Simulizi: Kurudi Kwa Moza

Simulizi: Kurudi Kwa Moza

SEHEMU YA 126

Neema nae alifika usiku na familia yake yani wale watoto wake mapacha, akiwa amechoka sana ila alikuta ndani kwake kama kuna mtu na kuhisi ni Salome, kisha akagonga mlango na kweli Salome alienda kuwafungulia na kuwapokea huku akionyesha tabasamu zito sana. Neema alikaa na kuzungumza na mwanae,
“Hukuondoka kabisa nini toka siku ile?”
“Niliondoka mama”
“Sasa umejuaje kama leo ndio narudi?”
“Sikujua ila huwa narudi kila jioni, halafu nikahisi kama mnarudi vile ndiomana nikapika kabisa”
Neema alitulia tu ila huyu Salome wake wa kipindi hiki alikuwa akimshangaza sana, kwanza Salome wake ni muoga ila kaweza kulala hapo nyumbani kwa siku zote alizokuwa safarini, halafu Salome wake alikuwa mvivu ila huyu kazi zote anafanya, kama hapo kawapikia kabisa kwahiyo walienda kujimwagia maji tu na kula huku akimpa salamu Salome za kutoka kwa bibi zake na ndugu zake wengine,
“Ila wamekukumbuka, haswaaa bibi yako anaomba uende ukamsalimie”
“Nitaenda tu hata wasijali”
“Ila mwanangu umebadilika sana”
“Kwanini mama?”
“Ulikuwa mvivu sana zamani, yani kama leo ningekuta hujafanya chochote. Halafu ulikuwa muoga sana yani ningekuta umeenda kuishi kwa marafiki huko”
“Nimekuwa mama”
“Amakweli umekuwa sasa”
Aliongea ongea nae kisha akamuaga na kwenda kupumzika huku wadogo zake Salome wakiwa wamelala muda tu walipomaliza kula kutokana na uchovu wa siku hiyo. Basi Salome nae akaenda chumbani kwake, kwahiyo ilijulikana kuwa nae amelala.
 
SEHEMU YA 127


Kwenye mida ya saa tano usiku ndio Sara, Ana na Kulwa walirudi nyumbani na kumuacha Doto akiwa amelazwa hospitali, kwahiyo walifika wakiwa wamechoka sana. Mlinzi aliwauliza kuwa imekuwaje huko hospitali,
“Amelazwa, ni ameumia sana”
“Eti Salome alisema hamuendi hospitali”
Ana akauliza,
“Yeye Salome yuko wapi yani huyo msichana ni nuksi tena nuksi kabisa. Ni kweli hospitali tumeenda badae maana mwanzoni tulijikuta kwa mganga. Hivi wewe unamuonaje huyu Salome, kwanza yupo?”
“Hayupo, ametoka”
“Basi nitakuja tuongee vizuri”
Mlinzi alishangaa sana kwa Ana kuongea vizuri vile na yeye kitendo hicho kilimshangaza sana ingawa mambo ya Salome ndio yalikuwa yanamshangaza zaidi.

Waliingia ndani huku wakiamini kwa vyovyote vile mama yao amebaki kwa Yule mganga, walitamani kumuuliza Ana ila walimuogopa maana ana muda wake wa kubadilikia watu.
Ana aliwaacha ndugu zake ndani na kutoka tena kwenda kuongea na mlinzi wao.
“Hebu niambie, kwanza wewe unamuonaje huyu Salome!”
“Kwakweli sijui nisemaje ila simuelewi yani huwa simuelewi kabisa kabisa”
“Unahisi anaweza akawa ni mchawi?”
“Inawezekana maana haeleweki kabisa. Na mama mmemuacha wapi?”
“Yani habari ya mama sijui tukuelezeje ila kwa kifupi amebaki kwa mganga. Hivi mtu akitaka kuacha uchawi anafanyaje? Anaenda kwa mganga kutolewa au anafanyaje?”
“Kwa mganga ni kuuzidisha uchawi sijui sasa mtu anawezaje kuacha uchawi, unataka kumpeleka Salome?”
“Hapana, kuna jambo nataka kulifanya. Utalijua tu”
Kisha Ana akarudi tena ndani na kuwaona dada yake na kaka yake pale wakijadiliana na kukubaliana kesho wawahi hospitali kisha waende kumchukua mama yao maana hakuna aliyejua kuwa mama yao atarudije ila kitu pekee walichojua ni kuwa yupo kwa mganga wa kienyeji.
“Sasa basi tuchemshe chai tunywe tu na ile mikate tuliyonunua”
“Ndio tufanye hivyo hakuna namna”
Kwahiyo Sara akaenda kuandaa chai ili waweze kunywa.
 
SEHEMU YA 128


Mishi akiwa ndani kwao, mara alijiwa na rafiki yake ule usiku, ikabidi atoke kumsikiliza,
“Mmmh mbona usiku sana, saa sita kasoro hii!”
“Ni usiku kweli ila sijaweza kulala na habari hii”
“Habari gani?”
“Leo nilikuwa hospitali kumuona ndugu yangu, gafla nikaona kuna mgonjwa analetwa na ameungua vibaya vibaya ndio wametoka kumfunga funga mabandeji na kumpaka dawa, kila mtu kashikwa na huruma pale, ikabidi nimsogelee kumpa pole. Jamani ni Doto Yule mpenzi wako”
Mishi akashangaa sana na kumuuliza rafiki yake,
“Una uhakika ni Doto?”
“Ndio ni Doto maana nilisikia ndugu zake wakimuita Doto”
Mishi alikaa kimya kwa muda kwanza kwani tukio la Doto lilimshangaza toka muda alikuja kuongea nae, akakumbuka kuwa alienda pale kuongea nae ila alitaka kumpiga kibao na mara hakumuona huyo Doto mwenyewe halafu muda huu anapata habari kuwa Doto ameungua na maji ya moto haikumuingia akilini kabisa.
“Au Doto amekufa, aliyekuja kwangu huku ni mzimu!”
“Hapana hajafa bhana, ni mzima ila ameungua sana”
“Unajua watu kufa huwa wanachelewa chelewa kidogo, usikute amekufa anangoja tu muda wa kufa kabisa hapo”
“Kwanini unasema atakuwa amekufa?”
“Sababu Doto alikuja kuongea na mimi jioni jioni hivi na akataka kunipiga mara gafla akatoweka hata nikaogopa”
“Alitoweka?”
“Ndio alitoweka”
“Alitowekaje?”
“Hata sijui nikuelezee kwa namna gani ila alitoweka”
“Inawezekanaje mtu atoweke jamani? Mbona haiwezekani au ulikuwa unaota Mishi! Na kwanini alitaka kukupiga?”
“Hakuna kitu bhana, ila endelea kushangaa kutoweka kwake”
Mishi akainuka pale ila cha kushangaza alitokea kwenye sebule ya kina Doto, na pale sebleni alikuwepo Kulwa, Sara na Ana wakinywa chai kwahiyo nao wakapatwa na mshtuko kumuona ndani kwao.
 
SEHEMU YA 129


Mishi akainuka pale ila cha kushangaza alitokea kwenye sebule ya kina Doto, na pale sebleni alikuwepo Kulwa, Sara na Ana wakinywa chai kwahiyo nao wakapatwa na mshtuko kumuona ndani kwao.
Wakainuka wote kwa mshangao na kutaka kumfata ila Mishi akaanza kutafuta sehemu ya kutokea na bahati akauona mlango wa kutoka nje na kufungua akakimbia, wakataka wamfate maana hakuna aliyekuwa anaelewa kuwa imekuwaje vile yani kila mmoja alishikwa na uoga wa hali ya juu huku akishangaa mara gafla kabla hawajatoka nje akatokea Salome huku akicheka sana, wakajikuta wakisema kwa pamoja tena kwa mshangao,
“Salome!!”
“Ndio ni mimi, mnadhani mnaota?”
“Umekujaje kimiujiza?”
“Mbona huyo aliyeondoka hamkumuuliza kuwa amekujaje?”
Wakamuangalia Salome, kisha wakamuacha na kwenda getini ambako walimkuta Mishi ndio akiishia getini kutoka, Ana alimfata mlinzi na kumuuliza,
“Mbona umemuachia atoke?”
“Sikumuelewa na yeye pia anaonyesha hajielewi, sijamuona kuingia ila nimemuona kutoka kwakweli sikumuelewa”
“Na Salome yupo ndani”
Mlinzi alishtuka sana kusikia kuwa na Salome yupo ndani wakati hakumuona akiingia,
“Mbona sijamuona akiingia?”
“Ndio ushangao hapo, Yule msichana ni mchawi hata naogopa kulala ndani ya nyumba”
Muda kidogo Kulwa na Sara nao walitoka wakidai kuwa hawawezi kulala ndani ya nyumba yao maana Salome hakuwa mtu wa kawaida, basi wakakubaliana kuwa watoke nje hata waende wakakodi hoteli ya karibu na kulala huko, mlinzi alitamani pia kuondoka ila alihofia kazi yake huku akiwa na mashaka sana, aliwashuhudia tu wakipanda kwenye gari na kutoa gari nje kisha kuondoka zao.
Mlinzi alikuwa na mashaka sana ila Salome alimfata Yule mlinzi pale getini na kumwambia,
“Umefanya jambo jema sana kutokufatana nao”
“Ila naogopa pia, hivi wewe Salome ni mtu wa kawaida kweli?”
“Kwanini mimi nisiwe mtu wa kawaida?”
“Sijakuona ukiingia ila gafla nakuona ukitokea ndani”
“Yani hiyo tu ndio inafanya mimi nisionekane mtu wa kawaida? Mbona Yule msichana pia hukumuona akiingia na umemuona akitoka, je nae ni mchawi? Ila usiogope sana, hata mimi natoka siwezi kuendelea kulala humu ndani peke yangu”
“Unaogopa?”
“Ndio naogopa pia, mimi ni mtu wa kawaida kwahiyo kitu cha ajabu kama hivi kikitokea lazima niogope”
Salome alitoka na kumuacha Yule mlinzi pale getini, kwakweli aliogopa sana huku akiangalia ile nyumba kwa uoga ila alijipa moyo sababu yuko nje kwahiyo alihisi lolote baya likitokea basi atakimbia.
 
SEHEMU YA 130


Mishi alikuwa na uoga wa hali ya juu maana hakudhania kama ingetokea muda angerudishwa kimaajabu kwakina Doto, kwakweli alichanganyikiwa sana. Njiani aliona vijana watatu alianza kukimbia huku akipiga kelele kwani alijua ni lazima angebakwa tu, ila wakati anakaribia nyumbani kwao walitokea vijana wengine na kumpiga teke kisha kuanza kumbaka, Mishi alipiga kelele sana na watu walijitokeza kumsaidia kisha wale vijana wakakimbia, wale waliomsaidia Mishi walikuwa ni ndugu zake, na walimrudisha nyumbani huku wakimpa pole na kumuonea huruma sana, mama yake alikaa karibu na binti yake chumbani kumpa moyo,
“Yani mwanangu tulikumbwa na uoga wa hali ya juu ndiomana wote tulikuwa macho tukikutafuta, maana mwenzio alivyosema umetoweka kila mmoja alishikwa na mashaka hapa. Ilikuwaje mwanangu?”
“Hata sielewi mama”
“Ulitowekaje?”
“Hata sielewi mama”
“Haya ni maajabu sana mwanangu, sijui hata tufanye nini yani hadi naogopa. Hapa naogopa hata kulala”
“Sio wewe tu mama, hata mimi mwenyewe naogopa hata kulala”
“Ndugu zako wote hapo nje wapo kwaajili wamepata habari ya kutoweka kwako, wale mafirauni waliokuwa wanakufanyia kitendo cha kikatili hatujawapata mwanangu, yani tutawatafuta popote pale”
“Mnadhani mtawapata mama? Hata msijisumbnue, kesho nitakupeleka mahali nilipopewa hii laana”
“Laana! Umepewa laana kivipio mwanangu?”
“Mama, ni aibu hata kusema ila nimepewa laana na binti mdogo kabisa yani nadhani yote haya yanatokea kwa laana yake. Mama nipo tayari kuolewa na mzee Juma”
“Kheeee upo tayari kuolewa tena?”
“Ndio, bora niwe mke wa mtu labda itapotea hii laana. Naomba niolewe mama”
“Sasa mwanangu mbona gafla sana, na kwa huyo mtu tutaenda saa ngapi?”
“Tutaenda kesho, lakini baada ya mimi kuolewa. Naomba ukaongee na mzee Juma kesho asubuhi mwambie nipo tayari kuolewa nae, iwe kesho, tufunge ndoa hata ya fasta ila niolewe tu mama”
Mamake Mishi alimshangaa sana binti yake kwa maamuzi hayo ila kwavile hakujua ni kitu gani kilimsumbua binti yake huyo, ikabidi tu akubaliane nae kwani hata yeye tukio la binti yake kutoweka lilimshtua sana.
 
SEHEMU YA 131


Sara, Kulwa na Ana walifika kwenye hoteli moja ndogo kisha kulipia vyumba vitatu vya kulala kwani Ana na Sara bado ilikuwa haiivi kulala kwenye chumba kimoja, kwahiyo kila mmoja aliingia kwenye chumba chake kisha wakakubaliana kuwa asubuhi waamshane mapema ili wawahi kurudi nyumbani na waandae chakula cha kumpelekea mgonjwa.
Cha kushangaza walipoamka kila mmoja alijikuta kwenye chumba chake nyumbani kwao, kwahiyo kila mmoja alikuwa na mshangao peke yake kuwa imekuwaje tena. Sara aliinuka na kuangalia vizuri, alikumbuka fika kuwa mara ya mwisho alilala kwenye chumba cah hoteli sasa imekuwaje kujikuta wamelala ndani kwao? Alikuwa na mashaka sana, akaamua kutoka nje na kwenda sebleni, ni kweli ilikuwa ni ndani kwao, muda kidogo alimuona Kulwa akitoka na Ana akitoka na wote wakiwa na mshangao huku wakiulizana,
“Jamani imekuwaje?”
“Labda tukuulize Ana imekuwaje!”
Sara alisema hivyo ila hiyo kauli ilimkera Ana kwani ilionyesha wazi kuwa yeye ana nguvu za ajabu na ndio amefanya hivyo kwao, ila Ana aliwajibu kawaida tu
“Jamani, mimi na nyie tulikuwa eneo moja kwahiyo swala la kuniuliza kuwa imekuwaje hata mimi sijui. Cha muhimu tumesharudi nyumbani basi tukamuandalie chakula kaka na tumpelekee hospitali”
Ikabidi wakubaliane kufanya hivyo ingawa hawakujua kuwa ni chakula gani wataenda kumpelekea hospitali kwa wakati huo, na wakaona kuandaa itawachukua muda mrefu kwahiyo wakajadiliana kuwa waende tu hospiatali kisha wataenda kumnunulia chakula huko huko. Ikabidi waende kujiandaa tu muda huo, kila mtu alijiandaa upesi upesi kwani kila mtu alikuwa na mashaka kupita maelezo ya kawaida, na walipomaliza walitoka nje, walipofika getini mlinzi alishtuka sana na kuwauliza
“Mmeingiaje humu ndani?”
Hawakumjibu kitu kwani hata cha kumjibu kingekuwa ni kitu gani, ila mlinzi aliendelea kusema
“Kwa stahili hii sidhani kama kuna umuhimu wa mimi kuendelea kulinda hapa, ikiwa watu wanavyoingia ndani siwaoni ila nawaona wakati wa kutoka tu”
Wakina Sara hawakumjibu zaidi ya kumsalimia tu, kisha wakatoa gari na kuondoka zao.
Walivyofika hospitali walimkuta ndugu yao akiwa anaendelea afadhali kidogo kisha wakamuuliza chakula cha kumletea,
“Hapana msihangaike, Salome alikuja hapa saa kumi na mbili na kaniletea mtori. Kaninywesha hadi nimeshiba kabisa, Yule binti ana moyo wa huruma sana”
Ana akadakia,
“Ana moyo wa huruma wakati ndio chanzo cha kuungua kwako”
“Ana nyamaza usitake niongee sana, yeye ni chanzo wakati chanzo ni wewe na mama, si wewe na mama ndio mmenimwagia maji ya moto! Unafikiri sikumbuki eeh! Nakumbuka vizuri, ni nyie ndio mmefanya niteseke hivi”
“Mmmh basi yaishe, cha muhimu upone tu na uendelee salama”
Wakaongea ongea nae pale na kumuaga kuwa wataenda tena mchana kumuona, naye aliwaitikia kisha wakaondoka na kuanza safari ya kumfata mama yao ambaye walimuacha kule kwa mganga.
 
SEHEMU YA 132


Nyumbani kwa Neema, siku hiyo alishangaa asubuhi asubuhi binti yake amepika na kuondoka halafu muda kidogo akarudi,
“Kheee ulienda wapi Salome?”
“Kaka yangu amelazwa”
“Kaka yako!”
“Ndio, mtoto wa Yule mama wa kule mke wa baba”
“Kheee anaumwa nini tena”
“Eti aliungua na maji ya moto”
“Basin a mimi tutaenda wote kumuona mchana”
Salome alimkubalia mama yake kuwa mchana wa siku hiyo ataenda nae kumuona hospitali, huku akionekana kushughulikia chakula cha mgonjwa. Yani Salome alikuwa akifanya vitu ambavyo alijua badae vitaleta majibu gani.

Wakina Sara walienda hadi kwa Yule mganga ambaye walimuacha mama yao na walikuta bado mama yao akiwa ndani ya kile kibanda cha mganga kumbe kulipokucha bado mganga aligoma kumuhudumia kwahiyo alikuwa akimbembeleza, ilibidi watoto wake wamsubiri tu.
Rose aliendelea kumuomba Yule mganga amsaidie,
“Sasa wewe mganga unavyokataa hivyo, mimi atanisaidia nani? Maji yamenifika shingoni sasa”
“Sijui nani atakusaidia kwakweli ila mimi siwezi, maisha yangu nayapenda sana. Watoto wangu bado wadogo, wengine wananitegemea kwakila kitu, sipo tayari kuwaacha. Nilikuwa nakupa moyo tu jana ila kukusaidia siwezi”
“Inamaana na wewe unamuogopa huyo anayetutisha kwenye nyumba yetu!”
“Wewe Rose una dawa nyingi sana, fanya dawa zako na wewe kuweza kutokomeza hali hiyo”
“Ni kweli nina dawa nyingi lakini sijui jinsi ya kuzitumia”
“Na mimi siwezi kukwambia namna ya kufanya na siwezi kukusaidia kwakweli, labda uende kwa waganga wengine”
Rose alitumia muda mrefu sana kumshawishi huyu mganga ila jitihada zake ziligonga mwamba, ikabidi aanze kumfikiria mganga mwingine wakati akili yake imepata jibu juu ya mganga mwingine wa kwenda akaamua kufanya hivyo, ndipo alipotaka kutoka kwa mganga Yule ila alishangaa Yule mganga akimzuia na kumwambia kuwa atamsaidia, Rose alifurahi na kukaa chini ili kusikiliza Yule mganga atamsaidiaje, kisha Yule mganga akaanza kupiga tunguli zake, na alipomaliza akaanza kuongea nae,
“Kwanza kabisa, Yule mtoto wako ambaye kaungua na maji ya moto hamtakiwi kumpeleka hospitali”
“Mmmh mganga sijui kama watoto wangu watarudi tena hapa, kumbuka usiku sikuwaona au bado wapo nje?”
“Sijui ila hutakiwi kumpeleka hospitali”
“Basi ngoja nijaribu tena kuwatafuta”
Rose alitoka mule kwa mganga huku akiwa na mawazo sana kuwa watoto wake walielekea wapi ila alishangaa kufika nje, kuona gari yake na watoto wake ndani ya gari na ilionyesha wazi walikuja kumfata mama yao. Alijiuliza kuwa mbona usiku wa jana hakuwaona, kwamaana hiyo waliondoka au imekuwaje hapo, hakupata jibu kabisa. Aliwafata na kuwauliza kulikoni mbona usiku wa jana hakuwaona alipotoka kwa mganga, Sara alikuwa wa kwanza kumjibu mama yao,
“Mama tumekuja kukufata wewe, Doto kalazwa hospitali twende ukamuone”
“Kwahiyo Doto mmempeleka hospiatali?”
“Ndio mama”
“Nyie watoto jamani mbona mnanitafutia ubaya!”
“Ubaya upi mama? Doto yupo hospitali na tungemchelewesha tu tungemkosa, naomba twende mama”
Rose alikuwa ameduwaa tu nje huku akiwa hajielewi kuwa afanye kitu gani, Kulwa alishuka kwenye gari na kumpakia mama yao kinguvu kisha akapanda kwenye gari na kuondoa gari hiyo. Rose alikuwa kimya tu kwani bado alikuwa akitafakari bila ya jibu, mganga kamwambia kuwa mtoto wake asipelekwe hospitali na huku washampeleka hospitali kwahiyo hata akienda kumbembeleza tena mganga ni kazi bure kwa wakati huo. Ikabidi atulie tu kwenye lile gari, na alijiuliza tena kuwa mganga alikuwa na maana gani kuwa mtoto wake asipelekwe hospitali! Bado hakuwa na jibu, hadi wanafika hospitali ilikuwa ni mchana tayari, ila walipofika walizuiliwa na kuambiwa kuwa muda wa kuona wagonjwa umeisha, ikabidi Sara aulize
“Jamani mbona asubuhi mlituruhusu wakati muda ulikuwa umeisha?”
“Asubuhi aliyewaruhusu aliwaruhusu kimakosa, njooni jioni ndio muda uko wazi”
“Sasa mgonjwa wetu hajala”
“Ameshakula, kuna ndugu yenu kashampa chakula. Atatoka muda sio mrefu”
Yule nesi alisogea kidogo, na muda sio mrefu wakamuona Salome akiwa ameongozana na mwanamke mmoja, Rose alipomuangalia vizuri Yule mwanamke aligundua ni Neema ambaye ni mama yake na Salome.
Salome na mama yake hata hawakuangalia upande, walikuwa wanaondoka tu ila Rose alimuita Neema,
“Neema”
Neema akageuka na kumuona kuwa ni Rose, uoga ukamshika kwani bado alikuwa anamuogopa Rose vilivyo, ila Rose alimsogelea Neema na leo kwa mara ya kwanza alimsalimia vizuri kabisa,
“Hujambo Neema”
“Sijambo shikamoo”
“Mbona unaniogopa hivyo!”
Salome akadakia,
“Anakuogopa sababu umezoea kumtishia”
Neema alimkatisha mwanae kuwa asiendelee kuongea maneno hayo, Rose alimwambia Neema
“Sina ugomvi na wewe na nimefurahi kukuona. Natumai umetoka kumuona mwanangu, mwanao pia nimempokea vizuri kwenye nyumba yangu ila mwanao ni mshirikina”
Neema akashtuka
“Mshirikina!”
Salome akacheka sana, kisha akamshika mama yake mkono na kumlazimisha kuwa waondoke eneo hilo, ila Neema alikuwa mbishi kufanya hivyo. Salome alimwambia mama yake,
“Mama, sijakuleta hapa kuja kubishana na huyu mtu. Halafu nina mambo mengi ya kufanya siku ya leo, tafadhali tuondoke nyumbani”
Neema alikuwa mbishi mbishi kwani bado alitaka kusikia kuwa kwanini mwanae kaitwa mshirikina ila ikabidi akubaliane tu na mwanae kuwa waondoke, ambapo salome alikodi bajaji iwapeleke nyumbani kwao ila kitendo cha Salome na mama yake kuondoka na ile bajaji, Rose alienda kuwaomba watoto zake kuwa waifate hiyo bajaji hadi wajue wanapoishi Salome na mama yake, kwahiyo walifanya hivyo na kuanza kuifatilia ile bajaji.
 
SEHEMU YA 133


Nyumbani kwakina Mishi mamake alipoenda tu kumwambia mzee Juma kuhusu maamuzi ya Mishi wala hakubisha Yule mzee kwani siku zote alitamani Mishi akubali amuoe ukizingatia kashakula hela zake nyingi sana, kwahiyo hakutaka hata kupoteza muda ni siku hiyo hiyo akaita watu na kumuoa msichana huyo, ilifungwa tu ndoa ya kawaida yani haikuwa na shamra shamra zozote kwani ni ndoa ya haraka halafu haikupangwa ila Mishi alifurahi kuolewa na mzee huyu na hakumwambia kama alibakwa au alikutwa na matukio yaliyomfanya akubali kuolewa nae, ingawa alikuwa akijiuliza sana kuwa inakuwaje kuwaje mambo hayaeleweki kabisa.
Alipomaliza kufunga ndoa, akatembelewa na mgeni na kuambiwa kuwa kuna mgeni wake, alitoka kwa mashaka sana kwani bado hakuwa na imani na jambo lolote na uoga ulikuwa umemtawala. Alipoenda kuzungumza nae alishangaa kuwa ni Salome, akataka hata kurudi kwa ndugu zake ila alishangaa miguu yake ikigoma kufanya hivyo, kisha Salome akaanza kuongea nae,
“Usiniogope mimi sio mla watu, wala sio mchanganya wanaume kama wewe”
Mishi alikuwa kimya tu akimsikiliza,
“Umefanya uamuzi wa haraka sana kuolewa, hivi unajijua kama hapo ulipo una mimba? Au unataka hiyo mimba umsingizia Yule mzee wa watu?”
“Nina mimba ya nani?”
“Mi nitajuaje na umebakwa na watu wengi. Unajua wakati wa kubakwa ni vigumu kujizuia tofauti na ukitaka mwenyewe, sasa vipi unataka kumsingizia mzee wa watu!”
“Hapana sikuwa na nia hiyo ila nimeamua tu kutoka moyoni kuolewa”
“Kama umeamua kutoka moyoni mwambie ukweli, Yule mzee anakupenda na atakuelewa tu. Halafu kama umeamua kweli kwa moyo wako, tulia na mumeo. Ni mwanaume gani anaweza kukubali kufunga ndoa ya haraka haraka kiasi hiko? Anakupenda mwenzio, ni wa kawaida tu Yule hata sio mtu mzima kihivyo, mpende sababu umeamua mwenyewe uache tabia ya kuumiza moyo wake”
“Nimekuelewa na ninakuahidi nitampenda sana na nitamwambia ukweli wa kila kitu”
“Usiniogope, mimi ni binadamu wa kawaida tu kama wewe. Kwavile umesema utatulia kwa mumeo, naifuta laana yangu kwako”
Salome aliondoka, na Mishi alikuwa anamuangalia hadi alipoishia, hata alipoulizwa na mama yake kuwa mtu huyo alikuwa anaongea nae nini bado hakuweza kumjibu kwani kwake bado lilikuwa ni swala la aibu.

Wakiwa ndani ya bajaji, Neema alimshangaa mwanae amelala mpaka wanafika nyumbani ndio anamshtua kuwa washuke na waingie ndani, walipoingia ndani mara na wao wakina Rose walikuwa wamefika ila Salome alifanya jambo na kumfanya mama yake kuingia chumbani ili wakigonga mlango wa sebleni wasimkute mama yake na wamkute yeye. Basi kweli wakagonga mlango wa sebleni na kusikia sauti ya Salome ikiwakaribisha,
“Fungua mlango ingia”
Basi wakafungua na kuingia, Rose alikuwa wa kwanza kuingia mule ndani ila alishtuka sana kwani alijiona yupo nyumbani kwake na aliyewakaribisha alikuwa ni Patrick na sio Salome.
 
SEHEMU YA 134




Basi wakafungua na kuingia, Rose alikuwa wa kwanza kuingia mule ndani ila alishtuka sana kwani alijiona yupo nyumbani kwake na aliyewakaribisha alikuwa ni Patrick na sio Salome.
Kila mmoja alipoingia alishtuka, kisha Patrick akawauliza kwa kejeli,
“Mnashtuka nini sasa? Mnashtuka kuniona kwenye nyumba yangu mwenyewe? Hapa si nyumbani kwangu, kwahiyo siruhusiwi kuja?”
Wote walikaa kimya kwani kila mmoja alikuwa akijiuliza kuwa imekuwaje tena wamerudi nyumbani kwao wakati walikuwa wakiingia kwakina Salome na aliwakaribisha, Patrick aliwashangaa kuwa hawasemi chochote akajua wanamfanyia kiburi bila ya kujua kilichowasibu.
“Nyie jifanyeji kiburi tu, mmenikuta kwenye nyumba yangu, hata salamu kutoa hamjatoa eti mnashangaa shangaa. Haya endeleeni kushangaa tu mkimalia mtaniambia”
Patrick akakaa chini akiwaacha wao wamesimama huku bado wakishangaa tu, Rose nae alikaa chini huku akitikisa kichwa chake na kusema,
“Hivi ni kweli au naota?”
Alidakia Ana na kumjibu mama yake,
“Ni kweli mama, tumerudishwa nyumbani tena bila ridhaa yetu. Anayetufatilia kwa hakika ana nguvu zaidi yetu”
Wote walikuwa kimya tu, Rose alipumua kwa nguvu maana mambo yalikuwa yakimchanganya zaidi na kuanza kuhisi huenda swala la kumpeleka Doto hospitali ndio limeendelea kuzua hayo wanayoyaona. Alipojitafakari vilivyo akamuangalia Patrick sasa na kuanza kumuomba msamaha maana kwa hakika Patrick alihisi wamemdharau,
“Tafadhali tusamehe bure ila yaliyotupata kwa siku ya leo hapana kwakweli”
“Yaliyowapata yapi hayo?”
“Mume wangu unanichukia bure tu ila familia yetu inafatiliwa na wachawi”
“Wachawi kushinda wewe uliyemuua mama yangu!! Yani mimi naongea na wewe bure tu ila wewe Rose ni mwanamke mbaya sana, umeniulia mama yangu, umefanya niiache familia yangu iteseke, nimeacha ndugu zangu wakiteseka huku mimi nikila raha ya maisha. Nimeacha mwanangu akiteseka huku wanao nikiwalea maisha ya kifahari, wewe ni mwanamke mbaya sana Rose”
“Naomba unisamehe kwanza, halafu hayo si maneno ya kuongelea mbele ya watoto”
“Unataka nikaongelee wapi? Umenitesa sana wewe mwanamke, na kwa taarifa yako ndugu zangu wanakuja hapa sio siku nyingi”
“Patrick! Ndugu zako wanakuja!”
“Ndio ndugu zangu wanakuja hapa na watakuwa wanakaa hapa”
“Haiwezekani Patrick, huwezi kufanya jambo bila kunishirikisha mimi. Humu ndani mimi ndio mama mwenye nyumba”
“Mke wangu ni Neema na ndio mama mwenye nyumba”
“Neema kivipi? Kumbuka Patrick, ulimuacha Neema na kunioa mimi, iweje leo useme mke wako ni Neema! Umechanganyikiwa wewe sio bure”
Kisha Rose akawaangalia watoto wake na kuwaambia,
“Hivi na nyie hamuwezi kwenda kufanya mambo mengine hadi make msikilize mazungumzo ya mimi na baba yenu!”
Patrick akadakia,
“Waonyeshe baba zao watoto wako, mimi sio baba yao. Na kibaya zaidi hata huyo mtoto wako wa mwisho nae sio wangu, nilijivunia nimepata mwanamke kumbe ananiacha ndani anaenda kuzaa na mwanaume mwingine nje”
Wakina Sara baada ya kuona jicho kali la mama yao ikabidi watoke nje na kuwaacha sebleni kwani Patrick aligoma kwenda kuongelea popote pale zaidi zaidi ya hapo sebleni.
“Jamani Patrick twende tukaongelee chumbani mambo hayo”
“Twende chumbani ili ukaniroge? Rose umeniroga kwa miaka mingi sana, akili yangu imefunguka sasa na huwezi kunishawishi juu ya kuniroga tena, mwanamke mbaya wewe”
Rose alijaribu kila njia ya kumtuliza Patrick ila leo alikuwa hatuliziki kabisa, inaonyesha wazi aliamua na alidhamilia.
 
SEHEMU YA 135

Kule nje walienda moja kwa moja kwa mlinzi wao na kumuhoji kuwa Yule baba yao alienda saa ngapi pale nyumbani, ila mlinzi alivyowaona alishtuka sana badala ya kumuuliza yeye aliwauliza wao,
“Mmeingia muda gani humu ndani?”
“Tunataka kukuuliza baba amekuja muda gani?”
“Humu ndani mbona mmekuwa na mambo ya ajabu sana sijapata kuona, yani siwaoni kuingia ila gafla nawaona ndani”
Basi akafikicha fikicha macho yake na kuiona gari ambayo walitoka nayo ikiwa imepaki uwani, yani hapo ndio akashangaa kabisa kuwa hata gari ilivyoingia hakuiona yani aliona mambo ya ajabu na kuhisi nyumba yote hiyo ni wachawi.
“Mama akirudi namuomba mshahara wangu naacha kazi”
“Usiache kazi bhana, uache kwasababu gani? Hata hivyo mama yuko ndani”
Mlinzi akashtuka tena,
“Yuko ndani? Ameingiaje?”
“Tulikuja nae”
“Hii nyumba hapana, imenishinda kwakweli yani imenishinda kabisa siwezi kuendelea kuishi humu”
“Usiondoke, haya mambo yatarekebishwa tu hata usiende popote”
“Hapana siwezi, yani watu unawaona wakati wa kutoka tu ila wakati wa kuingia huwaoni!”
“Inamaana nae baba hujamuona wakati wa kuingia?”
Ana aliuliza kwa makini swali hilo kwani alitaka kujua kama ni kiini macho wamefanyiwa au ni kitu gani,
“Mzee yeye kafika vizuri, tumesalimiana nae hapa na kuuliza mko wapi na akaingia ndani kuwangoja. Yani nyie ndio mmenifanyia maajabu, na toka mzee aje sijatoka kabisa hapa getini leo, haya niambieni mmeingiaje”
“Yani hata sisi wenyewe hatujui kwahiyo utakuwa unatushutumu bure tu”
Ila huyu mlinzi alishikilia wazo lake tu kuwa yeye ataomba mshahara wake aondoke kwenye nyumba hiyo, wakati wanaongea na Yule mlinzi alifika mtu na kugonga geti alipomfungulia alikuwa ni Salome, walibaki wanamtazama kama dakika kadhaa ndio kumkaribisha ila Salome alitabasamu tu na kuingia ambapo moja kwa moja alienda ndani na kuwakuta Rose na Patrick wakiwa kwenye majibizano makubwa sana. Alipoingia tu kama kawaida yake aliingilia yale mazungumzo,
“Wewe mama ushaambiwa usamehewi, sasa ya nini kulazimisha msamaha!”
“Hata maandiko yanasema samehe saba mara sabini”
Salome alicheka sana ten asana kisha akamwambia,
“Hivi leo ndio unatambua maandiko yamesema hivyo, je ulipokuwa unamuua bibi wa watu asiyekuwa na hatia ulikumbuka maandiko? Ulipomtumia Ashura ajifanye anaundugu na Neema ili tu azidi kumkandamiza ulitumia maandiko? Wakati Salome anateseka na maisha wakati baba yake anakula raha ulitumia maandiko? Na zaidi ya yote, uliowafuga ndani kwenye chumba chako cha siri unatumia maandiko?”
Patrick akashtuka sana kusikia kuwa mkewe kuna watu anawafuga pia kwenye chumba cha siri,
“Kheee wewe mwanamke kweli ni shetani yani wewe una matendo hata shetani anayaogopa. Kwahiyo kuna watu umewafuga ndani kwako?”
“Salome jamani usizidi kunikandamiza jamani, nisameheni”
“Nani akusamehe mwanamke shetani kama wewe? Yani umefanya maovu mengi napo umeona hayatoshi ila ukaongezea na kuwafungia watu kwenye chumba cha siri!”
“Anafuga watu ndio huyu, hujui tu baba ila ndio hivyo anafuga watu huyu. Siku ukinijua vizuri utaelewa nimejuaje siri zako na njia zako, sipendi unavyowatesa wale watu, waachie waendelee na maisha yao mengine”
Kisha Salome akamgeukia Patrick na kumwambia,
“Wasichana wa kazi wote wanaopotea kwenye nyumba yako halafu anasema kawafukuza ni muongo, anawafungia kwenye chumba cha siri, ikitokea mtu kaumia kwenye nyumba hii damu ikamtoka basi asitoke mlangoni maana akitoka tu anajikuta kwenye chumba cha siri, huyu mama ni mpumbavu sana, anafanya mambo ya kijinga. Watu wa watu wamekonda sababu ya kufungiwa, ni bora ujue ndugu yako amekufa kuliko kujua ni msukule, huyu mama ni mbaya sana”
Sara na Kulwa walikuwepo mlangoni na walisikia yote ambayo mama yao alikuwa akishutumiwa, muda huu Ana alikuwa getini na mlinzi ila wao wakati Salome ameenda ndani walienda kukaa mlangoni, kwahiyo kila kitu kilikuwa wazi kwenye masikio yao na kuelewa kirahisi kuwa wote wanaohisi wamepotea kumbe mama yao amewafungia kwenye chumba cha siri, ndipo Sara nae alipojiwa na swala la Ommy, akaweza kufikiria ni jinsi gani Ommy alikuwa akiteseka kwenye hiko chumba cha siri, alijikuta akiingia ndani na kumwambia mama yake,
“Mama tafadhali mfungulie Ommy wangu”
Sara machozi yalimlengalenga kwani leo alielewa mchezo vizuri kabisa kuwa mama yao ni mchawi tena mchawi haswaa wala sio wa kusingiziwa kama wengine. Rose hakuweza kuvumilia hizi shutuma akaamua kukimbilia chumbani, kwahiyo sebleni alibaki Salome, Patrick na Sara.
Hizi habari za mkewe kuwa na chumba cha siri zilimshtua sana Patrick kwani aliweza kupata kumbukumbu kuwa kuna rafiki yake aliwahi kupotea kwenye nyumba yake hiyo na hakujulikana alipoenda hadi leo hajui ila hapo kapata jibu kuwa huenda nay eye amefungiwa kwenye chumba cha siri, akamuangalia mwanae Salome na kumuuliza,
“Wewe umejuaje hizi habari za huyu mwanamke kufungia watu kwenye chumba cha siri”
“Nilijua toka siku ya kwanza nilipokuja kufanya kazi humu”
Sara na Patrick walishangaa na kujikuta wakimuuliza kwa pamoja,
“Ulipokuja kufanya kazi humu!!”
“Ndio, ila msinihoji zaidi yani nyie mjue tu kwamba nilijua.”
“Sasa tutafanyaje ili awatoe”
“Najua cha kufanya ila njia yangu ni hatari sana, hatari kwake na kwa familia yake ndiomana nataka awatoe mwenyewe kwa hiyari yake”
Wakajikuta wakimuangalia Salome na ilionyesha wazi hawamuelewi elewi maana vitu vingine aliongea kamavile ni mtu wa aina nyingine na sio wa kawaida, Kulwa nae aliingia ndani na kuwaambia kuwa kasikia kila kitu na anashangazwa na habari hizo za mama yake kuwa kuna watu amewaeka msukule, basi akawa anajadiliana pale na dada yeka kisha Salome aliomba kutoka na baba yake ambapo alikubali na kuondoka na Salome halafu wakawaaga pale.
 
Back
Top Bottom