SEHEMU YA 138
Rose baada ya mlinzi wake kuondoka asubuhi ya siku hiyo, na yeye alifanya safari ya kumtafuta mganga wake aliyemfikiria kichwani, alimtafuta sana bila ya mafanikio ila njiani akakutana na rafiki yake wa muda mrefu sana ambaye aliwahi kumshauri kuhusu swala la waganga kwahiyo alivyokutana nae alifurahia sana, na kuanza kumshirikisha kuhusu swala lake linalomsumbua kichwa.
“Basi mwezi uliopita mwenzio nilipatwa majanga hayo balaa, yani kuna mavitu yalichanganya kichwa change kama nini ila kuna kijana huyo ni matata, kwanza kijana haogopi kitu yani hakuna takataka yoyote inayomshinda. Huyo kijana ni kimbilio la watu wengi sana, wanaotafuta watoto, wanaotafuta mali yani kila kitu. Nina uhakika huyo kijana hawezi kushindwa, hao waganga wako wamechoka halafu waoga”
“Huyo atakuwa mzuri kweli, nilijaribu kumtafuta hata Yule wa mwanzo aliyewahi kunipa dawa ya kufukia ndani kwangu ila sijampata”
“Unadhani Yule unampata kirahisi hivyo? Yule hakuwa mganga ni jinni lile, na anapatikana kwa waganga wanaojiweza tu, Yule mganga tuliyeenda kipindi kile alikuwa anajiweza ndiomana ikawa rahisi kukutana na Yule wa dawa. Ingawa masharti mengi umeyavuruga ila kwa Yule ndio kiboko”
“Naomba nipeleke ndugu yangu, nipo tayari kutoa kitu chochote kile ila niepukane na aibu hii maana kwangu ni aibu na fedheha”
Basi huyu rafiki wa Rose akajitolea kumpeleka Rose, na kwavile alimuomba ampeleke siku hiyo hiyo akajitolea kufanya hivyo ingawa ni mbali sana hiyo sehemu.
Patrick hakujisikia kuondoka kabisa nyumbani kwa Neema, na alichofanya Salome ni kwenda kumchukulia Patrick nguo zake zote na kumfanya afurahi zaidi kurudi kwa Neema, alimuomba Neema asimfukuze eneo hilo kwani alizidi kufunguka mawazo ya kuhusu mali zake na nyumba zake ambazo zingine alikuwa hata haendi kuzitembelea kwavile alishazisahau ila Neema akawa kama amemkumbusha kwahiyo alifurahi sana kumalizia muda wake kwa Neema, na pia watoto wale mapacha wa Neema aliwaona ila aliogopa kuuliza kuwa wale watoto ni wa nani, ila alijikaza na kuuliza,
“Samahani Neema, na hawa watoto wako wengine baba yao yuko wapi?”
Neema akacheka kisha akamwambia,
“Baba yao ni wewe”
“Ni mimi? Kivipi?”
“Najua huwezi kukumbuka au kujua, hii kitu niliiweka siri siku zote za maisha yangu”
“Niambie kivipi?”
Basi Neema ilibidi amueleze Patrick ilivyokuwa,
“Kuna kipindi nilikuwa nauza baa, na ulikuja kunywa sijui ulikuwa na mawazo gani ila ulikunywa sana hadi ulilewa. Ikawa kila mwanamke anayepita mbele yako unamshika, ilibidi nidanganye kuwa umenihitaji mimi na kwenda na wewe chumbani, ila kwa nguvu ya pombe uling’ang’aniza kulala na mimi, kwavile nilikuwa bado nakupenda sikuweza kukataa, nililala na wewe ila usiku wake niliondoka na kukuacha umelala fofofo. Kulipokucha uliondoka halafu na mimi niliacha kazi pale kwenye ile baa, sikuwahi kumwambia mtu yeyote kilichotokea baina yangu na yako, na baada ya mwezi nilijigundua kuwa nina ujauzito hapo ndipo nilipoamua kufanya siri hadi nimejifungua. Ilikuwa ni siri yangu hata ndugu yangu Yule Ashura sikuwahi kumwambia chochote, ingawa sasa nimegundua hakuwa ndugu yangu, yani kama hakuwa ndugu yangu alikuwa na mipango gani kwangu? Ni siri yake kwakweli, ila hakuwahi kujua kuwa watoto wangu ni wa nani sababu mar azote alizoniuliza nilimwambia kuwa nilibakwa”
Patrick alishangaa sana hii habari, na kujaribu kuvuta kumbukumbu ya siku aliyolewa sana, alikumbuka tu kuna siku alilewa sana ila hakukumbuka ni kitu gani alikifanya,
“Na hiyo siku niliyolewa sana ndio siku iliyobadilisha maisha yangu kabisa, maana tangu siku hiyo niliporudi nyumbani ndio nikafanywa kama ndondocha yani sikuwa na uwezo wa kwenda sehemu yoyote ile bila ruhusa ya Rose, yani kipindi hiko ndio mateso yalizidi kwangu maradufu”
“Pole sana, basi hivyo ndivyo ilivyokuwa kuhusu hawa watoto. Yani ni wanao kabisa”
“Kwakweli nimeteseka sana mimi, siku ile ilipelekea kunywa sana pombe baada ya kumuona mke wangu akiniwekea dawa kwa macho yangu, mimi sio mlevi kiasi kile ila siku ile nililewa sababu ya mawazo. Ila kitendo cha kurudi nyumbani ndio nikawa ndondocha kabisa, yani hakuna kitu nilichokuwa nafanya kwa akili yangu.”
Patrick aliomba aitiwe watoto wale ili awaangalie kwa karibu maana hakuamini amini kuwa alikuwa na watoto, maana alijua kuhusu Salome ila hakujua kama ana watoto wengine.
Neema aliwaita watoto wake, nae Patrick aliwakumbatia kwa furaha hata wale watoto walibaki kushangaa tu kwani hawakutegemea huyo mtu kuwafurahia kiasi kile tena huku akiwaita wanangu, walikuwa wakishangaa shangaa tu ikabidi Neema awaambie,
“Baba yenu huyo”
Na wao wakashangaa na kufurahi maana hawakufikiria kutambulishwa baba, kwani siku zote walipokuwa wakiulizia kuhusu baba yao Neema alikuwa akiwafokea sana.
Patrick akazidi kupata uchungu dhidi ya Rose na mali zake, ilimuuma sana na kumfanya sasa awaze namna ya kurudisha mali zake kwenye mikono yake ili watoto wake wafaidi.