Simulizi: Asante kwa Kunifuta Machozi (Hisia Zangu)

Simulizi: Asante kwa Kunifuta Machozi (Hisia Zangu)

SEHEMU YA 33 KATI YA 50

?Mh! Kweli mtu hawezi kuona tatizo lake, Latifa wewe hukulala na Big siku ile ukarudi kesho yake mchana? Bora hata mimi nimerudi asubuhi,? akasema Lilian kwa kujiamini.

Wakacheka tena.

Lilian akaamua kuingia bafuni, akaoga haraka kisha akatoka na kujitupa kitandani.

?Sitaki usumbufu leo, hata darasani sitakwenda, nahitaji kupumzika siku nzima ya leo,? akasema Lilian.

?Sawa mama, umesomeka!? Lucy ndiye aliyejibu.

Lilian akavuta shuka, kama vile alikuwa amelala usiku. Akajitahidi kuvuta usingizi.

***

WIKI MOJA BAADAYE

Lilian hakuamini macho yake, aliendelea kukaza macho yake kwenye kioo cha simu yake ili kupata uhakika wa alichokuwa akikiona, lakini bado kiliendelea kuwa vilevile.

Namba iliyokuwa ikimpigia ndiyo iliyomchanganya Lilian. Namba ya mpenzi wake Edo ya nchini Tanzania.

?Mh! Inamaana Edo yupo Bongo?? akajiuliza.

Alijiuliza sana, lakini baadaye akagundua maswali yake yasingekuwa na maana kama asingepokea simu na kuujua ukweli. Mara moja akabonyeza kitufe cha kupokea.

?Haloo,? akaita Lilian.

?Surprise! Surprise!? akasema Edo.

?Baby really?? akauliza Lilian.

?Yeah baby, nipo jijini Dar es Salaam,? akasema Edo kwa furaha.

?Uko wapi nikufuate mpenzi wangu??

?Ha! Ha! Ha! Huo ni wimbo wa Ray C! Sikia nipo hapa chuoni.?

Lilian alihisi kuzimia!







KWA sekunde kadhaa alibaki amesimama ameduwaa kabisa, bila kujua cha kufanya. Hakujua kama alikuwa na furaha au huzuni. Hakuna alichojua kuhusu tukio lile! Furaha ya Edo kuja na huzuni ya kuja kumtibulia penzi lake jipya kwa Pam!

Edo kuwa Tanzania, tena chuoni! Lilikuwa jambo kubwa na la kushtukiza kuliko kawaida. Alibaki hewani, akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu kabisa.

Edo alikuwa amemchanganya sana.

?Baby are sure?? akauliza Lilian.

?Yes baby, kwani nina utani na wewe?? akasema Edo.

?Najua huna, uko maeneo gani sasa??

?Kwani wewe uko wapi??

?Utawala.?

?Hata mimi pia nipo hapa Utawala.?

Lilian akazidi kuchanganyikiwa. Kama ni mshtuko ulikuwa wa kipekee kabisa kuwahi kutokea katika maisha yao ya kimapenzi.

?Hebu geuka, angalia upande wa kituoni, kuelekea Survey!? akasema Edo.

Lilian akafanya hivyo!

Hakuamini!

Edo alikuwa amesimama upande wa pili. Ghafla Lilian akataka kuvuka barabara, Edo akamwonyesha ishara kwamba asifanye hivyo. Akatulia kwa muda, kisha Edo akavuka na kumfuata.

Walirukiana na kukumbatiana kwa nguvu. Kwa zaidi ya dakika mbili walikuwa wameng?ang?aniana bila kuachiana. Walikuwa na mengi ya kuongea.

?Mambo baby?? Lilian alimwambia Edo akijitoa kifuani mwake.

?Poa.?

Tayari macho ya Lilian yalikuwa yameshajaa machozi kila kona. Hakutegemea kabisa kukutana na Edo muda ule, ingawa kichwani mwake alikuwa na mawazo sana na mpenzi wake mpya Pam.

?Umependeza sana mpenzi,? akasema Lilian.

?Hata wewe pia mama, umependeza mpaka kidogo nikusahau!?

Wakacheka sana!

?Kwa nini umekuwa bonge hivyo? Unakula nini?? Edo akauliza tena.

?Kama kawaida, vyakula vya hapa chuoni si unavijua!?

Walizungumza mengi, mwisho Edo akamwambia Lilian watoke waende kwenye hoteli aliyofikia. Lilian hakubisha, alikubali haraka sana.

?Tusubiri daladala hapa,? akasema Lilian.

?No! Nimekuja na teksi.?

?Sawa, wapi sasa??

?Tabata.?

?Sawa.?

Wakavuka barabara, Edo akampigia simu dereva ambaye alikuwa ameegesha kwenye maegesho, muda mfupi baadaye, gari aina ya Toyota Corolla liliegesha mbele yake. Edo akasogea na kufungua mlango wa siti za nyuma.

?Karibu malkia wangu,? akasema Edo akiachia tabasamu mwanana.

?Ahsante mfalme wangu!?

Wakacheka!

Baada ya Lilian kuingia ndani ya gari, alifuata Edo ambaye alibamiza mlango kwa nguvu. Dereva akawasha gari na kuliondoa kwa kasi.
 
SEHEMU YA 34 KATI YA 50

Njia nzima walikuwa wakizungumza mambo mbalimbali kuhusu maisha baada ya kutengana kwa muda mrefu. Edo alikuwa akimpenda sana mpenzi wake. Alimweleza kila kitu kuhusu uzuri wa nchi ya Malaysia.

Muda wote, Lilian alikuwa na mawazo na Pam, hakujua ingekuwaje kama angempigia. Hakutaka kabisa kitu hicho kitokee.

?Kifupi bado kidogo tu nimalizie masomo yangu. Nimefurahi kukukuta mzima mpenzi wangu. Najua unakosa misaada yangu kwa kipindi hiki lakini usijali mambo yanakaribia kuwa mazuri na utaratibu utaendelea kama kawaida,? akasema Edo.

?Najua baba, wala hupaswi kuniambia mpenzi wangu. Najua mazingira ya nje.?

?Nashukuru kwa kuelewa.?

Ukweli uliokuwa ndani ya Lilian, ni kwamba hakuwa na shida ya pesa hata kidogo, Pam alikuwa akimwezesha kwa kila kitu. Kutokana na mazungumzo ya hapa na pale, Tabata hapakuwa mbali sana.

Walifika wakiwa hawajachoka hata kidogo, ni kama hawakuwa kwenye safari. Walishuka garini, Edo akamlipa dereva kisha wakatembea wakiwa wameshikana mikono wakielekea ndani ya hoteli aliyofikia Edo.

Walipoingia tu chumbani, walivutana kwa nguvu kisha wakaanza kubadilishana mate. Muda mfupi baadaye, wote wakiwa wanahema kwa kasi, wakajikuta wakiwa watupu! Hakuna aliyekuwa na hiyari ya kufanya tendo hilo.

Jambo lililomshangaza Edo ni kwamba, Lilian alionyesha dalili zote za kuhitaji tendo la ngono. Ilikuwa ni maajabu sana kwa Edo. Lilian ambaye siku zote alikuwa mgumu akionyesha msimamo, iweje leo akubali kirahisi namna hiyo?

?Hapana, kuna kitu. Lazima...? akajisemea moyoni mwake.

?Baby please, I?m hot,? Lilian akasema kwa Kimombo.

Wote walikuwa kama walivyozaliwa, ilikuwa kazi ngumu sana kwa Edo, lakini alijitahidi sana kuzuia hisia zake. Mara moja akajiondoa mikononi mwa Lilian.

?Vipi?? Lilian akauliza akiwa amekunja uso wake kwa hasira.

?Siyo makubaliano yetu Lilian.?

?Najua mpenzi, lakini mwili wangu umewaka kwa tamaa ya mapenzi, sina namna. Nisaidie mpenzi.?

?Lilian, lakini wewe ni bikira.?

?Najua mpenzi, nimeamua kukupatia hii zawadi leo.?

?Hapana.?

?Lakini si wewe ulikuwa unang?ang?ania kila siku tukutane? Iweje leo unakataa tena unakuwa mkali kiasi hicho?? akasema Lilian.

?Tutafanya hivyo lakini mpaka tupime ukimwi.?

?Kwahiyo mimi naonekana nina ukimwi siyo??

?Kwa nini usifikiri labda mimi ndiye naonekana nina ukimwi? Tunahitaji kuwa waangalifu mpenzi. Tuna mipango mingi sana mbele yetu kuhusu maisha yetu. Hatuwezi kuwa rahisi kiasi hiki. Kama kweli unanipenda, tutoke sasa hivi, twende tukapime tuwe na uhakika na afya zetu kisha tuendelee na mambo mengine,? akasema Edo.

?Sawa,? akasema Lilian kwa hasira, akainuka kitandani na kukimbilia bafuni ambapo alioga, alipotoka alimkuta Edo ameshavaa anamsubiri yeye.

?Haya twende,? akasema Lilian.

?Ok!?

Edo akabamiza mlango, akaingiza ufunguo kwenye kitasa, akafunga. Wakaanza safari ya kwenda kituo cha afya.





MOYONI Edo alikuwa na mawazo mengi sana. Alijaribu kumfikiria Lilian wake, si yule mwenye msimamo tena. Nini kimetokea hadi msimamo wake ubadilike? Ni kweli alikuwa na hisia, tena hisia kali sana za kimapenzi, lakini isingekuwa rahisi kuingia kwenye mtego wa namna ile.

Alikuwa na wasiwasi mwingi sana moyoni mwake. Hakujua ilivyokuwa, lakini alijishangaa kwa namna alivyoingiwa na wasiwasi wa ghafla.

?Siwezi kuwa mjinga kiasi hiki, lazima kuna kitu,? akajisemea moyoni mwake Edo wakati akipiga hatua kutoka kwenye chumba chake na kushika korido kuelekea nje.

Lilian alikuwa akitembea bila wasiwasi kabisa, hakuonekana kufikiria jambo lolote baya kichwani. Alikuwa katika hali ya kawaida kabisa.
 
SEHEMU YA 35 KATI YA 50

?Lilian na msimamo wake wote ule? Leo anawezaje kubadilika? Anawezaje kukubali kirahisi namna hii? Lazima atakuwa ameshaanza haya mambo. Angekuwa bado ningejua tu...hapa kuna kitu,? akazidi kuwaza Edo.

Edo hakuwa na gari, hivyo walitoka kwa miguu hadi kwenye kituo cha teksi, wakaingia kwenye mojawapo.

?Wapi bro?? dereva teksi akauliza.

?Tabata Health Centre.?

?Sawa, si pale kwa Dk. Manungu??

?Sina hakika, naijua tu hiyo hospitali, sifahamu jina la mmiliki.?

?Sawa. Kaka, huyo ni daktari maarufu sana, alikuwa Muhimbili, sasa ni mstaafu ndiyo akaamua kufungua senta yake hapa Tabata.?

?Kikubwa ni kutufikisha hapo kaka, kanyaga mafuta tafadhali,? akajibu Edo akionekana kutohitaji maneno mengi kutoka kwa dereva yule.

Gari likapepea!

Hapakuwa mbali sana, dakika kumi tu baadaye, teksi hiyo aina ya Toyota Carina, lenye rangi nyeupe na mstari wa kijani pembeni, iliegeshwa mbele ya hospitali hiyo ambayo iliaminika sana katika Kitongoji cha Tabata.

?Kiasi gani??

?Elfu tano zinatosha bro.?

?Sawa.?

Edo akaingiza mkono mfukoni, akatoa pochi yake kisha akachomoa noti moja ya elfu kumi kati ya nyingi zilizotunisha pochi hiyo. Akamkabidhi dereva, kisha akamshika mkono Lilian na kuondoka.

?Chenji yako kaka...? akasema dereva yule akitoa noti moja ya elfu tano kupitia dirishani.

Edo akageuza shingo kumwangalia, akaachia tabasamu changa ambalo alijitengenezea. Akachanganya midomo, akasema: ?Ni lini utakunywa soda wewe? Kazi njema!?

Dereva akachekelea!

Hakuwa amezima gari lake, lilikuwa silence! Alichokifanya ilikuwa ni kuachia mguu aliokanyaga breki taratibu, mikono yake ikiwa kwenye usukani, kisha akahamisha mguu wake wa kulia kwenye kibati cha mafuta, akakanyaga taratibu, teksi ikayoyoma!

?Pesa bwana...kweli pesa inaongea,? akajisemea dereva yule wakati akiendelea kuongeza spidi kurejea kituoni kwake.

Siku yake ilikuwa inakaribia kuisha vizuri.

***

?Karibuni tafadhali,? sauti ya dada mrembo, aliyekuwa mapokezi katika hospitali hiyo ilitoka akiwatazama Edo na Lilian.

?Ahsante, tunahitaji huduma ya ushauri na kupima.?

?Oooh! Karibuni sana, bila shaka kabisa. Huduma inapatikana, piteni na hii korido, mtakata kulia pale mbele, room ya kwanza mtaiacha, mtaifuata ya pili ambayo mlangoni imendikwa VCT. Ni hapo mtaingia.?

?Ahsante sana.?

Edo akamshika mkono Lilian kisha wakaongozana kuelekea chumba cha mshauri. Kwa namna walivyoelekezwa, haikuwa vigumu kufika.

Edo akagonga mlango, kisha wakaingia. Wakapokelewa na mshauri mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha kuzunguka. Akawakaribisha na tabasamu mwanana kabisa.

?Karibuni na mjisikie huru!? akasema mshauri huyo.

?Ahsante sana.?

?Karibuni tena...mimi naitwa Dk. Siwema, ni mwanasaikojia, mtaalamu wa ushauri nasaha kwenye mambo mengi katika jamii lakini kwa sasa nimebobea zaidi kwenye elimu rika na ukimwi. Naomba tufahamiane tafadhali,? akasema Dk. Siwema akitabasamu.

?Mimi ni Edward lakini nimezoeleka zaidi kama Edo, huyu ni mpenzi wangu, yeye anaitwa Lilian au Lily.?

?Nimefurahi sana kuwafahamu Edo na Lily, acha nami niwaite hivyo,? akasema Dk. Siwema huku akicheka.

Wote wakacheka.

?Ndiyo! Sasa naomba niwasikilize.?

?Sisi tumekuja hapa kwa ajili ya kupima afya zetu.?

?Kivipi??

?Tunataka kupima virusi vya ukimwi.?

?Vizuri sana, hilo wazo mmeamua pamoja au kuna mmoja amekuwa na shinikizo kwa mwenzake?? Dk. Siwema akauliza.

Wote walibaki kimya, ni kama walikuwa wanategeana hivi...

?Aaaah! Nataka swali hili anijibu Lily.?

?Siwezi kusema kama kumekuwa na shinikizo lakini lilikuwa wazo la mwenzangu. Sijaona kama ni vibaya, ni wazo zuri tu, ndiyo maana nimeamua kuja naye hapa.?
 
SEHEMU YA 36 KATI YA 50

?Je, mmewahi kukutana kimapenzi?? akauliza Dk. Siwema.

?Hapana,? wakajibu wote kwa wakati mmoja.

?Kwa nini??

?Tulikubaliana kufanya hivyo siku tutakapoona,? akajibu Edo.

?Je, sasa mpo tayari kuoana??

?Tutaona tu, lakini muda bado. Wote bado tunasoma. Mimi nipo Malaysia na mwenzangu anamalizia UD (University of Dar es Salaam), lakini kwa kweli uzalendo umetushinda, tukaamua kuliko kusalitiana ni bora tuanze tu wenyewe.?

?Sawa. Je, mpo tayari kushauriwa pamoja majibu mpokee pamoja??

?Ndiyo, tupo tayari.?

?Vizuri sana. Najua siku hizi elimu ya ukimwi ipo wazi sana hivyo hakuna mambo mengi sana mapya ya kuwafundisha hapa. Jambo la msingi mnalotakiwa kujua ni kwamba, kwanza mmefanya vizuri sana kuamua kujuana afya zenu kabla hamjaanza kufanya chochote.

?Ni wazo zuri, lakini vizuri pia mkiendelea kuwa makini hata baada ya majibu yenu. Mnapaswa kuwa waaminifu katika uhusiano wenu, hapo ndipo mtakapoona raha ya uhusiano. Sasa turudi katika suala lenu. Vipi kama ikitokea mmekutwa wote mmeathirika??

?Ikiwa tutakuwa tumeathirika wote, kwa kweli tutaumia sana, lakini itabidi tuendelee na uhusiano wetu huku tukipeana moyo,? akajibu Edo.

?Niwatoe hofu, ukimwi usiwaogopeshe sana, hata kama mkikutwa nao au mmoja wenu akawa ameathirika, hampaswi kuchanganyikiwa. Mkifuata ushauri vizuri, mtu anaweza kuishi zaidi ya miaka ishirini baada ya kujua kama ana maambukizi.

?Ninao marafiki wengi sana ambao wameathirika na maisha yao yanaendelea kama kawaida. Msijali. Kupima ni kujua ukweli wa afya zenu. Hata kama msipojua leo, kuna siku mtajua mkiwa mmeshachelewa.

?Ni afadhali mjue mapema, muanze kufuatilia masharti mapema na kwa usahihi ili muweze kuishi maisha marefu. Nasisitiza, msiwe na wasiwasi, sawa jamani??

?Sawa dokta.?

?Sasa mpo tayari nichukue vipimo vyenu??

?Ndiyo!?







HOFU kuu iliwavaa wote. Ingawa ni kweli walikuwa tayari kwa vipimo, lakini kwa ndani hawakujiamini.

Lilian alijua wazi kuwa yeye hakuwa bikra. Tayari alishavunja ahadi yake kwa kutoka na Pam. Hilo lilikuwa kosa kubwa maana hakumjua vizuri Pam.

Hata hivyo, hofu yake haikuwa kubwa kutokana na kwamba, hakuwa na ufahamu sana na habari za maambukizi ya ukimwi. Kwa Edo kulikuwa na mashaka zaidi.

Edo pamoja na kwamba alikuwa mwaminifu katika kipindi chote alichokuwa na Lilian, kabla yake alishawahi kutoka na wasichana kadhaa.

Hilo lilimpa hofu kidogo, lakini akajipa moyo.

?Ni vizuri kujijua afya yangu. Nafikiri ni sahihi kupima,? akawaza.

?Ok! Nafikiri tunaweza kuanza sasa,? akasema Dk. Siwema.

Muda huohuo Dk. Siwema akaweka vifaa tayari, haikuwa kazi kubwa, maana alitumia kifaa kidogo na kwa urahisi. Aliwatoboa vidole, kisha akachukua damu na kuweka kwenye kipimo ambacho majibu yake hutoka haraka, wateja wakiwa hapohapo.

Zoezi lilipokamilika, Dk. Siwema aliwaangalia. Wote wakaonekana kuwa na wasiwasi sana.

?Majibu yenu yapo tayari, naweza kuwapa sasa?? Dk. Siwema akaanza kuzungumza.

?Tupo tayari kabisa, tupo tayari,? akasema Lilian.

?Kama tulivyokubaliana, naomba iwe vilevile. Majibu yote ni majibu, kwa hiyo naomba muyapokee kama yalivyo, sawa jamani?? akasema Dk. Siwema.

?Sawa...? wote wakajibu.

?Majibu yaliyopatikana kwenye damu ya Edo yanaonyesha kuwa, Edo huna uambukizi...? akasema Dk. Siwema kisha akatulia kwa muda.

?Uko negative, hongera sana kwa hilo,? akasema tena.

Edo alitabasamu, Lilian akawa anasubiri kwa majibu yake. Uso wa Dk. Siwema ni kama ulikuwa na ujumbe tofauti ambao alikuwa akijaribu kuuficha au kutafuta mbinu sahihi za kuufikisha.

?Kwa upande wako Lilian...? akasema Dk. Siwema kisha akameza funda kubwa la mate.
 
SEHEMU YA 37 KATI YA 50

Akaendelea: ?Damu yako inaonekana ina matatizo kidogo... na ni kweli kabisa kuwa damu yako ina maambukizi ya ....? kabla Dk. Siwema hajamalizia kusema, Lilian alimkatisha.

?Haiwezekani, nasema haiwezekani. Nyie mna njama zenu. Unasemaje? Oooooh! Pam... Pam umeniua Pam,? akasema kwa sauti ya juu.

Edo aliinamisha kichwa chini, machozi yakimwagika machoni mwake kama mfereji unaomwaga maji kutoka mlimani!

Edo ndiye aliyechanganyikiwa zaidi, akasimama na kumshika Lilian mikono yake. Naye akasimama. Wakajikuta wamekumbatiana. Wote walikuwa wakilia.

?Lilian kwa nini lakini, kwa nini?? Edo akasema akipiga kelele kwa uchungu.

?Edo siyaamini haya majibu, siyaamini kabisa,? akasema Lilian.

?Naomba mtulie kwanza jamani, hebu ketini,? akasema Dk. Siwema kwa sauti ya kusihi sana.

Wakaketi.

?Sikilizeni...? akasema tena Dk. Siwema.

?Sina sababu ya kudanganya kwa lolote. Ninyi nyote ndiyo najuana nanyi kwa mara ya kwanza leo hii.

?Kusema kuwa naweza kuandka majibu ya uongo, haiwezekani. Halafu Lilian unapaswa kutulia kama nilivyosema awali. Hakuna kitu cha kutisha hapo.

?Ni kweli umeathirika, lakini siyo mwisho wa maisha yako. Bado kuna mambo mengi ambayo unaweza kufanya bila kuathiri maisha yako. Tulia...nawahitaji mje tena hapa kesho kwa ushauri zaidi.

?Lilian unatakiwa kupima pia kinga zao za mwili ili kujua mahali pa kuanzia na kukuweka katika hali salama, uendelee kuyafurahia maisha kwa muda mrefu zaidi,? akasema Dk. Siwema.

Yalikuwa maneno makali sana kwa Lilian. Alihisi kichwa kumgonga kabisa. Hata hivyo hakuwa na namna zaidi ya kukubaliana na hali halisi.

Ni kweli kabisa, alikuwa ameathirika. Kwa shingo upande, Edo akimwongoza, kutoka nje ya chumba cha daktari. Safari yao ikawa moja kwa moja hadi barabarani walipochukua teksi iliyowarudisha hotelini.

***

?Nataka uwe mkweli kwangu Lilian,? akaanza kusema Edo.

?Ndiyo.?

?Ulinisaliti?? akauliza Edo kwa ukali.

?Haikuwa dhamira yangu Edo mpenzi nilileweshwa!?

?Nataka kujua, ulinisaliti??

?Ndiyo!?

?Na nani??

?Kuna baba mmoja hivi, anaitwa Pam. Ni yeye tu ndiye niliyetoka naye, sikuwa na mwingine zaidi yake. Ilitokea kwa bahati mbaya. Rafiki zangu walitaka nitoke nao kwenda klabu, huko ndiyo mwanzo wa yote.

?Walinidanganya nikanywa pombe, nilipolewa ndiyo akanishawishi, baada ya hapo sikuweza tena kuachana naye. Sikujua kama angekuwa na maambukizi. Najuta mimi,? akasema Lilian akilia.

?Nakupenda sana kutoka ndani ya moyo wangu, sijui nitaishi vipi bila wewe. Angalia...umeharibu ndoto zangu. Umenipotezea dira ya maisha yangu. Kwa nini umenitenda hivyo?? akasema Edo kwa uchungu sana.

?Nisamehe mpenzi wangu. Najua huu ni mwisho wa mapenzi yetu, lakini tafadhali naomba unisamehe. Hata kama utakuwa na mwanamke mwingine badala yangu, lakini nisamehe kwa kukuumiza moyo wako.

?Naomba radhi kwa kukutesa hisia zako. Nisamehe tafadhali, haya yaliyotokea sikuyajua kabisa,? akasema Lilian.

Edo alibaki kimya!

?Umenisamehe Edo?? akauliza Lilian.

?Sikia, nakupenda sana. Hata moyo wangu unajua hilo, akini kwa hili samahani sana...hebu nipatie muda nipumzike kidogo kwa sasa.

?Tafadhali naomba uondoke hapa hotelini. Niache peke yangu. Nahitaji muda wa kuwa mwenyewe kwa sasa,? akasema Edo.

Lilian hakutaka kubishana naye. Alijiandaa na kujichukulia vitu vyake pale chumbani kisha akatoka nje, ambapo umbali mfupi sana kabla ya kulifikia geti alimpigia Pam.

Simu ya Pam iliita mara moja tu, akapokea: ?Yes dear, niambie mama.?

?Uko wapi Pam?? akasema Lilian akionekana kulia.

Kilio chake kilisikika kupitia simu aliyokuwa akizungumza na Pam.

?Una nini? Kuna msiba au??
 
SEHEMU YA 38 KATI YA 50

?Bora ingekuwa msiba.?

?Tatizo ni nini??

?Pam tuonane kwanza please!? akasema Lilian akizidisha kilio.

?Wewe una nini??

?Pam kwa nini hukusema mapema??

?Kusema nini??

?Pam umeniua Pam, umenipa ukimwi. Umeharibu ndoto zangu, umesababisha mpenzi wangu hanitaki tena. Kwa nini Pam? Kwa nini?? akasema Lilian akizidi kulia.

Pam akacheka sana!

?Unanicheka??

?Sikucheki bali unachekesha!? akasema Pam akizidi kukaukia kwenye simu.

Pam anacheka!

Lily analia!

Lilian alihisi dunia chungu, alitamani kuchimba shimo ili aingie humo, asionekane na mtu yeyote!

Hilo halikuwezekana!







KICHEKO! Vipi mtu acheke wakati amepewa taarifa mbaya! Jambo hilo kwa Lilian lilikuwa tatizo kubwa sana. Hisia zake zilivurugika hakika.

Alijiuliza maswali mengi sana bila kupata majibu ya moja kwa moja. Pam bado alikuwa hewani...

?Pam...? Lilian akaita.

?Nakusikia.?

?Una nini? Au unajua ulichokifanya??

?Huna jipya Lilian, nadhani jambo la msingi kama ulivyosema tuonane, nitajua cha kufanya.?

?Utajua cha kufanya??

?Ndiyo nitajua cha kufanya.?

?Unamaanisha nini??

?Namaanisha kuwa nitajua cha kufanya baada ya kuonana na wewe.?

?Saa ngapi??

?Leo jioni.?

?Sawa.?

Lilian alijihisi kuchanganyikiwa sana. Akachukua gari lililompeleka moja kwa moja chuoni. Aliposhuka, alitembea kwa kasi kulekea chumbani kwao. Bahati nzuri aliwakuta rafiki zake wote wapo.

Aliyekuwa na shida naye zaidi alikuwa ni Lucy....... akamvaa...







?Nataka uniambie ulikuwa na maana gani?? akasema Lilian akitetemeka kwa hasira huku machozi yakiendelea kuchuruzika machoni mwake.

?Manaa gani kivipi?? akauliza.?

?Hujui eeh??

?Ndiyo sijui.?

?Paaaaa...? kilikuwa kibao kilichotua shavuni mwa ..... barabara.

?Hivi wewe umechanganyikiwa? Kwanini unanipiga kiasi hicho??

?Ni kwa sababu wewe ni muuaji?? akasema Lilian kwa kujiamini.

?Muuaji??

?Ndiyo...wewe ni muuaji tena mkubwa sana.?

?Unasemaje wewe??

?Paaaaa...? kibao kingine kikatua tena.

Hakuweza kukubaliana na jambo hilo. Naye akarudisha, Lilian safari hii alicharuka, akarusha ngumu, mwenzake naye akarudisha.

Zikapigwa!

Leila na mwenzake hakukubaliana na ugomvi ule, tena mbele ya macho yao. Wakaingilia kati na kuamulia. Mpaka ugomvi unaisha, hakuna aliyekuwa tayari kueleza kisa cha ugomvi ule.

Hata hivyo aliyekuwa na jibu alikuwa ni Lilian pekee ambaye alikuwa amecharuka kuliko mbogo!

***

Kilikuwa kipindi ambacho Lilian alihitaji kukaa peke yake kuliko kipindi chochote katika maisha yake.

Kwa Lilian kuwa na ukimwi ni sawa na kukata tiketi ya kifo. Akili yake ilivurugika kabisa. Alijitahidi kuusaka usingizi lakini haikuwezekana.

Akili yake yote ilikuwa kwa Pam. Huyu ndiye aliyekuwa na majibu yake yote. Aliusubiria kwa hamu kubwa sana muda alioahidiana na Pam wakutane.

***

Pam alikuwa mwenye tabasamu muda wote, jambo ambalo lilimkasirisha sana Lilian lakini hakuwa na la kufanya. Pam ni kama alikuwa anajua alichotiwa...

?Lilian...? Pam akaita baabda ya kumuona Lilian akilia muda wote.

?Abeee...?

?Tatizo ni nini hebu kuwa serious??

?Lakini Pam kama ulikuwa unafahamu hali yako, kwanini ulinifuata na kufanya mapenzi na mimi?

?Umeniharibia kila kitu Pam, ndoto zangu za maisha zote zimeharibika. Ni kwa nini umenifanyia hivyo lakini?? akasema Lilian kwa sauti ya majuto lakini akionyesha heshima kwa Pam, akiwa na imani kuwa huenda akamsaidia.

?Ni kweli nimeathirika,? akasema Pam.

?Unasemaje??

?Ni kweli kanisa nimeathirika lakini halikuwa kusudi langu kukuambukiza na wewe. Hili si kosa lako. Kuna mwanamke mmoja ndiye amesababisha matatizo yote haya.

?Kumbuka mimi kuna wakati huwa na mawazo kupindukia, sina mfariji yeyote ndiyo maana nikaona uwe wangu ili unipe raha. Lakini hata hivyo ukimwi siyo ishu kubwa kama unavyofikiria.

?Mimi naishi na ugonjwa huu, baada ya muda huwa nakwenda Afrika Kusini kubadisha damu. Hakuna kinachoshindikana. Angalia mpaka sasa naishi kwa amani kabisa.
 
SEHEMU YA 39 KATI YA 50

?Nitakupeleka na wewe huko ukabadilishe damu. Haya mambo hayana nguvu mbele ya fedha. Sawa mama??

?Paaaa...? Lilin aliinuka haraka sana, kisha akamshushia kibao kizito sana.

Eneo hilo halikuwa na maana tena kwake.

Aliinuka muda uleule kisha akaondoka zake.

?Ahsate sana, nashukuru sana Pam!? akasema Lilian wakati akiondoka zake.

Pam alijitahidi sana kumuita ili arudi wazungumze, lakini hilo halikuwezekana. Lilian alikuwa na maumivu ambayo hakuwahi kuyapata kabisa moyoni mwake.

***

Maisha ya Lilian yalibadilika, hakuw na uchangamfu kama aliokuwa nao awali. Akajikuta anakuwa mtu wa kukosea kila kitu kila wakati.

Masomo kwake yalikuwa magumu sana. Akiwa hana hili wale lile, akiwa amepoteza matumaini kabisa, siku moja akiwa amejifungia chumbani kwao, wenzake wakiwa wameingia kwenye kipindi, alisikia simu yake ikiita.

Alipotupa macho yake kwenye kioo cha simu yake, akagundua kuwa aliyekuwa akimpigia alikuwa ni Edo. Akastuka sana. Mapigo ya moyo wake yalibadilika. Mara moja akapokea...

?Lilian...? akaita Edo.

?Unasemaje Edo? Tafadhali naomba uniache na matatizo yangu, maumivu niliyonayo yananitosha...? akasema Lilian.

?Hapana nina jambo jipya kabisa la kukuambia.?

?Jambo jipya??

?Ndiyo nina jambo jipya.?

?Jambo gani?? akasema Lilian akionekana kuwa na hamu ya kusikia jambo hilo kutoka kwa Edo.

?Nimekusamehe Lilian!? akasema Edo.

?Unasemaje Edo??

?Nimekusamehe!?

Lilian alibaki kama aliyechanganyikiwa kabisa! Hakujua la kufanya.





DIRA ya maisha ya Lilian ilibadilika kabisa. Kama ni basi, lilikuwa limegeza uelekeo. Ni kama liligeukia upande lilipotokea.

Alijiona asiye na thamani tena. Kujitunza kote katika maisha yake hapakuwa na maana tena. Lilikuwa tendo la siku moja tu, mara moja tu, lililogharimu maisha yake yote.

Rafiki zake akina L, aliwaona kama nuksi katika maisha yake. Aliyemchukia zaidi alikuwa ni Lucy. Kampani yake yote ya Lucy, Latifa na Leila aliichukia kabisa.

Pamoja na yote hayo, simu ya Edo aliyekuwa akizungumza naye, ambaye alimwambia alimsamehe, ilimshangaza na kumshtua. Zilikuwa habari mpya kwake. Pengine ni habari njema lakini zisizo na uthibitisho.

Hajui kilichopo moyoni mwa Edo.

?Edo ananichora au ni mkweli?? akawaza.

Edo anisamahe mimi? Akawaza tena. Ulikuwa wakati wa kuwaza na kuwazua. Wakati wa kujiuliza maswali na kujijibu mwenyewe.

?Edo...? Lilian akaita simuni.

?Yes darling...? (Ndiyo mpenzi) akaitikia Edo.

?What?? (Nini?) akang?aka Lilian.

Kuitwa mpenzi lilikuwa jambo jingine jipya na la kushangaza hasa.

?What?s wrong with you my dear?? (Una tatizo gani mpenzi?) akauliza Edo kwa kimombo.

?You calling me darling again??

(Unaniita mpenzi kwa mara nyingine?) akaualiza Lilian.

?Kwani kuna tatizo gani?? akauliza Edo.

?No!? (Hapana) akajibu Lilian.

?Why not?? (Kwanini hapana?)

?Kwa hakika sifai tena kuwa na wewe, niache nife na ukimwi wangu. Niache nife peke yangu...? akasema Lilian, tayari machozi yalianza kumwagika machoni mwake.

?Inawezekana unachowaza ni sahihi lakini pia si ajabu ikawa si sahihi. Naomba nikutane na wewe tuzungumze.?

?Kukutana na mimi??

?Ndiyo.?

?Lini??

?Leo.?

?Saa ngapi??

?Muda wowote jioni. Hebu panga wewe.?

?Sawa...saa moja usiku vipi??

?Ni sawa tu, wapi??

?Kwa sababu umechagua muda, pendekeza na eneo pia mpenzi.?

?Pendekeza wewe.?

?Mh!? akaguna Edo.

Kimya cha muda kikapita, baadaye Edo akaanza kuzungumza simuni: ?Acha nitajua mwenyewe. Cha msingi, saa moja juu ya alama uwe tayari, nitakuwa hapo chuoni.?

?Sawa.?

?Zingatia muda tafadhali.?

?Nimekuelewa Edo.?

Wakakata simu zao.

***

Hakuna jambo gumu kama kulazimisha furaha, lakini Lilian alilazimisha furaha. Kichwani mwake, alihisi ameshafika mwisho wa maisha yake.
 
SEHEMU YA 40 KATI YA 50

Hakuwa na elimu sahihi juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi. Hakujua tofauti ya virusi vya ukimwi na shambulio la ukimwi. Kifupi hakujua lolote kuhusu ugonjwa huo.

Alichojua yeye, ukimwi ni kifo. Alijua hilo tu. Alichofundishwa ni kwamba ukimwi unaua. Hakuwa na kitu kingine kichwani mwake. Kugundulika kuwa virusi hivyo vilikuwa vinaishi ndani ya damu yake, kuliharibu kila kitu.

Mazungumzo yake na Edo kidogo yalimpa faraja, aliamini kama mpenzi wake, mtu ambaye alimwamini, kumheshimu na kumpenda, mtu ambaye ndiye pekee aliyejua siri ya ugonjwa wake, yupo pamoja naye na anahitaji kukutana naye, kidogo angepunguza uzito wa mzigo aliokuwa nao moyoni mwake.

Furaha ya kutengeneza ikaonekana. Alisubiri kwa hamu sana muda wa kutoka na Edo ufike. Ni kweli muda ulikwenda taratibu sana. Sana. Sana.

Lakini hata hivyo, saa 12 jioni ilifika. Muda ambao alitakiwa kuanza kujiandaa. Hakutumia muda mwingi sana. Ajipambe kwa lipi? Ajirembe kwa sababu gani? Alichokifanya ni kuingia bafuni, akaoga haraka na kutoka. Alivaa simpo tu. Suruali ya jeans nyeusi na blauzi nyekundu. Akajifunga kilemba kichwani, kisha mkoba wa rangi ya bluu ya kung?aa.

Tayari mshale wa saa ulikuwa umegota kwenye 6, wa dakika ukiwa kwenye 23, wa sekunde ukiendelea kutembea. Zilibaki dakika 37 tu kufikia muda wa miadi.

Akayazuia machozi yake kwa nguvu. Akaficha hisia zake za maumivu. Kwa kuhofia kujiumiza sana moyo wake na fikra za mateso zilizojaa majuto, muda huo akaamua kuutumia kusoma kitabu.

Akafungua kabati dogo, kisha akachukua kitabu cha nguli wa riwaya Afrika Mashariki, Ben Mtobwa. Kiliitwa Roho ya Paka. Alishakisoma mara nyingi sana, hakuona tabu kukirudia. Akafungua ukurasa wa kwanza kabisa wa hadithi ilipoanzia, akaanza kusoma tena.

?Ilikuwa ghafla, kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini na kuujeruhi moyo wa Inspekta Kombora. Kati ya yote aliyoyatarajia jioni ya leo, simu kama hiyo, ya maafa, haikuwamo kabisa akilini mwake. Kwa jumla, ilikuwa kama iliyopigwa muda huu kwa ajili ya kumsimanga au kumdhihaki....?

Ndivyo macho yake yalivyoanza kutembea juu ya maandishi ya kitabu cha gwiji huyo. Akaendelea kusoma zaidi. Kama utani, Ben Mtobwa akafanikiwa kumteka Lilian.

Sekunde moja tu ilisababisha asahau mzigo wa mawazo uliokuwa kichwani mwake.

Akazama katika hadithi hiyo ya kusisimua....

***

Mlio wa simu ulimgutusha. Akapuuza. Mawazo yake yalikuwa kwenye kitabu. Ikaita tena kwa mara nyingine, kichovu sana, akachukua simu yake na kuangalia mpigaji!

Akashtuka!

Alikuwa ni Edo!

Tayari alikuwa ameshasahau kabisa kuwa alikuwa na miadi na Edo. Mara moja akabonyeza kitufe cha kijani kuruhusu simu, kisha akaipeleka sikioni.

?Nimeshafika mpenzi, bila shaka upo tayari,? akasema Edo.

Lilian akachanganywa tena na neno ?mpenzi?. Lakini hakuwa na la kufanya, akajibu kichovu: ?Ndiyo, nipo tayari tangu nusu saa iliyopita.?

?Sawa njoo basi twende.?

?Nakuja.?

Lilian alipoyatupa macho yake kwenye saa iliyokuwa ukutani, akagungua kuwa tayari ilikuwa saa 1:18 usiku. Akarudisha kitabu kabatini, akatoka nje.

?Edo ana habari gani mpya?? akawaza akimfuata.


UZURI wa Lilian bado uliendelea kuonekana kwa nje lakini ndani yake hakuwa msichana mrembo tena. Alitembea kivivu, bila mpangilio kama zamani. Alijitoa thamani kabisa.

Mikogo yote ilikaa pembeni, ndani ya moyo wake kulijaa majuto. Hakuchukua muda mrefu tayari alikuwa ameshafika barabarani ambapo Edo alikuwa ameegesha gari lake.

Edo alipotupa macho yake na kumuona Lilian akimfuata, alijawa na huzuni moyoni. Alimuona Lily hana furaha kabisa. Lilian alionyesha wazi kilichokuwa ndani yake.

Alikuwa kwenye majuto makubwa. Lilian alikuwa mpya kabisa. Mpya kwa kila kitu. Taratibu alivuta mlango wa siti za nyuma, ukafunguka. Akaingia.
 
SEHEMU YA 41 KATI YA 50

?Habari yako Edo??

?Poa.?

?Mbona huna furaha??

?Nipo sawa Edo.?

Edo hakuzungumza kitu, aliangalia pembeni, nje kupitia dirisha la upande wa kushoto ambao alikuwa amekaa, aliporudisha macho yake ndani, akakutanisha macho na dereva wa gari lile.

?Twende kaka,? akasema Edo.

Gari likawashwa, likaanza kuondoka.

?Lakini huna sababu ya kuwa na mawazo kiasi hicho mpenzi.?

?Sifurahishwi na namna ninavyokuona. Natamani kuona tabasamu lako tena. Kwa nini unakuwa hivi?? akauliza Edo.

?Edo, unajua kila kitu. Unafahamu kuhusu malengo yetu, unajua kuhusu makubaliano yetu. Sasa angalia...kila kitu kimebadilika. Kila kitu kimeharibika. Nawezaje kufanya chochote tena Edo?

?Kumbuka mimi sina thamani tena kwako, siyo kwako tu sina thamani kwa mwanaume yeyote kwa sasa. Maisha yangu yamebadilika kabisa,? akasema Lilian kwa sauti iliyojaa uchungu moyoni.

?Hapana, usiseme hivyo. Ungekuwa huna thamani kwangu, nisingekuwa na wewe muda huu. Ni kwa sababu una thamani ndiyo maana uko na mimi muda huu,? akasema Edo kwa sauti tulivu.

?Unachokifanya sasa ni kunipa moyo tu. Hilo baasi. Siyo zaidi ya hivyo,? akasema Lilian.

?Nikuombe kitu?? akauliza Edo.

?Ndiyo.?

?Tusizungumze chochote muda huu mpaka tufike tunapokwenda, sawa??

?Sawa,? akajibu.

Hapakuwa na mazungumzo zaidi. Gari lilishika njia hadi kwenye mzunguko wa Mlimani City, kwenye makutano ya Barabara ya Ardhi na Sam Nujoma. Dereva akakata kushoto kuifuata Barabara ya Sam Nujoma kuelekea Mwenge.

Dakika moja tu baadaye, tayari walikuwa kwenye mataa ya Mwenge, zilipokutana Barabara za Sam Nujoma, Ali Hassan Mwinyi, Bagamoyo na ile ya Coca Cola.

Taa ya kijani ilipowaka, dereva akanyoosha kuifuata Barabara ya Coca Cola. Mbele kidogo kabla ya kukifikia kiwanda cha soda alikata kulia na kupitia jirani kabisa na salon maarufu ya Naznat.

Wote walikuwa kimya kabisa, wakafika kwenye Barabara ya Mwai Kibaki, jirani kabisa na Clouds Media. Wakaishika barabara hiyo, ambapo mbele kidogo, mkono wa kulia, dereva alikata na kuegesha.

?Jack?s Pub...? Lilian alisoma maandishi kwenye bango dogo barabarani wakati dereva akikata kuelekea kwenye Pub hiyo.

?Kumbe tulikuwa tunakuja hapa?? Lilian akauliza.

?Ndiyo...hujapenda??

?Pazuri, haina shida.?

Wakashuka garini na kuelekea kwenye meza iliyokuwa na viti viwili tu. Ilionekana wazi meza za namna hiyo zilitengwa maalum kwa ajili ya wapenzi au watu wawili pekee waliokuwa na mazungumzo ya siri.

Yule dereva alikaa sehemu nyingine. Muda mfupi baada ya kukaa, alifika mhudumu na kuwasikiliza.

?Juisi ya embe ipo?? akauliza Edo.

?Ipo ya maembe peke yake, kuna nyingine imechanganywa na maziwa na nanasi. Utapenda ipi??

?Embe pekee, glasi mbili tafadhali.?

?Sawa bosi,? akaitikia yule mhudumu.

?Sikia Lilian...nimekuita hapa ili kuzungumza na wewe. Najua ni kiasi gani una maumivu, lakini lazima tuzungumze. Nimegundua jambo moja muhimu,?alianza kuzungumza Edo akimwangalia Lilian usoni.

?Kwa sasa uko kwenye majuto. Najua una maumivu na unahitaji mtu wa kukupa faraja. Nina uhakika, mwanaume uliyetoka naye, hawezi kukupa faraja. Bado mimi ni wako na ninakupenda,? akasema Edo.

Lilian akaanza kulia.

?Stop crying please!? (Acha kulia tafadhali)

?Niache nilie Edo.?

?Hapana. Unakosea. Nini kinachokuliza? Hakuna unachoweza kubadilisha...? akasema Edo, kisha akakatisha baada ya kumuona mhudumu akifika mezani kwao.

?Tutayarishie makange ya kuku na ugali dona tafadhali,? akasema Edo.

?Sahani mbili??

?Ndiyo.?

Edo akaendelea: ?Mimi ndiye wa kukupa faraja. Nimeshakuambia...nimekusamehe kutoka moyoni. Bado nipo na wewe. Hata kama haitakuwa kimapenzi tena, lakini sitakubali kuona furaha yako inaondoka kwa sababu yangu.

?Mimi ni wako, wewe ni wangu. Naomba uwe na amani na uendelee na masomo vizuri. Wiki ijayo narudi Malaysia. Tafadhali nataka nikuache ukiwa na amani. Acha kujifikiria peke yako. Hata mimi nina maumivu makali. Nami pia naumia. Ndiyo maana nataka kuwa sawa na wewe.?

Lilian akainuka!

Edo naye akasimama.

Lilian akazunguka upande wa pili aliokuwa amekaa Edo.
 
SEHEMU YA 42 KATI YA 50

Akamsogelea, wakakumbatiana.

?Ahsante kwa msamaha wako, nimekuelewa. Itakuwa hivyo Edo,? akasema Lilian.

?Unaniahidi??

?Nakuahidi Edo.?

Baadaye kidogo chakula kilifika mezani, wakaanza kula huku wakizungumza. Walishasahau kabisa machozi na huzuni walizokuwa nazo muda mfupi uliopita.

***

Edo alirudi Malaysia. Kwa taabu Lilian aliweza kufuatilia masomo yake kwa miezi miwili ya mwazo. Baadaye hakuweza tena. Kila alipokumbuka kuwa anaishi na VVU, alihisi akili yake ikimruka.

?Sitaweza kuendelea na masomo kwa staili hii. Nitachekwa nikifeli. Ni afadhali nipumzike kwa muda kwanza,? akawaza Lilian.

Uamuzi alioufikia ulikuwa ni kuandika barua ya kuomba kuhairisha mwaka wa masomo hadi mwaka uliofuata. Katika barua yake, alieleza sababu mbalimbali za kutunga, uongozi wa chuo ukakubaliana naye.

?Sitakwenda nyumbani, nitakuwa hapahapa Dar,? alijisemea Lilian akiwa kitandani, akisoma barua ya majibu aliyopewa na uongozi wa chuo ambao ulikubaliana na maombi yake.







SONONEKO lilijaa moyoni mwa Lilian, aliingia katika historia mpya kabisa ambayo katu hakuitegemea kama angeipitia. Kichwa chake kilikuwa kizito sana. Hakuwa na uwezo wa kufanya chochote tena.

Aliamini kuhairisha mwaka mmoja wa masomo, pengine kungeweza kuwa dawa. Alijihisi mzito kuliko kawaida. Kwa uchovu mkuu, woga moyoni na hofu isiyo na kifani, aliburuza begi lake akatokea kwenye lango kuu la hosteli yao.

Alikuwa na mawazo mengi sana. Bado aliendelea kufikiria kukaa Dar es Salaam. Isingekuwa rahisi kwake kwenda nyumbani kwao ambapo angekutana na maswali mengi ambayo asingekuwa na majibu yake.

?Siwezi kwenda nyumbani kabisa, siwezi,? aliwaza.

Mawazo yake yalikuwa sahihi kwa hakika. Isingekuwa rahisi kwake kwenda nyumbani kwao. Akawaambie nini? Hakuwa na la kusema.

Bado aliwaza: ?Sawa, nitakaa hapa Dar, nitakaa kwa nani??

Mawazo hayo ndiyo yaliyosababisha safari yake ya kwenda kusipojulikana iishie katika Bar ya Udasa pale chuoni ambapo kwa kutuliza kichwa chake, akaagiza mvinyo mweupe na kuanza kunywa!

Pengine kweli bwana, huenda pombe huwa inasaidia kwa kiasi fulani hivi....mara akili yake ikafunguka...mawazo yake yakamtuma kwenye kitu kipya kabisa ambacho kwake aliona ahueni kubwa. Alimkumbuka shangazi yake, Juliana!

?Nitakwenda kwa anti. Bora niende kwake.?

Wazo hilo lilipita moja kwa moja. Akajiinua kitini na kuchukua begi lake la magurudumu kisha akaanza kulikokota!

Alipofika nje ya baa hiyo, alivuka barabara na kusimama kituoni, upande wa pili. Mara daladala likitokea Makumbusho kuelekea Ubungo likasimama mbele yake. Akajipakia na kwenda kukaa siti ya nyuma kabisa. Mawazo tele kichwani mwake.

?Maisha haya mpaka lini?? akawaza.

Alishuka Ubungo na kupanda daladala la Gongo la Mboto, hapo angetafuta usafiri wa kwenda kwa shangazi yake Juliana, Pugu ? Kajiungeni.

***

Alikuwa na umri wa miaka 29. Binti mbichi kabisa, akiwa mtoto wa mwisho kuzaliwa katika uzao wa babu yake na Lilian. Ni shangazi yake, lakini alikuwa na umri unaokaribiana kabisa na wake.

Wote walikuwa wadada wa kadiri. Juliana alipomaliza masomo yake ya kidato cha sita, Shule ya Sekondari Mkwawa, Iringa alikwenda kusoma uhasibu katika Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha (Institute of Accountancy Arusha ? AII) kilichopo jijini Arusha. Alipohitimu, kwa bahati nzuri akafanikiwa kupata kazi katika Kampuni ya Think Big Production ya jijini Dar es Salaam. Kwa uwezo wake kazini, miaka mitatu tu ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, aliteuliwa kuwa mhasibu mkuu.

Akahama Tabata alipokuwa akiishi awali na kupewa nyumba ya ofisi, Pugu ? Kajiungeni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa kuzingatia shida ya usafiri, Juliana alipewa gari na ofisi yake ili limsaidie kumwahisha ofisini.

Alifanya kazi kwa juhudi sana. Akawa na heshima kubwa kwenye kampuni hiyo iliyokuwa na ofisi zake Barabara ya Nyerere, mbele kidogo ya Tazara jijini Dar es Salaam.

Aliishi na msichana wake wa kazi katika nyumba hiyo kubwa. Aliitwa Neema.

***
 
SEHEMU YA 43 KATI YA 50

Ilikuwa Jumamosi, moja kati ya siku zake mbili za mapumziko ya mwisho wa juma. Juliana hupumzika Jumamosi na Jumapili. Akiwa hana hili wala lile, alisikia kengele ikipigwa kutokea geti kubwa la kuingilia nyumbani kwake.

Neema aliamka haraka na kwenda kufungua. Lilian akaingia. Juliana alishangaa sana, maana si tu hakuwa na taarifa ya ugeni wake, bali hawakuwasiliana kwa simu kwa zaidi ya miezi miwili.

?Karibu, mwenzetu mbona kimyakimya?? Juliana alisema wakati akimpokea Lilian.

?Ahsante anti, we acha tu, tutazungumza.?

?Kuna tatizo?? Juliana aliuliza.

Alikuwa na kila sababu ya kuuliza kutokana na namna Lilian alivyoonekana usoni. Ni wazi alikuwa na jambo zito lililokuwa likimsumbua.

?Tupo anti, usijali tutazungumza tu.? Begi lake likapelekwa ndani, Lilian akafikia kwenye bustani nzuri, nje ya nyumba hiyo. Ni hapo walikuwa wamepumzika Juliana na Neema. Walikuwa kama mtu na ndugu yake ? Juliana mwenyewe hakupenda kabisa ijulikane kuwa, Neema alikuwa msichana wake wa kazi.

Alimpenda sana kwa bidii yake ya kazi.

***

?Haya niambie anti yangu, kuna tatizo gani?? Juliana alimwuliza akiwa na hakika kabisa kuwa Lilian alikuwa na tatizo lililomsumbua.

?Nimeahirisha mwaka wa masomo anti, nakuomba sana...sitaki kwenda nyumbani. Naomba nipumzike hapa kwako kwa mwaka mmoja, mpaka nitakaporejea chuoni,? akasema Lilian.

?Ni sawa, lakini kuna nini? Nini kimekufanya uhairishe masomo??

?Anti ngoja niwe mkweli kwako. Wewe ni zaidi ya shangazi kwangu. Wewe ni rafiki yangu na ninategemea utakuwa msiri wangu.?

?Sawa, niambie una nini??

?Anti tatizo ni mapenzi. Kuna mtu amenivuruga sana kichwa changu,? akadanganya Lilian.

Alizungumza ukweli kiasi, maana ni kweli mapenzi ndiyo yaliyomtibua, lakini kuna alichoacha!

?Mh! Nilijua tu,? akasema Juliana akitabasamu.

?Lakini ni ujinga kuyapa nafasi mapenzi katika maisha yako, kiasi cha kuhairisha masomo. Uamuzi wako nadhani haupo sawa na sidhani kama jambo hilo linaniingia akilini,? akasema Juliana kwa sauti yake ya taratibu lakini ikionekana wazi kuwa na hasira kidogo ndani yake.

Lilian akachanganyikiwa!

Kulikuwa na dalili zote za kufukuzwa na shangazi yake. Moyoni, aliapa kabisa kutomwambia siri iliyosababisha afikie uamuzi huo. Alitaka kuifanya siri yake ya moyoni.

Juliana hakujua kilichokuwa ndani ya moyo wa shangazi yake. Alichukulia suala lake kama uzembe tu wa fikra katika uhusiano. Laiti angeingia moyoni mwake na kujua siri aliyokuwa nayo!

Angejua!!!









SIRI ilitulia ndani ya moyo wa Lilian. Aliificha ndani ya kifua chake na hakuwa tayari hata kidogo kufungua kinywa chake kueleza ukweli.

Alijua ni kwa namna gani angejizidishia mateso ya kihisia ndani ya moyo wake. Alibaki kuwa mwenye mawazo lakini akijiapiza kufa na siri hiyo moyoni mwake.

?Anti,? akaita Lilian.

?Unasemaje? Una nini kipya cha kuniambia?? sasa Juliana alionekana dhahiri kuwa na hasira isiyo na kifani.

?Usinifanyie hivyo anti.?

?Ni kitu gani nisichokijua kuhusu mapenzi? Kipi kigeni kwangu kuhusu uhusiano? Najua kila kitu, ndiyo maana nakushangaa, eti unakuwa tayari kuhairisha mwaka wako wa masomo kwa sababu kuna mpumbavu tu amekuvuruga.

?Sikia... wewe una maisha yako, yeye naye ana maisha yake. Si mume wako huyo. Ingekuwa mmeoana, labda ungepaswa kuumia lakini boyfriend tu. Hebu get serious bwana. Sitaki kusikia upuuzi wako hapa,? akasema tena anti yake kwa hasira ileile.

Lilian akamwaga machozi!

Ilikuwa ni haki yake kulia. Afanye nini sasa? Amwambie ukweli? Nani kasema?

?Siwezi kusema, itakuwa tatizo mara mbili ya hivi, lazima nitumie akili zaidi,? akawaza Lilian.

Juliana alijaribu kuzungumza kama mzazi, akichukua nafasi ya kaka yake, kumshauri Lilian akiwa hajui kabisa kuwa nguvu aliyokuwa akiitumia ilikuwa siyo mahali pake. Hilo hakulijua kabisa.

?Nina ombi moja kwako anti.?
 
SEHEMU YA 44 KATI YA 50

?Ndiyo.?

?Naomba nikae hapa kwa wiki mbili tu nikitafakari, kisha nitakujibu cha kufanya.?

Juliana alikaa kimya kwa muda.

Alionekana amezama kwenye tafakuri ya muda akimfikiria shangazi yake. Kidogo ombi lile lilionekana kumwingia.

?Na ninataka iwe wiki mbili kweli. Sikia... sina tatizo lolote kwa wewe kuishi hapa kwangu. Nina nyumba kubwa, kuna kila kitu ndani. Utakula, utalala, utavaa na kufanya kila kitu. Kwa hiki Mungu alichonijalia, sina tatizo kabisa ndugu zangu wakikitumia.

?Lakini kumbuka, naumizwa na uamuzi wako. Sitaki kuona mapenzi yanaharibu maisha yako. Umeshapita vizingiti vingi Lilian. Kwa nini uje kuharibu mwishoni??

?Nakuelewa anti, najua ni kwa kiasi gani unaumia, nisamehe tafadhali.?

?Yamekwisha.?

?Ahsante shangazi,? akajibu Lilian alijitahidi kuachia tabasamu usoni mwake.

Tabasamu lilikuwa zito lakini kwa sababu ya vijishimo mashavuni mwake, liliweza kuonekana sawasawa.

***

Kutokana na upweke mara nyingi alipenda kwenda kushinda kwenye saluni ya kike iliyokuwa jirani na nyumbani kwa shangazi yake. Alipenda kwenda pale kwa sababu ya ucheshi wa dada aliyekuwa akihudumia katika saluni hiyo.

Aliitwa Maimuna lakini rafiki zake walimkatishia na kumwita Mai. Alikuwa msichana mrembo kwelikweli. Mwenye kila kitu kizuri mwilini mwake. Nyama za mwili wake zilikuwa zimeshikana vyema.

Alikuwa mrefu kiasi, mwenye shepu sawasawa, umbo likionekana kufanana kabisa na tarakimu namba nane. Alikuwa na makalio makubwa. Hipsi pana, miguu minene, mizuri na kiuno chembamba kama cha nyigu!

Kifupi alikuwa mrembo kupitiliza. Pamoja na urembo wake, hakuwahi kuonekana akiwa karibu na wanaume. Wanaume wengi mtaani walimmezea mate. Wenye roho za kupenda haraka, walijaribu kutupa ndoano zao, wakaambulia patupu!

Mai alikuwa na msimamo sana!

Urafiki wake na Mai ulishamiri kwa wiki moja tu. Lakini Mai hakufurahishwa na ukimya kupitiliza wa shoga yake. Kwa alivyomuona, haraka sana aligundua alikuwa kwenye tatizo kubwa ambalo hakutaka kumshirikisha mtu.

Leo hii hayupo tayari kumuona shoga yake akiendelea kuwa mwenye mawazo wakati yeye yupo. Wakiwa wawili tu saluni, mchana huu. Mai ameamua kuvunja ukimya.

?Lilian...? akaita Mai.

?Abee...?

?Mimi ni rafiki yako siyo??

?Ndiyo.?

?Tunaaminiana siyo??

?Hakika.?

?Kwa ninavyokuona, naona una mzigo wa mawazo. Kuna kitu kinakusumbua na kinakutesa, lakini kwa bahati mbaya, inaonekana huna mpango wa kumweleza mtu yeyote jambo hilo.

?Sidhani kama uamuzi huo ni sahihi. Acha kujikondesha mtoto wa kike. Mimi ni shoga?ko kama ulivyosema na umesema unaniamini, nakuamini pia. So please, tell me, what?s wrong with you my dear?? akasema Mai kwa sauti tulivu, yenye kusihi na ushawishi wa hali ya juu.

Kama Mai angesomea masomo ya saikolojia, bila ya shaka angeifanya kazi hiyo kwa ubora wa hali ya juu sana. Aliweza kuwa mshauri mzuri.

?Mbona hakuna tatizo? Nipo sawa kabisa Mai, I?m absolutely okay, nothing wrong with me... please be happy my sister,? akasema Lilian akitengeneza tabasamu ambalo Mai aliligundua haraka kuwa halikuwa halisi.

?Your smile is not real Lilian. Tafadhali niambie, unasumbuliwa na nini? Nipo hapa kwa ajili yako,? akasema Mai kwa sauti tulivu.

?Let me tell you the truth... it?s true that a have a big problem. Angalia....? akasema Lilian machozi yakimlenga, huku akijionyesha mwili wake kwa Mai.

?I?m HIV Positive.... you think what is next to me? I?m finished Mai. I?m nothing....? (Nina virusi vya ukimwi... unafikiri nini kinafuata? Nimekwisha Mai. Mimi si lolote...).

?Hapana... pole sana kwa kusumbuliwa na tatizo kubwa kihisia lakini lisilo kubwa kinadharia. Tuliza moyo. Ishu yako ni ndogo sana...? akasema Mai.

?Unamaanisha nini? Kuwa na ukimwi ni tatizo dogo??
 
SEHEMU YA 45 KATI YA 50

?Matatizo ni matatizo tu Lilian, ila ukimwi umepewa sifa ya kuwa tatizo kubwa, lakini si kweli. Ngoja... nitakuambia ukweli leo na nitakusaidia uishi maisha safi. Subiri kidogo,? akasema Mai akifuata pochi yake.

Aliporejea, alikuwa na simu. Akaonekana akitafuta kitu katika simu yake, kisha akamkabidhi Lilian. Juu ya kioo cha simu hiyo, kulikuwa na mwanaume mtu mzima, amesimama kando ya gari la kifahari.

?Ni nani huyu? Na kwa nini umenionyesha hii picha?? akauliza Lilian.

?Huyu ni Sadick Kisummi. Ni marehemu kwa sasa. Amefariki miaka nane iliyopita. Mwaka mmoja baadaye, alifuata mkewe. Alikuwa mpenzi wangu. Huyu ndiye chanzo cha matatizo yangu. Ndiyo sababu mpaka sasa sihitaji kuolewa.

?Mzee Kisummi alinipa ukimwi. Hivi ninavyozungumza na wewe, ninaishi na virusi vya ukimwi takribani miaka kumi sasa. Awali niliogopa kama wewe, niliishi kwa mawazo na mashaka kama wewe, lakini kumbe nilikuwa najiumiza tu. Yupo sista anaweza kukusaidia.

?Utaishi kwa amani na utarudi kwenye masomo yako kama kawaida. Kifupi utakuwa Lilian mpya, pengine mwenye furaha zaidi kuliko Lilian ninayezungumza naye sasa hivi hapa.?

?Kweli??

?Kabisa.?

Lilian akatabasamu!

Mwanga wa maisha mapya ukafunguka. Alimwamini sana Mai. Alimsogelea na kumvutia kwake. Wakakumbatiana.

Machozi hayakuwa hiyari yake tena, yakamwagika kama maji! Mashavu yake yakawa tepetepe!







?USILIE mpenzi, tafadhali usilie. Unatakiwa kujipa moyo?angalia, huu ni mwanzo mzuri kwako. Mwanzo mwema wenye matumaini makubwa,? akasema Mai akiwa bado yu kifuani mwa Lilian.

?Ni kweli usemayo, na ndivyo nifanyavyo sasa. Machozi haya si ya huzuni tena Mai rafiki yangu. Umenifumbua macho. Naona kila kitu kwa upya kabisa mbele yangu. Usijali.?

?Tulia...tena naona, hebu twende nyumbani sasa hivi,? akasema Mai.

?Nyumbani??

?Ndiyo. Nyumbani kwangu.?

?Ofisi??

?Nitafunga. Kwanza, nani wa kuniuliza? Ni salon yangu mwenyewe.?

?Najua...lakini wapo wa kukuuliza, wapo mabosi wako.?

?Bosi wa hapa ni mimi.?

?Si kweli. Wateja wako ndiyo mabosi wako. Vipi wakija wakukose? Sioni kama ni busara. Huu ni mwanzo mzuri kwetu, lakini kamwe usiharibu kazi.?

Lilian alizungumza kwa sauti ya taratibu iliyojaa ushawishi. Kwa hakika alionekana kuzungumza mambo ya msingi ambayo yalimwingia Mai kwa kiasi kikubwa sana.

?Ahsante kwa ushauri. Nimekuelewa shoga yangu,? akasema Mai.

?Poa, ngoja nijirudishe nyumbani, baadaye nitakutafuta ukimaliza kazi.?

?Sawa.?

Lilian akaaga.

Akaondoka zake.

***

Lilian alikuwa na mabadiliko makubwa sana katika maisha yake. Ushauri wa Mai ulikuwa na nguvu kama aliyeshauriwa na mtaalamu wa masuala ya ushauri mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka kumi!

Haikuwa hivyo!

Lilian alimwelewa kwa haraka Mai kutokana na mfano halisi na wa wazi kutoka kwake. Kitendo cha kumhakikishia kuwa, hata yeye alikuwa akiishi na virusi hivyo kulimpa faraja kubwa sana moyoni mwake.

Kwake, ukimwi ukawa si tatizo kubwa sana. Kichwani mwake aliwaza jambo moja tu; kuzungumza na shangazi yake Juliana.

?Atanielewa kweli?? akawaza.

?Lakini ndiyo ukweli. Kwa nini nisimwambie wakati huu ambao nina hakika kuwa, sina mashaka tena? Lazima nimshirikishe,? akajijibu mwenyewe.

Hata hivyo, akili yake ilikwenda mbali zaidi, akafikiri mambo mengine makubwa zaidi. Aliamini, pengine kwa kumwambia ukweli, angeweza kumnyanyapaa na kumkatisha tamaa.

Aliwaza pengine asingempa ushirikiano na angewatangazia ndugu zake wote kuwa amepata ugonjwa huo. Alikwenda mbali zaidi, akaamini kuwa, pengine wangefikiri kuwa, amepata ugonjwa huo kutokana na tabia zake mbaya.
 
SEHEMU YA 46 KATI YA 50
?No! Sina sababu ya kumweleza, na si yeye tu, sitamwambia mtu mwingine yeyote,? akawaza mwenyewe kichwani mwake.

Wazo hilo akalipitisha moja kwa moja. Likamwingia kichwani na kulikubali.

Alichokuwa akisubiri kwa hamu ni siku ya kukutana na mshauri aliyemsaidia shoga yake, Mai! Haikuwa mbali sana ? ni Jumamosi tu! Siku mbili baadaye!

***

Kilikuwa chumba kidogo, kizuri na kilichopangiliwa vitu vizuri. Rangi ya parachichi iliifanya ofisi ile kuwa yenye kuvutia sana. Samani zake pia zilikuwa nadhifu.

Nyuma ya kiti kikubwa cha kuzunguka, alikaa dada mrembo, aliyekuwa amevaa miwani myeupe yenye fremu nyeusi. Vijishimo mashavuni vinaongeza urembo wa michana huyu.

Nyusi zilizojaa juu ya macho yake, zikiwa hazijawekwa kikorombwezo chochote, zinaongeza idadi ya maksi ya uzuri wa mwanamke huyu wa makamo.

Waweza kumuita mdada, lakini hata ukimuita mama hutakuwa umekosea sana, maana tayari ni mama wa watoto wawili. Ana umri wa miaka 32 tu, na bado amejitunza vyema na kuendelea kuwababaisha wanaume wakware wa mjini wanaopenda vya mteremko!

Kwa huyu si wa mteremko!

Ni dada mwenye heshima zake. Msomi, aliyeshiba taaluma ya ushauri wa saikolojia ya maisha. Kwa sasa amebobea katika ushauri nasaha, utafiti na upimaji wa magonjwa ya ngono na ukimwi.

Yes! Aliitwa Sista Isabela!

Mbele ya meza yake kubwa, ikiwa na mafaili machache mezani, walikaa wadada wawili ? wazuri kama yeye! Ni Mai na Lilian.

Baada ya salamu na utambulisho, Mai alimweleza kila Sista Isabela kuhusu hali ya Lilian na hofu aliyokuwa nayo. Sista Isabela akatabasamu.

?Nashukuru sana Mai kwa kunisaidia kazi. Ninavyokuamini, najua nina kazi ndogo sana kwa Lilian,? akasema akitabasamu zaidi na kuufanya uzuri wake utamalaki maradufu.

?Ni kweli kabisa,? akasema Lilian.

?Utapenda kwenye mazungumzo yetu Mai awepo au akusubiri nje??

?Mai ndiye aliyenitoa mimi matongotongo. Sina shida akiwepo, labda kama taaluma yako haikuruhusu, lakini kwa upande wangu. Ni sawa akiwepo.?

?Sawa...nimekuelewa vizuri kabisa, lakini naomba Mai umsubiri tu nje, acha nizungumze naye kwa uhuru zaidi.?

Wote wakacheka.

Mai akasimama na kupiga hatua za kivivu kuelekea nje. Ndani ya ofisi wakabaki wawili tu ? Sista Isabela na Lilian.

?Naamini sasa utakuwa huru zaidi. Nikuambie tu Lilian, umekuja mahali sahihi kabisa. Tuliza kichwa chako, kuwa huru na ondoa wasiwasi wako kabisa. Kila kitu kitakuwa sawa,? akasema Sista Isabela.

?Najua unafahamu mengi kidogo kwa sasa kuhusu ukimwi. Hatutajifunza wala kuzungumzia sana kuhusu ukimwi. Tayari unao. Nataka kujadili kuhusu maisha. Kuhusu maisha yako mapya baada ya kujua tayari umeambukizwa.

?Hebu tuanze na hili. Ni jambo gani linalokupa hofu zaidi baada ya kujua kuwa umeambukizwa? Namaanisha, ni wapi unahisi kuna giza nene mbele yako? Hapo ndipo ninapotaka kuanza napo,? alisema Sista Isabela kwa sauti tulivu, akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Lilian.

Lilian akatulia kwa muda. Akajikohoza kidogo, kisha akavuta pumzi ndefu sana, halafu akazishusha taratibu kabisa.

?Kiukweli nina hofu na mengi. Kwanza mimi ni msichana mrembo, naogopa kukonda... kuonekana kama mgonjwa-mgonjwa. Sina mtoto, natamani sana kuwa na wanangu. Nataka kuolewa, ndoto hiyo imefutika, tena tayari nilikuwa na mpenzi wa kweli ambaye alikuwa tayari kunioa, haiwezekani tena.

?Ona maisha yangu yalivyoharibika. Nimehairisha mpaka mwaka wangu wa masomo. Naua nitarudi, nitamaliza na nitapata kazi... halafu fedha nitazopata zitakuwa na faida gani? Naona kama nimekwisha! Ni giza tu mbele yangu!? akamaliza kusema Lilian akihema kwa kasi.
 
SEHEMU YA 47 KATI YA 50

?Tuliza moyo. Yote hayo si matatizo. Labda nikuhakikishie kuwa, huwezi kukonda na kuonekana kama mgonjwa ? dhaifu. Utaolewa, utazaa watoto tena wasio na uambukizo na utayafurahia maisha yako mpaka siku Mungu atakapoamua vinginevyo na si kwa sababu ya ukimwi,? akasema Sista Isabela kwa kujiamini.

?Mh! Kuolewa? Kuzaa watoto wasio na uambukizo? Itawezekanaje? Hapo sasa unanidanganya!? akasema Lilian akitoa macho.

?Hakuna udanganyifu mdogo wangu. Sikia...? akasema Sista Isabela, sasa akianza kupekua kitu kwenye kompyuta mpakato iliyokuwa mezani mwake.

Lilian akatulia akisubiri kumsikiliza!





TATIZO la elimu ya ukimwi kutolewa nusunusu lilionekana kumjaa sana Lilian. Tangu anapata ufahamu na kusikia habari za ukimwi, kitu pekee alichojua ni kwamba ukimwi ni hatari!

Ukimwi unua!

Hivyo tu!

Hakuwahi kusikia kuwa, ukimwi ni ugonjwa ambao kwa sasa una namna ya kupunguza makali yake. Kuishi kwa amani na kuendelea na taratibu zote za maisha hata baada ya kuathirika.

Ubongoni mwake alijua, kupata ukimwi ni tiketi ya kifo, basi! Ukipata ukimwi, ndiyo mwisho wako. Si kweli. Juhudi za wataalamu mbalimbali wa afya duniani, zimesadia kuufanya ugonjwa huu kutokuwa tishio sana katika zama hizi.

Hilo tu ndilo ambalo Lilian hakulijua kabisa. Sister Isabela akaonekana kuangalia kitu kwa makini sana kwenye kompyuta yake. Lilian akionekana kuwa na mawazo sana.

?Sikia...umewahi kusikia kuwa, siku hizi wamama wajawazito ni lazima wapimwe ukimwi?? Sister Isabela akauliza.

?Ndiyo, nimesikia.?

?Unajua ni kwa nini??

?Ili kujua afya zao.?

?Halafu?!!!?

?Kwa kweli sijui zaidi ya hapo,? akajibu Lilian huku akitingisha kichwa kukataa kuwa na ufahamu na jambo hilo.

?Ngoja nikuambie. Kupima ukimwi ni hiyari, lakini mama mjamzito, kwa kuwa ndani ya tumbo lake ana kiumbe chenye haki ya kuishi, kwa masilahi ya kiumbe hicho, kupima sasa inakuwa si hiyari tena.

?Tunapima ili kujua kama mama ameathirika. Kumbuka kuathirika kwa mama, si sababu ya mtoto kuwa na ukimwi. Iko hivi; kama mama atakutwa ameathirika, mtoto hawezi kuwa na ukimwi. Hapo sasa ni kazi ya madaktari kujitahidi kuhakikisha kuwa, mtoto haambukizwi!? akasema Sister Isabela.

?Habari mpya sana kwangu hizi. Kwahiyo sasa, inakuwaje mtoto anakuwa katika tumbo la mwanamke mwenye virusi halafu asiambukizwe na mama yake?? akauliza Lilian.

?Elimu yake ni pana kidogo lakini kwa sasa unatakiwa kufahamu kuwa, eneo pekee ambalo mtoto anaweza kuambukizwa ni wakati wa kuzaliwa.

?Lakini kwa sababu madaktari watakuwa wameshajua, mama atapatiwa dawa maalumu ya kupunguza kasi ya kusambaa kwa virusi na dawa na kuimarisha zaidi chembe hai zake nyeupe za damu, lakini pia atashauriwa namna kuitunza afya yake.

?Pia atapatiwa dawa za kumkinga mtoto wakati wa kuzaliwa, ambazo zitasaidia mtoto asiambukizwe. Hata hivyo kuna umakini zaidi wa kitaalamu wa kuhakikisha mtoto anakuwa salama angalau kwa asimilia 80.

?Madaktari watakuwa makini sana kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu afya ya mama. Wakiona kuna dalili nyingi za mtoto kuambukizwa, mara moja hatua zaidi huchukuliwa ikiwepo kujifungua kwa upasuaji.

?Ni elimu pana ambayo inahitaji muda kujifunza taratibu. Nikutoe hofu kuwa, ukimwi siyo kifo. Maisha yanaweza kuendelea kama kawaida baada ya kuwa na virusi hivyo,? akasema Sister Isabela.

Lilian alivuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu kabisa. Alikuwa amejifunza kitu kipya kabisa katika maisha yake. Hofu iliyokuwa imemjaa, ikaanza kushuka taratibu moyoni mwake.

?Naanza kukuelewa Sister Isabela,? akasema Lilian.

?Najua...najua sana. Lakini Mai alisema eti, inawezekana mwanamke akawa na uambukizo na mwanaume akawa hana, lakini mwanaume asipate. Ni kweli??

?Kabisa! Ilivyo ni kwamba, mwanamke ana hatari kubwa ya kuambukizwa kuliko mwanaume. Hiyo ni kwa sababu za kibaolojia. Jambo kubwa linaloshauriwa ni mwanamke kuandaliwa vya kutosha kabla ya tendo.

?Jambo hilo likifanyika kikamilifu, mwanaume hawezi kuambukizwa. Hata hivyo watu wanaoruhusiwa
 
SEHEMU YA 48 KATI YA 50

kufanya hivi ni wanandoa, ambao mmoja wao kwa bahati mbaya atakuwa ameathirika.

?Hata hivyo, ushauri wa mwisho na mkubwa zaidi kwa wanandoa wa aina hiyo, ni kutumia mpira muda wote, mpaka pale watakapohitaji mtoto ambapo lazima wawe karibu na wataalamu ambao watawaelekeza njia bora na salama zaidi ya kufanya ili mwanamke kupata mimba na kumuacha mwanaume akiwa hana virusi vya ukimwi,? akasema Sister Isabela.

Lilikuwa somo gumu sana, lakini Isabela alijitahidi kuzungumza kwa lugha nyepesi ambayo Lilian alimwelewa kwa urahisi zaidi.

Mpaka anaondoka ofisini kwake, alikuwa Lilian mpya kabisa. Mwenye mtazamo mpya na fikra mpya kabisa. Alimshukuru sana shoga yake Mai.

***

Lilian akiwa ndiyo kwanza anafungua geti la kuingia nyumbani kwa shangazi yake, Juliana, simu yake iliita. Alipoitazama kwenye kioo, akakutana na jina la Edo!

Moyo ukamlipuka!

Mara moja akapokea.

?Edo baba yangu... umenikumbuka leo?? Lilian akazungumza akiwa mnyonge, ushahidi mkubwa ikiwa ni sauti yake.

?Ndiyo mpenzi!?

Lilin akashtuka tena!

Anaitwa mpenzi?

?Lilian...? Edo akaita.

?Yes Edo!? (Ndiyo Edo)

?Usinyongee, wewe ni wangu. Siwezi kukutupa mama. Sasa sikia, nina bonge la surprise!?

?Surprise? Which kind of that?? (Mshtukizo? Ni mshtukizo gani huo?)

?Kesho saa 8:30 mchana kwa saa za huko, nitakuwa airport, naomba usiache kuja kunipokea!?

?Waooo kweli??

?Sijawahi kukudanganya. Kwa heri kwa sasa Lilian, tafadhali kuwa na utulivu. Nina habari njema sana kwako hiyo kesho nikija.?

?Sawa mpenzi wangu....oooh! No... sawa Edward...? akasita Lilian.

?No! No! No! It?s okay... mimi ni mpenzi wako. Uko sahihi kabisa. Hakuna kilichobadilika,? Edo akasema na kukata simu.

Lilian akabaki anashangaa!

Aliisubiri kwa hamu sana hiyo kesho!

***

Macho ya Lilian yalikuwa yanaangalia kwenye lango kuu la abiria wanaowasili kutoka sehemu mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Abiria walikuwa wakitoka huku wakiburuza mizigo yao kwenye vitoroli. Kwa mbali, akamwona Edo akiwa anasukuma kitoroli chenye mizigo yake.

Lilian hakuamini.

Edo alikuwa amejawa na tabasamu. Kwa shauku, Lilian akajikuta akianza kukimbia akimfuata Edo aliyekuwa akitembea kama hataki, kuelekea alipokuwepo!

Ilikuwa siku mpya kwa Lilian.





LILIAN alimuona Edo akiwa katika umbo lake la kupendeza. Akiwa katika utanashati wake uleule. Alitembea kwa madaha sana. Mbio za Lilian nusura zidondoshe mabegi yake. Alimvaa na kumkumbatia haraka.

Lilikuwa tukio la dakika moja tu, lililoibua hisia za wengi waliokuwa pale uwanjani.

?Pole na safari Edo, siamini kama ni wewe, siamini kama nimekuona. Siamini kama ungenitafuta,? akasema Lilian.

?Usijali mpenzi wa ngu, nakupenda sana. Achana na yote kama yalivyo. Kwa sasa nahitaji kupata mahali pa kupumzika kwanza, mengine yatafuata.?

?Sawa baba, pole sana. Unapenda wapi??

?Tabata.?

?Sehemu gani??

?Nimeshafanya mawasiliano na ile hoteli ninayopenda kufikia. Twende hapo.?

?Sawa.?

Wakatoka na kwenda kuingia kwenye moja ya teksi zilizokuwa eneo lile. Edo akamwelekeza dereva wanapoelekea. Safari ya kwenda Tabata ikaanza.

***

Edo alikuwa wa kwanza kushuka garini, akafuta Lilian. Edo akamlipa dereva ambaye alikuwa bize akihakikisha mizigo yote ya abiria wake ikashuka salama.

?Ahsante sana kaka, karibu tena Tanzania,? akasema dereva yule aliyejitambulisha kwa jina la Alphonce.

?Usijali.?

?Chukua hii, next time, muda wowote nitafute. Pale ndiyo kijiwe changu cha kudumu,? akasema Alphonce akimkabidhi Edo kadi yake ya mawasiliano.

Wenyewe wamezoea kuiita business card.

?Ahsante sana kaka Alphonce.?

Walipokelewa na mhudumu ambaye aliwasaidia mizigo na kuipeleka ndani. Tayari kila kitu kilikuwa sawa katika hoteli hiyo. Waliingia na kuweka mizigo vema kisha wakaketi kwenye sofa kubwa kwa mtindo wa kuangaliana.

?Pole sana kwa safari Edo,? Lilian alikuwa wa kwanza kuanza kuzungumza.

?Ahsante sana Lilian.?

?Najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, sina majibu kabisa.?

?Maswali ya nini??

?Nilikukosea sana Edo. Mimi sistahili kuwa karibu yako kabisa. Nilivunja ahadi yetu na mwisho nikapaa matatizo.?

?Hapana, achana na mambo hayo. Ndiyo maana nipo hapa. Elewa kwamba, unaninyima raha sana, moyo wangu unateseka kwa ajili yako.
 
SEHEMU YA 49 KATI YA 50

?Kifupi nimeshindwa kabisa kufanya chochote bila wewe. Nashukuru Mungu nimemaliza masomo salama. Lakini kwa shida sana.

?Nilikuwa na kufikiria wewe. Nimechanganyikiwa kabisa. Nashindwa kufikiria maisha yangu bila wewe. Ni vigumu kukutoa maishani mwangu,? akasema Edo kwa sauti iliyojaa hisia kali za kimapenzi.

?Unamaanisha nini Edo??

?Siwezi kuishi bila wewe.?

?Unamaanisha nini??

?Siwezi kuwa na mwanamke mwingine bila wewe.?

?Edo mimi ni mwathirika tayari.?

?Hata kama.?

?Sasa itawezekanaje??

?Ndiyo maana nipo hapa. Kuna kitu cha kufanya.?

?Kipi??

?Nahitaji kutoka na wewe usiku wa leo. Tutazungumza zaidi. Kwa sasa nahitaji kulala.?

?Sawa, lakini lazima nizungumze na shangazi kwanza.?

?Shangazi??

?Ndiyo.?

?Kivipi??

?Naishi kwa anti.?

?Sijakuelewa.?

Lilian akaanza kumsimulia kila kitu kuhusu alivyochanganywa na tatizo lake, namna alivyoamua kuhbairisha mwaka wake wa masomo na jinsi alivyokutana na Mai ambaye alimsaidia kumpeleka kwa mshauri ambaye alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kumbadilisha mtazamo.

Alizungumza yote lakini suala la mshauri aliyemsaidia lilimvutia zaidi na kumchanganya kichwa chake. Edo alifurahishwa sana na ushauri wa Mai.

?Ndiyo maana naona afya yako bado ni nzuri kabisa. Huwezi kuamini, nilikuja pia kukueleza kuhusu tatizo lako. Nilitaka kukushauri namna nilivyoshauriwa.?

?Ulivyoshauriwa? Unamaanisha nini??

?Zungumza na anti yako, mengine tutazungumza jioni.?

?Sawa.?

Lilian muda uleule aliwasiliana na shangazi yake, Juliana na kumweleza kila kitu kuhusu Edo. Kitu ambacho hakumwambia ni kuhusu hali yake. Alimweleza tu kuwa, yule mchumba wake aliyemsababishia akashindwa kuendelea na masomo, alikuwa amerejea.

Kwa Lilian halikuwa jambo zuri sana, lakini kwa sababu alimwambia yupo naye, pia alimweleza alifika kutokea Malaysia kwa ajili yake, hakuwa na pingamizi zaidi ya kukubaliana naye.

?Sawa, kumbuka wewe ni mtu mzima, kuwa makini.?

?Nimekuelewa anti.?

?Najua unajua cha kufanya.?

?Bila shaka anti.?

Zoezi lililofuata lilikuwa ni kuoga ? waliingia bafuni kwa zamu, kisha wakajitupa kitandani na kulala. Hakuna kilichofanyika kwa wawili hao zaidi ya kulala tu!

***

Meza yao ilipendeza hakika. Glasi mbili za maji ya matunda zilikuwa zimetulia mezani ? hazijaguswa tangu zilivyotua. Walikuwa wakisubiria oda ya chakula walichoagiza.

Wali na samaki!

Pamoja na uzuri wa meza yao na namna walivyovaa mavazi ya kuvutia, nyuso zao zilionekana kujaa majonzi mazito. Ilikuwa vigumu kuelewa kuwa yalikuwa majonzi ya furaha au huzuni.

Ukweli ni kwamba, walikuwa na majonzi ya furaha!

Uso wa Lilian ulikuwa umechakazwa kwa machozi, Edo akiendelea kuzungumza kwa kujiamini sana.

?Yes! Nilichoamua ni sahihi, ninachokizungumza kipo sawa na hakuna wa kukibadilisha. Nimeamua kukuoa. Nitakuoa hivyohivyo ulivyo,? alisema Edo akijitahidi kuzuia machozi yake.

?Hakuna mwanamke mwingine nitakayeweza kumpenda kama wewe. Moyo wangu wote upo kwako. Sio rahisi kumpenda mwingine!? akasema Edo.

?Edo itawezekana vipi wakati mimi ni mwathirika??

?Itawezekana tu!?

?Kuhusu wazazi??

?Hatutawaeleza kuhusu hili mapema. Hii itakuwa siri yetu. Kumbuka utaishi mimi na wewe. Hakuna mwingine zaidi yetu. Haya ni maisha yetu. Nataka tufungue ukurasa mpya.?

?Lakini Edo si nitakuambukiza mpenzi?? akasema Lilian kwa uchungu mwingi.

?Hakuna kitu kama hicho. Zipo njia za kufanya. Tutaweza kuishi kwa amani na watoto wetu watakuwa salama,? akasema Edo kwa kujiamini.

?Kivipi?? Lilian akauliza kwa woga.

Hakujua kama Edo alikuwa akifahamu kuhusu elimu aliyopewa na mshauri wake.

?Nimetafuta ushauri wa wataalamu kule Kuala Lumpur. Wamenielekeza kila kitu. Bado naweza kuishi na wewe bila tatizo. Ndiyo maana pia nimefurahi sana kusikia kuwa umekutana na mshauri na amekusaidia mengi.

?Nimekusamehe yote mpenzi wangu. Sitaki kukuhukumu kwa yaliyopita. Kifupi ujue kuwa nakupenda na siwezi kuishi bila wewe. Kwa sasa nahitaji kuonana na mshauri wako kwa maelekezo zaidi!? akasema Edo.

Lilian alikiri ndani ya moyo wake kuwa, hakuwahi kukutana na muujiza mkubwa katika maisha yake kama huo.
 
SEHEMU YA 50 KATI YA 50..............MWISHO

Alisimama na kunyoosha mikono yake yote miwili, Edo akaipokea. Wakashikana kwa nguvu, kisha wote kama walioambiana, wakainamisha vichwa vyao na kukutanisha midomo yao.

Wakapigana mabusu!

Lilian alishindwa kuzuia machozi yake.





ZILIKUWA hisia kali za mapenzi, hisia ambazo ilikuwa vigumu sana kuzizuia. Wawili hao waliendelea kugandana kwa muda. Bado Lilian hakuamini kilichotokea!

?Nakupenda sana Lilian, wewe ni wangu, sina kitu cha kubadilisha,? akasema Edo.

?Ahsante sana mpenzi wangu. Nafurahi kwa haya yote. Siamini kama kweli tungekuwa hivi tena.?

?Sahau yote mama. Leo hii, usiku wa leo, utakuwa usiku wetu. Nataka kuujua mwili wako kwa mara ya kwanza.?

?Bado mapema, isitoshe hatujajua njia sahihi za kuhakikisha hupati matatizo. Kumbuka nahitaji kukuona katika maisha yangu, sitaki upate matatizo!? akasema Lilian.

?Kwa kauli yako, ina maana wewe utakufa mapema kwa sababu una uambukizo? Achana na mawazo ya kizamani hayo. Hata hivyo kuna kitu cha kufanya. Njia rahisi na salama zaidi kwetu kwa sasa ni mpira.

?Tutatumia mpira. Nadhani utakuwa sawa kihisia na sitakuwa kwenye uwezekano wa kupata maambukizi!? akasema Edo.

Lilikuwa tukio la kushangaza sana kwa Lilian. Edo amekuwa mtu wa tofauti sana kwake. Mara moja, neno likamponyoka: Nakupenda Edo.?

?Nakupenda pia.?

Ni muda huo, mhudumu alifika akiwa na chano kilichokuwa na vyakula. Wote wakatulia na kuketi sawasawa!

?Karibuni sana jamani... ila nawaomba muinuke muende mkanawe pale mbele kwenye sinki,? mhudumu yule mrembo akasema baada ya kuweka sahani za vyakula mezani.

Wakainuka na kwenda kunawa. Wakati wote huo, yule mhudumu alisimama akiwasubiri. Waliporejea na kukaa, ndipo yule mhudumu akaondoka na kuwaacha!

Kazi ikaanza!

Walikula kwa furaha huku wakizungumza. Walilishana kwa furaha na mahaba mazito. Ulikuwa mlo mzuri, walioufurahia pamoja.

***

?Sikiliza bwana Edward, kwa kawaida hatushauri sana watu wenye hali mbili tofauti kuingia kwenye ndoa. Kwa kawaida ushauri huu ninaokupatia huwa ni kwa wale ambao tayari ni wanandoa.

?Kwa wachumba ambao hawajafunga ndoa, tukigundua mmoja ni mwathirika huwa tunawashauri waachane na siyo kuwashauri bali wenyewe tu huachana baada ya hapo. Lakini kwa sababu inaonekana huwezi kumwacha mwanamke wako na umeonekana kuwa na mapenzi ya dhati, ndiyo maana nakushauri kwa undani ili uweze kuilinda afya yako.

?Kwanza ujue kuwa, mwanamke ana nafasi kubwa zaidi ya kupata uambukizo kutoka kwa mwanaume, lakini ana nafasi ndogo sana ya kumwambukiza mwanaume. Jambo kubwa unalotakiwa kuzingatia,hakikisha unafanya maandalizi ya kutosha kabla ya tendo.

?Njia ya mwanamke ikiwa yenye ulaini wa kutosha, yenye utayari wa tendo, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufurahia tendo bila kuambukizwa. Hata hivyo, ushauri wangu mkuu, tumia mpira mpaka utakapoamua kuzaa na mwanamke wako.?

Maneno haya yalijirudia usiku huo wakati Edo akiwa kando ya Lilian, kitandani wakijitayarisha kuhamia katika ulimwengu mwingine.

Ndivyo ilivyokuwa, Edo hakufanya makosa. Alizingatia yote na baada ya dakika arobaini na tano mbele, walikuwa wamehamia kwenye kisiwa cha kupendeza sana.

Kisiwa kisichoweza kufananishwa na kingine chochote duniani!

Kisiwa cha huba!

***

?Sijawahi kuona upendo kama huu,? akasema Sista Isabela aliyekuwa mbele ya Lilian na Edo ofisini kwake.

Hakutegema kama kuna mwanaume ambaye angeweza kumsamehe mpenzi wake kwa kumsaliti na kupata maambukizi ya ukimwi na kisha kukubali kumuoa.

Kwake lilikuwa jambo la ajabu sana. Isabela alibaki akimshangaa Edo. Kuna wakati alijisahau kabisa kuwa yeye ni mshauri na alitakiwa kufanya kazi yake kama mshauri na siyo vinginevyo.

?Usijali Sista. Ni mapenzi tu. Mapenzi ni kichaka, ni siri kubwa. Hizi ni hisia zangu za ndani juu ya mwanamke huyu. Kiumbe ambaye kwa kweli kwa namna yoyote, nisingeweza kuishi bila yeye.

?Ndiyo maana nimeamua kutafuta ushauri zaidi. Nilipojiridhisha kuwa maisha yangu yatakuwa sawa, nikaamua iwe hivyo. Nitamuoa Lilian,? akasema Edo.

?Mungu awatangulie. Nimeshazungumza mengi. Uzuri hata Malaysia wamekusaidia sana. Nawatakieni kila heri. Mkiwa na tatizo lolote au mkiona mnahitaji usaidizi wangu katika jambo lolote msisite kuniambia.

?Kwa sasa Edo, tafadhali endeleeni kutumia mpira kwanza, siku mkiwa tayari kupata mtoto, mje ili niwape maelekezo ya kina, ili jambo hilo lifanyike bila athari yoyote!?

?Sawa.?

Walisimama na kumkumbatia Sista Isabela kwa wakati mmoja. Isabela alikuwa katikati, Edo akawa mbele yake, Lilian nyuma.

Wakaagana!

***

Taarifa za Edo kutaka kuoa zilipokelewa vizuri sana na wazazi wake. Hakuna aliyekuwa na pingamizi. Mara moja posa ikapelekwa nyumbani kwa akina Lilian na mambo yakaenda vizuri.

Miezi minne baadaye walifunga ndoa ya kihistoria jijini Dar es Salaam. Lilian alimsamehe Lucy, rafiki yake ambaye ndiye aliyemuunganisha na Pam aliyemsababishia maambukizi.

Hata hivyo, hakumwambia siri hiyo. Si Lucy tu, hata wazazi na ndugu wengine wote, hawakujua kabisa kuhusu suala la Lilian kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Jambo la kufurahisha zaidi, walirudisha rasmi urafiki wao wa akina L. Ni Lucy, Leila na Latifa ndiyo waliokuwa wapambe wa kike katika harusi yao iliyofana.

Miaka miwili baadaye, Lilian na mumewe Edo, walijaliwa mtoto wa kiume waliyempa jina la Fredrick. Alifanana kila kitu na baba yake ? Edo.

Habari za kufurahisha zaidi ni kwamba, mtoto Fred hakuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Miezi sita baadaye, Edo na mkewe walihamia kwenye nyumba yao, Mbezi ? Msakuzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kumalizika kwa ujenzi.

Siku ya kwanza wanahamia katika nyumba hiyo waliamua kufanya sherehe. Ilikuwa sherehe mbili kwa wakati mmoja. Kwanza kuzindua nyumba na pili, mtoto Fred alikuwa anabatizwa!

Walialikwa ndugu pekee na marafiki wachache. Ni hapo ndipo wanandoa hao walipoamua kuvunja ukimya. Alizungumza Edo...

?Nawashukuru wote kwa kuja. Ninyi hapa, asilimia kubwa ni ndugu zetu wa damu ambao mnatuhusu kwa kila kitu. Wachache ni marafiki ambao tumeshibana.

?Kushibana huko, maana yake mmeshakuwa ndugu. Niseme kwamba, mimi na mke wangu Lilian tuna furaha. Tunajisikia vizuri leo hii kuhamia katika nyumba yetu na pia kwa sababu mwanetu amebatizwa.

?Kuna jambo tumeona ni vyema kuwashirikisha. Tunaamini litawasaidia lakini na sisi tutakuwa tumetua mzigo moyoni. Naomba muelewe kwamba, sisi hatuna tatizo na jambo hilo. Tunaishi kwa amani na hatutaona sababu ya mtu yeyote kuhuzunikia jambo hilo,? akasema Edo akiwaangalia watu ambao tayari walishakuwa na wasiwasi.

?Kifupi mke wangu Lilian anaishi na virusi vya ukimwi!?

Watu wote walishtuka!

?Hakuna sababu ya kushtuka. Pamoja na hilo, mimi sina maambukizi. Na hata mwanetu Fred, hana tatizo. Jambo hili si la bahati mbaya. Kabla hatujaoana, tulifahamu hili na tulikubaliana,? akaendelea kuzunguumza Edo.

Awali watu wengi walionekana kuumizwa sana na uamuzi wa Edo kumuoa Lilian huku akijua mwenzake alikuwa mwathirika, lakini baadaye walimuelewa na wakawa makini sana kumsikiliza.

Historia yao ya mapenzi iliwaumiza wengi. Kweli wakaonekana kuwa na penzi la kweli. Wazazi wa Edo awali walionekana kuchukizwa na jambo hilo.

Mwisho wa mazungumzo ya Edo, walisimama na kuwafuata Edo na mkewe Lilian, kisha wakakumbatiana kwa pamoja. Wazazi wa Lilian ambao walikuwa wakilia tangu waliposikia Edo akisema kuwa, Lilian alikuwa na maambukizi, nao walisimama na kwenda kuungana nao!

Wakakumbatiana pamoja na kutoa machozi ya furaha. Sherehe iligeuka vilio, lakini kwa bahati nzuri, machozi ya wengi yalikuwa ya msisimko na mshangao.

Wengi walishangazwa na penzi la kweli la wawili hao.

?Ahsante Edo kwa kunipenda...wewe umekuwa furaha ya maisha yangu. Nitakupenda milele baba,? akasema Lilian.

?Nami nitakupenda pia mama.?

Wakatazamana na kucheka pamoja!

Edo akawatazama watu waliokuwa eneo lile, akaonyesha ishara watulie na wasilie tena, wakafanya hivyo. Akaanza kuzungumza tena...

?Nawaombeni sana, tena sana. Tusiwanyanyapae waathirika wa ukimwi. Tuwapende na kuwapa moyo. Ukimwi siyo kifo kama wengi wanavyofikiria,? akasema Edo kisha akarudisha macho yake kwa mkewe, akamwambia:

?Wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu. Mwanamke uliyekuwa umekaa ndani ya moyo wangu siku zote. Nakupenda na naahidi kukutunza siku zote.

?Sina hofu. Najua utakufa, lakini siyo kwa sababu eti una ukimwi. Wewe utakuwa wangu siku zote, mpaka Mungu atakapoamua kukuchukua wewe au mimi. Nakupenda sana mama Fred.?

?Nakupenda pia baba Fred.?

Vicheko vikasikika katika eneo lote la nyumba ile mpya!



MWISHO.
 
Back
Top Bottom