Simulizi: Harakati za maisha

Wap Jack Daniel
 
SEHEMU YA AROBAINI NA SABA

Mume wangu mwenyewe ni huyu,
na huyu mwingine ndiye ambaye alipewa gari auze,yaani hawa wote lao moja na sina amani kabisa kuanzia sasa kutokana na maneno aliyotamka mume wangu.
aliongea kwa Jazba mke wa Shabani akiwaeleza maaskari.

Kiongozi vipi tena unampiga mwanamke na kumtishia maisha?umemwambia utamuua ,ulikuwa na maana gani,au hujui kwamba kutishia ni kesi mbaya kuliko hata kuua kwenyewe eeeh,hebu inuka kwanza hapo.ni mmoja wa wale maaskari akimwambia Shabani asimame.

Aisee kijana kuwa na adabu kwanza unawezaje kuamini maneno ya upande mmoja? una ushahidi gani kama mimi nimetamka maneno ya kumtishia mke wangu?
Unapaswa kuwa na busara pindi unapoletewa habari kama hizi haswa kwa wanandoa.Shabani aliongea kwa kujiamini kiasi cha mimi kushangaa.

Sawa tufanye hujamtishia,vipi kuhusu kumpiga , halafu nyie ni watu wazima kwanini umpige mkeo huoni kama unamdhalilisha eeeh?
Kwanza haya masuala tutazungumzia kituoni hapa siyo mahala pake.aliongea yule afande mwingine.

Lakini Shabani alikataa kuongozana na wale jamaa akidai kituoni atafika mwenyewe, wale askari waliangaliana kisha wakaona haiwezekani.

Aisee kaka tuheshimiane,
Kama tungetaka ufike kituoni bila uwepo wetu tungekupigia simu,lakini hapa unaondoka na sisi na gari lako nitaendesha mimi usijali.aliongea askari fulani machachari ambaye hata sare zake zilimbana ,labda ndiyo hawa mapot wa digital.

Jamani mimi naona kama vipi tunaweza kuzungumza tu,maana mshitaki yupo na mshitakiwa nipo.kwanini tusirekebishe haya mambo kuliko kufedheheshana?
alishauri Shabani.

Aisee mimi sitaki kuongea na huyu hapa,kanipiga kaniumiza ,na hapa nina karatasi la PF3 ,natakiwa nifike hospital nikafanyiwe vipimo maana kanikaba shingoni nahisi kuna mishipa haipo sawa.
aliongea kwa kudeka mke wa Shabani.

Sasa mama kwani huyu wewe unamuitaje?hebu tufafanulie.
aliuliza afande mmoja.

Huyu ni baba wa watoto wetu,.alijibu yule mwanamke.

Kwanini ni baba wa watoto wenu na si mume kama alivyosema yeye kuwa ni mumeo?
walihoji wale maafande.

Kanipa talaka kwa mujibu wa Shari'ya ya dini yetu ya kiislamu,hivyo si mume wangu tena labda ni mpaka atakaponirudia na niwe mkweli huyu baba mimi simtaki tena sihitaji awe mume wangu,nahitaji kuishi kivyangu kwani ni lazima niwe na yeye eeeh.
aliongea kwa sauti ya juu yule mwanamke kiasi cha watu kusogea na kujionea sinema ya bure,huku wenye viherehere wakimtupia lawama Shabani kuwa kwani anapiga mwanamke kwenye dunia ya sasa.

Daniel sikutia neno lolote maana kila nikimwangalia yule mwanamke hasira zilininyemelea.

Sasa mamdogo hivi mtu akupige kweli halafu uwe hivyo inawezekanaje,hebu jishushe mbona yanazungumzika haya eeh ,afande mmoja aliongea huku tayari akiwa upande wa Shabani,nadhani saikolojia yake ilisoma kitu,alijua lazima Shabani atatoa mavumba hivyo akaamua kumbadilikia yule mwanamke.

Halafu afande sikuelewi,tena siwaelewi kabisaa,mlisema gari haina mafuta nimeweka au sikuweka,mkasema mna kiu hamjanywa maji si niliwapa mbona sasa siwaelewi elewi.mke wa Shabani aliropoka.

Baada ya kusema vile maaskari waligeuka mbogo hawakutaka kumsikiliza yeyote. walimbeba jamaa yangu Shabani kama mzigo wakamsweka kwenye gari kisha wakaondoka kwenye upeo wa macho yangu.

Nilitabasamu tu huku nikimsikitikia jamaa yangu maana ni bora upelekwe kituoni kwa kesi za utafutaji lakini siyo kutishia au kupiga,kila aliyekuwepo pale mgahawani alitamani kusikia chochote,watu walinizonga kutaka kujua nini kimetokea kwa jamaa ambaye nilikuwa napiga naye stori.

Jamani mimi sijui chochote,huyu nilikuwa naongea naye masuala yetu ,hivyo nimeshangaa tu kwa hayo mliyoyaona yakiendelea mimi mwenyewe ni mgeni kama nyinyi,
niliwajibu huku nikiondoka eneo lile sikuwa na wasiwasi na Shabani kwakuwa namjua si mwepesi kivile wakukaa mahabusu labda mwingine si yeye .

Dah huu mwaka nao bora uishe tu yaani majanga hayaishi, Sasa sijui niende nikaongee na yule mwanamke ili wayamalize?
Kama kuachana ni bora waachane kwa amani kila mtu ashike hamsini zake haina maana kuaibishana vile

Kwanza Shabani licha ya kuwa umri umeenda hawezi kosa mwanamke,
Pesa ya kula anayo,anaweza kuvuta Shangingi lolote akamalizia uzee wake, wanawake waaminifu bado wapo wengi tu tatizo sisi wanaume wengi huwa tuna pupa ndiyo maana huwa ni rahisi kuangukia pabaya.nilijiwazia

Nilifika home nikabadilisha nguo kisha nikaenda kwenye pub fulani ambapo huwa napendelea kutulia mara nyingi haswa kwakuwa mmiliki huwa tunaheshimiana na nikiwa sina vyangu huwa ananidhamini.
Pia ni sehemu tulivu isiyokuwa na watu wengi,niliagiza vyombo nikaanza kukata maji taratibu huku nikiperuzi ghafla simu ya Shabani iliingia huku nikiipokea kwa pupa.

Eee bro nambie vipi uko wapi.
Niliuliza.

Nipo home vipi najua ulikuwa na wasiwasi labda kuwa huwenda nikawekwa lockup.aliongea huku akicheka.

Wasiwasi ni muhimu kaka, maana hawa wanawake mimi mwenyewe nawajua namna wanavyoweza kubambikizia kesi ukajikuta unakuwa sehemu mbaya.hebu niambie imekuwaje.niliuliza.

Mwenzako akitembea maili mbili wewe nenda maili nne,
Hatukufika kituoni tulielewana tu katikati ya safari nikawa nishamalizana nao, yeye si aliwapa maji Mimi nimewapa chakula washibe kabisa. aliongea Kisha tukacheka sana.

Basi sawa bro ila usimpige siku nyingine mambo hayawezi kuwa rahisi hivyo tahadhari ni muhimu . Nilishauri.

Usijali na katangulia nyumbani japo Mimi kuanzia leo nitalala chumba kingine maana talaka nimempa ila kutoka hataki, nashangaa si amejenga aende kwake kama alivyokuwa amepanga ili niwe huru.
aliongea kwa hisia kali Shabani.

Mimi hapo Sina Cha kushauri zaidi japo ningependa kuona mnaelewana na kuishi kama zamani. tuliongea mengi sana Kisha nikakata simu.

Baada ya nusu saa huku nikiwa namalizia beer zangu niondoke, simu iliita, ikiwa na namba ngeni tena inatokea nje ya nchi huku ikiwa ni code ya nchi ninayoifahamu, nilipokea kwa hofu kidogo huku nikitoka eneo lile .
Alikuwa ni boss wangu .

Daniel nadhani ofisini kazi zimepungua, na pia kuna taarifa nimepokea Sasa hivi kutoka Mkoa X hivyo nadhani kuanzia kesho unatakiwa uende huko , na Kuna mwenyeji wako atakupokea. Kesho ukifika ofisini meneja atakupa utaratibu mzima na dereva .aliongea kwa sauti yenye mamlaka.

Moyo ulipiga huku nikiwa Sina namna wala pingamizi, ila sehemu aliyosema niende ilikuwa ni vijijini ambako kwanza umeme hakuna,hata nyumba za wageni sikuwa na uhakika kama zipo na pia shida ya maji ilikuwa ni kilio cha wilaya ile.

Kiunyonge niliacha bia na kuondoka zangu kama vile mtu aliyeonewa na hakika nilionewa kweli ila sikuwa na namna.

Jifunze,
Elimika,
Burudika.

Itaendelea.....................
 
JD tumezoea unatuchapa vi 2 iweje unatupa kamoja ka mkwezi 😂
 
SEHEMU YA AROBAINI NA NANE

Ilikuwa ni saa nne asubuhi nilikuwa nachukua vilivyo vyangu na kuweka kwenye handbag yangu tayari kwa kuianza safari ya mkoa ambao naufahamu kwa kupita tu,ilikuwa ni moja ya safari ngumu kwangu kwa kipindi kile.ni kweli nilikuwa napenda kusafiri lakini kwa kipindi kile niseme tu safari ilikuja wakati siyo ila sikuwa na namna.ningefanyaje sasa?
Ningepingana na mamlaka?
Isingewezekana.

Kinyonge nilitoka na kwenda juu alipo meneja nikapokee maelezo fulani kama tulivyokubaliana,

Niambie Daniel kwema?
Upo sawa?
aliniuliza huku akishusha miwani yake midogo na kutabasamu.

Nipo sawa mkuu hakuna shida yeyote mbona.nilijibu kwa kujichangamsha.

(Huku akicheka)
Dani bwana yaani sura yako inaonesha sana haupo sawa au hujaipenda hii safari najua kuna
vitu ambavyo kiukweli vinaumiza sana najua kupokea taarifa jana mara leo tena asubuhi hii unajiandaa na safari kiukweli inakuwia vigumu sana.

Una mambo yako mwenyewe hujayapanga,na pia kila mmoja anapenda kuwa karibu na familia,lakini kiufupi ndiyo hivyo wewe nenda ndugu yangu,huwezi jua waweza pata fursa kibao zenye kukufanya uongeze kipato chako hususani huu mkoa unaoenda una fursa kibao
(Huku akiniorodheshea).

Alikuwa ni meneja akijifanya kunihurumia na kunifariji lakini hata hivyo mimi nilikataa kuonekana eti siipendi safari.

Wala usihofu mkuu mimi ni mtumishi kwenye hii taasisi na najivunia kuwa hapa na nafurahi kuona natumwa sehemu mbalimbali hii inaonesha ni jinsi gani mnaniamini hakika nafarijika sana.nilidanganya.

Meneja kusikia vile hakusema neno badala yake aliinuka kwenye kiti chake na kunipa mkono huku akionesha kufurahi sana,kisha tukaagana nikaondoka.

Nilimkuta dereva akinisubiri huku akiwa kanuna sana baada ya kuniona,ni jamaa ambaye huwa simkubali hata kidogo kutokana na kuwa ni mbishi na jeuri fulani hivi,lakini pia hata yeye huwa najua hanipendi hakuna yeyote mwenye sababu za maana kwanini hamkubali mwenzie labda niseme tu hakukuwa na ile chemistry baina yetu.

Safari ilianza huku tukiliacha jiji lenye mitaa na mataa yake,hapa chungu akaanza kukikoleza moto huku akiovertake ovyo sana,nilimwangalia huku nikiona ni visa ananifanyia, yaani hii Dunia hakika Kuna watu na viatu.

Kumbuka tangu tumetoka au tumeianza safari hakuna aliyemuongelesha mwenzie Mimi nikiwa bize na simu na yeye bize na usukani, kiumri alikuwa kanizidi na ndiye dereva mwenye umri mkubwa kwenye taasisi yetu pia ndiye aliyedumu zaidi kuliko wengine ambao walibadilisha mazingira, kuacha kazi , kufukuzwa n.k

Aisee kaka punguza mwendo kidogo kama kufika tutafika tu wala usijali.
nilivunja ukimya baada ya kushindwa kuvumilia, siwezi Kaa roho juu kama vile nimepanda gari la mashindano.

(Kwanza alicheka)
Kiongozi nina zaidi ya miaka thelathini na kitu naendesha gari, boss wako mwenyewe kabla hajapanda cheo nilikuwa namuendesha mimi na hajawahi kuniambia hivi , kwanza gari imetimia Kila kitu yanini itembee kama mkokoteni? nawahi nataka kurudi leoleo kumbuka kesho Kuna mtu nampeleka mahali. alijibu kwa dharau sana huku akiongeza speed.

Ujue hii ni gari ya kipekee sana mkuu yaani licha ya kumaliza gia lakini bado inadai gear nadhani Kuna kitu hakipo sawa Kati ya injini na gearbox. aliongea mwenyewe

Sikumjibu Chochote nikaamua kunyamaza kwani kuendelea kumdisturb ningesababisha mambo mengine.

Kumbuka nilikuwa sijakula chochote tangu jana yake hivyo Kuna mahali tulifika nikaona ni muda muafaka tule kwasababu , kwanza ninakoenda ni rural area hivyo sikuwa na imani ya Moja kwa moja juu ya upatikanaji wa vyakula nikaona bora tule hapa mjini lakini dereva alikataa eti anachelewa

aisee kaka tunapoenda ni karibu mbona ni kama kilomita mia tu, Sasa si mwendo wa lisaa tu tutakuwa tumefika eeh, kumbuka meneja alisema sipaswi kulala.
yule jamaa hakika alikuwa ni wa aina yake kwani kwenye safari zote dereva hutii anachoambiwa lakini kwa yule Mzee ilikuwa ni tofauti.

Hatimaye tulifika sehemu husika ambako hata miundombinu mingi ilikuwa bado kidogo yaani ilikuwa ni kushoto sana tu, nikipokelewa na mwenyeji wangu ambaye alikuwa ni mchangamfu sana aliongea kama vile tunafahamiana siku nyingi kumbe ndiyo kwanza tunaonana ila nilipenda namna alivyo.

Karibu sana kaka hii ndiyo wilaya yetu ya (akitaja jina)
Imepata hadhi ya wilaya yapata miaka mitano tu iliyopita lakini alhamdulillah tumepata bahati ya kuonekana na serikali kuu hivyo mambo mengi yameenda haraka mno na hapa tulipo ndiyo kitovu cha mji wetu. (huku akizungusha shingo kuangaza angaza huku na huko)

Hakika mpo vizuri na nimepapenda kwakweli,hongereni wakazi kwa kushirikiana na serikali kuifikisha hapa ilipo hakika ndani ya miaka kumi ijayo najaribu kuvuta picha patakuwaje hapa. nilipasifia ili kwenda sambamba na mwenyeji wangu.

Sasa kaka muheshimiwa DC alikuwa anakuhitaji maana kapata taarifa ya ujio wako hivyo kabla ya kuanza ratiba zozote ni vyema tufike tukatambuane.mwenyeji wangu alikuwa mcheshi sana.

Nilifika ofisini kwa mheshimiwa nikakutana naye tukaongea mawili matatu huku nikikaribishwa vizuuuri kabisa .

Kuna kipande cha barabara kutoka barabara kuu mpaka hapa, nadhani umejionea mwenyewe ni kama kilomita sitini hivi na licha ya kufanya ukarabati mara kwa mara lakini imekuwa ikiharibika haswa kipindi cha mvua, hivyo tumeshaongea na wahandisi kadhaa na michakato inaendelea vizuri.

Wewe umekuja hapa kama fundi maana tumesikia ndiyo taaluma yako, maana vifaa vilivyopo vimekaa muda mrefu Sasa tukaona kabla ya kuanza kazi ni vyema vikafanyiwa checkup. Hii ni kwaajili ya maslahi ya ya taifa pia kujenga nchi yenye taswira nzuri Duniani.kuna wageni kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakifika hapa, napenda ufahamu kuwa wilaya yetu inapakana na hifadhi ya taifa.ni aibu barabara inayofika wilayani kukosa lami.wakati halmashauri inaingiza mapato kutoka vyanzo mbali mbalimbali.najivunia uwepo wako Daniel kwa pamoja tujenge taifa letu.aliweka kituo yule mkuu wa wilaya.

Nilitikisa kichwa kukubaliana naye huku moyo ukilipuka kwa uoga,ni Bora kutengeneza chombo cha mtu binafsi, hata kikizingua unajua namna ya kujitetea, lakini serikali isikie tu timu ya watu hamsini inakuwa inakutegemea wewe na baadhi ya watu hupitisha vitu kabla hata havijaonesha kama vitafanya kazi vizuri.

Tuliagana huku nikiambiwa Kuna watu nitakutana nao kesho yake kwaajili ya kujua naanzia wapi , lakini pia malazi na sehemu za kupata chakula zilikuwa vizuri tofauti na nilivyofikiria. ni kawaida kwa watu waishio jijini Dar es salaam kuchukulia poa maeneo mengi yasiyo kuwa maarufu .

Dereva wangu alipoona Kila kitu kipo sawa akaondoka na kuniacha huku baridi na hali ya hewa ya kule vikinisumbua , nilitamani nipate moja mbili lakini nikaona huku ni ugenini si jambo zuri unaweza mtu ukahitajika na wakubwa muda wowote, halafu ukaonesha taswira mbovu na mbaya ambayo itashusha thamani yako.

Jifunze,
Elimika ,
Burudika.

Inaendelea.................
 
SEHEMU YA AROBAINI NA TISA

Asubuhi siku inayofuata niliamka mapema sana (hii ni desturi yangu haswa nikiwa ugenini)

Niliwasha PC yangu na kuendelea kujikumbusha baadhi ya vitu ili kujiweka timamu kiakili na hata kimwili pia.
Baada ya muda mfupi yule mwenyeji wangu aliyenipokea jana wakati nafika alikuja huku akiwa na watu wawili waliovaa reflector na kunitambulisha kwao.

Hawa ndio utakao shirikiana nao kwenye kazi,tunatumai ndani ya siku chache zijazo vyombo vitakuwa tayari kwa kufanya kazi.aliongea yule mwenyeji wangu na kisha kuondoka.

Wale jamaa wawili walibaki kimya tu huku nikibaini jambo kati yangu na wao,

Niligundua kuwa hawajapenda mimi kushirikiana nao,kwasababu muda wote walikuwa wakinitazama kisha wanaangaliana wao kwa wao na kutabasamu kidharau.

Niliingia ndani nikabeba handbag yangu yenye vifaa muhimu ninavyovijua kisha tukaondoka kuelekea mahali vilipo vifaa, wenzangu walikuwa mbele mmoja anaendesha gari mwingine yupo pembeni yake akiwa na kijinotebook fulani akikisoma na kuandika baadhi ya vitu,walikuwa wanaongea kiswanglish sana huku wakicheka na kufurahi licha ya mimi kuchangia hoja fulani au kuiunga mkono ,lakini walionesha hawapendi kunishirikisha lolote lile. mwanaume nikajisemea mdomo koma.
Nikatulia tuli.

Tulifika ndani ya Yard ndogo vilipo vifaa kisha nikashuka huku mlinzi fulani mzee wa makamo akitupokea kwa shangwe na upendo alikuwa mkarimu mzee wa watu.

Lakini jamaa nilishangaa hawashuki kwenye gari licha ya kuwa tumefika halafu nilielekezwa kuwa wale ndiyo wakunipa muongozo,wanioneshe which is,what is , that is......hakika nilishangaa sana mbona sioneshwi
chochote?

Dah ,my God, Please help me mbona hii kazi ni ngumu?
Nawezaje kufanya kazi na watu nisioelewana nao?
Huu si mwanzo wa kufanyiana Majungu na fitina?
Halafu mtu humfahamu unawezaje kumchukia,ama kweli Duniani kuna watu na viatu . nilijiwazia sana huku nikijihurumia .

Nilichukua simu kisha nikampigia mama yangu,si kawaida yangu kumpigia mara kwa mara tena kwa muda unaokaribiana kwani ni jana tu tulitoka kuongea ila nilijikuta tu napiga simu .

Haloo Dani hujambo mwanangu,vipi hamjambo wote?ilikuwa ni sauti ya mama yangu kipenzi.

Mimi mzima mama na kuhusu familia natumai ni wazima wa afya,na mimi nipo mkoa wa (nikitaja jina)
Nimefika tangu jana.nilimjibu kwa sauti ya chini.

Heeeeee Daniiii vipi tena upo huko tena,vipi utokako ni kwema? Maana ulivyo na mikosi mwananguuu sihitaji kusikia habari isiyokuwa nzuri.
Mama aliongea akionesha ni mwenye presha.

Usijali mama yangu ni kawaida tu mimi nimekuja huku kama sehemu ya mgawanyo wa majukumu tu ila nipo kulekule makao makuu (headquarterz) nilimjibu.

Haya nakutakia majukumu mema yenye mafanikio mwanangu kila ufanyalo kumbuka kumtanguliza Mungu.alijibu shortcut bimkubwa huku tukiagana.

Nilifurahi sana kuongea na mama na haswa sentensi yake ya mwisho ilinipa nguvu na faraja,
Nilikuwa Daniel mpya kabisa mwenye kujiamini .

Oyaaa babu eeh unafika saiti halafu unaongea na simu tu inakuwaje?
Tena inaonesha ni simu binafsi .
Hata huulizi kuwa unaanzia wapi unamalizia wapi, kipi kifanyiwe kazi, upo tu lakini tambua hii ni kazi ya serikali,inatakiwa umakini na wepesi sasa kama kila kitu tutakuwa mpaka tuambizaneeeeeee....napata mashaka hapa kazi tu , hakuna lelemama.aliongea jamaa fulani ambaye alikuwa anaendesha gari huku akimtazama mwenzake huku wakibinua midomo ile ya kukosa imani.

Nilitambua hila zao,ila nilinyamaza haiwezekani wao wanalaumu badala ya mimi niwalaumu wao .
(Mpaka leo niliwachukia sana wale wajuba)

Walinionesha kazi za kufanya huku wakinikabidhi vijana ambao tuliwakuta pale kisha wakaondoka huku wakidai ndani ya masaa mawili wangerudi.

Kidume hata njaa sikuisikia,
Sikuwa na hamu ya breakfast niliingia mzigoni nikaivaa ile kazi,
Nikaisambaratisha D9 na kuichinja tena, nawashukuru vijana niliokabidhiwa walionesha ushirikiano mkubwa na letu likawa moja ,lugha za matusi ,uhuni mwingi
Huku tukitaniana kama vile tunajuana siku nyingi kulifanya nizidi kuwa na amani mahali pale.

Licha ya majamaa kurudi na kunichukua ili nikapate lunch lakini niligoma huku nikila pamoja na wale vijana wangu,maisha ni haya haya, hayahitaji matabaka na uboss usio na maana, wahenga walisema
Ukienda Roma basi ishi kama waroma.

Hata wao walishangaa namna ambavyo nachangamana nao bila kuwabagua lakini Daniel nimeishi maisha yote ya uswahilini na huwa naishi kulingana na mazingira yanavyonitaka.

Kila siku jioni nilikuwa nakutana na yule mwenyeji wangu ambaye huwezi amini nilichukua muda hata kulijua jina lake , tulikuwa tunaongea huku akinipa moyo na kunifariji mno.huku nikimueleza kuwa wale wasimamizi siwasomi,akadai ndiyo tabia zao haswa kwakuwa ni mafundi kama mimi ila huwa hawaaminiki,hivyo kila fundi akija huwa lazima akutane na changamoto ya wakuda wale.

Wale wasikusumbue wao kazi iliwashinda na hawaeleweki wapo kwenye vitengo gani ,mpaka unakuja wewe ni kwamba si bora hivyo nakuombea kwa Mungu uweze kufanikiwa maana jamaa huwa nahisi ni wachawi wale.alifafanua mwenyeji wangu niliyemsikia akiitwa Medi na baadhi ya watu.

Lakini Daniel tangu ufike kuna vitu nashangaa hujaulizia,ni vitu muhimu japo siyo vya lazima.aliongea huku akitabasamu yule Medi.

Kama vitu gani hivyo maana ningekuwa na shida navyo ningeuliza
Hebu nisaidie kutaja... niliuliza.

Hujaulizia baa wala sehemu ya starehe, nikasema hataki tukale vyombo na nyama choma ama nini,
Nikawaza pengine ni mtumishi wa Mungu.lakini nikashangaa hujaulizia nyumba za ibada pia,upo kundi gani?
aliuliza kiutani.

Hebu twende baa yeyote nzuri kisha nitakujibu maswali yako nikitulia huko . nilimjibu huku akicheka na kudai tayari majibu kashapata

Baada ya muda mfupi tulikuwa kwenye pub moja tukiwachangia wenye pub zao huku tukichangia pato la serikali na jamaa yangu Medi huku nikiwa huru maana siku zote nilijibana sana.
Lakini baada ya muda fulani niliwaona wale wasimamizi wangu wakiingia huku wanikodolea macho kwa mshangao.

Jifunze,
Elimika,
Burudika.

Loading..................
 
SEHEMU YA HAMSINI

Walitafuta meza wakakaa Kisha wakamuita jamaa fulani ambaye nadhani ndiye alikuwa meneja wa pale, waliongea naye kama dakika kumi na tano hivi Kisha wakatoka huku wakinitazama Mimi hadi wanapotelea,

Kengele ya hatari ililia huku nikijua napelelezwa ama nafuatiliwa , nikajikuta hata yule mwenyeji wangu ambaye alinipokea kwa mara ya kwanza huenda lao Moja ila wanajifanya kama wapo tofauti lengo tu huenda wananipeleleza hivyo nikaongeza umakini ila baada ya muda kadri alivyokuwa anakata maji yule Medi nikatambua huyu ni mlevi tu Wala hayupo na wale

Nilipiga maji sawasawa siku hiyo haswa ukizingatia nina zaidi ya miezi kadhaa sikugusa kilevi,
Piga maji haswa kama nilipania
na baada ya kukuta mimi na mwanangu Medi tunaongea
Broken English zaidi kuliko kiswahili nikaona ni muda wa kuagana ili tuondoke, na ikawa hivyo huku nikichukua usafiri maarufu kama bodaboda nirudishwe napokaa

Asubuhi niliwakuta saiti wale jamaa huku wakiwa wamechangamka fulani hivi yaani ile kumchangamkia mtu kinafiki . tulisalimiana

Sasa Dani ee au leo upumzike tu maana pengine utakuwa haupo sawa maana Jana Kuna sehemu tulikuona tulishangaa hata hujatupungia mkono tunywe soda? aliongea mmoja wapo.

Nipumzike?
Ili iweje na nyinyi ni kama akina nani Hadi mniambie hivyo, Mimi waajiri wangu ndiyo walionituma hii kazi na ndiyo nitakaowapa mrejesho wa kile walichonituma, ndiyo wenye mamlaka ya kusema nipumzike, sasa siwaelewi. Niliuliza kwa sauti yenye ukali kidogo

Hapana kaka sisi tumeshauri tu kuwa kwa hali tuliyokuona nayo jana ni vema ungepumzika hii kazi ni yako na siku zipo nyingi, hivyo kwakuwa ni kazi inahitaji utimamu tukaona kwa leo ungepumzika tu.
waliongea kwa sauti ya upole haswa baada ya kuona Mimi nakuja juu.

Sikilizeni, siku zote mtu asiye kunywa pombe huwaona au kuwachukulia watu wote ni walevi, na huwa mnashindwa kutofautisha Kati ya mtu mnywaji na mlevi, Sasa tambueni kuwa Mimi ni mnywaji wa pombe na si mlevi.

Nayajua majukumu yangu, natambua Nini kimenileta huku na nitakabidhi kazi kwa muda niliopangiwa kama ambavyo nimeaminika na walionituma,
Sidhani kama Kuna haja ya nyinyi kuweza kunishauri chochote kile. Na nawaombeni tuheshimiane, na kuwe na mipaka baina yetu sihitaji maneno wala ushauri usiozingatia nidhamu.
niliongea kwa jazba na Kwa kujiamini.

Waliondoka huku wakiwa na aibu kwanza hawakuwahi kufikiri kama ningewatolea shombo, na nilifanya makusudi maana walizidisha dharau .

Nilitoka na kwenda kutafuta mchemsho ili kutoa hangover maana ukweli niliamka nazo siku ile nikiwa kwenye mgahawa ulioonekana si wa siku nyingi huku watu wenye nafuu kipesa wakipata vifungua kinywa pale nilitulia , kwenye kiti huku hata mchemsho wenyewe ukinishinda.

Mmmh pombe hizi halafu nimeleta ukali tu lakini wale jamaa wamegundua kuwa sipo vizuri,

Ila si mbaya , jitihada za unachokifanya huwa hazionekani hata utumie nguvu kiasi gani huwezi kuwaaminisha watu, Bali ni matokeo ya kile ulichofanya,
Results matters only .
Hata ukilima ekari mia kama kipato chako ni gunia moja tu basi huna ulichokifanya.

Nitahakikisha kila kitu kipo sawa na wale wambea walitaka niwakubalie eti nipumzike kwa amri yao ili waanze kusema mtu mwenyewe hafanyi kazi analewa tu ,never haiwezekani kwanza sihitaji mazoea nao kabisa.nilijiwazia.

Nilirudi kisha tukaendelea na kazi na vijana wangu huku nikigundua ile rangi yangu niliyowaonesha kuwa ni mkali, nikagundua design fulani wananiogopa lakini nilianza kuwatania huku kazi zikienda hata chakula cha mchana tukawa tunapiga pale pale ili wasiniogope.

Naam,
baada ya siku kumi na moja niliwapigia simu maboss zangu na kuwaambia kuwa kazi imekamilika,nikaambiwa nisubiri wawasiliane na watu wa kule niliko,kisha nikaambiwa nitabaki zaidi ya wiki mbili ili nijiridhishe juu ya utendaji wa kazi wa vitu nilivyorekebisha.

Hii ilinipa unyonge sana nilikosa raha,
Haya mambo gani tena?
Mbona sehemu nyingine unatengeneza chombo unakabidhi kisha unafuatwa na kurudi,leo imekuwaje,yaani nianze kwenda saiti tena na mimi ,ama kweli hii kazi huenda inataka kunitoka ,naona watu wananitafutia kila aina ya makosa ili tu nifukuzwe kazi.nilijiwazia moyoni.

Baada ya siku mbili vyombo viliingia site huku mimi nikienda na kwa bahati nzuri siku ya kwanza iliisha hakuna kifaa kilizingua ikawa karibu Kila siku naenda ili kusikilizia muungurumo tu, chombo gani hakipo sawa ili nitimize azma niliyoambiwa.

Siku moja nikiwa kwenye mti fulani nachezea simu Kuna gari ya maliasili land rover ilikuwa inakuja huku ikichepuka kuingia kwenye Diversion iliyotengenezwa mahususi kwa muda ili kupisha matengenezo ya kipande cha barabara kuu.

Nikiwa sina hili wala lile kwani niliona ni gari tu kama gari zingine sikuwa na time nayo ila ilisimama karibu na Mimi huku nikisikia naitwa kwa sauti ya kike
Daniiiiii huku anayeita akifungua mlango na kushuka .

Naam, ilikuwa ni sura ya mtu ninayemfahamu si mwingine alikuwa ni Fatma au Fetty mke wa afande mmoja wa jeshi la polisi aitwaye Hussein.

Tulisalimiana huku moyo ukinidunda kwa kukataa kitu, sikujua moyo wangu unakataa Nini wallah,

Daniel unafanya nini hapa, wewe ni mkandarasi? ni nani labda ningependa nijue na unakumbuka siku zile ulinificha kabisa kazi yako?
aliuliza kwa sauti yake ya kike nzuri.

Nipo, ni Harakati za maisha tu, nipo nasaka vibarua dada yangu. Nilimjibu kifupi huku nikimtazama mwanamke ambaye alivaa sare zilizoiva huku ile kofia yao ya duara aliyovalia pembeni ikimpendeza sana .Kwa mara ya kwanza nilimuona Fatma akiwa kwenye mavazi ya kazi yake.

Dah basi sawa karibu kwenye Mkoa wetu ndugu , na hii ndiyo wilaya yetu. Aliongea kwa madaha huku vijana maaskari waliokuwa nyuma ya ile gari wakinitazama sana .

Kwani unatoka wapi dada yangu. Niliuliza.

Aaaaa unajua huku upo karibu sana na hifadhi , na geti letu halipo mbali sana ni kilomita chache tu kutoka hapa, na Mimi mwenzio nimepanda cheo(huku akicheka)hivyo sikai Tena kota za kule nakaa hapo center, karibu sana . alifafanua huku nikimtazama mabegani akiwa
Mashallah ni afisa mkubwa tu kiasi chake nikampa hongera zake huku nimeduwaa.

Mwanamke mzuri ambaye alidai ana mtoto mmoja tu, akiwa hataki kuzaa tena kwaajili ya kuwa bize kulitumikia taifa. Kweli afande Hussein alikuwa sahihi kuwa na wivu

Mwanamke English figure, weupe wa asili akiwa na tumbo zuri flat
(Siyo Hawa vitumbo mchongoma)
sauti tamu, sura tamu yaani mtamu nilitamani utamu wake, lakini moyo ulikuwa unakataa akili zangu ndogo zenye kusahau jambo haraka zilitaka ila Sasa moyo haukutaka kabisa.

Naona Dani Mimi nikuache tutawasiliana,sema nipe namba zako maana sina ni Mr alifuta kipindi kile.
aliongea kwa sauti tamu huku nikishindwa Cha kufanya.

Je nitatoa namba Mimi Daniel kweli?

Ni huyu mwanamke ambaye mumewe alidhani nimetembea naye kiasi cha Mimi kuwekewa mtego, mganga aliniambia kuwa ndiye chanzo cha matatizo yangu.

Ni Fatma huyu ambaye kamsababishia matatizo jamaa yangu Jastini, huku Mimi mwenyewe nikiponea kwenye tundu la sindano.Leo nimpe namba?

Kumbuka Daniel napenda wanawake wazuri bwana, maisha yanahitaji vitu vizuri tafuta pesa,tumia pesa , nimezaliwa, naishi , nitakufa.
Hapa katikati kwenye kuishi lazima nile maisha.
Mimi ni mwanaume, sijazaliwa ili nije kushangaa. Sasa itakuwaje nitatoa namba?

Weekend njema wadau wangu.

Jifunze,
Elimika,
Burudika.

Itaendelea.................................
 
Jamani Samson kila siku misala mipya haukomi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…