SEHEMU YA 27, 28, 29, 30
"Unasemaji wewe bishoo" Felix aliuliza kwa dharau.
"Ni mimi ndiye niliyebuni mbinu ya kumtumia Moses ili kumfanya Elizabeth Neville aseme kila kitu. Ni Moses nilisema sio mtoto mdogo wa Moses mgonjwa asiojiweza kwa lolote. Mpango haukuwa huo" Richard alisema.
"Sikiliza we bishoo. Mpango 'A' ukifeli siku zote tunaingia katika mpango 'B'. This is our principle katika hizi kazi. Usituletee mawaidha ya huruma hapa. Hapa hatuhubiri" Felix alisema.
"Mpango huu niliubuni mimi narudia tena. Na haukuwa na plan 'B'. Plan ilikuwa ni 'A' tu ambayo ilikuwa kumleta Moses hapa. Sio huyu mtoto asiye na hatia. Ni plan 'A' tu na tumeshafeli" Richard alikuja juu.
Kule nje. Katika gari alilokuja nalo Felix kutoka Mbeya kulikuwa na mwinuko mdogo katika buti la gari la Felix. Ulitokea mwinuko na kisha buti kurudi tena chini. Ilikuwa ni ishara kwamba ndani ya buti kulikuwa ni mtu. Ni nani? Ameingiaje? Hakuna aliyekuwa anajua.
Baada ya dakika tano buti la gari likainuka tena. Kwa kutumia macho mawili ambayo yalikuwa kwenye buti yaliyachunguza mazingira yale. Yalikuwa macho ya kijasusi. Yakitathmini nini sasa cha kufanya kwa wakati ule.
"Hapa ndipo anapoishi jamaa. Yaani nimekaa kwenye buti kwa muda mrefu sana. Sijui nini kinachondelea huko duniani. Sijui Moses na Joyce kiliwakuta nini pale ofisini kwangu. Lakini kwakuwa nipo hapa majibu ya maswali yangu yote yatajibiwa nikipita mlango ule" Dokta Yusha aliwaza peke yake akiwa ndani ya buti katika gari la Felix.
Akiwa bado anachungulia kupitia upenyo mdogo alilishuhudia gari lengine liingia mle ndani. Alimwona daktari akishuka kutoka siti ya mbele.
Kumbe baada ya meseji ya Mwanasheria mlevi Dokta Yusha alipiga hatua moja mbele. Aliingia kwenye buti la gari la Felix bila mwenyewe kujua.
"Wamemleta daktari bila shaka kwa ajili ya mtoto Anna. Sasa kwanini wamteke Anna? Wana lengo gani hawa jamaa?" Dokta Yusha alijiuliza maswali mfululizo akiwa katika buti.
Alimshuhudia yule daktari akikaguliwa pale mlangoni na kisha kuingia ndani.
"Tutaonana giza likitawala" Aliwaza.
Saa sita kamili usiku giza likiwa totoro Dokta Yusha alitafuta namna ya kutoka nje ya buti ya gari bila kujulikana. Taratibu alifungua buti na kujitupa chini mithili ya mzigo. Harakaharaka alijiviringisha hadi uvunguni mwa gari. Akiwa kule uvunguni aliiona miguu ya mtu ikielekea kule kwenye gari. Akajua kwa vyovyote jamaa kasikia kishindo chake wakati alipojiangusha. Akakaa tayari kukabiliana nae. Jamaa alisogea hadi katika gari ya Felix. Aliwasha tochi na kuanza kulimulika gari. Kule chini Dokta Yusha alijibana vizuri ili asimulikwe. Akajisogeza kuelekea upande wa pili. Jamaa na tochi yake akaelekea ule upande aliokuwa kajificha Dokta Yusha. Kwa kasi Dokta Yusha akajiviringisha kurudi ule upande akiotokea jamaa. Jamaa akasimama, akainama kidogo ili achungulie uvunguni. Lilikuwa ni kosa la mwaka. Alikutana na teke la uso! Lililoipangusa vizuri pua yake. Jamaa aliona vimulimuli. Alikosa umakini kabisa. Lilikuwa kosa lengine. Harakaharaka Dokta Yusha alitoka uvunguni na kumkaba yule jamaa kwa nyuma. Bonge la kabali. Jamaa alijitahidi kujitoa lakini wapi. Dokta Yusha alikaza hasa. Jamaa alianza kuishiwa nguvu. Hewa ilikuwa ngumu kuipata. Dokta Yusha alikaza roba kwa mkono wake wa kushoto, huku mkono wake kulia akipeleka usoni. Kwa kutumia vidole vyake viwili aliviingiza machoni kwa jamaa. Aligandamiza. Jamaa akataka kupiga kelele. Kelele hazitoki kutokana na ile roba. Ilikuwa kasheshe!
Dokta Yusha akakaza zaidi ile roba. Jamaa alienda kuzimu taratibu. Dokta Yusha akamvuta yule jamaa na kumsweka uvunguni mwa gari. Kwa kunyata akaanza kuelekea katika ile nyumba. Akazunguka na kuelekea upande wa kushoto wa nyumba. Akalikuta dirisha. Akachungulia. Kilikuwa chumba kitupu. Hakuna kitu. Akasogea kwa mbele kuelekea nyuma ya ile nyumba. Akaliona dirisha lengine lakini lilikuwa limefungwa. Akazidi kuelekea mbele, dirisha la tatu. Alichungulia. Uso kwa uso alikuwa anatazamana na Elizabeth Neville!!!
"Elizabeth Neville" Dokta Yusha alisema kwa sauti ndogo. "Kumbe Elizabeth yupo humu?"
Dokta Yusha akaona hatari iliyopo kuendelea kukaa katika nyumba ile. Sehemu aliyopo Elizabeth Neville lazima itakuwa sehemu ya hatari.
"Nitaweza kweli kumkomboa Elizabeth Neville mwenyewe. Hapana. Namhitaji Mwanasheria mlevi" Dokta Yusha akawaza. "Peke yangu itakuwa ngumu. Lazima nitafute namna ya kutoka humu. Lazima nirejee na Mwanasheria mlevi kuja kuumaliza mchezo. Sasa nitatokaje?"
Dokta Yusha akaelekea ukutani. Alienda kutafuta namna ya kutoka nje kupitia ukutani. Ulikuwa ukuta mrefu ambayo kwake hakuwa anashindwa kuupanda. Alipougusa tu. Akahisi kitu cha baridi kikigusa shingo yake.
Bastola.
***
Dokta Yusha akaelekea ukutani. Alienda kutafuta namna ya kutoka nje kupitia ukutani. Ulikuwa ukuta mrefu ambayo kwake hakuwa anashindwa kuupanda. Alipougusa tu. Akahisi kitu cha baridi kikigusa shingo yake.
Bastola.
***
Mwanasheria mlevi bado alikuwa katika harakati za kumsaka Dokta Yusha pamoja na yule jamaa mvamizi aliyemteka mtoto Anna na kuwaacha Moses na mkewe wakiwa majeruhi. Alitafuta kwa kila namna lakini hakujua kabisa wameelekea wapi. Mwisho aliamua kumpigia Mkurugenzi wa usalama wa Taifa ili kumueleza kilichotokea.
"Mzee za sahivi" Mwanasheria mlevi alianza simuni baada ya simu yake kupokelewa.
"Nakusikiliza Mwanasheria" Aliitika.
"Huku Mbeya bado hali mbaya. Moses na mkewe hali zao sio nzuri hata kidogo. Mtoto Anna hajapatikana hadi sasa sambamba na Dokta Yusha. Nimejitahidi kadri niwezavyo ili kupata angalau fununu kwamba watakuwa wapi lakini sijafanikiwa" Mwanasheria mlevi alisema.
"Mmh this is unbelievable!! Wamepoteaje hao watu? Sasa una shauri ofisi ifanye nini kwa sasa?"
"Hii vita imekuwa ngumu sana. Tunapambana na watu tusiowajua lakini pengine wao wanatujua. Sasa ili twende sawa naomba uniongezee mtu. Kwa sasa nipo peke yangu bila dira yoyote. Lazima tuongeze mtu kwa ajili ya ushauri na mapambano. Hivi Daniel yu wapi. Daniel Mwaseba anatosha sana kuumaliza mchezo" Mwanasheria alisema huku sauti yake ikionesha matumaini.
"Daniel yupo likizo katika mji mmoja huko Ureno unaitwa Faro. Ana likizo ya mwezi mmoja ambao hata wiki mbili hana tangu ameondoka. Lakini neno langu ni amri kwake. Nitahakikisha anarejea, akusaidie kuifanya hii kazi kisha arejee tena huko Faro"
"Nashukuru sana mkuu kwa kuwa na nia ya kutekekeza ombi langu. Mlete Daniel mjini hapa aturahisishie kazi, lazima akate mizizi" Mwanasheria alisema.
Wakaongea maongezi kidogo kesho wakatakiana usiku mwema na kulala.
"Daniel Mwaseba again. Hawa sasa wamezoea vibaya. Huku ni kumpa kichwa tu Daniel kila kazi yeye. Safari hii simwiti ng'o. Wataifanya kazi wenyewe" Mkurugenzi wa usalama wa Taifa alikuwa anawaza wakati akiutafuta usingizi.
"Siwezi kulala wakati mwenzangu sijui yupo wapi? Siwezi kuwa msaliti kiasi hicho. Lazima nipambane usiku huu kujua mbivu na mbovu" Mwanasheria alitoka katika hoteli aliyopanga na kutoka nje. Aliangalia saa yake, ilikuwa saa nane na dakika tisa usiku. Alichukua pikipiki yake na kuelekea katika hospitali ya K's.
"Yalipoanzia mambo haya ndipo patakaponipa majibu. Mtu hawezi kufanya mambo yale mchana kweupe bila kuacha alama yoyote nyuma yake"
Dakika kumi baadae alikuwa nje ya hospitali ya K's. Alikaa katika kibanda kidogo ambacho mchana hutumiwa na mshona viatu. Alitulia tuli huku akiangalia kwa makini hospitali ile iliyoleta kizaazaa mchana. Alitumia dakika thelathini na moja tu. Ndipo alipoona tukio la kushangaza.
Aliiona gari aina ya Noah ikija kwa kasi. Kisha wakashuka watu wanne waliojazia wakiwa na mavazi meusi. Walisimama nyuma ya Noah yao wakipeana maelekezo.
"Wale sio watu wazuri. Kuna kitu kinaenda kutokea hapa. Ngoja niwe na subira" Mwanasheria alijionya mwenyewe.
Baada ya majadiliano jamaa waliingia ndani ya hospitali. Waliingia watu watatu wakimuacha mmoja palepale ndani ya gari. Ilichukua dakika saba tu, wale watu walitoka mkukuumkukuu, waliingia katika gari yao na kuondoka kwa kasi, Mwanasheria mlevi naye alikuwa nyuma yao juu ya pikipiki.
***
"Sasa tumekamilika. Hapa Martin Hisia, pale Richard Phillipo na kule Binunu Issa. Soon tunaenda kuimaliza hii kazi ya Mheshimiwa Lucas, na pengine ikawa ndio kazi yangu ya mwisho kama nilivyomuahidi Binunu" Usiku wa manane akiwa kitandani Martin alikuwa anawaza. "Kesho asubuhi tunaianza hii kazi. Kwa mikakati tuliyoipanga na Binunu jioni, hii misheni imekuwa soft sana. We are going to make it hureeeh"
Upande wa Mwanasheria bado alikuwa juu ya pikipiki yake akiwafata wale watu wanne waliokuwa ndani ya Noah nyeusi. Jamaa walipofika Mafiat walikata kulia njia iliyokuwa inaelekea Tunduma. Dhamira ndani ya moyo wake ilimwambia wale majamaa wana kitu na kule hospitali walifanya kitu. Ni kitu gani hiko? Swali hilo lilimfanya Mwanasheria aongeze kasi ya pikipiki kuwafata wale jamaa ili kukifahamu.
Noah ilipofika katika kituo cha daladala cha Kadeghe ilisimama kidogo. Mwanasheria naye alisimama ghafla usawa wa ukumbi wa Dhando akiwa makini na wale jamaa. Alimwona mtu mmoja akishuka ndani ya ile Noah huku akiwa ameweka simu yake sikioni.
" Hawa jamaa ni wakina nani lakini? Hawaaminiani hata wenyewe. Wako pamoja lakini kuongea na simu tu imebidi wasimame ili aongelee nje" Aliwaza Mwanasheria akiwa kaiinamia pikipiki yake akijifanya kuitengeneza.
Majamaa wawili walishuka kwa siri katika ile Noah na kuchepuka katika barabara inayoelekea mahakama kuu. Walienda kidogo na kukata kulia njia iliyokuwa inaelekea hosteli za Goodwill. Walipofika usawa wa uwanja wa mpira wa kikapu wa chuo kikuu cha Mzumbe walikata tena kulia na kuifata barabara iliyowafikisha tena katika barabara kuu.
Ghafla! Mwanasheria mlevi akiwa kaiinamia pikipiki yake alijikuta akipigwa teke la nguvu la makalio. Aliruka juu kilevi huku akitoa makelele ya ajabu.
"Yeleuwiii Mambo gaani haya mbona hatujapinga boko na nyinyi?" Mwanasheria mlevi alisema kimasihara.
"Usijifanye chizi. U mzima na umekuwa ukitufatilia tangu K's hospitali. Ukiwa mpole waweza kutoka katika mikono hii mibaya. Twambie ukweli kwanini unatufatilia?" Jamaa mmoja kati ya wake wawili aliuliza.
"Mimi natoka zangu Mbeya Carnival kupata kinywaji. Nimefika hapa pikipiki yangu imezinguaa. Mimi sijui mambo ya K's wala kufatilia. Mimi ni Mwanasheria, Mwanasheria lakini mlevi" Mwanasheria alisema huku akilia kilevi.
Jamaa walipata utata juu ya yule mlevi anayejiita Mwanasheria. Wamchukue ama wamwache.
"Twende naye Ngome huyu ndo ulevi wake wa kuwafatilia watu asiowajua utakwisha. Ni mjanja tu huyu lakini anakijua anachokifanya" mmoja wa wale watu alisema.
Walimbeba juujuu Mwanasheria na kuelekea naye katika gari lao. Walipofika naye tu yule jamaa akiyejifanya akiongea na simu naye aliingia na safari ya kuelekea Ngome ilianza.
Gari ilipofika Nzovwe jamaa mmoja akamnusisha kitambaa cheupe Mwanasheria. Baada ya sekunde thelathini alilala na hakujua tena nini kilikuwa kinaendelea hapa duniani.
Muda uleule wakati Mwanasheria mlevi akidhibitiwa na majamaa wanne wenye Noah na ndio ulikuwa muda uleule Dokta Yusha alihisi ubaridi katika shingo yake. Ubaridi wa bastola. Alijaribu kuangalia kwa jicho la wizi alishangaa. Alikuwa anatazamana na mtu asiyevaa nguo lakini alikuwa na viatu chini. Alikuwa anaitwa Gon!! Naye alitekwa na kuingia katika mikono haramu.
***
ITAENDELEA BAADAE KIDOGO
Pseudepigraphas