Simulizi: Mimi na Mimi

"Yoyote atokae kwake tayari kwenda kulima: akageuka nyuma basi hafai kwa ukulima......"


Kama nimekosea mtanisamehe
 
Dah kuwa mrembo ni raha sana bwana sauti moja tu mwamba huyu hapa. Mama ujengewe sanamu hakikisha hupotei kwenye huu uzi maana ukipotea tu jua litatuwakia
Hahahahaha Dah! Kweli, maana sisi tulibembeleza siku nzima na nusu lakini wapi, Warembo tuwape maua yao
 
Halafu huyu Elton Tonny ameishatufanya kama mateja, hajui tu maana tulishawajenga vichwani akina Ankia, Tesha Miriyam, Mariam, Bertha na wengineo tunawaona kabisaaa akilini so asipotupa episode tunawamiss pia au uwongo jamani?
 
KAMA KUANDIKA BRO UNAJUA.
 
MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA THELATHINI NA SABA

★★★★★★★★★★★★★★★★★★★


Miryam akaendelea tu kuniangalia machoni, huku uso wake ukionyesha aina fulani ya msisitizo kunielekea, nami nikawa naona namna ambavyo watu wengi kwa upande wa eneo hilo walitutazama sana kutokana na jinsi hali hiyo ilivyotengeneza picha fulani utadhani ilikuwa ni ishu ya mapenzi na mafumanizi.

Akiwa ameendelea kunishika tu mkononi, akasema, "Kaka, nakuomba... naomba tuongee..."

Dah! Yaani kwa jinsi ambavyo sauti yake tamu ilitamka maneno hayo nikahisi kulegea kabisa. Ilikuwa ushawishi tosha kwangu hata kama angeniambia niahirishe kupanda daladala, nisingempinga! Natania tu, ila niliipenda sana sauti yake.

Lakini nikaendelea tu kumwangalia usoni, nikijiuliza ni kipi ambacho mwanamke huyu mtu mzima angetaka kuzungumza na mimi kwa uharaka sana mpaka kikamtoa jasho namna hiyo. Huenda kuna kitu alikuwa anataka kuniambia kuhusu mdogo wake, na labda alikuwa kwenye maeneo haya kutokea kwa mwenyekiti ndiyo akapata kuniona na kuniwahi kabla sijaondoka.

Nikiwa namtazama kwa macho yenye utulivu tu, nikatikisa kichwa kukubali ombi lake, naye ndiyo akaniachia taratibu huku akijifuta jasho sehemu ya paji la uso wake mpaka shingoni kwa kitambaa chake. Alikuwa amevaa T-shirt jeupe la mikono mifupi ambalo lilimbana kiasi, huku kutokea kiunoni akijifunga kwa kimtandio fulani laini kufikia kwenye hips kilichoonyesha kwamba alikuwa amevalia suruali nyeusi yenye kubana pia ndani mwa umbile lake la miguu, pamoja na ndala nzuri za kike miguuni. Nywele zake kichwani alizibana kwa juu, zikiwa na ulowani kiasi kwa mbele na kudondokea pande za uso wake alipojipangusa kwa kitambaa.

"Naomba tukakae sehemu tuongee..." akaniambia hivyo.

Nikatazama pembeni kiufupi, nikiwa nawaza sehemu ipi ingefaa kukaa pamoja naye na kuzungumza, nami nikaona moja iliyofaa. "Twende pale," nikamwonyesha sehemu hiyo.

Ilikuwa pale ambapo siku ya kwanza kabisa kuamkia huku Mbagala mimi na Ankia tulienda kununua chakula baada ya kutoka kwenye ofisi ya mwenyekiti kuhalalisha ishu yangu ya upangishwaji, hivyo mimi na Miryam tukaanza kuelekea upande huo.

Siyo wapita njia, siyo bodaboda, yaani karibu kila mtu aliyetuona hakuweza kujizuia kututazama, jinsi ambavyo mwanamke huyu alikuwa amejaliwa sura nzuri na mwili wenye kuvutia, na mimi nilivyokuwa na mwonekano mzuri pia, ilikuwa ni kama tumefika eneo hilo la Mzinga kwa wakati huu ili kulipendezesha kama siyo kujionyesha tu.

Ila kuna wengine walikuwa na macho ya husuda yaani, mtu anakuangalia hakumalizi utadhani wewe ndiyo kitu ambacho kingemnyima usingizi! Ilikuwa muhimu sana kutotazama yeyote kati yao maana si wote wakuangaliao sana wanakuwa wamekupenda, kwa hiyo nikamfikisha bibie sehemu hiyo na kwenda kukaa pamoja naye kwenye viti vya plastiki upande mmoja wenye meza ya chakula.

Kwa sababu ilikuwa ni lazima kuhudumiwa kwa kuonekana kuwa wateja, akawa amekuja mhudumu mmoja wa hapo na kutuangalia kwa subira, nami nikamtazama Miryam machoni.

Nikamwambia, "Agiza chochote dada, nita..."

"No, wewe agiza, nitalipia," Miryam akanikatisha kwa kusema hivyo.

Kulikuwa na hali fulani hivi ya uajabu katika haya yote, nami nikawa nimezubaa kiasi na kuendelea kumwangalia usoni utadhani nilikuwa namtafakari ama sikutaka kutii alichopendekeza.

Yeye akaacha kuniangalia na kumwambia mhudumu, "Soda. Naomba niletee soda ya Pepsi... na mishikaki."

"Mingapi?" mhudumu akauliza.

"Miwili tu," Miryam akajibu.

Nikaacha kumtazama baada ya yeye kusema hivyo, nami nikamwambia mhudumu, "Pepsi pia. Basi."

Huyo dada akaenda zake, nami nikawa nimetulia tu baada ya kuliweka begi langu kwenye kiti cha pembeni, nikisubiri kumsikiliza mwanamke huyu. Lakini nilipomtazama, nikakuta ameinamisha uso wake kiasi kwa njia iliyoonyesha huzuni sana, kisha akaweka mikono yake mezani na kuviunganisha viganja vyake vyeupe huku akinitazama kwa utulivu.

"Ulikuwa unarudi nyumbani?" akaniuliza hivyo kwa sauti ya chini.

"Siyo nyumbani. Ni kwa rafiki tu. Naenda kufanya mishe fulani, halafu...." nikaishia hapo.

"Halafu?" akauliza.

Niikatulia nikimtazama machoni, kisha nikasema, "Halafu ndiyo mengine yatafata. Labda nitaua muda huko mpaka likizo yangu ikiisha then... nitarudi kazini."

Mhudumu akawa ameleta soda zetu na mishikaki, naye Miryam akaendelea tu kuniangalia kama vile anasubiria niseme kitu kingine.

Nikamwambia, "Nilipita pale home kuaga ila nikakuta umetoka, kwo'..."

"Unaondoka kwa sababu ya kila kitu kilichotokea, eti?" akauliza.

"Hapana. Yaani..."

"Hasa kwa sababu ya yaliyotokea baina yangu mimi na wewe."

"Hapana Miryam, usifikirie hivyo. Siondoki kwa sababu hizo."

"Ndiyo, najua ni lazima useme hivyo, ila naelewa vizuri sana kwamba hilo siyo kweli. Najua unaondoka kwa sababu nia yako imechoka. Haujachoka kumsaidia Mariam, hilo umeonyesha wazi, lakini... nia yako nzuri ndiyo imechoka... na sababu ni mimi," akasema hivyo kwa sauti tulivu.

Nikawa nataka hata kumwambia hapana, siyo jinsi ambavyo alifikiria, lakini nikabaki kimya tu na kuendelea kumwangalia usoni.

"Kaka... ninaomba unisamehe," akasema hivyo.

Sauti yake ilibadilika kiasi aliposema hivyo na kuwa kama vile anaibana kwa makusudi. Nikaelewa kwamba alikuwa anajitahidi kuficha kilio, na hilo likanitia simanzi.

Akaendelea kusema, "Nisamehe kwa sababu... toka mwanzo, sikukuelewa vizuri. Unajua... umekuwa ukinisaidia sana, lakini shukrani niliyokupa kwa msaada wako wote ilikuwa mateke tu. Na ulikuwa sahihi. Mimi nilidhani naona kila jambo nililofanya kuwa sawa, kwamba kila kitu kingeenda kama nilivyotarajia, lakini... ukweli ni kwamba nilikuwa nimejaa kiburi tu... mpaka sasa..."

Nikatazama mezani tu baada ya yeye kusema hivyo, kwa sababu simanzi yangu ilizidi kutokana na kuangalia namna macho yake yalivyojaa machozi aliposema hayo.

"Hhh... nitakwambia kitu fulani. Sijawahi kumwambia mtu yeyote, ila... kilichokuwa kinafanya kiburi changu kikue zaidi, mpaka kunigeuza kuwa kama kipofu nisiweze kuona ukweli wa mambo aliyofanya Joshua... ni sababu tu nilitaka kutimiza ahadi," akaniambia hivyo.

Nikamtazama machoni.

"Kabla ya wazazi wangu ku.. kuaga dunia... baba yangu alitamani sana familia yetu iwe na muungano, na akafikiri kutugawia mali mapema kungetupa furaha, na amani... hasa kutoka Joshua. Ila baada ya kufanya hivyo, alitambua amani ya kweli ingepatikana si kwa kuwatenganishia furaha watoto, bali kwa kuwawekea misingi ya ukaribu ili wajifunze kuikuza zaidi wakiwa pamoja. Sikutaka chochote kabisa, hata kama angeamua kumpa Tesha, au Mariam, au Joshua, au nani, chochote ambacho kilikuwa chake, isingekuwa na shida kwangu. Ni matendo ya Joshua ndiyo yalimfanya baba aumie kwa sababu ya kutoa kila kitu mapema, na ilikuwa imechelewa kubadili mambo tena. Hata mimi nilichukizwa sana na matendo ya Joshua, sikutaka kuhusiana naye kwa lolote baada ya yeye kuonyesha hajali familia... lakini baba... akaniomba...." akaishia hapo na kuangalia chini.

"Akakuomba umwahidi kuipigania amani ya familia yenu?" nikamuuliza.

Akajifuta chozi na kusema, "Siyo kupigania... ila tu nisijitenge na familia. Sikuwa naishi huku. Ningeendelea kuwa na kazi niliyokuwa nayo, ningeendelea kuishi nilipokuwa naishi, yaani, kama ni haya mambo ya sijui Joshua kafanya nini, mara mama au baba kaniambia nini, ingekuwa kwa umbali niliojiweka kutoka kwao. Namaanisha... nilitaka yawe ya kusikika tu, kama wakihitaji msaada kwa hiki au kile, ningejitahidi kushiriki kwa lolote, lakini sikutaka kabisa kuwa karibu na hayo mambo. Nilifikiri maisha yangekuwa rahisi tu kwa upande wangu nikifanya hivyo, lakini wazazi wetu walipofariki ghafla... ndiyo nikagundua kwamba nilikuwa mbinafsi sana. Labda ndiyo ilikuwa njia ya Mungu ya kunifundisha..."

"Hapana Miryam, usiseme hivyo. Kilichowapata haikuwa makosa yako," nikamwambia hivyo kwa upole.

"Najua. Lakini ndiyo iliniamsha. Iliniamsha ili niache kuishi kwenye ulimwengu wa ndoto niliodhani ulinifaa, ili nibebe majukumu ya kutunza wanafamilia wangu. Na kwa kweli... nilikuwa tu nikiyaepuka. Nawapenda wadogo zangu, mama zangu, lakini kabla ya vifo vya wazazi wetu... labda tu na me nilikuwa najipenda mwenyewe mno kupita kiasi, ndiyo maana walipofariki... ilinibidi kuacha. Ilinibidi niugawe huo upendo niliokuwa najipa mwenyewe kwa ndugu zangu, wote... kutia ndani Joshua..." akasema hivyo.

Nikabaki namwangalia tu kwa utulivu. Ilikuwa imeshaeleweka zaidi sasa kwangu kwa nini mwanamke huyu alijitahidi sana kutafuta amani kwa kuwaunganisha ndugu zake wote wa karibu. Ili tu kuenzi hitaji la wazazi wake, alikuwa tayari hadi kufumbia macho visa vya kibinafsi vya Joshua kufanikisha hilo, na kwa hapo nikawa nimeelewa ni namna gani alivyokuwa mwanamke mwenye uthamini wa kina sana kuelekea vitu kama ahadi.

Akaendelea kusema, "Nimemwona Joshua akiwa mchanga, nimemwosha, nimemfunza kutembea, mpaka anaanza shule nimekuwa pamoja naye. Alikuwa kijana mzuri sana. Jinsi ambavyo tulilelewa labda, na nyutu zetu kuwa tofauti tu na malezi na watu tuliojichanganya nao, labda ndiyo sababu iliyofanya akabadilika... lakini sikukaa kuwaza hata siku moja kwamba angeweza kumfanyia Mariam kitu kama hicho..."

Miryam akaanza kudondosha machozi aliposema hivyo, akiongea kwa kuukaza uchungu mwingi aliokuwa akihisi.

"Hhh... nilikuwa natumaini labda... kweli... mema yanaweza kuushinda uovu.... na ndiyo maana hata Joshua alipofanya visa vingi vya ajabu, nilisamehe... nikitarajia ipo siku angeona nguvu ya wema ambayo ingemfanya abadilike. Alipoanza kufanya... ohh God... alipoanza kufanya hayo maigizo... nilifikiri subira yangu ndiyo imezaa matunda... kwamba nilikuwa... nilikuwa nimefanikiwa kumfanya abadilike, na hivyo nilete amani ambayo wazazi wetu walitaka... ahh..."

Miryam akawa anajifuta machozi na kujitahidi sana kujikaza, nami nilikuwa namwonea huruma mno. Nilitambua pia kuwa watu wengine waliokuwa wameketi sehemu za pembeni walitutazama sana kutokana na kutoelewa kilichomliza bibie, lakini sikujali maoni yao hata kidogo. Fikira zangu zote zilikuwa kwa huyu mwanamke.

Akajikaza zaidi, kisha akaniangalia kwa uimara na kusema, "Nimejifunza. Kwa mara nyingine tena... nimejifunza. Sitarudia... KAMWE... kuendekeza kiburi nikijiaminisha kuwa natafuta amani."

Nikaangalia chini kwa huzuni.

"Joshua ametumiwa kunipa somo kubwa. Sitaki tena kuamini mtu kisa tuna-share damu. Undugu hauko kwenye damu tu. Sitapata ndugu wa kweli wa kusimama pamoja nami katika yote kwa kuangalia damu, wala ukoo, wala muda tu tuliojuana, no... nitapata ndugu wa kweli... kutoka kwa mtu kama wewe," akaniambia hivyo.

Nikamwangalia usoni.

"Wewe ni zaidi ya ndugu kaka yangu. Kama mama mkubwa anavyosema, wewe ni baraka katika familia yetu. Ni upumbavu tu ulionizuia kuliona hilo na kukuchukulia kama... ahh... naomba nisamehe. Nakuomba unisamehe sana kaka yangu," akaongea kwa hisia.

Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanakimbia kwa kasi mno, nami nikashindwa hata kuongea na kutazama tu chini.

"Najua nilikutendea bila heshima. Haukustahili kila kitu nilichokufanyia, au maneno niliyokwambia. Nakuomba tafadhali unisamehe... na... ninakuomba usiondoke..." akaniambia hivyo.

Nikamtazama machoni kwa mara nyingine tena, zamu hii nikiwa kama vile nataka kusikia vizuri zaidi kile alichotoka kusema.

"Mariam bado anakuhitaji. Sana. Wewe ni... umeweza kumfanya awe sawa tena, ukiondoka ata... naogopa hali yake itakuwa mbaya sana. Hatakuwa sawa tena na mtu mwingine kwa sababu ameshakuzoea wewe, sikuliona hilo ndiyo sababu... siku... hhh..."

Dah, alikuwa anatia huruma! Mie hapo nikawa najikaza tu kiume ili hisia zangu zisinilazimu kutoa chozi.

"Najua sina haki... hhh... sina haki ya kukuomba hili, ila tafadhali. Usiondoke kaka yangu. Please," akaniomba kwa upole.

Mkono wangu mmoja ulikuwa mezani, naye akakiingiza kiganja chake kwenye kiganja changu na kukishikilia kama kuweka msisitizo.

Nilipatwa na hisia za kulemewa kiasi kutokana na kutafakari mengi yaliyokuwa yakiendelea kupingana na ombi la mwanamke huyu. Hapa ndiyo nilikuwa njiani kuondoka kabisa kuepuka hizi drama za maisha ya familia ambayo hata haikunihusu, lakini bado zikawa zinanivuta ili niendelee kubaki. Miryam alikuwa anajua kuteka hisia, siyo poa. Aliniangalia kwa macho yenye huzuni yaani, ah! Ungemwona!

Sekunde chache za ukimya kutoka kwangu zilitosha kumwambia kuwa nilikuwa nafikiria la kufanya, naye akasema, "Najua una mambo yako pia, na... sitaki ionekane kama, yaani... nataka kusema hata ukiona uhitaji wa... ku... kulipwa, nitakulipa. Sitaki uhisi nimekukosea heshima lakini, najua hukumsaidia Mamu ili ulipwe, ila... namaanisha tu... tupange lolote lile unaloona linafaa, maadamu tu ubaki kumsaidia mdogo wangu."

Nikawa namtazama tu usoni.

"Chochote kile unachotaka, kilicho ndani ya uwezo wangu, tafadhali. Mariam anakuhitaji sana," Miryam akasema hivyo.

Nikashusha pumzi kiasi, kisha nikasema, "Sawa."

Nikaona uso wake ukigeuka na kuwa wa matumaini.

"Nitabaki," nikamwambia.

Huku akiwa amenishikilia kiganja bado, akasema, "Asante. Asante sana. Kwa lolote lile utakalohitaji, niam...."

"Actually, ndiyo, nitahitaji malipo kumweka sawa huyo dogo. Aaa, sijui tufanye kwa kila mwezi, eh?" nikamkatisha kwa kusema hivyo.

Hakutarajia niongee hivyo bila shaka, lakini akasema, "Sawa. Ni sawa. Utataka shi'ngapi kwa mwezi?"

"150," nikamjibu.

"150?" akauliza kwa umakini.

Nikaachia tabasamu hafifu ili atambue jambo fulani. Baada ya kutambua kuwa nilimtania tu, Miryam akaniangalia kwa utambuzi na kutabasamu kiasi pia.

Nikamwambia, "Usijali. Natania tu. Sihitaji malipo. Nitabaki kumsaidia mdogo wako kwa sababu nampenda kama mdogo wangu pia. Atakuwa sawa tena. Kuwa na amani."

Akabaki akinitazama kwa utulivu, naye akasema, "Nashukuru sana."

Kuna kitu kilichokuwa kinafanya nipate hisia ya uvuguvugu, joto laini moyoni, kama vile tu mara ya kwanza kabisa mwanamke huyu aliponikumbatia usiku ule nimemsindikiza Tesha kwao tulipotoka kunywa, na hisia hii ilinitia amani sana. Ilinifanya niendelee kumtazama tu, ikiwa kama vile sehemu yote kutuzunguka ilipunguzwa sauti mpaka mwisho na ni sisi wawili pekee ndiyo tuliokuwa hapo.

Tuliendelea kuangaliana machoni kwa muda wa sekunde nisizofahamu idadi lakini ilionekana kama tumemaliza dakika kabisa, na ndipo hisia hiyo ikakata baada ya Miryam kukiondoa kiganja chake kutoka mkononi mwangu. Ikawa kama sauti zimerudi tena, nami nikajisawazisha vyema kwa jinsi niliyokuwa nimekaa na kuvuta soda yangu kama zoba vile. Sijui nini kilikuwa kinanipata yaani!

Sikuwa na kiu ya soda wala, ila nikaanza kuishusha taratibu huku bibie Miryam akifanya hivyo hivyo kwa yake pia. Hisia kali za uchungu alizokuwa nazo wakati akizungumza nami dakika chache nyuma zikawa zimetulia zaidi wakati huu. Akauliza kuhusu mishe niliyokuwa naenda kufanya kwa rafiki yangu, ikiwa ilikuwa na umuhimu sana, nami nikamwambia hapana, haikuwa na umuhimu kupita umuhimu aliokuwa nao Mariam. Na hata hivyo bado sikuwa nimemaliza matumizi ya kodi ya kukaa kwa Ankia niliyokuwa nimeshalipia, kwa hiyo ingekuwa vizuri sana kurudi tena pale.

Nikawa nimemuuliza kuhusu hali ya Mariam, aliendeleaje pale hospitali, na ikiwa kuna chochote ambacho daktari aliongea naye, ndiyo akaniambia kwamba alikuwa ameshamtoa Mariam kwenye ile hospitali pale juu na kumpeleka kwenye hospitali nyingine kubwa maeneo ya Kijichi kule; iliyokwenda kwa jina la Epiphany. Daktari yule kutoka kwenye hospitali ya kwanza tuliyompeleka Mariam alikuwa amezungumza naye kuhusiana na ile ishu tulipodhania binti huyo alibakwa, na ndiyo Miryam akawa amempeleka mdogo wake kule Epiphany kwa vipimo bora zaidi.

Akasema kwamba binti aliamka ile jana mapema tu, lakini mpaka wakati huu hajaweza kusema lolote. Matabibu wa huko walikuwa wamemwambia ni ile hali ya mshtuko aliyokuwa nayo Mariam ndiyo iliyosababisha asiongee wala kuitikia lolote kutoka kwa ndugu zake walipomsemesha, lakini Miryam akawa ameamua kunitafuta ili nifanye miujiza yangu kumtoa binti katika hali hiyo kwa kuwa alijua ni mengi zaidi yanahusika kupita hali ya kupata tu "mshtuko."

Yeye pamoja na mama zake walikuwa na mpango wa kwenda hospitalini mida hii hii alipotoka kwa mwenyekiti, hivyo akawa ameniomba niambatane naye kwenda kumwona binti pia, nami nikakubali hilo. Wakati huu nilikuwa na utayari wote wa kumwona Mariam tena.

Miryam hakuacha kunishukuru kwa utayari wangu wa kutoa msaada kwa mdogo wake na kusema hata kama sitaki malipo lakini atakuwa ananipa kiasi chochote kile anachoweza kama shukrani tu, na nisikatae la sivyo angejihisi vibaya. Hakutaka kumzungumzia Joshua hata kidogo tena, sote tukijua jamaa amesondekwa huko rumande, kwa kuwa umakini wake wote Miryam kwa wakati huu alitaka uwe kwa Mariam tu. Kwa kumwelewa mimi nikaridhia yote, nasi tukapoza koo zetu kwa soda mpaka kumaliza, kisha akalipia na sote tukanyanyuka.

Tukaanza kuondoka na kutembea pamoja kurudi tena kule Masai. Huku begi langu likiwa upande wa kushoto mgongoni, nilitembea pembeni ya mwanamke huyu huku nikiona namna ambavyo jamii ya Mzinga ilitutazama kana kwamba tulikuwa tumependeza sana ama kitu gani, lakini sisi kwa pamoja tulijali tu safari yetu ya kurudi maskani bila kuhangaika na watu.

Kutembea na Miryam ilinifanya nijihisi ugeni fulani hivi. Hatukusemeshana tena yaani, lakini mara moja moja tungeangaliana na kuendelea tu na safari yetu fupi taratibu. Hata kuna sehemu fulani tukawa tumewapita watoto wakiwa wamekaa nje ya saluni na baada ya wao kutuona, mmoja akasikika akisema 'mkaka handsome,' na mwingine akadai 'eeh, na mke wake.' Nilijikausha tu kwa kufanya kama vile sijali walichosema, lakini niliweza kuona namna ambavyo Miryam alitabasamu kiasi kwa chini kuonyesha kwamba utani ulikuwa umemwingia. Hata mimi nilijihisi vizuri, na ile hisia ya uvuguvugu (warmth) ilikuwa ikinipata sana moyoni kwa wakati huu.

Amani tu ilikuwa inajijenga ndani yangu kwa kuhisi nimechukua uamuzi sahihi, hata kama nilijua kwa upande wa Bertha suala hili lingeweza kuzua utata. Lakini Bertha angeshughulikiwa baadaye, kwa sasa nilitaka kuangalia kile kilichokuwepo mbele yangu na kutimiza haja ya moyo wangu. Ndiyo. Nilikuwa nimeamua kuufata moyo wangu, kitu ambacho nilikuwa nimehofia kwa muda mrefu kufanya, sasa nikawa nimekifanya. Itaeleweka baadaye ni kwa nini.

★★

Kwa hiyo mimi na bibie Miryam tukawa tumekaribia kuzifikia nyumba za makao yetu baada ya kupapita Masai Bar. Tukiwa ndiyo tumelikaribia duka la Fatuma pale kwa Ankia, kiganja chake Miryam kikawa kimegusa cha kwangu mikono yetu ilipokaribiana kwa kutembea kwa ukaribu.

Mimi nikadhani alinigusa kwa makusudi ili labda anisemeshe, kwa hiyo nikauangalia mkono kwanza na kisha kumwangalia yeye upesi usoni. Yeye pia akanitazama usoni na kusimama kabisa, akionekana kusubiri niongee. Kulikuwa na kahisia ka roho kudunda kwa nguvu kiasi kutokana na jinsi ambavyo tuliangaliana, na ikawa wazi kwamba hakuwa amenigusa mkononi kwa kusudi.

Nikamwambia, "Nilifikiri unataka kunisemesha."

"A... hamna... mikono tu imegusana," akasema hivyo kwa sauti yake tamu kama asali.

Nikatikisa kichwa kukubali, nasi tukasonga mbele mpaka kufikia usawa wa geti la nyumba yake Ankia. Hakukuwa na watu wengine kwa nje kutokana na muda kuwa saa saba, si unajua, jua kali, ama labda ndiyo ulikuwa muda wa kutulia ndani kwa ajili ya misosi.

Miryam akanitazama na kusema, "Kwa hiyo... naenda kujiandaa, halafu... tutaenda pamoja, si ndiyo?"

"Ndiyo. Nakuja sasa hivi, ngoja nikaweke begi," nikamwambia hivyo.

"Sawa. Asante," akasema hivyo na kisha kuelekea kwake.

Nikatulia kidogo nikimwangalia kwa hisia fulani hivi, lakini nikaona niachane nayo na kuelekea tu ndani kwa Ankia.

Wazia ni jinsi gani ambavyo mwanamke huyo alifurahi sana nilipoingia ndani na kumwambia ndiyo nimerudi! Alijaa shangwe tele yaani. Akauliza ni nini ambacho kilifanya nikaamua kubadili mawazo yangu, na ndiyo nikamwelezea kwa ufupi kuwa nilikutana na Miryam Mzinga muda mfupi nyuma, na ndiyo akafanya kunishawishi nirudi ili niendelee kumsaidia mdogo wake. Ankia akasema sasa alielewa mambo vizuri.

Akaniambia kwamba muda ule nilipokuwa nimemaliza tu kuwaaga wakina Bi Zawadi na Bi Jamila na kuondoka, Miryam ndiyo akawa amerudi kutokea kule kwa mwenyekiti; ikionekana tulikuwa tumepishana kidogo tu. Ndiyo wakawa wamemwambia kwamba nilienda hapo kwao kuaga, na kilichofuata ikawa ni Miryam kuondoka tena bila kuwaambia anaenda wapi. Kwa hiyo inaonekana mwanamke huyo alinikimbilia na kuniwahi kabla sijapanda daladala ili ndiyo aniombe msamaha na kunishawishi nirudi. Dah!

Nikawa nimeelewa sasa, nami nikamwambia Ankia kiukweli Miryam alinigusa mno kwa maneno yake mpaka nikahisi hakuna njia ya kutoroka tena, naye akacheka kidogo kwa kuelewa nilikuwa natania tu. Ndiyo nikamjulisha kwamba tulikuwa tunaenda kumwona Mariam kule hospitalini alipokuwa kwa wakati huu, na kama angependa kuja basi twende naye.

Ankia hakukawia kukubali, maana hata yeye alitaka kwenda kutoa support ya kihisia kwa binti, hivyo akaenda kutupia T-shirt na kujifunga kitenge safi kwa chini, pamoja na kilemba kichwani. Mimi nilikuwa na mwonekano wangu safi bado kwa hiyo tukafunga tu nyumba na kuelekea kwa majirani zetu.

Mama wakubwa walifurahi sana, sana kuniona tena. Upesi tu baada ya mimi kuingia ndani humo nikaanza kuwatania kama kawaida yetu kwa kuwasifia jinsi walivyokuwa warembo wakifurahi, naye Bi Zawadi akanikumbatia kabisa kwa furaha. Wakawa wananiambia jinsi ambavyo Mariam angefurahi sana kuniona na walijua ningeleta maajabu yangu ili binti huyo arejeshe hali nzuri kwa afya yake, na ndiyo Miryam akaja mpaka sebuleni kutokea chumbani.

Inaonekana alioga kabisa, na sasa alikuwa amebadili mavazi yake kwa kuvaa blauzi nyeupe na sketi ndefu iliyochanua kufikia miguuni, na kichwani alizibana nywele zake kwa juu. Kwa wakati huu, nilipenda sana kumtazama. Kwa nini, kwa sababu yaani yeye aliponiona tu na kunitazama pia aliachia tabasamu hafifu la kirafiki kunielekea, kwa hiyo nilijawa na amani sana kumwangalia. Ilikuwa inanipa motisha, hata sijui ya nini, lakini ilikuwepo.

Kwa hiyo baada ya yeye kufika hapo, nikawa nimemwambia kwamba Ankia angekuja pamoja nasi ikiwa hangejali, naye akasema haikuwa na shida kabisa na hata kushikana viganja na Ankia kirafiki. Mama wakubwa wangekwenda hospitalini pia, hivyo kwa kuwa wote tulikuwa tayari, milango ikafungwa na Miryam akalitoa gari lake mpaka nje, kisha mama wakubwa na Ankia wakaenda kupanda. Nilipokuwa nimemaliza kufunga geti kwa nje na kuliloki, nikaelekea garini kukuta nimeachiwa siti ya mbele na wanawake ili nikae pembeni yake Miryam, nami nikaingia tu na safari kuanza.

★★

Tukiwa mwendoni kuelekea huko ndiyo Miryam akawa amemfahamisha Ankia kuwa Mariam alikuwa kwenye hospitali iitwayo Epiphany hapo maeneo ya Kijichi si mbali sana na alipofanyia kazi. Ankia akadokeza kuwa aliifahamu ila kwa kuipita tu kipindi cha nyuma alipokwenda dukani kwa Miryam, na aliikumbuka kuwa kubwa pia. Mie nikaendelea kutulia kama sipo vile.

Tulipofikia maeneo ya Zakhem, Miryam akasimamisha gari kwanza ili aelekee kwenye mgahawa mmoja hapo wa kisasa ili anunue chakula ambadho alitaka kuwapelekea wadogo zake. Kukaa kwa dakika kadhaa ndani ya gari huku nikiwasikiliza mama wakubwa na Ankia wakizungumza kuliongeza kiwango cha uradhi kilichokuwa kimeanza kuwepo moyoni, nami pia nikawa naongea pamoja nao mpaka bibie Miryam aliporejea.

Alikuwa na mifuko yenye vyakula na matunda, na inaonekana alinunua vingi kiasi kwa ajili yetu sote ili tukifika kwa Mariam tushiriki mlo pamoja naye. Nikauliza ikiwa hilo liliruhusiwa pale kwenye ile hospitali, lakini Miryam alionekana kuwa na uhakika kabisa kwa kusema haingekuwa na shida. Nilipenda sana jinsi ambavyo alinijibu moja kwa moja na kwa heshima, ikionyesha alitaka kunitendea kwa usawa, na alitaka nilione hilo.

Kwa hiyo mwendo wa dakika chache baada ya hapo ukawa umetufikisha hospitalini, na ilikuwa kubwa sana, ya kibinafsi. Jengo hilo lilibeba maghorofa yenye vyumba vipana na kuzungukwa na vioo vizito vilivyolifanya kuonekana kuwa maridadi, na baada ya kuegesha gari lake, Miryam akatuongoza kuelekea upande wa ndani mpaka kufikia kwenye lifti, kisha tukapandishwa kufika ghorofa la tano.

Inawezekana hapa hapakuwa na sheria sheria za kuwabana waliofika kama kwenye hospitali zingine, kwa kuwa baada tu ya kufika huko juu Miryam akatuongoza mpaka kufikia kaunta la mapokezi na kuongea na muuguzi-mhudumu kumjulisha kwamba tulikuwa tunaelekea kwenye chumba fulani, na huyo muuguzi akawa amemtikisia tu kichwa kukubali.

Bibie akatuongoza, tukipita vyumba vichache kwa pande mbili za korido refu, na kulikuwa na watu wengi ambao ndiyo walikuwa wamefika na kuingia chumba hiki au kile, ikionekana kuwa mida ya kutembelea wagonjwa. Ndiyo kwenye mlango wa tano mbele yetu akaonekana Tesha akitoka na kutuona pia. Akakutana nasi na kunifata moja kwa moja mpaka kunishika begani huku akiwa anatabasamu kiasi, naye akawaamkia mama zake wakubwa. Macho yake yalionekana kupona kwa muda huu.

"Dah, kaka bora umekuja. Ulitoweka ghafla mpaka nikafikiri haurudi yaani," Tesha akaniambia hivyo.

Nikatabasamu tu kiasi na kumshika begani pia.

"Vipi, Mamu amelala?" Miryam akamuuliza.

"Hamna, yuko macho. Nilikuwa naenda kukojoa, ila... sa'hivi umeshakata," Tesha akasema hivyo.

"Kisa?" Ankia akauliza huku akitabasamu.

"Si nimemwona JC? Niende chooni kufanyaje sa'?" Tesha akasema hivyo.

Mama wakubwa wakatabasamu pamoja na Ankia.

Bi Jamila akamuuliza Tesha, "Anaendelea vizuri lakini? Ameshakusemesha?"

Tesha akatikisa kichwa kukanusha na kusema, "Alivyo kama jana tu, sema JC najua umefika atafurahi sana... ataongea tu."

"Kweli," Bi Jamila akasema hivyo na kunishika begani.

Nikampa tabasamu hafifu, nami nikamtazama Miryam na kukuta ananiangalia kwa utulivu.

"Ndiyo umeleta msosi dada?" Tesha akamuuliza Miryam.

"Eeeh, nimeona niiwahi hii mida ili tule pamoja naye. Twendeni sasa asibaki mwenyewe," Miryam akasema hivyo.

"Ngoja kwanza," Tesha akamzuia.

Wote tukamwangalia usoni.

"Vipi tukimfanyia kama ka-surprise? JC namaanisha," Tesha akasema.

"Eee, JC ndo' atakuwa surprise, Mamu atafurahi akimwona, sote tunajua. Au unataka tumfunge kwenye boksi na makaratasi?" Ankia akauliza kiutani.

Wengine wakatabasamu, naye Tesha akasema, "Siyo hivyo. Yaani, sisi wengine tutangulie, halafu JC abaki hapa mlangoni. Nikimwita tu ndo' aingie."

"Hayo yote ya nini Tesha?" nikamuuliza.

"Eti? Si tuingie tu pamoja?" Miryam akasema.

"Da' Mimi hauangalii movie wewe, ndo' maana. Hiyo inaitwa 'dramatic entrance,' yaani stelingi anaingia kimtindo, halafu kila kitu kina-change. Fffuup..." Tesha akasema hivyo huku akionyesha ishara kwa viganja vyake.

"Ila Tesha..." Miryam akasema hivyo.

"Ahahahah... haina shida Mimi, acha tu afanye hivyo. Kama ni sawa JC..." Bi Zawadi akaongea.

"Sawa. Nitasubiria hapo nje," nikawaambia.

"Aina hiyo. Nataka niione reaction ya Mamu, itakuwa siyo ya nchi hii. We' mwanangu ushakuwa dawa yake, haipingwi," Tesha akasema hivyo huku tukielekea mlangoni.

Baada ya kuufikia, kweli wote wakawa wameingia huko ndani na kuniacha nikisubiri kwa nje, nami niliweza kuona kupitia uwazi mdogo wa kioo mlangoni kwamba chumba hicho kilikuwa kipana na kirefu kuelekea mbele zaidi, kukiwa na vitanda kadhaa vya wagonjwa vilivyopangwa kwa mistari miwili na kuacha uwazi katikati kwa ajili ya njia.

Karibia kila sehemu yenye kitanda kulikuwa na watu ambao walikaa na wagonjwa wao na kuwapatia mahitaji na uangalizi kwa wakati huu wa kutembelea wapendwa wao walioumwa, na inaonekana sehemu aliyokuwepo Mariam ilikuwa mbele zaidi kwa sababu kwa hapo nisingeweza hata kuwaona ndugu zake walipoishia.

Nikiwa nasubiri, simu yangu ikaanza kuita, nami nikakuta mpigaji akiwa ni Bertha. Duh! Nikapokea, naye ndiyo akaniambia kwamba huko alikokuwa kuna mambo yalikuwa ni moto kwa hiyo angechelewa kurudi hotelini, hivyo kama mimi nilikuwa tayari kwenda niende tu; angekuja kunikuta baadaye.

Lakini nikamwambia ukweli kuwa bado sikuwa nimegeuka kurudi kwake, kwa sababu kuna jambo fulani lilikuwa limetokea ambalo lilisababisha nibadili maamuzi ya kwenda kukaa pale hotelini, na ningekuja kumwelezea vizuri zaidi tukionana tena. Nilitarajia labda angeanza kulalamika baada ya kusikia nimemwambia hivyo, lakini akasema tu sawa, haina shida, tungeonana na kuongea baadaye.

Alipokata simu, nikawa nawaza ni nini kwa wakati huu kilichokuwa kimefanya asiwe mkali na mpelekeshaji sana kwangu kiasi kwamba hadi akanikubalia tu hivyo haraka-haraka, lakini mawazo yangu yakakatishwa baada ya simu yangu kuita tena na kuona mpigaji kuwa Tesha. Nikaelewa hiyo kuwa ishara ya kuitwa sasa ili niende kuwa "surprise" kwa ajili ya Mariam, nami nikakata simu na kuingia chumbani/wodini.

Kwa sababu ya kuwa daktari nilikuwa nimeshazoea mazingira ya kuona wagonjwa wakiwa katika vyumba vya matibabu kama hivi, hivyo nilipita tu bila kukazia fikira zangu kwa watu wengine ambao ingekuwa rahisi kukengeuka kuwaangalia shauri ya hali zao. Hii haikuwa wodi ya vyumba maalumu vya kibinafsi maana ilikaa kama vile wodi za hospitali za serikali, sema tu ilikuwa na mwonekano maridadi zaidi na vifaa vya gharama.

Baada ya kuwa nimewaona mama wakubwa, Tesha, na Ankia wakisimama upande wa kitanda kimoja cha wagonjwa, nikajua ndiyo hapo binti alipokuwa, nami nikaanza kusogea taratibu kupaelekea. Nikasimama umbali mfupi kutoka mwisho wa kitanda hicho, na sasa nikawa nimemwona Mariam.

Binti alikuwa amelala kitandani hapo, huku sehemu ya kitanda kutokea kiunoni ikiwa imenyanyuliwa juu kiasi ili kichwa chake kiwe juu; aweze kuona mambo ya mbele vizuri. Nywele zake zilikuwa zimeachia, yaani zilifumuliwa, na zilikuwa laini kama za Miryam tu, zikilazwa pande za kichwa chake na kumfanya aonekane kama msomali hivi.

Alitulia, sana, macho yake yakielekea upande ambao dada yake alikuwa amekaa karibu naye, na uso wake haukuonyesha hisia yoyote ile. Kumwangalia tu namna hiyo kukanifanya niyakumbukie tena yale yaliyompata ule usiku, nami nikahisi huzuni kiasi.

Tesha aliponiona, akamwambia Mariam, "Mamu... ta-da! Surprise!"

Alisema hivyo huku akimwonyeshea binti kwa mkono kunielekea, naye Mariam akawa ameangalia upande wangu na kuniona. Ankia, Bi Jamila na Bi Zawadi wakaniangalia na kumtazama binti tena huku wakitabasamu, naye Miryam akatabasamu pia na kumshika mdogo wake begani.

"Mamu, umemwona kaka JC?" Bi Zawadi akamwambia hivyo.

Mariam alikuwa ananiangalia kwa umakini sana, yale macho utafikiri alikuwa anajiuliza mimi ni nani, lakini najua hiyo ilikuwa ni wonyesho tu wa yeye kutotarajia kuniona. Nikasogea mpaka kufikia usawa wa miguu yake huku sasa nikimpa tabasamu pia, lakini bado akawa ananiangalia utadhani alikuwa ananiogopa. Mara kifua chake kikaanza kushtua, huku sura yake ikikunjamana kiasi, na ikawa wazi kwamba alikuwa ameanza kulia baada ya machozi kuonekana yakimtiririka kutoka machoni.

"Mamu..." Miryam akamwita hivyo kwa kujali na kumshika usoni.

Tabasamu lililokuwa nyusoni kwetu wote likatoweka, kwa kuwa sasa Mariam alianza kulia kwa hisia sana, lakini hakutoa sauti. Alilia, kama mtoto yaani, huku Miryam na mama wakubwa wakijaribu kumtuliza. Sote tuliingiwa na simanzi yaani, lakini nilielewa kwamba kilio chake kilibeba maana pana zaidi ya kuwa na huzuni tu. Alifurahi kuniona.

Nikawapita mama wakubwa taratibu na kusogea karibu zaidi na Miryam, ambaye alijitahidi kumtuliza mdogo wake na kumpangusa machozi, naye aliponiangalia, nikamtikisia kichwa mara moja. Akaelewa, hivyo akanipisha ili nisogee karibu zaidi na mdogo wake. Mariam alikuwa anaendelea kulia kwa kwikwi, huku kichwa chake kikitetema na akiwa kama hataki kunitazama machoni kwa wakati huu.

Nikakaa pembeni yake, huku wengine wakituangalia, nami nikamwambia, "Mamu... usilie. Nimekuja tucheze. Nimekuja tucheze Mamu."

Binti akaendelea tu kulia huku akitazama chini na vidole vyake akivifikicha mara nyingi. Miryam sasa akawa amesimama karibu na Ankia baada ya kuwapita mama wakubwa.

"Usilie bwana. Tutachezaje sasa ukiendelea kulia? Kama unataka tu kulia, basi na me naanza tu kulia sasa. Tukae hapa tulie wote. Na siyo mimi tu. Na Miryam na yeye anaanza kulia. Na mama mkubwa, na Ankia. Wote. Na Tesha na yeye anaanza kulia. Ona, ona na yeye sasa ameanza kulia..." nikamwambia hivyo Mariam, kwa njia fulani ya kitoto.

Akamwangalia Tesha, naye Tesha kweli akakunja sura kimaigizo kuonyesha kwamba alitaka kulia. Mama wakubwa wakawa wanatabasamu kwa hisia.

"Umeona? Sisi wote tutalia ukiendelea kulia. Unataka kuona tunalia? Unataka kumwona dada analia?" nikamuuliza binti hivyo.

Akiwa ameinamisha uso sasa, akatikisa kichwa kukanusha.

"Sasa mbona ulie? Kama hutaki tulie, basi inabidi uache kulia. La sivyo hatutacheza, eh? Unataka tuache kucheza?" nikamuuliza tena huku namnyooshea kidole kama namkanya.

Akatikisa kichwa kukataa.

"Haya acha kulia sasa Mamu. Eti? Jifute machozi," nikamwambia hivyo.

Akawa anafikicha vidole vyake bado, na kwa njia yenye kusita akawa kama anataka kuinyanyua mikono ila anaacha.

Nikamwambia, "Ahaa, hautaki kuacha? Haya. Me naondoka. Usipojifuta machozi, sichezi tena na wewe..."

Baada ya kusikia hivyo, Mamu akaanza kupeleka macho yake huku na huku kwa kubabaika, kisha akainyanyua mikono yake na kuanza kujifuta machozi usoni. Nikawa namtazama kwa hisia sana, akinifanya nifarijike mno moyoni, nami nikamwangalia Miryam na kukuta akiwa anatokwa na machozi na Ankia akimbembeleza kwa kusugua mgongo wake taratibu.

Mariam akaendelea tu kujifuta usoni hata pale machozi yalipokuwa yameisha, nami nikamshika mikononi ili aache. Akawa kama anataka kuniangalia lakini kwa woga fulani hivi, akirudisha macho chini kila mara.

Nikamwambia, "Mariam... nataka nikwambie kitu fulani muhimu. Wewe una nguvu sana. Sawa? Wewe ni msichana mwenye nguvu... na imara sana. Lakini najua umeumia. Hata sisi huwa tunaumia. Sisi wote. Lakini ukae ukijua hili... wote hapa, tunakupenda, sawa? Hata kama nini kimetokea, hatutaacha kukupenda. Dada, Tesha, mama zako, Shadya, Ankia huyo hapo, na mimi... tunakupenda sana. Usiogope mtu yeyote. Yaani usimwogope mtu yeyote, kwa sababu hatuwezi kuruhusu nyani yoyote akuumize. Si unawajua wale manyani? Wale wabaya wale? Hawawezi kukuumiza tena, kwa sababu sisi tuko nawe. Usiogope hata kidogo. Tena hhee... ngoja nikwambie. Yaani, nataka nije nikufundishe mchezo wa karatee, unaujua?"

Mariam akatikisa kichwa kukubali.

"Hiyo hiyo! Tutacheza karatee, yaani mtaani... hakuna mtu atakusogelea tena. Mtu akija kukutisha, unamtandika ngumi!" nikamwambia hivyo.

Mariam akaniangalia usoni baada ya kuwa nimemwonyesha ngumi na kuirusha hewani kiasi.

Tesha akaongezea, "Eeh Mamu! Yaani wakija kutusogelea tena tunawadunda! Wakileta sijui nini, kooh! Hawatasogea kabisa."

Bi Zawadi akasema, "Na sisi tumeshajifunza karatee. Muulize Miryam! Naruka kama Jakisheni. Wee! Hakuna mtu atakusogelea tena!"

"Kabisa," Bi Jamila akasema hivyo huku akikunja ngumi.

Walikuwa wanampa binti matumaini, kitu ambacho kikafanya Mariam amtazame Miryam pia. Wakati huu, mwanamke huyo alikuwa ameshajikausha machozi, naye akaunga mkono jambo hili kwa kuonyesha ishara ya kupiga ngumi kwa ujasiri. Ankia pia akakunja ngumi na kumpiga Tesha mpaka kumuumiza, nao wakacheka kidogo baada ya Tesha kumwangalia kwa kuudhika kiasi.

Hali ya wepesi kihisia iliyojijenga ndani ya Mariam baada ya jambo hilo ikamfanya anitazame usoni moja kwa moja sasa, nami nikamwambia, "Umeona? Haupaswi kuogopa lolote mama. Tuko... pamoja."

Akainamisha uso wake tena huku akionekana kutaka kulia, na kiukweli hali hii iligusa sana.

Yaani, hali alizokuwa nazo huyu binti na kile ambacho alikuwa ametoka kupitia hiyo juzi vilinifanya nifikiri kwamba hata hili jaribio nililofanya hapa huenda lisingezaa matunda, lakini itikio lake likawa bora zaidi hata ya nilivyodhani. Ilikuwa kama vile maneno yangu aliyatafakari kwa kina kilichopita uelewa wake wa akili ya kitoto aliyoionyesha, na hiyo ilimaanisha maendeleo yake mazuri hayakuwa yamepotea kabisa toka nilipoanza kumsaidia hadi hayo majanga yalipomkuta.

Nikataka kumwambia asilie tena maana alikuwa ameahidi kutolia, lakini akajifuta chozi upesi kabla halijamtoka, kisha akaniangalia usoni kwa mara nyingine. Jinsi ambavyo alinitazama zamu hii, yaani haikuwa kwa njia yoyote ambayo nilikuwa nimezoea. Yalikuwa macho mapya, akiniangalia kama mtu... kama mtu mwingine, mtu mzima, na si mtoto tena. Ilikuwa kama vile macho yake yananiambia kwamba ameelewa, na yalitoa shukrani ya ndani sana ya moyo wake. Sijui kwa nini tu hisia zangu ziliniaminisha hivyo.

Nikiwa sijatarajia hili, Mariam akanyanyua kiganja chake na kukiweka hewani kunielekea, naye akasema, "Hi-five."

Nilibaki nikimtazama machoni tu kama vile sijaelewa alichotoka kufanya. Nikawaangalia wengine pia, nao walikuwa wakitabasamu kwa furaha utadhani ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa huyu binti kuongea.

Nikatabasamu pia na kukigongesha kiganja changu kwenye chake, kisha nikakiingizia vidole na kuendelea kukishikilia. Alinitia moyo sana! Ile amani niliyoihisi Miryam aliponiomba msamaha leo haikupita amani niliyoihisi baada ya Mariam kunisemesha namna hiyo aisee.

Nikajikuta nakivuta tu kichwa cha Mariam na kukilaza kifuani kwangu, nikimkumbatia kwa kile nilichohisi kuwa upendo wa dhati kubwa kumwelekea binti huyu. Alinifanya nijihisi kuwa mtu bora sana, ubora wa mbali kabisa kutoka kwenye ule utu wangu mbaya niliojiaminisha kuwa ndiyo ulifaa kuwa wangu. Hisia zilinikaba na nikashindwa kuvumilia tena, nikiwa nimeweka kichwa changu juu ya kichwa cha binti Mariam, machozi yakanitoka.



★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★
 
Mpeni maua yake maana dogo ni MKALI llevo za aristabaus msiba na ben mtobwa na mh. Eric shigongo akasome!!!@ fikiria kuandaa muvi tuone madam Bertha akiwa Irene Uwoya au Weka Sepetu nk na JC akiwa JB au yule msukuma au hemed PhD[emoji16][emoji3][emoji886][emoji7][emoji2956][emoji2956]
 
Yeah....
 
MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA THELATHINI NA NANE

★★★★★★★★★★★★★★★★★★★


Nilikuwa ndani ya hisia nzito sana ya furaha na faraja iliyofanya nisitambue upesi kwamba chozi lilinitiririka mbele ya watu hawa wote, ndipo nikawatazama kwa ufupi na kukuta wote wanatuangalia mimi na Mariam kwa hisia sana. Ni Miryam ndiye aliyekuwa akidondosha machozi pia huku akijifunika mdomo kwa kiganja chake, nami nikawa nimemwona daktari akija upande wetu pamoja na muuguzi.

Nikajifuta chozi upesi na vizuri sana ili Mariam asione kwamba nilikuwa nimelia wakati nimemkumbatia, kisha nikamwachia taratibu na kumwangalia usoni. Alikuwa ametazama chini tu, huku bado nikiona shida yake ya kutetemeka kichwa kiasi ikiwepo kwa wakati huu shauri ya mishtuko aliyokuwa amepitia, lakini nilikuwa nimefarijika kwamba angalau maendeleo ya utimamu wake hayakuwa yamepotea. Alinisemesha vizuri sana.

Huyo daktari alikuwa ni mwanamke mtu mzima, mnene kiasi, mweusi na mrembo pia, akiwa amekuja ndani ya wodi hii kuangalia wagonjwa wote, na baada ya kufikia sehemu ambayo Miryam na Ankia walikuwa wamesimama, akatusalimu wote kwa njia nzuri na kuuliza hali ilikuwa vipi kumwelekea msichana huyo aliyekuwa ameletwa jana.

Bi Zawadi ndiyo akamwambia kwamba yaani siyo muda mrefu tu binti Mariam alikuwa ametoka kusema maneno fulani ya "kizungu" baada ya kuniona mimi, ambaye alikuwa amenizoea sana kutokana na kumsaidia kabla ya kuletwa hospitalini hapa hiyo jana.

Daktari huyu akaja karibu yangu na Mariam, nami nikampisha. Akajaribu kumsemesha binti, akimuuliza hiki na kile, na Mariam akawa anajibu aidha kwa kutikisa kichwa au kuchezesha mabega, lakini hakusema neno lolote kwa daktari huyo wala kuonyesha hisia. Kwa hiyo daktari akafanya kuangalia utendaji wake wa mapigo ya moyo kwa kumpima, kisha akasema itakuwa sawa tu kwa binti kuondoka hospitali leo leo jioni, kwa kuwa afya yake iliruhusu.

Lakini akasema kuna dawa atatakiwa kutumia ili kutuliza zaidi msukumo wake wa damu, maana ingawa alikuwa na umri mdogo lakini presha yake kupanda kwenye damu ilikuwa kali mno; hasa kutokana na hali yake yeye kama yeye na yale aliyokuwa amepitia. Kuna mambo ya kina zaidi akawa amesema atahitaji kuzungumza na Miryam, hivyo akasema tunaweza kupata mlo upesi kisha dada mtu aende kuonana naye.

Baada ya hapo daktari akasepa, akimwacha muuguzi anasaidiana na wanawake kumbadilishia binti mrija wa mkojo, na sisi wanaume tukasogea pembeni kwanza. Miryam akanifata mimi na Tesha, naye akaniambia kwamba, ukifika wakati wa kwenda kumwona daktari ili kuzungumza naye kwa kina, niende pamoja naye. Akaniweka wazi kuwa inaonekana mazungumzo hayo yalielekea ishu ya vipimo vya ndani zaidi mwilini mwa Mariam kuona ikiwa binti alikuwa ametendewa vibaya kimwili, nami nikawa nimekubali kuambatana naye muda huo ukifika.

★★

Basi, baada ya Mariam kusaidiwa kufanya usafi, sote tukajiunga pamoja naye na kuanza kupata mlo pamoja. Kulikuwa na vyakula mbalimbali, dada mtu akiwa amenunua kama vyote utafikiri aliviiba kwenye tafrija, lakini binti alikula zaidi nyama ya kuku na kitimoto kwa sababu alizipenda sana.

Kuwa naye kwa wakati huu, sisi wote yaani, ilimfanya Mariam ajihisi salama, anapendwa, na hivyo ikawa rahisi kwake kuonyesha hamu aliyokuwa nayo kwenye kula vyakula alivyofagilia. Miryam angemlisha na kumtendea kama vile ana miaka miwili yaani, nasi sote tukaendelea kupeana ushirika mzuri hadi saa za kutembelea wagonjwa zilipokata na baadhi ya wauguzi kuja kutufukuza. Kistaarabu lakini.

Najua Miryam alikuwa akitumia pesa nyingi sana kumweka mdogo wake katika haya mazingira, na najua asingeacha kufanya yote awezayo ili hali nzuri kwenye pande zote za familia yake irejee.

Mpango kwa hapo ikawa kwamba Shadya abaki kumpa binti uangalizi, halafu Miryam angewarudisha mama zake wakubwa pamoja na Ankia nyumbani, kisha baadaye ndiyo bibie angerudi na kumchukua mdogo wake ili wampeleke nyumbani. Hakukuwa na makolokolo mengi wala ya kubeba, na Shadya alikuwa mwenye utayari sana kubaki na kusaidia kwa lolote lile ili kuiunga mkono familia hii.

Lakini kwanza, mimi na bibie Miryam tulihitaji kwenda kuzungumza na yule daktari, kwa hiyo tulipotoka kwa pamoja tulienda na kumtafuta, na baada ya kumpata, tukakaribishwa ofisini kwake na kuzungumza. Alikuwa ameshafahamishwa kuwa mimi ni daktari pia nayemsaidia binti kupambana na tatizo lililofanana na ASD, lakini sasa akawa ametuongezea ishu nyingine.

Akatuambia kwamba shida yake inayofanana na ASD ilitokana na kitu kinachoitwa kwa ufupi PTSD, hali fulani ambayo husababishwa na mshtuko au msongo mkubwa kutokana na matukio mabaya yanayoweza kumpata mtu maishani mwake. Kwa Mariam, ilikuwa ni kitu kilichosababishwa na maumivu ya kuwapoteza wazazi wake, lakini baada ya kilichompata juzi, hicho kiwango cha PTSD kilikuwa kimepanda, na hivyo angehitaji kusahaulishwa mambo hayo haraka iwezekanavyo, kwa njia zozote zile yaani ingehitajika binti aishi kwa amani kuu na furaha tele kutokea hapa.

Tukiwa watu wake wa karibu bila shaka tulijua mambo yapi ambayo binti alifurahia, na daktari akasema ameona hata leo binti aliitikia upesi ujio wangu kwa njia chanya ingawa bado anaumia, kwa hiyo mtu kama mimi sikupaswa kabisa kuondoka kwenye maisha yake. Hilo lingemsaidia haraka maana alikuwa na umri mdogo bado, kwa hiyo kiwango chake cha kuwa imara kingeongezwa nguvu kupitia mambo mengi mazuri aliyopenda, na kumjengea kumbukumbu bora ili utimamu wake uimarike pia kadiri siku zilivyosonga. Somo likawa limeeleweka.

Kuhusu ishu ambayo baada ya kumpima binti Mariam kuthibitisha ikiwa alikuwa amebakwa, haikuonekana kwamba hilo lilitokea, alikuwa safi kabisa, isipokuwa tu tungepaswa kuendelea kumwangalia kwa ukaribu zaidi maana huwezi kujua sikuzote. Angeweza kuwa hajachubuka na nini, ila kuna uwezekano alikuwa ameingiwa kwa njia ambayo haikuonekana wazi.

Jambo hili lilimtatiza sana Miryam, ambaye hakujua hayo yote yanamaanisha nini, na ni nini kinahitajika kufanywa. Kutokana na daktari huyo kuhitajika haraka kwenda kwa mgonjwa, akawa ameniomba nimweleweshe tu bibie Miryam baadaye, ila akamtia moyo kuwa asihofu; kila kitu kingekuwa sawa. Akatutakia heri na kutuaga.

Tukiwa tunaenda kujiunga na wengine, nikamwambia Miryam kwamba tungekuja kulizungumzia suala hilo baadaye ili nimweleweshe vizuri juu ya mambo yaliyohitajika kufanywa kutokea hapo, na la muhimu lingekuwa kukazia fikira zetu zote kumsahaulisha binti mambo mengi mabaya yaliyotokea juzi, na nikamwomba awasihi watu wa familia yake na hata marafiki wa karibu wasije kukaa na kuzungumzia vitu kama hivyo huku na binti akiwa pamoja nao, naye akaridhia hayo yote. Yaani Mariam ndiyo alikuwa kama yai letu, ingekuwa ni "kum-handle with care!"

★★

Baada ya kuwa tumemwacha daktari, Miryam aliwapeleka wanawake wengine nyumbani, huku mimi na Tesha tukiamua kwenda sehemu nyingine kutulia mpaka muda ambao Mariam angerudishwa kwao. Hakukuwa na lolote la maana sana kufanya, ila kwa mida ya saa tisa mchana kulikuwa na mechi ya kimataifa kati ya Taifa Stars na nchi gani sijui ya wazungu huko, kwa hiyo tukaenda tu kwenye pub moja maeneo ya Zakhem na kukaa hapo kuitazama ili kuua muda.

Tesha alitaka kunywa kidogo kwa hiyo akanunua bia mbili tu, na alitaka kuninunulia pia ila nikakataa; nikipendekeza tu niletewe soda, basi. Tukawa tunaongea mawili matatu, akiniambia ni namna gani alivyokuwa amehuzunishwa sana na mambo yote yaliyokuwa yametokea kwenye familia yake, ila alifarijiwa sana na msaada wote niliokuwa nimeutoa kwao.

Aliona kwamba bila mimi kiukweli kwa sasa angekuwa ameshazikwa, hivyo alihisi ana deni kubwa mno la kunilipa ambalo hakudhani angewahi kufanikiwa kulipia. Lakini akasema kwa lolote lile kuanzia sasa na kuendelea, nijue tu kwamba kama ningemhitaji, asingesita kuniunga mkono kwa asilimia zote. Yaani lolote lile. Nikamshukuru tu na kumwambia asiwe na hofu, la muhimu kutokea hapa ni kufanya kila kitu ili kumweka Mariam sehemu nzuri tena, naye akasema hilo ni uhakika.

Imefika mida ya saa kumi na moja baada ya mechi kuisha, tukaondoka maeneo hayo na kutembea mpaka Rangi Tatu. Tesha akawa amemtafuta dada yake kuuliza yaliyoendelea, naye Miryam akamwambia kwamba alikuwa amesharudi hospitalini mida hii hii kumchukua mdogo wake. Tesha akasema sawa, yuko pamoja nami hivyo tungekutana wote nyumbani baada ya muda mfupi.

Alipoagana na dada yake, Tesha akapendekeza tutembee taratibu tu kutokea hapo mpaka Mzinga ikionekana kuwa njia nzuri ya kukata wakati mpaka kufika kwao. Sikuona shida yoyote kukubaliana na wazo hilo, kwa hiyo mdogo mdogo tukaendelea kushuka. Katika maongezi mawili matatu Tesha akawa amenikumbusha kuhusu yule mwanadada aitwaye Dina, ambaye tulienda kule Uhasibu siku kadhaa nyuma kumtembelea.

Akasema anawasiliana naye sana, na hata hii ishu ya kutekwa juzi alikuwa amemwambia na Dina akasema angekuja kuwasalimia. Lakini Tesha akagusia namna ambavyo kila mara alipowasiliana na Dina, mwanadada huyo alipenda sana kuniulizia, na mara nyingi Tesha alimtania kuhusu kunitaka ila akawa anajihami.

Ila ilikuwa wazi kwamba Dina alitaka Tesha aniunganishe kwake, na sasa ndiyo jamaa akaniambia nimfikirie huyo rafiki yake endapo nikihitaji poza roho kuondoa misongo kibao. Nikamwambia tu ningeangalia na jinsi ambavyo mambo yangekwenda maana kwa sasa, akili yangu yote ilikuwa kwa Mariam, Mariam, Mariam, na Bertha kama ketchup pembeni. Basi.

★★

Tumekuja kufika kwao Tesha imeshaingia saa kumi na mbili kuelekea giza la saa moja, nasi tukawakuta wapendwa wetu wote wakiwa hapo; kutia ndani na Ankia. Mariam alikuwa amekaa pamoja na Miryam kwenye sofa moja, na baada ya kuniona tu, binti akaonyesha wazi kwamba alifurahia ujio wangu hapo kwa kunigeukia vizuri zaidi na kunitazama kama vile anataka kunisemesha, naye Miryam akaniambia nikae karibu yake ili bila shaka binti ajisikie vizuri.

Nikakaa pamoja na Mariam na kuanza kumsemesha hiki na kile, huku Miryam pia akiniunga mkono kwa kuongea pamoja nasi ili kumfurahisha mdogo wake, na ingawa Mariam hakuzungumza lolote lile lakini alionekana kuwa na amani sana. Upendo mwingi ambao angeupata kutokea hapa ungemsaidia sana huyu binti, na kila mmoja alionyesha kutaka hilo lifanikiwe kwa asilimia kubwa.

Mambo yaliyoendelea baada ya hapo ikawa ni kupata mlo wa pamoja tena ambao uliandaliwa na Shadya, Ankia, na bibie Miryam mwenyewe, nasi tukamaliza na kuendelea kukaa pamoja hadi kufikia saa nne. Usingizi wa mtoto ukawa umemvuta Mariam mapema, hivyo Miryam akamwongoza kuelekea chumbani ili akanywe dawa kwanza kisha ndiyo alale. Kalikuwa hakataki kuniacha kutokana tu na jinsi kalivyoniangalia wakati dada yake alipokasimamisha ili waende chumbani, lakini hatimaye wakawa wametuacha.

Muda uliposogea mpaka kuingia saa tano, Ankia akaona aage ili mimi na yeye tuelekee pale kwake kwa ajili ya mapumziko. Kwa mara nyingine tena, Bi Jamila na Bi Zawadi wakatoa shukrani za dhati kunielekea kwa sababu ya kuamua kubaki Mzinga ili kumsaidia binti yao, nami nikazipokea baraka zao kwa uthamini.

Nikawaambia wote kuwa kesho ningejitahidi kuja pia ili nicheze na binti taratibu kama ilivyokuwa mwanzo, isipokuwa zamu hii ingekuwa kwa njia tofauti kiasi. Njia tata zaidi ya mwanzo. Hawakuwa na neno.

Baada tu ya Miryam kuja sebuleni tena, mi' na Ankia tukanyanyuka ili kuondoka sasa, na tukawa tumemuaga bibie pia. Miryam akasema sawa na kuashiria kutaka kutusindikiza nje, hivyo tukaelekea mpaka kibarazani tukiambatana na Tesha pia. Ardhi iliyopambiwa vitofali vidogo-vidogo ya hapo nje ilionekana kulowana kiasi, kitu kilichomaanisha mvua ilikuwa imeshuka kidogo muda ambao tulikuwa ndani, na sasa ilikuwa imekata.

"Kaka, nazisubiri hizi mvua kwa hamu sana. Zipige haswa yaani," Tesha akaniambia hivyo.

"We! Usiombe hivyo. Hatutaki mabalaa mapema sisi. Kama kunyesha zinyeshe, lakini kawaida," Ankia akamwambia huku akivaa ndala zake.

"Haupendagi mvua Ankia..." Miryam akamwambia huku anatabasamu.

"Kwa kweli me mvua a-ah. Yaani ingekuwa bora tu... anga... mawingu yatande, lakini maji yasishuke," Ankia akasema.

"Mmmmm, unajua kujishaua wewe!" Tesha akamwambia.

"Ish, hivi unafikiri?" Ankia akasema.

"Kinachofanya usipende mvua kubwa ni nini?" Tesha akamuuliza Ankia.

"Radi na matope," nikamwambia.

"He! JC umejuaje?" Ankia akauliza.

"Nimekisia tu," nikamwambia hivyo.

"Afu' radi siyo Ankia tu, hata da' Mimi. Ahahah, siku ipige mvua ya maana na radi, unamkuta dada chini ya uvungu!" Tesha akasema hivyo, nasi tukacheka kwa pamoja.

Miryam akampiga Tesha kidogo begani huku akitabasamu, naye akasema, "Me siyo mwoga kihivyo bwana."

"Tulia, nitakuja nichukue mkanda tu," Tesha akamwambia.

Ankia akapiga mhayo kidogo na kusema, "Haya jamani, sisi tuwaache sasa. Tutatembeleana na kesoow."

"Yeah, ila... nilikuwa nataka niongee kidogo na..." Miryam akasema hivyo na kunitazama.

"Ahaa, sawa. Me ngoja nitangulie sa' JC," Ankia akaniambia.

"Haya," nikamwambia.

"Twende nikusindikize wewe, usije ukabebwa hapo nje," Tesha akamwambia Ankia huku naye akivaa malapa yake.

Nikabaki hapo kibarazani pamoja na bibie Miryam tukiwaangalia wawili hao walipokuwa wakielekea geti, kisha ndiyo akasema, "Hatujaongea kuhusu ile ishu aliyoisema daktari muda ule."

Nikamwangalia na kusema, "Ee ndiyo, kuhusu Mariam..."

"Yeah."

Nikamwambia, "Okay. Yaani ni kwamba, unakuta sometimes... mwanamke kama hivyo anaweza akawa ameingiwa vibaya, lakini kusiweze kuonekana michubuko au chochote kinachoweza kuashiria kwamba force imetumika. Kuna hiki kipimo wanaita colposcopy, ndiyo wametumia kumpima nafikiri... maana huwa kinaangaza hadi sehemu za ndani zenye uwezekano wa kuumia... kama tu camera ndogo na safi..."

Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa.

"Yeah. Sasa, kwa maelezo ya daktari, inaonekana hicho kipimo hakija-detect tatizo lolote lile kabla ya... kabla ya huyu msichana kuingiwa vibaya, ila kwa Mariam ninaamini yuko safi. Ambacho tu tunatakiwa kuangalia ni ikiwa uwezekano, yaani... IKIWA TU uwezekano upo kwamba aliingiwa, na hicho kifaa hakija-detect, basi ndiyo atapaswa kufanya routine ya vipimo ili kuwa na uhakika zaidi," nikamwelezea.

Akaonekana kutafakari maneno yangu, naye akauliza, "Kwa hiyo ni kama kusema, vipimo vinaonyesha mdogo wangu yuko safi kwa asilimia 70, ila kwa kuwa hatuna uhakika wa hizo 30, ndo' anatakiwa kuendelea kupima?"

"Uko sahihi. Ila nina-bet asilimia 99 Mariam yuko safi. Hiyo moja tu ndiyo tunatakiwa kuihakikisha," nikamwambia hivyo kwa kufariji.

Akatabasamu kiasi na kutikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akasema, "Sawa. Kwa hiyo, hiyo routine itaendaje?"

"Mmmm... nafikiri tufanye hivi. Baada ya wiki moja, mpeleke akapime baadhi ya magonjwa ya STI. Si unaelewa?"

Akatikisa kichwa kukubali.

"Wiki ya pili, mpime mimba. Ya tatu, mpime vitu kama... Syphilis, hepatitis... na HIV. Yaani ndani ya huu mwezi mmoja mbeleni ndiyo tutakuwa na uhakika wa asilimia zote kwamba yuko sawa kabisa akishapimwa namna hiyo. Na... hatakiwi kuambiwa chochote kuhusu haya, yaani... asije kubaki anakumbukia tu... yaliyotokea," nikamwambia.

Miryam akashusha macho yake kwa njia iliyoonyesha huzuni.

"Miryam... uko sawa?" nikamuuliza kwa upole.

Akaniangalia na kusema, "Ee, niko poa. Ila haya yote... yaani sometimes nawaza tu kama ningekuwa nimekusikiliza na kuchukua hatua mapema, haya yote yasingetokea. Part kubwa ya maumivu ya Mamu nimeisababisha. Na ninaogopa..."

Nikamwangalia kwa uelewa, nami nikamwambia, "Haina faida kujilaumu Miryam. Sasa hivi la muhimu ni hali njema ya mdogo wako, na ninajua atakuwa sawa tu. Haya tunayafanya ili kuwa na uhakika... kuweka tahadhari tu, na ni ya muhimu. Huu mwezi ukishapita, yatabaki kuwa historia."

Akatikisa kichwa kukubaliana na hilo, naye akasema, "Asante."

Nikawa nimewaza kitu fulani, nami nikamuuliza, "Vipi kuhusu... Joshua, na Khadija? Umeshasikia lolote kuwahusu?"

Uso wake ukageuka na kuwa makini kiasi, naye akasema, "Sijasikia. Na sitaki kujua lolote kuwahusu."

Aliongea kwa sauti tulivu lakini ilisikika kwa njia iliyoonyesha uchungu wa aina yake, nami nikatikisa tu kichwa kuonyesha nimemwelewa.

"Kwa hiyo... kesho utakuwa na..." Miryam akawa anataka kuniuliza kitu fulani lakini akaacha baada ya Tesha kuwa amerejea tena.

"Kesho nitakuja ndiyo. Aa, kuna sehemu naenda asubuhi, kwa hiyo mida ya baadaye tutakuwa pamoja na Mamu," nikasema hivyo baada ya Tesha kufika karibu.

Miryam akasema, "Sawa."

"Ankia ashalala, eti?" nikamuuliza Tesha.

"Hamna, hajadondo bado. Anakusubiria," Tesha akasema hivyo na kunipandishia nyusi zake kimchezo.

Nikatabasamu kiasi na kusema, "Sawa, tutaonana kesho. Usiku mwema."

"Usiku mwema mwanangu," Tesha akasema hivyo na kugonga tano pamoja nami.

Nikiwa nimeanza kuvaa viatu vyangu, Miryam akasema, "Usiku mwema."

Nikamwangalia usoni kwa sekunde mbili tatu hivi, ile kitu tunaita "ku-admire" sura ya mtu mwingine ikiwa ndiyo naifanya wakati huu, nami nikamwambia, "Na kwako pia."

Kisha baada ya hapo nikaondoka na kuelekea upande wetu ili kupumzika mapema, kwa sababu nilikuwa nimefikiria kufanya jambo fulani mapema ya kesho kabla sijarejea tena kwenye familia hii ili niendelee kumsaidia Mariam. Ingekuwa ni muhimu sana, kwa hiyo nilipoingia tu kwa Ankia sikujizungusha na mengi; ikawa ni kuvua, kwenda kujimwagia kwanza, kisha ndiyo nikaagana na mwenye nyumba wangu na kuingia kulala.


★★★


Asubuhi ya Jumatatu hii haikukawia kufika, mpaka nikahisi ni kama vile nilifumba macho na kufumbua papo hapo pakawa pamekucha. Ni kwamba tu inaonekana mwili ulikuwa umechoka mno, na usiku wa kuamkia sasa ndiyo uliokuwa mrefu zaidi kwangu kulala kwa amani, maana nilimaliza utaratibu mzuri wa kusinzia wa masaa nane kabisa mpaka kuja kuamka mida hii ya saa moja.

Nikajitoa kitandani, na leo nilikuwa nimewahi hadi kumkuta Ankia akiwa kwenye taratibu zake za usafi. Na kalipenda kweli kusafisha vitu hata kama hakukuwa na uchafu. Tukasalimiana vizuri, akiwa anauliza sababu iliyofanya leo niwahi mno kutoka chumbani, ndiyo nikamwambia kuna sehemu nataka kuelekea kwanza kabla ya kuja kutumia muda pamoja na Mariam wangu. Akasema hata yeye pia angetoka baada ya kunywa chai, kwa hiyo labda tungekuja kuonana jioni.

Baada ya hiyo kwenda, nikaelekea nje na kufanya usafi wa mwili kama kawaida yangu, kisha ndiyo nikaingia chumbani na kuanza kujiandaa. Nikavaa vizuri kwa mtindo wangu wa kwenda kwa Bertha kibosile kule, isipokuwa tu sikuwa na dhumuni la kwenda kwa huyo mwanamke muda huu. Nikavuta simu na kumpigia mtu wangu wa faida sana aliyenisaidia mpaka tukawapata Tesha na Mariam ile juzi, yaani askari Ramadhan.

Akapokea, na kama kawaida yake, tayari kwa asubuhi hii alikuwa ameshaingia kazini na kuanza kushughulika na mambo yao mengi, na hivyo akanitaka nimwambie upesi ikiwa kuna taarifa mpya nilitaka kumpa. Nikamwambia taarifa mpya kwa sasa bado, ila nilichokuwa nahitaji ni kujua mahali ambapo Joshua na mke wake walikuwa wamewekwa.

Akasema tu hawakuwa wamewekwa pamoja, huyo Joshua akiwa katika kituo kilichopo Mbagala Maturubai, na mke wake alikuwa ametolewa dhamana ya muda mfupi siku ya jana. Akadai kwamba ni ndugu zake na huyo mwanamke ndiyo waliokuwa wamemdhamini, na walitaka hadi kumtoa Joshua lakini wakakataliwa. Nikamshukuru kwa taarifa hiyo na kumwambia tungetafutana wakati mwingine tena ili nimjulishe yale ya upande wa Bertha na Chalii Gonga, ndiyo tukawa tumeagana.

Hapo nikawa nimepata nilichokihitaji, na sasa ingekuwa kwenda kuchukua nilichokitaka. Kutoka kwa huyo Joshua. Mpango ulikuwa kwenda kuitafuta hiyo Maturubai sasa hivi ili nikaonane na huyo jamaa, na hiyo tu ilikuwa ni sababu tosha iliyofanya nisiwaambie watu wa familia yake Miryam kuhusu hilo. Nilikuwa na lengo, na niliombea niwe sahihi juu ya kile nilichowaza, hivyo baada ya kukamilika kimtoko nikamwacha Ankia hatimaye na kuingia mwendoni.

★★

Haikuchukua muda mrefu sana nami nikawa nimefika huko kwenye kituo cha polisi cha Maturubai. Nilikuwa nimekitafuta kupitia ramani lakini kufika ilihitaji mwongozo wa konda kwenye usafiri na bodaboda mpaka kufikia eneo husika. Hii ikiwa ni mida ya saa tatu kasoro asubuhi, nikaelekea ndani ya kituo hicho, na aisee!

Kilikuwa kibaya!

Sikuwahi kufika kwenye kituo cha polisi kilichokuwa na matunzo duni kama hiki. Yaani palionekana kama vile palikuwa pamepigwa na bomu la nyuklia halafu baada ya miaka mia moja ndiyo hawa watu wakaja kuchukua mabaki ya hili jengo na kuamua kulifanya liwe kituo cha polisi. Sitanii. Lakini kiukweli kupaona sasa kukanifanya nielewe kwa nini askari Ramadhan aliamua kuwaleta wakina Joshua huku. Paliwafaa kabisa!

Baada kuingia hapo ndani, nikamkuta afande mmoja akiwa amekaa nyuma ya kitu kama kaunta, mbaba, mweusi kiasi mwenye sura iliyokomaa, nami nikampa salamu. Kisha nikawa nimemuulizia Joshua, naye aliponiuliza nina uhusiano gani naye, nikamwambia mimi ni daktari wa binti ambaye mwanaume huyo alikuwa amemfanyia uhalifu juzi hapo, na nilihitaji kuzungumza naye.

Afande akasema huu haukuwa muda wa kuwafungulia hao watu wala kuwatembelea, eti muda hususa ikiwa ni saa nne na kuendelea. Nikamwambia mi' nahitaji tu kuonana na Joshua kwa muda mfupi ili nimuulize jambo fulani muhimu sana, na nilikuwa nimeshazungumza na askari Ramadhan ambaye ndiye alinielekeza kuja hapa. Nikaona nimpe na jamaa elfu kumi tu kama pole ya usumbufu, naye akakubali. Mapopo kwa hela!

Akaniambia nisogee naye kuelekea upande uliokuwa na selo ya walioshikiliwa. Tulipoufikia huo mlango, mpaka nikashangaa, yaani ulikuwa mwembamba ingawa wa chuma nzito kiasi, na askari huyu akafungua kufuri kubwa kwa nje na kisha kuita kwa sauti ya juu, "Wewe! Njoo hapa."

Inaonekana alikuwa akimwita Joshua bila shaka, na ni ukimya tu ndiyo uliofuata baada ya hapo.

"Wewe ndiyo... njoo hapa. Nyanyuka," askari akarudia tena kusema hivyo.

Sauti za vuu na vuu zikasikika sakafuni, yaani ndani ya hiyo selo kutuelekea sisi, ndiyo hatimaye Joshua akawa ametoka. Ah, aisee! Kumwona tena kulinitia hasira sana kwa kukumbuka kile alichotaka kumfanyia Mariam, lakini kama ingekuwa ni kwa mtu mwingine kabisa ambaye ndiyo amekutana naye hapo, basi angemwonea huruma kutokana na jinsi alivyokuwa akifanana.

Wakati huu alikuwa ndani ya kaushi nyeupe na bukta nyeusi kwa chini. Mwili wake ulionekana kuchafuka, huku akitembea kwa kuchechema kiasi kwa sababu ya maumivu sehemu fulani ya mwili wake. Usoni, jicho lake la kulia lilikuwa limejaa kama puto dogo yaani kutokana na kuvimba mpaka kutoweza kufunguka, na pua yake ilikuwa imeumuka pia. Taya yake ya kushoto ilikuwa imetanuka zaidi kwa chini, kitu kilichoonyesha kwamba fizi zake zilivimba pia, kwa hiyo kiujumla ni kwamba alikuwa na maumivu mengi sana usoni na mwilini. Mkono wangu ulikuwa mbaya kweli!

Akiwa tu ndiyo ametoka na kuonekana haelewi somo, akawa ameangalia upande niliosimama na kuniona, naye akanitazama usoni na jicho lake moja kwa njia ya kushangaa. Nikaona anameza na mate kabisa, sijui alifikiri nimekuja kumwongezea kipondo kingine?

Yule afande, baada ya kufunga mlango wa selo tena, akamwambia Joshua, "Kaa hapo. Kaa hapo chini."

Lakini Joshua akaendelea tu kusimama na kuniangalia kama vile hakusikia alichoambiwa.

"Wewe, hujanisikia?" askari akamwambia hivyo kiukali na kumpiga begani kwa nguvu kiasi.

Joshua akatoa sauti kuonyesha maumivu, huku akijirudi-rudi kwa kuchechema. Hapo begani ndiyo nilipokuwa nimepasulia chombo kizito cha udongo usiku ule nimemkunyuga, kwa hiyo nilielewa aliumia kwelikweli.

Nikamwambia askari, "Haina shida mkuu. Mwache tu asimame."

Askari huyu akamwangalia Joshua, naye jamaa akaniangalia huku amejishika bega.

"Nasikia mke wako wamemdhamini," nikamwambia hivyo.

"Eee. Me wamekataa. Umewaambia wanikatalie, ili... uje kuniongezea maumivu, si ndiyo?" Joshua akaniuliza hivyo.

"Ningependa sana kufanya hivyo, lakini me siyo mjinga kama wewe," nikamwambia.

"Kwa hiyo nini... umekuja kunitoa?" akaniuliza tena.

"Ahah... unaota ndoto za mchana..."

Nikamwambia hivyo huku nikisogea karibu na aliposimama yeye na askari.

"Siwezi kufanya upuuzi kama huo. Hii ndiyo sehemu sahihi unayotakiwa kuwepo. Na tena ukitoka hapa, ndiyo utaenda kukaa kule papana zaidi. Utapaita nyumbani... ndiyo utakutana na wengi walio kama wewe, hata zaidi yako," nikamwambia hivyo.

Akaonyesha sura ya kukosa amani, naye akasema, "Tafadhali bro... nisaidie. Najua nimekosea ila... ninaweza kubadili... kubadilika yaani... ahh... hii sehemu ni mateso kaka... nisaidie..."

"Ulipata nafasi nyingi sana za kusaidika, lakini ukazitupia dampo. Zamu hii utapata unachokistahili," nikamwambia hivyo kwa mkazo.

Akabaki kunitazama na kupumua kwa kutetereka.

"Kijana, tumia muda wako vizuri. Huyu anahitaji kurudi ndani," askari akaniambia hivyo.

Nikamsogelea Joshua karibu zaidi na kusema, "Nataka kujua ukweli."

"Kuhusu nini?" akaniuliza kwa hofu.

"Nimekuangalia tokea mwanzo. Kufanya yote uliyoyafanya... sidhani kama ilikuwa kwa sababu tu ya kutaka mali upate pesa. Kuna sababu nyingine, si ndiyo?" nikamuuliza.

Akaanza kubabaika, akitazama huku na huko na jicho lake kama Nick Fury.

"Niambie sababu iliyokusuka kurudia makosa yale yale tena na tena... mpaka udiriki kutuma watu wambake mdogo wako ili tu kumharibu, na we' ndo' upate faida yako ya kishenzi," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.

Akashusha pumzi na kusema, "Lile shamba bwana... kuna mtu analitaka. Sasa... ehh... mimi ndiyo... nilikuwa...."

"Ongea ueleweke! We' vipi?" askari akamfokea.

"Jamaa nilifanya makubaliano naye... a..alikuwa anataka kulinunua sasa... mimi... tukafanya makubaliano, nilimwambia mwenye shamba ni ndugu yangu na ningehakikisha analipata ila... nikamwomba malipo yaani... nimfanyie kama udalali maana, nilikuwa na uhakika kwamba Miryam angeliachia shamba, maana Mariam ni mgonjwa... ila ndo' kama vile sasa.... akaanza kuzungusha, na...."

"Na wewe ukawa umekula hela uliyopewa kabla jamaa hajakutana na mwenye shamba ili kulichukua, si ndiyo?" nikamuuliza hivyo kwa kumkatisha.

Akaangalia chini kwa kukosa la kusema.

Nikapiga ulimi mdomoni na kutikisa kichwa kwa kutoamini haya yote, nami nikamwambia askari, "Kaka, unajua huyu jamaa ni mpumbavu sana?"

"Hata mi naona. Wewe utauzaje mali isiyo yako?" askari akamwambia hivyo Joshua.

"Halafu unasema Miryam akaanza kuzungusha, ulikuwa umeongea naye?" na mimi nikamuuliza hivyo.

Likabunda tu namna hiyo hiyo.

"Kwa hiyo we' ukala hela ya watu, halafu ukafikiria nini, ah... 'nitamuua tu Mariam, Miryam atasaini paper, kikishahamishiwa jina langu nitakiuza,' easy money. Are you fucking crazy? Kuiba... sisi wote hapa tumeshaiba, hata kama ni kudokoa shilingi mia utotoni, ilikuwa ni kuiba, lakini.... kuua? Kumuua ndugu yako wa damu ili tu upate hiyo shilingi mia? Joshua we' ni mtu wa aina gani? Tena mpaka unatuma watu wakambake, hivi kweli... ah! Unajua watu kama nyie ndiyo mnaosababisha tusitembelewe na wageni kutoka sayari zingine!" nikaongea hayo kwa hisia.

Mpaka afande akacheka kidogo na kutikisa kichwa.

Joshua akanitazama na kusema, "Bro... me nikuombe msamaha tu kwa...."

"Whoa there! Ishia hapo hapo. Usiniombe mimi msamaha, haitakuwa na faida yoyote kwako. Niambie nini kinaendelea sasa hivi kwa huyo jamaa'ako... basi," nikamwambia hivyo kwa uthabiti.

"Alikuwa amenipa muda... ni..nikamilishe hilo zoezi..." Joshua akasema hivyo kinyonge.

"Zoezi la kumuua mdogo wako?" askari akamuuliza.

"Hapana... yeye hajui kuhusiana na hayo. Yeye alitaka tu... hilo shamba... ajengee mambo yake, na ndiyo anachosubiri mpaka sasa hivi. Ila... nilimcheleweshea... kwa hiyo akawa anataka nimrudishie hela yake la sivyo angenizingua... ni..ana... ana nguvu sana, ana pesa..." Joshua akaeleza kwa masikitiko.

"Itakuwa vizuri akija kukuchinja ili taifa lipunguze mbwa wengi kama wewe," askari akamwambia hivyo.

"Ni nani huyo jamaa? Wa wapi?" nikamuuliza Joshua.

"Huwezi kumjua..." Joshua akaniambia hivyo.

"We' ulimjuaje? Usilete ujuaji hapa, unapoteza muda, sema haraka!" askari akamwamrisha.

"Bro... nakuomba... nitakwambia ni nani, ila kwanza nisaidie kutoka hii sehemu," Joshua akaniomba.

"Usijali kuhusu kutoka hapa, utaondoka tu. Niambie jina la huyo mtu," nikasema hivyo.

"Halitasaidia kwa lolote... na ni mtu mkubwa..." Joshua akasema.

"We' unaogopa nini? Si uko sehemu salama, au? Unalindwa kabisa... niambie ni nani huyo, urudi ndani, afande aendelee na kazi zingine. Kama shida ni pesa unayodaiwa, sema ni kiasi gani, useme huyo mtu ni nani, tutamtafuta, tutamrudishia hela yake ili asije kumsumbua Miryam. Sijui unanielewa?" nikamwambia hivyo.

"Huwezi ukafanya chochote bro... me nakwambia..." Joshua akaendelea kusema tu upuuzi wake.

"Ish, hivi huyu...? Yaani najaribu kuku.... halafu we.... aisee! Mkuu, mrudishe tu chumbani kwake... asante," nikasema hivyo.

"Tembea!" askari akamwamrisha jamaa aingie selo.

"Kaka, please..." Joshua akawa ananiomba.

"Wewe, nimesema pita huku! Nitakugonga virungu usitembee kabisa?!" askari akamwambia kwa ukali.

Mimi sikutaka tena kujali kelele za huyo jamaa, nami nikaanza kuondoka hapo nikiwa nawaza kurudi tu nyumbani na mengine yangefuata baadaye. Inaonekana askari alikuwa anamsukuma Joshua arudi kupumzika chumbani kwake, na ile tu ndiyo nimeukaribia mlango...

"Manyanza.... Frank Manyanza..."

Joshua akawa amesema hivyo. Nilipigwa na kitu fulani mbele ya hatua zangu kilichofanya nisimame ghafla, nami nikageuka nyuma kumwangalia Joshua. Sasa wote yeye na askari walikuwa wamesimama usawa wa mlango wa kuingilia selo, huku Joshua akiniangalia kama anataka kulia.

"Nini?" nikauliza hivyo kwa sauti ya chini kiasi.

"Huyo jamaa... ndi..ndiyo jina lake. Frank Manyanza," Joshua akathibitisha.

Nikapiga hatua chache kuwasogelea tena, nikiwa makini sana, nami nikamuuliza Joshua, "Frank Manyanza? Ndiyo anayetaka shamba la Mamu?"

Akatikisa kichwa kukubali.

"Kwa nini?" nikamuuliza hivyo tena.

"Nimekwambia ana hela... ana.. anataka kujenga madude yake, sijawahi hata kukutana naye live, namjulia kwa mwakilishi wake tu... yeye nimemwona kwenye picha... basi. Ni... ana hela, anaweza kuwa hatari sana ndiyo maana nilifanya hayo yote... na sijui sasa hivi itakuwaje yaani..." akajibu hivyo kwa wasiwasi.

Nikaangalia chini nikiwa nahisi... kushangaa.

Afande akaniuliza, "Unamjua?"

Nikiwa nimebaki kutatizika kiasi, nikatikisa kichwa kukubali.

"Ih?! Umemjulia wapi?" Joshua akarusha swali kwa wasiwasi.

"Usiniulize mimi, niambie ukweli. Una uhakika wa asilimia zote kwamba ni huyo unayemsema ndiyo alikulipa?" nikamuuliza kwa mkazo.

Akasema, "Nn..diyo. Ni yeye. Sikudanganyi."

Nikatazama chini kwa kukosa amani kiasi.

"Unam... unamjuaje?" Joshua akaniuliza.

"Haikuhusu. Umepita huko kooote kwa faida gani sasa? Kuishia jela? Ngoja nikwambie kitu Joshua. Mungu huwa anatukutanisha na watu kwa makusudi yake. Usifikiri nilitua tu paap, na kuja kukutibulia mipango yako kimazingara... hapana. Mungu tu ndiye aliyenileta huku ili niweze kuisaidia ile familia... na ninakuhakikishia hili... nitaendelea kuwasaidia mpaka mwisho. Mungu ana maana yake, hata kama mimi bado sijaijua, lakini nitaiishi. Ila wewe ukishakaa jela... ndiyo utajua ulikuwa hujui," nikamwambia hivyo kwa mkazo sana.

Joshua akawa ananiangalia kwa uso uliojaa majuto mengi.

"Imeisha hiyo. Mweke ndani mkuu," nikamwambia hivyo afande.

Kisha nikageuka zangu na kujiondokea. Kweli yaani kuna mambo mengi yaliyokuwa yanatokea mpaka nikawa nawaza ikiwa yalipangwa, ama ilikuwa ni hatma tu. Subiri, hicho ni kitu kimoja, au siyo? Lakini hilo halikujalisha.

Hivi sasa kilichokuwa muhimu kufanya ilikuwa kusahihisha upuuzi wote wa Joshua uliosababisha maumivu mengi sana, na kwa jinsi mambo yalivyokuwa yameeleweka kwangu wakati huu, inaonekana ni kama Mungu alikuwa ananipa nguvu ya kuwa hilo suluhisho tena na tena na tena. Hata sasa, utata wote wa suala la shamba la binti Mariam ningekwenda kuutatua, ili nisaidie kuilinda haki yake haijalishi alikuwa chini ya hali ipi. Ilikuwa ni yake, na yake peke yake.

★★

Nikachukua usafiri, moja kwa moja kurudi Rangi Tatu, kisha nikapanda mwingine kuelekea Makumbusho. Nilikaa kwenye siti ya daladala hii nikiwa na mawazo sana juu ya kile ambacho Joshua alikuwa ametoka kuniambia muda mfupi uliopita. Moja kati ya mambo ambayo unakuwa hujatarajia kabisa, ile kwamba kumbe ni kitu ambacho unakijua ila tu hukuwa umekijua. Hata tu kukifikiria yaani.

Hii ishu ya kumpambania Mariam ilikuwa imeanza kupanda daraja kufikia sehemu ambazo sikudhani ningeweza kufikia kabisa, lakini angalau niliona ni kwa mwongozo wa Mungu tu nilikuwa hapa kuwa suluhisho. Maswali mengi ya ni kwa nini hali hii ilizidi kuwa yenye kuchanganya na kusisimua kwa wakati ule ule yalivamia kona zote za fikira zangu, lakini nilichokuwa naenda kupambania kwa sasa ni kuumaliza upande wa hayo mambo yote sasa hivi. Yakome kabisa.

Nimekuja kufika Makumbusho kwenye mida ya saa nne na nusu huko, asubuhi hii hii, nami kama kawaida nikatafuta Uber na kutoa agizo la kupelekwa sehemu niliyotaka kwenda. Haikuwa Royal Village kama nilivyokuwa nimezoea kwa hizi wiki chache zilizopita, zamu hii nilikuwa naenda sehemu ambayo, niliomba tu Mungu yaani ingemaliza huu utata wote wa suala la shamba la Mariam.

Haikuwa na umbali mrefu sana kwa usafiri huu, na baada ya kufika eneo husika, nikalipa nauli, kisha nikashuka na kusimama mbele ya jengo moja refu kishenzi. Kubwa vibaya mno kati ya majengo kadhaa yenye ubora wa hali ya juu ulioonyesha kwamba watu wa humo walikuwa ni wa kwenda na wakati, na pesa. Kwa anayejua maeneo haya vizuri akikwambia jengo la MWANGA HOTEL linafananaje, ndiyo utaelewa kwamba huo ni mfano bora kufananisha jengo hili lililokuwa mbele yangu. Vioo pande zote kuanzia chini mpaka juu!

Sikutaka kupoteza muda kuangalia hiki ama kile kwa sababu hii haikuwa mara ya kwanza kufika hapo, kwa hiyo nikaelekea tu ndani huko, nikipishana na watu mbalimbali ndani ya sehemu zenye vitu maridadi sana. Moja kwa moja nikaelekea mpaka kwenye lifti na kupandisha hadi ghorofa la nane huko, nami nikatoka na kwenda sehemu yenye meza ya msaidizi wa mkuu wa kitengo cha ghorofa hii ili nipate huduma.

Kufika hapo, nikamkuta mwanamke huyu mwislam, aliyevalia kwa unadhifu sana na hijab yake kichwani. Alikuwa mweupee kama Miryam tu, na mpaka nimefika mbele yake, alikuwa akiingiza vitu fulani kwenye kompyuta yake, kwa hiyo hakuniangalia upesi.

Nikasema, "Habari za asubuhi?"

Akasema, "Salama. Tafadhali, subiri pale niku...."

Akaishia hapo baada ya kuniangalia, akiwa na lengo la kunionyesha sehemu ya kukaa ili nisubirie. Lakini baada ya kuwa amenitazama, akaachia tabasamu pana la furaha lililofanya uso wake upendeze sana, nami nikatabasamu kiasi pia.

"Heey! Jamani, ni wewe?!" akauliza hivyo.

"Ni mimi," nikamwambia hivyo.

"Za siku? Huonekani..."

"Ahh, nilikuwa likizo. Ila niko hapa hapa Dar, so... leo nikaona nije kutembelea."

"Aisee! Naona una likizo nzuri maana unazidi kuwa handsome tu..."

"Ahahahah, umeanza!"

"Ahahaaa, kweli. Ila ni muda umepita jamani!"

"Sana."

"Karibu. Umekuja kuonana na Mr. Manyanza?" akaniuliza hivyo.

"Yeah. Nilikuwa maeneo ya karibu nikaona nipite kumsemesha kidogo. Yupo?" nikamuuliza.

"Yupo, ila yuko bize. Hana hata appointment yoyote, kazifuta nyingi maana kuna load kubwa ya kazi anashughulikia..."

"Ahaa, sawa. Sema, me nataka nizungumze naye kwa ufupi tu... ni muhimu sana. Sitammalizia boss muda wala."

"Mh? Ngoja nimpigie, kama ni wewe anaweza...."

"Oh no, usimpigie. We'... nipeleke tu ofisini kwake kwa hizi staarabu zenu, maana anaweza akakukatalia kwa phone. Twende tumshtukize," nikamwambia.

"Wewe! Unataka anichape?" akaongea kwa maringo.

"Ahahahah, anakuchapa vipi bwana? Labda tu kakibao kwa huko nyuma," nikamtania.

Akacheka kidogo na kusema, "Halafu wewe! Mhm, haya twende. Ila nilikuwa nimekumiss..."

Usishangae, nilikuwa mtu maarufu!

Akanyanyuka kutoka kitini na kujiunga nami, nasi tukaanza kuelekea upande wa ofisi ya huyo boss wake. Huyu mwanamke alikuwa na shepu! Kama vile wale midoli wanaovalishwaga nguo ili kuvutia wateja, namna hiyo. Alikuwa mrefu pia, mwenye uzungu kama wote, halafu hapa alikuwa ni secretary wa huyu jamaa lakini kimwana alitembelea gari la Prado utadhani yeye ndiyo alikuwa bosi. Hawa watu walikuwa wa maana!

Tukafikia milango mipana ya vioo ambayo ilituruhusu kuona vizuri undani wa ofisi ya bosi wake, naye akafungua tu na kwa pamoja tukaingia. Hapo mbele yetu ilikuwa ni sehemu pana na safi sana ambayo iliwekwa meza ya kioo kizito yenye muundo wa ukweli kama tu logo ya apple, ndefu na pana, kukiwa na viti viwili vikubwa vyeusi upande huu wa mwanzo, halafu kwenye mkunjo wa katikati upande mwingine ndiyo kulikuwa na kiti cha bosi.

Hapo alionekana mwanaume mtu mzima, akiwa ndani ya suti safi kabisa, umakini wake wote ukiwa kwenye mafaili kadhaa na makaratasi yaliyokuwa mezani kwake, huku akiandika mambo fulani na kwenye kompyuta yake pia.

Tukawa tunaikaribia meza yake, na bila kututazama, mwanaume huyo akasema, "Faima... nimekwambia sitaki disturbance yoyote ile hata kama ni Mama Samia ndo' amekuja!"

Secretary huyu, Faima, akacheka kidogo kwa pumzi, naye akasema, "Ni mtu muhimu zaidi ya huyo, boss."

Jamaa akapandisha macho yake, na baada ya kuniona, akaegamia kiti chake vizuri zaidi na kuendelea kunitazama tu. Mimi pia nikawa namwangalia kwa utulivu.

Huku akiwa anatabasamu, Faima akamwambia, "Samahani, ameomba kuongea na wewe kwa muda mfupi. Anasema ni muhimu. Dakika tano tu."

Mtu mkubwa akamtikisia secretary wake kichwa mara moja, naye Faima akaondoka na kuniachia uwanja hapo.

"Well, hii ni surprise. Sikutarajia," jamaa akasema hivyo huku akitabasamu kiasi.

"Yeah, sorry kuvamia namna hii, ila ni muhimu kuongea nawe ana kwa ana," nikamwambia.

"Ana kwa ana? Kweli itakuwa muhimu sana," akasema hivyo.

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Za huko ulikokuwa?" akaniuliza.

"Safi tu. Shikamoo mzee?"

"Marahaba mwanangu. Karibu."



★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★
 
Kaniambia hanitaki eti alidhani nitamlilia wakat Elton Tonny kashashusha mzigo
 
Kaniambia hanitaki eti alidhani nitamlilia wakat Elton Tonny kashashusha mzigo
Hili dude ni unpredictable kabisaaaaa
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…