SEHEMU YA 50 - 54
Kule chini kulikuwa na njia moja tu iliyoelekea upande wa kulia. Wote wanne wakitanguliwa na Daniel Mwaseba walianza kuifuata njia ile. Kila mmoja akijaribu kumlinda mwenzie. Walikuwa wanaenda taratibu katika njia nyembamba iliyotengenezwa kwa ufundi mkubwa. Ilikuwa kimya, kila mmoja akiwaza lake moyoni.
Walitumia dakika arobaini na tano wakiwa wanatembea katika njia ile nyembamba. Wote walishangaa urefu wa njia ile. Kwa makadirio yao walijua kwamba walishatoka eneo la Sabasaba. Na bado mbele njia ilikuwa bado inaelekea mbele. Walizidi kutembea huku hofu ikianza kuwaingia moyoni mwao. Walianza kuhisi kwamba walikuwa wanaelekea katika kifo!!
Dakika kumi na tano baadae ile njia ilianza kuwa pana kidogo. Sasa walikuwa wanauweza wa kupita wakiwa sambamba wawiliwawili. Hivyo Daniel Mwaseba alikuwa bega kwa bega na Dokta Yusha na Mwanasheria mlevi alikuwa bega kwa bega na Inspekta Jasmin.
"Yaonesha twakaribia kufika walipo hawa majamaa. Umakini wahitajika zaidi" Daniel alinong'ona kwa sauti ndogo iliyosikiwa na wote.
Walitembea kama dakika tatu tangu onyo lile la Daniel.
Ghafla!! katikati ya ile njia kulikuwa amesimama mtu mwembamba aliyekuwa amevaa nguo nyeusi tupu. Alikuwa mithili ya kivuli, juu shati jeusi, chini suruali nyeusi na juu kofia nyeusi. Alikuwa amesimama upande huku akiwa ameushika ukuta kwa mkono wake wa kulia. Alikuwa anawatazama wale askari wanne akiwa kimya. Daniel Mwaseba alikuwa ndiye wakwanza kumuona mtu yule. Hakustuka.
Alilitegemea hilo. Waliendelea kusonga mbele. Yule jamaa nae akaanza kupiga hatua kuwafuata, walikutana katikati.
Hawakuongea.
Daniel alirudi nyuma na kalamu yake ikiyotoa mwanga mkali eneo lile lote. Ile nafasi yake pale mbele ikachukuliwa na Inspekta Jasmin. Na Inspekta Jasmin hakuuliza alipokuwa tu sambamba na Dokta Yusha pale mbele. Alimuelekezea bastola yule jamaa huku akiongea kwa sauti kubwa.
"Nyoosha mikono juu mbwa wewe!! Upo chini ya ulinzi!!" Inspekta Jasmin aliamrisha. Lakini hakusikilizwa.
Jamaa bado alikuwa anawafata huku akiwa kimya.
"Unaelewa unachoambiwa wewe??" Dokta Yusha nae alidakia.
Jamaa mweusi alisimama wima. Akawaangalia askari wale wanne kisha akasema...
"Karibuni sana shimoni" Jamaa alitamka maneno yake ya kwanza.
"Acha jeuri. Huu ni mwisho wako wewe na wanaharamu wenzako. Na tunaanza na wewe" Dokta Yusha alisema.
Daniel Mwaseba alikuwa pembeni akimwangalia mtu yule aliyekuwa akijiamini sana. Alikuwa anamwangalia chini hadi juu.
Aligundua kitu.
Alikumbuka nchini Cuba.
Na muda huohuo Inspekta Jasmin aliachia risasi katika bastola yake iliyoelekea moja kwa moja katika utosi wa jamaa mweusi. Jamaa haikumdhuru kabisa ile risasi, ilipita pale utosini huku ikiacha shimo dogo lisikokuwa hata na chembe ya damu. Askari wote watatu walibaki midomo wazi wakiwa hawaamini, kasoro Daniel Mwaseba tu aliyekuwa akitabasamu.
"Mzimuuuu!!" Jasmin alipiga kelele.
Ghafla yule mtu mweusi alirusha teke lilimpata dokta Yusha kifuani. Alisukumwa kwa nguvu na uzito wa teke lile na kujigonga vibaya ukutani. Inspekta Jasmin na Mwanasheria mlevi walianza kurudi nyuma kwa woga huku yule jamaa akiwafata taratibu huku akicheka. Kwa kasi yule jamaa alirusha mateke mawili yaliyowapata wale maaskari wawili sehemu ya kifua. Wote walianguka chini wakigumia kwa maumivu.
Dokta Yusha akiwa pale chini karibu na kingo ya ile njia alitoa bastola yake na kumuelekezea yule jamaa. Jamaa hakuwa hata na chembe ya hofu na ile bastola. Risasi tatu za moto zilitua katika tumbo za jamaa mweusi. Risasi zile ziliacha matundu matatu tumboni lakini bado yakimuacha yule jamaa mweusi akiwa kasimama wima. Imara kabisa.
"Mnajisumbua, mnaharibu bure risasi zenu. Sifi kwa risasi za binadamu mimi" Jamaa mweusi alisema kwa majigambo.
Daniel Mwaseba akiwa pale pembeni na kalamu yake mkononi alikuwa akiyasikia yote yale na kuona matendo ya yule jamaa mweusi.
Jamaa mweusi alimsogelea Inspekta Jasmin ambaye alikuwa katika harakati za kuinuka pale chini. Alimshika shingoni kwa nguvu na kumpeleka ukutani akiwa kawapa mgongo wakina Daniel. Hiyo ndiyo nafasi pekee ambayo Daniel Mwaseba alikuwa anaitafuta.
Kwa kasi Daniel Mwaseba alimfata yule jamaa na kuchomoa kifaa kidogo kilichokuwa mgongoni mwa yule jamaa kwa nguvu. Ghafla jamaa mweusi alimuachia Inspekta Jasmin pale shingoni na kudondoka chini.
Ulikuwa ndio mwisho wake.
"Ni nini umefanya Daniel?" Mwanasheria mlevi aliuliza akistaajabu.
"Yule sio mtu, ni machine!! Nimewahi kukutana nayo machine kama ile nchini Cuba. Nilikuwa nimeenda
Cuba miaka mitano iliyopita kurudisha nyaraka za siri zilizoibwa na jasusi kutoka Cuba ndani ya Ikulu ya Dar es salaam kipindi cha utawala cha rais Kazulu. Zilikuwa nyaraka muhimu sana kwa usalama wa nchi yetu. Jasusi wa mweusi mwenye asili ya Cuba alipandikizwa katika idara yetu ya usalama wa Taifa na kuweza kuziiba nyaraka hizo za siri. Nilitumwa mimi na rais Kazulu kwenda Cuba kuzirejesha nyaraka zetu. Ilikuwa misheni ngumu zaidi kuwahi kuifanya.
Nakumbuka nilipambana sana nami kufanikiwa kufika hadi Ikulu ya Cuba mahali ambapo zilifichwa nyaraka hizo. Haikuwa kazi ndogo hata kidogo, hadi nafika katika mlango wa chumba ambacho nyaraka za siri zilikuwa zimewekwa nilikuwa hoi bin taaban. Nimechoka kwa mapambano. Nikiwa mikono mitupu bila silaha yoyote ile. Ndipo nilipokutana na machine baada tu ya kufungua mlango. Alikuwa kama huyu mkiyepambana nae leo.
Sasa mimi nilikuwa peke yangu bila silaha huku nikiwa nimechoka baada ya kupambana na makomandoo wa Cuba wakiozilinda nyaraka zile kwa nguvu zao zote. Na kwa bahati mbaya sana nilikutana na machine bila ya kujua kwamba alikuwa ni machine.
Ilikuwa ni balaa!!!
Tulipigana kwa muda wa saa tatu mfululizo. Machine alinifanya niwe nyang'anyang'a. Nilijaribu kila mtindo wa mapigano lakini bado machine alisimama imara na kukabiliana na mimi. Mpaka nilipomchoma bomba ya kifua na kuacha tundu tu ndipo nilipogundua kuwa hakuwa binadamu. Alikuwa machine. Sasa ikanipasa kutumia akili badala ya nguvu. Nikaacha kupiga na kukwepa zaidi. Huku nikitafuta udhaifu wa ile machine. Kuna muda nilimpiga roba kwa nyuma, ndipo nilipoiona betri ndogo mgongoni mwake. Niliichomoa kwa nguvu, na machine ilidondoka chini. Nilisaka mle ndani na kufanikiwa kupata nyaraka. Nyaraka muhimu sana hapa nchini, nyaraka za 001!!! Daniel alielezea kwa kirefu.
"E bwana wee!! Zilikuwa zinahusu nini hizo nyaraka?" Mwanasheria mlevi aliuliza huku akiuhusudu uwezo wa Daniel Mwaseba.
"Katika misheni ile nilipewa marufuku ya kutozifunua zile nyaraka. Ni nyaraka nyeti sana hivyo nilisisitiziwa kutozisoma. Nilizirudisha nchini bila kuzisoma kama nilivyotakiwa na rais wa kipindi kile" Daniel Mwaseba alisema.
"Daniel we kiboko!!" Dokta Yusha alisema kwa hamasa.
"Niwaambie kitu?" Daniel aliuliza.
"Twambie" Wote walijibu.
Pamoja na kupambana kwa nguvu sana lakini juhudi zangu zimeenda bure. Nyaraka ya 001 zimepotea tena Ikulu!!"
"Heee ilikuwaje hadi zikapotea tena?" Mwanasheria mlevi aliuliza.
"Mapenzi, mapenzi ndiyo sababu. Cuba hawakukata tamaa pamoja na kuzipoteza nyaraka zile. Walidhamiria kuzirejesha zile nyaraka. Ndipo wakamtuma jasusi hatari wa kike kuja kuzisaka zile nyaraka. Bila kujua rais Dr Joseph akaingia mkenge, alianzisha uhusiano na yule mwanamke aliyekutana naye katika uwanja wa Taifa. Cuba walifanya hila zao na kuhakikisha huyo jasusi wa kike anapata nafasi ya kuwa mhudumu wa rais katika sherehe za Uhuru. Na kwa kutumia hila za kike na udhaifu wa wanaume dhidi ya wanawake rais Dr Joseph akazidiwa ujanja na kujikuta akianzisha uhusiano na yule jasusi wa kike. Alidhani dhamira ya mwanamke ni mapenzi na pengine pesa. Hakujua. Mwanamke alitumwa kuzisaka nyaraka za 001. Nyaraka nyeti na za siri sana kwa Taifa letu" Daniel Mwaseba alieleza.
"Aisee kumbe nchi ina mambo ya siri sana ambayo sisi wengine hatuyajui. Ndo nasikia leo habari kuhusu hizo nyaraka. Wananchi pia bila shaka nao hawaelewi, maana wao wanahangaika tu na habari za kina Dokta Luis Shika" Mwanasheria mlevi alisema.
"Jasusi wa kike alifanikiwa kuziiba nyaraka za 001. Na ni yeye huyohuyo alifanikisha wizi mkubwa wa dhahabu huko Geita. Cha kushangaza sasa. Alitoa taarifa kabla kwa katibu mahsusi wa machimboni aitwaye Bertha Fidelis kabla wizi wa dhahabu haujatokea. Bertha nae alitoa taarifa serikalini lakini hazikupewa uzito unaotakiwa. Tani mbili za dhahabu zikaenda na maji.."
"Sasa usalama wa Taifa haukunusa kabisa harufu ya wizi huo. Na inamaana hadi leo hawajagundua kitu? Na vipi kuhusu hizo nyaraka?" Inspekta Jasmin aliuliza.
Idara ya usalama wa Taifa walianza kumsaka huyo jasusi kimyakimya ili wajue kuhusu wizi wa Dhahabu, huku ishu ya 001 ikiwekwa siri kwa watu wachache sana, kwakuwa kulikuwa na uzembe katika ngazi za juu, lakini hawakufanikiwa. Elizabeth Neville alikuwa kayeyuka mithili ya upepo. Walishindwa kazi, ndipo nikarudishwa mimi kutoka huko Faro, Ureno. kumsaka huyo jasusi wa kike. Maana rekodi zilionesha bado yupo hapahapa nchini, hakuwa ametoka nje ya mipaka yetu"
"Hivi mlisikia kifo cha Jane Munuo?" Daniel aliuliza " najua hakuna anayejua. Ninyi mmeletwa katika operesheni hii mkiwa hamjui chochote. Mnatumiwa tu na viongozi kwa maslahi yao.
Sasa baada ya kuiba nyaraka ya 001 ikulu jasusi huyo wa kike alianzisha uhusiano na Mheshimiwa Lucas. Najua mnajua kwamba kila mtu anajua Lucas ndiye atakuwa mrithi wa rais Joseph. Hivyo huyo jasusi alienda kwa Lucas sio kwa bahati mbaya, alienda kutafuta siri ambayo itawafanya wamwendeshe Lucas watakavyo pindi atakapokuwa rais. Ili wizi wa 001 uendelee kuwa siri. Rais ajaye asithubutu kusema wala kuhangaika kuisaka. Na walifanikiwa. Jasusi huyo alifanikisha Lucas kutekwa na kwenda kufanyiwa kitendo kibaya sana. Mheshimiwa Lucas aliingiliwa kinyume na maumbile na watu huku akirekodiwa, na hizo records anazo huyo jasusi wa kike.
Lakini pamoja na hayo yote huyo jasusi alizidiwa ujanja. Katika uhusiano wao Mheshimiwa Lucas alifanikiwa kuiba nyaraka za 001 kabla hazijasafirishwa kwenda Cuba..
Hapo ndipo shughuli ilianza. Jasusi wa kike alikuwa anazihitaji sana zile nyaraka, huku Lucas akiihitaji sana ile records.
Lakini jasusi wa kike alifanya ujanja.
Unajua sisi wanaume ni dhaifu sana kwa wanawake. Jasusi alimtumia mwanadada changudoa aitwaye Jane Munuo. Huyo ndiye aliyefanikisha kuibiwa tena nyaraka za 001 mikononi mwa Lucas na kuzirejesha kwa jasusi wa kike. Mheshimiwa Lucas alikasirika sana baada ya kugundua zile nyaraka zilikuwa zimeibwa na Jane Munuo. Alidhamiria kumuua!
Na alimuua kweli katika baa ya Hongera!
Bila kujua kwamba alikuwa anarekodiwa na mwandishi wa habari wa gazeti la udaku, Zulfa, wakati anafanya mauaji. Na wakati Zulfa akirekodi hakujua kwamba macho ya yule jasusi wa kike yalikuwa yanamwona pale Hongera baa. Hakufika nayo popote ile video ya mauaji aliyoyafanya Lucas. Maisha ya Zulfa yaliishia Sinza Madukani baada ya kusababishiwa ajari mbaya ya gari na yuleyule jasusi wa kike. Na ndipo alipotokomea na ile video pia. So huyo jasusi alikuwa na vitu vitatu vya siri sana, na alikuwa anatafuta njia ya kutoka nchini na kuelekea Cuba.
Hakufanikiwa.