Simulizi: For You

Simulizi: For You

FOR YOU

Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!

★★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA THELATHINI NA SITA

★★★★★★★★★★★★★★★★★★


Muda mfupi baadae, Torres alimjulisha Kendrick Jabari kuhusiana na mambo yaliyokuwa yametokea huko "chini" baada ya kumfikisha mdogo wake na Lexi. Kendrick akamwambia angehitaji kuja kushughulika na Kevin yeye mwenyewe kwa kitendo alichokifanya siku hiyo. Akaomba kuongea na Lexi, hivyo Lexi akaitwa na Torres ili aweze kuongea na "boss." Lexi alikuja na kumweleza Kendrick jinsi ambavyo njia aliyotaka kuitumia ili kumleta Azra upande wake ilikuwa ngumu, lakini akasema hatakata tamaa hata kidogo. Ingawa Kendrick alimhakikishia kwamba anamuunga mkono, akasema haingekuwa jambo la busara kuendelea kubaki naye kwenye sehemu yao hiyo ya mwisho kwa ajili ya ulinzi, hivyo walitakiwa kumpeleka sehemu nyingine.

Kwa sababu Kendrick alikuwa ndiyo ameondoka kutoka Geita pamoja na Mensah na kwenda Dar es Salaam kwenye ile kampuni yake ya pili ya madini, akamwambia Lexi ampeleke Azra huko, ili na yeye hatimaye aweze kuonana naye. Kendrick akamwambia Lexi alielewa kwamba mwelekeo waliokuwa wanapita kwa wakati huu ulikuwa na ugumu, lakini kamwe hangeacha kumuunga mkono. Lexi akamshukuru na kumwambia angekwenda kuongea na Azra kabla ya kuondoka ili kuona wakati huu akili yake ingekuwa imekaa vipi.

Wakaagana baada ya hayo, naye Lexi akaenda kujipanga ili kumfata Azra na kuongea naye. Alipochukua simu yake ya 'kawaida' na kuiwasha, alikuta jumbe kadhaa kutoka kwa Nora, ambaye alimwambia kwamba amemkumbuka sana na hampati hewani, hivyo akiziona jumbe zake basi amtafute ili wazungumze. Lexi bado alikuwa anapambana na hisia zake kumwelekea mwanamke huyo, lakini kwa sasa kilichokuwa cha muhimu zaidi ilikuwa ni Azra. Akaghairi kumjibu Nora na kuizima tena simu, kisha akamfata Azra kwenye chumba alichokuwa.

Mdogo wake alimfungulia kistaarabu tu, naye Lexi akafurahi sana kwa sababu hakukuta ameshatoroka kupitia dirisha na kuruka kutoka juu, ikimaanisha ni kama alikuwa amepata sababu ya kuendelea kukaa hapo. Akamwomba wakae ili wazungumze, naye Azra akatii. Waliketi kitandani, kukiwa na nafasi pana iliyoachwa baina yao, naye Lexi akaanza maongezi kwa kumshukuru kumpatia nafasi ya kumwambia ukweli.

Alianza kumwelezea kuhusu maisha yao miaka mingi nyuma, tokea wakati ambao Azra alizaliwa mpaka anakua binti mkubwa, kufikia wakati ambao watu wabaya walikuja kuisambaratisha familia yao. Alimsimulia mambo mengi kwa hisia sana, na kumwomba msamaha kwa sababu hakuweza kuwasaidia yeye na pacha wake wakati Weisiko alipowashambulia. Akamweleza alidhani Weisiko aliwaua wote usiku ule, na ndiyo sababu mpaka sasa alikuwa akifanya mambo mengi kulipiza kisasi, na mpango wake wa kumshika Weisiko siku moja ili kumlipa kwa yote aliyofanya hakuwa ameusahau, ila alikuwa anasubiria wakati mwafaka.

Lexi hakujua kwamba Azra wa wakati huu alimwona Weisiko kama mtu fulani muhimu kwake, hivyo haya yote aliyokuwa akimwambia yalimwacha mwanamke huyu mdogo kwenye njia panda. Alikuwa akiwaza labda Lexi ametunga tu hadithi hiyo ili kumlaghai, lakini kwa sababu gani? Haingepatana na akili kudhani labda anamdanganya tu kwa kuwa mambo yote aliyasema kwa njia iliyoonyesha yalikuwa kweli kabisa, na hapo bado Lexi hakujua ikiwa ni Weisiko ndiye aliyeokoa maisha ya Azra.

Ili kuthibitisha mambo zaidi, Lexi akatoa simu nyingine aliyopewa na Torres na kumwonyesha baadhi ya picha zao za zamani alizosaidiwa kupata na Torres, na hapo Azra akauona ukweli mwenyewe. Alijiona akiwa bado mdogo, akapata kumwona mama yake mzazi, baba yake, na mwingine aliyemwona kama "kaka yake," yaani pacha wa "dada" huyu aliyekuwa anamwambia haya yote.

Pamoja na kwamba Azra alikuwa amefunzwa kuzuia hisia zake, hakuweza kuzuia machozi yasimtoke wakati huu. Lexi akajua hapa ukweli ulikuwa umemwingia, naye akamsogelea karibu na kumkumbatia. Azra bado alikuwa anapambana na akili yake mwenyewe kuweza kuamini kila kitu, lakini moyo wake ukamshinda nguvu na kumfanya aanze kulia kwa hisia sana. Alilia sana huku akiwa ameinamisha kichwa chake kwenye bega la Lexi, naye Lexi akamvutia kwake vizuri hata zaidi na kumbana kwa upendo.

Mtu na mdogo wake hatimaye ikawa ni kama wamepatana kihisia, naye Lexi akamwachia na kuanza kumfuta machozi. Akamwambia asijali kuhusu yale aliyojengewa kwenye akili yake kwa muda wote huo waliokuwa wametengana, kwa sababu angemsaidia kuondoa mashaka yoyote kwenye akili yake na kumwonyesha upendo aliostahili tofauti na jinsi wengine walivyomtumia kama silaha tu. Akamhakikishia kwamba kuanzia sasa hangeruhusu jambo lolote liwatenganishe tena, na angemsaidia kuona upande sahihi wa vita hivi walivyokuwa wanapigana ni upi. Azra hakusema chochote bali kumtazama tu "dada yake" kwa hisia, naye Lexi alipomkumbatia tena kwa upendo, Azra akarudisha kumbatio lake taratibu pia.

Lexi akafarijika sana kuona kwamba Azra alimwelewa, na ambacho kingefuata sasa ilikuwa ni kumtembeza mdogo wake kwenye dunia ndogo aliyokuwa ameitengeneza, ili waendelee kuikuza pamoja. Baada ya kuachiana, Lexi akamwambia Azra wangeenda kupata chakula kwanza, kisha wapumzike kwa sababu hawakulala usiku wote mpaka asubuhi hiyo, halafu kuna safari fupi ambayo wangeifanya baada ya hapo ili aende kumtambulisha kwa mtu fulani muhimu.



Ilikuwa ajabu kidogo kwa Azra kuketi pamoja na familia ya Mess Makers na kupata chakula asubuhi hiyo, kwa sababu wengine walikuwa wakimwangalia sana kuona alikuwa na staarabu za aina gani. Lexi alijitahidi kumsemesha kwa shauku na kumshawishi ale, naye Azra akawa anakula taratibu tu bila kusema lolote, bila kutabasamu, bila kuonyesha itikio lolote. Torres angalau alijaribu kumsemesha kama Lexi tu, lakini wengine waliiona hali hii kuwa ya ajabu sana.

Baada ya kuendelea kupata chakula kwa dakika kadhaa, Kevin, ambaye hakuwa pamoja nao, alifika hapo na kuanza kumwomba samahani Lexi kwa kila jambo alilofanya na kusema kipindi chote cha nyuma. Akamwambia kwamba ni hali fulani tu ya upweke ndiyo iliyokuwa ikimfanya atende kwa ubinafsi, lakini kuanzia sasa angejirekebisha na kutenda kwa busara. Akamwomba samahani na Azra kwa kujaribu kumuua, lakini Azra akampuuzia tu na kuendelea kula. Lexi pia hakumjibu lolote Kevin, hivyo Torres akamwambia tu aketi pamoja nao ili ale, kwa sababu bado alikuwa ni mmoja wao.

Kevin akakaa kinyonge na kuanza kula, huku akiwa anamwangalia Lexi kwa jicho la wizi. Alikuwa akijifanya tu kama toba yake ilikuwa ya moyoni, lakini alichokuwa amekiweka akilini kufanya kingewaharibu sana Mess Makers muda siyo mrefu.


★★★★


Siku hii kwa ACP Nora ilianza kama kawaida kwa yeye kwenda ofisini. Kutokea siku iliyopita mpaka wakati huu hakuwa akihisi nguvu-kazi yake ambayo sikuzote anakuwa nayo, hasa kwa sababu mambo mengi yalikuwa yakizidi kumchanganya. Yaani ilikuwa ni kama hafanyi lolote kabisa ijapokuwa alijitahidi kuangalia mambo kadha wa kadha, na baada ya kukaa ofisini kwa muda fulani akaamua tu kujilaza kwenye sofa ili kupumzisha akili. Lexi alipopita tena kwenye kichwa chake, akaamua kumtumia ujumbe akiuliza ikiwa alikuwa sawa, na angerejea wakati gani. Hii yote bado ilionyesha ni jinsi gani alivyokuwa na matumaini chanya kumwelekea "mwanamke" huyo, na asingekubali wazo lolote baya kumhusu mpaka ajithibitishie ukweli mwenyewe.

Akiwa anawaza afanye nini baada ya kujilaza hapo, simu yake ikaita, naye akatabasamu kuona ni Asteria ndiye aliyekuwa akipiga. Akapokea na kusalimiana naye, na mdogo wake huyo akamwambia alihitaji kumwona kwa sababu alitaka waongee ana kwa ana. Nora akamwambia kuwa bado alikuwa ofisini, naye Asteria akasisitiza kwamba ilikuwa ni muhimu amwone, hivyo angekuja mpaka hapo ofisini kwake. Nora hakuwa na jinsi ila kukubali kwa sababu ya king'ang'anizi cha mdogo wake, naye akamwelekeza jinsi ya kufika hapo na ofisi ya kwenda. Baada ya kuagana naye, Nora akaongea na Halima, yule msaidizi wake, akisema alikuwa na mgeni ambaye angefika muda siyo mrefu, hivyo amruhusu tu kuingia atakapofika.

Nora akaendelea tu kujilaza kwenye sofa mpaka usingizi ukampitia. Akaja kushtuka baada ya kuamshwa na Asteria muda mfupi baadae, naye akampokea kwa furaha. Asteria alishangaa kukuta kwamba Nora hakuwa amebadili nywele alizomsuka siku kadhaa nyuma, naye Nora akamwambia mambo yalikuwa mengi sana na yeye hakuwa na muda mwingi wa kujipendezesha kama Asteria.

Kwa kauli hiyo, Asteria akamwambia angetumia muda huu pamoja naye kumsuka pia, kwa sababu kwenye mkoba wake alibeba rasta nyingine. Nora akapinga akisema haingekuwa sawa kufanyia hayo ofisini, lakini Asteria akakomaa tu na kusema haikuonekana kama Nora ana kazi nyingi mno, naye angemsuka upesi huku akimwambia jambo alilotaka kusema.

Dada mkubwa akaona amridhishe tu mdogo wake kwa sababu hata hivyo ulikuwa umepita muda hawajaonana, kwa hiyo akamwambia Halima asiruhusu yeyote kuingia ofisini mpaka amalizane na mgeni wake. Baada ya hapo, Asteria akaketi kwenye sofa huku Nora akikaa chini katikati ya miguu ya mdogo wake, kama kawaida ya wanawake wakisukana. Kwa Asteria, Nora alijiachia sana, kama tu jinsi ambavyo alikuwa ameanza kujiachia kwa Lexi, naye Asteria akamwambia kuhusu mambo mengi aliyokuwa amefanya kwa siku za hivi karibuni huku akiendelea kumtengeneza kichwani.

"Okay, tuachane na habari za Wasafi Festival... niambie ulichokuwa unataka kuniambia sasa," Nora akasema.

"Eh, afu' umenikumbusha, hivi festival yao wataifanya lini tena? Nataka niende," Asteria akauliza.

"Ilikuwa ni expression tu Aste, me hayo mambo sifuatilii..."

"Mmmm... ungejuaje sasa kuhusu Wasafi Festival?"

"Hivi kweli Aste huelewi maana ya expression? Na nani atafanya mafestival sasa hivi na haya matukio ya kuuana-uana?"

"Ahahahah... chill bwana..."

"Kama umeghairi ulichokuwa unataka ku..."

"Nimepata boyfriend mwingine," Asteria akamwambia.

"Mh! Lini?"

"Juzi tu hapo..."

"Enhe..."

"Enhe nini, si ndiyo nakwambia sasa..."

"Yaani ulichokuwa unataka kuniambia ni kwamba umepata boyfriend mwingine?"

"Yah..."

"Sawa. Hongera..."

"Hongera nini? Nishauri bwana..."

"Nikushauri nini wakati tayari umemkubali?"

"No, nataka unishauri kama nimefanya uamuzi sahihi kumkubali. You know... nahisi labda nime-rush... halafu... na Oscar bado huwa nina..." Asteria akaishia tu hapo.

"Hey sikia. Usihisi kama vile unatakiwa kuwa committed kwa mtu ambaye hayupo. Ikiwa umempenda huyu mwingine na anakufanya ufurahi, basi mpe nafasi. Na wewe ujipe nafasi hiyo ya kufurahia pamoja naye," Nora akamshauri.

"Uko sahihi dada. Lakini hata sijui ni kwa nini tu yaani... every time nikiwa naye, fikira zinanirudisha kwa Oscar tu..."

"Aste, usiubebe mzigo huo tafadhali. Oscar hayupo tena. Please just, jaribu kusonga mbele. Boyfriend wako mpya hatakuwa kama Oscar, kwa hiyo acha kutegemea tu vitu ambavyo ulivipata kwa Oscar. Mpende yeye kama yeye, na utaona mambo mengi mazuri tu mbona..."

Asteria akashusha pumzi na kusema, "Ni kweli, uko sahihi. Nitafanya hivyo."

Nora akatabasamu na kuuliza, "Anaitwa nani?"

"Christopher..."

"Ni mzuri eeh?"

Asteria akacheka kidogo na kumwonyesha picha ya huyo mwanaume kwenye simu yake. Nora akamsifia na kuuliza kama alikuwa anasoma chuo pia, lakini Asteria akamwambia alikuwa anafanya kazi kwenye kampuni ya kutengeneza filamu. Nora akampongeza na kumwambia awe mwangalifu sana na mwanaume huyo, naye Asteria akaanza kumuuliza Nora kuhusu mtu wake pia. Nora hakuwa na jibu la moja kwa moja, hivyo kwa utundu Asteria akachukua simu ya Nora na kuanza kutafuta picha za wanaume humo ili kuangalia kama angemwona mpenzi wa dada yake.

"Achana na simu yangu bwana, humo hautaona picha ya mwanaume yeyote," Nora akamwambia.

"Umeificha wapi? Najua imo humu na siyo memes peke yake tu," Asteria akasema.

"Ahahahah... haya komaa. Kwa hiyo hapa ndiyo umemaliza kunisuka? Mm?"

Nora akauliza huku akijishika kichwani. Lakini akatambua kwamba Asteria alikuwa kimya ghafla. Akamtazama na kukuta ameishikilia simu yake (Nora) huku anaangalia jambo fulani kwa umakini sana.

"Vipi?" Nora akauliza.

"Huyu dada... namfahamu," Asteria akajibu.

Nora kusikia hivyo akachukua simu yake na kukuta ilikuwa picha ya Lexi.

"Unamfahamu? Kutokea wapi?" Nora akauliza.

"Simfahamu kama kumfahamu lakini... nilishawahi kumwona... akiwa na Oscar," Asteria akamwambia.

Nora akajitahidi kutoonyesha itikio la mshangao na kuuliza, "Alikuwa na Oscar wapi?"

"Niliwahi kumwona hotelini alikokuwa anaishi Oscar. Siku hiyo tulikuwa wote, mara ghafla tu Oscar akaniambia nijifiche bafuni mara moja kwa sababu dada yake alikuwa anapitia mzigo wake hapo, na hakutaka anione..."

"Kwa nini alikuwa hataki akuone?"

"Baadae alisema tu eti dada yake huyu ni mkali sijui kwa hiyo kunikuta naye angemzingua. Masuala mengi kuhusu huyo dada yake hakuwahi hata kuniambia, yaani me mwenyewe nikawa sina uhakika kama ni dada yake au mtu wake tu. Ila hakuonekana kuwa mtu wake maana alifika tu na kuondoka," Azra akaeleza.

"Kwa hiyo ulimwona kwa kuchungulia?"

"Ndiyo."

"Unakumbuka kitu alichopewa na Oscar? Na waliongea nini?"

"Sikumbuki wakiongea, ila Oscar alimpa tu begi dogo halafu... huyu dada akaanza kama kusukumana naye... kiutani tu. Nilitoka na kumlalamikia sana Oscar siku hiyo mwanzoni nikidhani alikuwa ana-cheat... ila akanihakikishia alikuwa dada yake. Sikuwahi kumwona tena lakini," Asteria akaelezea.

Nora akaangalia pembeni akiwa anawaza sana. Sasa mashaka yake aliyokuwa akijitahidi kuyapuuzia yalikuwa yameongezwa hata zaidi na kile ambacho mdogo wake alimwambia.

"Ni nani kwani?" Asteria akamuuliza.

"Aa... ni mtu tu nimekutana naye kikazi. Sikufikiri angekuwa anajuana na Oscar wako," Nora akasema.

"Aaaa... mzuri kweli huyu dada. Yaani hiyo siku nililalamika mpaka Oscar akachoka ahahah..." Asteria akaongea.

Nora alikuwa ameanza kuchoka akili. Kuipumzisha kidogo muda mfupi uliopita kukawa kumesahaulika kwa kuwa sasa rundo la mawazo lilianza kujaa kichwani. Asteria akamalizia kumsuka kwa mtindo mzuri sana huku akimwambia mambo kadhaa kuhusu mpenzi wake mpya, naye Nora akamshukuru baada ya kumaliza na kusema alitakiwa kuendelea na kazi, hivyo wangetafuta muda wa kuwa pamoja wakati mwingine. Asteria akamshukuru pia kwa ushauri mzuri, kisha akaondoka jengoni hapo hatimaye.

Halima aliingia muda mfupi baada ya Asteria kuondoka na kumuuliza Nora ikiwa angependa kuletewa chakula ofisini hapo, lakini Nora akakanusha na kusema hangekula. Alibaki ofisini hapo akiwa anazunguka huku na huku akihisi kama amechanganyikiwa. Ikiwa Lexi alifahamiana moja kwa moja na Oscar mpaka kuitana kaka na dada, lakini kwenye mafaili yao isionyeshe uhusiano wa namna hiyo baina yao, hiyo ilimaanisha jambo kuu lililofichika kati ya hawa wawili lilikuwa ni jambo lile lile lililopelekea mpaka kifo cha Oscar kutokea.

Ikawa wazi kwake zaidi sasa kwamba Lexi angekuwa mmoja wa Mess Makers, na kuingia kwake kwenye maisha yake ilikuwa ni kwa makusudi kabisa. Mambo mengi yalipita akilini mwake. Alikaa, alinyanyuka, alizunguka ofisi nzima akijiuliza angefanya nini sasa. Hakuwa na uthibitisho wa moja kwa moja kuonyesha kwamba kile alichowaza kilikuwa sahihi, lakini ukweli huu haungehitaji uthibitisho wowote ule; alijua tu ni kweli. Akachukua simu yake na kutuma ujumbe huu mfupi kwa Lexi:

Lexi, ninakuhitaji sana leo. Tafadhali nakuomba uje kwangu. Nahisi kama nitachanganyikiwa nisipokuona. Please nakuomba uje. Nitasubiri.


★★★★


Ni ndani ya wakati huo huo ndiyo Mess Makers walikuwa wameingia jijini Dar es Salaam kutokea kule kwenye sehemu yao ya maficho. Wote waliokuwa kule, yaani Lexi, LaKeisha, Victor, Torres, pamoja na Azra walikuwa kwenye gari moja lililoelekea kule kwenye kampuni ya Kendrick ili kumkutanisha na Azra, isipokuwa Kevin, ambaye alibaki kule mafichoni kwao kama kawaida. Wakati huu mwanaume huyo hakuweka kipingamizi cha kubaki huko tena akiwa peke yake, kwa sababu alikuwa akijifanya mwema. Torres alikuwa amejiunga kwenye safari hii kwa kuwa alihitaji kushughulikia mambo fulani huko kwenye kampuni ya Kendrick, mambo ambayo yalihusiana na mpango wao uliofanya waibe zile trilioni 20 kutokea mwanzo.

Wote walikuwa ndani ya gari moja, Torres akiendesha na Victor akiketi pembeni yake, huku Lexi akiwa ameketi pamoja na Azra na Lakeisha siti za nyuma. Wakati huu Azra hakuwa amefungwa mikono kwa ajili ya tahadhari, kwa sababu Lexi alitaka kumwonyesha kuwa walimwamini. Mdogo wake huyo alikuwa ametulia sana, akisikiliza kwa umakini jinsi wengine walivyoongelea mambo mbalimbali kwa shauku, naye akavutiwa na jinsi walivyoonekana kuwa na uhusiano wa karibu sana. Lexi angemsemesha mara kwa mara ili kumfanya ajihisi huru, lakini Azra hakuwa amesema chochote kile tokea mwanzo wa safari hiyo.

Sasa wakiwa bado mwendoni, Lexi akaiwasha simu yake ya kawaida, na jumbe ambazo Nora alikuwa amemtumia zikaingia. Wakati alipokuwa akiusoma ujumbe wa mwisho, Azra akauona, na kwa haraka akawa ametambua kwamba Nora aliyeandikwa hapo ni ACP Nora. Akamtazama sana dada yake na kuona jinsi alivyoweka uso wenye kujali baada ya kusoma ujumbe huo, naye Lexi akafunga tu simu yake na kutazama mbele.

"Are you gonna meet her? (utakutana naye?)" Azra akauliza kwa sauti ya chini.

Lexi na Lakeisha wakamtazama. Hata Victor na Torres mbele ya gari walimsikia akinena kwa mara ya kwanza wakiwa pamoja, nao hawakujua anamaanisha nini kwa swali lake.

"Pardon? (samahani?)" Lexi akamuuliza.

"ACP Nora... she wants to meet with you, right? (ACP Nora.. anataka mkutane, si ndiyo?)" Azra akauliza.

"Aam... yeah. She does (ndiyo.. anataka)," Lexi akasema.

"Anaongelea nini?" LaKeisha akauliza.

"ACP Nora... anataka tukutane," Lexi akajibu.

"Kwa nini?" akauliza LaKeisha.

"Ni muda umepita tokea mara ya mwisho umewasiliana naye eti? Amekumiss?" Torres akauliza kiutani.

"Bullshit! Atakuwa ame-set tu mtego. Nenda unase," Victor akasema.

Lexi akabaki kimya tu.

"Why did you save her that night? Was that one of your plans? (kwa nini ulimwokoa usiku ule? na hiyo ilikuwa ni moja ya mipango yenu au?)" Azra akauliza.

Lexi akamtazama na kusema, "No. She was just... in trouble. I would have helped anybody under those circumstances... including you (Hapana. Alikuwa tu kwenye shida. Ningesaidia yeyote ambaye angekuwa chini ya hali kama zile.. kutia ndani wewe)."

"You were there that night too weren't you? (na wewe ulikuwepo usiku ule pia, siyo?)" LaKeisha akamuuliza Azra.

Azra akabaki kimya na kutazama mbele.

"You were assigned to spy on her so that you would get to us. What happens now if your 'bosses' find out you've switched sides, huh? Or haven't you? Are you on our side now or... (ulikuwa umepewa kazi ya kumfatilia Nora ili utupate sisi. Nini kitatokea sasa hivi mabosi wako wakijua kwamba umeenda upande mwingine? au hauko upande mwingine? Uko upande wetu sasa hivi au...)" LaKeisha akawa anamchokoza Azra.

"Keish... enough. Please," Lexi akamwambia aache.

"Hey, I'm just trying to make conversation. That's how we get to know each other, right? (ninajaribu kutengeneza mazungumzo. si ndiyo tunajuana kwa njia hiyo, eti?)" LaKeisha akasema.

"Right (kabisa)," Victor akajibu.

"So... how do you do this thing with your arms when you hit someone and they just... paralyze? Don't tell me you use witchcraft (kwa hiyo.. huwa unafanya vipi yale mambo yako unapiga mtu halafu anapooza? Usiniambie unatumia uchawi)," LaKeisha akamuuliza Azra.

Victor akacheka.

"Keish!" Lexi akasema hivyo kumzuia.

"Nini?" LaKeisha akamuuliza pia.

"Its not witchcraft. Its a fighting technique (siyo uchawi.. ni mtindo wa kupigana)," Azra akajibu.

"What kind of a technique do you use? (ni mtindo gani huo unaotumia?)" Victor akauliza.

"Marmakkala," Azra akasema.

"No... way!" Torres akasema kimshangao.

"What the hell is that? (hiyo ndiyo nini?)" LaKeisha akauliza.

"Azra are you serious? Yaani unatumia, sorry... you use marmakkala when fighting? How did you learn that? (Azra hautanii? yaani.. unatumia marmakkala kwenye kupigana? umejifunza vipi hiyo?)" Torres akauliza.

"It was taught to me by an old master (nilifundishwa na mwalimu mwenye umri mkubwa)," Azra akasema.

"Where? (wapi?)" Torres akauliza.

"Kerala," Azra akajibu.

"India... of course (India.. bila shaka)," Torres akasema.

Lexi akamwangalia Azra kwa umakini. Hii ndiyo iliyokuwa mara ya kwanza kwake kufunguka kuhusu ni wapi alipokuwa wakati wametengana, na kujua alipelekwa mbali hivyo ili tu kugeuzwa kuwa silaha kukamhuzunisha.

"Bwana si mtuambie mnaongelea nini nyie bata!" LaKeisha akasema kwa kukerwa.

"Akikusikia unamwita bata atakuzimisha, shauri yako," Victor akamwambia.

"Haelewi Kiswahili bwana. Hayo makalakala ndiyo nini?" LaKeisha akauliza.

"Marmakkala ni form fulani ya zamani sana ya kupigana. Tena nikisema zamani namaanisha ancient. Ina resemble Tai-chi lakini ina utofauti kidogo. Sasa naelewa Azra anachokuwa anafanya ni kupiga sehemu za mwili anazojua ni dhaifu ili kuwalegeza maadui, siyo kwamba anawa-paralyze kabisa. Ni form ngumu na hatari pia... sikudhani kuna watu bado wanaitumia maana ilidhaniwa kupotea miaka mingi iliyopita. Azra anaweza kukuua kwa kukupiga ngumi kidogo tu shingoni. Ni technique fulani special sana," Torres akaeleza.

"Hiyo inawezekanaje? Ina maana kwani mimi nikikupiga namna hiyo shingoni sitaweza kukuua? Kuna utofauti gani na ngumi ya kawaida hapo?" LaKeisha akauliza.

"Ni technique Keisha. Style maalum iliyo na mafunzo yanayochukua muda ku-master. Azra akikuangalia tu anaona jinsi mishipa yako ilivyokaa na hiyo inamfanya ajue pa kukupiga na jinsi ya kukupiga ili ulegee, siyo kwamba tu anatumia nguvu," Torres akasema.

Azra akatabasamu kwa mbali. Ni kwamba alielewa kile ambacho Torres alisema, na ujuzi huo wa jamaa ukampendeza.

"Bado sielewi," LaKeisha akasema.

Lexi akashusha pumzi na kumuuliza, "Unaikumbuka ile anime ya Avatar?"

"The Last Airbender?" LaKeisha akauliza.

"Yeah..." Lexi akasema.

"Enhee... tena huo ni mfano mzuri Lexi," Torres akasema.

"Imefanyaje?" LaKeisha akauliza.

"Kuna character mule wa kike, sikumbuki jina lake, lakini alikuwa anawapiga watu wengine na kufanya washindwe hata ku-move na kutumia bending," Lexi akasema.

"Ty-lee," Azra akakumbusha jina Lexi alilokuwa amesahau.

Lexi akatabasamu kuona kwamba Azra sasa alikuwa ameanza kujiachia.

"Oooh... kumbe ni kama hivyo..." LaKeisha akaonekana kuelewa.

"Yeah, lakini ile ya katuni ni kitu ambacho siyo kweli waliongeza chumvi. Azra hawezi kufanya upooze kabisa kwa muda mrefu, lakini anaweza kufanya upoteze nguvu kwa muda mfupi na... hata kukuua... akiamua," Torres akaongezea.

"Hmm... kumbe tuko na mtu ambaye akitugeuka tu sisi wote tunapoozeshwa. Anaonekana kama yuko tayari kutulipua muda wowote na hayo mashavu yake," LaKeisha akasema kikejeli.

Wengine wakacheka isipokuwa Azra.

"We endelea tu kumchokonoa," Victor akamwonya LaKeisha.

"Atanifanya nini? Kwanza hata haelewi Kiswahili," LaKeisha akasema kwa kujiamini.

"Kwa hiyo utaenda kuonana na ACP Nora?" Azra akamuuliza Lexi.

Lexi akamtazama kwa umakini. Torres na Victor wakiwa mbele ya gari wakaangaliana huku wakipeana tabasamu la mshangao. Ni ile kutambua kwamba Azra alielewa Kiswahili muda wote walipokiongea, nao wakamgeukia LaKeisha na kukuta ameachama mdomo kimshangao.

"Aam... sioni haja ya kukutana naye. Mambo ni mengi sasa," Lexi akamwambia Azra.

"Sijui sana... about your plans but... I think you should meet with her. She might become suspicious (sijui sana kuhusu mipango yenu lakini, nafikiri unapaswa kuonana naye. Anaweza akaanza kuwa na mashaka)," Azra akasema.

"Yeah Lexi... Azra yuko sahihi. Umemdodge Nora kwa muda fulani sasa. Unajua jinsi alivyo, akihisi kuna nuksi haitakuwa nzuri kwetu. Besides, ukikutana naye itakuwa vizuri ili tujue amepata nini upande wake," Torres akasema.

"Je kama ni mtego?" akauliza LaKeisha.

"She can take of herself (anaweza kujilinda)," Azra akasema.

Lexi akamtazama mdogo wake kwa ufupi, ambaye alikuwa amesema jambo lililoonyesha alimwamini kwa kiasi fulani.

Kutoka ndani ya moyo wake, Lexi alitaka sana kumwona Nora na kujua ni nini kilichokuwa kimemsibu wakati huu mpaka atume jumbe zile. Akatabasamu tu kumwelekea Azra na kisha kuwaambia wenzake kwamba wakifika tu kule kwenye kampuni ya Kendrick, yeye angewaacha ili kwenda kuonana na Nora.

★★

Baada ya muda mfupi waliwasili kule walipotakiwa na kupokelewa na Mensah kwenye sehemu ya maegesho ya kibinafsi. Azra alikuwa makini sana kuangalia mazingira yaliyomzunguka kwa sababu alitaka kuhakikisha hawekwi kwenye mtego, na Lexi alipotambua hilo akamtuliza kwa sauti ya chini akimhakikishia kwamba alikuwa salama.

Mess Makers wote waliofika hapo walikuwa wamevaa mabegi madogo yenye vifaa vyao muhimu, nao wakaongozwa kupitia upande huo wa nyuma wa jengo hilo na kuchukua lifti ya kibinafsi ya "boss" mpaka kwenye ghorofa ya mwisho. Mensah akawaongoza mpaka kwenye ofisi maalum ya Kendrick, ambayo ilikuwa na mwonekano kama wa sebule ya gharama sana, na wote wakaingia kumkuta "boss" wao akiwa ameketi kwenye sofa moja hapo.

Kendrick alistaajabu sana baada ya kumwona Azra kwa macho yake mwenyewe. Akasimama huku akiwa anamwangalia binti kwa umakini mpaka wote walipofika usawa wake na kumsalimu. Akawa anamwangalia sana Azra huku akitabasamu kwa furaha, naye Lexi akaachia tabasamu la furaha pia. Kendrick akaanza kumfata Azra ili amshike, lakini Azra akarudi nyuma huku akisimama kwa mtindo fulani wa kujihami, naye Kendrick akasimama. Lexi akamsogelea Azra na kumtuliza, akisema mwanaume huyo ndiye aliyekusudia kumkutanisha naye.

Wengine wakawa wamekaa pembeni wakisikiliza Lexi alipoanza kumwelezea Azra kwa kina kuhusu jinsi Kendrick alivyookoa maisha yake mpaka wakafikia hatua ya kurudi nchini humu kuwalipa kisasi wabaya wao. Akamwambia kuwa ingawa bado hakuwa amewakumbuka vizuri, walimhitaji sana kuwa upande wao, na siyo ili tu kuongeza nguvu yao wakiwa timu, bali kurudisha uhusiano wao wakiwa ndugu. Azra alionekana kama alihitaji muda fulani wa kutafakari mambo, kwa sababu kiukweli hakuwa hata amewaambia kwamba mwanaume aliyedhani ni baba yake ndiye waliyekuwa wanasema aliwaua wazazi wake halisi. Lexi akamwambia aondoe hofu, na kwamba walikuwa pamoja naye haijalishi alifanya nini kipindi cha nyuma kwa sababu alikuwa ametumiwa tu vibaya.

Baada ya hayo, Kendrick akamwambia Torres kuwa sasa wangeanza kufanyia kazi kile ambacho kiliwaleta hapo, na ilikuwa vizuri kwamba Azra alikuwepo ili apate kujionea mambo mengi. Lexi akamwambia Kendrick kuwa alihitaji kwenda kuonana na ACP Nora mara moja kwa sababu hakutaka kumfanya ahisi jambo fulani baya kwa kutoweka kwake tokea siku chache nyuma, na ili aone kama amepata jambo lingine kuwahusu Mess Makers. Kendrick akamsihi awe mwangalifu, naye Lexi akakubali na kumsogelea Azra karibu, kisha akamshika usoni kwa upendo huku akimwambia angerejea hapo muda si mrefu. Azra alikuwa akimtazama kama vile mtoto mdogo asiyetaka mama yake amwache, naye Lexi akamkumbatia na kisha kuondoka hapo hatimaye.

Kendrick na Torres wakamkaribisha Azra ajiunge nao kutazama mambo ambayo walikuwa wamepanga kufanya hapo baada ya Lexi kuondoka, na mchakato huo muhimu ukaanza upesi.


★★★★


KEVIN


Mwanaume huyu alikuwa amebaki peke yake kule "chini" kwenye sehemu ya maficho ya Mess Makers baada ya wengine kuondoka pamoja na Azra kwenda kwa Kendrick. Sasa alikuwa amepata nafasi ya kufanya jambo fulani ambalo, kwa maoni yake, lingewakomesha wengine kwa jinsi walivyokuwa wanamtendea. Aliona kama wamemdharau sana tokea alipogundulika na serikali kuwa mmoja wa Mess Makers, na sasa akawa anataka kuwaonyesha jinsi alivyohisi kwa muda mrefu.

Kilichokuwa kinamuuma ni ile hali tu aliyohisi ya kuwekwa pembeni sana, hasa kutakiwa kukaa hapo bila kwenda popote kwa sababu ya kitu alichokiona kama "kigezo" cha kumlinda, lakini ikamfanya ahisi kama mfungwa. Kwa hiyo alikuwa anataka kuwaonyesha wenzake jinsi ilivyokuwa ngumu kukaa kama "mfungwa," na hivyo akaamua kuwafichua wenzake!

Alikuwa amepanga kuwafichua wenzake kwa kutuma taarifa kuwahusu kupitia mitambo ya Torres ya kiteknolojia. Mwanaume huyu alikuwa ametumia muda mwingi kumwangalia Torres kila mara alipofanya kazi kwenye kompyuta zake huko "chini," na hivyo kwa kiasi fulani alijua njia nzuri ya kufanya mpango wake ufanikiwe. Alikuwa anataka kuwatumia watu wote waliowatafuta habari zao kadhaa ambazo zingethibitisha wenzake ndiyo Mess Makers, lakini kwa njia ambayo haingefichua sehemu yao ya maficho, na haingefichua kwa wenzake kwamba ni yeye ndiye "aliyewachomesha" (snitch).

Lengo lake lingekuwa na faida kwake ikiwa lingefanya kazi kwa njia mbili. Kwanza, ikiwa baada ya kufanya jambo hilo wenzake wangekamatwa kabla hawajarudi huku, basi ingekuwa ni shangwe kwake kwa sababu ni yeye tu ndiye angebaki kwenye sehemu hiyo ya maficho iliyokuwa kama jumba la kifahari. Pili, ikiwa wangefanikiwa kurudi kwenye nyumba hiyo ya maficho kabla ya kukamatwa, basi nao wangetakiwa kuendelea kukaa tu hapo hapo kwa kujificha kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwake, na hivyo angekuwa amewakomesha pia kwa sababu mipango yao ingevurugika. Kwa hiyo alitakiwa kufanya haya yote kwa umakini sana na kwa uangalifu ili lolote lile likitokea, yeye asipatwe na shida.

Nia yake ya kufanya haya yote ilichochewa na chuki na ubinafsi wa hali ya juu, na baada ya kumaliza kupangilia njia zake za kufanya hayo, akaanza kubofya. Huyo ndiyo alikuwa Kevin!


★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★

WHATSAPP +255 787 604 893
 
Huyu Kevin anachokitafuta atakipata.
Ila pia Mess Makers ni wazembe sana. Wameshagundua hatari ya kuwa na Kevin lakini bado wapo naye tu.
Kwa usalama wa kundi Kevin alitakiwa awe ameshakuwa neutralized mapema sana😡
 
Huyu Kevin anachokitafuta atakipata.
Ila pia Mess Makers ni wazembe sana. Wameshagundua hatari ya kuwa na Kevin lakini bado wapo naye tu.
Kwa usalama wa kundi Kevin alitakiwa awe ameshakuwa neutralized mapema sana😡
Ni kweli sema wenyewe hawajajengeka namna hiyo. Wanathamini sana familia kama vile Vin Diesel wa Fast and Furious 😂
 
IMGJ_9771.jpg
 
FOR YOU

Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!

★★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA THELATHINI NA SABA

★★★★★★★★★★★★★★★★★★


Hatimaye Lexi akawa amefika nje ya hoteli aliyokaa Nora. Usiku ulikuwa umekwishaingia sasa, na maghorofa ya hoteli hiyo yalionekana yakimeremeta kwa taa zake nyingi. Alikuwa amekwishamtumia Nora ujumbe kwamba angefika hapo, na kusema angemweleza pia alikokuwa na kwa nini hakupatikana kwa siku hizo chache. Akaizima tena simu yake na kushuka kutoka kwenye gari na kuelekea huko ndani mpaka alipofika nje ya mlango wa chumba cha Nora. Akashusha pumzi ya kujiweka sawa, kisha akaugonga mlango kistaarabu na kusubiri. Hazikupita sekunde nyingi, nao mlango ukafunguliwa.

Lexi alihisi mapigo yake ya moyo yakidunda kwa kasi zaidi baada ya kumwona Nora kwa mara nyingine tena. Alivutiwa zaidi na jinsi alivyosuka wakati huu, na kufanya ajiulize ikiwa aliamua kujipendezesha kwa ajili yake. Nora alikuwa amesimama ndani hapo huku ameushikilia mlango na kumwangalia Lexi kwa hisia sana, kwa sababu kihalisi alikuwa amemkumbuka mno "mwanamke" huyu. Ijapokuwa kuna mambo mengi yaliyokuwa yakipita akilini mwake, akaachia tabasamu la mbali kuonyesha amefurahi kumwona, naye Lexi akatabasamu pia.

Nora akamkaribisha ndani, na baada ya Lexi kuingia akaufunga mlango na kushusha pumzi ndefu huku akiwa amefumba macho yake, naye akamgeukia taratibu.

"Pole, nimekufanya usubiri sana?" Lexi akamuuliza.

"Hapana. Nami ndiyo nimefika tu," Nora akajibu.

"Okay... sawa. Umekula?" Lexi akauliza.

Nora akatikisa kichwa kukubali.

"Ona... kulikuwa na mambo fulani ya kifamilia hapa katikati na... nilihitajika huko. Yalikuwa mambo mengi ndiyo maana nilikuwa sipatikani. Nisamehe kwa kukufanya uni-miss sana," Lexi akasema.

"Usijali... haina shida. Kwa hiyo... familia yako... mambo yako vizuri sasa?" Nora akauliza.

"Yeah, tumejitahidi kuyajenga. Kila kitu kiko sawa," Lexi akasema.

"Umefanyaje mkononi?" Nora akauliza.

Lexi akajitazama sehemu ya mkono wake iliyofungwa kwa bendeji, ambapo aliumizwa na yule mnyama wake, Zelda.

"Aam... niliumia tu kidogo wakati niko huko. Siyo kitu serious sana," Lexi akasema.

Nora akabaki kumtazama kwa njia ambayo ilimwambia Lexi kwamba mwanamke huyo alikuwa anawaza jambo fulani kumhusu.

"Vipi wewe? Mambo yamekwendaje huku wakati sipo?" Lexi akamuuliza.

Nora akabaki kumtazama tu.

"Uko sawa mheshimiwa?" Lexi akauliza kwa njia ya kujali.

Nora akamsogelea karibu na kuuliza, "Wewe unaonaje? Niko sawa?"

Swali hilo likamfanya Lexi atambue kuwa kweli kuna jambo hapa halikuwa sawa. Wazo la kwamba huenda Nora alikuwa amegundua yeye ni nani likamwingia, lakini akajitahidi kutoonyesha itikio lolote la kubabaika.

"Naona kama vile hauko sawa. Una hasira na mimi kwa sababu sikukujibu hizi siku mbili, eti?" Lexi akauliza.

"Sina hasira nawe. Nimeumia tu," Nora akasema.

Lexi akabaki kimya.

"Ila sijaumia kwa sababu ya wewe kutonijibu... la. Nimeumia kwa sababu... nilifikiri nimepata kitu fulani ambacho nakijua, ila sasa nimetambua kuwa sikijui kabisa," Nora akasema.

Kauli hiyo ilimtikisa sana Lexi moyoni. Nora alisema maneno hayo kwa hisia nzito sana, na Lexi tayari akawa ameshakisia mwanamke huyu alielekea wapi ingawa alitaka kuhakiki zaidi.

"Mheshimiwa... mbona unaongea hivyo? Sielewi, niambie unamaanisha nini..." Lexi akasema.

"Oh Lexi... kwa nini lakini? Kwa nini ilipaswa kuwa wewe? Why was it supposed to be like this?" Nora akauliza na kuanza kudondosha machozi.

Lexi tayari akawa ameelewa. Nora alijua. Alijua kila kitu. Lakini utata ni kwamba alijua jinsi gani, na kwa sababu hiyo Lexi akaona aendelee kulazimisha mambo.

"Mheshimiwa... sielewi... tafadhali niambie, unamaanisha nini? Unaniogopesha..." Lexi akamwambia.

"Ahah... nakuogopesha. Hivi wewe ni nani? Kwa nini umeingia kwenye maisha yangu kama mwangaza mpya wa furaha lakini kumbe ni kitovu kikuu cha maumivu Lexi? Unafurahia sana kuumiza watu, eti? Furaha yako ipo kwenye huzuni za wengine, si ndiyo? Tell me. Najua unajua nachomaanisha. Tusizungukane kama watoto, just... tell me. Hakuna mtu mwingine hapa. Niambie tu. Kwa nini unafanya mambo haya yote? Kwa nini unaumiza watu wengi sana? Pesa? Ni pesa tu? Au kuna kingine dada yangu?" Nora akaendelea kuuliza.

Lexi alikuwa anamwangalia sana asijue la kusema. Angeanzia wapi kumwelezea maana ya mambo yote yeye na wenzake waliyokuwa wamefanya? Kuona kwamba hakuwa amemwitia labda maaskari ili wamkamate kulionyesha kwamba mwanamke huyu aliumizwa sana na ukweli alioujua kiasi kwamba alitaka kusikia kutoka kwa Lexi pekee sababu yake ni nini, ili amhukumu yeye kama yeye. Hii ilionyesha bado kuna vitu aliviona ndani ya Lexi vilivyompa matumaini ya kwamba huenda alikuwa na sababu iliyompelekea kufanya mambo mabaya, ingawa hiyo haingehalalisha matendo hayo yaliyopingana na sheria.

Lexi akabaki kutazamana na Nora tu kwa hisia sana, akijiuliza aseme nini sasa. Ajaribu kumwelewesha vizuri sababu zake, au amdanganye tu?

★★

Wakati hayo yakiwa yanaendelea, Luteni Michael, akiwa pamoja na Alex, Mario, Hussein, Rachel, Tariq na Zachary, walikuwa wanarejea jijini Dar es Salaam kutokea mkoa mwingine walipokuwa wamekwenda kutafiti masuala ya Mess Makers. Ulikuwa ni uamuzi wa Kanali Oswald Deule, ambaye kwa kujifanya mtaalamu sana aliwaagiza kwenda huko lakini hawakupata matokeo yoyote chanya.

Sasa wakiwa njiani kuelekea kule ambako jengo lao la utafiti lilikuwepo, wakatumiwa taarifa na Bobby zilizowaacha wote midomo wazi. Alikuwa amewatumia vigezo kwa njia ya simu vilivyowaonyesha watu sita ambao walitambulishwa kuwa Mess Makers. Kulikuwa na picha zao, majina yao, na taarifa chache zilizothibitisha kwamba wao kweli ndiyo waliokuwa Mess Makers. Hawa walikuwa ni Lexi Sona, Oscar Amari, Victor Quawey, Mensah Dodzi, Kevin Dass, na Kendrick Jabari!

Ni wawili tu ndiyo ambao hawakuwepo kwenye orodha hiyo, yaani LaKeisha na Torres.

Luteni Michael akamuuliza Bobby taarifa hizo alizipata vipi, naye akasema zilikuwa zimerushwa tu kutoka kwenye chanzo kisichojulikana, na alipojaribu kukifatilia akashindwa kukipata. Taarifa zilizothibitisha kwamba watu hao walikuwa ni kutoka kundi la Mess Makers ni pamoja na rekodi za sauti za maongezi yao wakati ule walipoiba dhahabu kwenye treni, wakati ambao Kendrick Jabari alifanya mpango wa kumteka ACP Nora ili kumuua kupitia kwa wanaume wale saba, na wakati ambao Salim Khan alikufa.

Ingawa hakukuwa na taarifa nyingi sana, mambo hayo tu yalitosha kabisa kuthibitisha kwamba ilikuwa ni kweli hasa kwa kuona uwepo wa Oscar na Kevin kati ya watu hao. Bobby alimwambia Luteni Michael kuwa mambo hayo yalikuwa yamesambazwa mpaka kwenye vyombo vya habari, na bila shaka yangekuwa yameshafika mpaka kwa wakuu wao. Wanajeshi waliopata taarifa hizo walishangaa sana kujua kwamba Kendrick Jabari alikuwa hai, kwa sababu walimfahamu kuwa na cheo cha Kapteni miaka kadhaa nyuma kabla ya tukio lililosababisha "kifo" chake.

Ikabidi Luteni Michael amtafute Kanali Oswald, ambaye naye tayari alikuwa amezipata na kumwambia waanze kutafuta ni wapi ambapo watu hao wangekuwa kupitia kwa Manengo na Bobby. Walikuwa wakimlenga zaidi Kendrick Jabari, hasa kwa sababu ya utata wa yeye kuhusika na Mess Makers wakati ilidhaniwa alikuwa amekufa kitambo. Manengo akawa amefanikiwa kujua kwamba Kendrick Jabari alikuwa nchini humo kwa zaidi ya mwaka sasa kutokea Ghana, na alikuwa akimiliki kampuni zilizohusiana na madini. Hakuwahi kuonwa hadharani lakini aliziendesha kampuni hizo kwa muda mrefu, na ikashangaza kwamba hakuwa ametambulika kwa muda wote huo.

Baada ya kufatilia taarifa za mawasiliano ya kawaida za Kendrick na wengine, kama walivyofanya tu mara ya kwanza kwa Kevin Dass, Manengo akabaini kuwa kwa sasa mwanaume huyo alikuwa kwenye moja ya kampuni zake pamoja na wenzake wawili, na eneo hilo lilikuwa hapo hapo jijini. Upesi, taarifa hizo zikatumwa kwa Luteni Michael ili yeye na wenzake wapitilizie huko huko. Kanali Oswald akawaambia kwamba angetuma taarifa kwa vyombo vya usalama vya maeneo ya huko kwenye kampuni ya Kendrick ili waagize vijana mahiri kwenda kuwakamata watu hao wakati Luteni Michael na wengine wakiwa njiani kuelekea huko.

Safari ya timu ya Luteni Michael ikageuza mkondo haraka sana. Luteni Michael alijawa na hamu kubwa mno ya kuja kumwonyesha Nora ukweli huo kumhusu Lexi ambao tokea mwanzo aliuhisi, lakini Nora na kila mtu akamwona mjinga. Alikuwa na hasira sana pia iliyomfanya atake kuwa wa kwanza kumshika Lexi ili amwonyeshe nini maana ya dharau kama aliyomwonyesha siku ile kwenye chumba cha Nora.

★★

Kufichuliwa kwa timu ya Mess Makers kulianza kusambaa kutoka kwenye vyombo vya habari, na pia mitandao ya kijamii haikuwa nyuma kuifanya hiyo kuwa mada iliyoongoza zaidi a.k.a "number one trending." Zilifika kwa wakuu wa jeshi, yaani Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko, na hata Raisi Paul Mdeme pia, na wote walikuwa wameachwa midomo wazi kwa kutoamini kabisa ukweli huo. Waliwasiliana na kuanza kuulizana iliwezekana vipi kwa Kendrick Jabari kuwa hai muda wote huo na wenyewe wasijue, na kilichoshangaza hata zaidi ni kumwona mtoto wa Meja Casmir akiwa hai pia.

Jenerali Jacob alimkumbusha Weisiko sasa kwamba kwa sababu ya kutokufuatilia kwake mambo vizuri usiku ule, mwanaume huyu alikuwa amesababisha madhara makubwa yaliyoletwa na wawili wale na kundi lao wakati huu. Ikawa wazi sasa kwamba hii ishu yote ya "Mess Makers" ilitokana na Kendrick Jabari na mtoto wa Casmir kama njia yao ya kuwalipizia kisasi. Ingawa bado hawakuweza kuelewa wawili wale walitaka kuwalipizia kisasi kwa njia gani kikamili, bado kuwa kwao hai ilikuwa ni tatizo kwa Majenerali na Raisi kwa sababu ni watu waliojua ukweli wote kuhusiana na Demba Group miaka nane iliyopita.

Raisi Paul Mdeme alikuwa amewasiliana na Jenerali Jacob na kumwambia kuwa haya yote yalikuwa makosa yao yeye na Weisiko kwa kukosa kuwamaliza wawili wale miaka mingi iliyopita, na sasa mambo mengi hata zaidi yangevurugika. Jenerali Jacob alipandwa na hasira sana. Hivi siyo jinsi alivyotaka mambo yaende hata kidogo, kwa sababu vyombo vya habari kujua kuhusu watu hao mapema namna hiyo kungeweza kufichua siri zao nyingi sana.

Akamwamuru Weisiko afanye juu chini ili kuwakamata watu hao upesi, kwa njia zozote zile ambazo tayari zilikuwa zimewekwa, afanye lolote lile ili kuwapeleka watu hao upande wao waweze kuwashughulikia wenyewe. Weisiko akamwambia tayari hilo lilikuwa likifanyiwa kazi, na bila shaka wangehakikisha wanafanikiwa; iwe isiwe.

★★

Lexi bado alikuwa kwenye chumba cha hoteli pamoja na Nora, akiwa bado anatafuta namna ya kujieleza kwake, lakini akashindwa. Nora alikuwa anaongea maneno yenye kuonyesha hisia nyingi za kuvunjika moyo, akimwambia kwamba kwa sababu ya mambo hayo, angetakiwa kumfunga pingu na kumpeleka jela yeye mwenyewe ikiwa hangempa sababu nzuri ni kwa nini alifanya mambo mabaya kuielekea serikali hii.

Lexi aliwaza; ikiwa kweli Nora angetaka kumtia mikononi mwa sheria, basi angekuwa amemwekea mtego mapema wakati alipofika hapo. Aliona ukweli wa kwamba mwanamke huyu hakuwa na hasira wala chuki kumwelekea, bali aliumia sana kwa sababu alidhani yeye ni tofauti. Sasa akawa anapambana na hisia zake mwenyewe hata zaidi, kwa sababu ilionekana ni kama alitakiwa kujigawa mara mbili kutoka kwenye yale aliyofanya, na kile alichohisi moyoni. Hata kama angesema nini, alijua mwanamke huyu asingemwamini kirahisi.

Wakati Nora alipokuwa akiendelea kusubiri jibu kutoka kwa Lexi, simu yake ikaita. Akaitoa kutoka mfukoni mwa suruali yake na kupokea bila kuangalia ni nani, huku bado akiwa anamtazama Lexi machoni. Lakini baada ya kutambua kwamba ilikuwa ni Bobby ndiye aliyempigia, akaweka umakini wake hata zaidi. Mwanaume huyo akamjulisha mambo yote yaliyokuwa yakiendelea, akisema Mess Makers walikuwa wamefichuliwa na mtu fulani asiyejulikana.

Mwonekano wa sura ya kushangaa kiasi usoni kwa Nora ukamwambia Lexi kuwa kuna jambo lilikuwa likiendelea; jambo baya. Nora hakuongea chochote kile zaidi ya kuitikia na kuendelea tu kumsikiliza Bobby, ambaye akamwambia kwamba alikuwa amemtumia taarifa hizo zenye kushangaza kwenye mfumo wake wa siri wa kutunza mambo. Huo ulikuwa umeunganishwa kwenye "tablet" yake Nora, hivyo upesi akampita Lexi na kuifata ilipokuwa kwenye mkoba wake. Akamgeukia Lexi na kumtazama kidogo, kisha akaiwasha na kuanza kutafuta habari hizo. Alikuwa anataka kuona uthibitisho zaidi ikiwa Lexi angekuwapo pia kwenye taarifa hizo, na baada ya kumwona, akachoka sana. Akafumba macho yake na kutikisa kichwa chake kidogo, akiwa amehisi kuvunjika moyo hata zaidi.

Alipogeuka nyuma tena ili amwonyeshe vizuri zaidi sasa Lexi ukweli yeye mwenyewe, akashangaa kukuta kwamba Lexi tayari alikuwa ameondoka. Yaani ilikuwa ghafla na kwa njia ya haraka, naye hakuwa ametambua hilo. Kwa haraka akafikiria kwamba ni lazima tu Lexi angekuwa amekimbia ili labda kwenda kuwaonya wenzake, na kwa sababu Bobby alikuwa amemtumia taarifa za walikokuwa wenzake na Lexi, Nora akaamua kwamba angekwenda huko huko pia. Akarudi sehemu yenye droo upesi na kutoa bastola yake, kisha akazifunga nywele zake vizuri kwa nyuma na kutoka hapo haraka sana.

Moto sasa ungeanza kuwa mkali zaidi!


★★★★


Kendrick alikuwa bado pamoja na vijana wake kule kwenye kampuni yake, na sasa walikuwa wamemaliza kufanya yale ambayo Torres alihitaji kufanya. Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza, na hatua ya pili ndiyo ingekamilisha mpango wao maalum waliokuwa wameuweka. Azra alipata kujionea mambo mengi hapo yaliyothibitisha kwamba watu hawa waliofahamika kama "Mess Makers" hawakuwa wabaya kama alivyodhani, na hisia mpya ya kujiona kuwa "sahihi" ikamwingia kwa sababu ya kuwa upande wao. Kendrick akamwambia kwamba kuna mambo mengi wangetimiza pamoja, mambo ambayo yangekuwa faida kwa watu wengi sana kutokana na yale waliyoyafanya.

LaKeisha pamoja na wengine walikuwa pembeni, na mwanamke huyu alikuwa ameboeka, hivyo akaamua tu kuzama kwenye mitandao ya kijamii; akitafuta udaku wa hapa na pale. Si ndiyo akazibamba sasa zile taarifa! Mwanzoni alihisi ni kama masihara, lakini alipofuatilia vizuri, akatambua kwamba kundi lao lilikuwa limevurugwa.

Upesi akawaonyesha wenzake mambo yalikuwa vipi, na wao pia wakapigwa na butwaa zito baada ya kuona mambo hayo. Wakaanza kujiuliza iliwezekana vipi wao kuweza kutambulika kirahisi namna hiyo mpaka kwenye mitandao ya kijamii, na fikira ya kwanza ilikuwa ni ACP Nora. Walidhani labda mwanamke huyo ndiye aliyefanya jambo fulani kuwafichua baadhi yao. Walianza kuzivunja laini na simu zao zote za kawaida, nao wakaanza kujiandaa kutoka jengoni hapo haraka iwezekanavyo.

Walitumia lifti ile ya kibinafsi kushuka mpaka kule chini ili waelekee kwenye magari yao, pale waliposhtushwa na magari matatu yaliyokuwa yamefika upande huo na kusimama umbali fulani kutoka kwao. Waliweza kuyatambua kwa haraka kuwa magari ya wanajeshi maalum, au majasusi, nao wakajiuliza walifikaje hapo haraka hivyo na hata walijuaje wangekuwa hapo.

Majasusi hao maalum wakashuka wakiwa wamevalia nguo nyeusi na kushikilia bunduki huku wakiwaelekea wakina Kendrick, nao walikuwa wakiwaambia wajisalimishe haraka sana. Kendrick na vijana wake wakaanza kukimbilia pande ambazo kulikuwa na nguzo nene zilizoshikilia ghorofa ili wajifiche, wakati huo Victor akawa ametoa bastola yake ndogo na kuwafyatulia risasi ili kuwachengua, na majasusi hao wakajikinga kwenye baadhi ya magari na nguzo za pembeni. Victor akawahi na kujirusha kwenye nguzo moja, kitu kilichofanya adondoshe begi lake, huku majasusi wale wakianza kusogea taratibu na kufyatulia risasi nyingi sana upande wa Mess Makers, zilizotoboa kuta, magari, na kupasua sehemu za nguzo zile walizojifichia.

LaKeisha alikuwa anatukana kwa hasira kwa sababu ya kutoelewa haya yote yaliwezekana vipi, lakini wakati huo huo tayari Torres akawa amemwelekeza Mensah cha kufanya, kwa kuwa walikuwa wamejifichia sehemu moja. Kwenye moja ya mabegi waliyokuwa nayo, kulikuwa na zile nguo zao za mapambano, naye akamwambia Mensah avae moja haraka sana ili awashughulikie majasusi wale. Alijua mwanaume huyu alikuwa na shabaha nzuri sana, na kwa hapa aliyekuwa na bastola ni Victor pekee, hivyo akamwambia Victor amrushie bastola Mensah, na baada ya Victor kufanya hivyo, Torres akamwambia Mensah awalenge majasusi wale sehemu za miguu au mikono ili kuwaangusha chini, lakini ahakikishe haui yeyote kati yao. Mensah alikuwa anataka kuwaua wote kwa sababu alihisi hasira, lakini Torres akasisitiza afuate alichomwelekeza.

Baada ya Mensah kumaliza kuvaa nguo yote, majasusi wale walikuwa karibu zaidi na nguzo waliyojifichia Kendrick na Azra, ambao walijitahidi kujibana hapo kwa uangalifu, nao wakatoa onyo la mwisho kwamba ikiwa wasingetoka basi wangewaua wote. Lakini papo hapo Mensah akatokea mbele yao, akiwa amejiviringisha kutoka alipokuwa amejibanza na Torres, naye akaanza kufyatua risasi kwa ustadi sana. Majasusi walikuwa wameanza kumfyatulia na yeye pia, lakini zikawa zinadunda, huku za kwake Mensah zikiwapata mmoja baada ya mwingine na kuwaangusha chini.

Walibaki majasusi 7 kati ya 15 waliofanikiwa kujikinga kwenye magari, huku wenzao wakiwa chini wanajivuta-vuta huku wakisikilizia maumivu ya risasi zilizowapata miguuni na sehemu za mikono. Mensah akajiviringisha mpaka kwenye gari moja na kujibanza, akihisi kama kuna vitu vingi vya moto vikiuchoma mwili wake kutokana na kumiminiwa risasi nyingi, lakini hakuwa ameumizwa sana kutokana na nguo yake kumlinda.

Kutokea kwenye nguzo nyingine, LaKeisha akamuuliza Torres kwa kikabila cha Hausa ikiwa na wao wangepaswa kuvaa nguo zao za mapambano, lakini Torres akasema muda usingetosha, na majasusi hao bila shaka walikuwa wanapanga kufanya jambo fulani kwa ukimya huo waliouweka. Mensah akasema risasi za kwenye bastola yake zingeisha haraka, hivyo labda kuvaa nguo zao kungesaidia. Lakini vipi kuhusu Kendrick na Azra, ambao hawakuwa na nguo za aina hiyo hapo? Victor pia alikuwa amedondosha begi lake mbali na alipokuwa, hivyo na yeye asingeweza kuweka kitu mwilini cha kumlinda.

Majasusi wale walikuwa wanafanya mpango wa kuwazunguka taratibu, naye Kendrick akasema kama Mensah angeweza, basi asogee mpaka pale ambapo majasusi wale walioumia walidondoshea bunduki zao na kuzichukua ili kuwapa wenzake. Mensah akachungulia kidogo, na hapo hapo risasi zikafyatuliwa upande wake na kufanya ajikinge tena, na hivyo akamwambia Kendrick haingekuwa rahisi sana kwa sababu nguo yake isingeweza kustahimili nguvu kubwa ya risasi za majasusi hao kwa muda mrefu.

Azra alipochungulia kidogo, akaona kweli majasusi hao waliobaki walikuwa wanazunguka kwa mtindo wenye ustadi, na sasa walikuwa wakikaribia sehemu aliyojikalisha Victor. Akataka sana kumwonya, lakini hiyo ingemhatarisha zaidi yeye na Kendrick kwa sababu majasusi wangeona walipokuwa wamejibanza, naye akashindwa kujua afanye nini ili kumsaidia mwanaume huyo.

Jasusi mmoja alikuwa akisema kwamba hakukuwa na haja ya kujificha tena, kwa kuwa walikuwa na mabomu, hivyo wajitokeze kabla ya wao kuwarushia. Torres alijua hiyo kuwa njia yao ya kuwalaghai tu, kwa sababu kama wangekuwa na mabomu hapo wangekuwa wameyarusha, ila wasingeweza kwa sababu na wao yangewaua.

Wakati mchezo huu mdogo wa "nasaka mke wangu" ulipokuwa ukiendelea, Kendrick na wengine wakashtushwa baada ya kusikia sauti za vishindo na mayowe ya kadiri kutoka kwa baadhi ya majasusi wale. Wakaanza kusikia na sauti za risasi, lakini hazikupigwa kuelekea upande wao, bali ule walikotokea majasusi wale. Mensah alipochungulia, akamwona mtu akiwa anawachanganya majasusi hao, na kwa haraka akatambua ilikuwa ni Lexi baada ya kuona nguo alizovaa kuwa kama zao za mapambano. Torres akauliza ni nini kinaendelea, naye Mensah akawafahamisha wote kwamba ilikuwa ni Lexi.

Kusikia hivyo, Azra akanyanyuka na upesi kujibinua sarakasi nyingi mpaka karibu kabisa na Victor, naye akamvuta na kuangukia naye pambeni, kwa sababu ni wakati huo huo tayari jasusi yule alikuwa amefika usawa wake na kuanza kufyatua risasi, hivyo akawa amesaidia Victor asipigwe. Mensah akamwona jasusi huyo na kumpiga risasi kifuani, naye akaanguka chini.

"Shit!"

Neno hilo lilimtoka Mensah baada ya kutambua kwamba alitenda kwa uharaka lakini akawa amesababisha kifo. Kendrick, LaKeisha na Torres walichungulia pia na kumwona Lexi akijitahidi kuwashughulikia majasusi wengine waliobaki, naye Mensah akajisogeza sehemu nzuri ili kuwalenga miguuni wanaume hao. Walikuwa wanammiminia Lexi risasi mwilini kila alipotoka kwa mmoja na kumfata mwingine, na nguo yake pia ikawa inapungukiwa na uwezo wa kuzizuia risasi zile.

Mensah aliwalenga vizuri majasusi hao walipokuwa wamekengeushwa na Lexi, naye akawatandika risasi miguuni na kuwafanya waanguke chini huku wakiugulia maumivu. Upesi Mess Makers wakawafata wote na kuwanyang'anya bunduki zao, maana bado kuna wengine walikuwa wakijitahidi kuonyesha uimara kwa kufyatua risasi ingawa nao walikuwa wamejeruhiwa kwa risasi. Mensah alikuwa amewatandika risasi kwa ufundi ambao ungewafanya wasinyanyuke, lakini wasingekufa.

Walipokaribiana, Torres akamuuliza Lexi ilikuwa vipi mpaka watu hawa wakajua utambulisho wao, naye Lexi akawaonya wote kuwa wangepaswa kuondoka haraka sana kwa sababu wengine walikuwa wanakuja kuwakamata. Kabla hawajafikiria kufata magari, hapo hapo tena yakaingia magari mawili ya maaskari wengine wakija upande wao kwa kasi. Lexi akawaambia wenzake waondoke haraka sana, na yeye angejaribu kuwazubaisha maaskari hao ili wenzake waponyoke. Kendrick akawa anakataa, akisema walipaswa kuondoka kwa pamoja, lakini Lexi akalazimisha na kumwambia angetoka akiwa salama, hivyo watangulie na yeye angefata. Akafanya kama kuwaamuru kabisa, nao wakaanza kuelekea kwenye gari ambalo halikuwa lao, kwa sababu ya kwao yalikuwa yameharibiwa kwa kupigwa risasi.

Lexi akawageukia maaskari wale, wakiwa 8, waliokuwa wameshafika hapo na kushukia umbali mfupi wakiwa na mabunduki yao, na wakiwa wamewaona majasusi wale waliopigwa risasi, naye akaanza kuelekea upande wao huku akiwa amenyoosha mikono yake juu. Mmoja wao alikuwa anafoka kwa sauti akisema Lexi apige magoti na wengine walioingia kwenye gari watoke, lakini Lexi akaendelea tu kuwafata bila woga.

Mmoja wa maaskari hao akafyatua risasi mguuni kwa Lexi, lakini Lexi akaanza kukimbia kuwaelekea kwa kasi sana, huku akipindisha mwili wake huku na huko. Maaskari hao wakawa wanafyatua risasi zao ambazo hazikuwa na nguvu kali sana kama za bunduki walizotumia majasusi, naye Lexi akawafikia na kuanza kuwapiga kwa mitindo ya sarakasi nyingi.

Torres akawa amefanikiwa kuliwasha gari waliloingia, naye akaligeuza na kuanza kuelekea upande wa kutokea. Alipokaribia usawa ambao Lexi alikuwa akipambana na wale maaskari, alitaka kusimama hasa kwa sababu wengine walikuwa wanamwambia afanye hivyo ili wamsaidie Lexi na yeye aingie kwenye gari, lakini Lexi akatoa ishara kwamba wasisimame na waondoke haraka sana. Torres alihuzunika mno, lakini alikuwa anajua kile ambacho Lexi anafanya, yaani kuwatanguliza wao badala yake yeye.

Akapitiliza tu na kuwafanya LaKeisha na Mensah wabaki wakilalamika kwa nini alimsikiliza Lexi wakati alikuwa kwenye shida. Torres aliliondoa gari hapo kwa kasi sana, huku akisema Lexi alifanya hivyo kwa sababu alijua wakitoroka wao, hata kama yeye angekamatwa basi wangeweza kutafuta njia ya kumsaidia. Lakini Kendrick alijua ingekuwa ngumu kufanya hivyo sasa hivi kwa sababu tayari wengi wao walijulikana, hivyo ikaonekana ni kama wamemwacha Lexi peke yake kwenye shimo lenye simba wakali. Akafumba macho yake akihisi huzuni kuu moyoni, na gari lao likafanikiwa kutoka eneo hilo.

Lexi alijitahidi kupambana na maaskari hao waliokuwa watata sana, naye akafanikiwa kuwafanya wote wapoteze fahamu. Alihisi kuchoka na maumivu kiasi kwa sababu ijapokuwa nguo yake ilisaidia kuzuia risasi, zilikuwa zimedunda kwa njia iliyofanya ahisi kama mtu aliyepondwa na kokoto ndogo ndogo mwilini. Akawa anapumua kiuchovu, naye akaamua kuivuta "mask" yake na kuitupa pembeni, halafu angeelekea kwenye gari mojawapo kati ya yale waliyokuja nayo maaskari ili aondoke hapo.

Akaanza kulielekea moja, na ile tu alipoufikia mlango wa gari hilo, sauti aliyoifahamu vizuri sana ikamsemesha kwa nguvu.

"Tulia!"

Lexi akanyanyua macho yake na kukuta ni Nora, akiwa amesimama kutokea umbali mfupi mwanzoni kabisa kwenye mwingilio wa eneo hilo la maegesho. Alikuwa ameshika bastola huku ameilekeza kwa Lexi, naye akaanza kutembea polepole kumwelekea huku akiwa amekunja sura yake kuonyesha hasira. Akasimama baada ya mwendo huo mfupi, naye Lexi akaachia mlango wa gari na kubaki anamtazama kwa umakini.



★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★

WhatsApp +255 787 604 893
 
Back
Top Bottom