Tupio la XXII - Ommy awasiliana na Nasreen
Ilipoishia…
Kiingereza 150,000 kwa mwezi
Hakutaka hata kusoma kwingine, akauliza
“Hii ya kusoma mwezi mmoja naweza kuanza lini!?” aliuliza na kuonesha pale aliposoma
“Ni wewe tu, hata kesho njoo uanze…” alijibiwa Omari kisha akaondoka.
“Da! Laki moja na nusu hata mjeda akizingua nitajilipia, ngoja kesho nije nianze…” Omari alijisemea.
Sasa endelea…
Omari alirudi nyumbani na jioni wakati wa chakula aliwashirikisha wazazi wake juu ya maamuzi yake ya kusoma kule ‘mjini posta’ badala ya Mwenge.
Mama yake hakuwa na kipingamizi na baba yake alisema…
“Kama nilivyokuahidi mwanangu, nitakulipia ada na nauli za kuendea huko masomoni kwako, najuwa huwezi kupata muda wa kufanya shughuli za pwani hivyo hutokuwa na hela.”
“Asante sana baba, tayari nimejiandikisha kuanza kesho…” Omari alihitimisha, kisha mazungumzo mengine ya kifamilia yaliendelea ingawaje si mama Omari wala Omari mwenyewe aliyemwambia afande habari za chupa na mambo yake.
---
Mwezi ulikatika na Omari akawa anaongea ‘kingreza’ ingawaje hakikunyooka, walimuambia ili awe mahiri zaidi inabidi ajiunge na awamu ya pili ambapo angesoma tena mwezi mmoja, lakini Omari alisema…
“As for now is enough…” walimu wake walifurahi pale na wote wakacheka kwa pamoja.
“Another time when get money will come” Alisisitiza kisha akaaga na kuondoka.
Lakini kumbe Omari aliwaza juu zaidi, hivyo akaondoka hadi Mwenge na kujisajili pale kwa Ras Simba, na aliporudi nyumbani aliwaeleza wazazi wake kuwa kesho ataendelea na masomo kwenye kituo cha Mwenge.
Hapo Mwenge alijifunza zaidi ya kuongea, maana alijifunza pia muundo wa lugha yenyewe kwa ujumla na baada ya miezi mitatu tayari Omari alikuwa na misamiati mingi kichwani na aliweza kuitumia ipasavyo ingawaje kwenye uharaka wa kuongea hakuwa spidi kubwa.
Baada ya miezi minne tangia aanze masomo, sasa aliweza kuitafsiri vizuri mwenyewe ile karatasi aliyoikokota kwenye chupa kule baharini.
Wakati yupo hapo Mwenge kujifunza lugha ya Kiigereza, alikutana na watu wengine ambao nao walikuwa wanajifunza, wengine walikuwa waliomaliza kidato cha nne, wengine wa kidato cha sita, wengine wa las saba kama yeye, wengine wasanii wa bongo flavor na maigizo ili mradi kulikuwa na watu wa namna tofauti tofauti.
Kwa kutumia uzoefu wa wenzake hapo kwa Ras Simba aliweza kupata kudodosa juu ya namna ya kwenda Dubai, China na baadaye sana ndio akachomekea Bahrain.
“Da, mwanangu kuingia Bahrain inabidi uwe na visaaaa…” Jamaa mmoja aliyekuwa anasoma naye ambaye alionekana kuwa ni mraibu wa dawa za kulevya kiasi alimuambia…
“Yani kutoka nje ya nchi hii inabidi upate kitabu babuuu…” aliendelea…
“Yani paspotibuku…”
“Kama haitoshi, inabidi uwe na yelokadi…”
“Yelokadi ni kakitabu fulani hivi ka njano ila nini mwana, inabidi wakudunge sindano mabegani…”
“Wenyewe wanaita yelofiva na zingine nini sijui nimesahauu…”
“Ila sikia mwana, zipo yelokadi za mchongo, hizo huchomi wala nini, ukienda pale mnazi mmoja nini, utawakuta wana watakudaka tu kuuliza kama, kama unataka yelokadi, basi unawagea ganji kidogo nusu saa nyingi wanakuletea kadi mpyaaaa, watachukua tu majina yako na nakala za pasbuku yako kwa ajili ya kujaza kadi yako…”
“Lakini mwana, ukirudi kuja kuriniu wenyewe wanavishtukia…, kama vipi we nenda tu kachome upate kadi yako mukide!
Nusu teja huyo alimueleza Omari mambo yote muhimu, inaonekana yeye ni mzoefu wa safari, sijui alikuwa punda!?
---
“Sina passport, sina yellow card, sina visa, mmmh, safari bado ngumu…” Omari aliwaza siku hiyo alipokuwa anarudi nyumbani.
Yule nusu teja pia alimuambia kuwa ili alingie Manama lazima apitie Sudani au Saudi Arabia…
“Bongo hatuna ubalozi na Bahrain mwana, inabidi uende hadi Khatourm au Jeda kukata visa ndio uchukue pipa uingie mjini Manamaaa!, vinginevyo, utarudia eapoti mwana” alikumbuka pia maeno hayo.
Omari katika dodosa dodosa yake pia aliambiwa visa rahisi kwa yeye ni ile ya utalii kwa muda mfupi na ambayo pia atatakiwa aoneshe uwezo wa kujihudumia akiwa huko na ushahidi wa tiketi ama hela ya tiketi ya kurudi alipotoka.
“Da kumbe wenzetu wanabana sana, sijui na sisi wageni wanaokuja kwetu huwa wanafanyiwa hivyo!?...” Omari alikuwa anajiuliza.
Kiufupi Omari alidhamiria kwenda Bahrain kukutana na mwenye barua, lakini ndio akawa anakutana na changmoto kama hizo ambazo baadhi amezivalia njuga ikiwemo suala la lugha ya kiingereza. Suala la safari bado alikuwa hajamshirikisha mama yake wala baba yake na wazazi wake hao walidhani mtoto wao kweli anantaka kuwa beach boy wa kutembeza watalii.
Usiku ule Omari hakupata usingizi wenye utulivu hasa akikumbuka yule nusu teja alivyo mwambia kuwa bila dola elfu moja safari haitokamilika…
“Tiketi ya kwenda na kurudi muda mwingine unaweza kupata kwa dola mia sita, lakini nakwambia bora uwe na dola elfu moja ndio utakuwa na ahueni, bila dola alfu hotoboiii…” sauti ya nusu teja ilimjia tena kichwani.
“Hadi sasa ni milioni moja tu…” Omari aliwaza
“Sasa hii si dola mia nne, bado dola mia sita hapa, du” Alijisemea.
Zile hela zilizozidi kwenye milioni moja alizitumia nyingine kununulia simu na nyingine alimpatia mama yake na kiasi alitumia kwenye matumizi yake ya kawaida na kwakuwa alikuwa haendi pwani tena kujishughulisha alikuwa hana kipato, bahati nzuri baba yake alimlipia ada zote na nauli kama alivyo ahidi.
Wiki moja baada ya kumaliza miezi mitatu kwa Ras Simba Omari akaanza kurudi tena kule pwani kwa ajili ya shughuli zake, akakuta kuna vijana wengine wemechukua nafasi yake, hivyo mgao ulikuwa mdogo akaacha ile kazi na kuamua kushida maeneo ya ‘kokobichi’ mida ya jioni kila siku ili ajifunze kuongeza na wazungu lakini pia kujifunza kazi yenyewe ya ‘ubichiboi’.
Juhudi zake za kukaa coco beach hazikuzaa matunda, ingawaje alifanikiwa kukutana na wazungu lakini wote walikuwa tayari na waongozaji wao…
“Oyaa, watasha wengi wapo Zenji, timba Zenji, wakishuka tu eapoti unaanza kubonga nao, au utaenda bichi wanakozagaa sana kisha unaongea nao, wakikuelewa mbona unatoka!...”
Beach boy mmoja alimueleza Omari mbinu kama aliyotumia yeye kuingia kwenye fani …
“Kama una makaratasi unaweza kwenda kuomba kazi kwenye kampuni tuaz ili uanzie humo upate uzoefu…” Huu ulikuwa ushauri wa jamaa mwingine mwongoza watalii pia.
“Kama uko mambo safi nini, jichanganye kwenye mahoteli makubwa wanakofikiaga, kwenye maswiminpuul nini mtakutana unaweza kuongea nao kirahisi mbona!...” Beach boy mwingine alimpa mbinu ‘ghali’.
Omari akawa anaanza kukata tamaa jinsi ya kuichanga hiyo dola mia sita aongezee kwenye nauli kwa kufanya kazi ya ubichiboy.
Hata hivyo aliwaridhisha wazazi wake kwa picha kadhaa alizofanikiwa kupiga na watalii akiwa maeneo ya ufukweni lakini hazikuwa na matokeo kwenye fedha…
“Bado sijapata wa kumtembeza mimi kama mimi, nimeanza kuzuga tu na hawa ili nipate uzoefu…” alikuwa akiwaambia wazazi wake maendeleo ya jitihada zake.
Siku iliyofuata hakutoka ndani bali alijifungia tu akiwaza nini cha kufanya.
“We Omari, vipi leo! Unaumwa? Mbona hutoki humo ndani na joto lote hili…”
Sauti ya mama yake ilisikika.
“Leo mama sijisikii vizuri, napumzika…” Omari alijibu.
Mle chumbani aliipitia mara nyingi ile barua na kujitia moyo huenda siku moja atafanikiwa. Atafanikiwaje, hata yeye alikuwa hajui.
Jioni yake akapata wazo la kupiga simu ile namba…
“Kesho nitaenda sehemu tulivu ili nimpigie simu Nasreen...” alijisema na kujikuta anatabasamu.
Omari alivyobadili tu zile fedha jambo la kwanza alienda kununua simu za bei nafuu ‘itel’ ilikuwa ni smartphone lakini ni 'lower end' kabisa kwa bajeti aliyoipanga. Simu yake ilikuwa na uwezo wa kuwa na application za facebook na whtaspp pia.
Kesho yake Omari mida ya mchana alitoka kwenda Msasani beach club, hakuwa mgeni hapo kwani siku za weekend alikuwa akija mara kwa mara kuwaangalia Akudo Impact waliokuwa wakitumbuiza hapo, na alikuwa anaingia bure kwakuwa walinzi wa getingi walikuwa wanamfahamu kuwa ni mtoto wa Afande mwenzao.
Sasa siku hiyo alienda hapo mida ya mchana, na kuagiza kinywaji baridi, akiwa ndani ya ukumbi kwenye utulivu akaamua kupiga simu…
“Halo, assalaam alaykum…” Sauti nyororo kutoka upande wa pili ilijibu…
“Waalaikum salaam, are you Nasreen?” Omari alitema ung’eng’e…
“Wafaq aismi Nasreen, min hadhih min fadlik wamin ain hasalat ealaa raqami?”
Sauti nyororo iliongea kutoka upande wa pili na ilikuwa ya ukali kidogo ila nzito kama vile aliyekuwa anaongea alikuwa ametoka usingizini akimaanisha ‘ndiyo mimi naitwa Nasreen, je wewe ni nani na namba yangu umeipata wapi?’
Omari wala hakuelewa na akawa kama ametolewa mchezoni vile akajikuta anasema…
“Whasap, will send yu meseji wasap…”
Sauti ya Nasreen ikasikika “Ok send me a massage” na simu ikakatwa.
Omari alifurahi na kuchukia kwa wakati mmoja, hakujua hata aandike nini. Leo rasmi akaisevu ile namba kwenye simu yake.
Hakuwa mjuzi sana wa mambo ya whatsapp, lakini alijitahidi kuandika ujumbe na kuutuma…
“My name is Omari Juma. I am coming from Tanzania. I found the message you wrote in the bottle. I want to come and see you. Thank you.”
Hivyo ndiyo alivyoandika Omari akimaanisha kuwa ameiona ile karatasi kwenye chupa na anataka aende Barhain kumuona Nasreen.
Haikupita sekunde nyingi simu ya Omari ikatoa mlio wa ujumbe wa whatsapp…
Nasreen: “Wow, Its so great you found it, ‘been waiting for so long, where did you find it?, where? When are you coming to Manama?”
Omari: “My English is not good, but the problem is passport, visa and ticket”
Nasreen: “Okay, send me photo shot of the message you found”
Omari akachukuwa nakala ya ile meseji kisha akaipiga picha na kuituma.
Omari: “I sent you a photo, did you see?”
Nasreen: “Ok, I’ve just seen it, but I need to see the original, and if you don’t mind make a video call so that I make sure I’m talking to the one who real found the bottle.”
Omari: “Okay, will call you in fews minutes, I have to go back home”
Nasreen: “Ok, Omari, I’m so eager to see you and the message”
Omari akazima data kisha akatoka mle ukumbini haraka na kudandia DCM iliyomfikisha Ukwamani.
Akiwa chumbani kwake, akaitoa ile barua ‘original’ na akawasha data kwenye simu kisha akapiga video call…
Inaendelea…