SEHEMU YA 66
Kwa upande wa Salome ilikuwa furaha sana kwake na alijikuta akigundua siri nyingi sana za Rose maana muda wote Rose alijua anayejibishana nae kwenye ujumbe mfupi ni Ashura kumbe kuna mtu mwingine, na huyo ashura mwenyewe ni marahemu wa muda mrefu sana.
Salome alikuwa ameingia na chakula chumbani na alikuwa anakula humo, mara Sara alienda kumgongea na kuingia ila alipomkuta anakula chumbani alishtuka sana, ikabidi Salome amuulize ameshtuka kwasababu ipi,
“Hapa nyumbani hakuna mtu anayeruhusiwa kula chakula chumbani”
“Mmmh kwanini?”
“Sijui ni kwanini ila mama anakataa kabisa mtu kula chakula chumbani”
“Hujui sababu kweli! Labda ungesema mama anaogopa panya watazaliana au mende watajaa. Ila ni leo tu haitajirudia kula chakula chumbani”
“Na kwanini umechagua kulala chumba hiki?”
“Sababu hiki ni chumba alichokuwa analala mpendwa wangu Moza, namkumbuka sana ndiomana nimekuja kulala hapa”
“Ila unafikiri Moza tulimzika! Alitoweka kimiujiza”
“Alitoweka!”
“Ndio alitoweka, yani kuna binti alitumbukia kwenye kaburi walipompeleka hospitali basin a mwili wa Moza ulipotea”
“Maskini Moza wangu, kwahiyo hakuna kaburi la Moza!”
“Ndio hakuna”
“Kwa staili hiyo inamaana basi Moza hakufa, labda kwa mfano hakufa!”
“Mmmh usiongee habari hizo, mimi ni muoga nitashindwa kulala hapa usiku”
“Basi usijali”
“Ila huku ndani kuwa nako makini sana, ulisaidia macho yangu yakaona tena na mdomo wangu ukaweza kuongea ila chakula nilichopika siku ile kuna kilichopotea na sijui kimeenda wapi. Kuwa makini sana na humu ndani kuna mambo ya ajabu sana”
“Usijali, nipo makini sana”
Sara alijikuta akimpenda sana huyu Salome yani alimpenda sana kutokana na jinsi alivyomsaidia matatizo yake ya kurogwa na mdogo wake. Walipomaliza maongezi, Sara akamuomba Salome waende nae sebleni ambapo alifanya hivyo na pale sebleni walikuwepo wale mapacha na mr.Patrick ambae toka amerudi hakwenda kabisa chumbani kwa mke wake. Baada ya kimya kirefu pale sebleni, Salome akaanza kusema,
“Hata hamniulizi jamani kuwa nimejuaje kama huyu baba ni baba yangu”
Pacha mmoja akadakia,
“Eeh tuambie umejuaje!”
“Unajua mimi nimeishi bila kumjua baba kwa miaka yote hii mpaka sasa nilikuwa kidato cha tatu ila baba yangu simjui. Alipotokea msamalia mwema na kuniambia kuwa huyu ni baba yangu nilifurahi sana ndiomana sikutaka hata kupoteza muda zaidi ya kuja hapa ili nifurahi na ndugu zangu wengine. Jamani ndugu zangu, mimi ni ndugu yenu ni mtoto wa Mr.Patrick kama mlivyo nyie”
Mmoja akahamaki,
“Wewe si ulituambia pale kuwa wewe ndiye mtoto wa pekee wa mzee Patrick, haya saivi unasema na sisi ni watoto wa huyu mzee. Hapana, sisi ni watoto wake wa kambo. Labda Ana sijui”
Sara akadakia,
“Ana nae ana baba yake mwingine, ni hakika kabisa wewe Salome ndiye mtoto wa pekee wa baba”
Mama yao akiwa ameambatana na Ana walitoka chumbani na waliisikia vilivyo kauli ya Sara na iliwakera sana. Rose kabla ya kukaa alianza kwa kumuuliza Sara,
“Hivi wewe Sara una nini wewe? Kitu gani kinakuwasha mdomoni kwako?”
Kisha Rose alikaa na kumuangalia Salome na kusema,
“Haya na wewe nani kakukaribisha kwenye nyumba hii?”
“Nimekuja kwa baba yangu”
Salome alijibu kwa kujiamini kabisa.
“Sikuelewi”
“Mamdogo Ashura kaniambia kuwa hapa ni kwa babangu, hata ameshakwambia kuwa nakuja hapa”
“Kwahiyo hapa kwangu unalala chumba gani sasa?”
“Kile chumba alichokuwa analala dada Moza”
Rose akamuangalia mume wake na kumwambia waelekee chumbani ana mazungumzo nae, kwahiyo sebleni walibaki watoto tu. Ambapo Ana alimuangalia Salome na kumwambia,
“Utaondoka kama ulivyokuja, hakuna anayekutambua hapa. Ndiomana unalala chumba cha marehemu”
Kisha akaenda zake chumbani kwake, ila Sara alimuangalia Salome na kumwambia,
“Hata usijali, nitakuwa na wewe bega kwa bega”
Wale mapacha wakainuka na kwenda chumbani kwao ila Sara aliinuka na Salome na kumkaribisha Salome kwenye chumba chake,
“Humu ni chumbani kwangu Salome, muda wowote unaruhusiwa kuingia. Ukiwa na shida ya kitu chochote unaruhusiwa kuja kuchukua”
“Asante dada”
“Nimefurahi sana kupata mdogo mwenye upendo kama wewe, kwanza umeniponya macho yangu na mdomo wangu. Halafu ngoja nikuhadithie kitu bhana”
Basi Sara akaanza kumueleza Salome jinsi Ana alivyokuwa akishangaa mwalimu wake amepona kimiujiza,
“Niambie Salome, ni wewe uliyemsaidia Yule mwalimu”
Salome akacheka kidogo,
“Hapana bhana si mimi ila nimefurahi kusikia kuna mtu alifanyiwa hivyo na amepona pia”
“Mmh si wewe kweli! Sasa mimi ulijuaje kama naumwa?”
“Nilioteshwa na nilioteshwa dawa za kuja kukupa ndiomana nimekwambia hawatakusumbua tena”
“Ila mimi nimefurahi sana umekuja kuishi hapa, naomba uishi hapa milele yote”
Salome akacheka tu na kufurahi pale na Sara kisha usiku ulipoingia alimuaga na kwenda kulala kwani nyumba hiyo huwa chakula kinakuwa mezani na mwenye njaa anaenda kula mezani na kama siku hiyo hakijapikwa basi kila mmoja anajijua mwenyewe.