Simulizi: Msegemnege

Kweli Msegemnege Jumamosi tena 😂si uhai huo kufika majaaliwa.
 
Inavutia sana ila kaka JBourne59 weekend hadi weekend parefu sana,ikifika weekend hadi tunakua tumeshaanza kusahau mtiririko wa hadithi kaka,fanya walau jumanne au jumatano utupe walau viji TUPIO😂 viwili tuende sawa kaka,kama utakua na muda maana nje ya jf najua pia unatakiwa kufurahia pension na Shemeji Hamida😂
 
[emoji28]kijana tapeli wewe
 
Tupio la XXII - Ommy awasiliana na Nasreen


Ilipoishia…



Kiingereza 150,000 kwa mwezi

Hakutaka hata kusoma kwingine, akauliza

“Hii ya kusoma mwezi mmoja naweza kuanza lini!?” aliuliza na kuonesha pale aliposoma

“Ni wewe tu, hata kesho njoo uanze…” alijibiwa Omari kisha akaondoka.

“Da! Laki moja na nusu hata mjeda akizingua nitajilipia, ngoja kesho nije nianze…” Omari alijisemea.



Sasa endelea…



Omari alirudi nyumbani na jioni wakati wa chakula aliwashirikisha wazazi wake juu ya maamuzi yake ya kusoma kule ‘mjini posta’ badala ya Mwenge.

Mama yake hakuwa na kipingamizi na baba yake alisema…

“Kama nilivyokuahidi mwanangu, nitakulipia ada na nauli za kuendea huko masomoni kwako, najuwa huwezi kupata muda wa kufanya shughuli za pwani hivyo hutokuwa na hela.”

“Asante sana baba, tayari nimejiandikisha kuanza kesho…” Omari alihitimisha, kisha mazungumzo mengine ya kifamilia yaliendelea ingawaje si mama Omari wala Omari mwenyewe aliyemwambia afande habari za chupa na mambo yake.
---


Mwezi ulikatika na Omari akawa anaongea ‘kingreza’ ingawaje hakikunyooka, walimuambia ili awe mahiri zaidi inabidi ajiunge na awamu ya pili ambapo angesoma tena mwezi mmoja, lakini Omari alisema…

“As for now is enough…” walimu wake walifurahi pale na wote wakacheka kwa pamoja.

“Another time when get money will come” Alisisitiza kisha akaaga na kuondoka.

Lakini kumbe Omari aliwaza juu zaidi, hivyo akaondoka hadi Mwenge na kujisajili pale kwa Ras Simba, na aliporudi nyumbani aliwaeleza wazazi wake kuwa kesho ataendelea na masomo kwenye kituo cha Mwenge.

Hapo Mwenge alijifunza zaidi ya kuongea, maana alijifunza pia muundo wa lugha yenyewe kwa ujumla na baada ya miezi mitatu tayari Omari alikuwa na misamiati mingi kichwani na aliweza kuitumia ipasavyo ingawaje kwenye uharaka wa kuongea hakuwa spidi kubwa.

Baada ya miezi minne tangia aanze masomo, sasa aliweza kuitafsiri vizuri mwenyewe ile karatasi aliyoikokota kwenye chupa kule baharini.

Wakati yupo hapo Mwenge kujifunza lugha ya Kiigereza, alikutana na watu wengine ambao nao walikuwa wanajifunza, wengine walikuwa waliomaliza kidato cha nne, wengine wa kidato cha sita, wengine wa las saba kama yeye, wengine wasanii wa bongo flavor na maigizo ili mradi kulikuwa na watu wa namna tofauti tofauti.

Kwa kutumia uzoefu wa wenzake hapo kwa Ras Simba aliweza kupata kudodosa juu ya namna ya kwenda Dubai, China na baadaye sana ndio akachomekea Bahrain.

“Da, mwanangu kuingia Bahrain inabidi uwe na visaaaa…” Jamaa mmoja aliyekuwa anasoma naye ambaye alionekana kuwa ni mraibu wa dawa za kulevya kiasi alimuambia…

“Yani kutoka nje ya nchi hii inabidi upate kitabu babuuu…” aliendelea…

“Yani paspotibuku…”

“Kama haitoshi, inabidi uwe na yelokadi…”

“Yelokadi ni kakitabu fulani hivi ka njano ila nini mwana, inabidi wakudunge sindano mabegani…”

“Wenyewe wanaita yelofiva na zingine nini sijui nimesahauu…”

“Ila sikia mwana, zipo yelokadi za mchongo, hizo huchomi wala nini, ukienda pale mnazi mmoja nini, utawakuta wana watakudaka tu kuuliza kama, kama unataka yelokadi, basi unawagea ganji kidogo nusu saa nyingi wanakuletea kadi mpyaaaa, watachukua tu majina yako na nakala za pasbuku yako kwa ajili ya kujaza kadi yako…”

“Lakini mwana, ukirudi kuja kuriniu wenyewe wanavishtukia…, kama vipi we nenda tu kachome upate kadi yako mukide!

Nusu teja huyo alimueleza Omari mambo yote muhimu, inaonekana yeye ni mzoefu wa safari, sijui alikuwa punda!?
---


“Sina passport, sina yellow card, sina visa, mmmh, safari bado ngumu…” Omari aliwaza siku hiyo alipokuwa anarudi nyumbani.

Yule nusu teja pia alimuambia kuwa ili alingie Manama lazima apitie Sudani au Saudi Arabia…

“Bongo hatuna ubalozi na Bahrain mwana, inabidi uende hadi Khatourm au Jeda kukata visa ndio uchukue pipa uingie mjini Manamaaa!, vinginevyo, utarudia eapoti mwana” alikumbuka pia maeno hayo.

Omari katika dodosa dodosa yake pia aliambiwa visa rahisi kwa yeye ni ile ya utalii kwa muda mfupi na ambayo pia atatakiwa aoneshe uwezo wa kujihudumia akiwa huko na ushahidi wa tiketi ama hela ya tiketi ya kurudi alipotoka.

“Da kumbe wenzetu wanabana sana, sijui na sisi wageni wanaokuja kwetu huwa wanafanyiwa hivyo!?...” Omari alikuwa anajiuliza.

Kiufupi Omari alidhamiria kwenda Bahrain kukutana na mwenye barua, lakini ndio akawa anakutana na changmoto kama hizo ambazo baadhi amezivalia njuga ikiwemo suala la lugha ya kiingereza. Suala la safari bado alikuwa hajamshirikisha mama yake wala baba yake na wazazi wake hao walidhani mtoto wao kweli anantaka kuwa beach boy wa kutembeza watalii.

Usiku ule Omari hakupata usingizi wenye utulivu hasa akikumbuka yule nusu teja alivyo mwambia kuwa bila dola elfu moja safari haitokamilika…

“Tiketi ya kwenda na kurudi muda mwingine unaweza kupata kwa dola mia sita, lakini nakwambia bora uwe na dola elfu moja ndio utakuwa na ahueni, bila dola alfu hotoboiii…” sauti ya nusu teja ilimjia tena kichwani.

“Hadi sasa ni milioni moja tu…” Omari aliwaza

“Sasa hii si dola mia nne, bado dola mia sita hapa, du” Alijisemea.

Zile hela zilizozidi kwenye milioni moja alizitumia nyingine kununulia simu na nyingine alimpatia mama yake na kiasi alitumia kwenye matumizi yake ya kawaida na kwakuwa alikuwa haendi pwani tena kujishughulisha alikuwa hana kipato, bahati nzuri baba yake alimlipia ada zote na nauli kama alivyo ahidi.

Wiki moja baada ya kumaliza miezi mitatu kwa Ras Simba Omari akaanza kurudi tena kule pwani kwa ajili ya shughuli zake, akakuta kuna vijana wengine wemechukua nafasi yake, hivyo mgao ulikuwa mdogo akaacha ile kazi na kuamua kushida maeneo ya ‘kokobichi’ mida ya jioni kila siku ili ajifunze kuongeza na wazungu lakini pia kujifunza kazi yenyewe ya ‘ubichiboi’.

Juhudi zake za kukaa coco beach hazikuzaa matunda, ingawaje alifanikiwa kukutana na wazungu lakini wote walikuwa tayari na waongozaji wao…

“Oyaa, watasha wengi wapo Zenji, timba Zenji, wakishuka tu eapoti unaanza kubonga nao, au utaenda bichi wanakozagaa sana kisha unaongea nao, wakikuelewa mbona unatoka!...”

Beach boy mmoja alimueleza Omari mbinu kama aliyotumia yeye kuingia kwenye fani …

“Kama una makaratasi unaweza kwenda kuomba kazi kwenye kampuni tuaz ili uanzie humo upate uzoefu…” Huu ulikuwa ushauri wa jamaa mwingine mwongoza watalii pia.

“Kama uko mambo safi nini, jichanganye kwenye mahoteli makubwa wanakofikiaga, kwenye maswiminpuul nini mtakutana unaweza kuongea nao kirahisi mbona!...” Beach boy mwingine alimpa mbinu ‘ghali’.

Omari akawa anaanza kukata tamaa jinsi ya kuichanga hiyo dola mia sita aongezee kwenye nauli kwa kufanya kazi ya ubichiboy.

Hata hivyo aliwaridhisha wazazi wake kwa picha kadhaa alizofanikiwa kupiga na watalii akiwa maeneo ya ufukweni lakini hazikuwa na matokeo kwenye fedha…

“Bado sijapata wa kumtembeza mimi kama mimi, nimeanza kuzuga tu na hawa ili nipate uzoefu…” alikuwa akiwaambia wazazi wake maendeleo ya jitihada zake.

Siku iliyofuata hakutoka ndani bali alijifungia tu akiwaza nini cha kufanya.

“We Omari, vipi leo! Unaumwa? Mbona hutoki humo ndani na joto lote hili…”

Sauti ya mama yake ilisikika.

“Leo mama sijisikii vizuri, napumzika…” Omari alijibu.

Mle chumbani aliipitia mara nyingi ile barua na kujitia moyo huenda siku moja atafanikiwa. Atafanikiwaje, hata yeye alikuwa hajui.

Jioni yake akapata wazo la kupiga simu ile namba…

“Kesho nitaenda sehemu tulivu ili nimpigie simu Nasreen...” alijisema na kujikuta anatabasamu.

Omari alivyobadili tu zile fedha jambo la kwanza alienda kununua simu za bei nafuu ‘itel’ ilikuwa ni smartphone lakini ni 'lower end' kabisa kwa bajeti aliyoipanga. Simu yake ilikuwa na uwezo wa kuwa na application za facebook na whtaspp pia.

Kesho yake Omari mida ya mchana alitoka kwenda Msasani beach club, hakuwa mgeni hapo kwani siku za weekend alikuwa akija mara kwa mara kuwaangalia Akudo Impact waliokuwa wakitumbuiza hapo, na alikuwa anaingia bure kwakuwa walinzi wa getingi walikuwa wanamfahamu kuwa ni mtoto wa Afande mwenzao.

Sasa siku hiyo alienda hapo mida ya mchana, na kuagiza kinywaji baridi, akiwa ndani ya ukumbi kwenye utulivu akaamua kupiga simu…

“Halo, assalaam alaykum…” Sauti nyororo kutoka upande wa pili ilijibu…

“Waalaikum salaam, are you Nasreen?” Omari alitema ung’eng’e…

“Wafaq aismi Nasreen, min hadhih min fadlik wamin ain hasalat ealaa raqami?”

Sauti nyororo iliongea kutoka upande wa pili na ilikuwa ya ukali kidogo ila nzito kama vile aliyekuwa anaongea alikuwa ametoka usingizini akimaanisha ‘ndiyo mimi naitwa Nasreen, je wewe ni nani na namba yangu umeipata wapi?’

Omari wala hakuelewa na akawa kama ametolewa mchezoni vile akajikuta anasema…

“Whasap, will send yu meseji wasap…”

Sauti ya Nasreen ikasikika “Ok send me a massage” na simu ikakatwa.

Omari alifurahi na kuchukia kwa wakati mmoja, hakujua hata aandike nini. Leo rasmi akaisevu ile namba kwenye simu yake.

Hakuwa mjuzi sana wa mambo ya whatsapp, lakini alijitahidi kuandika ujumbe na kuutuma…

My name is Omari Juma. I am coming from Tanzania. I found the message you wrote in the bottle. I want to come and see you. Thank you.

Hivyo ndiyo alivyoandika Omari akimaanisha kuwa ameiona ile karatasi kwenye chupa na anataka aende Barhain kumuona Nasreen.

Haikupita sekunde nyingi simu ya Omari ikatoa mlio wa ujumbe wa whatsapp…

Nasreen: “Wow, Its so great you found it, ‘been waiting for so long, where did you find it?, where? When are you coming to Manama?”

Omari: “My English is not good, but the problem is passport, visa and ticket”

Nasreen: “Okay, send me photo shot of the message you found”

Omari akachukuwa nakala ya ile meseji kisha akaipiga picha na kuituma.

Omari: “I sent you a photo, did you see?”

Nasreen: “Ok, I’ve just seen it, but I need to see the original, and if you don’t mind make a video call so that I make sure I’m talking to the one who real found the bottle.”

Omari: “Okay, will call you in fews minutes, I have to go back home”

Nasreen: “Ok, Omari, I’m so eager to see you and the message”

Omari akazima data kisha akatoka mle ukumbini haraka na kudandia DCM iliyomfikisha Ukwamani.

Akiwa chumbani kwake, akaitoa ile barua ‘original’ na akawasha data kwenye simu kisha akapiga video call…


Inaendelea…
 
Tupio la XXIII - Junior na Kipaji kingine


Ilipoishia...


Hitimisho la kikao hicho ikawa ni St. Anne kuamua kumfadhili mtoto katika masomo yake kwa programu maalum watakayo muandalia.

Mama Onesmo alifurahi kupunguziwa mzigo wa kugharamia ada na pia kutambuliwa kwa uwezo wa mtoto wake kitaaluma.

Waliondoka pale eneo la shuleni na kuwahi kurudi nyumbani ambapo jioni hiyo kulikuwa na kuandaa kwa ajili ya jumuiya asubuhi.



Sasa endelea..


Usiku ule Vai akiwa usingizini aliota ndoto ya ajabu. Ndotoni aliambiwa na mtu asiyemfahamu kuwa asikubali mtoto wake asomeshwe nje ya Morogoro…

“Usikubali, watakunyang’anya mwanao…” Sauti ya mtu wa ndotoni ilimuasa Vailet.

“Watampeleka nje ya nchi, atakaa huko, watampa uraia huko, atabanwa na majukumu mengi ya masomo na miradi mbalimbali, kuonana kwenu itakuwa tabu ingawaje nawe watakuchukua ukae naye huko…” Sauti ile iliendelea kuasa..

“Mwisho wa yote ataingizwa katika imani za kumtumikia Ibilisi…” Sauti ile ilimaliza.

Asubuhi akaikumbuka ile ndoto yote na jinsi alivyoaswa akaona ni vyema amshirikishe mama Rose.

Baada ya kusalimiana Vai akaanza…

“Shoga, leo nimeota ndoto ya ajabu sana…”

Mama Rose naye akajibu ..

“He, basi leo sote tumeota ndoto za ajabu, haya hebu nisimulie yako name nitakusimulia yangu…”

Vai akamuelezea mwanzo hadimwisho kadri alivyokumbuka ile ndoto, kisha naye mama Rose akaanza kusema…

“Makubwa, nami nimeota hivyo hivyo lakini kwa mtindo tofauti. Nimeota wamekuja wazungu wakawa wanakunyang’anya mwanao nawe ukawa unamshikilia hutaki atoke mikononi mwako, ukawa unapiga kelele unaomba msaada lakini hao wazungu walikuwa na silaha hakuna mtu aliyesogea kukusaidia, hata mimi nilishindwa kusogea nikabaki kupiga kelele tu hadi nikashtuka usingizini…”

Wakashauriana pale mwishowe wakaamua jioni watakavyokuja wana maombi kusali basi waliweke suala hilo mezani ili waone jinsi ya kuyaendea maombi.
---


Shule ilipofunguliwa, Mama Junior alifika shuleni kwa mwanawe na kuomba kuonana na mkuu wa shule. Walivyoonana akamueleza kuhusu mtoto Onesmo amekubali asomeshwe na shule lakini asiondolewe kwenda popote zaidi ya shule hiyo hadi atakapo maliza darasa la saba. Huko mbele watakaa tena kuona lipi litafaa.

“Mama Onesmo, kwani nani amekudokeza kuwa mtoto ataondolewa hapa shuleni?” Mkuuwa shule aliuliza.

“Hapana Sista, hakuna aliyenidokeza, ila tu sipendi kukaa mbali na mwanagu.” Vai alijitetea.

“Eee, mwaka huu tumepanga mwanao afanye mtihani wa darasa la nne, hivyo atasoma masomo rasmi ya darasa la nne, akifaulu mwaka unaofuata tutamsomesha darasa la tano na la sita kwa wakati mmoja huku tukimuangalia uwezo wake wa kuhimili masomo hayo ili tukiona anazidiwa basi tutamkaririsha darasa….”

Sister Consolata alimueleza mama Junior mpango wa idara ya taaluma shuleni hapo juu ya Onesmo.

Vai aliondoka shuleni hapo akiwa na furaha baada ya kusikia kuwa hawakuwa na mpango wa kumuhamisha mtoto kwenda shule nyingine.
---


Kutokana na umbile dogo la Onesmo na pia umri kulinganisha na wengine darasani, alikuwa akipata manyanyaso mara kwa mara kutoka kwa wanafunzi watukutu darasani mwake. Shule ilikuwa ya bweni. Hali ile iliendelea hadi siku moja Onesmo alipomwagiwa uji kwenye mwili wake lakini bahati nzuri uji haukuwa wa moto sana ila ulimuunguza kiasi, Onesmo alilia sana siku hiyo hadi kiongozi wa bwalo hapo shuleni alipomsaidia kumsafisha na kumbembeleza hadi akatulia.

“Asante anko Jose, ukiwa unarudi nyumbani leo utaokota hela.” Onesmo yalimtoka maneno ambayo hakuna aliyeyatilia maanani pale jirani si hata Joseph aliyekuwa msimamizi wa bwalo la chakula.

Jioni kwenye kipindi cha michezo, Junior alitaka kunyanyasika tena, lakini wakati 'timu kunyanyasa wenzao' hawajaanza kumsukasuka Onesmo, akanyoosha mkono mmoja kama ishara ya kuwaambia subirini kwanza…

“Subirini kwanza, kuna ajali imetokea, baba yako Fredi amegongwa na pikipiki, sasa hivi…” Onesmo alisema.

“Nini wewe unasema!, nani amegongwa na bodaboda?!!...” Sauti ya Fred ambaye ndiye aliyekuwa kinara kwenye kumnyanyasa ikasikika.

“Ndiyo, kama unabisha nenda kwa Patroni uombe kuongea na baba yako…” Onesmo alisema kwa kujiamini.

Mbio, Fredi akakimbia kwenda kwa mlezi wa kiume wa wanafunzi na kumuomba aongee na baba yake…

Baada ya mahojiano kidogo, Patron akatoa simu yake na kumpigia mzazi wa Fred…

“Halooo!...” Upande wa pili wa simu ukajibu

“Hallow, mzee Wiliam habari za leo?” Alijibu Patron

“Hapa ni hospitali ya Kiegea, ninayeongea ni muuguzi wa hapa, mwenye simu amepata ajali amevunjika mguu, tupo tunamuandaa kwa ajili ya kuhamishiwa rufaa mjini, hivyo nakushauri uende rufaa muda huu…” Ile sauti ya upande wa pili ilisikika

“Fred, nenda bwenini kwanza nikukuja…” Patron alijaribu kumghiribu Fred…

“Niambie Patron, baba amegongwa na bodaboda?!!...” Fred aling’aka kwa sauti huku akianza kulia

“Umejuaje Fred…!!?” Aliuliza kwa kushangaa yule Patron

“Basi Onesmo kasema kweli…” Fredi akaangua kilio

Sauti ile ya Fred ikavutia walimu na wafanyakazi wengine pale shuleni wakasogea kutaka kujua kulikoni.

“Eee kuna ajali imetokea, baba yake Fred amagonjwa na pikipiki na kuvunjika mguu, anahamishia hospitali ya rufaa kutokea Kiegea.

“Oh maskini, wamekupigia simu?” Aliuliza Mwalimu wa zamu…

“Hapana, mimi ndiye nilipiga simu…” Alijibu Patrol

“Imekuwaje kwani hadi wewe ndie upige simu, ulijuwa kuwa kuna ajali?” Aliuliza mwalimu mwingine

“Hapana, ni Fredi alikuja kwangu akiniambia anataka kuongea na baba yake ndio nikapiga simu…”

“We Fred, kwanini ulitaka kuongea na mzazi wako nje ya utaratibu wa kawaida…, eeeh!” Mwalimu wa zamu alihoji…

“Junior huyo, aliniambia baba yangu amegongwa na bodaboda ndio nikaja kwa Patron…” akiwa bado Analia kwa sauti ya chini alijibu na kufanya watu wote pale wapigwe na butwaa

“Junior again, call him, hurry up!” Sister mmoja ambaye alikuwa mwalimu pia aliamrisha Junior aitwe.

“Akija usimkaripie, tumuhoji taratibu…” Patron kwa busara alishauri.

“Nimeshachoka!, kila saa Junior kapigwa, kila saa Junior kafanywa hivi kila saa Junior Junior, I’m fed up with him…” Sista yule aling’anka.

Sista Hyacinta ni mmoja wa walimu wakali sana hapo shuleni na anasifika na wanafunzi eti kuwa ana roho mbaya.

Punde si punde Onesmo akafika mbele ya hadhara ile na Patron akaanza kumuuliza…

“You!, what did you tell Fred?”

“Sorry Sir and Madam, Fred his friends wanted to bully me, so I stopped them by telling bad news…” Onesmo alijibu

“What bad news did you tell them…?” Sister Hyacinta alimuuliza

“I, I, I (ai ai ai) I told then Fred’s dad got an accident…”

“What!???” Mwalimu wa zamu alishangaa

“How did you know?!” akauliza

“I (aiiiiiiiiii) I know Sir, I even know you didn’t sleep ata your home yesterday!” Onesmo akaropoka…

Flap!

Sister Hyacinta kibao (kofi) likamtoka na kumnasa Onesmo. Onesmo akaanza kulia huku akishikilia shavu lake…

“Lets go to the office, that is bad manner Junior!” Mwalimu wa zamu alisikika na wote wakaanza kuondoka aneo lile kuelekea ofisi ya mwalimu ya nidhamu.

(kwa sauti ya kunong’ona Mwalimu mmoja akamuuliza Mwalimu wa zamu)

“Ni kweli hukulala nyumbani jana?”

“Sijui hata amejuwaje, maana jana nilikula kona saa nne za usiku kwa kisingizio cha udharura shuleni, hivi sijarudi nyumbani hadi saa hizi…”

Yule mwalimu akaanguo kicheko cha chinichini na kusema…

“Kumbe Onesmo kasema kweli, msimuadhibu, mpeni tu onyo na mkumbusheni somo la bad manners”
---


Hospitali ya rufaa, mzee William alifanyiwa upasuaji na kufungwa vyuma (antenna) na dawa za kutuliza maumivu na za kupambana na maambukizi ya bakteria kisha akaruhusiwa kurudi nyumbani.

Fred hakuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya mawasiliano ya baba yake, baba yake ndiye alisema atakuja shuleni kesho yake kumtoa wasiwasi Fred.

Onesmo hakuadhibiwa, lakini walitaka kujuwa alifahamu vipi kuhusu ajali na kuhusu mwalimu kutokulala nyumbani ambapo kila akiulizwa Onesmo alikuwa anajibu…

“Najuwa tu, hata wewe (anataja muda) umefanya kadha wa kadha…”

Onesmo aliweka hadharani baadhi ya mambo ya watu kila wakimhoji hadi wakamfukuzu aende bwenini.

“Hahahaaa, leo tumejua siri zenu…” Yule mwalimu wa kunong’ona alirudia tena kunong’ona akiwaambia walimu wenzake akiwemo mwalimu wa nidhamu ambaye siri yake ilikuwa ya aibu zaidi.



Inaendelea…
 
Tupio la XXIV - Usilolijua ni sawa na usiku za giza totolo!


Ilipoishia…



“Karibu shoga uketi, hapa ndio ofisi ya jumla….” Alisema Mourine

Queen hakujibu kitu alikuwa anashangaa tu mazingira ya pale na mlolongo mzima wa kufika eneo lile.

Wote wakaketi kwenye viti vilivyokuwepo pale na kusubiria. Kulikuwa na magazeti yote ya siku hiyo hivyo wote wakashika magazeti kupotezea muda, wala haikuwa kawaida yako kusoma magazeti.


Sasa endelea…


Sekunde kadhaa baadaye mlango mmoja ukafunguliwa na akatokea mtu mmoja wa makamo aliyevalia nadhifu akiwa amechomekea shati lake vizuri, viatu vyake vikiwa vimeng’arishwa ipasavyo.

“Karibuni sana…” Alianza kusema

“Queen umechelewa sana kuja, kwanini?!” yule mbaba kumbe alikuwa anamtamba Queen.

Kabla Queen hajajibu, akaingia dada mmoja naye akiwa amevalia nadhifu akiwa na kifungua kinywa na kuweka pale kwenye meza ndogo baada ya kusogeza magazeti pembeni kidogo, kisha akageuka na kuondoka alipowaambia karibuni.

“Queen na Mourine mtakuwa timu nzuri sana, actually ni team tayari…” aliendelea kuchombeza yule baba.

“Endeleeni kuburudika na staftahi wakati kutisubiri kikao kinachokuhusu”

Muda wote huo Queen alikuwa haelewi moja wa mbili.

“Umri wako unaruhusu, elimu uko vizuri, haiba inaruhusu, afya yako tutarudia kuipima tena, huna historia ya uhalifu, kuhusu kazi kwa bidii tunajuwa uhodari wako, uvumilivu unao, karibu sana Queen eeee naona muda wa kikao tayari nifuateni…”


Queen anaelezea…


Yule baba alikuwa anajiongelesha lakini hata sikuwa naelewa vizuri kinachoendelea hadi nilipoingia kwenye kikao…

Katika kila chumba cha kikao, kulikuwa na watu wengine sita na kufanya jumla tuwe watu nane mle ndani maana Mourine hakuingia kwenye kikao kile, yeye alirudia mlangoni baada ya kuashiriwa arudi.

Miongoni mwao alikuwepo mmoja akiwa amevalia sare za jeshi la Polisi na manyota nyota yake hata sijui ndio cheo gani kile.
---


“Karibu sana Queen, pole sana kwa kupoteza wazazi…” Alianza kuongea mmoja wa wale watu ambaye yeye alionekana ni mtu mzima zaidi kuliko wote mle ndani.

“Hapa ni ofisi ya jumla ya Polisi, Jamhuri inakuhitaji uitumikie katika kazi kwenye jeshi hili, hivyo utapitia utaratibu wa kawaida kisha utaenda chuo kikuu Kilimanjaro kwa miezi mitatu halafu utarudishwa chuo kikuu cha hapa Kurasini kwa miezi mingine utakayoambiwa kisha utaajiriwa rasmi na kuanza kulitumikia jeshi kwa nafasi utakayopangiwa…”

“Mama yako ameifanya kazi hii kwa weledi mkubwa hata baba yako pia lakini yeye alikuwa chini ya Wizara ya nchi na wana heshima kubwa sana katika nchi hii…”

“Kwakuwa umechelewa kuja, utaungwa kwenye mpango wa dharura (Crash program) hivyo mara baada ya kikao hiki utaendelea na hatua za kawaida za awali na ukiwa okay utaenda chuo kikuu Kilimanjaro wiki hii.”

Hapo nilizidi kuchanganyikiwa kwa maelezo yale, yani mama yangu mimi alikuwa Polisi? Kila siku si alikuwa anaenda kula kazini kwake badarini, baba naye eti alikuwa wizara ya nchi wakati tulimuona akiwa anahangaika na biashara zake, mmh.

Nilijikuta nakubali tu kufuata utaratibu.

Moja ya utaratibu ulionishangaza ni kuvuliwa nguo zangu na kukaguliwa, tena na mwanaume! Mwe!, nikawa naona aibu, ingawaje hao hao wanaume nimewavulia sana nguo na kufanya makubwa, leo mimi Queen naona aibu hahahha.

Baada ya vipimo vyao nikaambiwa majibu yatatoka baada ya siku tatu, hivyo Mourine anilete.

Kutoka chumba kile nilipitishwa milango mingine na hatimaye tukatokea kwenye parking za magari ambapo nilimkuta shogaangu Mourine.

“Tukapande gari lile paleee…” Mourine aliongea na kuniongoza.

Ukimya ulitawala na hatimaye tukashushwa maeneo ya ‘Posta baharini’ jirani na benki ya NBC kisha gari lile likatokomea nami sasa nikapata muda wa kumsuta shogaangu…

“Yani wewe Mourine, kumbe muda wote nipo na wewe kumbe wewe ni polisi?!!”

Mourine akawa anatabasamu tu.

“Tunavyochomoka chomoka kwenye misala yote tukiwa viwanja kumbe mwenzangu una yako unayoyafanya hadi tunasalimika! Sasa naanza kupata picha…” alikuwa analalamika Queen.

“Haya wewe umeanza lini?” Queen alimuuliza shogaake…

“Huu mwaka wa sita sasa shoga, na hapa natakiwa niende kozi wanipe ua langu niwe sajini wa kituo….”

Queen alizidi kupigwa na butwaa…

“Hebu twende nyumbani kwanza ukanieleze vizuri maana hata sielewi elewi”

Wakaitisha Uber ni kwenda Tabata.
---


Mourine anaelezea…


Miaka mitatu iliyopita, niliamriwa na mkuu wangu wa kazi kuwa nikufuatilie na kujenga urafiki na wewe, nikafanya kila niwezalo nikakutoa kwa Jacquelene ambaye naye ni mwenzetu lakini yeye alikuwa anaremba kukulengesha inavyotakiwa. Hivyo jukumu hilo nikapewa mimi, na ndio maana nikatengeneza ugomvi kule Sinza kisha kufanya uhasama wa uongo na Jaq ili uwe nami na kweli nikafanikiwa tukahamia Tabata.

Mengine sijui lakini kazi yangu nimeifanya vyema na umefuzu katika mpango maalumu wa kupitia mazingira magumu ya kazi za ukahaba na mazingira hatarishi yote hii ilikuwa ni kukuandaa ili uje ulitumikie vyema jeshi.

Nilifurahi sana moyoni siku ile uliponiambia umepiga simu ofisi ya jumla na ukaambiwa kuwe mimi ndio nikulete, lakini sikutaka nianze kufunguka mimi bali upate kutoka huko. Hivyo shogaangu naelewa yote tangia mwanzo na sasa nashukuru kazi hii nimeikamilisha sasa nitapata nafasi ya kwenda kozi.

Queen akawa anashangaa tu kisha akasema…

“Ama kweli, humu duniani haifai kumdharau mtu yoyote yule, hata kama kahaba hahahahaha…”

“Enhe, wamekuambiaje kwenye kikao?” Aliuliza Mourine

“Mmh mwenzagu, wamenivua nguo, na mwanume akawa ananikagua, eti nikawa naona aibu heheee”

“Wamenipima pima weee mavipimo yao na kisha wakaniambia keshokuta majibu yatakuwa tayari hivyo mtondo unipeleke tena…” Alisema Queen

“Halafu shogaangu, ndio nini kunipitisha kwenye vichochoro vile visivyoeleweka wakati kulikuwa na njia nzuri tu ya kuingia na gari? Queen aliuliza

“Wale wauza vocha pale ni wenzetu na ile ndio njia ya kwa miguu, kama tungekuwa tumetoka na gari yetu basi tungeingilia sehemu nyingine, lakini gari yako haijasajiliwa isingeruhusiwa kuingia, utaratibu ungekuwa mrefu, bora hata hivyo umejifunza kitu…” Mourine alijibu.

“Sasa nikienda huko chuo kikuu nikigraduate kazi yangu itakuwa nini…” Queen alikuwa na wahaka!

“Huko Kilimanjaro utasomea mambo ya awali, baada ya hapo ndipo utasomea unachotakiwa kukufanyia kazi, na utaelezwa huko huko chuoni, mie mchanga wa pwani huoo nimeshamaliza kibarua changu…” Mourine alimpa mashamsham mwenzake.

“Kazi zangu je itakuwaje, duka langu, mambo yangu mengine…” Queen alihoji

“Kwani mie umeona nazuiwa kufanya mishe zangu? Duka lako litaendelea kama kawaida lakini kaka yako mlokole handsome boy usimwambie, tafuta lugha yoyote ya kumdanganya.” Alisisitiza Mourine.

“Hapa sasa mambo yameshakuwa mengi, itabidi nimkabidhi Alex mambo yangu ayaendeshe, mie nisingizie naenda Nairobi kwenye mambo ya Kampuni nilioachiwa na baba…” alisema Queen.

“That sounds good!, naona sasa akili yako inafunguka…”

Waliongea siku hiyo kwa kirefu sana maongezi ambayo hayakuwa ya kawaida kwao, yalionekana ni kikazi zaidi na Queen alianza kuelekea kwenye hali ya kiutumishi.
---


Itaendelea wakati mwingine in shaa Allah
 
Aiii hapa kwa ommy pamenoga bwana
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…