17
Nilipomtazama yule msichana kwa umakini huku nikijaribu kuyatuliza vizuri mawazo yangu, nikaiona ile sura ya Rahma wa usiku, na wala haikuwa akili ya pombe, alikuwa ni Rahma. Hali ile ikanifanya nitokwe na jasho jepesi mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakianza kwenda mbio.
“Wewe ni Rahma wa Singida?” ghafla nilimuuliza swali kama mtu hamnazo.
“Hehee! Nilitaka nikuone tu, kumbe unanikumbuka eh?” yule msichana aliuliza kwa sauti ya mkwara huku akiachia tena kicheko.
Sasa abiria wengine hawakugeuka kutuangalia maana walishamzowea Rahma. Nilibaki nikimtumbulia macho huku nikiwa sijui niseme nini. Nikaanza kuvuta kumbukumbu kichwani kwangu, picha iliyonijia ni kwamba rafiki yangu Majaliwa alimtambulisha kwangu mwanamke wa Kiarabu aliyeitwa Rahma, kisha tulikula na kunywa, basi! Nilipojaribu kukumbuka mengine kichwa changu kiligoma kabisa kuyakumbuka!
“Mbona uko kimya, au unajaribu kulikumbuka sebene la usiku?” Rahma aliniuliza baada ya kuniona niko kimya nikimtumbulia macho, aliyasema hayo huku akiyakwepa macho yangu na kutazama chini kwa aibu.
“Sebene lipi, mbona silikumbuki!” nilimuuliza Rahma huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu lakini sikuweza kupata picha.
“Unajifanya kuzuga! Kisa cha kunikatia shanga zangu utadhani ulikuwa na kisasi na mimi ni nini!” Rahma alisema kwa mshangao huku akiachia mguno.
“Halafu vile ulivyonibinua na kunivuta nywele zangu kama ulikuwa na hasira na mimi ndo nini? Yaani hapa kichwa chote kinaniuma utadhani mgonjwa wa malaria, kwa kweli ulivyonifanyia usiku sitakuja kukusahau? Mwanamume ulikuwa kama chatu mwenye hasira kali!”
“Acha fiksi zako wewe!” nilisema kwa mzaha huku nikicheka, japo moyoni nilikuwa nashangaa.
“Fiksi? Hak’ya mungu naapa sijawahi kukutana na mwanamume wa aina yako anayejua kumchezesha mtu kwata! Yaani ulinipelekea moto hadi nikawa nahisi unataka kukivunja kizazi changu, na huo mkao ulioniweka sikuweza hata kukurupuka!” Rahma alisema huku akikunja uso wake na kumeza mate mithili ya mtu aliyelambishwa ndimu kisha akatingisha kichwa chake taratibu.
“Ya kweli hayo?” nilimuuliza Rahma nikiwa siamini kile alichokuwa akikisema lakini nilipomtazama usoni nikaona kuwa hakuwa akiongopa bali alikuwa akimaanisha. Hata hivyo bado kichwa changu kiligoma kabisa kuyakumbuka hayo aliyokuwa akiyasema Rahma!
“Jason, mimi ni gwiji kwenye suala la mahaba, tena si gwiji tu bali kungwi la makungwi na sijawahi kumsifia mwanamume ila wewe acha nikupe heshima yako, yaani ulinimudu kila idara hata hujanipa nafasi ya kuucheza mchezo…”
“Nikupe nafasi ili unifunge magoli ya kizembe!” nilitania ili kujaribu kunogesha maongezi japo sikuwa nakumbuka lolote. Dah, sikuwahi kunywa pombe kiasi cha kupoteza kumbukumbu za mambo niliyofanya!
“Haha, nilijua tu unajifanya hukumbuki kumbe ulikuwa unazuga. Yaani hapa nilipo nimechoka balaa, mwili wote kama si wangu! Kiuno chote hoi!” Rahma alisema huku akikunja sura yake.
“Mmh, basi pole!” ndilo neno pekee nililomudu kulitamka kwa wakati ule.
“Wewe nibeze tu na pole yako ya uongo na kweli, yaani hadi sasa bado najihisi kizunguzungu. Ilibaki kidogo tu nishindwe kuamka alfajiri ili niwahi basi…” Rahma alisema huku akiyafinya macho yake. Nikakumbuka kuwa wakati naingia kwenye basi nilimkuta akiwa amejiinamia huku ameyafinya macho yake.
“Halafu mbona hukuniambia kuwa na wewe una safari leo ningekuamsha tuondoke pamoja! Kwa jinsi nilivyokuacha umelala chakari sikujua kama leo unasafiri!” Rahma aliniuliza huku akiniangalia machoni.
“Huenda nilisahau kukwambia. Samahani kama sijakwambia,” nilisema huku nikijilaumu kwa kutokumbuka mambo yaliyotokea usiku kati yangu na Rahma.
Hakika katika maisha yangu sikuwahi kunywa pombe nyingi kiasi cha kushindwa kukumbuka mambo niliyofanya! Kama Rahma angekuwa na tabia ya udokozi angeweza hata kuniibia na nisijue nani kaiba.
“Kwa zile pombe kali ulizokuwa ukigida jana, mwanamume nilikuvulia kofia, yaani unakunywa kiama!” Rahma alisema huku akinipigia saluti.
“Basi nikajua utaunguza hadi utumbo na shughuli usiiweze tena. Wakati tunaelekea kwako nilidhani nimeokota garasa na tukifika ndani basi mbuyu ungelala puh! Duh, kumbe nilijidanganya! Si nikakutana na gwaride ambalo sijawahi kupigishwa tangu nizaliwe!” Rahma aliongea huku akitoa macho na kuchezesha mikono kuyasindikiza maneno yake. Kope zimemsimama kama miba ya nungunungu!
Nilimtazama Rahma usoni nikaona kuwa hakusemea utani, alimaanisha kiasi cha kunifanya nijikute nikiachia kicheko kikubwa kilichowafanya abiria wengine ndani ya lile basi wageuke kuniangalia kwa mshangao.
“We nicheke tu,” Rahma alisema akiwa amenuna, kisha akaachia kicheko hafifu cha kishambenga, kama ilivyokuwa haiba yake, na kuniangalia kwa aibu.
“Pole mwaya,” nilisema huku nikitabasamu lakini Rahma alijifanya kununa, nilipeleka mkono wangu kwenye mbavu zake na kumtekenya, akaruka huku akiachia kicheko.
“Yaani wewe! Jinga kabisa!” Rahma alisema kwa utani huku akinitia singi usoni. Wote tukacheka.
Kisha kilitokea kitambo fulani cha ukimya, nilikuwa najaribu kuyatafakari maneno ya Rahma huku nikijaribu kuvuta kumbukumbu lakini bado picha ya kile kilichokuwa kimetokea usiku kati yangu na Rahma ilikataa kuja kichwani kwangu.
Nikiwa katika kutafakari, Rahma alinisemesha, “Jason naomba unisamehe tafadhali, kabla sijakuuliza swali ambalo ni la kibinafsi kabisa.”
Nilimtazama Rahma kwa wasiwasi kidogo kisha ilibidi nilikohoa kidogo kurejkebisha sauti yangu na kumuuliza, “Ni swali gani hilo, mbona unanitisha!”
“Hapana, wala usiogope. Swali lenyewe ni la kawaida sana lakini ni kwa watu wanaojuana na waliozoweana zaidi, kwa wasiozoweana kama hivi mimi na wewe ni lazima tuombane radhi kwanza,” Rahma alisema huku akinitazama kwa tabasamu.
“Hatujazoeana vipi wakati unayajua mauno yangu na unaujua hadi mkato wa chumba changu!” nilimtania Rahma huku nikiachia kicheko hafifu.
“Hebu acha masihara yako bwana, ujue mimi niko
serious,” Rahma alilalamika huku akinitazama kwa macho malegevu yaliyojaa aibu.
“Sawa, Rahma, niko radhi wewe niulize tu hicho unachotaka kuniuliza,” nilimwambia Rahma huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani.
Kusikia hivyo, Rahma alitulia kidogo na kuinamisha uso wake chini kama vile alikuwa amelisahau swali alilotaka kuniuliza, kisha baada ya kitambo kifupi aliinua uso wake kunitazama usoni kwa macho yaliyojaa haya.
“Hivi Jason umeoa?” Rahma aliuliza huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wangu. Nilihisi kuwa alikuwa anajitahidi kudhibiti donge la wivu kooni mwake na hivyo nikaachia tabasamu kubwa lililonifanya nionekane mtanashati zaidi.
“Ningekuwa na mke sidhani kama ningekupeleka nyumbani kwangu,” nilimjibu Rahma kwa sauti tulivu.
“Inategemea maana ninyi wanaume hamtabiriki. Okay… labda una mchumba? Au tusemee…
girlfriend tu?” Rahma aliniuliza tena huku akiendelea kunitulizia macho yake usoni kwangu.
“Hapana, sijaoa. Sina mwanamke wala mchumba na… pia sina
girlfriend,” nilimwambia Rahma pasipo mzaha wowote. Rahma akashangaa sana.
“Haiwezekani!” Rahma aliniuliza huku akinitumbulia macho yake malegevu.
“Kwan nini isiwezekane?” nilimuuliza Rahma huku nikimkazia macho.
“Kama huna mwanamke, mchumba au
girlfriend basi una wanawake wengi, kwa jinsi ulivyo. Nina maana kuwa mwonekano wako, utanashati na umbo lako la kimazoezi, ni lazima utakuwa unawapanga foleni!” Rahma aliniambia kwa sauti dhaifu ya kinyonge huku akinikazia macho. Muda huo alionekana kuwa mbali na mzaha.
“Dah, kwani naonekana mkware sana, eh?” nilimuuliza Rahma huku nikijitazama kama niliyekuwa najikagua.
Itaendelea...