Simulizi - change (badiliko)

big up! author. hisia zangu ni kwamba dolnad ndio jambazi au jitu linaloua watu. na ndo aliekuwa anamfatilia namouh toka mwanzo walipokuwa wamesisima mvua. lakini sijui kwanini alimuoa namouh.
😂😂😂😂 achana na hisia mkuu wewe endelea kumfutilia Elton Tonny tu.
Asante Mkuu kwa similizi yenye kuvuta utulivu wa akili. 🙏
 
CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

Enjoy!

★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA ISHIRINI

★★★★★★★★★★★★★

Namouih akabaki kumtazama tu kimaswali, naye Suleiman akafungua mlango wa gari hilo na kushuka, akiwa anamwangalia mke wa mwajiri wake kwa njia ya kawaida tu.

"Suleiman! Unafanya nini?" Namouih akauliza kwa uthabiti.

"Habari za saa hizi madam?" Suleiman akamsalimu.

"Hujasikia nilichouliza au?"

"Nimesikia..."

"Sasa?"

"Niko hapa kukulinda madam."

"Excuse me?"

Suleiman akabaki kimya.

"Kuni... kunilindaje? Yaani... unanifatilia kwenye gari lingine ili kunilinda? Nani amekwambia ufanye
hivyo?"

Suleiman akaendelea kumwangalia tu.

"Suleiman sitaki dharau. Nikikuuliza swali nijibu," Namouih akasema kwa hisia kali.

"Ni boss ndiyo ameniagiza nikufate... nihakikishe unakuwa salama," Suleiman akamwambia.

"Ahah... hivi kweli... yaani umekosa kazi ya kufanya?"

"Hii ndiyo kazi yangu madam."

"Wewe ni mtumishi wake, siyo wangu mimi. Naomba tuheshimiane. Unanifatilia namna hiyo, ningekuitia polisi je? Unani... mnafanya haya bila mimi kujua inaleta faida gani?"

"Ni ili uwe salama...."

"Usalama kutokana na nini? Naomba mwambie... oh God! Okay. Unataka kuhakikisha niko salama si ndiyo? Haya twende. Twende nifate," Namouih akamwamuru mwanaume huyo.

Kisha mwanamke huyu akaanza kuelekea upande ule wenye jengo ambako ndiyo angemkuta Salome, na Suleiman akaanza kumfata pia. Namouih alikuwa amevaa gauni zuri sana na refu la rangi nyeupe lenye urembo wa maua-maua mengi mekundu, lililombana kiasi na kuchora umbo lake vyema nyuma, hivyo Suleiman kumfatilia kwa nyuma akitembea kulimfanya mwanaume huyo aanze kumwangalia mke wa mwajiri wake kwa matamanio. Sikuzote Suleiman alikuwa mtu mmoja wa ukimya sana aliyetii kila jambo aliloambiwa kufanya na Efraim Donald, lakini Namouih hakuwahi kumpa mwanaume huyu umakini wake wa hata asilimia chache kwa hiyo kiukweli jambo hili lilimkera sana.

Wakawa wamefika kule ndani, na Namouih akawa amemwona Salome upande fulani akiwa ameketi kwenye meza ya wateja, na akimpungia mkono Namouih. Namouih akamfata mpaka hapo, naye Salome akasimama na wanawake hawa wakakumbatiana.

Walipoachiana, Namouih akamgeukia Suleiman na kusema, "Huyu ni Salome. Ndiyo mtu unayetakiwa kunilinda kutoka kwake. Umeelewa?"

Salome akakunja uso kimaswali, naye Suleiman akainamisha uso wake. Alikuwa anamkumbuka
Salome pia kwa sababu usiku ule wa sherehe aliwaona wote pamoja na Efraim Donald.

"Nakuomba urudi huko unakojua na usije kurudia kufanya hivi tena. Nitaongea na Efraim baadaye. Nenda," Namouih akamwambia Suleiman.

Mwanaume huyo akatii na kuondoka, naye Namouih akamwangalia Salome na kukuta anamtazama kwa njia iliyoonyesha wazi kwamba alikuwa haelewi kinachoendelea.

"Oh... sorry kwa hilo. Yaani siwezi kuendesha siku moja bila kukutana na kitu chenye kukwaza," Namouih akamwambia.

"Ni nani huyo?" Salome akauliza huku wote wakiketi sasa.

"Ni... kama chauffeur wa mume wangu... alikuwa ananifatilia ili kunilinda eti... yaani jamani!"

"Hahahah.... Mume wako hataki uibiwe na vibenteni eeh?"

"Siyo hivyo, ni basi tu hiyo ishu ya juzi me kupotea kidogo ndiyo eti inamfanya afikiri nahitaji kutendewa kama yai vile."

"Mume wako ana degree kubwa sana ya upendo kwako eti Namouih?"

"Ndiyo alivyo. Yuko protective sana, lakini siyo mtu mwenye gubu. Ananipenda, nampenda, sema bado kuna mambo mengi ambayo... huwa yanakatisha tamaa," Namouih akasema kwa hisia.

"Mhm... inaonekana ni vitu serious. Mimi niliachika kwa mume wangu sababu mambo mengi tulikuwa hatuelewani. Inapendeza sana nikiona mwanaume anamtendea mke wake kama wa kwako anavyokutendea... lakini wewe ni kama vile inakukera. Kuna vitu fulani bado hakutimizii?" Salome akauliza.

Namouih akashusha pumzi na kutikisa kichwa kukubali.

"Ah... samahani yaani, nimekimbilia huko hata sijakuagizia kinywaji..."

"Hapana, haina shida. Hata hivyo najua unahitaji kurudi kazini kwa hiyo hatutatumia muda mwingi. Nilihitaji tu kama... kaushauri maana... ahah... hali yangu inashangaza kidogo," Namouih akasema.

"Ndiyo... ni sawa. Niambie. Unapitia nini rafiki yangu?"

"Sijui nikwambieje. Hivi... ungeshauri nini kama tuseme... labda mwanaume anakuwa anashindwa
au hampi mke wake haki yake ya ndoa... wewe unafikiri ni mambo gani yanayosababisha hali hiyo?" Namouih akauliza.

"Mmm... ni vitu vingi, kwa hiyo inategemea na hali halisi ya kile kinachoendelea ndani ya ndoa. Mimi siyo expert wa masuala ya ndoa ila kidaktari zaidi naweza kusema labda ni zile hali mara nyingi zinazosababishwa na mtu kuishiwa hamu ya kutaka mapenzi au kutoa mapenzi baada ya kukaa na mwenzi kwa kipindi kirefu... au ndo masuala ya ku-cheat, vitu kama hivyo... inategemea na kinachoendelea. Kwa hiyo kama ni ushauri, naweza kusema la muhimu ni kwa wenzi kuongea, wafunguke kuhusu mambo wanayotaka na wasiyotaka, labda hiyo italeta faida kwa sababu mahitaji yao wote yanakuwa wazi kwa mmoja na mwenzake wakishaongea," Salome akamweleza.

"Natamani hata kwa hali yangu ingekuwa namna hiyo lakini yaani hata sielewi..."

"Kuna tatizo la namna hiyo kwenye ndoa yako Namouih?"

"Ndiyo Salome. Toka Efraim amenioa hajawahi kushiriki nami tendo la ndoa," Namouih akasema.

"Yaani hata mara moja?!"

"Ndiyo."

"Kwa nini?"

"Shida ndiyo hiyo. Hakuna sababu. Hanisemeshi kuhusiana na hilo Salome yaani, nimejaribu mara nyingi sana kuligusia lakini ni kama hajali... siwezi hata kujua kama labda ana tatizo fulani la kiafya lililofichika maana rekodi zake zote ni safi. Hadi huwa tunagombana yaani kwa sababu inaonekana ni kama vile namlazimisha, sijui ana shida gani..."

"Pole sana Namouih..."

"Unajua jinsi ilivyo ngumu kwa mwanamke... kumtaka mwanaume wake halafu akawa anapewa rejection tu..."

"Ndiyo, naelewa."

"Sasa... nakuwa najiuliza sijui nifanye nini. Ahah... kuna siku hadi nikamwambia naweza nikatoka nje nikakutana na limtu litakalonitimizia haja zangu..." Salome akacheka.

"Maana ni kama yeye ameshindwa yaani..."

"Ahahah... atakuua ukifanya hiyo kitu!"

"Na alikuwa mkali kweli niliposema hivyo..."

"Ndiyo maana kumbe kamweka hadi na bodyguard wake akufatilie?"

"Agh, utamweza!"

"Ahah... kwa kweli ina... nitumie neno gani yaani... huwa inachosha," Salome akamwambia.

"Kabisa," Namouih akasema.

"Kama hadi na maongezi yanashindikana, unahisi hii itaelekea wapi?"

"Yaani hata sielewi. Tumekutana na matatizo mengi hapa katikati, vioja, vikwazo, lakini tunaendelea kusonga mbele... ila hiyo haimaanishi nimeridhika. Maneno ya watu kwamba siwezi kuzaa wala nini yanakuwa yanaonekana kwamba ni kweli, na hiyo ni kwa sababu tu mume wangu hana hata time kucheza kidogo na mimi... ni zaidi ya mwaka, unaweza kuamini?" Namouih
akasema kwa hisia.

Salome akatikisa kichwa kwa kusikitika.

"Ndiyo hivyo. Nimeshaanza kuhisi kukata tamaa kiasi kwamba sasa hivi mtu akija kuniambia nitoke na hao vibenteni unaowasema, naweza nikakubali... wakati ni jambo ambalo sikuwahi kufikiria kabisa," Namouih akaongea kwa huzuni.

Salome akakishika kiganja chake na kusema, "Pole dear. Nakuona kama mdogo wangu yaani anayehitaji msaada sana lakini mimi nakuwa siwezi kutoa unaostahili."

Namouih akatabasamu kwa mbali na kumwangalia.

"Kama mume wako hakupi sababu, basi itakuwa ni juu yako kufanya maamuzi yatakayokupa faida. Ila yasiwe mabaya maana inaweza kusababisha shida. Kikubwa ni maongezi tu Namouih. Una-time
wakati mzuri sana ili uongee naye kwa njia nzuri, akuelewe, ili kama ikiwezekana na yeye afunguke... naona anakupenda, sidhani kama hili litakuwa jambo la... milele kwenye ndoa yenu. Ni kama tuseme unapokuwa unampenda mtu ambaye ni rafiki lakini yeye hajui, au labda anajua lakini hakutilii maanani. Anayepaswa kupiga hatua ya kwanza ni wewe, siyo? Eee... kwa sababu kuna hiki kitu kwamba unaweza kukuta kweli hataki kukubali kuwa nawe, lakini anashindwa kukwambia abda kwa kuwa anahofia atakupoteza kama rafiki. Wewe ndiyo unatakiwa umwonyeshe kwamba una uimara, kwamba utamwonyesha kuelewa hata kama ataamua kinyume na unavyotazamia..."

Maneno hayo ya Salome yalimgusa sana Namouih, naye akaangalia chini akiwa anayatafakari kwa kina.

"Ndivyo ilivyo hata kwa mume wako. Ikiwa maongezi yatagonga mwamba hata baada ya kujitahidi kumwonyesha uelewa, basi amua utakachoona kuwa sahihi, lakini uwe mwangalifu kisije kukuumiza au kuwaumiza nyie wote," Salome akamalizia.

Namouih akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa na kusema, "Asante sana Salome. Uko vizuri
sana... nilihitaji mno maneno kama haya."

"Karibu dear. Ila bado tuna muda wa kutosha kuendelea kuzungumza kwa hiyo jisikie huru kabisa kufunguka mpenzi," Salome akamwambia.

Namouih akatabasamu, na wanawake hawa wakaendelea kuongea kuhusu mambo mengi ya
maisha na kutiana moyo kwa maneno mazuri sana; hasa kutoka kwa Salome. Walitumia kama saa
zima na nusu hapo, na ndipo Salome akahitaji kurudi kazini hatimaye. Wakanyanyuka pamoja na kwenda nje, wakiwa wanaongelea uwezekano wa Salome kuja kwenda kumtembelea Namouih nyumbani kwake kwa sababu mwanamke huyu alikuwa anataka kumkaribisha, na Salome alikuwa anahitaji kuangalia ratiba yake ili aamue siku ambayo ingefaa halafu ndiyo amjulishe rafiki yake huyo.

Kwa hiyo wakaachana baada ya hapo, Salome akielekea upande mwingine wa jiji, na Namouih
akielekea upande ambao ungempeleka kule msituni ili akakutane na Draxton.

★★

Dakika kadhaa kupita, Namouih akawa bado mwendoni kuelekea kule msituni huku akiendesha gari lake kwa umakini. Umakini katika maana ya kwamba alikuwa anaangalia endapo kama na wakati huu angekuwa anafatiliwa, kwa hiyo alifanya kama kuzunguka-zuguka kwanza badala ya kwenda moja kwa moja huko ili awe na uhakika kwamba hakuwa na kupe mkiani. Wakati huu ni kweli hakuona nuksi yoyote, kwa hiyo akaingia zake huko msituni na kuelekea kwenye nyumba ya Draxton, lakini bado akiwa makini.

Ikiwa imefika mida ya saa tisa alasiri sasa, hali ya hewa kuzungukia maeneo ya huku ilikuwa ya wingu lililotanda, tofauti na maeneo ya jijini, na ni kweli haingechukua muda mrefu sana na mvua zingeanza kunyesha kwa kuwa misimu ilikuwa karibu kubadilika. Bila shaka maeneo ya huku ndiyo zingeanza mapema kutokana na miti kuwa mingi, na ndiyo maana Draxton alikuwa amekuja kuiimarisha nyumba yake kwa ajili ya hilo. Namouih alipoifikia nyumba hiyo aliweza kumwona
Draxton akiwa amepanda kwa juu, kama vile anapigilia misumari sehemu iliyoifunika nyumba, bila
shaka akiziba sehemu ambazo zingepitisha maji.

Mwanamke akashuka kutoka ndani ya gari lake na kuanza kuelekea huko, na alipofika karibu na nyumba hiyo, Draxton akaacha kufanya kazi yake na kumpungia mkono kutokea hapo juu, na Namouih akampungia mkono pia. Kwa kushangaza kiasi, mwanaume huyo akaruka kutoka huko mpaka chini na kusimama wima, na jambo hilo likafanya Namouih atabasamu kidogo. Draxton
alikuwa amevaa T-shirt nyepesi yenye rangi nyeusi iliyokuwa na mikono kifupi, suruali ya kijani ya
mazoezi (track) na viatu vyeupe vya mazoezi.

Akawa anamtazama Namouih kwa njia ya kawaida, kisha akasema, "Karibu."

"Asante. Haujaumia miguu?" Namouih akauliza.

"Ahah... la, niko sawa," Draxton akajibu.

"Hongera. Unaipenda kweli nyumba yako," Namouih akamwambia.

"Yeah, haka kambibi kamesimama hapa kwa muda mrefu. Mara kwa mara nahitaji kuka-treat kidogo ili kajisikie vizuri," Draxton akaongea kiutani.

"Ahahahah... kambibi kako," Namouih akasema.

Draxton akatabasamu na kuiangalia nyumba hiyo.

"Blandina ameniambia kwamba ulienda kumwona leo asubuhi... asante Draxton," Namouih akasema.

"Usijali. Nilihitaji sana kufanya hivyo pia maana roho ilikuwa inaniuma... sikutaka aanze kunichukia ila nilimlazimu yaani..."

"Hapana, hawezi kukuchukia... unajua anakupenda sana..."

Namouih akasema hivyo huku akianza kumfata.

"Sitaki kuwa mbeya lakini nahitaji nikwambie kuwa amesema ulipoenda hiyo asubuhi na
kumwambia unabaki... alikuwa anatamani akukumbatie kabisa, ila hana uhakika kama hata hicho ni kitu unachotaka... kwa hiyo nakushauri tu ujitahidi kuyajenga naye Draxton hata kama.... ni
vigumu... angalau kidogo tu," Namouih akasema kwa ushawishi.

Alikuwa amemkaribia Draxton zaidi sasa, na mwanaume huyu akapiga hatua mbili kurudi nyuma huku akionekana kufanya ile kawaida yake ya kufumba macho taratibu na kuinamisha uso wake. Leo ndiyo siku ambayo Namouih alitaka kujua hiyo ilimaanisha nini.

Draxton akaacha kufanya hivyo na kuanza kuigeukia tena nyumba yake huku akisema, "Sawa Namouih, nitajitahidi. Twende ndani tafadh...."

"Draxton..." Namouih akamkatisha.

Draxton akamgeukia na kumtazama machoni.

"Kwa nini huwa unafanya hivyo?" Namouih akauliza kwa sauti ya chini.

"Kufanya nini?" Draxton akauliza pia kwa upole.

"Kila mara... nikikusogelea... unainamisha uso wako kama vile... kuna kitu kinakusumbua yaani... huwa haupendi nikikusogelea eh?" Namouih akauliza.

"La, si hivyo Namouih. Hhh... sijui nisemeje... samahani kwa kukufanya uhisi vibaya... iko tu nje ya uwezo wangu..." Draxton akamwambia.

"Unamaanisha nini?"

"Upande wangu wa pili una nguvu kama kwa mnyama wa kawaida... kama kusikia mbali, na kuvuta harufu za vitu au watu... kama mbwa tu. Hata nikiwa hivi kawaida ninakuwa na huo uwezo pia,"
Draxton akamwambia.

"Oooh harufu... kumbe unakuwa unavuta harufu yangu?"

"Ndiyo."

"Ahahahah... sawa. Me nikafikiri labda ni shida... lakini bado inakuwa kama tatizo vile maana unajivuta sana nikusogelea... ina maana marashi yangu yanakupa effect fulani nzito au?"

"La, siyo marashi. Ni harufu YAKO," Draxton akamwambia.

Namouih akakunja uso kimaswali.

"Kila mtu ana harufu yake. Ninaweza kutofautisha watu kwa harufu zao... na... wewe harufu yako... kwangu ni nzuri sana... nakuwa nashindwa kujizuia... kuihisi..." Draxton akaongea hivyo huku anamwangalia kwa umakini machoni.

Namouih akaachwa kinywa wazi kiasi baada ya kusikia maneno hayo, huku anamwangalia machoni kama anajaribu kuyaelewa maneno hayo kwa undani.

Draxton akaacha kumtazama na kusema, "Tunaweza kwenda ndani?"

"Ndiyo, tunaweza," Namouih akajibu.

Draxton akatangulia kwenda huko, na kwa sekunde chache Namouih akabaki kusimama hapo kama vile bado anamtafakari mwanaume huyo, kisha naye akaelekea ndani taratibu na kufikia kukaa kwenye sofa moja. Draxton yeye alikuwa amekaa kwenye mkono wa sofa la upande
mwingine hivyo alikuwa kwa juu kidogo.

"Umeshapata chakula?" Draxton akauliza.

"Nilikunywa chai ya kutosha saa nne, so bado niko full, mpaka baadaye," Namouih akajibu.

"Sawa."

"Huwa unaleta chakula huku unakula mwenywe tu eti?"

"Ndiyo, huwa napika hapo... nakula," Draxton akajibu.

"Wewe unajua kupika?"

"Yeah."

Namouih akamtazama kwa yale macho ya kuhukumu.

"Ahahahah... nini sasa?" Draxton akauliza.

"Siwezi kuamini mpaka nije nione. Nani alikufundisha kupika?" Namouih akauliza.

"Mama yangu," Draxton akasema.

"Oooh..."

"Yeah. Mara nyingi kama alihisi njaa angeniambia 'Max, make some omelette.' 'Max, your lady needs a stomach leisure,'" Draxton akasema na kucheka kidogo.

Namouih akacheka pia, naye Draxton akabaki kutabasamu.

"Mlikuwa karibu eeh?" Namouih akauliza.

"Sana. Huwa namkumbuka sana..." Draxton akasema kwa hisia.

"Ni yeye mwenyewe tu ndiye aliyekuita kwa jina la Max?" Namouih akauliza.

Draxton akatikisa kichwa kukubali.

Namouih akawa anamtazama kwa hisia sana, akiona aina fulani ya simanzi la mbali usoni mwake.

"Vipi ukiniuliza maswali ya wakati huu? Bila shaka unayo mengi," Draxton akamwambia.

"Aam... ndiyo, nina maswali mengi..."

"Haya niko kizimbani sasa," Draxton akasema kiutani.

Namouih akacheka kidogo, kisha akasema, "Kuna siku fulani, mimi na Blandina tulikuwa barabarani, akagonga mtu... mweupe. Niliona tattoo fulani ambayo... mgongoni kwake... na wewe unayo. Are you one and the same?" Draxton akatikisa kichwa kukubali.

"Kwa hiyo unapoanza kubadilika, mwili wako unakuwa mweupe kama wa mzungu afu'... ukirudi unakuwa na ngozi hii ya kawaida?"

"Ndiyo. Sijui ni kwa nini lakini naweza kukisia kwamba hilo linahusiana na heritage ya wazazi wangu. Mama alikuwa mweusi, baba mweupe. Alipochanganya vitu vyake vya kitaalamu ndiyo ikawa kama hivi... ila sina uhakika kwa njia gani," Draxton akamwambia.

"Oooh...."

"Yeah. Nikianza kubadilika nakuwa mweupe, nikirudi kawaida nakuwa hivi. Lakini nywele za kichwani huwa zinabaki kuwa nyeupe, kwa hiyo inanibidi ninyoe na kupaka dawa ili... nisionekane kuwa babu," Draxton akasema.

"Ahahahah.... mbabu," Namouih akasema kiutani.

Draxton akatabasamu pia.

"Okay. Halafu... siku ile tumekugonga usiku ulikuwa unafanya nini? Maana haukuwa hata na nguo... mwili mzima," Namouih akauliza.

Draxton akatulia kidogo, kisha akasema, "Njoo. Nifate."

Mwanaume akaanza kuondoka kuelekea nje, naye Namouih akanyanyuka na kumfata bila kuelewa angeongozwa kwenda wapi. Wakatoka upande huo wa nyumba na kuelekea sehemu za nyuma,
wakiingia msituni zaidi. Ingawa hakuelewa kikamili kwa nini aliletwa huku, Namouih alikuwa na imani kwamba Draxton angempa jibu lililopita matarajio yake, hivyo angetakiwa kuwa tayari kwa ajili ya lolote ambalo angesikia au kuona. Wakafika kwenye eneo lenye miti mingi mikubwa zaidi ya ile waliyoipita kuzungukia msitu wote, naye Namouih akasimama na kupatazama kwa umakini. Miti miwili ilifungwa kwa minyororo mizito sana sehemu za shina, naye Draxton akafika hapo na kuunyanyua mmoja, kisha akamwangalia Namouih.

"Kuna nyakati ambazo huyu mnyama hulazimisha kutoka, na inakuwa labda ili apate chakula au... fujo tu. Nilijifunza kutabiri wakati ambao angejaribu ku-force kutoka, na mimi nikaamua kuwa nahakikisha kwamba muda huo ukifika ninakuwa sehemu anayotakiwa kuwa. Hapa ndiyo hiyo sehemu. Huwa nakuja, najifunga minyororo mikononi, shingoni, na miguuni halafu natulia. Chakula nakuwa nimeshakiweka hapo ili yeye akitoka minyororo inamzuia kwenda mbali, lakini atakula na kutulia mpaka napokuja kuamka asubuhi nikiwa mimi," Draxton akaeleza.

Namouih kiukweli hakuwa ameelewa jambo lolote alilosema mwanaume huyo, naye akabaki kumtazama tu usoni.

Draxton akauachia mnyororo, kisha akasema, "Usiku mlionigonga kwa gari, ndiyo nilikuwa nimeanza kubadilika, lakini sikuwa nimeifikia minyororo mapema hapa, kwa hiyo sikufanikiwa kujifunga haraka. Sikumbuki kilichoendelea, lakini inaonekana akili yangu ilipoingiliana na ya upande wangu wa pili nilianza kukimbia ovyo ovyo mpaka nilipofika huko barabarani... na nyie ndiyo mkanigonga. Hapo ndiyo mkafanya nikaishia katikati ya badiliko langu."

"Katikati ya badiliko?" Namouih akauliza.

Draxton akaanza kumfata mpaka alipofikia mbele yake na kusimama, kisha akasema, "Kuna mimi, kawaida. Ninapobadilika kabisa kuwa mnyama, hiyo ni mbaya. Lakini kuna wakati huwa naishia katikati ya hiyo kawaida na mbaya, kwa hiyo ni kama nakuwa nusu-mwanadamu, nusu-mnyama."

"Na hapo bado unakuwa huwezi kuji-control?" Namouih akauliza kwa sauti ya chini.

"Ni tofauti. Hapo nakuwa naona mambo kama mwanadamu, lakini nitatenda kama mnyama... hasa
nikikorofika. Kwa kipindi fulani nilijaribu kutafuta njia ya kuji-control nikiwa hivyo, lakini siyo rahisi kwa sababu ningepitiliza na kuwa mnyama kabisa. Angalau kwa usiku huo mlisaidia nikarudi huku mimi mwenyewe la sivyo kama ningefika mbali na kugeuka mnyama... mabaya mengi yangetokea," Draxton akaongea huku ametazama chini.

"Kwa hiyo unasema asante kwa sababu tulikugonga kwa gari?" Namouih akauliza.

"Ndiyo," Draxton akajibu.

Namouih akaangalia chini kwa ufupi, kisha akamtazama tena na kuuliza, "Huwa unamwekea chakula gani... huyo jamaa?"

Draxton akatabasamu kwa mbali na kusema, "Nyama. Huwa naenda machinjioni, nanunua hata mbuzi mzima namleta hapa, asubuhi nakuta mifupa."

Namouih akapandisha nyusi kwa mshangao kiasi, kisha akauliza, "Kila siku?"

"La. Hii huwa inatokea mara chache sana. Inaweza kutokea kila mwezi mara moja au hata baada ya miezi kadhaa. Vipi, ulikuwa unafikiri nabeba watu kila siku kama chakula?"

"Ahahah... siyo hivyo. Ila ungenilaumu kama ningefikiria namna hiyo?"

Draxton akatikisa kichwa kukanusha.

"Maisha yako ni ya ajabu sana," Namouih akasema.

Draxton akainamisha uso wake na kutikisa kichwa kukubali.

"Sawa. Okay... really Draxton, bado nina maswali mengi sana sijui kama...."

"Usijali, nitakujibu. Twende nikakuwekee na biskuti," Draxton akamwambia.



Namouih akatabasamu na kukubali, kisha wawili hawa wakaanza kurudi kule kwenye nyumba. Draxton alikuwa ananwambia jinsi ambavyo msitu huo ulikuwa mkubwa tofauti na namna ulivyoonekana, na wengi waliupuuzia tu ndiyo maana ilikuwa finyu sana kwa watu kuja huku mpaka kuifikia nyumba yake iliyojificha. Namouih akaketi kwenye sofa tena baada ya kufika ndani, naye Draxton akampatia boksi la biskuti.

"Eet Sum Moore," Namouih akasoma maandishi kwenye boksi hilo.

"Ushawahi kula?" Draxton akauliza.

"Ndiyo, ni nzuri. Nasma anazipenda. Mdogo wangu," Namouih akamwambia.

Draxton akaonyesha kuelewa, kisha akaketi kwenye sofa la pembeni.
Namouih akatoa biskuti mbili na kumpatia, naye Draxton akapokea. Wote wakatafuna kipande kimoja huku wakiangaliana, naye Namouih akatabasamu kidogo.

"Ungependa kujua nini kingine kuhusu mimi?" Draxton akauliza.

"Aam... Una mambo mengi sana ambayo kwa njia kubwa yanastaajabisha. Nakuwa na maswali mengi kiasi kwamba mpaka nashindwa kujua ikiwa mengine ni sahihi kukuuliza," Namouih akasema.

Draxton akatabasamu kiasi na kuuliza, "Toka umejua nina miaka 95 nimekufanya unione kama mbabu fulani hivi... grumpy eti?"

"Ahahahah... hapana, kawaida tu. Una sura changa sana na pigo za ujana mpaka huwa nasahau we' ni mbabu," Namouih akamwambia.

Draxton akatabasamu tu na kutafuna biskuti.

Wakatazamana kwa ufupi, kisha Namouih akauliza, "Ulizaliwa wapi?"

"Tusla. Ipo Oklahoma, Marekani," Draxton akajibu.

"Umeishi kwenye nchi nyingi eeh?"

"Siyo nyingi sana. Venezuela na Tanzania ndiyo nimeishi kwa muda mrefu zaidi."

"Ulikuja Tanzania mwaka gani?"

"1990."

"Ahah... me ndiyo nazaliwa!" Namouih akasema kwa shauku.

Draxton akatabasamu.

"Wazazi wako wote walikuwa ni wataalamu wa masuala ya wanyama?" Namouih akauliza.

"No. Mama yangu alikuwa akifanya kazi kwenye kituo cha redio huko Los Angeles... California. Alikuja kukutana na baba, wakapendana, baadaye ndiyo baba yangu akamhusisha kwenye suala la... you know. Mama alikubali kujitoa kwa ajili ya jaribio, na ikafanikiwa. Baba aliongea na vichwa vikuu kule alikokuwa ameajiriwa kuwaambia kuhusu mimi, lakini hawakumwamini... hasa kwa sababu jambo hilo alilifanyia nje ya kazi zao rasmi. Ila kuna rafiki yake mmoja alionyesha kumwamini, na ndiyo akampa muda wa kuhakikisha anakuja kutoa uthibitisho halisi kwamba alifanikiwa, ikimaanisha mimi nizaliwe..."

"Subiri, unamaanisha kwamba, bado ulikuwa hujazaliwa baba yako alipoongea na hao wakuu?"

"Ndiyo, yaani... alikuwa ndiyo amefanikiwa kumfanya mama atungishe yai langu kupitia njia fulani
ajuayo baba pekee... yaani hakuna mtu mwingine anayejua. Ingetakiwa nizaliwe ili uthibitisho uonekane wazi, lakini kuna jambo lilizuka. Kuna hali ya kutoelewana ilitokea baina ya baba na hao wakuu, kwa hiyo akanitorosha mimi na mama ili tuwe salama," Draxton akaeleza.

"Inaonekana hao watu walitaka tu kuja kukutumia kama kifaa cha experiment... wakumiliki yaani,
wakutendee kama specimen za maabara tu..." Namouih akasema.

"Yeah."

"Okay. Kwa hiyo ulikuja kujua hayo ukiwa na miaka mingapi?"

"10."

"Mama yako ndiyo alikwambia kila kitu?"

"Ndiyo."

"Aliitwa nani?"

Draxton akatabasamu kwa mbali na kusema, "Ivy."

Namouih akatabasamu pia, kisha akauliza, "Na baba yako? Mliishi pamoja baada ya kutoroka?"

Draxton akatikisa kichwa kukanusha huku akisema, "Sikuwahi hata kumjua personally. Zaidi niliona tu picha zake, habari zake, basi. Hatukuwahi hata kuongea kwa sababu alikufa nikiwa na miaka
miwili."

Namouih akamtazama kwa hisia, kisha akauliza, "Na mama yako?"

"Alikufa nilipofikisha miaka 25. Cancer. Kuanzia hapo ni kama sikuendelea kukua tena."

"Pole Draxton."

"Asante. Miaka 70 imepita lakini bado hicho ni kitu kinachoniumiza sana. Hangetakiwa kufa."

"Draxton kuna vitu huwa tu ni lazima vitokee, na wewe haungeweza kum...."

"Ningeweza Namouih... ningeweza. Sema tu sikujua jinsi gani," Draxton akamkatisha.

"Unamaanisha nini?" Namouih akauliza.

Draxton akamtazama na kusema, "Damu yangu... damu yangu ina uwezo wa kuponya."

Namouih akakaza macho kimaswali.

"Sikuzote mama alipojiumiza vibaya, au mimi kumuumiza, ningetumia damu yangu ku-heal majeraha yake. Angeniambia mara kadhaa kwamba baba alisema damu yangu ina uwezo hata wa kuzuia kifo, lakini hakuwahi kumwambia jinsi gani," Draxton akamwambia.

"Mh! Kiukweli Draxton unazidi kunishangaza sana. We' ni kiumbe wa aina gani?"

"Ningekuwa najua ningesema, lakini mpaka leo sijajua baba alifanya nini kunitengeneza namna hii. Hiyo ndiyo njia niliyotumia kuponya vidonda vyako ulipoumia ule usiku."

"Oh! Yeah, ndiyo, nakumbuka nilishangaa kukuta sina hata mkwaruzo. Aisee! Kwa hiyo unanipaka damu yako kwenye kidonda halafu kinapona... Draxton huo ni muujiza!"

"La, Namouih, siyo kitu kizuri. Mwanzoni kinaweza kuonekana kuwa, lakini siyo..."

"Kwa nini useme hivyo?"

"Kwa sababu sina uhakika inakuwa na effect gani mwilini mwa mtu mwingine... endapo itazidi. Mama yangu alipougua sana, nilidhani damu yangu ingeweza kuuondoa ugonjwa wake, ili kuthibitisha theory ya baba kwamba naweza kuzuia hata kifo... lakini nilipompa... ndiyo
akazidiwa..." Draxton akamwambia huku ameangalia chini.

"Ulifanyaje?"

Draxton akabaki kimya.

"Ulimpa anywe? Ulimpa anywe damu yako?"

Draxton akamwangalia tu usoni.

"Na ilikuwa ni yeye ndiyo alikwambia umpe, siyo?"

"Tubadili mada Namouih," Draxton akasema.

"Draxton nisikilize, haikuwa makosa yako..."

"Namouih please... inatosha. Sitazungumzia hilo tena," Draxton akamwambia hivyo na kunyanyuka.

Namouih akanyanyuka pia na kumsogelea, kisha akamshika mikononi na kusema, "Draxton..."

"Samahani Namouih, sikutakiwa kuongelea hilo. Naomba uniulize kitu kingine tofauti na...."

"Draxton nisikilize. Nakuelewa. Nakuelewa vizuri sana. Baba yangu aliugua saratani pia, na hakuna kitu kilichokuwa kizito kwangu kuliko fikira za hatia kila mara nilipohisi kushindwa kumsaidia. Sijilinganishi na wewe, lakini unatakiwa ujue kwamba jitihada zozote ulizofanya kwa mama yako zilikuwa za upendo, na bila shaka alizithamini aana. Nakuomba tu usijichukie kwa kilichompata," Namouih akasema kwa upole.

"Namouih... siwezi kulinganisha hali yangu na ya mtu yeyote yule kwa sababu mimi siyo mtu mzuri.
Kujichukia ni lazima...."

"Hapana Draxton, wewe ni mtu mzuri. Usingekubali kubaki kunisaidia endapo kama usingekuwa na moyo wenye kujali. Ningekuwa nimeshakufa kama ungetaka kuniua lakini hukufanya hivyo. Nimeshatambua kinachokusumbua Draxton. Ni chuki. Chuki dhidi yako wewe mwenyewe. Unajichukia sana mpaka unatafuta njia zozote kujiondoa duniani lakini usiendelee kujichukia namna hiyo. Umepewa baraka kubwa sana kuwa na maisha marefu. Ithamini Draxton," Namouih
akaongea kwa upole.

"Baraka? Jinsi hii? Nageuka kuwa mnyama mkatili anayeweza kuua watu.... hii siyo baraka Namouih. Ni laana," Draxton akasema kwa mkazo.

"No..." Namouih akasema hivyo kwa hisia na kupandisha kiganja chake mpaka shingoni kwa Draxton, akiishika kwa wepesi na vidole vyake laini.

Draxton akamtazama kimshangao kiasi, akiwa hajatarajia jambo hilo.

"Siyo laana Draxton. Sijui kwa nini maisha yako hivi ila kwa kila mtu yana kusudi fulani. Labda ni kwa sababu unajichukia sana ndiyo maana upande wako wa pili unapambana nawe mpaka leo, kwa sababu unauona tu kama kitu kinachohitaji kuondolewa. Sijui sana kuhusu yale uliyopitia mpaka leo, ila ninajua wewe ni mtu mzuri. Nakuamini Draxton," Namouih akaongea hayo huku bado akiwa ameishika shingo ya mwanaume huyo.

Draxton akafumba macho taratibu na kuinamisha uso wake, akifanya ile kawaida ya kuvuta harufu nzuri ya Namouih kwa ukaribu, naye Namouih akaondoa mkono wake shingoni kwake baada ya kutambua kwamba bado alikuwa amemshika namna hiyo, lakini hakusogea nyuma na kubaki amemwangalia tu.

"Kwa nini Namouih? Kwa nini unaniamini wakati mimi ni kitu chenye kutisha?" Draxton akauliza
huku akiwa ameinamisha uso wake bado.

"Ni kwa sababu sasa hivi sikuoni kuwa mtu anayetisha. Mambo fulani kuhusu wewe... yanaendana na mambo fulani kuhusu mimi. So I can relate," Namouih akasema kwa sauti ya chini.

Draxton akamtazama machoni kwa umakini, naye Namouih akawa anamwangalia sana pia.

Kuna hisia fulani mpya iliyokuwa imeanza kujijenga ndani ya hali hii, hisia ambayo hata wao hawakuielewa vizuri, na ilikuwa kwa sababu wote walifanana kwenye baadhi ya mambo yaliyohusu maisha yao ingawa kwa njia tofauti. Simu ya Namouih ikaanza kutoa mlio wa kuita, na macho yake yakashtuka kidogo kutokana na kuzubaa kiasi alipokuwa anamwangalia Draxton, kisha akaitoa mfukoni mwa suruali yake. Haikuwa ikiita kwamba amepigiwa na mtu, kwa sababu mtandao haukufika vizuri maeneo ya huku, bali ilikuwa ni kengele ndogo aliyokuwa ametegesha awali, yaani
"alarm." Ilikuwa ikimkumbusha kwamba muda wa kuondoka ulikuwa umewadia.

"Aam... Draxton... nina... appointment fulani kikazi...."

"Usijali. Unaweza kwenda."

"Hatujatumia hata muda kidogo kumzungumzia Felix... am sorry kwa kuuliza maswali mengine tu...."

"Ni sawa Namouih, tutakutana tena. Nashukuru kwa maneno yako. Wahi tu, tutawasiliana," Draxton
akamwambia.

Namouih akamtazama kiufupi, kisha akageuka na kuifata pochi yake aliyokuwa ameiacha kwenye sofa. "Ukiipaka rangi hii nyumba itapendeza sana," akamwambia Draxton baada ya kumgeukia.

"Ndiyo. Sema, sitaki kuvuta attention ndiyo maana inatakiwa kuonekana kama haionekani," Draxton akasema.

Namouih akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, kisha akaanza kuelekea nje huku Draxton akimfata
taratibu. Namouih alikuwa akitembea kulielekea gari lake huku akajiuliza ni nini kilichomsukuma na
kumpa ujasiri mpaka akamshika mwanaume huyo shingoni na kumsemesha kwa ukaribu mno. Hii
haikuonekana kuwa ni kwa sababu tu mambo yao yalifanana, bali kwamba alikuwa ameanza kumjali sana. Hawakuongea lolote mpaka walipolifikia gari la bibie, naye akafungua mlango na kumwangalia Draxton, aliyekuwa amesimama mbele ya gari.

"Angalia usigonge nyau," Draxton akamwambia kiutani.

Namouih akacheka kidogo huku akiwa amefumba mdomo, kisha akatikisa kichwa kukubali na kuingia ndani ya gari lake. Akashika usukani na kumtazama sana Draxton pale nje akiwaza vitu vingi, huku mwanaume akiwa amenyanyua kiganja chake juu kumpa kwa heri, kisha mwanamke
akaliondoa gari hapo na kuelekea jijini hatimaye.

★★

Baada ya Namouih kuondoka msituni huko, alielekea moja kwa moja nyumbani kwake. Siyo kwamba alikuwa anaenda kukutana na mtu yeyote kama alivyomwambia Draxton ila alisema hivyo kama kigezo tu cha kumruhusu aondoke mapema kwa kuwa sasa alikuwa amejua kwamba mume wake alimfatilia. Kwa hiyo alikuja kufika nyumbani mida ya saa kumi na mbili jioni, naye akakuta gari la Efraim Donald likiwa nyumbani tayari kumaanisha aliwahi kurudi siku hii. Bado Namouih alikumbuka vyema jinsi alivyoudhika sana baada ya kumkamata Suleiman anamfatilia muda fulani mapema ya leo, hivyo alijua angetakiwa kuongea na mume wake kuhusiana na hilo; lakini kama tu mambo mengine, kwa njia nzuri.

Akafika ndani na kumkuta Efraim Donald akiwa ameketi na Suleiman wakitazama mechi pamoja, na baada ya Efraim kumwona mke wake, akasimama na kumwambia aende hapo ili wakae wote. Namouih akamwangalia tu yeye na Suleiman, kisha akaanza kuzielekea ngazi na kupandisha juu kwenda chumbani bila kuwasemesha lolote. Efraim Donald akaamua kumfata mke wake huko huko ili wazungumze vizuri maana aliona bado alikuwa amekerwa sana. Akaingia chumbani na kumkuta Namouih anaongea na simu yake, naye akamsikia akisema kwamba atakutana na huyo mtu muda si mrefu, kisha akakata na kuanza kuvua hereni.

Efraim Donald akamsogelea na kusimama karibu yake, lakini Namouih hakumwangalia hata
kidogo, naye akasema, "Unaondoka tena?"

Namouih akatoa mguno wa kukubali huku akiendelea kufungua hereni.

"Unaenda wapi?" Efraim akauliza.

"Nakutana na Blandina. Tuna maongezi," Namouih akajibu.

"Mbona unaingia ndani nakusemesha hata huitikii?" Efraim Donald akauliza.

Namouih akamwangalia usoni na kusema, "Samahani."

Efraim Donald akakunja uso kimaswali, kisha akauliza, "Umekuwaje?"

"We' kwani unanionaje?" Namouih akauliza kwa ustaarabu tu.

"Okay, najua umekasirika kwa sababu ya Suleiman... lakini Namouih nilikuwa nataka kuhakikisha uko sawa. Mambo mengi mabaya yanaweza kutokea..."

Namouih akawa anamwangalia tu usoni.

"Kwa nini unaniangalia hivyo?" Efraim akauliza.

Namouih akamsogelea karibu zaidi na kuishika kola ya T-shirt aliyovaa kama anaitengeneza. Efraim Donald alikuwa amechanganywa kidogo na hali hii iliyokuwa inaendelea.

"Efraim... ninajua unanipenda. Na umeonyesha upendo wako kwangu kwa njia nyingi sana ambazo
nathamini... haziwezi kulingana na aina yoyote ya fadhili nilizowahi kuonyeshwa kwenye mahusiano. Ninakupenda pia, lakini ninahitaji tu ujue kwamba kwa kipindi hiki... moyo wangu umekuwa ukihisi baridi kali sana, na hiyo ni kwa sababu wa kwako umeshindwa kunipatia joto
linalotakiwa ili nisiumie zaidi. Ninajua unaelewa ninachomaanisha. Moyo wangu unaelekea kuganda Efraim, na kwa sababu wewe ni kama umepuuzia hilo ingawa unaliona... itanibidi niangalie njia nyingine halali ya kuuokoa ili nisije kujipoteza kabisa..." Namouih akasema maneno hayo kwa hisia sana.

Efraim Donald alishangaa, naye akaanza kutikisa kichwa chake kama haamini kabisa kile alichotoka kusikia.

"Namouih! Unamaanisha nini kusema njia halali? Una... unaongelea talaka?!" Efraim Donald
akauliza kwa kutoamini.

Namouih akawa anamtazama kwa njia ya kawaida tu, kisha akasema, "Ulikuwa unasema nikupe muda, lakini muda umepita vya kutosha. Tutaliongelea hili suala vizuri zaidi kwa kuwa na mimi sasa nimekuweka wazi kuhusu kile nachofikiria. Naomba ukae utafakari maneno yangu ili tuje tuongee vizuri, lakini tafadhali usichukue muda mrefu... mume wangu."

Efraim Donald akabaki kumtazama kama vile ameduwaa, naye Namouih akampita na kwenda upande wa pili wa chumba, akianza kuvua nguo yake, kisha akaelekea bafuni kuoga. Mwanaume huyu akakaa kitandani akiwaza vitu vingi sana. Njia ya Namouih ya kuongea ilikuwa ya uhakika kabisa, yaani hakutania hata kidogo. Ikiwa kweli hakutaka kumpoteza mke wake angehitaji
kumwambia ni jambo gani lililokuwa linamsumbua mpaka ashindwe kumpa haki yake, la sivyo,
angempoteza mwanamke huyo mzuri sana kwa talaka.


★★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★★


Usikose sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali ya CHANGE. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.

WhatsApp no: +255 678 017 280

e-mail: eltontonny72@gmail.com
 
CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

Enjoy!

★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA ISHIRINI NA MOJA

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Namouih akawa amemaliza kuoga na kuvaa kwa njia ya kawaida tu, kisha akaelekea kule chini ya nyumba ili kusaidiana na Esma kuandaa chakula kwa ajili ya jioni kwa kuwa alitaka sana kujishughulisha. Wakati huu Efraim Donald alikuwa amekaa tena sebuleni pale akiendelea kutazama mechi, na Suleiman alikuwa pamoja naye bado kama kumpa ushirika. Bado maneno ya mke wake yalitembea sana kichwani, na alikuwa ameshaanza kuwaza njia mbalimbali za kutafuta suluhisho kuelekea tatizo lake lakini hali hii kwa ujumla ilikuwa tata kuizungumzia kwa wakati huu,
kwa hiyo akawa ameamua kukaa kimya tu.

Namouih wa sasa alikuwa ametilia maanani maneno ya rafiki yake, Salome, kwamba afanye jambo
ambalo alijua lingempa faida yeye na mume wake ili kufanya uhusiano wao uwe bora. Hii bila shaka ingeonekana kuwa njia isiyo sahihi ya kutafuta suluhisho lakini alikuwa ana imani kwamba ingefanikiwa kwa kiwango kikubwa. Siyo kwamba alitaka kutalikiana na Efraim, ni kwamba alitaka mume wake aone namna uzito wa jambo hili ulivyokuwa mpaka kumfanya Namouih awaze kitu kama hicho, na huenda hiyo ingesaidia kumleta Efraim kwenye mwanga ili kweli hali ibadilike. Lakini endapo kama isingebadilika, basi kweli Namouih angechukua maamuzi hayo.

Kwa hiyo mwanamke huyu akaendelea tu kusaidizana na Esma huku wakipiga story huko jikoni
mpaka walipomaliza kutengeneza mlo mzuri, kisha naye akaelekea kwenye sofa na kuketi; akianza
kuperuzi mitandao ya kijamii. Efraim Donald alikuwa kimya tu, na Suleiman alihisi aibu maana
alielewa kwamba leo alitibua, lakini hakuna hata mmoja wao aliyeongea baada ya Namouih kukaa hapo. Mpira ukawa umeisha ilipofika saa mbili, na Namouih akanyanyuka na kwenda kusaidia kuandaa meza ya chakula ili waweze kula mapema tu. Bado wanandoa hawa hawakusemeshana lolote lile mpaka wanakaa mezani kula na kumaliza, kisha wakarudi kukaa kwa kutulia pale kwenye masofa.

Ndipo Efraim sasa akamuuliza Namouih alikuwa anaenda kukutana na Blandina wapi, na kwa sababu Namouih hakutaka kabisa masuala ya kuanza kuchokonolewa, akamwambia alikuwa anaenda kwake ili waongee maana rafiki yake bado hakuwa sawa sana kihisia na alihitaji rafiki. Efraim Donald akasema sawa, ampe salamu zake pia, ila akamwambia awe mwangalifu sana maana ni usiku, na kama ikiwezekana basi Suleiman amsindikize, lakini Namouih akamwangalia mume wake kwa jicho fulani lililomwambia Efraim Donald kwamba hiyo ilimaanisha HAPANA ya hefufi kubwa kabisa, kwa hiyo mume akaona atulize tu boli.

Ilipofika saa nne, Namouih akaingia chumbani tena na kuvaa nguo za mtoko; T-shirt nyepesi nyeusi yenye kubana na suruali ya jeans iliyobana pia yenye rangi ya blue na urembo wa kuchanika chanika mapajani, viatu virefu vyeupe, na nywele zake alizitengeneza kwa mtindo mzuri sana na kujipa mwonekano kama siyo mtu aliyetoka kwenda kwa rafiki yake tu bali kwenda kujiburudisha
sehemu fulani. Akabeba na pochi ndogo na kuanza kushuka ili aondoke, na baada ya Efraim
Donald kumwona, akamwangalia sana mpaka mke wake alipofika chini kabisa na kumuaga, akisema kama angechelewa sana basi angelala huko huko kwa Blandina, kisha akatoka na kuchukua gari lile aina ya Vanguard kama kawaida na kuondoka.

Efraim Donald akacheka kwa chini tu huku akitikisa kichwa kwa namna ambavyo mke wake huyo
alimwonyesha yuko makini na aliyoyafanya, na mwanaume huyu akabaki tu kutulia hapo nyumbani
kwake kama mtu asiyeelewa mambo yanayomzunguka vile, akijua wazi kwamba angetakiwa kumaliza kabisa suala lile Namouih alilozusha kwa njia ambayo ingeleta faida ili amtulize mke wake.

★★

Blandina alikuwa amekwenda sehemu ile waliyopenda kwenda mara nyingi na Namouih kupata
vinywaji na maongezi, na ndiko alikokuwa anamsubiri rafiki yake. Namouih hakumwambia mume wake kama alikuwa anakwenda sehemu ya hadharani kama hivi usiku maana alielewa angeanza mambo yake ya ubaniaji kwa kigezo cha kumlinda, lakini hata kama angetaka kumwambia kuhusu kuja huku angekuwa amefanya hivyo ila hakuona ulazima. Blandina alikuwa amependeza pia kwa kuvaa kigauni chepesi na kifupi chenye rangi mbalimbali kama upinde wa mvua, ambacho kama angekaa basi kimgevutika na kuacha sehemu kubwa ya mapaja yake wazi.
Mwanamke huyo tayari alikuwa amejiagizia vinywaji kadhaa na mishkaki ya ng'ombe, naye akawa
amekaa kivyake huku akiangalia namna watu walivyojiachia na wapenzi wao na wengine kupiga
midomo sana kutokana na utamu wa pombe.

Namouih akawa amefika hatimaye, naye akamfata Blandina sehemu aliyokuwa amekaa na kumkumbatia kwa furaha. Kama ilivyo kawaida, ujio wa mwanamke mrembo kama Namouih sehemu ya namna hiyo ulinyanyua macho ya wengi
kumwelekea, akionekana kuwa mrembo zaidi kuliko mwanamke yeyote aliyekuwa hapo. Yeye akaketi pembeni ya rafiki yake tu, na mhudumu akaja kumuuliza angependa kupata vinywaji gani.

"Ninaomba uniwekee Serengeti Lite 10 hapa kwenye meza tafadhali," Namouih akasema.

Blandina akakodoa macho kimshangao kiasi. Mhudumu yule akaondoka kwenda kufata vile
alivyoagizwa baada ya Namouih kumpatia pesa.

"Kumi? Utazimaliza zote?" Blandina akamuuliza.

"Eee... na we' mbona umechukua nne tu, ongeza zingine," Namouih akasema.

"Aam... sikupanga kunywa sana leo. Hilo vibe lote umelitoa wapi?"

"We' acha tu. Nataka nipige pombe hapa mpaka kieleweke usiku wa leo..."

Blandina akacheka kidogo.

"Halafu... Dantu na Marietta wanakuja kesho. Wamekwambia?" Namouih akamuuliza.

"Yeah, Dantu amenipigia simu mchana kuniambia. Tutakutana pale...."

"Zakhem..."

"Zakhem. Ni kitambo kweli, nimewamiss hao mashosti," Blandina akasema.

"Mimi pia. Angalau kesho tutaenda pamoja kupiga nao umbeya," Namouih akamwambia.

"Ahahahah... we' ulienda wapi leo?"

"Misele. Nilikutana na yule rafiki yangu niliyekwambia, Salome, akanipa-nipa advice na nini ndiyo...
nikarudi."

"Advice? Kama sikosei na wewe umevurugwa eeh?"

"Si sana, ila nilikuwa nataka tu kuziondoa stress. Speaking of sress, mambo yamekwendaje leo?"

Blandina akanywa fundo moja na kusema, "Kawaida tu. Nashukuru kwamba uliongea na Edward kwa ajili yangu yaani hiyo jana... nilipoteza akili nzuri kabisa."

"Vipi na leo Draxton alipokufata... hujanisimulia vizuri unajua, ilikuwaje?" Namouih akauliza.

Vinywaji kumi alivyokuwa ameagiza mwanamke huyo vikafikishwa na kuwekwa mbele yake, naye
akafunguliwa vitatu na kuanza kunywa taratibu.

"Alifika ghafla tu yaani... ndiyo nilikuwa nataka kuondoka. Akaanza kuomba samahani, anasema ooh hakutaka kuniumiza yaani ila anataka tu kunipa kilicho bora ili niridhike zaidi, unajua namna
anavyoongeaga its so... sweet," Blandina akasema.

Namouih akatabasamu.

"Nitakwambia ukweli yaani nilikuwa natamani hata nim... nimkumbatie, nimng'ang'anie, lakini tena kuna hii fikira ikawa inaniingia tu kunifanya nione kwamba huo ungekuwa ni upumbavu... maana inaonekana inamfurahisha sana mimi kuwa kama mpuuzi mbele yake..."

"Hapana Blandina... haiko hivyo..."

"We' utajuaje Nam? Yule me niko kwenye mahusiano naye yaani ni full kujivuta tu... haeleweki, haelezeki. Asa' kama leo asubuhi kaja anasema ananipenda, lakini anachotaka tu ni kuwa na hali ya amani kati yetu mimi na yeye baada ya kunifanya nilie kama mtoto mdogo... alikuwa anataka nimpe sadaka au? Anazidi kunichanganya tu Nam yaani... mpaka sielewi kwa nini inakuwa hivi... sijui amenifanya nini tu...."

"Unampenda, Blandina... hilo ni wazi. Bado unampenda sana. Nisikilize. Unahitaji- aaah!!"

Blandina akashtuka baada ya Namouih kutoa sauti hiyo kama ameumia, na ni wakati huo huochupa chache za vinywaji vyao zilidondoka chini na kupasuka kwa kuwa kuna mtu alikuwaamempamia kwa nguvu sana Namouih pale alipokuwa amekaa na kusababisha hilo litokee. Yaani Namouih alikuwa amepamiwa mgongoni kwa nguvu hivyo akawa amevisukuma vinywaji na
kuviangusha chini. Marafiki hawa wakatazama nyuma na kumwona mwanaume mfupi kiasi mwenye mwili mnene na imara akiwa ameshika sigara, na ndiyo huyo aliyempamia Namouih kutokana na yeye na wenzake watatu waliokuwa wanapita usawa huo kusukumana-sukumana kizembe na kwa sifa.

"We' mshenzi una kichaa?!" Namouih akauliza kwa jazba huku akisimama.

Wahudumu kadhaa walikuwa wameanza kufika hapo ili waisafishe sehemu hiyo, na yule mwanaume mfupi akamwambia Namouih, "Unamwita nani mshenzi, malaya wewe?"

Blandina akasimama na kumshika Namouih mikononi, akiwa anataka kumrudisha nyuma ili kuzuia ugomvi mkubwa kuanza.

"Wewe ndiyo mshenzi! Njia yote hiyo huko ukaona unilalie mimi tu?" Namouih akasema kwa ukali.

Rafiki za mwanaume huyo wakaanza kucheka, na mwanaume huyo akamwambia Namouih, "Nitakufanya kitu kibaya wewe mpumbavu usipofunga huo mdomo wako! Unafikiri najali hako kasura kako ka' mkorogo wa mavi?"

Wahudumu wakawa wanajaribu kutuliza hali hapo, naye Namouih akasema, "We' mpuuzi nini?
Nisipoongelea mdomo unataka niongelee mapua yako yaliyokaa kama kiti cha baiskeli au?"

"Basi Namouih, acha!" Blandina akajaribu kumzuia.

Namouih akasonya kwa hasira kwa sababu pombe ilikuwa imemwagikia nguo yake, na kwa sababu mwanaume yule alikuwa amekasirishwa sana na maneno ya ukali ya Namouih, akachukua chupa moja ya Serengeti na kumfata akiwa na lengo la kumpiga nayo kwa nguvu sana, lakini ni wakati huo huo Blandina alikuwa amefanikiwa kumvuta Namouih na kufanya mwili wake uingie sehemu aliyokuwa amesimama badala yake, hivyo chupa hiyo ikampiga Blandina vibaya sana pembeni ya kichwa chake!

Blandina alilia kwa sauti ya juu na kuanguka chini, na jambo hilo likaanzisha vurugu kwa baadhi ya
wanaume kujaribu kumdhibiti yule jamaa aliyempiga Blandina kwa chupa, lakini naye alikuwa akisaidiwa na marafiki zake waliozidi kuongezeka tu, na ndipo mabaunsa wakaingia na kuanza kuwadhibiti wengi wao na kufanikiwa kuwatoa wafanya fujo wale ndani hapo. Blandina sasa akawa amelala chini huku akilia sana kwa sababu ya kuhisi maumivu makali, na Namouih alikuwa anahangaika kuwaambia watu wamsaidie kumtoa hapo ili wampeleke hospitali kwa sababu
sehemu hiyo ya kichwa chake iliyopigwa ilikuwa inavuja damu. Watu watatu pamoja na Namouih
wakamsaidia Blandina kusimama, nao wakaanza kumwongoza kuelekea nje mpaka walipofikia usawa wa sehemu ambayo gari la Namouih lilikuwa limeegeshwa.

Lakini kumbe wanaume wale waliowafanyia fujo hawakuwa wameondoka eneo hilo kabisa, nao
wakiwa wanne, wakafika hapo na kuwafukuza wale watu waliokuwa wamemshikilia Blandina ili
wamkamate Namouih. Blandina akaanguka tena chini, huku wanaume hao wakiwa wamemshikilia Namouih sasa na kutishia kumchoma kwa kisu, na baadhi ya watu eneo hilo wakiwa pembeni wanaangalia tu, na ndipo bila kutarajia, kila mmoja wa hao wanaume akavutwa kwa nguvu sana na kuangukia pembeni. Namouih alipoangalia vizuri, akatambua kwamba ilikuwa ni Draxton ndiye
aliyefika hapo!

Wanaume wale wakaanza kumfata Draxton ili wamshambulie, lakini ilikuwa hivi: Draxton alikuwa akishika tu mkono wa mwanaume mmoja na kuupindisha kidogo, ungevunjika. Angepiga ngumi usoni kwa mwanaume mwingine, meno yake yote yangedondoka. Akamsukuma mwingine kwa njia iliyoonekana kuwa kidogo sana, lakini akaangukia mbali na kuviringika mara kadhaa ardhini, kisha yule mfupi aliyempiga Blandina kwa chupa akakipitisha kisu kwa nguvu kumwelekea Draxton akiwa na lengo la kumkata usoni, lakini Draxton akakinga mkono yake na kufanya kimkate kiganjani, kisha akampiga mwanaume huyo kwa kichwa usoni na kusababisha avunjike pua vibaya sana na kubaki anagaagaa chini kwa kuhisi maumivu.

Watu bado walikuwa pembeni wakishuhudia tukio hilo na walikuwa wakiongezeka sana, ndipo Draxton akamgeukia Namouih na kumuuliza kama alikuwa sawa. Namouih akatikisa kichwa kukubali, halafu akamwonyeshea Blandina, akisema walihitaji kumwahisha hospitali upesi. Draxton akamwahi Blandina hapo chini na kukishika kichwa chake, naye Namouih akafika hapo pia huku sasa baadhi ya watu wakianza kusogea karibu yao. Draxton akanyanyua kichwa cha Blandina kidogo, naye Blandina akawa analia kwa maumivu sana huku amekaza macho yake, na ndipo
mwanaume huyu akapitisha kiganja chake kilichokuwa kimekatwa kwa kisu chini ya kichwa cha Blandina na kukiweka kwenye jeraha lake.

Namouih akamwangalia Draxton kwa umakini, akiwa ameelewa ni nini ambacho mwanaume huyo alikuwa anafanya. Alikuwa anaiingiza damu yake ndani ya jeraha la Blandina ili kumponya, kama tu alivyofanya kwa Namouih, lakini hakuna mtu mwingine yeyote hapo ambaye angeweza kutambua hilo. Watu waliokuwa karibu sasa wakawa wanasema mwanamke huyo alihitaji kuwahishwa hospitali na wenyewe tayari walikuwa wameita maaskari ili waje kuwakamata wafanya fujo hao
waliokuwa wamedebwedeshwa baada ya kula kichapo kutoka kwa Draxton, na mwanaume huyu
akamnyanyua Blandina kwa uangalifu sana baada ya kuhakikisha damu yake imemwingia vizuri, kisha akamwingiza ndani ya gari la Namouih na yeye kukaa humo pia, halafu akamwambia Namouih aingie kwenye usukani ili waondoke.

Ilikuwa ni tukio moja ambalo halikutazamiwa kabisa kutokea usiku huo, na bado ilikuwa ni saa tano tu ikielekea saa sita usiku. Namouih alikuwa anawaza sana kuhusu hali ya rafiki yake, naye akawa anamuuliza Draxton ikiwa walitakiwa kumpeleka Blandina hospitali, lakini mwanaume huyu
akamwambia Namouih wampeleke nyumbani kwake; yaani nyumbani kwa Blandina. Namouih akauliza ikiwa rafiki yake angekuwa sawa kabisa, naye Draxton akamhakikishia kwamba angekuwa sawa tu. Namouih alikuwa ameuchukua mkoba wa Blandina pia wakati wanatoka kule, hivyo walipoifikia nyumba yake akatoa funguo na kwenda kufungua geti, kisha akarudi tena na kuliingiza gari lake ndani.

Draxton akambeba Blandina kwa uangalifu tena na kumpeleka mpaka chumbani kwake, kisha akamlaza kitandani baada ya Namouih kuweka taulo hapo ili shuka lisichafuliwe na damu. Namouih alikuwa anauliza ikiwa wangehitaji kumfunga rafiki yake kwa bendeji, lakini Draxton
akakanusha kutokufanya hivyo kwa sababu ilihitajika damu yake iingiliane vyema na damu ya jeraha la Blandina ili sehemu ya ngozi yake iliyojeruhiwa iungane upya. Kwa sasa Blandina alikuw amepitiwa na usingizi ule wa hali mbaya kama mgonjwa, hivyo Namouih na Draxton wakawa wamekaa naye kitandani; Blandina akiwa amelala katikati yao.

Draxton akamwangalia Namouih na kutambua kwamba alikuwa ameanza kulia kwa sauti ya chini, bila shaka akiwa ameumizwa sana na kilichompata rafiki yake, naye akamwambia, "Usiwe na hofu. Atakuwa sawa."

"Hhh... najua. Ni kwamba tu... mimi ndiyo nimemsababishia hili... yaani sikuzote mimi huwa ni wa
kusababisha matatizo tu..." Namouih akasema huku akijifuta machozi.

"Nini kilitokea mule ndani? Wale wanaume walitaka nini?" Draxton akauliza kwa utulivu.

"Si tulikuwa tumekaa, tunaongea, mara kale kamwanaume kafupi kakanipamia kwa nguvu kweli.
Nilipoka-confront... ndiyo kakachukua chupa.... Ilikuwa inatakiwa inipige mimi... ila tena
nimemsababishia Blandina maumivu... aah... yaani jamani me mpaka nachoka... sa'hivi mtu
akinichanganya tu vibaya ninawaka kwa hasira kwa sababu stress haziishi, yaani haipiti siku kukawa hamna...."

Namouih akaishia hapo baada ya Draxton kukishika kiganja chake kama kumtuliza. Mwanamke huyu akamwangalia Draxton usoni kwa hisia sana.

"Usiwaze tena kuhusu hayo. Kila kitu kitakuwa sawa. Blandina atakapoamka, atajikuta akiwa bila
jeraha wala maumivu. Nakuomba tu usionyeshe kubabaika akiuliza ilikuwaje... umwambie kwamba
hakuumizwa kivile, na ndiyo maana amewahi kupona... unaelewa?" Draxton akasema kwa upole.

Namouih akatikisa kichwa kukubali.

Draxton akakiachia kiganja cha Namouih na kumwangalia Blandina usoni kwa kujali.

Namouih, akiwa bado anamtazama mwanaume huyo, akauliza, "Ulifikaje pale haraka hivyo? Sikutegemea kukuona sehemu ile."

"Nilirudi huku mida fulani baada ya wewe kuondoka, nikawa nimepanga kuja hapa ili nikutane na Blandina lakini sikumkuta. Kwa sababu ilikuwa saa nne nikawaza angekuwa wapi na... nilitaka tu kuhakikisha yuko salama, kwa hiyo nikaifuatilia namba yake kwa ile app.... Natamani tu kama ningekuwa nimefika mapema, hii isingetokea," Draxton akaongea kwa hisia.

Namouih akamwangalia rafiki yake kwa huzuni sana, na ni hapa ndiyo simu yake ikaanza kuita, mpigaji akiwa ni Efraim Donald. Akapokea, na mume wake huyo alikuwa anauliza kama mke wake anarudi nyumbani lakini Namouih akamwambia hapana, angelala kwa Blandina leo. Akamuaga baada ya kusema kwamba angekwenda nyumbani ikifika asubuhi, kisha akakata simu na kurudi kumwangalia rafiki yake. Draxton sasa alikuwa ameanza kuupitisha mkono wake kwenye kichwa cha Blandina kama kumbembeleza, na Namouih akatambua kwamba sehemu ile ya kiganja chake iliyokuwa imekatwa kwa kisu haikuwa na alama tena. Yaani ilikuwa kama haikukatwa kabisa!
Akamwangalia tu usoni, akiwa anazidi kustaajabishwa na mfumo mzima wa mwili wa mwanaume huyo, kisha ndiyo akamwambia anakwenda kunawa mikono yake, naye akanyanyuka na kumwacha
hapo.

Akaingia sehemu ya bafuni na kwenda kuanza kunawa mikono palipokuwa na sinki dogo na kioo
ukutani, naye akaamua kunawa kabisa na uso wake, na pale alipoanza kuufuta tu maji kwa viganja vyake, akashtuka mno moyoni baada kuona jambo la ajabu sana kupitia kioo cha hapo. Ilionekana kwamba nyuma yake kulikuwa na mtu aliyesimama, na hakuwa mwingine ila baba yake aliyekufa siku nyingi sana, Mzee Masoud! Namouih akageuka kwa taharuki nzito, lakini hapo alipomwona hapakuwa na mtu yeyote, na mapigo ya moyo wake yakaanza kukimbia kwa kasi sana akiwa ameingiwa na hofu. Akageukia kioo tena, na macho yake yakatanuka zaidi kwa mshangao baada ya kumwona Agnes akiwa amesimama huku mdomo wake uliokatwa ulimi ukiwa wazi! Namouih akageuka tena huku akipiga kelele, lakini hapakuwa na mtu sehemu hiyo. Sasa ikawa ni kama anaona mende wengi sana wakimfata upesi, nao wakaanza kumpandilia mwilini kwa kasi kubwa.

Namouih alilia kwa sauti ya juu akijaribu kuwatoa mende hao, na kelele zake zikawa zimevuta umakini wa Draxton chumbani pale. Mwanaume akatoka upande wake aliokuwa amekaa kitandani na Blandina na kulielekea bafu hilo, kisha akamwita Namouih na kuuliza kulikuwa na tatizo gani. Lakini Namouih akaendelea kusikika akipiga kelele, hivyo Draxton akaingia ndani hapo na kumkuta anajipiga-piga mwilini kama vile anajaribu kufuta au kuondoa uchafu fulani mwilini mwake. Akamsogelea na kumshika mabegani, lakini Namouih akawa anamsukuma huku
akiendelea kulia tu, hivyo Draxton akamtikisa kwa nguvu huku akimwita kwa sauti ya juu sana, ndipo Namouih akamwangalia usoni huku akipumua kwa hofu.

"Vipi?" Draxton akauliza.

Namouih akaanza kuangalia huku na huko, na kwa uhakika kabisa hakukuwa na mende sehemu hiyo. Zilikuwa ni fikira zake. Lakini kwa nini zilikuwa zinamfanyia vioja hivi? Alifikiri mwanzoni kwamba msababishi alikuwa Draxton lakini mwanaume huyo hakuonekana kuwa aina ya mtu wa kucheza na fikira za wengine; yeye alikuwa wa suala tofauti kabisa. Ndoto mbaya zilikuwa zinasua kwa Namouih, lakini sasa viini macho vilikuwa vinashika kasi.

"Namouih..." Draxton akamwita tena kwa kujali.

Namouih akaanza kujitahidi kupumua kwa utaratibu, kisha akasema, " Niko sawa Draxton. Niko
sawa."

"Kwa nini unapiga kelele? Umeona nini?"

Namouih akamwangalia tu machoni.

Draxton akamsogelea karibu zaidi na kusema kwa sauti ya upole, "Niambie."

Namouih akainamisha uso wake, kisha akaanza kusema, "Huwa ninaota... au kuona vitu fulani
vinavyotisha sana. Sijui ni kwa nini tu lakini vinaniumiza sana... nakuwa najaribu kupotezea kila ikitokea lakini ikishatokea... nakosa amani yaani... naona watu waliokufa na viumbe wenye kuogopesha... sasa hapa sasa hivi... nimemwona Agnes, na baba yangu... mara mende wengi sana wakaanza kuni.... yaani Draxton... hii hali inanipa msongo sana ni kama... hazitaacha..."

Draxton akaushika uso wa mwanamke huyu kwa kiganja chake, na Namouih akamwangalia kwa
utulivu usoni.

"Pole. Labda unahitaji tu kupumzika vya kutosha. Inawezekana ni trauma kwa sababu ya mambo mengi uliyopitia hizi siku chache za nyuma," Draxton akasema.

Namouih akatikisa kichwa kukubali, kisha akakishika kiganja cha Draxton usoni mwake na kumwangalia kwa hisia, halafu akauliza, "Ikiwa mimi na wewe tungekutana chini ya hali tofauti.... unafikiri nini ingekuwa hatma yetu?"

Swali hilo la Namouih lilikuja kwa njia fulani ambayo ilimchanganya kiasi Draxton, na kwa sekunde chache akabaki tu kumwangalia machoni bila kusema neno lolote.

"Namaanisha... ikiwa maisha yako yasingekuwa magumu namna hiyo, na mimi nisingekuwa nimepita kubaya na kuendelea kuhangaika hata sasa... unadhani tungeongoza maisha yetu kwa njia nzuri... ambayo ingewafaa zaidi wale tunaowapenda?" Namouih akauliza.

Draxton akatikisa kichwa kukubali, naye akakishusha kiganja chake kutoka usoni kwa Namouih na
kusema, "Kama tu ulivyoniambia... hata mimi sijui kwa nini maisha yako hivi... lakini yana kusudi. Kuna vitu tumepewa wengine hawana, na hata ingawa muda mwingine vinaweza kutufanya tuhisi ni kama tumebeba mizigo mizito... ikiwa bado kuna sababu ya kuendelea kuishi hasa kwa ajili ya wapendwa wetu hata ingawa tunahisi kulemewa... tunatakiwa kuyathamini. Ndivyo ulivyonifunza leo."

Namouih akaendelea kumwangalia kwa hisia.

"Endelea kuwa imara kama ulivyo, lakini ukihisi kuchoka... pumzika. Wakati mwingine uchovu wako
unaweza kukuzidia kwa sababu unajitahidi kuonyesha uko imara kupita kiasi... so muda mwingine just... pumzika... kwa njia ambayo itakufaa. Na usiache kukumbuka kwamba sisi pia tupo hapa kwa ajili yako," Draxton akamshauri.

Namouih akakilaza kichwa chake kifuani kwa mwanaume huyo baada ya kuhisi faraja ndani ya moyo wake, naye Draxton akakikumbatia kichwa chake kwa mkono mmoja kama kumpa kitulizo cha kirafiki. Wawili hawa walikuwa wameanza kupatana sana kihisia, na Namouih alihisi usalama fulani mzuri akiwa pamoja na Draxton, kwa sababu alianza kumwona kama rafiki wa karibu zaidi. Baada ya sekunde chache, Draxton akanwongoza kurudi chumbani ili naye aweze kwenda
kupumzika, na Namouih akalala pembeni yake Blandina huku akimwangalia Draxton, aliyekuwa
ameketi kwenye kiti kidogo kwa chini huku akiegamia kitanda na kumshika Blandina mikononi, na
baada ya dakika kadhaa usingizi ukawachukua wawili hao.


★★★


Asubuhi ikafika. Namouih akawa ameamka kutoka usingizini na kujigeuza kitandani hapo, naye
akakuta rafiki yake akiwa bado amesinzia pembeni yake, lakini Draxton hakuwepo. Akajinyanyua na
kuvuta simu yake iliyokuwa pembeni ili kuangalia muda na kukuta ni saa mbili kamili. Akatoka kitandani na kwenda mpaka sehemu ya sebuleni, naye akaanza kusikia vitu kama vyombo vikijigonga-gonga kutokea jikoni, hivyo akaelekea huko kuona kama Draxton alikuwepo. Kweli
akamkuta mwanaume huyo hapo, akiwa anatengeneza chakula kidogo kwa ajili ya kiamsha kinywa, na Namouih akatabasamu kidogo.

Draxton akaonekana kufumba macho na kuinamisha uso wake kidogo, kisha akiwa hivyo hivyo
akasema, "Umeamkaje, Namouih?"

Hakuwa hata amemwangalia, naye Namouih akawa ametambua kwamba alijua uwepo wake hapo kwa kuvuta harufu yake.

"Nimeamka vizuri, sijui wewe?" Namouih akamsemesha pia.

Draxton akamwangalia sasa na kusema, "Nimeamka vizuri pia."

"Unatengeneza nini?" Namouih akauliza.

"Mayai. Kuna mkate pia, nataka Blandina ale light akiamka..."

"Ahahahah... sandwich..."

"Yeah."

"Hongera."

"Asante. Ndoto mbaya hazikukusumbua?"

"Hapana, sijaota... ndoto mbaya. Uliamka saa ngapi?"

"Kumi na mbili."

"Kumbe? Ulikuwa unafanya nini mpaka sasa hivi?"

"Niliondoka. Nilielekea kule tulikokuwa jana ili nikalifate gari la Blandina," Draxton akamwambia.

"Aaaa... umeenda kwa...."

"Nilipanda boda."

"Kwa hiyo umeshalileta?"

"Ndiyo."

"Na wewe la kwako? Si uliliacha huko huko?"

"Ndiyo, nitalifata baadaye. Nilikuwa nataka kwanza kumhudumia Blandina halafu..." Draxton akaishia hapo na kutabasamu.

Namouih akatabasamu pia na kusema, "Atafurahi sana."

"Unataka kuondoka?"

"Ndiyo, inabidi nirudi nyumbani ili niwahi kujiandaa kwenda kazini."

"Okay. Ingekuwa vizuri kama ukikaa ili tupate chai pamoja, maana ulisema unataka kuona mwenyewe kama najua kupika," Draxton akamwambia.

Namouih akacheka kidogo, kisha akasema, "Na kinanukia kweli. Nitajua tu lakini siku nyingine, acha leo iwe yako wewe na Blandina."

Draxton akatabasamu na kuzima jiko sasa baada ya kumaliza kutengeneza chakula.

"Asante kwa msaada wako jana Draxton... na maneno yako pia. Yaani... nikikumbuka namna ambavyo nilikuwa nakutendea mwanzoni mpaka nahisi aibu," Namouih akaongea.

"Usijali. Tuko pamoja Namouih. Nathamini sana maneno yako pia... ulinitia moyo sana," Draxton akasema.

Namouih akabaki kumtazama tu usoni kwa umakini, naye Draxton akatabasamu kwa mbali na kugeuka nyuma ili atoe vyombo kwa ajili ya kuweka chakula.

"Nafikiri itakuwa vyema tukikutana baadaye pia. Kuna mambo kuhusiana na Felix nahitaji
tuzungumzie pamoja," Draxton akamwambia.

Namouih akaweka uso makini, kisha akatikisa kichwa kukubali baada ya Draxton kumtazama.

"Okay. Tutawasiliana. Me ngoja niende, utampa huyu salamu zangu na kama hataweza kuja kazini leo, mwambie tu anijulishe ili nimwambie boss wetu kusiwe na shida," Namouih akasema.

"Okay."

Namouih akatikisa kichwa kama kutoa shukrani, kisha akaanza kuondoka na kwenda kulitoa gari
lake nje ili aelekee nyumbani, na ni Draxton ndiye aliyekwenda kumfungulia geti na kisha kulifunga
baada ya mwanamke huyo kuondoka. Mwanaume akarejea ndani na kwenda moja kwa moja
mpaka chumbani kwake Blandina, naye akakuta tayari mwanamke huyo akiwa ameshaamka, na akikaa kitandani huku akijishangaa kiasi. Alipomwona Draxton, Blandina akakunja uso wake kimaswali, ikieleweka kwamba hakujua yaliyokuwa yameendelea kutokea usiku wa jana, hivyo Draxton akamfata mpaka kitandani hapo na kukaa usawa wa miguu ya mrembo huyu.

"Draxton... nini kinaendelea?" Blandina akauliza kwa sauti ya chini.

"Unahisije mwilini, Blandina? Kuna maumivu sehemu yoyote?" Draxton akauliza kwa kujali.

"Unafanya nini hapa? Namouih yuko wapi?" Blandina akauliza pia.

"Namouih ameenda nyumbani... atatangulia kazini. Niko hapa kukuangalia ili kuhakikisha uko sawa," Draxton akasema.

"Nini... nini kilitokea? Jana si... nimepigwa na chupa kichwani? Mbona sihisi maumivu yoyote?
Mlinipeleka hospitali? Vipi wale wanaume walionipiga? We' ulikuja saa ngapi?"

Draxton akavishika viganja vya Blandina na kusogea karibu yake zaidi. "Its okay. Uko sawa sasa. Kila kitu kiko shwari. Usiwaze tena kuhusu hayo yaliyotokea, okay?" akamtuliza.

Blandina akainamisha uso wake akionekana kujiuliza maswali mengi, kisha akaanza kusema, "Wale wanaume... walirudi tena... wakamshika Namouih...."

"Blandina...."

"....mimi nikaanguka, si ndiyo? Nini kilifata baada ya hapo?" Blandina akauliza.

"Nilikuja na dawa, nikakupaka, ndiyo imekusaidia upone haraka. Wale wanaume wameshakamatwa na maaskari. Acha kuwaza tena kuhusu hayo mambo, sawa?" Draxton akamwambia kwa upole.

Blandina akatulia kidogo, kisha akavitoa viganja vya Draxton kutoka kwenye vyake na kuuliza, "Na wewe ulikuwa umekuja pale kufanya nini?"

"Kwa ajili yako," Draxton akajibu.

"Kwa ajili gani? We' si una mambo mengi ya kufanya? Kama ni amani ndiyo kitu pekee unachotaka basi unayo... mimi sina kinyongo wala. Sielewi kwa nini bado unanifata-fata wakati umeamua mwenyewe kuachana na mimi, lakini sitaki unizunguke-zunguke... unanichanganya. Endelea na mambo yako, na mimi...."

Blandina akaacha kuongea namna hiyo baada ya Draxton kumsogelea karibu zaidi na kumshika usoni kwa kiganja chake.

"Ninakupenda Blandina. Na inaniua nipokuona unateseka hivi. Ninaomba sana unisamehe kwa kukuumiza, na ninataka niendelee kuwa karibu nawe hata kama bado sijaweza kuyasafisha maisha yangu kwa asilimia zote," Draxton akasema.

"Unamaanisha nini?" Blandina akauliza.

Draxton akaufata mdomo wa Blandina na kuanza kumpiga busu taratibu, na ingawa mwanzoni
Blandina alichanganywa na jambo hilo, naye pia akaanza kuijibu busu ya Draxton kwa hamu kubwa sana iliyofanya igeuke kuwa denda tamu mno. Blandina hata akaushika uso wa Draxton ili kuiendeleza denda hii kwa kuwa hisia zake kwa mwanaume huyu zilikuwa zimependa juu mno, kisha Draxton akaivunja taratibu na kumwangalia machoni, huku Blandina akiwa anapumua kwa njia legevu kiasi.

"Namaanisha kwamba.... mimi pia ninataka kutulia nawe Blandina," Draxton akamwambia hivyo.

Blandina akaachia tabasamu kwa hisia sana, akiwa ameyafurahia mno maneno ya mwanaume huyo.

Draxton akatabasamu pia, kisha akamwambia, "Lakini bado nakuomba tuendelee kuipeleka hii
taratibu, mpaka nitakapokuwa vizuri zaidi. Utaweza kunivumilia mpenzi wangu?"

Blandina akatikisa kichwa kukubali huku akitabasamu kwa furaha sana, na alikuwa akifanya kama
kuyafuta-futa mashavu ya Draxton kwa vidole vyake mara nyingi mno kutokana na msisimko
uliomwingia, na wawili hawa wakaanza tena kunyonyana ndimi kwa hisia sana kuonyesha namna
walivyopendana mno, na sasa wakawa wamerudiana rasmi tena.


★★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★★


Usikose sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali ya CHANGE. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Itakuwa ikiruka hapa siku za Jumatatu, Jumatano, na Ijumaa. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.

WhatsApp no: +255 678 017 280

e-mail: eltontonny72@gmail.com
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…