SEHEMU YA 50 KATI YA 50..............MWISHO
Alisimama na kunyoosha mikono yake yote miwili, Edo akaipokea. Wakashikana kwa nguvu, kisha wote kama walioambiana, wakainamisha vichwa vyao na kukutanisha midomo yao.
Wakapigana mabusu!
Lilian alishindwa kuzuia machozi yake.
ZILIKUWA hisia kali za mapenzi, hisia ambazo ilikuwa vigumu sana kuzizuia. Wawili hao waliendelea kugandana kwa muda. Bado Lilian hakuamini kilichotokea!
?Nakupenda sana Lilian, wewe ni wangu, sina kitu cha kubadilisha,? akasema Edo.
?Ahsante sana mpenzi wangu. Nafurahi kwa haya yote. Siamini kama kweli tungekuwa hivi tena.?
?Sahau yote mama. Leo hii, usiku wa leo, utakuwa usiku wetu. Nataka kuujua mwili wako kwa mara ya kwanza.?
?Bado mapema, isitoshe hatujajua njia sahihi za kuhakikisha hupati matatizo. Kumbuka nahitaji kukuona katika maisha yangu, sitaki upate matatizo!? akasema Lilian.
?Kwa kauli yako, ina maana wewe utakufa mapema kwa sababu una uambukizo? Achana na mawazo ya kizamani hayo. Hata hivyo kuna kitu cha kufanya. Njia rahisi na salama zaidi kwetu kwa sasa ni mpira.
?Tutatumia mpira. Nadhani utakuwa sawa kihisia na sitakuwa kwenye uwezekano wa kupata maambukizi!? akasema Edo.
Lilikuwa tukio la kushangaza sana kwa Lilian. Edo amekuwa mtu wa tofauti sana kwake. Mara moja, neno likamponyoka: Nakupenda Edo.?
?Nakupenda pia.?
Ni muda huo, mhudumu alifika akiwa na chano kilichokuwa na vyakula. Wote wakatulia na kuketi sawasawa!
?Karibuni sana jamani... ila nawaomba muinuke muende mkanawe pale mbele kwenye sinki,? mhudumu yule mrembo akasema baada ya kuweka sahani za vyakula mezani.
Wakainuka na kwenda kunawa. Wakati wote huo, yule mhudumu alisimama akiwasubiri. Waliporejea na kukaa, ndipo yule mhudumu akaondoka na kuwaacha!
Kazi ikaanza!
Walikula kwa furaha huku wakizungumza. Walilishana kwa furaha na mahaba mazito. Ulikuwa mlo mzuri, walioufurahia pamoja.
***
?Sikiliza bwana Edward, kwa kawaida hatushauri sana watu wenye hali mbili tofauti kuingia kwenye ndoa. Kwa kawaida ushauri huu ninaokupatia huwa ni kwa wale ambao tayari ni wanandoa.
?Kwa wachumba ambao hawajafunga ndoa, tukigundua mmoja ni mwathirika huwa tunawashauri waachane na siyo kuwashauri bali wenyewe tu huachana baada ya hapo. Lakini kwa sababu inaonekana huwezi kumwacha mwanamke wako na umeonekana kuwa na mapenzi ya dhati, ndiyo maana nakushauri kwa undani ili uweze kuilinda afya yako.
?Kwanza ujue kuwa, mwanamke ana nafasi kubwa zaidi ya kupata uambukizo kutoka kwa mwanaume, lakini ana nafasi ndogo sana ya kumwambukiza mwanaume. Jambo kubwa unalotakiwa kuzingatia,hakikisha unafanya maandalizi ya kutosha kabla ya tendo.
?Njia ya mwanamke ikiwa yenye ulaini wa kutosha, yenye utayari wa tendo, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufurahia tendo bila kuambukizwa. Hata hivyo, ushauri wangu mkuu, tumia mpira mpaka utakapoamua kuzaa na mwanamke wako.?
Maneno haya yalijirudia usiku huo wakati Edo akiwa kando ya Lilian, kitandani wakijitayarisha kuhamia katika ulimwengu mwingine.
Ndivyo ilivyokuwa, Edo hakufanya makosa. Alizingatia yote na baada ya dakika arobaini na tano mbele, walikuwa wamehamia kwenye kisiwa cha kupendeza sana.
Kisiwa kisichoweza kufananishwa na kingine chochote duniani!
Kisiwa cha huba!
***
?Sijawahi kuona upendo kama huu,? akasema Sista Isabela aliyekuwa mbele ya Lilian na Edo ofisini kwake.
Hakutegema kama kuna mwanaume ambaye angeweza kumsamehe mpenzi wake kwa kumsaliti na kupata maambukizi ya ukimwi na kisha kukubali kumuoa.
Kwake lilikuwa jambo la ajabu sana. Isabela alibaki akimshangaa Edo. Kuna wakati alijisahau kabisa kuwa yeye ni mshauri na alitakiwa kufanya kazi yake kama mshauri na siyo vinginevyo.
?Usijali Sista. Ni mapenzi tu. Mapenzi ni kichaka, ni siri kubwa. Hizi ni hisia zangu za ndani juu ya mwanamke huyu. Kiumbe ambaye kwa kweli kwa namna yoyote, nisingeweza kuishi bila yeye.
?Ndiyo maana nimeamua kutafuta ushauri zaidi. Nilipojiridhisha kuwa maisha yangu yatakuwa sawa, nikaamua iwe hivyo. Nitamuoa Lilian,? akasema Edo.
?Mungu awatangulie. Nimeshazungumza mengi. Uzuri hata Malaysia wamekusaidia sana. Nawatakieni kila heri. Mkiwa na tatizo lolote au mkiona mnahitaji usaidizi wangu katika jambo lolote msisite kuniambia.
?Kwa sasa Edo, tafadhali endeleeni kutumia mpira kwanza, siku mkiwa tayari kupata mtoto, mje ili niwape maelekezo ya kina, ili jambo hilo lifanyike bila athari yoyote!?
?Sawa.?
Walisimama na kumkumbatia Sista Isabela kwa wakati mmoja. Isabela alikuwa katikati, Edo akawa mbele yake, Lilian nyuma.
Wakaagana!
***
Taarifa za Edo kutaka kuoa zilipokelewa vizuri sana na wazazi wake. Hakuna aliyekuwa na pingamizi. Mara moja posa ikapelekwa nyumbani kwa akina Lilian na mambo yakaenda vizuri.
Miezi minne baadaye walifunga ndoa ya kihistoria jijini Dar es Salaam. Lilian alimsamehe Lucy, rafiki yake ambaye ndiye aliyemuunganisha na Pam aliyemsababishia maambukizi.
Hata hivyo, hakumwambia siri hiyo. Si Lucy tu, hata wazazi na ndugu wengine wote, hawakujua kabisa kuhusu suala la Lilian kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Jambo la kufurahisha zaidi, walirudisha rasmi urafiki wao wa akina L. Ni Lucy, Leila na Latifa ndiyo waliokuwa wapambe wa kike katika harusi yao iliyofana.
Miaka miwili baadaye, Lilian na mumewe Edo, walijaliwa mtoto wa kiume waliyempa jina la Fredrick. Alifanana kila kitu na baba yake ? Edo.
Habari za kufurahisha zaidi ni kwamba, mtoto Fred hakuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Miezi sita baadaye, Edo na mkewe walihamia kwenye nyumba yao, Mbezi ? Msakuzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kumalizika kwa ujenzi.
Siku ya kwanza wanahamia katika nyumba hiyo waliamua kufanya sherehe. Ilikuwa sherehe mbili kwa wakati mmoja. Kwanza kuzindua nyumba na pili, mtoto Fred alikuwa anabatizwa!
Walialikwa ndugu pekee na marafiki wachache. Ni hapo ndipo wanandoa hao walipoamua kuvunja ukimya. Alizungumza Edo...
?Nawashukuru wote kwa kuja. Ninyi hapa, asilimia kubwa ni ndugu zetu wa damu ambao mnatuhusu kwa kila kitu. Wachache ni marafiki ambao tumeshibana.
?Kushibana huko, maana yake mmeshakuwa ndugu. Niseme kwamba, mimi na mke wangu Lilian tuna furaha. Tunajisikia vizuri leo hii kuhamia katika nyumba yetu na pia kwa sababu mwanetu amebatizwa.
?Kuna jambo tumeona ni vyema kuwashirikisha. Tunaamini litawasaidia lakini na sisi tutakuwa tumetua mzigo moyoni. Naomba muelewe kwamba, sisi hatuna tatizo na jambo hilo. Tunaishi kwa amani na hatutaona sababu ya mtu yeyote kuhuzunikia jambo hilo,? akasema Edo akiwaangalia watu ambao tayari walishakuwa na wasiwasi.
?Kifupi mke wangu Lilian anaishi na virusi vya ukimwi!?
Watu wote walishtuka!
?Hakuna sababu ya kushtuka. Pamoja na hilo, mimi sina maambukizi. Na hata mwanetu Fred, hana tatizo. Jambo hili si la bahati mbaya. Kabla hatujaoana, tulifahamu hili na tulikubaliana,? akaendelea kuzunguumza Edo.
Awali watu wengi walionekana kuumizwa sana na uamuzi wa Edo kumuoa Lilian huku akijua mwenzake alikuwa mwathirika, lakini baadaye walimuelewa na wakawa makini sana kumsikiliza.
Historia yao ya mapenzi iliwaumiza wengi. Kweli wakaonekana kuwa na penzi la kweli. Wazazi wa Edo awali walionekana kuchukizwa na jambo hilo.
Mwisho wa mazungumzo ya Edo, walisimama na kuwafuata Edo na mkewe Lilian, kisha wakakumbatiana kwa pamoja. Wazazi wa Lilian ambao walikuwa wakilia tangu waliposikia Edo akisema kuwa, Lilian alikuwa na maambukizi, nao walisimama na kwenda kuungana nao!
Wakakumbatiana pamoja na kutoa machozi ya furaha. Sherehe iligeuka vilio, lakini kwa bahati nzuri, machozi ya wengi yalikuwa ya msisimko na mshangao.
Wengi walishangazwa na penzi la kweli la wawili hao.
?Ahsante Edo kwa kunipenda...wewe umekuwa furaha ya maisha yangu. Nitakupenda milele baba,? akasema Lilian.
?Nami nitakupenda pia mama.?
Wakatazamana na kucheka pamoja!
Edo akawatazama watu waliokuwa eneo lile, akaonyesha ishara watulie na wasilie tena, wakafanya hivyo. Akaanza kuzungumza tena...
?Nawaombeni sana, tena sana. Tusiwanyanyapae waathirika wa ukimwi. Tuwapende na kuwapa moyo. Ukimwi siyo kifo kama wengi wanavyofikiria,? akasema Edo kisha akarudisha macho yake kwa mkewe, akamwambia:
?Wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu. Mwanamke uliyekuwa umekaa ndani ya moyo wangu siku zote. Nakupenda na naahidi kukutunza siku zote.
?Sina hofu. Najua utakufa, lakini siyo kwa sababu eti una ukimwi. Wewe utakuwa wangu siku zote, mpaka Mungu atakapoamua kukuchukua wewe au mimi. Nakupenda sana mama Fred.?
?Nakupenda pia baba Fred.?
Vicheko vikasikika katika eneo lote la nyumba ile mpya!
MWISHO.