SEHEMU YA 24
Mnaro nami nikakimbia mbio zangu zote, nikiwa nimebakiz hatua chache nikaona kama sitoiwahi kasi ile hivyo nikaamua kujirusha kupenya kwenye mlango ule kabla haujafunga....
Nikafanikiwa kuwahi, nikatua na kugeuka nyuma lakini sikumuona Mnaro, hata mazingira yalikuwa ni tofauti na ambayo nilikuwemo kabla, moja kwa moja nikagundua kuwa nilikuwa nimeingia Muifufu tayari. Kitu cha kushangaza ni kuwa sikuwa na nguo yoyote mwilini mwangu. Ikanibidi kuzunguka hovyo ndani ya pori lile kutafuta chochote cha kuvaa lakini sikupata kitu zaidi ya majani ya mgomba ambayo niliyaunganisha kwa kamba nilizotengeneza kutoka mgomba pia, kisha nikavaa kujisitiri halafu nikatembea kufuata maelekezo ya Mnaro ndani ya pori lile.
Ilinichukua kama saa zima mpaka kuanza kuona mji kwa mbali nikiwa ndani ya pori lile, nikawa makini zaidi na kugundua kuwa nilikuwa katikati ya miti ile iliyojipanga kwa mstari, nikatembea kuelekea nnje ya pori mpaka nilipoifikia mti ule wa mwisho upande wa kulia na kwenda kuweka mkufu ule ambao nilielekezwa kuuacha kwaajili ya Sauda ili atambue uwepo wangu ndani ya Muifufu, kisha nikaingia ndani ya mji ule bila hata ya kujua pa kuanzia.
Nilitembea nikirandaranda bila kuwa na pakwenda mwisho nikakuta gogo kubwa nyuma ya jumba lililojengwa kwa mawe, nikaamua kukaa hapo nikisubiri kupambazuke vizuri kwa maana kulikuwa na kagiza bado, tofauti na siku ambayo niliingia Muifufu kupitia nyumbani kwa Mnaro ambapo niliondoka kule ikiwa usiku lakini Muifufu kulikuwa mchana, leo kote palikuwa na giza.
Nikakaa pale mpaka nikajikuta nimepitiwa na usingizi.
Nilishituliwa na mlio wa mkali kama honi ya meli, nikaamka na kuona watu wakikimbia kuelekea huko ambako sauti hiyo ilitokea. Kulikuwa kumepambazuka tayari hivyo niliweza kuona kila kitu kwa ufasaha kabisa. Nikatamani kujua nini kilikuwa kinaendelea huko hivyo na mimi nikaungana na wakimbiaji wale kufuata mlio ule ambao nadhani ulikuwa ukilizwa kwa makusudi ya kuita watu.
Jambo ambalo nililugundua nikiwa katika kuwahi huko ni kuwa mimi nilikuwa tofauti na watu wote kutokana na kuvaa kwangu majani ya migomba, wenyeji wa eneo lile wangi walijifunga kaniki huku juu wakiwa hawakuvaa kitu, wengine walijifunga ngozi za wanyama mbalimbali lakini wengine ambao walikuwa na wachache tu walikuwa uchi.. uchi kabisa wa mnyama.
Nikaamua kuwa ni bora kufanana na wenyeji, vinginevyo ningeonekana mara moja kuwa mimi nilikuwa mgeni na sikujua madhara yangekuwa yapi kama ningeonekana mgeni.
Njia pekee ambayo ilikuwa rahisi kwenye kujifananisha na wenyeji wale ilikuwa kuwa uchi.. kuwa uchi hakuhitaji kuwa na chochote, ni suala la kuvua tu majani yale ya mgomba, niliwaza na kujiweka kujitoa polepole miongoni mwa wakimbiaji wale ambao bila shaka hakuna hata mmoja ambaye aliutambua uwepo wangu pale kwani hakuna ambaye alikuwa makini kwa mwingine.
Nikasimama na kuvua majani yale kisha safari ya ikaendelea nikijichanganya na ambao walitokea nyuma yangu, baadhi yao walikuwa uchi kama mimi hivyo kuniongeze ujasiri wa kuwa katika hali ile ya uchi hadharani jambo ambalo halikuwahi kutokea kabla maishani mwangu.
Tulikwenda mpka kufika kwenye uwanja mkubwa sana mbele ya jumba kubwa mno na la kifahari, jumba lile bado lingekuwa la thamani hata kama lingekuwa ndani ya dunia yetu hii yenye kila aina ya majengo. Katikati ya uwanja ule kulikuwa na mzee akiwa amekaa kwenye kiti akizungukwa na wasichana warembo kama nane hivi, pembeni yake alikuwa amesimama mwanaume wa kama miaka 40 hivi ambaye alikuwa mkubwa sana wa umbo na alikuwa na misuli ya ukakamavu hasa, mtu yule alikuwa mweusi tiii! Ngozi yake ambayo ilionekana kama ambayo imepakwa mafuta mengi sana ilikuwa ikin`gaa sana.
Watu wakaendelea kimiminika pale mpaka kukawa na kundi kubwa sana ambalo ilikuwa ngumu kuamini kuwa lote lilitokea ndani ya kamji kale kadogo.
Baada ya utulivu wa hekaheka za watu kupatikana, bwana yule mweusi sana akasimama na kuanza kuzungumza "wakazi wote wa Muifufu naomba mnisikilize kwa makini sana! Alfajiri ya leo kuna mtu kutola duniani ameingia Muifufu, mtu huyo ambaye mpaka sasa hatujamjua ameingia bila ruhusa wala taarifa kwa uongozi wetu na hatujui amewezaje kuingia wala hatujui ana lengo gani! Sasa tunataka kumpata mtu huyo ili kujua kilichomleta pamoja na kumuadhibu kwa kuingia kwake bila ruhusa, hivyo tunataka watu wote muwepo hapa! Kama kuna mtu kabaki nyumbani, awe mzee ama mtoto, mzima ama mgonjwa lazima aje hapa!. Tunatoa dakika kumi tu wote waliobaki nyumbani waje hapa". Mara baada ya kusema maneno yale minong`ono ya hapa na pale ikasikika huku baadhi ya watu wakikimbia, nadhani kurudi makwao kuwaleta ambao wamebakia nyumbani.