DYLAN [emoji666]
Story by Elton Tonny
Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
ILIPOISHIA....
Dylan, baada ya kuwa amepoteza kumbukumbu ya maisha yake ya zamani, anakaribishwa nyumbani kwa mwanaume aliyemsaidia kuokoka kifo kwenye maji, yaani Baraka. Anampatia baadhi ya nguo zake ili awe anavaa, naye anamwelezea Dylan kuhusu watu wa familia yake, na baadae kijana akapata kuwatambua vizuri baada ya kuwa wamerudi.
Emilia na Steven, watoto wadogo wa Baraka wanamwonyesha Dylan roho ya ukarimu kwa kumkaribisha vizuri, lakini Shani, mke wa Baraka, pamoja na Leila, binti yao mkubwa, hawaonyeshi upendezi wowote kumwelekea Dylan. Ijapokuwa Dylan anatambua kwamba siyo wote wangempokea vyema, anajitahidi kuwa mtaratibu na mwelewa; akitumaini kuweza kukumbuka maisha yake ya zamani haraka ili asiwabane hapo tena.
Usiku wakiwa wamekaa pamoja sebuleni wanaongelea kuhusu jina litakalomfaa Dylan kwa sababu alikuwa amelisahau la kwake. Baada ya kutafuta majina kadhaa, Emilia anachagua jina fulani zuri kwa ajili yake.
"Ethan. Tumwite Ethan," akasema Emilia.
Dylan akamwangalia sana Emilia huku akitabasamu, kisha akamshukuru kwa kumpa jina zuri, na kuanzia sasa, Dylan angeanza kufahamika kama ETHAN.
★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA TANO
★★★★★★★★★★★★★★★
"Steven, Emmy, em' nendeni mkalale, kesho shule," Shani akawaamrisha wanae wakiwa bado sebuleni hapo.
"Aah lakini mama, story zimenoga," akasema Steven.
"Em' nyanyuka huko. Unataka kuanza kusumbua asubuhi-asubuhi wakati unajua palivyo mbali," Leila akamwambia mdogo wake.
"Shule mnayosomea iko mbali?" Dylan akauliza.
"Wee! Yaani kila siku kutembea ni kama kifo," akasema Steven.
Leila akatabasamu kidogo na kusema, "Kifo unakijua wewe?"
"Ndiyo. Kila siku tunapotembea tunakifa," akasema Steven, na Dylan akacheka.
"Haya twende tukalale," Emilia akamwambia Steven, nao wakanyanyuka na kuelekea vyumbani.
Wakabaki wanne sebuleni hapo, Baraka, Shani, Leila, pamoja na Dylan. Nyumba yao ilikuwa na umeme lakini hawakuwa na TV. Hivyo mara nyingi waliketi pamoja kupiga story kama hakukuwa na fujo za Shani na Leila.
"Shule iko mbali kweli au Steven ametia tu chumvi?" Dylan akaanzisha mada.
"Hazikuwa... mbali... mwanzoni. Zimekuwa mbali sasa hivi kwa sababu daraja liliharibika," Baraka akaeleza.
"Kwa nini?" Dylan akauliza.
"Yaani... daraja hilo lilikuwa ndiyo njia ya kuvukia ule upande wa pili... si umeliona wakati tunakuja?" Baraka akamuuuliza.
"Ndiyo..." akajibu.
"Basi, kwa hiyo ilikuwa njia iliyorahisisha watu kwenda na kurudi. Lilipoharibika, ikatubidi tuwe tunazunguka mpaka upande wa mwisho wa bwawa ili kufikia upande wa pili... hata leo, ikiwa lingekuwa halijaharibika tusingechukua muda mrefu hivyo kufika," Baraka akaeleza.
"Mh! Kwa hiyo... Emilia na Steven huwa wanaenda shule kila siku kwa kutembea... wakizunguka namna hiyo?"
"Ndiyo. Inawabidi waamke saa 11 kuanza kujiandaa ili waondoke saa 12 kamili. Kila siku."
"Siyo Emilia na Steven peke yao. Sisi wote," akasema Leila huku anaendelea ku-chat.
"Liliharibikaje?" akauliza Dylan.
"Haijulikani. Yaani lilikuwa zima halafu tukashtukia limenyofoka-nyofoka tu. Ni kama kuna mtu alifanya hivyo," akasema Baraka.
"Mh baba Leila! Yaani mpaka leo bado unaamini hivyo? Nani angeliharibu katikati ya maji mengi bila sisi kumwona? Hata angesimamaje hapo?" Shani akamuuuliza mume wake.
Ni wakati huu ndipo Leila alinyanyuka na kwenda zake chumbani. Shani akanyanyuka pia na kwenda kuandaa mambo kwa ajili ya kesho, kisha akatangulia chumbani, akiwaacha wanaume wameketi hapo.
"Wewe pia unahitaji kupumzika. Ingia chumbani ukalale," Baraka akamwambia Dylan.
"Na wewe?" akauliza Dylan.
"Mimi huwa nakaa-kaa kidogo ndiyo naenda kulala."
"Basi nitakaa nawe kidogo pia."
"Hauhisi maumivu sehemu yoyote?"
"Hapana, niko sawa. Aam.... kwa nini unafikiri kuna mtu aliharibu daraja kimakusudi?" Dylan akauliza.
"Mhmm... ni mambo mengi. Wengi hawaniamini nikiwaambia hilo," akasema Baraka.
"Mimi niko tayari kukusikiliza," Dylan akamhakikishia.
Baraka akashusha pumzi, kisha akaanza kumwambia Dylan alichofikiri.
"Hapa kwenye maeneo yetu, kuna mashamba mazuri sana yanayomilikiwa na watu kadhaa wa huku. Mimi pia ninalo moja, na huwa nalitumia pamoja na familia yangu kwa ajili ya matumizi yetu binafsi..."
"Ndiyo..."
"Sasa, kuna watu fulani ambao walikuwa wanataka kuyachukua kwa kutoa kiwango fulani cha pesa, lakini watu wa huku, kutia ndani mimi, tulikataa. Hatukutaka kuyauza mashamba yetu kwa sababu yanatusaidia sana, na ukitegemea pesa yenyewe waliyotaka kutoa ilikuwa ndogo ukilinganisha na faida ambayo wangepata kutokana na mashamba yetu..."
"Walikuwa wanataka kuyachukua ili..."
"Ili wajengee miradi yao huku. Na wengi walifahamiana na diwani, kwa hiyo tulipokataa inaonekana walikasirika mno..."
"Mh! Kwa hiyo ikawaje?"
"Zilipita siku kadhaa baada ya wao kuahirisha kutulazimisha tulegeze msimamo wetu. Usiku mmoja...mvua kubwa ilikuwa inanyesha. Nilikuwa nimekuja sebuleni kuangalia usalama, usiku huo wa manane, nikaanza kusikia sauti za mlio wa helicopter...unafahamu helicopter?"
"Nd..ndiyo..."
"Ndiyo, nilizisikia. Zilikuwa zinatokea upande huo wa huko bwawani. Mwanzoni nikafikiri labda ilikuwa inapita tu, lakini zikaendelea tu kutoa hiyo sauti. Nikajiuliza mh... kulikoni? Labda helicopter imetua chini? Maana kwa karibu zinakuwa zinatoa makelele, lakini kwa sababu ya mvua kelele nyingi zilikuwa zinazibwa. Baada ya dakika chache, zikaacha. Hapo nikajua tayari ilizima au iliondoka, kwa hiyo nikakaa kidogo kuangalia kama jambo fulani lingetokea. Niliporidhika hakuna kitu nikarudi kulala. Asubuhi inafika wote tunaelekea huko, tunakuta watu wengi upande huu na upande ule wamekwama, wanashindwa kuvuka kwa sababu tayari daraja lilikuwa limeharibika. Wengi wakasema ooh ni mvua inaonekana iliharibu... mbona kamba na chuma za chini za kulishikiza hazikutoka? Mh.. Tukaomba msaada, wapi. Ahadi, ahadi, ahadi, wapi. Hapo nikawa nimeshatambua kulikuwa na jambo limejificha..." akasimulia Baraka kwa hisia.
"Mh! Poleni sana kwa kweli," Dylan akasema kwa kujali.
"We acha tu," akasema Baraka kwa huzuni.
"Hiyo ilikuwa ni lini?"
"Ni kama miaka miwili sasa hivi imepita. Hebu niambie, miaka miwili kweli, wameshindwa kutusaidia? Hmmm... inasikitisha sana."
Dylan aliendelea kusimuliwa mambo mengi kuhusu maeneo haya, akipata kujua maisha ya wakazi wa huko na changamoto ambazo wengi wa upande huu walikabili kutokana na daraja kuharibiwa. Lakini Baraka alimwambia kuwa bado waliendelea kuishi, na hilo lilitosha kwa sababu waliendelea kuwa pamoja kama familia na ni hicho tu ndicho kilijalisha. Dylan alipendezwa sana na utu wa Baraka, naye akaendelea kupatana vizuri na mwanaume huyo kadiri siku zilivyoendelea kusonga.
★★★★
Miezi minne ilipita baada ya hapo (mitatu ilipoisha ndiyo Camila alirudi Brazil), naye Dylan bado aliendelea kuishi kwa bwana Baraka. Jitihada za Baraka za kutafuta alikotokea kijana huyu bado hazikufanikiwa, na kwa kadiri kubwa hakutaka kumwacha tu Dylan bila msaada, hivyo aliendelea kumpa hifadhi kwake.
Wakati huu, Dylan alikuwa amezoeana vyema na wote, ijapokuwa Shani na Leila bado hawakupendezwa na uwepo wake hapo. Shani alimwona Dylan kuwa kama kitu fulani chenye kuwanyonya sana, na Leila alimwona Dylan kama mtu fulani wa hali ya chini asiyekuwa na faida yoyote kwake. Lakini yote kwa yote, Dylan aliendelea kuwa mtulivu na kujitahidi kuishi nao kwa amani.
Emilia ndiye aliyejenga ukaribu sana na Dylan, kwa kuwa Dylan alimwonyesha staha nzuri, na mara nyingi maneno yake yalimsaidia sana msichana huyu kihisia, ijapokuwa Dylan hakutambua hilo. Alimwona Dylan kuwa kama kaka mzuri, naye alitamani dada yake mwenye kutojali awe kama hivyo. Mitihani ya kuhitimu kidato cha nne ilikuwa ikikaribia sana, hivyo Emilia aliongeza bidii ya kusoma ili aweze kufanya vizuri.
Mara kwa mara, Dylan angeenda pamoja na Baraka kule alikofanyia kazi. Aliona jinsi baba huyo alivyojituma sana na ugumu wa kazi yake ulivyokuwa, na mara kadhaa alimsaidia kwa mambo machache ambayo hayakumuumiza kichwa. Kufikia wakati huu, kidonda chake kichwani kilikuwa kimeacha kutoa maumivu, lakini bado alivaa bendeji kichwani ili tu kuweka usalama. Rasi zake zilikuwa zimeongezeka na uso ulikuza ndevu nyingi, hivyo alionekana kama mtu fulani mwenye umri mkubwa sana. Alizoeana na watu kadhaa maeneo ya kule kwenye soko, ambao walipendezwa sana na upole na ustaarabu wake.
Ilikuwa ni siku fulani mida ya jioni, Dylan alikuwa akirudi nyumbani mwenyewe baada ya Baraka kumwambia atangulie, pale alipofika usawa wa daraja lile na kusimama kulitazama. Aliangalia jinsi chini kule palivyokuwa mbali, na jinsi maji kufikia upande wa pili yalivyokuwa mengi. Ngome nene za kulishikiza kule chini bado zilisimama, lakini sehemu yote ya kutembelea katikati mpaka mwishoni kwa pande zote ilikuwa imebomoka-bomoka vibaya sana.
Wakati alipogeuka akitaka kuondoka, kichwa chake kikapatwa na taswira ya mchoro fulani ambao ulikuwa na mwonekano wa daraja hilo. Alitulia kidogo, kisha akalitazama tena. Alipoendelea kuliangalia, mchoro huu ukazidi kujitengeneza kwenye akili yake; yaani ni kama akili yake ilikuwa inalichora daraja hilo.
Hakutambua ni kwa nini hii ilikuwa inatokea, lakini sababu ilikuwa ni kwamba alisomea masuala ya ukandarasi kwa miaka mingi, hivyo akili yake ilikuwa imeshazoea michoro mingi ya ujenzi kipindi cha nyuma. Bila yeye kutambua, akili yake ilikuwa inafanya kazi kumwonyesha jinsi ambavyo daraja hilo lingeweza kukarabatiwa, lakini akawa haelewi jambo hilo. Akageuka zake tu na kuendelea kuelekea nyumbani, akihisi labda kichwa chake kilikuwa kinamwonyesha vitu alivyoona tu zamani.
Alipofika nyumbani, alimkuta Steven nje akiwa anafua shati lake la shule, naye akatabasamu na kumfata pale.
"Steven..." akamwita.
"Naam... shikamoo kaka Ethan?" Steven akamsalimia.
"Marahaba, hujambo?" akamwitikia.
"Sijambo," Steven akajibu kivivu.
"Vipi, mbona kinyonge hivyo jembe?"
"Nimechoka. Mbali kweli."
"Pole."
"Asante."
Steven akainama ili atoe shati lake aanze kulikamua maji, pale Dylan alipoona alama fulani ya uvimbe kwenye mkono wake kutokea begani.
"Steven, nini hicho mkononi?" akamuuuliza.
"Naam? Wapi?"
"Hapo hivi. Umefanyaje, mbona pamevimba?"
"Aaaa... mwalimu alinipiga stick," Steven akajibu.
"Kwa nini amekupiga vibaya hivyo?"
"Nilikuwa nimesinzia darasani wakati anafundisha. Kwa hiyo akaniwasha fimbo kwa nguvu mgongoni... inauma!"
"Aisee... pole. Kwa nini unalala darasani wakati anafundisha?"
"Sifanyi makusudi kaka Ethan. Usingizi wa saa 11 mtamu, kila siku kuamka muda huo, kutembea, nakuwa nachoka. Najitahidigi nisilale lakini mara nyingine usingizi unakuwa unanilemea," Steven akaeleza.
"Dah, ila walimu na wenyewe bana! Wako kama wanyama, sijui wakoje..."
"Wakuda tu. We subiri, nami nikija kuwa mwalimu nitakuwa nafumua mtoto wake! Heeee..."
Dylan akacheka kidogo. Alimwonea huruma sana Steven, kwa kuwa alikuwa mdogo mno, na inaonekana kuna mambo mengi magumu alipitia shule kutokana na shida hiyo ya umbali.
"Umekula?" akamuuliza.
"Eee angalau nimekuta chapati na maharage kwenye hotpot. Zimetuliza maumivu," Steven akajibu.
Dylan akatabasamu na kumwambia akaanike nguo sasa. Yeye akaelekea ndani ili aweze kutoka kuoga na kubadili nguo.
Ilifika usiku, na wote wakawa nyumbani tayari. Wanawake walikaa nje mara nyingi hasa kwa sababu ya kupika, naye Baraka pamoja na Dylan wangekaa ndani wakiongea, au nje kama kungekuwa na uhitaji wa kufanya hivyo. Baraka alikuwa akimsimulia Dylan kuhusu mtu fulani mwenye fujo sana aliyeitwa Lazaro kule anakofanyia kazi, ambaye alitokeza ugomvi muda ule Dylan ametangulia kuja nyumbani. Dylan akamwambia ikiwa angehitaji msaada kumdhibiti basi amwambie, naye Baraka akacheka na kumwambia alisuluhisha jambo hilo. Wakaendelea na story mpaka muda wa kula ulipofika.
Ilikuwa ni wakati Leila anaingia ndani akiwa amebeba chombo kilichokuwa na chakula, pale alipoteleza kutokana na maji yaliyomwagika kidogo chini wakati Steven ameleta maji ya kunawa. Dylan alikuwa amepatwa na machale ya haraka yaliyomfanya atende upesi mno; akanyanyuka kutoka alipoketi na kumwahi Leila kabla hajadondokea kichwa chake chini. Alikishika kiuno chake kwa kasi na kukigeuza ili awe kwa chini yake, hivyo miili yao ilipoanguka, wa Dylan ukawa chini ya mwili wa Leila ili asiumie.
Wote walishtuka na kwenda hapo wakiwaangalia. Hotpot alilobeba lilikuwa na mboga za majani, nayo yote ikawa imemwagika. Leila akanyanyua uso wake na kumwangalia Dylan, ambaye alikuwa amemshikilia bado chini hapo.
"Uko sawa?" Dylan akamuuliza.
"Unafanya nini... em' niachie!" Leila akamwambia kwa ukali, huku akijitoa mwilini mwa Dylan.
"S..samahani..." Dylan akasema.
Shani akamshika Leila akimwangalia kwa makini, kisha akamuuliza, "Umekuwaje?"
"Sijui nani amemwaga maji hapa..." akasema Leila kwa kuudhika na kusonya.
"Muwe mnakuwa waangalifu bwana. Ethan asingekudaka, ungeumia vibaya," Baraka akawaambia.
"Ethan uko sawa?" Emilia akamuuliza Dylan.
Dylan alikuwa amejishika kichwa, huku akikaza meno yake. Kichwa chake kilikuwa kimepiga chini wakati anamdaka Leila, hivyo alihisi maumivu kiasi.
"Ndiyo niko sawa," akajibu kwa kuficha ukweli.
"Aagh mboga yote imemwagika jamani!" Shani akasema kwa kukwazika.
Emilia akatoka kwenda kuchukua dekio, naye akarejea na ndoo yenye maji ili apasafishe.
Wengine wakakaa ili kujiandaa kula, wakiwa wanamsubiria Emilia amalize. Kwa kuwa kulikuwa na mboga nyingine, wangetumia hiyo hiyo kulia ugali, kwa hiyo hakukuwa na shida sana upande wa chakula. Shida ikawa upande wa Dylan. Kichwa kilimsumbua, siyo kuuma, bali alianza kuona vitu vingi kama maruerue yaliyokuwa yanachanganya sana, nayo yalimnyima raha. Hata hamu ya kula ikamtoka kabisa.
Akala chakula kidogo sana, kisha akawaaga kuwa anaingia kulala, akiwaacha wanamwangalia wasijue amepatwa na nini. Muda wote ambao Dylan alikuwa amejilaza, alijaribu kuviunganisha vipande vidogo vidogo alivyoona kichwani ili atengeneze taswira nzuri, lakini akawa anashindwa. Mwishowe alipitiwa na usingizi baada ya muda mfupi akiwa kwenye msukosuko huo wa kichwani.
★★★
Dylan aliamka alfajiri mapema sana. Kulikuwa na giza nje bado, naye aliweza kuwasikia Emilia na Steven wakiwa katika harakati za kujiandaa. Steven sikuzote alikuwa mzito alipoamshwa mapema namna hiyo, lakini baada ya kuoga angejisikia afadhali na kujiandaa vyema kwa ajili ya shule. Walipomaliza, walitoka kwa pamoja baada ya Emilia kuonana na baba yake, kama ilivyokuwa kawaida. Dylan alitoka na kumkuta Baraka akiwa ameshaamka tayari, naye Baraka akashangaa kidogo kwa sababu Dylan hakuwa na kawaida ya kuamka alfajiri mno; sanasana mida ya saa moja au saa mbili asubuhi.
Dylan aliwaangalia Emilia na Steven wakiondoka, naye aliwaonea huruma sana kwa kuwa alijua vizuri jinsi ilivyokuwa ngumu kwao kila siku kutembea. Baadae, maman'tilie na dadan'tilie wakawa wameamka pia. Walikuwa na kawaida ya kusaidizana kuandaa vitu usiku kwa ajili ya siku inayofuata, hivyo asubuhi wangeondoka wakiwa wamevibeba kichwani, halafu baada ya kumfikisha mama yake mgahawani, Leila angeelekea alipofanyia kazi.
Baraka alikuwa na kawaida ya kwenda mgahawani kwa Shani aidha asubuhi au mchana ili kupata msosi, kwa hiyo tokea Dylan alipoanza kuwa anaenda naye kazini kwake, mara kwa mara walienda pamoja pale. Ijapokuwa Baraka na mke wake hawakuwa na maisha ya hali ya juu, walijitahidi sana kuwaandalia mahitaji watoto wao kwa kila kitu ambacho waliweza kufanya; na walijitoa kwa moyo wote, haijalishi ni changamoto zipi walipitia.
Asubuhi hii, Dylan alimwambia Baraka atangulie, naye angefata ndani ya muda mfupi ili kwenda kumsaidia kazi kadhaa huko.
Baada ya Baraka kuwa ametangulia, Dylan akafunga nyumba kisha akaelekea sehemu ile yenye lile daraja. Alisimama hapo, akilitathmini kwa makini sana. Ilikuwa ni kama aliingiwa na kitu fulani kilichomwambia kwamba angeweza kulitengeneza, naye alitaka kujihakikishia kwamba kweli angeweza. Akarudi tena nyumbani na kuanza kutafuta kalamu na karatasi. Alifanikiwa kupata penseli ndogo iliyochongwa vizuri, na daftari ambalo alitambua halikutumika tena. Baada ya kukuta karatasi kadhaa zilizokuwa bila maandishi, akalichukua pia, kisha akarejea darajani pale.
Alifika na kuketi kwenye jiwe dogo pembeni ya mwingilio wa kivuko hicho. Akafumba macho na kuvuta pumzi kisha kuishusha taratibu ili kutuliza akili yake. Akayafumbua macho na kuanza kulitazama daraja hilo kwa umakini tena. Jinsi lilivyokuwa limebomoka kuanzia katikati mpaka mwishoni, haikuonekana kuwa mvua ndiyo iliyoharibu, bali ni KITU fulani ndiyo kiliharibu. Akili yake yenye werevu mwingi ilimsadikishia kabisa kwamba daraja hilo lilikuwa limebomolewa kwa kutumia mashine fulani, hivyo Baraka alikuwa sahihi aliposema liliharibiwa kimakusudi.
Kadiri alivyoendelea kulitazama, ndivyo njia za michoro (patterns) zilivyoendelea kujichora kwenye akili yake. Hivyo, akawa anachora kwenye daftari mambo yote ambayo taswira yake ilimwonyesha, na mara nyingi hata alikuwa haangalii daftari! Alitumia saa zima akiwa ameketi hapo anachora, kisha akatazama daftari na kuona alikuwa ameweza kuchora njia za kulitengeneza daraja hilo. Alitabasamu, akitambua kwamba alikuwa ana ujuzi fulani kuhusu ujenzi, lakini bado hakukumbuka vizuri ilikuwa kutokea wapi.
Muda mfupi baadae akaondoka na kuelekea kwa Baraka, akiwa amelikunja daftari alilochorea na kuliweka nyuma kwenye mfuko wa suruali yake. Mambo kule yalikuwa kama kawaida; vyuma. Alimsaidia kukata, kurekebisha, kuunganisha, na kutengeneza vitu mbalimbali. Dylan alikuwa amejifunza mambo haraka kwa hiyo miezi michache aliyoanza kumsaidia kazi Baraka, na hata watu kadhaa waliomfahamu huko walimpelekea vitu vyao arekebishe, wakimwita yeye pia fundi. Kujifunza kwake haraka kulitokana hasa na kichwa chake chepesi kushika mambo, hivyo aliwapendeza wengi kwa ustadi wake mwingi.
Ilipofika mida ya jioni baada ya wawili hao kuwa wametoka kwa Shani kula, wakawa wameketi kwa nje mbele ya ofisi yake Baraka. Walikuwa wakipiga story na watu wengine wa eneo hilo, na wengi walimzungumzia yule jamaa aliyemletea fujo Baraka jana. Kisha baadae, wakawa wamebaki watatu tu hapo; Baraka na Dylan, wakiwa na kijana mwingine aliyeitwa Konde, ambaye aliuza nguo za dukani maeneo hayo.
"Weweee! Michepuko ndiyo dili! Hivi wewe huwonagi jinsi michepuko inavyojuwa kupendeza? Yaani malavidavi kama yowte... ahmm hoowney, karibu, mwaah... jamani baby nimeku-miss... mke ataweza hayo?" akasema Konde, akiwa anabishana na Baraka, huku Dylan anasikiliza akicheka.
"Mke wako tu ndiyo hawezi! Na tena siyo kwamba hawezi, ni wewe tu ndiyo umepoteza akili kwa michepuko yako!" Baraka akamwambia.
"Aa wapi! Mchepuko baba... acha kabisa. Yaani hee, hee, hee, mpaka unatamani kubaki naye tu! Kwanza wanajua kupendeza, ni wazuri sana," akasema Konde.
"Ni mzuri kwa sababu pesa zako zote unapeleka huko akatumie wakati kwa mke wako unaacha buku tu. Unamkomaza mkeo na majukumu af' humtunzi, atakuwa mzuri saa ngapi mbwa wewe?" akasema Baraka.
Dylan na Konde wote wakacheka.
"Eti jamani? Matunzo zero. Tunza mkeo achana na michepuko fala wewe. Angekuwa mbaya usingemwoa," akasema Baraka.
"Hakuna kitu wewe," Konde akakanusha.
"Tatizo wakishagaoa wanachukulia ndiyo basi tena na matunzo hawatoi, wakati waliwakuta wadada wa watu wanang'aa," Dylan akasema.
"Umeona?" akasema Baraka.
"Dah! Ethan! Yaani na wewe unamsapoti huyu mbabu wa kale?" Konde akasema.
"Kwenda huko bwege wewe!" Baraka akamwambia kiutani.
Wote walifurahia sana maongezi yenye kujenga lakini yenye utani mwingi. Ni wakati huu ndipo mteja alifika kwenye duka la Konde, hivyo akatoka hapo akiharakisha kumfata.
"Yaani vijana wa siku hizi!" akasema Baraka.
"Ahahah... wanajua kuhusika," akasema Dylan.
"Ahahah... Vijana wa kiume wapo kwa ajili ya kuonja-onja tu. Hata kama ameoa, anataka kuhalalisha kuonja, unafikiri wataacha kuwadharau wake zao?" akasema Baraka.
"Ahahah... zamani walikuwaga hawaonji-onji?"
"Aah... zamani wazee walionja nje lakini kwa siri sana. Mahusiano kwa vijana siku hizi ni fashion tu siyo stara tena, hawana hata hofu ya Mungu. Hawajui kutofautisha tamaa na upendo," akasema Baraka.
"Kweli kabisa."
Baraka akashusha pumzi, kisha akasema huku akisimama, "Naona tufunge tu tupandishe."
"Sawa. Aam... Baraka..." Dylan akaita.
"Naam..."
"...kuna jambo nataka kuongea nawe."
"Ahah... mbona serious sana? Ni jambo baya?"
"Hamna, ni... zuri. Nahitaji tu msaada wako."
"Sawa... niambie," Baraka akaweka umakini.
"Nahitaji kuwa nachukua vyuma kwenye hicho chumba chenye vyuma vingi ambavyo havitumiki," akasema Dylan.
"Kwa nini? Unataka kuvifanyia nini?"
"Nataka... kulitengeneza daraja."
"Eti? Daraja hilo lililoharibika?"
"Ndiyo."
Baraka alishangazwa na uhakika wa Dylan.
"Nini kimekufanya ufikie uamuzi huo?" Baraka akamuuliza.
Dylan akatazama chini.
"Kuna vitu umekumbuka? Ulikuwa... fundi wa madaraja au?" Baraka akauliza.
"Hapana...sijui...ila..." Dylan akashindwa amwelezee vipi.
Baraka alikuwa anamwangalia kwa maswali mengi sana. Dylan akamshika begani kwa kiganja chake.
"Najua inaweza kuwa ngumu kunielewa. Lakini... ninaomba tu uniamini. Ninajua ninaweza kufanya hili jambo," akamhakikishia.
Baraka akatafakari kidogo, kisha akasema, "Lakini ni refu. Utawezaje kulitengeneza mwenyewe?"
"Nahitaji tu muda, na kibali chako. Nikiwa na kila kitu nitakachohitaji, nitafanikisha," Dylan akasema kwa uhakika.
Baraka akashusha pumzi tena, kisha akatikisa kichwa kwa kustaajabishwa na kijana huyo.
"Sawa. Siyo kwamba vyuma hivyo huwa situmii, lakini unaweza kuchukua unavyohitaji," akamwambia.
"Ahah... asante sana," Dylan akafurahi.
"Kwa hiyo unataka kuanza lini?"
"Haraka iwezekanavyo. Na... nahitaji kufanya maandalizi kwanza, kwa hiyo jambo hili liwe kati yetu wawili mpaka nitakapomaliza," Dylan akasema.
Baraka akatikisa kichwa taratibu kukubali, akiona kwamba kweli kijana huyu alikuwa na nia hiyo ya kufanya jambo ambalo halingefikirika kwa yeyote. Dylan aliamini kabisa kwamba angeweza kuleta badiliko, na sasa kile ambacho kingefuata ilikuwa ni kazi tu.
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
WhatsApp +255 787 604 893