SIMULIZI: Mchungaji Mchawi (01)

SIMULIZI: Mchungaji Mchawi (01)

Joined
Aug 27, 2022
Posts
4
Reaction score
7
FB_IMG_16547154958177668.jpg


Story: MCHUNGAJI MCHAWI.
Mtunzi: NellovešŸ˜Ž
Episode: 01
WhatsApp: 0759941164

"Naitwa Juliana. Napenda kumshukuru sana Mungu mwenyezi kwa kunitendea muujiza mkubwa maishani mwangu. Sikuwahi kutegemea kama Mama yangu ataweza kutembea tena lakini kwa uwezo wa Mungu anatembea sasa" ilikuwa sauti ya mwanadada aliyesimama mbele ya madhabahu, mkononi mwake ameshika kipaza sauti anatoa ushuhuda.

"Mama yako yuko wapi?" Ilikuwa sauti ya mchungaji.

"Yule amekaa pale" alisema na kunyoosha kidole kuelekea mahali alipo Mama yake.

"Njoo Mama, njoo usiogope"
Aliita mchungaji kisha Mama yule wa makamo alisimama na kuanza kutembea kuelekea mbele.
"Mama unaitwa nani?"
"Naitwa Dorothea.
Namshukuru sana Mungu kwa kuniponya. Nilikuwa siwezi kutembea mimi, mguu wangu ulioza kabisa." Aliongea huku analia.
"Nimepoteza hela nyingi hospitalini na kwa waganga lakini sikuponywa ha..."

"Pole Mama, polepole sasa.
Enh! Ilikuwaje hadi unakuja kwa mchungaji?"

"Nilikuja hapa baada ya kusikia matangazo redioni kwamba kuna mchungaji anaponya sana" aliongea huku anatoa machozi.

"Tuambie Mama Ulipokuja ilikuwaje"
"Nilipokuja hapa niliguswa tu kidogo kisha nilipewa maji na mafuta ya upako. Nilipotumia tu nilipona kabisa".

"Halleluyaaaaaaaaah!!!!! Piga makofi na vigelegele. Mshangilie Mungu mpendwaaaa" sauti ya mchungaji iliunguruma, watu walishangilia mno.

"Hivi ndivyo utendaji wa Mungu ulivyo. Amekuumba ili uishi kwa amani. Naomba unisikilize mwanangu, Mungu hajakuumba ili uteseke na ndio maana mateso yanapokuja, yeye huwa tayari kukuondolea. Halleluyaaah!" Alizungumza mchungaji.

Baada ya hapo mchungaji alipiga hatua hadi nyuma ya madhabahu na kufunua kitambaa kirefu kilichofunika madhabahu ile. Aliingiza mkono na kugusa kitu alichokijua yeye mwenyewe kwa kidole kisha alipotoa mkono alilamba kidole kile huku akihisi nguvu za ajabu zikiingia mwilini mwake. Hili tukio la kulamba kidole halikuonekana na mtu yeyote,,, basi baada ya kufanya hivyo alirejea.

"Popote ulipo, naomba simama kwa miguu yako. Nahitaji kuomba nawe, nahitaji kumwambia Mungu akutoe katika shida uliyonayo, nahitaji kuomba mamlaka na nguvu za kufukuza mashetani yaliyofunga maisha yako, nguvu ya kutuma moto wa kwenda kuunguza wachawi wa maisha yako. Naisikia nguvu ya Mungu ndani yangu,,,, Motoooooooooooo!!!!!" alitamka maneno hayo kisha dakika chache baadae watu wengi walianza kuanguka na wengine walipiga kelele.

Wahudumu mbalimbali wa kanisa wakishirikiana na Mama mchungaji walijumuika kwa pamoja kutoa huduma kwa wote walioanguka na wenye mapepo. Mchungaji naye aliendelea kutoa huduma kwa kila mmoja aliyesogezwa mbele yake, alitumia kitambaa kirefu chenye rangi nyeupe kuwagusa wagonjwa na hakika kila aliyeguswa alipata kupona hapohapo. Miujiza iliendelea kufanyika kwa watu waliokuwa wamehudhuria kanisa hilo kubwa sana na lenye waumini wengi mno.

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa siku hiyo na kila siku ya jumapili na jumatano, siku ambazo zilikuwa kwenye ratiba ya ibada ya kanisani hapo. Watu mbalimbali wenye shida kadha wa kadha waliponywa kwa miujiza ambayo iliendelea kukua siku hadi siku yaani muujiza mkubwa uliofanyika jana ni mdogo kuliko ule utakaofanyika leo na kesho. Miujiza iliendelea kuwa mikubwa mikubwa mikubwa,,,, miujiza ikasambaa sana na kufanya waumini waongezeke maradufu katika kanisa hilo.

Kila mmoja aliyeitambua shida aliyonayo hakutaka kusubiri, alikuwa tayari kutumia nauli ya kiasi chochote kile na muda wa masaa yoyote cha msingi afike kwa mchungaji na kupata huduma.
Watu wa sehemu mbalimbali ndani ya nchi waliweza kufika na hakika walizingatia muda kwani waliposikia ibada ni jumapili wao walifika mapema jumamosi, wapo wengine walifika Ijumaa na kulala hapo wakisubiri uponyaji.

Waumini waliongezeka na kuongezeka,,, nao walipokuwa wengi zaidi, kanisa lilifanyiwa ukarabati na kuongeza ukubwa.
Kanisa lilijengwa kisasa zaidi kwani ziliwekwa TV,, pia ziliwekwa kamera kunasa matukio yote yanayoendelea kwa ajili ya kurusha kwenye vyombo vya habari kama Televisheni maana walikuwepo waumini wengine ambao walikuwa wanafuatilia huduma kwa njia hiyo ya Televisheni. Si ndani ya nchi tu bali sasa waumini walitoka hata nje ya nchi pia.

Ilikuwa jumapili moja hivi muda wa maombi,, kabla ya kufanya chochote aliisogelea madhabahu na kupiga magoti huku akitamka maneno fulani ya ajabu. Nguvu zilimuingia kisha alianza kuwaponya watu wenye shida mbalimbali.
"Halleluyaaah Mungu ni mkuu sana. Najua mmesadiki ya kwamba hakuna jambo linaloweza kumshinda" mchungaji alisema baada ya kumgusa na kumponya mtu aliyekuwa hawezi kuona yani kipofu.

"Ni muujiza mojawapo kati ya mingi mliyoishuhudia kwa macho yenu. Wengi huwa hamuamini mpaka muone. Sasa mmeona hivyo sina shaka mnaamini. Sasa Hiyo imani uliyonayo ikunyanyue hapo ulipo,,, na wewe unayenitazama kupitia TV hapo nyumbani nikusihi simama na uguse kioo cha TV yako." Watu walisimama kwa imani huku wengine wakianza maombi yao ya chini chini.
"Kuna sauti inaniambia kwamba yupo Mama alichukuliwa damu na wachawi wakati wa siku zake. Na sasa huyu Mama hazai na amehangaika sana lakini hakuna mafanikio hivyo ameshakata tamaa" alisema mchungaji huku anatembea tembea.

"Yupo mwingine amefungwa tumbo lake ili asizae. Sasa natamka mkono wa Mungu ukafungue hiyo minyororo na nira zote ulizofungwa,,, na wewe Mama uliyechukuliwa damu yako nakutamkia uponyaji kwa nguvu za kiungu zenye kufukuza uchawi huo." Aliposema tu hivi vilisikika vilio kutoka nyuma ya kanisa.
Wamama watano walianguka na kubebwa msobemsobe hadi mbele.
"Wawekeni hapo" alisema kisha aliendelea

"Kuna sauti inaniambia tena. Kuna mtu mmoja nafsi yake imezikwa. Mnaweza kumuona anatembea na mmekaa naye hapo lakini ni mfu na ndio maana hapendwi, kila afanyacho kinaharibika na anakataliwa hata na familia yake. Nimetumwa kuokoa Taifa la Mungu, Sasa nakuita huko kaburini ama kuzimu uliko. Njooooooo!!!!!!" alitamka hayo kwa sauti nzito ya kuunguruma.

"Njoooooooooo!!!!!" alitamka tena na kumalizia mara ya mwisho ndipo mwanaume mmoja nyuma ya kanisa alipoanza kuruka ruka kama mtu aliyepandwa na mapepo.

Watu waliogopa kukaa karibu naye maana alitishia kukamata watu huku midomo yake ikitoa udenda na kitu kama povu hivi. Sauti ya kuunguruma ilisikika kutoka ndani yake na midomo yake iling'ata na kutafuna nyama za mikono yake. Damu ilitapakaa,, watu waliogopa zaidi.

Mchungaji alishuka madhabahuni na kupiga hatua za taratibu kuelekea nyuma ya kanisa.
Alikuwa pamoja na watumishi wake wapatao watatu walioongozana naye hadi mahali alipokuwepo yule mwanaume aliyekuwa anatisha watu.

Alimsogelea yule mtu na kukemea kwa nguvu lakini katika hali isiyo ya kawaida mchungaji alisikia kichomi na kujihisi kama anapigwa kofi zito usoni mwake. Kofi hili lilimpelekea kujisikia kizunguzungu na kuona giza kwa mbali lakini kabla hali haijawa mbaya zaidi alichukua kitambaa chake cheupe na kujifuta usoni.
Basi mchungaji alipoona kile kichomi na hali mbaya imetoweka alichukua kitambaa kile na kukirusha kwa yule mwanaume. Kitendo cha kuguswa na kitambaa kile, alianguka chini na kutapatapa kama mtu anayepigwa fimbo na kuugulia maumivu yake.

Dakika tatu baadaye yule mtu aliacha vurugu, alisimama taratibu kisha alianza kushangaa shangaa kama mtu anayeweweseka. Mchungaji alimtazama na kumgusa kwenye paji la uso huku anatamka maneno yake aliyoyafahamu yeye mwenyewe kisha alirudi madhabahuni.

Hata hivyo alishangaa sana kuona hali yake inaanza kuwa mbaya kwa mara nyingine. Alisimama taratibu na kuelekea kwenye chumba maalum cha kufanyia maombi yake mwenyewe,,, hakutaka yeyote amfuate. Alifunga mlango na madirisha, alifunika kichwa kwa kofia iliyokuwa imeshonwa kwenye kanzu yake Nyeusi kisha alifumba macho na kunyoosha mikono. Dakika chache tu baadaye šŸ‘¹šŸ’€Fuvu lenye mapembe lilitokea na kuanza kuzunguka juu yake huku likifuka moshi, nayo ile hali mbaya ilipotea ghafla.

ITAENDELEA...
 
Story: MCHUNGAJI MCHAW.
Mtunzi: Nellove
Episode: 02
WhatsApp:0759941164

Ilipoishia...

Dakika chache tu baadaye [emoji83][emoji88]Fuvu lenye mapembe lilitokea na kuanza kuzunguka juu yake huku likifuka moshi,,, nayo ile hali mbaya ilipotea ghafla.

Endelea...

Ile hali mbaya ilipotoweka tu na lile fuvu lilipotea pia.
"Shukurani sana mtukufu mfalme wa kuzimu" alisema hayo akiwa ameinama kwa sekunde kadhaa.
Alipoinuka alijifuta futa usoni mwake kwa kitambaa chake cheupe ambacho kwa sasa kilikuwa na matone machache ya damu,, hali yake ilikuwa sawa kabisa bila matata ndipo alitoka na kurudi madhabahuni.
Hakuna mtu yeyote aliyepata kufahamu ni kipi hasa kilimsibu mchungaji,, ni yeye mwenyewe aliyejua ni nini kilikuwa kinaendelea na hata hivyo kila alipofikiria hakuacha kusema
"Sio bure,,, hapa kuna nguvu nyingine"

Ibada iliendelea akiwaombea watu na kuwaponya kwa nguvu zaidi.

† † †

HIVI NDIVYO SAFARI YAKE YA UCHUNGAJI ILIVYOANZA.

Kwa majina kamili anaitwa Joshua Mushi ambaye tangu ujana wake alipenda sana kuwa karibu na Mungu licha ya familia yake kutoonesha msisitizo katika hili. Familia yake ambayo ilikuwa na makazi mkoani Morogoro katika kijiji cha Matombo haikuwa ikienda sambamba sana na masuala yote yaliyomuhusu Mungu muumba. Imani yao kubwa ilikuwa kwa waganga ambao walikizunguka kijiji cha Matombo kwa kiasi kikubwa sana wakati huo kanisa lilikuwepo moja tu katika kijiji hicho.

Licha ya kuvunjwa moyo na kukatishwa tamaa na wazazi wake lakini joshua hakutaka kurudi nyuma kiimani,,, alisonga mbele. Alijitoa kwelikweli kumtumikia Mungu na kujitoa huku ndiko kulikopelekea ajenge mahusiano mazuri sana na mchungaji Nikodemo ambaye ndiye mchungaji wa kanisa la pekee lililokuwepo kijijini hapo matombo. Kila mara alipokuwa na utata kichwani mwake ama tatizo fulani, alimfuata mchungaji huyu kwa ushauri na msaada zaidi. Juhudi za kijana Joshua zilimfurahisha sana mchungaji Nikodemo kiasi cha kumuamini na kumpatia nafasi mojawapo ya kuwa miongoni mwa watoa huduma hapo kanisani.

Siku ziliendelea kusonga mbele, ilikuwa siku moja ya jumapili majira ya asubuhi. Joshua aliamka ili kujiandaa kwenda kanisani lakini kabla ya kufanya chochote kile cha maandalizi ubongo wake ulirejelea kumbukumbu za ndoto aliyoiota usiku huo. Maswali kemkem yalianza kumsogelea na kumpa bughdha.
"Hivi nitaweza kweli?" Alijiuliza na kutafakari kwa kina kisha alisema tena.
"Sidhani kama nitaweza" alisema na kunyanyuka kwa ajili ya kujiandaa kwenda kanisani.

Alichukua maji ya kwenda kuoga,,, hata hivyo alisimamishwa na sauti ya Mama yake aliyekuwa anafagia uwanja.
"Mbona maji asubuhi subuhi wapi tena!!?"
"Mama leo si jumapili? Nataka niende kanisani"
"Mnashinda kanisani tu kila saa alafu hakuna chochote mnachokipata,, ujinga tu,, msyuuuu!!!." Alisema na kusonya lakini Joshua hakujali hilo,, aliingia kuoga.

†

Ibada ilianza na kama kawaida ya Joshua aliwahi viti vya mbele kabisa.

Huduma mbalimbali zilifanyika zikihusu maombi ya kukomboa ndoto maana somo la siku hiyo lilihusu ndoto.
"Chanzo cha ndoto huwa tofauti tofauti. Yaweza kuwa ni shughuli zako zote za mchana, yaweza kuwa ni shetani, yaweza kuwa ni Mungu. Hivyo vyote ni vyanzo vya ndoto. Sasa utajuaje kuwa ndoto yako inatokana na chanzo gani? Utajuaje???" Mchungaji Nikodemo aliendelea,,

"Ili kufahamu kwamba ni kipi chanzo cha ndoto yako basi Zingatia ujumbe uliomo ndani ya ndoto hiyo na ukishagundua fanya haya yafuatayo" alisema mchungaji Nikodemo na kutulia kidogo, alitazama kushoto na kulia kisha aliendelea.
"Amka omba sana, ili kama ni ndoto ya kishetani iteketee na kama ni ndoto ya kimungu basi Bwana aiendeleze halleluyaaah!!!"
Haya maneno yalimgusa na kumsisimua sana Joshua aliikumbuka tena ndoto aliyoiota usiku.
"Inabidi baadae nionane na mchungaji anipatie ufumbuzi wa ndoto niliyoiota"

Ibada ilipomalizika Joshua alimfuata mchungaji na kumueleza ndoto yake.
"Nimeota niko msituni na kushuhudia wingu jeupe likishuka kutoka mbinguni. Lilishuka hadi usawa niliokuwepo ambapo si muda nilianza kuisikia sauti yenye mwangwi ndani ya wingu lile ikinisisitiza kwamba muda umefika hivyo nifanye kazi sasa. Nilipouliza ni kazi gani,, nikaambiwa ni kuchunga Taifa la Bwana. Niliogopa sana lakini nilijikaza na kuuliza tena kwamba nitawezaje kufanya kazi ya uchungaji?? Watu watanisikiliza kweli??? Nikajibiwa kwamba Nabii hakubaliki kwao kisha nikaambiwa natakiwa niende mahali panapoitwa Tungi." alimaliza kusema Joshua.

"Oooh halleluya halleluya!!! Shukuru sana umeisikia sauti ya Bwana. Hiyo si ndoto tu bali ni uhalisia wa sauti ya Mungu ikihitaji umtumikie katika nafasi ya uchungaji. Kama ulivyoambiwa kwamba Nabii hakubaliki kwao, pengine hiyo kazi ukiifanya hapa basi watu hawatakukubali. Cha kufanya ni kwenda huko ulikoelekezwa ukajenge kanisa. Umeambiwa ni wapi???"
"Tungi" alijibu Joshua.
"MUNGU ametaka uende huko nenda mwanangu"
"Lakini Tungi si ndio mji unaosifika kwa uchawi na ushirikina mwingi!?"
"Ni kweli lakini jua kwamba uchawi hauna nguvu zaidi kuliko Bwana MUNGU wetu,, hapo hapo tambua kwamba MUNGU hawezi kukupa jukumu ambalo litagharimu uhai na uzima wako. Yeye aliyekupa kazi atakupigania kama alivyompigania Daniel katikati ya simba wakali"

Joshua alirudi kwao njia nzima akiwaza hili na lile juu ya taarifa hii iliyokuwa juu yake. Anatakiwa aende Tungi kufungua kanisa na kuifanya kazi ya Bwana lakini kila alipofikiria Tungi ndio kiboko kwa uchawi hakika aliishiwa nguvu. Pia hakuwa na hela,, Atasafirije bila nauli?? Atatumia nini kujenga kanisa hilo??? Vifaa vitatoka wapi??
Pia aliwaza ikiwa ishu ya kwenda kanisani ambapo ni karibu tu,, Mama yake huwa anagomba,, vipi atakaposikia mwanae anataka kuhama mji kwenda kufungua kanisa? Atakubali?
Mmh!! unahisi ataanzaje Kukubali? Joshua alizama katika dimbwi la mawazo.
TUNGI TUNGI TUNGI,,, Tungi ilizunguka kichwani mwake,,, Tungi yenye magwiji wa uchawi loooh!!!

Siku na miezi ilikatika na kuzaa mwaka mmoja,, bado hakukuwa na hatua kubwa iliyopigwa katika suala hili japo alijiwekea utaratibu wa kutunza vijisenti kidogo alivyopata,, alivitunza kwenye kibubu.
Hata hivyo hakuacha kuwa karibu na Mungu,, alienda kanisani kila siku za ibada yaani hakutaka kukosa. Na kwa wakati huu kipawa cha uchungaji kilionekana waziwazi yaani kuwepo ndani ya kanisa la mchungaji Nikodemo ilikuwa inafanya kanisa lionekane lina wachungaji wawili wenye nguvu.

Ilikuwa siku moja ya Jumatano, siku ambayo pia ilikuwa ya ibada kanisani kwa mchungaji Nikodemo.
Joshua alikuwa katika maandalizi ila hata kabla ya kumaliza, Mama yake aliamua kumuwakia.
"Kanisani kila siku!!!?? Kazi za hapa nyumbani zinafanyika saa ngapi???,,, Siku zinaenda tu, shamba halilimwi, unategemea nini??"
"Mbona nilisema kwamba leo hatuchelewi kurudi. Nikirudi naenda tu"
"Hakunaaa!!! Au Unataka nilime mimi na uzee huu? Marehemu Baba yako angekuwepo angenisaidia" alifoka Mama yule ndipo kwa hekima Joshua aliamua kufanya kama Mama yake alivyohitaji.
Ratiba ya kanisani aliivunja na kuchukua jembe hadi shambani.

Alitengeneza matuta mawili na kuhamia tuta la tatu,,, aliinua jembe kwa nguvu na kuchimba ila ghafla alijisikia kizunguzungu kikali na kichwa kilianza kumuuma kwa nguvu sana. Kizunguzungu kiliongezeka kadri sekunde zilivyosonga mbele hadi akaanguka huku midomo na pua yake ikitoa povu lililochanganyika na damu. Ilikuwa bahati nzuri kwamba shamba lile lilikuwa karibu na njia hivyo wapitaji walipomuona walisogea karibu ili kumbeba.
"Inatakiwa tupate machela" alisema mmoja wao maana hali ya Joshua ilikuwa mbaya sana. Kijana mwingine kati yao alitumwa kwenda nyumbani haraka kuchukua machela na kutoa taarifa kwa watu wa karibu na Joshua.

Muda mfupi baadae Mama yake na watu wengine walifika mahali alipokuwepo Joshua,,, Haraka haraka walimbeba kwa kutumia machela wakati huo Mama yake alisogea hadi mahali palipo na tuta lile. Alipotazama tu aliona kitu kilichofanya aitupe mikono kichwani mwake.
"Mama yangu!!!! Nisipofanya haraka nitampoteza mwanangu mimi!!,,, Mwanangu atakufaaa" alijisemea Mama huyu aliyeonekana kuchanganyikiwa.
Walirudi naye hadi nyumbani na kutaka kumpeleka kwa mchungaji maana hospitali ilikuwa mbali sana.
Mama yake Joshua alikataa katakata, hakutaka kuruhusu mwanae apelekwe kwa mchungaji.

Hata mchungaji Nikodemo alipopata habari hizi na kufika pale nyumbani, alifukuzwa kama mbwa yaani hata kumuona mgonjwa ilishindikana. Mama Joshua hakutaka kabisa suala hili kushughulikiwa na wachungaji kwani alifahamu fika ni nini kimetokea na anatakiwa kufanya nini.
"Mganga Simba ndiye anayejua haya mambo,,, hivi yuko wapi siku hizi?" Aliuliza Mama huyu. Alimuuliza baba yake mdogo na Joshua wakati walipokuwa wawili tu ndani.

"Yule nilisikia amehama muda mrefu sana. Niliambiwa amehamia TUNGI"
"Ohoo!!! Sasa sijui tunafanyaje?" Alisema Mama Joshua na kushika tama kisha sekunde chache baadaye aliendelea kusema
"Tutanye juu chini tumuone mganga Simba maana yeye pekee ndiye atakayeweza kumsaidia huyu" alisema Mama Joshua.
"Ni kweli sasa hela inatoka wapi?"
"Hapo sasa ndipo pananipa mawazo mwenzenu" alisema Mama Joshua na kuwaza kisha alitamka haraka.

"Nimekumbuka jambo. Huyu huwa anahifadhi hela kwenye kibubu chake. Na ameanza muda mrefu sana,, bila shaka hizohizo zitatusaidia" alisema na kuingia ndani. Alizichukua hela zile na hakika zilikuwa nyingi tu kiasi cha kuwafikisha Tungi kwa mganga na kuweza kumlipa pia.
Hawakujua kwamba hizo hela Joshua alikuwa anajiwekea akiba kwa ajili ya huduma anayotaka kuanzisha hapo baadaye huko TUNGI.

"Kama Hela zimepatikana basi usiku wa leo tutoke hapa tuelekee Tungi kumuona mganga la sivyo tutampoteza" alisema baba mdogo wa Joshua.

Itaendelea...

[emoji1241]SAFARI YA TUNGI HIYOOO,,, (TUNGI YENYE MAGWIJI WA UCHAWI)

UNADHANI NI KIPI KIMEMKUTA JOSHUA.

[emoji1241]SOMA KWA MAKINI SANA...
KUMBUKA TUNAANGALIA NAMNA ALIVYOANZA SAFARI YA UCHUNGAJI AKIMTUMIKIA MUNGU WA KWELI
FB_IMG_16547154958177668.jpg
 
Story: MCHUNGAJI MCHAWI.
Mtunzi: Nellove
Episode: 03
WhatsApp:0759941164

Ilipoishia...

"Kama Hela zimepatikana basi usiku wa leo tutoke hapa tuelekee huko Tungi la sivyo tutampoteza" alisema baba mdogo wa Joshua.

Endelea sasa...

Maandalizi yalifanyika na majira ya saa nne za usiku wenye mbalamwezi, Baba mdogo wa Joshua pamoja na vijana wanne walifika pale nyumbani. Bila kupoteza muda walimbeba Joshua na kuanza kutembea hadi mahali walipoifikia barabara, ulikuwa mwendo wa dakika 30.

Kulingana na hali ya barabara ya mahali pale, usafiri wa pekee ni pikipiki maana barabara ilikuwa mbaya yenye mashimo hivyo gari haikuwa na uwezo wa kufika kule. Mahali walipofika palikuwepo na pikipiki zipatazo mbili ambazo ziliwekewa 'order' maalumu na Baba mdogo wa Joshua.

Basi baada ya mengine machache yaliyoendelea hatimaye safari ilianza,, nao walikuwa katikati ya barabara iliyozungukwa na msitu mnene kushoto na kulia. Pikipiki iliyokuwa imembeba Joshua ilitangulia, na katika pikipiki hii walikuwa watatu yaani dereva, Joshua aliyekuwa katikati na Baba yake mdogo ambaye alikaa nyuma kwa lengo la kumshikilia. Ile Pikipiki nyingine ilimbeba Mama Joshua, nayo ilikuwa nyuma.

Safari ilihitaji umakini wa hali ya juu la sivyo ajali zingetokea mara kwa mara kwani barabara ni mbovu licha ya hivyo mara kadhaa dereva mmoja aliyekuwa ametangulia, alikuwa anaona mtu kwenye vichaka vilivyokuwa kando ya barabara, amevaa kanzu nyeupe akiwa ameshika mshumaa. Mara nyingine alimuona mtu mwingine kule mbele wanakoenda akiwa katika sanda, kichwa chake kikiwa na mapembe mawili. Huyu mtu alikuwa anacheka, na kila alipocheka damu zilimwagika pwaaah kutoka mdomoni. Dereva huyu alikuwa akijiamini hivyo hakushituka wala hakumwambia mtu yeyote.

Safari iliendelea ndipo majira ya saa 7 za usiku walifika eneo liitwalo Mlali. Hapa barabara ilikuwa nzuri tu lakini shida ilikuwa moja, magari hayakuwepo kwani ilikuwa usiku sana hivyo safari iliendelea na pikipiki zilezile.
Majira ya saa nane na nusu usiku ndipo walifanikiwa kufika Tungi kwa mganga Simba. Ajabu ni kwamba licha ya usiku ule lakini kuna watu walikuwepo kwa mganga wakisubiri kupewa na kupata kile walichokifuata hapo. Walikuwepo watu wa rika mbalimbali, vijana na wazee walikuwepo. Alikuwepo hapo Binti mzuri aliyejifunika kanga hadi usoni,, huyu binti anaitwa Fabiana.

Hata hivyo mganga huyu kwa hakika alikuwa tofauti sana na waganga wengine kwani wakati wengine wanafanya kazi yao kwenye vibanda vya miti na matope huko porini, yeye alikuwa eneo zuri tu akifanyia kazi kwenye nyumba yake ambayo ni kubwa,, kubwa,, kubwa sana na nzuri. Huyu mganga ni mtoto wa mjini [emoji3526]

Usiku huo hawakupata nafasi kumuona mganga hivyo majira ya mapema sana asubuhi iliwalazimu kuomba kuingia maana hali ya Joshua hakika ilikuwa mbaya mno kwani hata kupumua alikuwa anapumua kwa shida sana. Watu waliokuwepo hawakuwa na tatizo maana waliiona hali ya mgonjwa,,, walimuonea huruma ndipo walikubali kumruhusu aingie kwanza.

Msobe msobe alibebwa mpaka ndani kwa mganga. Ndani ya chumba kimoja alichokiteua kutumika kwa kazi yake,,, Vitambaa vyekundu na vyeusi vilitawala sura nzima ya chumba hicho alichokuwepo mganga Simba aliyekuwa amekaa chini, mkononi mwake ameshika msinga. Mwilini mwake alijifunga shuka nyekundu na kaniki nyeusi wakati huo uso wake ulipakwa vitu fulani fulani vyenye rangi nyeupe. Harufu ya dawa za kienyeji ilitawala chumba kizima kiasi cha kusumbua pua za yeyote ambaye angeingia.

"Ingiaa,, karibu ukae, ingiaa,, karibu ukae. Mlazeni hapo" aliongea mganga Simba kwa sauti yake ya kuunguruma. Waliingia na kumlaza Joshua mahali palipokuwa na shuka nyekundu kisha nao walikaa chini ndipo ukimya mwingi ulitawala pale ndani. Wakati wote huo Mganga alikaza macho kumtazama Mama Joshua hadi Mama huyu alianza kuingiwa na woga.

"Kulikoni tena" aliwaza Mama Joshua, mganga simba aliendelea kumtazama.

"Kuna picha inanijiaa" alivunja ukimya ule mganga kwa sauti yake nzito. Aliongea huku anamtazama Mama Joshua aliyekuwa amevamiwa na maswali kibao.
"Wewe ni mke wa Mushi" alisema mganga Simba.
"Tawire mganga."
"Oooh! Hahaha, picha yako imenijia kwenye kumbukumbu zangu,, ni muda mrefu sana tangu tuonane."
"Ni kweli kabisa"
"Mzee Mushi yuko wapi?"
"Ni miaka mitano sasa tangu afariki" alijibu Mama Joshua.

"Oooh! Pole sana Mama. Haya kipi kimewasibu?"
"Mganga tumekuja hapa shida kubwa ni huyu mwanangu. Ile dawa uliyonipa miaka mingi nyuma,, dawa ya kuweka zindiko shambani ndio imesababisha haya matatizo yaliyomkuta alipokuwa analima ambapo kwa bahati mbaya aliikata dawa ile kwa jembe" alitoa maelezo Mama Joshua.

"Nimekusikia Mama nimekusikia. Mmefanya vyema Kumleta kwangu mimi mwenyewe. Mngejaribu kumpeleka sehemu nyingine mngempoteza kabisa" Alisema mganga Simba na kuyatupa macho yake mahali alipolazwa Joshua kisha mganga huyu alisimama.

Tangu jana Mchungaji Nikodemo alipofukuzwa, hakutulia kabisa. Na kila alipotaka kutulia, moyo wake ulimsakama sana na kumtaka afanye maombi ya nguvu juu ya Joshua.

Usiku mzima alikuwa katika maombi, akimuomba Mungu kumponya mtumishi wake. Licha ya muda mwingi kuwa katika maombi lakini hakuchoka. Aliendelea kuomba hadi asubuhi japo sauti ilipoteza nguvu.

Akiwa katika maombi alisikia sauti yenye mwangwi ikizungumza jambo.
"Ni mzima sasa" hii sauti ilimpa tumaini kubwa hata hivyo haikuwa tamati ya maombi,,, aliendelea kuomba kwa nguvu na juhudi kubwa akiamini maombi yake yanaenda kufanya kazi bila matata.
"Nakuita Joshua, nakuita kwa jina la Yesu. Amkaaaaaaaa!!!!"

Upande huu wa pili, mganga aliposimama alichovya msinga wake kwenye chungu kidogo chenye kimiminika cha rangi nyeusi,,, alichovya na kurusha pande zote. Baada ya hapo alichukua kitambaa cheusi kilichokuwa kimefungwa vyema. Alikifungua taratibu kisha akatoa kitu mfano wa unga na kunyunyiza juu ya mwili wa Joshua.
Alifanya kitendo hicho huku akitamka maneno aliyokuwa anayasikia yeye mwenyewe. Alifanya hivyo mara saba huku akiuzunguka mwili wa Joshua.

Zoezi lake hili lilipomalizika alichukua kitambaa na kukichovya kwenye chungu kingine ambacho hiki kilikuwa na kimiminika kilichokuwa na rangi nyekundu mithili ya damu.
Alifanya hivyo na kumsogelea mgonjwa kwa lengo la kumnyunyizia na kumpaka usoni kile kitu.
Sasa bwana Wakati huu ndio wakati pekee Joshua alipohisi kusikia sauti kwa mbali ikimuita mara kadhaa.
"Nakuita Joshua, nakuita kwa jina la Yesu. Amkaaaaaaaa!!!!"

Aliisikia sauti hii mara tatu. Ajabu ni kwamba kila alipoisikia sauti hii kuna nguvu kubwa iliingia ndani yake. Nguvu hii ndiyo iliyomfanya anyanyuke kwa nguvu pale,,, alinyanyuka hata kabla mganga hajampaka ile dawa yake. Kitendo cha Joshua kuamka pale, hali ilibadilika ghafla pale ndani. Upepo mkali kama kimbunga ulivuma kwa kasi sana na haikufahamika ulitoka wapi upepo ule. Upepo huu ulivurumusha kwa nguvu na kuvitawanya hovyo hovyo vitu vyote vya mganga.

Watumishi wawili wa mganga waliingia ndani mkuku mkuku maana hali iliyokuwa inaendelea iliwatisha mno. Sauti mbalimbali ziliendelea kusikika huku mara kadhaa zikisikika sauti kama vyombo vya ndani vikigongwa gongwa kwa nguvu na sekunde chache baadae tetemeko kali la ardhi lilitawala pale yani kila kitu kilikuwa vurugu vurugu. Hofu ilitanda pale ndani hasa baada ya kuwaona watumishi wa mganga wakianguka chini na kuanza kutapatapa ,wakitokwa na povu mdomoni huku wametumbua macho yaliyokuwa mekundu kama damu.

Mganga alitoa macho kwa mshituko na hasira, asijue la kufanya, na hata wakati alipojua la kufanya na kuchukua kibuyu fulani kilichokuwa kushoto kwake kile kibuyu kilimeguka na kusagika sagika, alipochukua dawa zake zilibadilika na kubaki vumbi na alipotaka kulazimisha mambo kwa kutumia ujuzi na utaalamu wake alishangaa ghafla kuna kitu kinamsukuma na kumtupa chini kwa nguvu aliyoshindwa kuihimili.

Mganga Simba alianguka chini na kama ilivyokuwa kwa watumishi wake alitapatapa huku povu likitoka mdomoni na puani pamoja na damu zilizokuwa zinatoka kwenye masikio na machoni. Kelele zilikuwa nyingi mno pale ndani, kelele zilikuwa za aina tofautitofauti. Kelele za maumivu, vilio pamoja na maombi yaliyokuwa yakifanywa na Joshua. Sauti ya maombi Ilisikika zaidi na kusambaa hadi nje kulikokuwa na wateja waliokuwa kumi kwa idadi. Nao hawakuacha kushangaa,,, ama hakika walipigwa na butwaa,, "Makubwa haya!! Leo Mganga anaponya watu kwa maombi"

Kila mmoja alikuwa na shauku ya kujionea maajabu haya yanayoendelea huko ndani hivyo mkuku mkuku waliingia ndani na kushangazwa na kila walichokiona. Kila kitu kilitawanyika hovyo, watumishi pamoja na mkuu wao walikuwa chini hawajiwezi. Joshua aliendelea na maombi.

"Naharibu ngome zote za kichawi zilizojengwa na kusimikwa mahali hapa kwa jina la Yesu. Mapepo na mizimu yote iliyotawala eneo hili na watu wa hapa naiteketeza kwa moto Yesu kristo. Na sasa kwa mamlaka niliyopewa naamuru uponyaji kwenu nyote mliopo hapa" alitamka hayo na kushuhudia wengine wengi pamoja na Mama yake wakianguka kisha baadaye kidogo walisimama wakiwa wamepona kabisa.

Dakika kadhaa mbele nao watumishi wa mganga walisimama wakiwa sawa kabisa na baadae kidogo mganga naye alisimama na kutazama huku na huku mithili ya mtu mwenye kuweweseka. Zilipita sekunde kadhaa tangu asimame na kushangaa shangaa,,, akili zilipokaa sawa alizungusha macho yake kwenye chumba chake kile. Alishangaa kuona jinsi kilivyoharibiwa pamoja na vitu vyake vingi vya kiganga kutawanyika hovyo hovyo. Baada ya kutazama sana hivyo vitu alimgeukia Joshua na kumsogelea haraka.

"Wewe ndiye uliyefanya haya?" Aliuliza mganga akiwa amekaza macho.

#Ikikupendeza like&share

[emoji257]UNAHISI NINI KITAENDELEA?

[emoji1241]KUMBUKA BADO TUNAIANGALIA SAFARI YAKE YA UCHUNGAJI.

Tukutane katika #Episode04

FB_IMG_16547154958177668.jpg
 
Back
Top Bottom