CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI
★★★★★★★★★★★★★
Namouih akabaki kumtazama tu kimaswali, naye Suleiman akafungua mlango wa gari hilo na kushuka, akiwa anamwangalia mke wa mwajiri wake kwa njia ya kawaida tu.
"Suleiman! Unafanya nini?" Namouih akauliza kwa uthabiti.
"Habari za saa hizi madam?" Suleiman akamsalimu.
"Hujasikia nilichouliza au?"
"Nimesikia..."
"Sasa?"
"Niko hapa kukulinda madam."
"Excuse me?"
Suleiman akabaki kimya.
"Kuni... kunilindaje? Yaani... unanifatilia kwenye gari lingine ili kunilinda? Nani amekwambia ufanye
hivyo?"
Suleiman akaendelea kumwangalia tu.
"Suleiman sitaki dharau. Nikikuuliza swali nijibu," Namouih akasema kwa hisia kali.
"Ni boss ndiyo ameniagiza nikufate... nihakikishe unakuwa salama," Suleiman akamwambia.
"Ahah... hivi kweli... yaani umekosa kazi ya kufanya?"
"Hii ndiyo kazi yangu madam."
"Wewe ni mtumishi wake, siyo wangu mimi. Naomba tuheshimiane. Unanifatilia namna hiyo, ningekuitia polisi je? Unani... mnafanya haya bila mimi kujua inaleta faida gani?"
"Ni ili uwe salama...."
"Usalama kutokana na nini? Naomba mwambie... oh God! Okay. Unataka kuhakikisha niko salama si ndiyo? Haya twende. Twende nifate," Namouih akamwamuru mwanaume huyo.
Kisha mwanamke huyu akaanza kuelekea upande ule wenye jengo ambako ndiyo angemkuta Salome, na Suleiman akaanza kumfata pia. Namouih alikuwa amevaa gauni zuri sana na refu la rangi nyeupe lenye urembo wa maua-maua mengi mekundu, lililombana kiasi na kuchora umbo lake vyema nyuma, hivyo Suleiman kumfatilia kwa nyuma akitembea kulimfanya mwanaume huyo aanze kumwangalia mke wa mwajiri wake kwa matamanio. Sikuzote Suleiman alikuwa mtu mmoja wa ukimya sana aliyetii kila jambo aliloambiwa kufanya na Efraim Donald, lakini Namouih hakuwahi kumpa mwanaume huyu umakini wake wa hata asilimia chache kwa hiyo kiukweli jambo hili lilimkera sana.
Wakawa wamefika kule ndani, na Namouih akawa amemwona Salome upande fulani akiwa ameketi kwenye meza ya wateja, na akimpungia mkono Namouih. Namouih akamfata mpaka hapo, naye Salome akasimama na wanawake hawa wakakumbatiana.
Walipoachiana, Namouih akamgeukia Suleiman na kusema, "Huyu ni Salome. Ndiyo mtu unayetakiwa kunilinda kutoka kwake. Umeelewa?"
Salome akakunja uso kimaswali, naye Suleiman akainamisha uso wake. Alikuwa anamkumbuka
Salome pia kwa sababu usiku ule wa sherehe aliwaona wote pamoja na Efraim Donald.
"Nakuomba urudi huko unakojua na usije kurudia kufanya hivi tena. Nitaongea na Efraim baadaye. Nenda," Namouih akamwambia Suleiman.
Mwanaume huyo akatii na kuondoka, naye Namouih akamwangalia Salome na kukuta anamtazama kwa njia iliyoonyesha wazi kwamba alikuwa haelewi kinachoendelea.
"Oh... sorry kwa hilo. Yaani siwezi kuendesha siku moja bila kukutana na kitu chenye kukwaza," Namouih akamwambia.
"Ni nani huyo?" Salome akauliza huku wote wakiketi sasa.
"Ni... kama chauffeur wa mume wangu... alikuwa ananifatilia ili kunilinda eti... yaani jamani!"
"Hahahah.... Mume wako hataki uibiwe na vibenteni eeh?"
"Siyo hivyo, ni basi tu hiyo ishu ya juzi me kupotea kidogo ndiyo eti inamfanya afikiri nahitaji kutendewa kama yai vile."
"Mume wako ana degree kubwa sana ya upendo kwako eti Namouih?"
"Ndiyo alivyo. Yuko protective sana, lakini siyo mtu mwenye gubu. Ananipenda, nampenda, sema bado kuna mambo mengi ambayo... huwa yanakatisha tamaa," Namouih akasema kwa hisia.
"Mhm... inaonekana ni vitu serious. Mimi niliachika kwa mume wangu sababu mambo mengi tulikuwa hatuelewani. Inapendeza sana nikiona mwanaume anamtendea mke wake kama wa kwako anavyokutendea... lakini wewe ni kama vile inakukera. Kuna vitu fulani bado hakutimizii?" Salome akauliza.
Namouih akashusha pumzi na kutikisa kichwa kukubali.
"Ah... samahani yaani, nimekimbilia huko hata sijakuagizia kinywaji..."
"Hapana, haina shida. Hata hivyo najua unahitaji kurudi kazini kwa hiyo hatutatumia muda mwingi. Nilihitaji tu kama... kaushauri maana... ahah... hali yangu inashangaza kidogo," Namouih akasema.
"Ndiyo... ni sawa. Niambie. Unapitia nini rafiki yangu?"
"Sijui nikwambieje. Hivi... ungeshauri nini kama tuseme... labda mwanaume anakuwa anashindwa
au hampi mke wake haki yake ya ndoa... wewe unafikiri ni mambo gani yanayosababisha hali hiyo?" Namouih akauliza.
"Mmm... ni vitu vingi, kwa hiyo inategemea na hali halisi ya kile kinachoendelea ndani ya ndoa. Mimi siyo expert wa masuala ya ndoa ila kidaktari zaidi naweza kusema labda ni zile hali mara nyingi zinazosababishwa na mtu kuishiwa hamu ya kutaka mapenzi au kutoa mapenzi baada ya kukaa na mwenzi kwa kipindi kirefu... au ndo masuala ya ku-cheat, vitu kama hivyo... inategemea na kinachoendelea. Kwa hiyo kama ni ushauri, naweza kusema la muhimu ni kwa wenzi kuongea, wafunguke kuhusu mambo wanayotaka na wasiyotaka, labda hiyo italeta faida kwa sababu mahitaji yao wote yanakuwa wazi kwa mmoja na mwenzake wakishaongea," Salome akamweleza.
"Natamani hata kwa hali yangu ingekuwa namna hiyo lakini yaani hata sielewi..."
"Kuna tatizo la namna hiyo kwenye ndoa yako Namouih?"
"Ndiyo Salome. Toka Efraim amenioa hajawahi kushiriki nami tendo la ndoa," Namouih akasema.
"Yaani hata mara moja?!"
"Ndiyo."
"Kwa nini?"
"Shida ndiyo hiyo. Hakuna sababu. Hanisemeshi kuhusiana na hilo Salome yaani, nimejaribu mara nyingi sana kuligusia lakini ni kama hajali... siwezi hata kujua kama labda ana tatizo fulani la kiafya lililofichika maana rekodi zake zote ni safi. Hadi huwa tunagombana yaani kwa sababu inaonekana ni kama vile namlazimisha, sijui ana shida gani..."
"Pole sana Namouih..."
"Unajua jinsi ilivyo ngumu kwa mwanamke... kumtaka mwanaume wake halafu akawa anapewa rejection tu..."
"Ndiyo, naelewa."
"Sasa... nakuwa najiuliza sijui nifanye nini. Ahah... kuna siku hadi nikamwambia naweza nikatoka nje nikakutana na limtu litakalonitimizia haja zangu..." Salome akacheka.
"Maana ni kama yeye ameshindwa yaani..."
"Ahahah... atakuua ukifanya hiyo kitu!"
"Na alikuwa mkali kweli niliposema hivyo..."
"Ndiyo maana kumbe kamweka hadi na bodyguard wake akufatilie?"
"Agh, utamweza!"
"Ahah... kwa kweli ina... nitumie neno gani yaani... huwa inachosha," Salome akamwambia.
"Kabisa," Namouih akasema.
"Kama hadi na maongezi yanashindikana, unahisi hii itaelekea wapi?"
"Yaani hata sielewi. Tumekutana na matatizo mengi hapa katikati, vioja, vikwazo, lakini tunaendelea kusonga mbele... ila hiyo haimaanishi nimeridhika. Maneno ya watu kwamba siwezi kuzaa wala nini yanakuwa yanaonekana kwamba ni kweli, na hiyo ni kwa sababu tu mume wangu hana hata time kucheza kidogo na mimi... ni zaidi ya mwaka, unaweza kuamini?" Namouih
akasema kwa hisia.
Salome akatikisa kichwa kwa kusikitika.
"Ndiyo hivyo. Nimeshaanza kuhisi kukata tamaa kiasi kwamba sasa hivi mtu akija kuniambia nitoke na hao vibenteni unaowasema, naweza nikakubali... wakati ni jambo ambalo sikuwahi kufikiria kabisa," Namouih akaongea kwa huzuni.
Salome akakishika kiganja chake na kusema, "Pole dear. Nakuona kama mdogo wangu yaani anayehitaji msaada sana lakini mimi nakuwa siwezi kutoa unaostahili."
Namouih akatabasamu kwa mbali na kumwangalia.
"Kama mume wako hakupi sababu, basi itakuwa ni juu yako kufanya maamuzi yatakayokupa faida. Ila yasiwe mabaya maana inaweza kusababisha shida. Kikubwa ni maongezi tu Namouih. Una-time
wakati mzuri sana ili uongee naye kwa njia nzuri, akuelewe, ili kama ikiwezekana na yeye afunguke... naona anakupenda, sidhani kama hili litakuwa jambo la... milele kwenye ndoa yenu. Ni kama tuseme unapokuwa unampenda mtu ambaye ni rafiki lakini yeye hajui, au labda anajua lakini hakutilii maanani. Anayepaswa kupiga hatua ya kwanza ni wewe, siyo? Eee... kwa sababu kuna hiki kitu kwamba unaweza kukuta kweli hataki kukubali kuwa nawe, lakini anashindwa kukwambia abda kwa kuwa anahofia atakupoteza kama rafiki. Wewe ndiyo unatakiwa umwonyeshe kwamba una uimara, kwamba utamwonyesha kuelewa hata kama ataamua kinyume na unavyotazamia..."
Maneno hayo ya Salome yalimgusa sana Namouih, naye akaangalia chini akiwa anayatafakari kwa kina.
"Ndivyo ilivyo hata kwa mume wako. Ikiwa maongezi yatagonga mwamba hata baada ya kujitahidi kumwonyesha uelewa, basi amua utakachoona kuwa sahihi, lakini uwe mwangalifu kisije kukuumiza au kuwaumiza nyie wote," Salome akamalizia.
Namouih akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa na kusema, "Asante sana Salome. Uko vizuri
sana... nilihitaji mno maneno kama haya."
"Karibu dear. Ila bado tuna muda wa kutosha kuendelea kuzungumza kwa hiyo jisikie huru kabisa kufunguka mpenzi," Salome akamwambia.
Namouih akatabasamu, na wanawake hawa wakaendelea kuongea kuhusu mambo mengi ya
maisha na kutiana moyo kwa maneno mazuri sana; hasa kutoka kwa Salome. Walitumia kama saa
zima na nusu hapo, na ndipo Salome akahitaji kurudi kazini hatimaye. Wakanyanyuka pamoja na kwenda nje, wakiwa wanaongelea uwezekano wa Salome kuja kwenda kumtembelea Namouih nyumbani kwake kwa sababu mwanamke huyu alikuwa anataka kumkaribisha, na Salome alikuwa anahitaji kuangalia ratiba yake ili aamue siku ambayo ingefaa halafu ndiyo amjulishe rafiki yake huyo.
Kwa hiyo wakaachana baada ya hapo, Salome akielekea upande mwingine wa jiji, na Namouih
akielekea upande ambao ungempeleka kule msituni ili akakutane na Draxton.
★★
Dakika kadhaa kupita, Namouih akawa bado mwendoni kuelekea kule msituni huku akiendesha gari lake kwa umakini. Umakini katika maana ya kwamba alikuwa anaangalia endapo kama na wakati huu angekuwa anafatiliwa, kwa hiyo alifanya kama kuzunguka-zuguka kwanza badala ya kwenda moja kwa moja huko ili awe na uhakika kwamba hakuwa na kupe mkiani. Wakati huu ni kweli hakuona nuksi yoyote, kwa hiyo akaingia zake huko msituni na kuelekea kwenye nyumba ya Draxton, lakini bado akiwa makini.
Ikiwa imefika mida ya saa tisa alasiri sasa, hali ya hewa kuzungukia maeneo ya huku ilikuwa ya wingu lililotanda, tofauti na maeneo ya jijini, na ni kweli haingechukua muda mrefu sana na mvua zingeanza kunyesha kwa kuwa misimu ilikuwa karibu kubadilika. Bila shaka maeneo ya huku ndiyo zingeanza mapema kutokana na miti kuwa mingi, na ndiyo maana Draxton alikuwa amekuja kuiimarisha nyumba yake kwa ajili ya hilo. Namouih alipoifikia nyumba hiyo aliweza kumwona
Draxton akiwa amepanda kwa juu, kama vile anapigilia misumari sehemu iliyoifunika nyumba, bila
shaka akiziba sehemu ambazo zingepitisha maji.
Mwanamke akashuka kutoka ndani ya gari lake na kuanza kuelekea huko, na alipofika karibu na nyumba hiyo, Draxton akaacha kufanya kazi yake na kumpungia mkono kutokea hapo juu, na Namouih akampungia mkono pia. Kwa kushangaza kiasi, mwanaume huyo akaruka kutoka huko mpaka chini na kusimama wima, na jambo hilo likafanya Namouih atabasamu kidogo. Draxton
alikuwa amevaa T-shirt nyepesi yenye rangi nyeusi iliyokuwa na mikono kifupi, suruali ya kijani ya
mazoezi (track) na viatu vyeupe vya mazoezi.
Akawa anamtazama Namouih kwa njia ya kawaida, kisha akasema, "Karibu."
"Asante. Haujaumia miguu?" Namouih akauliza.
"Ahah... la, niko sawa," Draxton akajibu.
"Hongera. Unaipenda kweli nyumba yako," Namouih akamwambia.
"Yeah, haka kambibi kamesimama hapa kwa muda mrefu. Mara kwa mara nahitaji kuka-treat kidogo ili kajisikie vizuri," Draxton akaongea kiutani.
"Ahahahah... kambibi kako," Namouih akasema.
Draxton akatabasamu na kuiangalia nyumba hiyo.
"Blandina ameniambia kwamba ulienda kumwona leo asubuhi... asante Draxton," Namouih akasema.
"Usijali. Nilihitaji sana kufanya hivyo pia maana roho ilikuwa inaniuma... sikutaka aanze kunichukia ila nilimlazimu yaani..."
"Hapana, hawezi kukuchukia... unajua anakupenda sana..."
Namouih akasema hivyo huku akianza kumfata.
"Sitaki kuwa mbeya lakini nahitaji nikwambie kuwa amesema ulipoenda hiyo asubuhi na
kumwambia unabaki... alikuwa anatamani akukumbatie kabisa, ila hana uhakika kama hata hicho ni kitu unachotaka... kwa hiyo nakushauri tu ujitahidi kuyajenga naye Draxton hata kama.... ni
vigumu... angalau kidogo tu," Namouih akasema kwa ushawishi.
Alikuwa amemkaribia Draxton zaidi sasa, na mwanaume huyu akapiga hatua mbili kurudi nyuma huku akionekana kufanya ile kawaida yake ya kufumba macho taratibu na kuinamisha uso wake. Leo ndiyo siku ambayo Namouih alitaka kujua hiyo ilimaanisha nini.
Draxton akaacha kufanya hivyo na kuanza kuigeukia tena nyumba yake huku akisema, "Sawa Namouih, nitajitahidi. Twende ndani tafadh...."
"Draxton..." Namouih akamkatisha.
Draxton akamgeukia na kumtazama machoni.
"Kwa nini huwa unafanya hivyo?" Namouih akauliza kwa sauti ya chini.
"Kufanya nini?" Draxton akauliza pia kwa upole.
"Kila mara... nikikusogelea... unainamisha uso wako kama vile... kuna kitu kinakusumbua yaani... huwa haupendi nikikusogelea eh?" Namouih akauliza.
"La, si hivyo Namouih. Hhh... sijui nisemeje... samahani kwa kukufanya uhisi vibaya... iko tu nje ya uwezo wangu..." Draxton akamwambia.
"Unamaanisha nini?"
"Upande wangu wa pili una nguvu kama kwa mnyama wa kawaida... kama kusikia mbali, na kuvuta harufu za vitu au watu... kama mbwa tu. Hata nikiwa hivi kawaida ninakuwa na huo uwezo pia,"
Draxton akamwambia.
"Oooh harufu... kumbe unakuwa unavuta harufu yangu?"
"Ndiyo."
"Ahahahah... sawa. Me nikafikiri labda ni shida... lakini bado inakuwa kama tatizo vile maana unajivuta sana nikusogelea... ina maana marashi yangu yanakupa effect fulani nzito au?"
"La, siyo marashi. Ni harufu YAKO," Draxton akamwambia.
Namouih akakunja uso kimaswali.
"Kila mtu ana harufu yake. Ninaweza kutofautisha watu kwa harufu zao... na... wewe harufu yako... kwangu ni nzuri sana... nakuwa nashindwa kujizuia... kuihisi..." Draxton akaongea hivyo huku anamwangalia kwa umakini machoni.
Namouih akaachwa kinywa wazi kiasi baada ya kusikia maneno hayo, huku anamwangalia machoni kama anajaribu kuyaelewa maneno hayo kwa undani.
Draxton akaacha kumtazama na kusema, "Tunaweza kwenda ndani?"
"Ndiyo, tunaweza," Namouih akajibu.
Draxton akatangulia kwenda huko, na kwa sekunde chache Namouih akabaki kusimama hapo kama vile bado anamtafakari mwanaume huyo, kisha naye akaelekea ndani taratibu na kufikia kukaa kwenye sofa moja. Draxton yeye alikuwa amekaa kwenye mkono wa sofa la upande
mwingine hivyo alikuwa kwa juu kidogo.
"Umeshapata chakula?" Draxton akauliza.
"Nilikunywa chai ya kutosha saa nne, so bado niko full, mpaka baadaye," Namouih akajibu.
"Sawa."
"Huwa unaleta chakula huku unakula mwenywe tu eti?"
"Ndiyo, huwa napika hapo... nakula," Draxton akajibu.
"Wewe unajua kupika?"
"Yeah."
Namouih akamtazama kwa yale macho ya kuhukumu.
"Ahahahah... nini sasa?" Draxton akauliza.
"Siwezi kuamini mpaka nije nione. Nani alikufundisha kupika?" Namouih akauliza.
"Mama yangu," Draxton akasema.
"Oooh..."
"Yeah. Mara nyingi kama alihisi njaa angeniambia 'Max, make some omelette.' 'Max, your lady needs a stomach leisure,'" Draxton akasema na kucheka kidogo.
Namouih akacheka pia, naye Draxton akabaki kutabasamu.
"Mlikuwa karibu eeh?" Namouih akauliza.
"Sana. Huwa namkumbuka sana..." Draxton akasema kwa hisia.
"Ni yeye mwenyewe tu ndiye aliyekuita kwa jina la Max?" Namouih akauliza.
Draxton akatikisa kichwa kukubali.
Namouih akawa anamtazama kwa hisia sana, akiona aina fulani ya simanzi la mbali usoni mwake.
"Vipi ukiniuliza maswali ya wakati huu? Bila shaka unayo mengi," Draxton akamwambia.
"Aam... ndiyo, nina maswali mengi..."
"Haya niko kizimbani sasa," Draxton akasema kiutani.
Namouih akacheka kidogo, kisha akasema, "Kuna siku fulani, mimi na Blandina tulikuwa barabarani, akagonga mtu... mweupe. Niliona tattoo fulani ambayo... mgongoni kwake... na wewe unayo. Are you one and the same?" Draxton akatikisa kichwa kukubali.
"Kwa hiyo unapoanza kubadilika, mwili wako unakuwa mweupe kama wa mzungu afu'... ukirudi unakuwa na ngozi hii ya kawaida?"
"Ndiyo. Sijui ni kwa nini lakini naweza kukisia kwamba hilo linahusiana na heritage ya wazazi wangu. Mama alikuwa mweusi, baba mweupe. Alipochanganya vitu vyake vya kitaalamu ndiyo ikawa kama hivi... ila sina uhakika kwa njia gani," Draxton akamwambia.
"Oooh...."
"Yeah. Nikianza kubadilika nakuwa mweupe, nikirudi kawaida nakuwa hivi. Lakini nywele za kichwani huwa zinabaki kuwa nyeupe, kwa hiyo inanibidi ninyoe na kupaka dawa ili... nisionekane kuwa babu," Draxton akasema.
"Ahahahah.... mbabu," Namouih akasema kiutani.
Draxton akatabasamu pia.
"Okay. Halafu... siku ile tumekugonga usiku ulikuwa unafanya nini? Maana haukuwa hata na nguo... mwili mzima," Namouih akauliza.
Draxton akatulia kidogo, kisha akasema, "Njoo. Nifate."
Mwanaume akaanza kuondoka kuelekea nje, naye Namouih akanyanyuka na kumfata bila kuelewa angeongozwa kwenda wapi. Wakatoka upande huo wa nyumba na kuelekea sehemu za nyuma,
wakiingia msituni zaidi. Ingawa hakuelewa kikamili kwa nini aliletwa huku, Namouih alikuwa na imani kwamba Draxton angempa jibu lililopita matarajio yake, hivyo angetakiwa kuwa tayari kwa ajili ya lolote ambalo angesikia au kuona. Wakafika kwenye eneo lenye miti mingi mikubwa zaidi ya ile waliyoipita kuzungukia msitu wote, naye Namouih akasimama na kupatazama kwa umakini. Miti miwili ilifungwa kwa minyororo mizito sana sehemu za shina, naye Draxton akafika hapo na kuunyanyua mmoja, kisha akamwangalia Namouih.
"Kuna nyakati ambazo huyu mnyama hulazimisha kutoka, na inakuwa labda ili apate chakula au... fujo tu. Nilijifunza kutabiri wakati ambao angejaribu ku-force kutoka, na mimi nikaamua kuwa nahakikisha kwamba muda huo ukifika ninakuwa sehemu anayotakiwa kuwa. Hapa ndiyo hiyo sehemu. Huwa nakuja, najifunga minyororo mikononi, shingoni, na miguuni halafu natulia. Chakula nakuwa nimeshakiweka hapo ili yeye akitoka minyororo inamzuia kwenda mbali, lakini atakula na kutulia mpaka napokuja kuamka asubuhi nikiwa mimi," Draxton akaeleza.
Namouih kiukweli hakuwa ameelewa jambo lolote alilosema mwanaume huyo, naye akabaki kumtazama tu usoni.
Draxton akauachia mnyororo, kisha akasema, "Usiku mlionigonga kwa gari, ndiyo nilikuwa nimeanza kubadilika, lakini sikuwa nimeifikia minyororo mapema hapa, kwa hiyo sikufanikiwa kujifunga haraka. Sikumbuki kilichoendelea, lakini inaonekana akili yangu ilipoingiliana na ya upande wangu wa pili nilianza kukimbia ovyo ovyo mpaka nilipofika huko barabarani... na nyie ndiyo mkanigonga. Hapo ndiyo mkafanya nikaishia katikati ya badiliko langu."
"Katikati ya badiliko?" Namouih akauliza.
Draxton akaanza kumfata mpaka alipofikia mbele yake na kusimama, kisha akasema, "Kuna mimi, kawaida. Ninapobadilika kabisa kuwa mnyama, hiyo ni mbaya. Lakini kuna wakati huwa naishia katikati ya hiyo kawaida na mbaya, kwa hiyo ni kama nakuwa nusu-mwanadamu, nusu-mnyama."
"Na hapo bado unakuwa huwezi kuji-control?" Namouih akauliza kwa sauti ya chini.
"Ni tofauti. Hapo nakuwa naona mambo kama mwanadamu, lakini nitatenda kama mnyama... hasa
nikikorofika. Kwa kipindi fulani nilijaribu kutafuta njia ya kuji-control nikiwa hivyo, lakini siyo rahisi kwa sababu ningepitiliza na kuwa mnyama kabisa. Angalau kwa usiku huo mlisaidia nikarudi huku mimi mwenyewe la sivyo kama ningefika mbali na kugeuka mnyama... mabaya mengi yangetokea," Draxton akaongea huku ametazama chini.
"Kwa hiyo unasema asante kwa sababu tulikugonga kwa gari?" Namouih akauliza.
"Ndiyo," Draxton akajibu.
Namouih akaangalia chini kwa ufupi, kisha akamtazama tena na kuuliza, "Huwa unamwekea chakula gani... huyo jamaa?"
Draxton akatabasamu kwa mbali na kusema, "Nyama. Huwa naenda machinjioni, nanunua hata mbuzi mzima namleta hapa, asubuhi nakuta mifupa."
Namouih akapandisha nyusi kwa mshangao kiasi, kisha akauliza, "Kila siku?"
"La. Hii huwa inatokea mara chache sana. Inaweza kutokea kila mwezi mara moja au hata baada ya miezi kadhaa. Vipi, ulikuwa unafikiri nabeba watu kila siku kama chakula?"
"Ahahah... siyo hivyo. Ila ungenilaumu kama ningefikiria namna hiyo?"
Draxton akatikisa kichwa kukanusha.
"Maisha yako ni ya ajabu sana," Namouih akasema.
Draxton akainamisha uso wake na kutikisa kichwa kukubali.
"Sawa. Okay... really Draxton, bado nina maswali mengi sana sijui kama...."
"Usijali, nitakujibu. Twende nikakuwekee na biskuti," Draxton akamwambia.
Namouih akatabasamu na kukubali, kisha wawili hawa wakaanza kurudi kule kwenye nyumba. Draxton alikuwa ananwambia jinsi ambavyo msitu huo ulikuwa mkubwa tofauti na namna ulivyoonekana, na wengi waliupuuzia tu ndiyo maana ilikuwa finyu sana kwa watu kuja huku mpaka kuifikia nyumba yake iliyojificha. Namouih akaketi kwenye sofa tena baada ya kufika ndani, naye Draxton akampatia boksi la biskuti.
"Eet Sum Moore," Namouih akasoma maandishi kwenye boksi hilo.
"Ushawahi kula?" Draxton akauliza.
"Ndiyo, ni nzuri. Nasma anazipenda. Mdogo wangu," Namouih akamwambia.
Draxton akaonyesha kuelewa, kisha akaketi kwenye sofa la pembeni.
Namouih akatoa biskuti mbili na kumpatia, naye Draxton akapokea. Wote wakatafuna kipande kimoja huku wakiangaliana, naye Namouih akatabasamu kidogo.
"Ungependa kujua nini kingine kuhusu mimi?" Draxton akauliza.
"Aam... Una mambo mengi sana ambayo kwa njia kubwa yanastaajabisha. Nakuwa na maswali mengi kiasi kwamba mpaka nashindwa kujua ikiwa mengine ni sahihi kukuuliza," Namouih akasema.
Draxton akatabasamu kiasi na kuuliza, "Toka umejua nina miaka 95 nimekufanya unione kama mbabu fulani hivi... grumpy eti?"
"Ahahahah... hapana, kawaida tu. Una sura changa sana na pigo za ujana mpaka huwa nasahau we' ni mbabu," Namouih akamwambia.
Draxton akatabasamu tu na kutafuna biskuti.
Wakatazamana kwa ufupi, kisha Namouih akauliza, "Ulizaliwa wapi?"
"Tusla. Ipo Oklahoma, Marekani," Draxton akajibu.
"Umeishi kwenye nchi nyingi eeh?"
"Siyo nyingi sana. Venezuela na Tanzania ndiyo nimeishi kwa muda mrefu zaidi."
"Ulikuja Tanzania mwaka gani?"
"1990."
"Ahah... me ndiyo nazaliwa!" Namouih akasema kwa shauku.
Draxton akatabasamu.
"Wazazi wako wote walikuwa ni wataalamu wa masuala ya wanyama?" Namouih akauliza.
"No. Mama yangu alikuwa akifanya kazi kwenye kituo cha redio huko Los Angeles... California. Alikuja kukutana na baba, wakapendana, baadaye ndiyo baba yangu akamhusisha kwenye suala la... you know. Mama alikubali kujitoa kwa ajili ya jaribio, na ikafanikiwa. Baba aliongea na vichwa vikuu kule alikokuwa ameajiriwa kuwaambia kuhusu mimi, lakini hawakumwamini... hasa kwa sababu jambo hilo alilifanyia nje ya kazi zao rasmi. Ila kuna rafiki yake mmoja alionyesha kumwamini, na ndiyo akampa muda wa kuhakikisha anakuja kutoa uthibitisho halisi kwamba alifanikiwa, ikimaanisha mimi nizaliwe..."
"Subiri, unamaanisha kwamba, bado ulikuwa hujazaliwa baba yako alipoongea na hao wakuu?"
"Ndiyo, yaani... alikuwa ndiyo amefanikiwa kumfanya mama atungishe yai langu kupitia njia fulani
ajuayo baba pekee... yaani hakuna mtu mwingine anayejua. Ingetakiwa nizaliwe ili uthibitisho uonekane wazi, lakini kuna jambo lilizuka. Kuna hali ya kutoelewana ilitokea baina ya baba na hao wakuu, kwa hiyo akanitorosha mimi na mama ili tuwe salama," Draxton akaeleza.
"Inaonekana hao watu walitaka tu kuja kukutumia kama kifaa cha experiment... wakumiliki yaani,
wakutendee kama specimen za maabara tu..." Namouih akasema.
"Yeah."
"Okay. Kwa hiyo ulikuja kujua hayo ukiwa na miaka mingapi?"
"10."
"Mama yako ndiyo alikwambia kila kitu?"
"Ndiyo."
"Aliitwa nani?"
Draxton akatabasamu kwa mbali na kusema, "Ivy."
Namouih akatabasamu pia, kisha akauliza, "Na baba yako? Mliishi pamoja baada ya kutoroka?"
Draxton akatikisa kichwa kukanusha huku akisema, "Sikuwahi hata kumjua personally. Zaidi niliona tu picha zake, habari zake, basi. Hatukuwahi hata kuongea kwa sababu alikufa nikiwa na miaka
miwili."
Namouih akamtazama kwa hisia, kisha akauliza, "Na mama yako?"
"Alikufa nilipofikisha miaka 25. Cancer. Kuanzia hapo ni kama sikuendelea kukua tena."
"Pole Draxton."
"Asante. Miaka 70 imepita lakini bado hicho ni kitu kinachoniumiza sana. Hangetakiwa kufa."
"Draxton kuna vitu huwa tu ni lazima vitokee, na wewe haungeweza kum...."
"Ningeweza Namouih... ningeweza. Sema tu sikujua jinsi gani," Draxton akamkatisha.
"Unamaanisha nini?" Namouih akauliza.
Draxton akamtazama na kusema, "Damu yangu... damu yangu ina uwezo wa kuponya."
Namouih akakaza macho kimaswali.
"Sikuzote mama alipojiumiza vibaya, au mimi kumuumiza, ningetumia damu yangu ku-heal majeraha yake. Angeniambia mara kadhaa kwamba baba alisema damu yangu ina uwezo hata wa kuzuia kifo, lakini hakuwahi kumwambia jinsi gani," Draxton akamwambia.
"Mh! Kiukweli Draxton unazidi kunishangaza sana. We' ni kiumbe wa aina gani?"
"Ningekuwa najua ningesema, lakini mpaka leo sijajua baba alifanya nini kunitengeneza namna hii. Hiyo ndiyo njia niliyotumia kuponya vidonda vyako ulipoumia ule usiku."
"Oh! Yeah, ndiyo, nakumbuka nilishangaa kukuta sina hata mkwaruzo. Aisee! Kwa hiyo unanipaka damu yako kwenye kidonda halafu kinapona... Draxton huo ni muujiza!"
"La, Namouih, siyo kitu kizuri. Mwanzoni kinaweza kuonekana kuwa, lakini siyo..."
"Kwa nini useme hivyo?"
"Kwa sababu sina uhakika inakuwa na effect gani mwilini mwa mtu mwingine... endapo itazidi. Mama yangu alipougua sana, nilidhani damu yangu ingeweza kuuondoa ugonjwa wake, ili kuthibitisha theory ya baba kwamba naweza kuzuia hata kifo... lakini nilipompa... ndiyo
akazidiwa..." Draxton akamwambia huku ameangalia chini.
"Ulifanyaje?"
Draxton akabaki kimya.
"Ulimpa anywe? Ulimpa anywe damu yako?"
Draxton akamwangalia tu usoni.
"Na ilikuwa ni yeye ndiyo alikwambia umpe, siyo?"
"Tubadili mada Namouih," Draxton akasema.
"Draxton nisikilize, haikuwa makosa yako..."
"Namouih please... inatosha. Sitazungumzia hilo tena," Draxton akamwambia hivyo na kunyanyuka.
Namouih akanyanyuka pia na kumsogelea, kisha akamshika mikononi na kusema, "Draxton..."
"Samahani Namouih, sikutakiwa kuongelea hilo. Naomba uniulize kitu kingine tofauti na...."
"Draxton nisikilize. Nakuelewa. Nakuelewa vizuri sana. Baba yangu aliugua saratani pia, na hakuna kitu kilichokuwa kizito kwangu kuliko fikira za hatia kila mara nilipohisi kushindwa kumsaidia. Sijilinganishi na wewe, lakini unatakiwa ujue kwamba jitihada zozote ulizofanya kwa mama yako zilikuwa za upendo, na bila shaka alizithamini aana. Nakuomba tu usijichukie kwa kilichompata," Namouih akasema kwa upole.
"Namouih... siwezi kulinganisha hali yangu na ya mtu yeyote yule kwa sababu mimi siyo mtu mzuri.
Kujichukia ni lazima...."
"Hapana Draxton, wewe ni mtu mzuri. Usingekubali kubaki kunisaidia endapo kama usingekuwa na moyo wenye kujali. Ningekuwa nimeshakufa kama ungetaka kuniua lakini hukufanya hivyo. Nimeshatambua kinachokusumbua Draxton. Ni chuki. Chuki dhidi yako wewe mwenyewe. Unajichukia sana mpaka unatafuta njia zozote kujiondoa duniani lakini usiendelee kujichukia namna hiyo. Umepewa baraka kubwa sana kuwa na maisha marefu. Ithamini Draxton," Namouih
akaongea kwa upole.
"Baraka? Jinsi hii? Nageuka kuwa mnyama mkatili anayeweza kuua watu.... hii siyo baraka Namouih. Ni laana," Draxton akasema kwa mkazo.
"No..." Namouih akasema hivyo kwa hisia na kupandisha kiganja chake mpaka shingoni kwa Draxton, akiishika kwa wepesi na vidole vyake laini.
Draxton akamtazama kimshangao kiasi, akiwa hajatarajia jambo hilo.
"Siyo laana Draxton. Sijui kwa nini maisha yako hivi ila kwa kila mtu yana kusudi fulani. Labda ni kwa sababu unajichukia sana ndiyo maana upande wako wa pili unapambana nawe mpaka leo, kwa sababu unauona tu kama kitu kinachohitaji kuondolewa. Sijui sana kuhusu yale uliyopitia mpaka leo, ila ninajua wewe ni mtu mzuri. Nakuamini Draxton," Namouih akaongea hayo huku bado akiwa ameishika shingo ya mwanaume huyo.
Draxton akafumba macho taratibu na kuinamisha uso wake, akifanya ile kawaida ya kuvuta harufu nzuri ya Namouih kwa ukaribu, naye Namouih akaondoa mkono wake shingoni kwake baada ya kutambua kwamba bado alikuwa amemshika namna hiyo, lakini hakusogea nyuma na kubaki amemwangalia tu.
"Kwa nini Namouih? Kwa nini unaniamini wakati mimi ni kitu chenye kutisha?" Draxton akauliza
huku akiwa ameinamisha uso wake bado.
"Ni kwa sababu sasa hivi sikuoni kuwa mtu anayetisha. Mambo fulani kuhusu wewe... yanaendana na mambo fulani kuhusu mimi. So I can relate," Namouih akasema kwa sauti ya chini.
Draxton akamtazama machoni kwa umakini, naye Namouih akawa anamwangalia sana pia.
Kuna hisia fulani mpya iliyokuwa imeanza kujijenga ndani ya hali hii, hisia ambayo hata wao hawakuielewa vizuri, na ilikuwa kwa sababu wote walifanana kwenye baadhi ya mambo yaliyohusu maisha yao ingawa kwa njia tofauti. Simu ya Namouih ikaanza kutoa mlio wa kuita, na macho yake yakashtuka kidogo kutokana na kuzubaa kiasi alipokuwa anamwangalia Draxton, kisha akaitoa mfukoni mwa suruali yake. Haikuwa ikiita kwamba amepigiwa na mtu, kwa sababu mtandao haukufika vizuri maeneo ya huku, bali ilikuwa ni kengele ndogo aliyokuwa ametegesha awali, yaani
"alarm." Ilikuwa ikimkumbusha kwamba muda wa kuondoka ulikuwa umewadia.
"Aam... Draxton... nina... appointment fulani kikazi...."
"Usijali. Unaweza kwenda."
"Hatujatumia hata muda kidogo kumzungumzia Felix... am sorry kwa kuuliza maswali mengine tu...."
"Ni sawa Namouih, tutakutana tena. Nashukuru kwa maneno yako. Wahi tu, tutawasiliana," Draxton
akamwambia.
Namouih akamtazama kiufupi, kisha akageuka na kuifata pochi yake aliyokuwa ameiacha kwenye sofa. "Ukiipaka rangi hii nyumba itapendeza sana," akamwambia Draxton baada ya kumgeukia.
"Ndiyo. Sema, sitaki kuvuta attention ndiyo maana inatakiwa kuonekana kama haionekani," Draxton akasema.
Namouih akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, kisha akaanza kuelekea nje huku Draxton akimfata
taratibu. Namouih alikuwa akitembea kulielekea gari lake huku akajiuliza ni nini kilichomsukuma na
kumpa ujasiri mpaka akamshika mwanaume huyo shingoni na kumsemesha kwa ukaribu mno. Hii
haikuonekana kuwa ni kwa sababu tu mambo yao yalifanana, bali kwamba alikuwa ameanza kumjali sana. Hawakuongea lolote mpaka walipolifikia gari la bibie, naye akafungua mlango na kumwangalia Draxton, aliyekuwa amesimama mbele ya gari.
"Angalia usigonge nyau," Draxton akamwambia kiutani.
Namouih akacheka kidogo huku akiwa amefumba mdomo, kisha akatikisa kichwa kukubali na kuingia ndani ya gari lake. Akashika usukani na kumtazama sana Draxton pale nje akiwaza vitu vingi, huku mwanaume akiwa amenyanyua kiganja chake juu kumpa kwa heri, kisha mwanamke
akaliondoa gari hapo na kuelekea jijini hatimaye.
★★
Baada ya Namouih kuondoka msituni huko, alielekea moja kwa moja nyumbani kwake. Siyo kwamba alikuwa anaenda kukutana na mtu yeyote kama alivyomwambia Draxton ila alisema hivyo kama kigezo tu cha kumruhusu aondoke mapema kwa kuwa sasa alikuwa amejua kwamba mume wake alimfatilia. Kwa hiyo alikuja kufika nyumbani mida ya saa kumi na mbili jioni, naye akakuta gari la Efraim Donald likiwa nyumbani tayari kumaanisha aliwahi kurudi siku hii. Bado Namouih alikumbuka vyema jinsi alivyoudhika sana baada ya kumkamata Suleiman anamfatilia muda fulani mapema ya leo, hivyo alijua angetakiwa kuongea na mume wake kuhusiana na hilo; lakini kama tu mambo mengine, kwa njia nzuri.
Akafika ndani na kumkuta Efraim Donald akiwa ameketi na Suleiman wakitazama mechi pamoja, na baada ya Efraim kumwona mke wake, akasimama na kumwambia aende hapo ili wakae wote. Namouih akamwangalia tu yeye na Suleiman, kisha akaanza kuzielekea ngazi na kupandisha juu kwenda chumbani bila kuwasemesha lolote. Efraim Donald akaamua kumfata mke wake huko huko ili wazungumze vizuri maana aliona bado alikuwa amekerwa sana. Akaingia chumbani na kumkuta Namouih anaongea na simu yake, naye akamsikia akisema kwamba atakutana na huyo mtu muda si mrefu, kisha akakata na kuanza kuvua hereni.
Efraim Donald akamsogelea na kusimama karibu yake, lakini Namouih hakumwangalia hata
kidogo, naye akasema, "Unaondoka tena?"
Namouih akatoa mguno wa kukubali huku akiendelea kufungua hereni.
"Unaenda wapi?" Efraim akauliza.
"Nakutana na Blandina. Tuna maongezi," Namouih akajibu.
"Mbona unaingia ndani nakusemesha hata huitikii?" Efraim Donald akauliza.
Namouih akamwangalia usoni na kusema, "Samahani."
Efraim Donald akakunja uso kimaswali, kisha akauliza, "Umekuwaje?"
"We' kwani unanionaje?" Namouih akauliza kwa ustaarabu tu.
"Okay, najua umekasirika kwa sababu ya Suleiman... lakini Namouih nilikuwa nataka kuhakikisha uko sawa. Mambo mengi mabaya yanaweza kutokea..."
Namouih akawa anamwangalia tu usoni.
"Kwa nini unaniangalia hivyo?" Efraim akauliza.
Namouih akamsogelea karibu zaidi na kuishika kola ya T-shirt aliyovaa kama anaitengeneza. Efraim Donald alikuwa amechanganywa kidogo na hali hii iliyokuwa inaendelea.
"Efraim... ninajua unanipenda. Na umeonyesha upendo wako kwangu kwa njia nyingi sana ambazo
nathamini... haziwezi kulingana na aina yoyote ya fadhili nilizowahi kuonyeshwa kwenye mahusiano. Ninakupenda pia, lakini ninahitaji tu ujue kwamba kwa kipindi hiki... moyo wangu umekuwa ukihisi baridi kali sana, na hiyo ni kwa sababu wa kwako umeshindwa kunipatia joto
linalotakiwa ili nisiumie zaidi. Ninajua unaelewa ninachomaanisha. Moyo wangu unaelekea kuganda Efraim, na kwa sababu wewe ni kama umepuuzia hilo ingawa unaliona... itanibidi niangalie njia nyingine halali ya kuuokoa ili nisije kujipoteza kabisa..." Namouih akasema maneno hayo kwa hisia sana.
Efraim Donald alishangaa, naye akaanza kutikisa kichwa chake kama haamini kabisa kile alichotoka kusikia.
"Namouih! Unamaanisha nini kusema njia halali? Una... unaongelea talaka?!" Efraim Donald
akauliza kwa kutoamini.
Namouih akawa anamtazama kwa njia ya kawaida tu, kisha akasema, "Ulikuwa unasema nikupe muda, lakini muda umepita vya kutosha. Tutaliongelea hili suala vizuri zaidi kwa kuwa na mimi sasa nimekuweka wazi kuhusu kile nachofikiria. Naomba ukae utafakari maneno yangu ili tuje tuongee vizuri, lakini tafadhali usichukue muda mrefu... mume wangu."
Efraim Donald akabaki kumtazama kama vile ameduwaa, naye Namouih akampita na kwenda upande wa pili wa chumba, akianza kuvua nguo yake, kisha akaelekea bafuni kuoga. Mwanaume huyu akakaa kitandani akiwaza vitu vingi sana. Njia ya Namouih ya kuongea ilikuwa ya uhakika kabisa, yaani hakutania hata kidogo. Ikiwa kweli hakutaka kumpoteza mke wake angehitaji
kumwambia ni jambo gani lililokuwa linamsumbua mpaka ashindwe kumpa haki yake, la sivyo,
angempoteza mwanamke huyo mzuri sana kwa talaka.
★★★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★★★
Usikose sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali ya CHANGE. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.
WhatsApp no: +255 678 017 280
e-mail:
eltontonny72@gmail.com