Simulizi: Bosi kapenda mke wa mtu

Simulizi: Bosi kapenda mke wa mtu

nasrimgambo

JF-Expert Member
Joined
Jan 10, 2017
Posts
1,902
Reaction score
2,488
KARIBUNI KUSOMA SIMULIZI HII

SEHEMU YA KWANZA



Ilikuwa ni siku ya joto na jua kali, huku kama kawaida watu walikuwa wengi,
wakiwa kwenye pilika pilika, wengine wakiwahi usafiri na wengine wakishuka
kwenye mabasi na daladala wakiwa wamewasili.

Wafanyabiashara wadogowadogo
walikuwa bize na wateja wao, wengine walikuwa wakitumia vipaza sauti kunadi
biashara zao.


Watu kadhaa walioonekana wana hali duni na wamechoka, baadhi yao wakiwa
wazee, watoto na wenye ulemavu walionekana wameshika bakuli wakiombaomba
kwa wapita njia, huku wapita njia wachache wakitoa sarafu toka mifukoni mwao na
kuweka kwenye bakuli hizo.


Hali ndivyo ilivyokuwa hapo stendi ya Mbezi Luis, palikuwa pamechangamka na
kelele mtindo mmoja. Na hiyo ndiyo ilikuwa kawaida ya eneo hilo lililopo magharibi
ya jiji la Dar es Salaam.


Siku hiyo, wapendao wawili, kijana Haruna na mke wake Zara walikuwa kwenye
banda lao lao la biashara ya kuuza nguo za mitumba, lililokuwa moja kati ya
mabanda mengi ya biashara ndogondogo yaliyopo hapo stendi. Walikuwa wazoefu
na waliwashawishi wateja wengi wanunue nguo kwao.


Jioni walifunga biashara yao wakiwa na nyuso za furaha kwa kiasi cha fedha
walichokipata siku hiyo. Na wakarejea walikoishi, mitaa ya Goba.
Ndoa yao ilikuwa bado changa kabisa walikuwa wameoana miezi sita tu iliyopita
na maisha yao yalikuwa ni ya kawaida kabisa. Walikuwa wamepanga chumba kimoja.
Na humo waliishi wao, kitanda chao, viti, kabati, vyombo, viatu, madumu na madude
mengine kibao yote kwenye chumba hichohicho kimoja, na choo kilikuwa cha nje cha
kushea na mpangaji mwezao mwengine.


Pamoja na maisha yao ya kuwa ya kawaida sana, Haruna na Zara walipendana
mno. Na mapenzi yao katika ndoa yao changa yalikuwa motomoto.
Haijalishi siku iliwachosha kiasi gani, kila waliporejea kwenye chumba chao
kimoja walikuwa kwenye ulimwengu wa peke yao wa mapenzi walisahau uwepo wa
viumbe wengine wote.


Na usiku wa siku hiyo haukuwa tofauti ulikuwa ni wa furaha na mapenzi kwao.
Zara akiwa peke yake chumbani aliwasha redio yao na kuweka mziki mzuri wa
mapenzi, akijua fika utamnyanyua Haruna huko nje alikokuwako na kumrudisha
chumbani.

Kisha akajitupa kitandani huku kaukumbatia mto na kutupia macho yake
kwenye mlango wa chumba, akifahamu fika kuwa punde tu, Haruna angefungua
mlango na kuingia ndani.

Na kweli, sauti ya mziki mzuri wa mapenzi ilimfikia Haruna aliyekuwa amekaa
kwenye baraza nje ya nyumba, akajikuta akiweka tabasamu usoni. Alifahamu kuwa
ilikuwa ni mbinu ya Zara ya kumuita arejee ndani.


Basi Haruna alinyanyuka toka barazani alipokaa na kuelekea ndani, akafungua
mlango wa chumba alichoishi na mkewe na kuingia. Na akamuona mkewe akiwa
yupo kitandani kashikilia mto, usoni akiwa na tabasamu, huku mziki wa kimapenzi
ukiendelea kupiga.


Hakika Zara alivutia sana machoni mwa Haruna. Haruna alijiona mwenye bahati
sana kuwa mume wa Zara. Basi taratibu Haruna alisogea hadi karibu na kitanda na
kumnyooshea Zara mkono wa kulia, Zara akanyoosha mkono wake wa kushoto na
Haruna akaukamata mkono huo, kisha akamvuta Zara na kumnyanyua toka hapo
kitandani akamsimamisha na kumkumbatia, na kumshikilia huku wakianza kucheza
wimbo uliokuwa ukiendelea kupiga toka kwenye redio yao.


Walikuwa kwenye huba zito. Wote walipendana. Zara alimtazama Haruna usoni
na kuanza kumwambia, “mpenzi wangu mwenyezi Mungu muumba wa ardhi na
mbingu awe shahidi, wa penzi langu kwako, lililo moyoni mwangu”, aliongea Zara
huku Haruna akibaki anamtazama mkewe huyo, huku wakiendelea kucheza taratibu
wimbo wa mapenzi, kisha akaendelea kuongea, “tutulizane mpenzi tupendane”.
Naye Haruna akafungua kinywa chake na kuanza kumwambia mkewe, “Mke
wangu naahidi kukupenda na kukujali milele. Mimi nimekuchagua uwe wangu,
wangu wa maisha wa kufa na kuzikana”.
Mara wakajikuta wamesukumana kitandani, huku wakitupiana mabusu, huku
wakitoa nguo zilizo miilini mwao, na kushikanashikana kimapenzi. Hakika ulikuwa ni
usiku wa aina yake kwao.
….……………………………………………………


Pengine mapenzi ya Haruna na Zara yalitokana na kufanana kwa historia za
maisha yao. Wote walikuwa wametoka familia zenye maisha ya kawaida sana.
Haruna alikulia mitaa ya Mburahati huku baba yake aliyeitwa Mzee Nzowa
alikuwa ni mtengeneza majiko ya mkaa na mama yake alikuwa anajishughulisha na
kuuza chakula na vitafunwa mtaani. Wazazi wake walimpenda sana na walifanikiwa
kumsomesha na Haruna alikuwa amehitimu shahada ya kwanza katika masuala ya
teknolojia ya mawasiliano.
Zara alikuwa amezaliwa mitaa ya Kigogo, alikuwa mtoto wa mwisho kwenye
familia yao ya watoto watatu. Baba yake alikuwa mlinzi kipindi Zara anazaliwa, ila
siku moja ajali mbaya ilisababisha babake apoteze miguu yake, hivyo kufanya
ashindwe kuendelea kutunza familia kupitia kazi yake ya ulinzi.

Na hivyo ilimbidi mama yake Zara ajiingize kwenye biashara za kuuza chakula
mtaani ili aweze kutunza familia yao.
Kupitia shughuli za kuuza chakula mtaani mama yake Haruna na mamake Zara
walifahamiana na kuunda urafiki, urafiki ambao uliwakutanisha Zara na Haruna na
wao wakawa marafiki.
Kutokana na urafiki wao, Zara alikuwako kwenye nyakati nyingi za muhimu za
maisha ya Haruna kama kwenye mahafali yake pamoja na sherehe zake nyingi za
kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.
Hata Haruna alipoingia chuo, Zara aliendelea kumtembelea hadi chuoni. Taratibu
uhusiano wao ukageuka kuwa mapenzi na hawakuficha wakaweka wazi kwa familia
zao.


Miezi kadhaa baada ya Haruna kuhitimu chuo, janga la mafuriko lililikumba jiji la
Dar es salaam na kuleta maafa makubwa na kubomoa nyumba na kuzoa mali za watu.
Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika yalikuwa ni Kigogo mtaa alioishi Zara ambapo
mafuriko yalibomoa nyumba yao na kufanya walale nje pale mafuriko yalipopita.
Haruna akiwa bado hajapata kazi yoyote ya maana aliamua kufanya maamuzi ya
kumuoa Zara.

Hakutaka kuona binti aliyempenda akilala nje kisa nyumba yao
imebomolewa na mvua, na aliona kuwa kwa kumuoa basi angeweza moja kwa moja
kumuondoa Zara kutoka kwenye kuishi maisha ya kulala nje, na pia wao kupata
nafasi ya kuanza maisha yao mapya kabisa kama mume na mke.
Basi ndoa ikafungwa. Na Haruna na mkewe Zara wakapanga chumba chao kimoja
mitaa ya Goba, huku wakibahatika kufungua biashara yao ya kuuza mitumba stendi
ya Mbezi baada ya babake Haruna, Mzee Nzowa kutoa fedha toka kwenye akiba zake
na kuwapa kama zawadi ya mtaji kwao, waanzie maisha.
Maisha yao yalikuwa na furaha sana hapo Goba. Walipendana na kujaliana.
Walifanya kazi kwa bidii kwenye biashara yao. Walikuwa na ndoto kubwa. Walipanga
kuja kuzaa watoto na kukuza familia. Walipanga kununua kiwanja na kujenga.
Walipanga kununua magari. Walipanga kusafiri na kwenda maeneo ya kitalii
kufurahia maisha na mapenzi yao hapo baadae.
Wao waliona maisha yao yana nuru kubwa. Walisadiki yote waotayo yatatimia.


Wao hawakujiuliza kama ndoto zao zitatimia, walijiuliza ni lini ndoto zao zitatimia,
waliona lilikuwa ni suala la muda kwa yao yote kutokea na walitumaini na kuamini
kuwa Mungu alikuwa upande wao na atawatetea kwenye safari yao ya maisha.
….……………………………
 
Basi maisha yao yaliendelea. Biashara yao nayo ikaendelea kuwafanya
wayamudu maisha. Naye Haruna alichakalika kutafuta kazi kwenye ofisi na mashirika
mbalimbali.


Hatimaye Haruna akapata kibarua kwenye moja ya kampuni zitoazo huduma ya
mitandao ya simu, iliyokuwa na ofisi zake maeneo ya Morocco katikati ya jiji.


Haikuwa kazi yenye maslahi makubwa, lakini kwa Haruna na Zara kwao ilikuwa ni
kazi iliyowapa fedha ya uhakika kila mwisho wa mwezi, na iliwafanya waone kuwa
Haruna walau alikuwa ameingia kwenye ulimwengu wa kuwa mtu mwenye ajira.
Hivyo Zara akaendelea na biashara peke yake.


Bosi wa Haruna aliyeitwa Thomas Makumbi, alinotisi uchapa kazi, uhodari,
umakini wa Haruna katika kazi zake. Na aliona kuwa kijana huyo atafika mbali. Na
walikuwa wakipiga stori nyingi sana kila mara walipokutana ofisini.


Siku moja Haruna na wafanyakazi wengine walikuwa pamoja na bosi wao bwana
Thomas kwenye kikao. Na kikao kilipoisha bwana Thomas aliruhusu wote watoke
ofisini ila akamuomba Haruna abakie humo kwenye chumba cha mikutano.


Haruna hakujua sababu ya bosi wake kumwambia abaki humo kwenye chumba
cha mikutano na uso wake ulionesha shauku kubwa ya kutaka kujua sababu ya
kuombwa kubakia. Bosi wake wakati huo alikuwa ametupia macho yake kwenye
mafaili aliyokuwa ameyafungua na akawa anayasoma, Haruna akabaki anamtazama.
Kisha bwana Thomas akafunika mafaili aliyokuwa akiyasoma na kuyaweka
mezani, kisha akavua miwani yake aliyokuwa ameivaa na kuiweka mezani, na kuanza
kuongea, “Nina habari ninayodhani ni njema kwako Haruna”, alisema bwana Thomas.
Haruna akawa yuko makini kutaka kusikia hiyo habari, nae Thomas akaendelea
kuongea, “Rafiki yangu amefungua kampuni mpya inayojihusisha na masuala ya
kusafirisha fedha kati ya Tanzania na nchi za nje kwa njia ya aplikesheni ya kwenye
simu. Na karibuni atatanua timu ya wafanyakazi kwenye kampuni yake hiyo, mimi
naona unastahili kabisa wewe kuwa sehemu ya timu hiyo”, alimaliza kuongea bwana
Thomas.


Ilikuwa ni habari njema kweli, kwa maana kazi aliyokuwa nayo Haruna wakati
huo haikuwa na mkataba, na maslahi yake yalikuwa madogo.

Hivyo kupata kazi
nyengine ya uhakika na pengine inayolipa zaidi ilikuwa ni habari njema sana, na hasa
habari hiyo ikiwa inatoka kwa bosi mwenyewe, ambaye ndie alikuwa anamsimamia
kazi yake aliyokuwa nayo wakati huo, ilikuwa ni habari njema.
 
Haruna alikubali, na kusema yuko tayari kwenda kufanya kazi kwenye kampuni
iliyoendeshwa na rafiki wa bwana Thomas.
Basi wiki mbili tu baadae Haruna aliwasili kwenye ofisi za kazini kwake kupya,
maeneo ya Victoria umbali mfupi tu toka kwenye jengo la ofisi alikotoka kuwa
mfanyakazi.


Kampuni hiyo aliyoanza kufanyia kazi iliitwa ‘Prompt Tranfers’. Bosi wa kampuni
hiyo aliitwa Sadro Bilali. Alikuwa rafiki mkubwa wa bwana Thomas, pia alikuwa ni
mtu maarufu na mashuhuri, aliyefahamiana na watu wengi maarufu, kuanzia
wanasiasa, wafanyabiasahara, viongozi wakubwa wa timu za michezo, wamiliki wa
vyombo vya habari hadi wasanii. Alikuwa ni mtu mwenye ushawishi mkubwa.
Bwana Sadro Bilali hakuwa tu tajiri aliyeanzisha hiyo kampuni mpya ya ‘Prompt
Transfers’ , bali pia alikuwa na biashara nyenginezo kubwa tu na aliwekeza kwenye
makampuni.


Mbali na hayo yote, Sadro alikuwa ni mjukuu wa Mzee Bakari Bilali ambaye
alikuwa ni miongoni mwa vijana waasisi wa chama kilichopigania uhuru miaka ya
1950, na baadae akaja kuwa mwanasiasa mkubwa.


Si hivyo tu, bali pia baba yake na Sadro alikuwa ni Madaraka Bilali ambaye nae
kama ilivyokuwa kwa Mzee Bakari Bilali aliendeleza gurudumu la urithi wa kisiasa
kwenye familia nae akawa mwanasiasa. Mzee Madaraka aliwahi kushika nyadhifa
mbalimbali serikalini na alikuwa ni miongoni mwa wanachama wenye ushawishi zaidi
kwenye chama kilichoshika mamlakani nchini.


Hivyo, Haruna na Sadro walitoka kwenye dunia mbili tofauti. Haruna tokea
Mburahati na Sadro kutokea Masaki. Haruna hakuwahi kufahamiana na mtu
aliyekuwa na uwezo na ushawishi na aliyetoka kwenye familia yenye uwezo, historia
na ushawishi nchini kama alivyokuwa bosi wake mpya, bwana Sadro Madaraka Bilali.
Kitendo cha kufahamiana na kuwa mfanyakazi wa Sadro tu ilionekana kuwa
mafanikio makubwa kwa Haruna. Aliona safari yake ya kutoboa imeanza kwa kuanza
tu kufanya kazi kwenye kampuni za watu wakubwa kama Sadro.


Haruna alimsimulia mkewe juu ya bosi wake mpya, alimwambia kuwa alikuwa ni
mtu mkubwa. Alimsimulia sana juu ya uwezo wake, jinsi ofisi za kampuni yake
zilivyokuwa kubwa na za kisasa, alimsimulia juu ya watu mashuhuri waliofika kwenye
ofisi zao na hivyo yeye Haruna kupata nafasi ya kuwaona pia.


Hata kwa Zara ilikuwa pia ni jambo kubwa kufahamu habari juu ya bosi huyo
mpya wa mume wake. Naye Zara aliyekulia huko kigogo hakuwahi kukutana na watu
waliokuwa na uwezo na ushawishi jinsi ambavyo Sadro alikuwa, bosi huyo alikuwa
ametokea dunia tofauti kabisa na ambayo yeye na mume wake walikuwa
wametokea.

….…………………………
Basi siku, miezi hatimaye miaka miwili ikapita na maisha ya Haruna na Zara
yalikuwa yamebadilika.

Sasa walihama toka kwenye chumba chao kimoja
walichopanga Goba na kuhamia mitaa ya Makongo ambako walipanga kwenye
nyumba kubwa huku biashara yao ikawa kubwa na Zara akahamishia biashara
maeneo ya Tegeta.


Wakafanikiwa kununua kiwanja mitaa ya Madale na kuanza kujenga nyumba yao
ya kwanza. Na kwa jeuri waliyoanza kujifunza sasa, walikuwa wenyewe wakiambiana
kuwa wakimaliza nyumba hiyo Madale, itabidi wanunue kiwanja maeneo ya Mbweni
ama Kigamboni ili wajenge ghorofa karibu na bahari kabisa.


Maisha kwao yalikuwa ni ya furaha kwao kilichokosekana kilikuwa ni kitu karaha
tu. Hata maisha ya familia zao zilibadilika. Haruna alijenga upya kabisa nyumba ya
wazazi wake huko Mburahati na kuwawekea ukuta na geti kabisa, huku wazazi wa
Zara waliwahamishia Kibaha ambako mama yake Zara alikuwa kanunua shamba na
wakawajengea nyumba kabisa.
Kama kawaida ya hela, huwa inajionesha kwenye muonekano wa aliyekuwa nayo,
basi, Zara nae sasa uzuri wake ukaanza kunoga na kudhihirika maana sasa alianza
kuvaa vizuri na kuweka nywele vizuri, hata ngozi yake ikanawiri na mwili kujengeka.


Sasa hata Haruna alijiona kwa hakika kuwa kumbe kwenye suala la mke alikuwa
kaopoa kwelikweli.


….……………
Basi siku moja, bosi Sadro aliandaa hafla ya kuukaribisha mwaka kwaajili ya
wafanyakazi wa kampuni yake ya ‘Prompt Tranfers’, na pia kwaajili ya wadau
mbalimbali wenye ushawishi kama vile wanasiasa, wasanii, wafanyabiashara wezake
na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Mualiko huo ulihusisha pia wenza wa wafanyakazi wa kampuni yake.

Hivyo
Haruna alimbeba mkewe, bi Zara na kwenda nae kwenye hafla hiyo, ambayo ilikuwa
imehudhuriwa na watu wenye nyadhifa na ushawishi na nafasi kubwa.


Sherehe hiyo ilimfungua macho kwelikweli Zara. Hakuwahi kwenye maisha yake
kudhani kuwa yeye, angeweza kuwa kwenye kutaniko kama la hafla ya aina hiyo.


Hafla ilikuwa imesheheni wakurugenzi na mameneja wa makampuni, viongozi wa
wizara mbalimbali. Kila upande aliogeuza uso macho yake aliona mtu aliyemfahamu
kupitia kwenye tivii.

Zara akaanza kuona kuwa sasa maisha alikuwa anayafumua na alikuwa anaelekea
kwenye nchi ya ahadi ya ndoto zake za mafanikio, ndoto alizokuwa nazo toka
alipokuwa binti mdogo akikua huko mitaa ya kigogo.


Zara alikuwa na ndoto kubwa za kufanikiwa na kuishi maisha mazuri. Ila hakuwa
akifanya vizuri shule na hata akaishia kidato cha nne kwa kufeli kwa sifuri kabisa.
Kwa muda mrefu aliishi kwa kutojiamini hadi pale mume wake, bwana Haruna
alipoanza kufanikiwa na kubadilisha maisha yao kabisa.


Ila sasa, usiku huo ulikuja kumtengeneza Zara mpya. Usiku ule wa kwenye
sherehe wa kukutana na watu wakubwawakubwa ulimfanya Zara asisimke toka
moyoni kwa hisia za ndani kabisa kuwa na yeye anataka kufanikiwa kwelikweli
kwenye maisha.


Wakiwa kwenye sherehe hiyo, Haruna na mkewe waliweza kusalimiana na Sadro
na mkewe. Mke wa bwana Sadro, aliitwa Shirah. Tofauti kabisa na ambavyo pengine
ingetegemewa kuwa Shirah angeweza kuwa mwanamke mwenye jeuri kutokana na
mafanikio ya familia aliyoko, mke wa Sadro alikuwa akiongea kwa namna ya
kinyenyekevu na alionekana kuwa mwema.
Wakati Haruna anamtambulisha mkewe bi Zara kwa bosi Sadro na mkewe, bwana
Sadro alinotisi uzuri wa Zara. Ghafla kwenye ubongo wake akajiambia, “wow, huyu ni
mwanamke mzuri sana”, mara akajikuta anamuuliza Zara jina lake tena hapohapo
waliposimama na wenzi wao, “samahani umesema unaitwa nani?”, nae Haruna
kabla mkewe hajajibu swali hilo akaingilia na kujibu yeye, “anaitwa Zara”, alisema
Haruna huku meno yote kakenua kisha akachukua mkono na kuweka begani kwa
Zara.


Sadro alikuwa akitenda kama mume aliyejivunia mkewe, akimtambulisha kwa bosi
wake na mkewe. Asichokuwa akikielewa ni kwamba, bosi wake alikuwa kamtamani
mkewe pale pale.


Palepale waliposimama kusalimiana, bi Shirah akamuuliza Zara anafanya shughuli
gani, na Zara akajibu kuwa anafanya biashara ya nguo, kitu ambacho Shirah
alifurahia kwa maana hiyo ilikuwa ni moja ya biashara alizofanya na akamwambia
Zara kuwa atamualika atembelee ofisi yake siku moja. Basi baada ya salamu hizo
wakaagana.


Usiku wa siku hiyo, Zara hakupata usingizi haraka, kichwa chake kiliwaza yeye
kufanikiwa tu, aliwaza sana juu ya watu aliokutana nao, hasa bwana Sadro, bosi wa
mume wake na mkewe bi Shirah, Zara alijikuta akitamani maisha yao.


Alitamani vile walivyokuwa, wanamiliki kampuni kubwa, wameajiri watu kibao,
wananyenyekewa na wafanyakazi wao, wanahusudiwa na watu wengine
waliofanikiwa pia. Zara alitamani yeye siku moja awe na mafanikio ama aishi maisha
ya aina hiyo.


Ila chini kabisa, chini kabisa ya uvungu wa ubongo wake pia alikuwa anamuwaza
bwana Sadro. Kwa namna ya ajabu sana alihisi kuwa jamaa huyo alikuwa amempiga
jicho fulani hivi la kumtamani, kipindi anasalimiana nae, ila hakuwa na uhakika na
akawa anajiambia kuwa huenda ni mawazo yake tu, pengine ndio uangaliaji wake.


Lakini bado, kichwani mwake kama angeamua kujisemea za ukweli kabisa bila
kujidanganya lililo moyoni mwake, basi Zara angejitamkia usiku uleule pale kitandani
alipolala chali huku akitazama dari la nyumba, kuwa ni kwamba yeye mwenyewe
alikuwa amemtamani bwana Sadro.


Wakati Zara akiwaza hayo usiku huo kitandani badala ya kutafuta usingizi na
kulala, mume wake, bwana Haruna alikuwa kalala fofofo pembeni yake, hana habari
kuwa kumbe mwenza wake alikuwa kwenye dimbwi lenye kina kirefu cha kutamani
maisha ya wengine na pengine kumtamani mwanaume mwengine.


Basi, kama kilichokuwa kinatokea kwenye kitanda cha wanandoa Zara na Haruna,
ndicho hicho hicho pia kilikuwa kinatokea kwenye kitanda ndoa ya bwana Sadro na
mkewe bi Shirah.


Bi Shirah akiwa amelala fofofo, mume wake ambaye alikuwa pembeni hapohapo
kitandani alikuwa kalala chali hana hata dalili ya usingizi huku akiwa anaangalia dari
la chumba chao. Kichwani mwake bwana Sadro kulikuwa hakuna anachowaza zaidi
ya uzuri wa mke wa Haruna, mke wa mfanyakazi wake.


Akili yake iliwaza na kuwazua akikukumbuka uzuri wa Zara. Alikumbuka umbile
lake na jinsi alivyopendeza usiku ule. Alikumbuka midomo yake ilivyong’ara kwa
rangi nyekundu. Alikumbuka sauti yake nzuri na ngozi yake mwororo.


Ila tofauti na Zara ambaye hakujitamkia ukweli kwa nafsi yake mwenyewe kuwa
amemtamani bwana Sadro. Sadro mwenyewe bila kusita alijisanua ya kwamba,
amemtamani Zara. Alijiambia moyoni, “mtoto mzuri kama Zara ameopolewaje na
mtu kama Haruna, haki ya Mungu nitampata”, alijiapia Sadro nafsini mwake.
 
Basi wiki kadhaa baadae Shirah alimualika Zara atembelee ofisi yake. Ilikuwa ni
ofisi iliyoendesha maduka kadhaa kwenye ‘mall’ kubwa iliyoitwa Mzizima City.


Mahala hapo palikuwa mashuhuhuri jiji zima, watu mashuhuri na wenye uwezo
walikuwa wakifika kwenye maduka yake na kufanya manunuzi ama kutazama sinema.
Zara alifurahi kufika mahala hapo, na kuanza kufikiria ingekuwaje kama ni yeye
ndiye ambaye angekuwa na maduka mahala hapo. Alimuonea wivu Shirah kuwa
alikuwa anamiliki maduka katika eneo la hadhi ya juu kama hapo.


Siku hiyo Shirah alikuwa amemualika Zara ili kumtambulisha kwenye kikundi cha
wanawake wafanyabiashara ambacho alikuwa anakiongoza kilichoitwa ‘Super Ladies’,
ambacho kilikuwa na lengo la kufundishana mambo mbalimbali na kutoa misaada
kwenye jamii kwa watu wenye uhitaji.
Zara alijiona sasa kweli anatoboa maana wanawake aliokutana nao walikuwa ni
wenye mafanikio makubwa ambayo hakufikia hata robo ila aliyatamani. Aliona kuwa
yuko kwenye kikundi sahihi cha wanawake.
Ulimwengu wa wanawake waliokuwa kwenye kikundi cha ‘Super Ladies’, ulikuwa
ni wa mbali na wa tofauti kabisa na ule ambao Zara alikokulia.


Basi kikao kilipoisha, Zara alimshukuru sana Shirah kwa kumualika, kisha akaaga
na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake. Aliingia kwenye lifti na kushuka hadi
sakafu ya kwanza ya jengo, na kisha kutoka kwenye lifti alipofika kwenye eneo la
mapokezi alimuona bwana Sadro yuko hapo akiongea na simu. Sadro alikuwa
amevalia suti, kwa kumtazama tu alionekana ni mtu mwenye mamlaka.
Zara alijikuta mapigo yake ya moyo yakimdunda kwa kumuona Sadro mahala
pale, kichwani mwake alijiambia kuwa bosi huyo alikuwa anavutia sana.


Mara Sadro nae akamaliza kuongea na simu na kugeuka upande aliokuwapo Zara,
na macho yao yakagongana. Wote kwa pamoja wakabaki wanaangaliana. Kisha kila
mmoja akaweka tabasamu usoni na wakasalimiana.


“Habari shemeji, mimi ni Zara mke wa Haruna Nzowa”, alisalimia Zara huku
akinyoosha mkono wake wa kulia kwa Sadro, naye akaupokea mkono huo, wakawa
wameshikana na akajibu salamu yake, “Nakukumbuka vizuri, tulikutana kwenye
sherehe ya kuukaribisha mwaka”.


Kwa muda huo mfupi tu, Sadro alipitisha macho yake usoni mwa Zara na kuona
uzuri wa mwanamke huyo, kuanzia macho yake, midomo, umbile la uso, akashusha
macho chini na kumtathmini muonekano wa mwili wake mzima.

Kwa sekunde kadhaa Sadro alijikuta kama haelewi kilichokuwa kinaendelea
mahala hapo aliganda tu anamtazama Zara machoni huku kaushikilia mkono wake,
alikuwa kapigwa na bum buwazi, hadi kwa mbali aliposikia sauti ya Zara ikimuita,
“shemeji, shemeji”, aliita Zara.
Sadro akashtuka na kugundua kuwa alikuwa hajauachilia mkono wa Zara. Basi
akauachia mkono huo na akajibalaguza akisema, “aah, naelekea kwa mke wangu,
Shirah, ofisini kwake”, aliongea Sadro na Zara akajibu kuwa alikuwa anatoka kwenye
kikao kilichokuwa ofisini kwa Shirah. Kisha Zara akaaga na kuondoka mahala hapo.
Sadro akaelekea kwenye lifti ili kuelekea kwenye ofisi ya mke wake.
Sasa kichwani mwa Zara ikawa wazi kuwa anamtaka bwana Sadro. Njia nzima
akiwa kwenye gari aliyokodi alikuwa anawaza jinsi ambavyo jamaa alivyokuwa kama
kapigwa na bumbuwazi wakati alipompa mkono kumsalimia. Kichwani mwake Zara
akaanza kujiambia kuwa huenda sio yeye tu anamtaka bwana Sadro na huenda
jamaa anamtaka yeye pia.
….……………………………………….
Jioni ya siku hiyo mawazo ya Zara yalikuwa yote yako kwa bwana Sadro. Roho
yake ilikuwa imesahau uwepo wa mume wake kabisa. Sasa nafsini mwake akaanza
kudhamiria kuwa lazima ajaribu kuwa nae.
Akiwa kwenye meza ya chakula nyumbani kwake, majira ya usiku, Zara alichukua
simu yake na kuingia kwenye moja ya mitandao ya kijamii na kusachi jina la Sadro
Bilali, na akapata akaunti ya jamaa huyo. Basi akatumia zaidi ya dakika arobaini na
tano akitazama tu picha zake.
Hatimaye akashindwa kuvumilia akajikuta ameingia kwenye ‘diem’ ya jamaa na
kisha akajikuta akitaka kumuandikia meseji, ila mara roho yake ikawa inasitasita.
Ila hatimaye akaandika ujumbe, “hey, shemeji ni mimi Zara”, ila sasa akaogopa
kubofya ‘send’ akawa njiapanda, akijiuliza, je, amtumie jamaa hiyo meseji ama
asitume.


Wakati Zara akiwa anawaza juu ya Sadro nyumbani kwake, bosi Sadro
mwenyewe alikuwa nyumbani kwake pia mitaa ya Bahari Beach, pembeni ya bwawa
la kuogelea. Kichwani mwake, alikuwa anawaza jinsi alivyokutana na Zara pale eneo
la mapokezi kwenye jengo la ofisi ya mke wake.


Ilikuwa ni mara ya pili kwa Sadro kumuona Zara. Na safari hii alizidi kumuona
kuwa ni mwanamke mrembo kuliko alivyokuwa amemuona mara ya kwanza kwenye
usiku wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wiki kadhaa zilizopita.

Hakujali kabisa kuwa Zara alikuwa ni mke wa mtu, tena mke wa Haruna,
mfanyakazi wake kabisa kwenye kampuni yake. Hakujali juu ya maadili ya kijamii
yaliyoweka mwiko kutamani mke wa mtu, yeye alijali tu kuwa alikuwa amemtamani
mwanamke huyo na alijiona kuwa alikuwa anastahili kuwa na mwanamke huyo.


Basi akiwa hapo anawaza huku anabofya bofya mitandaoni kwenye simu yake,
mara akaona meseji imengia ‘diem’ , meseji ilikuwa imeandikwa, “hey, shemeji ni
mimi Zara”, kulaleki.


Sadro alishangaa. Hakutegemea kupokea meseji ya aina yoyote toka kwa Zara. Ila
akajikuta akiweka tabasamu usoni. Akawa amebaki anaisoma hiyo meseji mara
mbilimbili akijitafakari aijibu vipi hiyo meseji. Akajiuliza inakuwaje, mwanamke huyo
kuanza kumdiem yeye, akaona kazi yake inaanza kuwa rahisi.


Maana alikuwa akijiuliza atamuanzaje Zara, mwanamke huyo mrembo, mke wa
mtu na kumfungukia kuwa anamtaka, ila ni kama mambo yakawa yanajipa yenyewe
mpaka kaanza yeye mwenyewe kumchokonoa diem.


Basi wakati Sadro anashangaa meseji ya Zara, yeye Zara alikuwa bado yupo
kwenye meza ya chakula nyumbani kwake, mikono ikimtetemeka, akiwaza meseji
aliyotuma, akifikiria Sadro ataipokeaje hiyo meseji na ataichukuliaje. Akawa kabaki
anaitazama simu yake, huku akiwa haamini kuwa alifanya alichokifanya.


Mara meseji ikaingia, ilikuwa ni ya kutoka kwa Sadro ikisoma, “aha, safi tu
shemeji. Nilifurahi kukuona tena pale mapokezi”, Zara akajikuta anatoa tabasamu.
Aliona kuwa walau meseji yake ilikuwa imejibiwa, yeye alihofia pengine isingejibiwa.
Basi mimeno yote ikawa imemtoka Zara. Hakuwa na haya kabisa. Roho yake
ilikuwa imedhamiria kabisa kutenda usaliti aliokuwa akielekea kuutenda. Alijisahau
kabisa kuwa alikuwa ni mke wa mtu. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Sadro, mtu
ambaye pia alikuwa ana mke wake.
Meseji ya pili ikaingia kwenye simu ya Zara, ikitokea kwa Sadro ikisomeka,
“Halafu unajua we ni mwanamke mzuri sana”. Zara alipoisoma hiyo meseji aliacha
mdomo wazi. Hakuamini kuwa kapokea meseji kama hiyo toka kwa Sadro. Alijisikia
raha kusifiwa uzuri. Hakuwa na haya hata kidogo.


Wakati Zara yuko kwake akiwa haamini kuwa Sadro alikuwa kamtumia meseji
isemayo kuwa yeye ni mwanamke mzuri sana, Sadro mwenyewe alikuwa bado
nyumbani kwake pale pembeni kwenye bwawa la kuogelea, huku akiwa anasoma
mara mbili ile mesejei aliyotuma kwa Zara.
Kichwani mwake aliwaza mwanamke huyo ataitafsiri vipi meseji hiyo. Ila hakuwa
na wasiwasi wowote.

Vyovyote Zara atakavyoipokea meseji aliyomtumia, haikuwa
shida kwake kwa maana mwanamke huyo ndiye alikuwa wa mwanzo kumtafuta yeye
na kumdiem.

Mara meseji ikaingia kwenye simu ya Sadro ikisomeka, “Hata wewe shemeji ni
mwanaume mzuri sana”, asalale.

Sadro alikenua meno, akainuka toka alipokaa
akaingia sebuleni kwake hadi kwenye kabati lake alilohifadhi mvinyo na akatoa
mvinyo akamimina kwenye glasi na kuanza kunywa.


Moyoni mwake alifurahi sana. Aliona kazi imekwisha lazima atampata tu Zara,
akajisemea, “huyu lazima nimle”. Jamaa alikuwa muhuni kinyama. Hakuogopa hata
mke wa mtu, hakujali kabisa.


Tena hadi hapo aliona huyo Zara alikuwa kajilengesha mwenyewe kudadeki.
Hakuogopa wala kujali juu ya Haruna. Hakujali kijana wa watu angejisikiaje ikiwa
atajua kuwa bosi wake na mkewe wanatongozana. Hakuogopa wala hakujali mkewe
bi Shirah angejisikiaje kama angejua yeye Sadro anatongozana na mke wa
mfanyakazi wake.


Basi Sadro akachukua tena simu yake na kutuma meseji nyingine iliyosomeka,
“naomba usiniite shemeji, niite tu Sadro”, akawa anaangalia hiyo meseji itajibiwaje,
mara meseji ikaingia kwenye simu yake ikisema, “okay, nitakuita hivyo”.


Baada ya meseji hiyo Sadro akaandika meseji nyengine na ilisomeka, “kusema za
ukweli kabisa, nimetokea kukupenda Zara”. Sasa Sadro akaikazia macho simu na
kuondoa tabasamu, ilikuwa ni kama muda wa uchinjaji wakati huo. Alitaka aone
atajibiwa vipi meseji hiyo. Alitaka Zara ajibu hiyo meseji kuwa hana noma ili amalize
kazi kabisa.


Na kweli, meseji ikaingia kwenye simu ya Sadro iliyosomeka, “mmh, ila hata mimi,
nimetokea kukupenda” , kulaleki.
Ilikuwa ni mbuzi kafia kwa muuza supu. Basi Sadro alinyanyua mvinyo wake na
kunywa. Moyoni akijisemea, “kazi imekwisha”.
Basi wakati huohuo, Zara alikuwa sebuleni kwake, huku akiwa anapitiapitia
meseji alizokuwa anatumiana na Sadro. Alikuwa mimeno yake yote nje,kwa roho
yake ya usaliti. Yani hakuwa na haya wala hakuogopa. Alidhamiria kabisa kuwa
atasaliti ndoa yake. Mwenyewe moyoni mwake alijiona kuwa yuko kwenye penzi
jipya.


Mara Haruna akaingia ndani, alikuwa anarejea toka kazini na kumkuta mke wake
amesiamama sebuleni na simu yake iko mikononi, akamkumbatia na kumpiga busu
shavuni na kuanza kumuuliza habari za siku hiyo. Masikini hakujua kuwa mkewe
tangu hapo alikuwa keshabadilika, hakuwa yule mke muaminifu aliyekuwa kafunga
nae ndoa miaka miwili iliyopita.
….………………………………………….

Basi mahusiano ya kisaliti baina ya Sadro Bilali na Zara yakaanza. Mara kibao
walikuwa wakiongea ama kuchati pamoja kupitia simu zao. Ni kama walikuwa
wamesahau kuwa wao walikuwa na ndoa zao na kwamba walichokuwa wakikifanya
kilikuwa ni usaliti kwenye ndoa zao na wenza wao wangeumizwa na kitendo chao
hicho.


Basi mazoea yao ya kuwasiliana yakakomaa, ikapita miezi kama mitatu hivi
wakiwa bado wanawasiliana kwa simu. Kila mmoja kati yao akaanza kuwaza hatua
inayofuata, je, watawezaje kukutana ana kwa ana na kufanya yao.


Sadro aliona kuwa ana suluhu ya shida hiyo, mara moja akampa kazi Haruna
asafiri kwenda nchini Komoro, katika mji wa Moroni ambako kampuni yake ilikuwa
imefungua ofisi mpya. Kazi hiyo ilikuwa ni ya wiki mbili, hivyo ndani ya wiki mbili,
Haruna angekuwa hayupo Dar es Salaam na hivyo wao huku bongo wangekuwa
wako huru kufanya uchafu wao wote.


Na kweli, Haruna maskini hakuwa na hili wala lile, alipopewa taarifa kuwa
anatakiwa asafiri kikazi kuelekea Komoro, alifurahia sana safari hiyo ya kikazi. Ilikuwa
ni mara yake ya kwanza kusafiri kwenda nje ya nchi na alikuwa amesikia sifa nyingi
kuhusiana na nchi ya Komoro, hivyo aliondoka nchini meno yote kayakenua kumbe
nyuma mali yake yaibiwa.


Basi siku ya kufanya usaliti wao ikawadia. Sadro akaagiza Zara akodi nyumba
kwenye huduma za ‘Air bnb’, ili wakutane huko, akidai kuwa yeye hawezi kukodi
kwasababu jina lake ni maarufu hivyo isije kutokea mtu akagundua nyendo zao.
Basi Zara nae bila hata kujishtukia, mke wa mtu kabisa akabuku nyumba kwenye
‘Air bnb’ nyumba yenyewe ilikuwa pande za Kigamboni, mbali kabisa na maeneo ya
Makongo alipoishi.


Majira ya saa moja usiku, yalimkuta Zara yupo huko kigamboni, kwenye nyumba
aliyokodisha. Nyumba yenyewe ilikuwa ni nzuri, ya ghorofa, ya kisasa, yenye bustani
na kutokea kwenye baraza ya juu ya nyumba maji ya bahari yalionekana, mawimbi
yake yakiwa yanasukumwa na upepo ambao ulileta kaubaridi barazani hapo.
Basi Sadro aliwasili na gari yake aina ya ‘Nissan Dualis’, ambayo ilikuwa ni gari
isiyojulikana na watu wengi waliomfahamu. Lengo hasa ilikuwa ni kutotambulika
kiurahisi. Kumbe akili bado zilikuwepo kidogo, alikuwa kumbe kwa mbaali bado
anaogopa kupata skendo ya kutembea na mke wa mtu.


Basi Sadro alifika kwenye nyumba ambayo Zara kakodi. Zara akaenda kumpokea
yeye mwenyewe, hakutaka walinzi wa hapo waongee nae, asijetokea mmoja wao
akamtambua kuwa ni Sadro Bilali aliyekuja kulala hapo.

Basi lengo la Zara lilifanikiwa. Zara alipojitokeza tu kumpokea mgeni wake,
mlinzi hakujisumbua kusogelea gari kuhoji lolote, aliendelea na mambo yake. Ilikuwa
kawaida kwa walinzi kupokea wageni wa aina hiyo ambao lengo lao la kukodi
nyumba hasa lilikuwa ni kupata tu faragha ya kufanya mambo yao ya sirini.


Mguu kwa mguu, Sadro na Zara waliongoza njia mpaka kwenye sebule ya
nyumba hiyo. Zara alikuwa kaweka mvinyo kwenye meza ya sebuleni hapo. Na
walipofika sebuleni Zara alimimina mvinyo kwenye glasi mbili zilizokuwapo hapo,
moja akampa Sadro na moja akaanza kunywa yeye.


Basi wakawa wamesimama wanatazamana kimahaba. Zara alikuwa anapendeza
sana usiku huo. Nywele zake ndefu alikuwa kazimwaga, midomo yake ilikuwa na
shedo nyekundu. Nyusi zake alizijaza wanja, nguo aliyovaa ilikuwa imemshika vizuri
mwilini, huku akiwa amejipulizia marashi yaliyonukia vizuri sana, yani kwa kifupi Zara
alikuwa kaupania usiku wa siku hiyo.


Basi Sadro alimtazama Zara kwa macho ya kumtamani kuanzia chini mpaka juu.
Akajikuta akinyoosha mikono yake na kuiweka kiunoni mwake, kisha akamkamatia
na akamvutia kwake, nakumkumbatia, na akajikuta akiweka midomo yake kwenye
midomo ya Zara na kuanza kumbusu.
Mara Zara akajitoa mwilini mwa Sadro. Akafungua nguo zake na kuzitupa chini.
Alikuwa amevalia nguo za ndani nyeusi, zile za kisasa zile wanazovaaga wazungu,
wenyewe wanita ‘lingerie’’, yani alikuwa kajipanga, mpaka Sadro mwenyewe
alikubali kuwa haikuwa mchezo.


Sidiria ilikuwa imeyabeba vizuri manyonyo ya Zara, huku nguo ya chini ilikuwa
imeendana vyema na shepu yake. Kidogo Sadro miudenda imtoke.
Mara Zara akasogea karibu na Sadro, akatupia mikono kifuani kwake akaanza
kumfungua vifungo vya shati, akamvua shati na kulitupia kule, akamvua singlendi
akaitupia kule. Akachukua mkono wake akaukamta mkanda wa kiunoni akamvutia
kwake akaanza kumfungua mkanda na kumvua suruali akaitupia kule, jamaa akabaki
na boksa.


Basi Zara akamshika Sadro mkono wa kulia na kuanza kumvuta kuelekea
chumbani. Kilichofuata huko ilikuwa ni mechi, usawa wa mchuano wa Yanga na
Simba kwenye ligi kuu Tanzania bara.
….……………………………………………
 
Basi hali ikawa ndio hivyo. Wiki mbili zile, ambazo Haruna alikuwa yuko Moroni,
nchini Komoro, mke wake na bosi wake, waliendelea kufanya ufuska, tena uliokuwa
unazidiana kila siku.


Yani kila siku ambayo walikuwa wananyanduana, basi kanuni yao ilikuwa ni moja
tu, mnyanduano lazima uwe mkali kuliko wa siku iliyopita. Yani walikuwa wanafanya
kukomesha. Kama jana walifanya hivi juu ya meza kesho ilikuwa lazima wafanye vile
sakafuni, kesho kutwa wanafanya vile jikoni, siku inayofuata lazima wafanye tukio
bafuni.


Yani ilikuwa ni vuruguvurugu kwenye hiyo nyumba ya ‘Air bnb’, waliyokodi huko
Kigamboni. Zara na Sadro walikuwa wameamua kuwa wanafanya usaliti kwa wenza
wao. Na kwa kweli walikuwa wanaufanya usaliti huo kwa nguvu zote za miili yao.
….………………………


Shirah, mke wa Haruna alianza kuhisi mume wake ana ahusiano na mwanamke
mwengine. Aliona tu jinsi ratiba zake zilivyobadilika alikuwa nyumbani harudi.

Mara
nyengine wakiwa kwenye tukio la maana alimuona jinsi jamaa alivyokuwa yuko bize
na simu akichekacheka na huyo aliyekuwa akichati nae. Mara nyingine alikuwa
Shirah akiwa yuko sebuleni na alimuona Sadro kupitia dirishani, akiwa barazani
mbele ya nyumba akiongea na simu huku akichekacheka. Moja kwa moja aling’amua
jamaa ana mwanamke mwengine.


Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Shirah kugundua kuwa mume wake alikuwa
na mwanamke mwengine. Sadro hakuwahi kuwa muaminifu kwenye ndoa yao
ambayo ilikuwa ina miaka mitano tu hadi wakati huo.


Mara ya mwisho kumfumania mume wake Shirah aliona kuwa amedhalilika sana,
aligombana na huyo mwanamke, na huyo mwanamke alikuwa ana mdomo mchafu
akamtukana matusi ya nguoni.


Shirah alishaamua kipindi hicho kuwa ataomba talaka toka kwa Sadro. Lakini
hakufanya hivyo, kwasababu ndoa yake hiyo ilikuwa inahusisha familia zao mbili
katika makubaliano maalum, hivyo hangeweza kuivunja tu hiyo ndoa.
Basi jioni moja, Sadro alikuwa anarejea toka Kigamboni, alifika chumbani kwake
na kumkuta Shiraha akiwa amekaa kitandani akimtazama. Sadro akasogea hadi
kwenye kitanda na kukaa.


Shirah akawa anamuangalia mume wake, na akaanza kumuongelesha akisema,
“Sadro una mwanamke mpya”, Sadro hakujibu, alimgeukia Shirah na kumtazama,
naye Shirah akaendelea kuongea, “tabia yako umeianza upya”, aliongea Shirah.

Sadro hakupinga, akabaki kutazama pembeni, bila ya woga wala kutaka kujitetea.
Shirah akaendelea, “Sadro najua haunipendi kimapenzi, ni sababu za kifamilia ndio
zilipekea ndoa hii. Ndio maana mwezangu huachi matendo yako ya kifuska na mimi
hilo nishalikubali kuwa hauna mapenzi na mimi na mimi wala sifosi mapenzi kwako.


Ila tu tofauti yako na mimi ni kwamba mimi angalau sina michepuko najitahidi
kulinda heshima ya ndoa yetu”.

Shirah akasimama toka kitandani, “Na hatimaye hata mimi naona hii ndoa yetu
sio kitu cha kukipigania, hatupendani, tuko tu pamoja kwaajili ya kufurahisha na
kufanikisha malengo ya biashara na mahusiano ya wazazi wetu”.


Shirah akaanza kuvuta mashuka ya kujifunika pamoja na mito, na kuendelea
kuongea, “Nahamia kwenye chumba kingine, nitakuwa nalala huko”, aliongea Shirah
na kuelekea mlango wa chumba na kuufungua na kutoka na kuelekea kwenye
chumba kingine kwenye nyumba yao na kulala huko.


Yani maisha ya Sadro na mkewe Shirah yalikuwa ni ajabu sana. Walikuwa wenza
wa ndoa, na walifunga ndoa yao miaka mitano iliyopita, ila ndoa yao ilikuwa na kisa
cha aina yake.


Shirah kama ilivyo kwa Sadro alikuwa ni binti toka familia kitajiri. Baba yake
aliitwa Mzee Chande. Alikuwa mfanyabiashara maarufu aliyemiliki viwanda vya
kutengeneza maji ya kunywa pamoja na maduka ya ‘Super market’ katika maeneo
kadhaa jijini na mikoa mingine.


Babake Shirah, Mzee Chande na babake Sadro, Mzee Madaraka Bilali walikuwa ni
mrafiki wakubwa toka utotoni, walisoma pamoja na kukua pamoja mitaa ya Upanga
huko miaka ya 1980. Urafiki wa wazee hao uliwafanya washibane sana hata
wakaamua kuwa ndugu kabisa kwa kuwafanya watoto wao Shirah na Sadro waoane.


Nao Shirah na Sadro walikubali kufunga ndoa hiyo ilhali wakijua kabisa
hawapendani. Ila kila mmoja wao kwa wakati ule waliokuwa wanafunga ndoa, alitaka
aaminiwe kwenye familia zao ili akabidhiwe biashara za kusimamia.


Hivyo waliona ndoa yao ilikuwa tiketi ya wazazi wao kuwaona sasa wamekuwa
na wanaweza kuendesha maisha yao wenyewe na kwamba hata biashara kubwa za
familia wangeweza kupewa na wakaweza kuzisimamia.


Na kweli baada tu ya ndoa yao, Shirah alipewa majukumu ya kuendesha
maduka kadhaa ya babake yaliko eneo la ‘Mzizma City’, ili ayasimamie, naye Sadro
akaachiwa acheze nafasi kubwa katika kuongoza kampuni za babake, hata akaweza
kufungua kampuni yake mwenyewe ya ‘Prompt Transfers’, ambayo ilikuwa ikifanya
vyema sana.


Hayo ndiyo yaliyokuwa maisha ya Shirah na mume wake Sadro. Kwa nje
walionekana kuwa wao ni wanandoa waliopendezana sana. Ila kwa ndani walikuwa
hawana mapenzi baina yao. Walikuwa pamoja kwasababu tofauti kabisa na
kupendana…………………………………………………………………………………………………………………
…………………………………….….………..INAENDELEA……………
 
Wadau mnaopenda hadithi karibuni kusoma hadithi yangu hii
 
Back
Top Bottom