Tupio la XXV - Makao
Ilipoishia…
Omari akachukuwa nakala ya ile meseji kisha akaipiga picha na kuituma.
Omari: “I sent you a photo, did you see?”
Nasreen: “Ok, I’ve just seen it, but I need to see the original, and if you don’t mind make a video call so that I make sure I’m talking to the one who real found the bottle.”
Omari: “Okay, will call you in fews minutes, I have to go back home”
Nasreen: “Ok, Omari, I’m so eager to see you and the message”
Omari akazima data kisha akatoka mle ukumbini haraka na kudandia DCM iliyomfikisha Ukwamani.
Akiwa chumbani kwake, akaitoa ile barua ‘original’ na akawasha data kwenye simu kisha akapiga video call…
Sasa endelea…
(Video call)
Omari: “Haloo!”
Nasreen: “ Hi, you are handsome!”
Omari: “Oh, thank you…”
Nasreen: “Is that your room?”
Omari: “Yes, me living with my parents”
Nasreen: “Owh, you’re living with your parents in the same room?!”
Omari: “No, no ,no, me live my room and my parents their room”
Nasreen: “Okaaay, now show me the original paper you found in the bottle”
Omari akaichukua ile karatasi orijino, akaikunjua kisha akaelekezea kwenye jicho la kamera ya simu yake…
Nasreen: “Yes, adjust the distance a bit so that I see well”
Omari akasogeza nyuma kidogo simu yake
Nasreen: “Yes, wow, that is the original one, good, now what about the bill attached?”
Omari akafunua mchago wake kisha akatoa kibunda cha elfu kumi kumi zilizokamilisha kuwa milioni moja
Nasreen: “What are those?! You are own money?”
Omari: “This is what I found on the bottle also…”
Nasreen: “I instructed to keep one bill, where is it?”
Omari akaelewa na kukumbuka alipoiweka ile noti moja ya Bahrain, akaitoa kwenye wallet kisha akamuoneshea kupitia camera
Nasreen: “Yes, that is 20 bill of Bahrain dinar, zoom a bit so that I can see well”
Omari akafanya kama alivyo elekezwa hadi Nasreen aliporidhika na muonekano kisha akasema…
Nasreen: “Oh yes, it’s exactly same number as recored before I put them in the bottle”
Nasreen: “Okay Omari, how much is that you showed me ealier”
Omari: “One Million Tanzanian Shillings”
Nasreen: “Wait a second…”
Nasreen akafanya hesabu zake haraka haraka kisha akasema
Nasreen: “It looks like you have all the money I put in the bottle, so wonderful”
Omari: “No, I spent about one lakhi and twenty buying this smartphone…”
Nasreen: “One lakhi?!!”
Omari: “Yes, one hundred thousand and twenty thousand Tanzania shillings”
Nasreen: “So you are telling me, you can buy a smartphone with just one hundred thousand in your country?”
Omari: “Yes”
Nasreen: “What’s the make of your phone?”
Omari: “Itel”
Nasreen: “I see”
Nasreen: “You are so honest Omari”
Waliendelea kuongea pale weee lakini wote wakivunja kiingereza ingawaje walikuwa wanaelewana.
Omari alikuwa na kichwa kizuri kwenye kuhifadhi mambo, ni kwamba alivyomaliza darasa la saba, kichwa chake hakikushughulishwa na mambo mengi hivyo kilikuwa na nafasi ya kutosha kuhifadhi vitu ndio maana hata kusoma kiingereza na kuongea aliweza kwa muda mfupi.
Baada ya kuongea sana na Nasreen hatimaye wakahitimisha kwa siku hiyo…
Nasreen: “I will call you tomorrow in shaa Allah after swalatil ‘isha”
Omar: “Ok, thank you”
Nasreen: “Bye”
Omari akawa na furaha sana kwa kuongea na rafiki wa mbali, rafiki aliye mpata kwa bahati nasibu (ee ndugu msomaji, hii sasa ndiyo bahati nasibu, wengi huchanganya kati ya bahati nasibu na kamari. Kamari ni mchezo unaodhulumu wengine na kumpa mmoja faida kiasi lakini mwendesha Kamari hufaidika zaidi, unaweza kusema bahati nasibu ni ‘zari’.
Siku hiyo Omari alilala akiwa na amani na wala hakumshirikisha yoyote mle ndani mwao.
---
Jana yake, baba yake Omari alisoma ‘oda’ kwenye ubao wa matangazo kazini kwake kwamba keshokutwa (kesho) mapema saa moja asubuhi anatakiwa aripoti makao makuu, hivyo afike ofisi ya siioo (CO ) akachukue barua ya maelekezo. Wakati akimueleza mke wake alionekana akiwa na wasiwasi mwingi kana kwamba kuna jambo baya litaenda kutokea kwake.
“Nimeitwa makao, sijui hata kuna nini, ni mimi tu kwenye kambi yetu ambaye nimeitwa, sijui ndio naenda kupewa barua ya kustaafu ama kuachishwa kazi…”
“…lakini kama ingekuwa kuachishwa kazi kwa makossa yangu lazima ningepelekwa kortimasho kwanza nihukumiwe…”
Afande Juma alikuwa hana furaha akiwa anamueleza jambo hilo mkewe. Akachukuwa buti zake mpya na kuanza kuzisafisha kisha kuzipiga dawa ya viatu (kiwi). Alitumia muda mrefu kuving’arisha hadi aliporidhika, viatu vilikuwa vinang’aa kiasi cha kuweza kujiona ukiviangalia hususani kwnye pua ya buti.
Asubuhi saa kumi afande juma aliamka, akaoga na kujiandaa kwa kuvalia nadhifu. Alivaa sare zake mpya ambazo alikuwa hapendi kuzivaa, akavaa na nishani zake zote alizozipata nchini baada ya kutekeleza fatiki kadhaa kwa umahiri lakini pia alivaa nishani yake aliyopata alipotoka mafunzo ya vilipuzi huko ughaibuni. Akavaa buti zake na akaving’arisha tena kwa pamba laini aliyokuwa nayo kwenye mfuko wa suruali. Hakika alipendeza.
Saa kumi na moja na nusu alitoka nyumbani hadi ukwamani stendi ya daladala ambapo alipanda gari za kwenda Mwenge, hapo Mwenge akapanda gari za kwenda Posta na akashukia kituo kiitwacho ‘Palm beach…” kutokea hapo alivuka barabara na kuelekea makao kwa kutembea kwa miguu. Kwa kuwa ilikuwa bado ni mapema, alitembea taratibu ili asitokwe na jasho pia asichafue viatu vyake.
Alienda moja kwa moja hadi lango kuu…
“Jambo afande!” baba Omari alisalimia kwa ukakamavu pale getini alipokutana na askari jeshi wa zamu aliyemruhusu kuingia sehemu ya mapokezi.
“Jambo!, habari za huko utokako lenzkoplo!” Aliitikiwa salaam baada ya kusalimia tena huku akipiga saluti kwa mkuu wa askari wa zamu waliokuwepo hapo mapokezi…
“Wewe lenzkoplo hebu jitambulishe kwanza!” Sauti nyingine ya kukoroma ilisikika, alikuwa ni mteule daraja la pili ambaye alikuwa amevalia mkumbulu maridadi kabisa(sash) akiwa anamnyooshea fimbo yake (walking stick) baba Omari…
“Emtii saba kenda (ngapi ngapi) alitaja namba, natokea miatano ishirini na moja keijei, lenzkoplo Juma Bakari Omari Sa! (sir)” Kwa ukakamavu kabisa afande Juma alijitambulisha kama inavyotakiwa… ingawaje mteule yule alimfanyia dhihaka jeuri tu ama kutaka kumpa kashkash kidogo kama ilivyo kawaida kwa mkubwa kumpa kashkash kidogo mdogo. Ni kawaida kwa kila aingiaye hapo lazima ajitambulishe kwa askari maalumu wa hapo mapokezi ambapo kuna wataalamu wa kada za ulizi jeshi.
Getini hapo baadhi ya watu ambao hawavai mavazi yao vizuri huzuiliwa kuingia na kuambiwa wakavae vizuri. Angalau usivae suruali ya kubana, ama mlegezo, ama jeans zilizo na viraka vya urembo na mfano wake, ama gauni fupi, au sketi fupi, ama za kuangaza ama nguo za kushikwa mwili na mfanowe…
Wengi wakijua siku hiyo anaenda makao, basi hujitahidi kuvalia ipasavyo, ila wale wa mara ya kwanza halafu hawajui dress code, hupata tabu sana! Na hivi ndivyo watu ama jamii inatakiwa iwe, uvae nguo sahihi sehemu sahihi, siyo unavaa shaghala baghala ama ‘shabby’ halafu unaenda sehemu zenye kutunza nidhamu, utajuwa hujui.
Mapokezi hapo aliandikisha kama kawaida na kupewa kadi maalumu ya wageni ambayo alitakiwa aivae muda wote akiwa ndani ya wigo.
“Eee kumbe umekuja kwenye paredi ya leo, basi nenda jengo lile ukasubiri, utakuwa wengine wapo humo…”
Afande mmoja wa pale mapokezi ambaye alikuwa amevaa kiraia alimuelekeza sehemu ya kusubiria baada ya kumsikiliza shida aliyoijia.
“Jambo afande!” Alisalimia alivyoingia jengo lile na kukuta askari wenzake wenye vyeo vikubwa zaidi yake. Aliitikia mmoja tu wengine wakiwa wamenyamaza kimya, siyo kwa dharau, bali ndio utaratibu wao wavaa mabakamabaka.
Alikuta kuna makundi mawili, moja la wenye nyota nyota mabegani na lingine wenye mbavu mbavu na wasio na mbavu na wenye kolokolo mikononi (likitu kama saa hivi)
Ni kwamba siku hiyo hapo makao, kulikuwa na paredi fupi ya kuwatunuku vyeo na nishani mbalimbali kwa baadhi ya askari. Afande Juma naye akawa mmoja wao.
---
Flash Back
Kulikuwa kunahitajika askari kadhaa kwenda Yugoslavia kusomea masomo ya kati ya milipuko na masomo ya juu ya milipuko.
Jenerali wa nyota moja, afande Gema, aliitisha mafaili ya askari wote aliokuwa nao kwenye mafunzo ya kati ya milipuko miaka kadhaa iliyopita huko Jamhuri ya Czech. Baadhi walikuwa wamekufa na wachache wamestaafu. Katika majina hayo afande Juma naye alikuwemo.
Brigedia Gema alikuwa mkufunzi wa kitengo cha mafuzo ya nje ya nchi. Akiwa anapata mafunzo yake ya juu huko Czechoslovakia, afande Juma naye alikuwa anapata mafunzo ya kati huko huko lakini kambi tofauti. Hivyo walikuwa wanafahamiana.
Afande Juma alikuwa mtaalam aliyefuzu vizuri, lakini faili lake lilichafuka kwa utovu wa nidhamu kwenye kikosi chake hususani tangia alivyotoka Dafur.
Flash Forward
Ile sherehe fupi ilifanyika, na katika paredi ile, afande Juma akarejeshewa mbavu zake mbili na ua, hivyo sasa akawa na mbavu tatu na ua moja na kufanya awe sajini mtumishi (staff sergeant). Ilikuwa siku ya furaha sana kwa stafu sajent Juma ambapo alikabidhiwa na fimbo yake rasmi ya kutembelea.
Flash Back Again
Baada ya Brigedia Gema kupitia faili la lenzkoplo Juma, ndipo akakutana na maelezo ya kiongozi wake kwenye kombania (oosii), na mtunza nidhami wa kambi ‘rejimento sajenti meja’ yote yakimuelezea tabia zake za ulevi na kwamba wanasubiri afikishe miaka 45 tu ambapo ilikuwa ni miezi michache baadaye astaafu wa achane naye.
Akaitisha faili la afande Juma kutoka kitengo maalumu ya mienendo ya wanajeshi, ndipo akakuta mapendekezo yaliyofanya afande Juma aitwe kwenye kurudishiwa mbavu zake. Ni kwamba kwa miezi miezi minne mfululizo afande Juma ameonesha nidhamu ya hali ya juu, kwamba ameacha kulewa na ana ushirikiano kazini na wenzake na mwenendo wake kwa ujumla umerudi kama zamani na hata afya yake imeimarika kuliko ilivyokuwa miezi sita nyuma.
Flash Foward
Baada ya sherehe ile, stafu sajenti Juma alitakiwa aripoti ofisi ya Mkuu wa mafunzo (CI-OT) kitengo cha mafunzo ya nje ya nchi.
“Jambo sir!” Ssgt Juma alihoti na kupiga salute kali akimsalimia Brigedia Jenerali Gema ambapo jenerali huyo wa nyota moja aliitikia kwa kukakamaa na kubana mikono kwakuwa kofia yake ilikuwa mezani, kisha akasimama akampatia mkono afande Juma kwa ishara ya kusalimiana.
Waliongea mengi, nasaha nyingi, kukumbushiana drill za nchini Czech kwingi na hatimaye afande Gema akasema...
“Nataka uende sinia kozi ya amnushen, wewe pamoja na wenzako kadhaa, na ukitoka huko itabidi uende semina fupi kwenye chuo chetu cha uongozi (endisii) ili nikupendekeze upatiwe kolokolo…”
“Mwezi mmoja baada ya leo utapata maelekezo kikosini kwako juu ya utaratibu mzima wa safari, roja sofa?”
“Roja ova sa!”
Baada ya maongezi mengine ya kawaida, waliagana na kuondoka.
Wakati anatoka getini pale alipo saini, safari hii sahihi yake ilianza na ‘ssgt’ badala ya ‘lc’ hadi yule askari jeshi akamtania…
“Sasa nani senior kati yangu na yako…” wote wakacheka.
Ni kwamba yule aliye mapokezi naye ni stafu sajenti, lakini kwa mujibu wa namba zao za jeshi, afande Juma ndiye alikuwa senior…
“Mimi Sinia, soma namba hiyo…” Afande Juma alijibu kisha wote wakacheka.
Alivyokuwa anatoka getini, yule askari jeshi aliyemfungulia mlango safari hii alikuwa amesimama kando na geti likihudumiwa na askari mwingine ambaye pia ni MP, ilibidi akauke kumsalimia…
“Jambo afande!” alisalimia yule MP wa kwanza huku yule mwenye kushughulika na geti akimfungulia geti dogo apite.
“Jambo, endelea!” alijibu salamu huku akiitoa fimbo yake kwapani na kuanza kutembea nayo kwa mikogo!
“Hapa kwanza nielekee maeneo ya Diamond Jubilee nikapate chakula…” alijisemea huku akitembea kuelekea upande huo wa diamond jubilee.
Inaendelea…