza kumtikisa, hakuna dalili yoyote ya kuinuka. Wakasaidia na Maziku lakini bado hali ilikuwa vilevile.
“Amekufa…..” Maziku alimweleza Tembo. Jambo ambalo Tembo hakuamini linawezekana kuwa jepesi kiasi kile.
Baada ya dakika kumi na tano likazuka vurumai jingine.
 
SEHEMU YA 92


Maziku ndiye aliyeanza kukumbana na dhahama hiyo. Akaanza kupigwa vibao bila kumwona mtu anayempiga. Tembo na yeye akiwa ameduwaa tu akashtukia Maziku akinyanyuliwa juu na kitu kisichoonekana na kisha akaachiwa na kutua chini bila kuhitaji ushahidi wa ziada iwapo amekufa ama la maana alitua juu ya jiwe na kupasuka pasuka.
Mamamia akasikia akipiga kelele baada ya sekunde kadhaa. Tembo akatimua mbio kuelekea zinapotokea kelele, kama ilivyokuwa kwa Maziku. Mamamia alikuwa akijaribu kujikinga uso wake mara mgongo wake huku akilia.
“Nipe macho eeh Mungu unayetupigania sasa…..” aliomba Tembo kwa imani huku akitambua hayupo wa kuwasaidia zaidi ya Mungu aliyewaumba.
Muujiza!! Ndo jambo pekee Tembo aliloweza kusema. Kabla hajachukua hatua.
Aliweza kumuona Tuntu, safari hii hakuwa tena katika mwili wa Adia. Huyu alikuwa yule Tuntu aliyemjia ndotoni.
Upesi wakati anamkaba Mamamia, na yeye akajikongoja upesi kuelekea alipokuwa.
Akafika na kumnasa kibao kikali cha mgongoni.
Tuntu akaduwaa kuwa Tembo alikuwa ameweza kumuona Tembo.
“Kila mmoja asali kwa imani yake, la sivyo tunakufa wote. Kila mmoja aombe kwa juhudu huku akiamini…” Tembo akawahusia wenzake kwa kuhamasisha. Wakati huo alikuwa akikabiliana ana kwa ana na Tuntu.
Nguvu za Tuntu zilikuwa kubwa lakini aliweza kuhimili vishindo. Wenzake wakaanza kusali wajuavyo wengine kwa sauti na wengine kimya kimya.
Amakweli Mungu wetu ana nguvu na akiitwa huitika.
Tuntu alilainika na kuishiwa nguvu, wale aliowakata ulimi wote wakarejewa na ufahamu wao zaidi na hawakumuogopa. Wakamvamia wakiwa na mapanga na marungu mikononi ambayo huwa wanayatumia kufanyia shughuli za kulima mashamba ya wachawi duniani.
 
SEHEMU YA 93


Wote wakiwa wanaunguruma kwa hasira walimfikia Tuntu aliyekuwa anakabiliana na Tembo.
Kilichotokea pale kilikuwa kipigo kitakatifu.
Oparesheni, ondoa shetani.
Tuntu alijaribu kila namna akawaita miungu wake lakini hawakusimama mbele ya jina kuu kupita yote duniani na mbinguni.
Mungu!!
Alipigwa hadi akalainika, Tembo akarejea kuwa Munyama mukubwa lakini katika namna nyingine. Safari hii katika ulimwengu wa kishujaa kweli.
“Haya imetosha!!” akaamrisha… wote wakaacha…. Akamsogelea Tuntu pale chini. Akamtazama na kugundua kuwa alikuwa katika hatua za mwisho kabisa za kukata roho.
“Tembo….. nisamehe mjukuu wangu…” alizungumza.
“Wahi duniani… wahi uwaambie watu ukweli…. Wahi waujue ukweli..” alisisitoza yule wa kuitwa Tuntu.. Tembo akabaki katika mshangao tu. Yule mtu hakuzungumza tena chochote. Akatulia tuli.
“Tembo…. Tembo… we Hathani, hapa mbona ni Chamandhi jamani.. uwanja wa timu ya Adham ule pale…..” Brenda ambaye alikuwa kimya na mwenye uoga kwa muda mrefu alizungumza huku akistaajabu. Wenzake wote wakageuka wote wakabaki midomo wazi waliolijua eneo lile la Chamanzi.
Hapakuwa kuzimu bali walifumbwa macho yao kishetani!!
Kigiza kilianza kuingia wakati Tembo akiongoza kundi la watu zaidi ya sitini kutoka katika mji wa giza.
Tembo alikuwa shujaa wa kweli katika hili. Wale wasiweza kuzungumza baada ya kukatwa ndimi zao walibaki kutabasamu na kuunguruma tu.
Mama mwenye mkono mmoja hakuwa na maumivu tena lakini alikuwa akiugulia kuupoteza mkono wake, lakini hakujuta sana kwani ilikuwa heri kupoteza mkono wake kuliko uhai.
 
SEHEMU YA 94


“Tutalala kwa bibi yangu… anakaa maenmeo ya huku huku na akisha asubuhi tutajua nini cha kufanya….” Tembo jemedari alikuwa akiliongoza kundi, nani angeweza kumpinga.
Wakatembea hadi katika nyumba kubwa iliyozungukwa na uzio wa miti ya miiba. Tembo akagonga hodi mara kadhaa mlinzi akafungua.
Kwa jinsi alivyokuwa amechafuka mlinzi hakuweza kumtambua hadi alivyomulika na tochi.
Tembo ana nywele kichwani tangu lini?? Mlinzi alijiuliza.
“Na hawa akina nani?” Mlinzi akahoji.
“Ni ndugu zangu hawa wote na watalala kwa bibi yangu…” alijibu. Mlinzi akasita akafunga geti kwanza kisha akaenda ndani kutoa maelezo hayo.
Bibi akaruhusu Tembo afunguliwe!!
Tembo na wafuasi wake wakaingia ndani.
Wakangoja nje wakati Tembo aliingia ndani kwenda kukutana na maajabu ya mwaka.
Bibi alikuwa ameketi kitandani na aliyekuwa amelala alisemekana kuwa ni mgonjwa!!
“Ni babu yako…”
“Babu? Babu gani tena mwingine zaidi. Babu yangu alikufa zamani..” Tembo alistaajabu. Bibi akashusha pumzi kidogo, akamtazama Tembo usoni kwa masikitiko kiasi.
“Babu yako…..” bibi akashindwa kuendelea.
Yule mgonjwa kitandani aliyekuwa amefunikwa shuka gubi gubi akazungumza.
“Mwambie, mwambie tu usiogope……”
Bibi akaduwaa kwani ni muda mrefu ulipita bila mgonjwa yule kuzungumza.
“Babu yako hakufa, lakini alipewa cheo huko kwa wenzake.”
“Wenzake gani sasa??” alihoji Tembo.
“Wachawi!!”
“Nini bibi??? Yaani unamaanisha kuwa babu ni mchawi?? Mbona balaa leo lanikumba mimi.” aliuliza huku akiwa wima.
Kama aliyeshtuliwa kutoka usingizini, yule mgonjwa aliinuka kisha akajifunua shuka lake.
“Naitwa TUNTUFYE KANYENYE!!!!”
 
SEHEMU YA 95 MWISHO



Tembo akaingiwa na ubaridi mkali kupindukia, akajihisi uoga kukutana na mtu ambaye anaamini alikutana naye kuzimu.
Akaanza kutetemeka, lakini mzee yule akabaki kumwaga risala.
Akaomba msamaha na mengineyo kisha kumwomba Tembvo aitangazie jamii nzima bila uoga wowote.
“Nilijua umri wangu umeenda sana nikaambiwa nikabidhi mikoba yangu kwa mwana ukoo, nikakuchagua wewe. Lakini bahati mbaya ama nzuri umekuwa shujaa na umeshinda vita hii. Hakika si utawala mzuri kumtumikia shetani. Tazama leo nakufa huku nikiwa nahitaji kuishi. Amakweli mungu wa kweli ni Mungu wenu nyinyi aliyeisimamisha miungu yote iliyotaka kuwachinjia mbali. Mungu wenu ni Mungu mkuu na kama ningeipata nafasi ya kuishi hakika ningeinama na kumsujudia yeye.” Alizungumza kwa hisia kali huku akimtazama Tembo.
Baada ya hapo hali ikawa mbaya, akalala na hakuamka tena.
Akafa kwa amani baada ya kumfumbua macho Tembo kuwa ni yeye aliyetakiwa kurithi mikoba ya kuzimu.
****
KIHITIMISHO!!!
ILIKUWA kama babu alivyohitimisha Tembo alijiweka hadharani na kutangaza juu ya muujiza huo. Akamsifu Mungu kwa maajabu yake na nguvu zake za kipekee.
Akajitolea kumtumikia katika ujana wake hadi uzee wake.
Somo la Tembo likawafungua wengi wasiokuwa na imani. Likawajaza nguvu zaidi waliokata tamaa.
Pesa alizozipata kwa njia ya kichawi sasa akazipata kihalali kabisa. katika ushuhuda wake zilichangwa milioni nyingi kwa ajili ya wale wahanga wa kukatwa ndimi zao. Wakapatiwa makazi.
Tembo akabakia kuwa Munyama Mukubwa sio kwa ajili ya pesa tena bali kwa jinsi alivyoishinda AJIRA TOKA KUZIMU.

MWISHO
 
Bado tunaendelea na Uchaguzi, Simulizi yenye kura 10 itarusha, tupia kura yako.

SAFARI NDEFU KUELEKEA KABURINI - NYEMO CHILONGANI ~ Simulizi ya Kusisimua ......(Kura 2/10)

DEAD LOVE ( PENZI LILILOKUFA ) - AZIZ HASHIM ~ Simulizi ya Maisha......(Kura 0/10)

MIKONONI MWA NUNDA - BEN R. MTOBWA ~ Simulizi ya Kijasusi......(Kura 4/10)


OOH!! KUMBE TAMU - YONA FUNDI ~ Simulizi ya Mapenzi......(Kura 0/10)
 
Bado tunaendelea na Uchaguzi, Simulizi yenye kura 10 itarusha, tupia kura yako.

SAFARI NDEFU KUELEKEA KABURINI - NYEMO CHILONGANI ~ Simulizi ya Kusisimua ......(Kura 2/10)

DEAD LOVE ( PENZI LILILOKUFA ) - AZIZ HASHIM ~ Simulizi ya Maisha......(Kura 0/10)

MIKONONI MWA NUNDA - BEN R. MTOBWA ~ Simulizi ya Kijasusi......(Kura 4/10)


OOH!! KUMBE TAMU - YONA FUNDI ~ Simulizi ya Mapenzi......(Kura 0/10)
Shukrani mkuu
 
Watu wanaogopa simulizi kwa sababu hamchelewi kuwavutia telegram
 
Back
Top Bottom