Tupio la XXIX – Mauzauza
Ilipoishia
“Nimemuogesha mwenyewe, nimemkagua, hana hitilafu yoyote, lakini bado hajaongea chochote, yupo jikoni anakunywa uji.” Mama Gift alisema.
“Basi vizuri, nimetokea Polisi, wamesema kesho asubuhi tuende na mtoto ili wafanye kazi yao…”
---
Sasa endelea…
Afande: “Eee kwa kuwa mmesema hana majeraha wala madhara ya kuingiliwa kimwili na hamuhitaji kesi yoyote basi hatuna budi kulifunga jalada, hivyo nitahitaji maelezo ya maandishi kutoka kwa mama wa mtoto…”
Mama Gift: “Sawa afande”
Afande: “Mtoto mwenyewe mpandishe hapo kwenye kiti nichukuwe maelezo yake…”
Mama Gift: “Mmmh, hajaongea huyu tangia nilipompata, huenda ikawa mambo ya kienyeji haya nitayashughulikia kienyeji ataongea tu…”
“Mama Kihwele, ungeacha tu Polisi wafanye kazi yao…” Balozi alipendekeza
“Hapana Balozi, nitachelewa, huyu inabidi niwahi kwenda naye Mpwapwa, tutapata majibu yote” Alijibu mama Gift kwa kujiamini.
Taratibu za kipolisi zilikamilika kisha Balozi na mama Gift wakarudi majumbani kwao lakini bado Gift akiwa haongei chochote inagawaje alikuwa anakula vizuri na afya ya mwili ilikuwa ipo sawia.
Flash forward
Mpwapwa kwa wakubwa
“Ni sisi!..”
“Tumemlinda kiti muda wote…”
“Mnatuwahisha kutoka…!”
Ni baadhi ya maneno yaliyokuwa yanantoka mtoto Gift kinywani mwake alipokuwa akitibiwa kienyeji huko kijijini Mpwapwa.
“Tulitumwa na wakubwa wetu tumchukue aende kufanya kazi muhimu Morogoro na ameshaimaliza kwa nafasi yake…”
“…Maruhani wake walikubali baada ya ushawishi wa Ruhani mkuu wetu wa mkubwa wetu…”
Maneno ya mtoto Gift yalikuwa yanawashangaza wazazi wake ambao wote siku hiyo walikuwepo hapo kijijini mpwapwa.
Ni kwamba Gift alikuwa ametekwa kimazingara, alitekwa ili aende kufanya kazi maalumu Morogoro, kazi ya kumuokoa mtoto ambaye malaika wa bibi yake ndio walikuwa na maelekezo hayo. Mtoto Onesmo alindwe kwa namna yoyote kwakuwa ana makusudi maalumu humu duniani ambayo ni manufaa kwa binadamu.
(Kuna uhusiano kati ya malaika wa mtoto Gift na malaika wa bibi wa Onesmo ambao wako katika falme moja.)
Baada ya matibabu ya siku tatu na kwa uchache wa malezo hapo juu, mtoto Gift alianza kuongea tena kwa ufasaha kabisa…
Flash forward
Gangilonga – Iringa
Baada ya wiki moja, wazazi waliondoka Mpwapwa na kurudi Iringa.
“Hebu tuelezee jinsi ilivyokuwa tangia siku ile nikutume sokoni…” Mama Gift alimuambia mwanae ajieleze…
Hapo ilikuwa ni jioni, nyumbani kwa Kihwele ambaye ni baba yake Gift, Balozi alikuwepo, Askari mpelelezi wa jalada lile pia aliitwa kwa kuombwa kuja kusikiliza, majirani pia walikuwepo.
Gift anaelezea.
Nilivyo nunua yale mahitaji, akaja mama mmoja akaniita kwa kuning’ona…
“Zawadi, zawadi “
Nilipogeuka ndipo nikamuona, alikuwa mama wa makamo aliyeonekana kama ananijua lakini mimi simkumbuki.
Akaniambia amenitafutia kazi ya kufanya Morogoro. Na kwamba yale mahitaji atayafikisha yeye nyumbani. Tulianza kutembea kurudi nyumbani kisha nikaona kizunguzungu na sikutambua kilichoendelea tena hadi juzi kule kwa bibi Mpwapwa.
Lakini juzi kabla ya kuondoka kule Mpwapwa niliota ndoto ndefu ya ajabu ambayo naikumbuka yote.
Niliota kuwa nimetafutiwa kazi ya dada wa nyumbani, nilikuwa naishi vizuri tu maana walikuwa hawanizuii kwenda kanisani. Mshahara wangu walikuwa wananilipa vizuri tu, walikuwa wananilipa elfu thelathini kwa mwezi na kila tarehe moja walikuwa wananipatia hela yangu ingawaje nilikuwa nawaambia waniwekee.
Jumapili ya kwanza nilipoenda kanisani nilichelewa lakini nilikuta watu wanendelea na ibada lakini mbele pale madhabahuni kulikuwa na joka kubwa sana aina ya chatu ambalo lilikuwa limezunguka hela.
Sasa wakati naingia nilisikia sauti ya kilio cha mtoto mdogo ambaye nilimtambua kuwa anaitwa Onesmo na akawa ananiita dada Zawadi dada Zawadi niokoe…
Kanisani mule hakuna aliyejali sauti zile za mtoto isipokuwa mchungaji ambaye alikuwa mama mmoja hivi alikuwa anamfokea kwa kumwambia tulia, tulia, tulia…
Kumbe yule mtoto Onesmo alikuwa anaogopa yule nyoka aliyekuwa anamtisha kwa ndimi zake. Basi nikaenda kumchukuwa yule mtoto na kumkabidhi mama yake kisha nikaondoka mle kanisani.
Lakini tena nikawa rafiki wa karibu na ile familia ya yule mtoto hadi siku wale mabosi wangu walikuwa wanahamia Dodoma nami nikahamia kwa ile familia ya Onesmo. Kuna sauti ikaniambia nisiondoke na chochote kutoka Morogoro wakati narudi Iringa, hivyo niligawa vitu vyote kwa watoto kisha nikapada basi hadi Iringa stendi mpya halafu nikapanda bajaji hadi mjini na nikashuka vizuri na kuanza kurudi nyumbani lakini nilipokaribia nikapatwa na kizunguzungu tena na kupoteza ufahamu hadi nilivyozinduka kule kijijini.
Watu wote waliokuwepo pale walipigwa na butwaa kwa simulizi ile, yule askari mpelelezi alichukuwa maelezo ili akaongezee kwenye jalada ili kama kuna lolote basi wangetumia yale maelezo kufanya kazi yao, lakini kwakuwa hakukuwa na kesi maelezo yaliwekwa kama kumbukumbu.
Majirani pamoja na balozi wote walimpa pole Gift na kumuombea ulinzi kwa Mungu kwa Imani zao mbalimbali.
Mama Gifti alishukuru kwa pole zile na baada ya dakika chache watu wote walitawanyika. Baba Gift na mama Gift iliwabidi warudi tena Mpwapwa tena baada ya siku chache baada ya kupata simulizi hiyo mpya ambako huko ndiko wakapata ufafanuzi wa kina.
Kwamba mtoto Gift alitekwa na viumbe visivyoonekana kwa macho, akabadilishwa jina na kuitwa Zawadi kisha kufanyishwa kazi za kiroho hadi malengo yalipotimia. Walielezwa mengi wakaridhika sasa kuwa mtoto wao yupo salama.
Flash back
Siku moja baada ya Gift kusimuliayaliyomkuta.
Polisi waliamua kufanya kazi yao kimya kimya, walishirikiana na idara ya upelelezi Polisi Morogoro kutambua nyumba liyokuwa akiishi mama Ustadhi ambaye alitajwa katika simulizi ya Gift.
Walikuta kweli kuna hiyo familia iliyokuwa ikiishi hapo lakini wamehamia Dodoma. Polisi walijuwa kuwa baba Ustadhi alikuwa ni mtumishi ofisi ya Halmashauri ya Mji kama dereva na mkewe alikuwa Mwalimu atika moja ya shule ya mzingi mjini Morogoro.
Polisi waliazimia kupata maelezo ya familia hiyo juu ya mtoto Gift.
Flash forward
Dodoma mjini.
Polisi kutoka Iringa kwa kushirikiana na askari polisi wa Dodoma, walifanikiwa kukutana na baba na mama Ustaadhi.
Nkuhungu nyumbani kwa Baba Ustaadhi.
“Ni kweli tukiwa Morogoro tulikuwa tukiishi na binti aitwaye Zawadi. Tulimpata kupitia madalali wa mitandaoni baada ya sisi kuweka ombi letu la kupatiwa binti wa kazi ili atusaidie kulea mtoto wetu mchanga.” – Baba ustaadhi alijieleza
“Tulijaza fomu zao online (house maid aid chap), kumbukumbu zipo tuliziprinti, na baada ya siku tatu tukaambiwa tukampokee mtoto stendi ya msamvu ambapo tuliambiwa anaitwa Zawadi…”
“Alisafirishwa tu kwenye basi la Upendo lakini hakuwa na msindikizaji…”
Askari baada ya kuomba nakala ya fomu walizojaza, mama Ustaadhi aliwapatia, wakazipitia na wakapiga picha kisha wakawarudishia ile fomu. Ikaishia kuwa kama kutakuwa na lolote watarejea kwa ajili ya msaada zaidi.
Polisi kitengo cha 'saiba' kikaingia kazini, kweli wakakuta huo mtadao wa kusaidia kupatikana kwa wafanyakazi wa ndani
www.housemaidaidchap.co.tz na kweli wakakuta kuna mtiririko huo uliomhusu mtoto Gift.
Katika fomu yake ilionekana imejazwa kuwa mtoto Zawadi ana miaka 17, kabila Mhehe, lakini hana baba wala mama bali alikutwa mtaani akiwa katika mazingira magumu.
Aliyemuokota na kujaza zile nafasi alikuwa anaitwa Nghenakwe Nghaminyigwe, hapakuwa na picha yake wala namba za simu.
Polisi walipofuatilia majina yale ilibidi wafunge jalada la upelelezi huo na kuacha kama ilivyo. Ni kwamba waliaza kupata mauzauza na walipotaka kujua asili ya majina ‘Nghenakwe Nghaminyigwe’ waliambiwa kuwa ni asiyejulikana na mwenye kuona mambo yake yeye mwenyewe na asili yake ni Ukaguruni.
Itaendelea