SEHEMU YA 132
Nyumbani kwa Neema, siku hiyo alishangaa asubuhi asubuhi binti yake amepika na kuondoka halafu muda kidogo akarudi,
“Kheee ulienda wapi Salome?”
“Kaka yangu amelazwa”
“Kaka yako!”
“Ndio, mtoto wa Yule mama wa kule mke wa baba”
“Kheee anaumwa nini tena”
“Eti aliungua na maji ya moto”
“Basin a mimi tutaenda wote kumuona mchana”
Salome alimkubalia mama yake kuwa mchana wa siku hiyo ataenda nae kumuona hospitali, huku akionekana kushughulikia chakula cha mgonjwa. Yani Salome alikuwa akifanya vitu ambavyo alijua badae vitaleta majibu gani.
Wakina Sara walienda hadi kwa Yule mganga ambaye walimuacha mama yao na walikuta bado mama yao akiwa ndani ya kile kibanda cha mganga kumbe kulipokucha bado mganga aligoma kumuhudumia kwahiyo alikuwa akimbembeleza, ilibidi watoto wake wamsubiri tu.
Rose aliendelea kumuomba Yule mganga amsaidie,
“Sasa wewe mganga unavyokataa hivyo, mimi atanisaidia nani? Maji yamenifika shingoni sasa”
“Sijui nani atakusaidia kwakweli ila mimi siwezi, maisha yangu nayapenda sana. Watoto wangu bado wadogo, wengine wananitegemea kwakila kitu, sipo tayari kuwaacha. Nilikuwa nakupa moyo tu jana ila kukusaidia siwezi”
“Inamaana na wewe unamuogopa huyo anayetutisha kwenye nyumba yetu!”
“Wewe Rose una dawa nyingi sana, fanya dawa zako na wewe kuweza kutokomeza hali hiyo”
“Ni kweli nina dawa nyingi lakini sijui jinsi ya kuzitumia”
“Na mimi siwezi kukwambia namna ya kufanya na siwezi kukusaidia kwakweli, labda uende kwa waganga wengine”
Rose alitumia muda mrefu sana kumshawishi huyu mganga ila jitihada zake ziligonga mwamba, ikabidi aanze kumfikiria mganga mwingine wakati akili yake imepata jibu juu ya mganga mwingine wa kwenda akaamua kufanya hivyo, ndipo alipotaka kutoka kwa mganga Yule ila alishangaa Yule mganga akimzuia na kumwambia kuwa atamsaidia, Rose alifurahi na kukaa chini ili kusikiliza Yule mganga atamsaidiaje, kisha Yule mganga akaanza kupiga tunguli zake, na alipomaliza akaanza kuongea nae,
“Kwanza kabisa, Yule mtoto wako ambaye kaungua na maji ya moto hamtakiwi kumpeleka hospitali”
“Mmmh mganga sijui kama watoto wangu watarudi tena hapa, kumbuka usiku sikuwaona au bado wapo nje?”
“Sijui ila hutakiwi kumpeleka hospitali”
“Basi ngoja nijaribu tena kuwatafuta”
Rose alitoka mule kwa mganga huku akiwa na mawazo sana kuwa watoto wake walielekea wapi ila alishangaa kufika nje, kuona gari yake na watoto wake ndani ya gari na ilionyesha wazi walikuja kumfata mama yao. Alijiuliza kuwa mbona usiku wa jana hakuwaona, kwamaana hiyo waliondoka au imekuwaje hapo, hakupata jibu kabisa. Aliwafata na kuwauliza kulikoni mbona usiku wa jana hakuwaona alipotoka kwa mganga, Sara alikuwa wa kwanza kumjibu mama yao,
“Mama tumekuja kukufata wewe, Doto kalazwa hospitali twende ukamuone”
“Kwahiyo Doto mmempeleka hospiatali?”
“Ndio mama”
“Nyie watoto jamani mbona mnanitafutia ubaya!”
“Ubaya upi mama? Doto yupo hospitali na tungemchelewesha tu tungemkosa, naomba twende mama”
Rose alikuwa ameduwaa tu nje huku akiwa hajielewi kuwa afanye kitu gani, Kulwa alishuka kwenye gari na kumpakia mama yao kinguvu kisha akapanda kwenye gari na kuondoa gari hiyo. Rose alikuwa kimya tu kwani bado alikuwa akitafakari bila ya jibu, mganga kamwambia kuwa mtoto wake asipelekwe hospitali na huku washampeleka hospitali kwahiyo hata akienda kumbembeleza tena mganga ni kazi bure kwa wakati huo. Ikabidi atulie tu kwenye lile gari, na alijiuliza tena kuwa mganga alikuwa na maana gani kuwa mtoto wake asipelekwe hospitali! Bado hakuwa na jibu, hadi wanafika hospitali ilikuwa ni mchana tayari, ila walipofika walizuiliwa na kuambiwa kuwa muda wa kuona wagonjwa umeisha, ikabidi Sara aulize
“Jamani mbona asubuhi mlituruhusu wakati muda ulikuwa umeisha?”
“Asubuhi aliyewaruhusu aliwaruhusu kimakosa, njooni jioni ndio muda uko wazi”
“Sasa mgonjwa wetu hajala”
“Ameshakula, kuna ndugu yenu kashampa chakula. Atatoka muda sio mrefu”
Yule nesi alisogea kidogo, na muda sio mrefu wakamuona Salome akiwa ameongozana na mwanamke mmoja, Rose alipomuangalia vizuri Yule mwanamke aligundua ni Neema ambaye ni mama yake na Salome.
Salome na mama yake hata hawakuangalia upande, walikuwa wanaondoka tu ila Rose alimuita Neema,
“Neema”
Neema akageuka na kumuona kuwa ni Rose, uoga ukamshika kwani bado alikuwa anamuogopa Rose vilivyo, ila Rose alimsogelea Neema na leo kwa mara ya kwanza alimsalimia vizuri kabisa,
“Hujambo Neema”
“Sijambo shikamoo”
“Mbona unaniogopa hivyo!”
Salome akadakia,
“Anakuogopa sababu umezoea kumtishia”
Neema alimkatisha mwanae kuwa asiendelee kuongea maneno hayo, Rose alimwambia Neema
“Sina ugomvi na wewe na nimefurahi kukuona. Natumai umetoka kumuona mwanangu, mwanao pia nimempokea vizuri kwenye nyumba yangu ila mwanao ni mshirikina”
Neema akashtuka
“Mshirikina!”
Salome akacheka sana, kisha akamshika mama yake mkono na kumlazimisha kuwa waondoke eneo hilo, ila Neema alikuwa mbishi kufanya hivyo. Salome alimwambia mama yake,
“Mama, sijakuleta hapa kuja kubishana na huyu mtu. Halafu nina mambo mengi ya kufanya siku ya leo, tafadhali tuondoke nyumbani”
Neema alikuwa mbishi mbishi kwani bado alitaka kusikia kuwa kwanini mwanae kaitwa mshirikina ila ikabidi akubaliane tu na mwanae kuwa waondoke, ambapo salome alikodi bajaji iwapeleke nyumbani kwao ila kitendo cha Salome na mama yake kuondoka na ile bajaji, Rose alienda kuwaomba watoto zake kuwa waifate hiyo bajaji hadi wajue wanapoishi Salome na mama yake, kwahiyo walifanya hivyo na kuanza kuifatilia ile bajaji.