SEHEMU YA 385
Leo muda wa kulala, Erica alienda kulala chumbani kwa dada yake kwani alimkumbuka sana ukizingatia ni kipindi kirefu alikuwa yupo shule.
“Dada jamani, nakumbuka kile kipindi ambacho wewe ulikuwa ukituambia sisi kuwa wewe ndiwe mama yetu”
“Ndio, mimi ni mama yenu maana mimi ni dada yenu wa kwanza”
“Eeeeh nipe habari za shule?”
“Kabla ya yote, nasikia siku hizi umekuwa mpishi hodari sana, nasikia unapika hadi watu wanajing’ata”
“Nani kakwambia dada?”
“Huko bibi yako anakusifia kila kukicha, kwakweli mdogo wangu umekuwa noma”
Erica alicheka na kusema,
“Jamani dada!”
“Ndio, basi kesho naomba unitengenezee keki ili niwapongeze Vaileth na Junior kwa kuoana, najua na mimi ya kwangu itakuwa nzuri balaa”
“Ya kwako na nani dada?”
“Nani mwingine zaidi ya Samir? Nampenda sana Samir naye ananipenda sana, mapenzi matamu ni kupendana. Asikudanganye mtu mdogo wangu, yani kupendana ni raha sana”
“Hongera sana dada”
“Asante na wewe ukikua utampata unayependana nae kama mimi nilivyompaya Samir”
“Mmmmh nishampata tayari”
“Niambie mdogo wangu, ni nani huyo?”
“Utamfahamu tu, jina lake linaanzia na E kama langu”
“Kheee umeanza kuchukua mtu kwa kufanana nae herufi ya jina!! Cha muhimu ni kupendana tu”
Erica alitabasamu tu na kuendelea na maongezi mengi sana na dada yake.
Kulipokucha, moja kwa moja Angel alienda kwa mama yake na kumuomba mama yake amnunulie simu,
“Ulisema nikiwa mkubwa ndio nitamiliki simu, naomba ninunulie simu mama”
“Usijali, hakuna tatizo. Simu yako ipo tu. Kwani unashida gani Angel?”
“nataka kuwasiliana na Samir”
“Tafadhari Angel usinitajie tena hilo jina hapa, nisije kufanya kitu kibaya, nakuomba sana usinitajie hilo jina”
Mama Angel alienda chumbani kwake, alijiuliza moyo wake na kuona kuwa anachotenda kumficha Angel sio kitendo sahihi ukizingatia Angel na huyo Samir wamependana, basi alijisemea,
“Nadhani ni wakati wa Angel kuutambua ukweli wa mambo kama baba yake mzazi ni Rahim, anatakiwa ajue kuwa huyo Samir ni ndugu yake maana ni mtoto wa baba mmoja. Asiniletee mambo ya mimi na Derrick bure!!”
Akawaza kwa muda kidogo ila bado hakujua ni jinsi gani aanze kumweleza mwane kuhusu ukweli halisi wa baba yake mzazi, alitambua kuwa mwanae anatakiwa kujua ukweli ila huo ukweli anausemaje? Hapo ndio palikuwa pagumu kwake, akajisemea tena,
“Inabidi nitafute wataalamu wa saikolojia ili wanishauri ni kitu gani naweza fanya ili binti yangu aufahamu ukweli kabla ya kuibua mengine”
Alifikiria sana ila aliamua tu kuendelea na mambo mengine.
Mchana wa siku hiyo, Erica alishaandaa keki aliyoambiwa na dada yake, kisha kuweka mezani halafu Angel aliwaita Vaileth na Junior, ili kwa pamoja wakate keki na kula ili kusherekea na kuwapongeza kwa ndoa yao.
Wakati wanafurahi pale, ndipo alipofika mgeni mahali hapo, mgeni huyo alikuwa ni Daima, ambapo aliuliza kwa makini,
“Kuna nini hapa?”
Alijibiwa na Erica bila ya kuficha kitu chochote kile,
“Tunampongeza Junior na Vaileth kwa hatua yao ya kufunga ndoa na kupata mtoto wao wa kwanza wa kiume”
Kwakweli Daima alihamaki kwa hasira sana,
“Kumbe ni kweli ndiomana ulikuwa hunitaki hapa wewe mtu mzima Vai”
Vaileth akajua tu pale lazima matusi yataanza kumtiririka Daima, hivyobasi aliamua tu kwenda chumbani, ikabidi Erick ndio amtoe nje Daima, ila Daima hakubisha na kutoka nae hadi nje ya geti kabisa kisha akamwambia,
“Naomba uondoke Daima”
Ila Daima alimuangalia Erick na kumwambia,
“Unajua sikuwahi kukuangalia vizuri ila leo nimekuangalia vizuri”
“Kivipi?”
“Kheee wewe kijana ni mzuri sana, yani leo ndio nimeuona uzuri wako”
“Kheee nenda zako bhana”
“Kwenda naenda ndio ila wewe ni mzuri sana, sio kama Junior, yani huyo mtu mzima atajuta tu kuolewa na Junior. Ila wewe ni mzuri sana, unafaa kuwa mume wa mtu”
Daima alitaka kumsogelea Erick ili ambusu ila muda huu, Erica alitoka ndani na kumvuta Erick kwa nyuma kisha akaingia nae ndani na kumuacha Daima akiwa mwenyewe pale nje, ambapo aliamua kuondoka tu kwa muda huo.
Erica aliingia ndani na Erick huku akimsema kwa kitendo cha kumsikiliza Daima,
“Ulikuwa ukimsikiliza wa nini yule lakini? Watu wengine sio wa kuwasikiliza kabisa, au alikuchanganya kukwambia anakupenda?”
“Hapana hajaniambia hivyo”
Mara simu ya Erick iliita kwa muda huo, akapokea ni baba yake ambaye alikuwa akipiga na alimuita mahali kuwa aende kwa muda huo. Basi alimweleza tu Erica pale kuwa anaenda kuonana na baba yao, basi Erica akamwambia,
“Naomba twende wote”
“Mmmh Erica, kaniita mimi lakini”
“Ndio kakuita wewe, najua kama leo sio siku ya kazi, kuna jambo ambalo baba kakuitia, naomba twende wote”
“Sawa hakuna tatizo”
Basi sababu walikuwa tayari, walienda tu kumuaga Angel na kuondoka zao, kwahiyo hata mama yao aliyekuwa chumbani hawakumwambia kuwa wanaenda wapi.
Moja kwa moja Erick alipofika sehemu ambayo baba yake kamuita, walienda na Erica na kumfanya baba yao ashangae kidogo,
“Kheee mmekuja wote?”
“Ndio, Erica kataka kuja pia”
“Kuna rafiki yangu alisema kuwa anahitaji kukufahamu ndiomana nimekuita hapa”
Muda kidogo yule rafiki wa baba Angel alifika, na alipoona wale watoto wapo wote alisema,
“Bila shaka hawa ndio Erick na Erica?”
“Ndio, umewaona eeeh!! Nilimwambia Erick aje mwenyewe ila na Erica akaja pia”
“Na nilijua tu kuwa lazima wangekuja wote”
Baba Angel alimuangalia rafiki yake kwa makini na kumuuliza,
“Umejuaje?”
“Aaaah hawa watoto wanapendana sana, nilijua tu kuwa lazima wangekuja wote”
Baba Angel alitabasamu kidogo na kusema,
“Ni mapacha hawa, lazima wapendane”
“Ila upendo wao ni zaidi ya unavyofikiria wewe”
Hii kauli baba Angel hakuielewa maana bado alijiuliza huyu rafiki yake kahisi nini kuwa hawa watoto watakuja wote? Kauli ya kupendana kupita na anavyofikiria yeye hakuielewa kwani kuna sehemu nyingi tu ambazo Erica na Erick hawaendi pamoja, basi aliwatambulisha pale na kuachana na ile mada asiyoielewa,
“Jamani huyu ni rafiki yangu mkubwa sana, anaitwa Mr.Noah”
Basi Erica na Erick walipena mikono na Mr.Noah na kisha kukaa pamoja ambapo waliagiza chakula na kuanza kula huku yule Mr.Noah akiwauliza Erick na Erica maswali kadhaa wakati wa kula chakula huku akionekana kuwaangalia sana watoto hawa kanakwamba kuna kitu kingine ambacho alihitaji kuongea halafu hakukiongea.
Walipomaliza, walijiandaa kwaajili ya kuondoka ambapo baba Angel alienda kupanda kwenye gari na watoto wake sababu yeye hakwenda na gari kwahiyo alichomuitia Erick kitu kingine ni kile kwenda pale na usafiri ili waweze kuondoka vizuri.
Usiku wa leo, Erica alimfata Erick chumbani kwake na kuanza kuongea nae kuhusu yule rafiki wa baba yao,
“Hivi yule rafiki wa baba umeweza kumuelewa kweli?”
“Sijamuelewa hata nimebaki kumshangaa tu”
“Anamaanisha nini kusema upendo wetu ni tofauti na baba anvyofikiria, au kaona kama tunapendana kwa namna tofauti?”
“kaonaje na yeye katufahamu leo”
“Mmmh sijui, usikute anatufahamu tangia zamani. Ila hii hali ya mimi na wewe kupendana zaidi imekuwa kubwa kwenye ukubwa wetu huu, kwahiyo yule sijamuelewa kabisa”
“Nadhani kuna kitu anajua kuhusu mimi na wewe, sijui ni kitu gani ila aaargh sijui ni kwanini jamani, mara nyingine najihisi hata kulia, kwanini nikupende hivi dada yangu? Ninakuwa na wivu na wewe, najikuta nikitamani unifanyie vitu vingi sana, najikuta nikitamani mimi niwe mpenzi wako na tuishi kama wapenzi wanavyoishi”
“Pole sana, mimi sasa ndio nimejikuta nikitamani hata Junior na Vaileth walivyoona iwe ni mimi na wewe”
“Aaaaarggh sisi ni ndugu ujue, kwanini lakini? Na kwanini wanazuia ndugu kuwa pamoja? Sitaki kukupoteza Erica na sitaki uwe na mwanaume mwingine, sijui nitafanyaje nikigundua”
Erica alihema kwa nguvu maana hakuwa na jibu kwani ni kweli hata yeye alijikuta akimpenda sana Erick kila siku inavyoenda ndivyo anavyozidi kumpenda.
Erick alimsogelea Erica na kumkumbatia, kwakwlei Erica alihisi akisisimka mwili mzima na kumtoa Erick pembeni,
“Mmmmh hapana, naogopa mimi naogopa”
Erica alitoka mule chumbani kwa Erick, basi Erick alikaa kitandani kwake na kujiinamia huku machozi yakimtoka na kujiuliza,
“Kwanini kila siku zinavyozidi kusonga mbele ndio hamu yangu ya kuwa na Erica inazidi? Kwanini Erica ni ndugu yangu? Nampenda sana, aaaarghh nadhani tutatengwa na ukoo, kwanini macho yangu yasitamani wasichana wengine yakaenda kumtamani Erica kweli!!! Aaaargggh”
Erisk alijikuta tu akitokwa na machozi, na mwisho wa siku aliamua tu kulala kwa muda huo maana hata angewaza sana bado asingepata jibu la mawazo yake.
Kulipokucha, baba Angel na mama Angel waliongea kuhusu Vaileth na Junior kuhamia kwenye hiyo nyumba ambayo Dora anataka kumzawadia Junior kama urithi wa kutoka kwa baba yake, ila mama Angel anaona kabla ya hilo watimize kwanza ahadi yao ya kufanya sherehe ndogo kijijini kwakina Vaileth ili kuwawezesha wazazi wa Vaileth nao kufurahi na binti yao,
“Ila mke wangu, sasa hivi unavyojua pesa imekuwa tatizo kidogo kwetu”
“Hakuna tatizo, yani hii namwambia Dora halafu utaona mambo yatakavyoenda, mbona ofisini kwa marehemu James wanachanga, hata wao walitaka kumfanyia sherehe kidogo Junior, basi tutawaomba tufanyie huko kijijini, halafu huko gharama haitakuwa shida, si unajua kijijini watu hata hawana makuu, raha ya sherehe wao ni wale na kunywa sio kama hapa mjini tulivyo na makuu, tunaweka hata vingine visivyokuwa na maana utakuta watu wanaviacha”
Baba Angel akacheka kidogo tu ila jukumu hilo aliona ni vyema kumuachia mke wake maana aliona akilibeba yeye basi litamshinda mara moja.
Baba Angel aliondoka zake kwenda ofisini, halafu mama Angel alimtafuta Dora na kuongea nae kuhusu hilo swala la sherehe ambapo Dora aliona hilo swala lipo sawa kabisa,
“Halafu uliongea na yule binti kitu anachoweza kufanya?”
“Ndio niliongea nae, alisema kuwa anaweza kufanya cherehani, ameomba kwenda kusomea hayo mambo ya kushona”
“Oooh hiyo haina kazi, najua utamsimamia, ili awe anashona halafu tumfungulie mahali ambapo atauza hata na vitambaa, vitenge na khanga huku akiwa fundi mwenyewe itamlipa sana hiyo”
“Kumbe Dora noma sana wewe, kuna muda unakuwa na akili timamu haswaaa”
Dora alicheka sana, na kupanga mipango mbalimbali haswaaa mipango ya kufanya sherehe nyumbani kwakina Vaileth.
Usiku wa leo, mama Angel alimueleza taarifa zote mumewe kuhusu hiyo sherehe na kila kitu alichoongea na Dora,
“Naona kaamua”
“Roho imemsuta, unajua alifanya vibaya, Junior ni mtoto halali kabisa wa James tena ni mtoto wa ndoa, sema tu mambo hapo kati yalitokea na kufanya baba na mama yake watengane, ila hilo haliwezi kukosesha Junior kupata haki zake. Ila mbaya mwingine ni yule shemeji Deo, yani ni mwanasheria ila hakutaka kujishughulisha na chochote kuhusu mali za Junior. Ila muache ataumbuka tu kwasasa, maana atashangaa kuona Junior amesharudi kwenye nyumba ya baba yake”
“Halafu hata kwenye harusi hakuja”
“Ndio hakuja, alimwambia mkewe kuwa mnajisumbua na huyo Junior, kwanza mnajipa mizigo maana mtahudumia watu watatu, Junior, mke wake na mtoto, akasema mtajuta sana. Badala mumkanye mtoto ndio mnahalalisha zinaa yake kwa kumfanyia harusi, mambo ya harusi mngemuacha agangamale nayo mwenyewe. Yani sijui kwanini Deo ana roho mbaya kiasi hiki, hampendi Junior hadi Junior mwenyewe anajua kama babake wa kambo hampendi”
“Yule nae sijui vipi, kama huyu Junior kuharibika hata na wao wamechangia kwa kiasi kikubwa sana. Mtoto hana uangalizi, kazi ya mama ni kulalamika tu na kusema mtoto amemshindwa tabia, yani Mungu amsaidie tu Junior aweze kupata akili ya maisha”
“Naamini Vaileth atamuweka sawa, kwani ni binti ambaye akili yake ipo vizuri, Vai atashughulika na Junior ndiomana nimefanya juu chini waoane tu.”
Wakajadiliana pale na kuamua tu kulala.
Siku hizi Dora na mama Angel walikuwa wakishirikiana vilivyo kuhakikisha kuwa sherehe kwenye kijiji cha wakina Vaileth inafanyika, na itakuwa nzuri tu, kwahiyo walifanikiowa kuweka kila kitu sawa na kushirikiana vyema na upande ule wa ndugu wa Vaileth katika maandalizi, kwanza na wao walifurahi sana, haswaa mama yake Vaileth ambaye a,ishajikatia tamaa ya binti yake kuolewa, kwahiyo ile ilikuwa ni furaha nyingine baada ya ile furaha ya kwanza ya mahari kupita.
Siku moja kabla ya shughuli, ilibidi mama Angel akaongee na mama mzazi wa Vaileth ili amwambie ukwlei kuhusu vaileth kuwa na mtoto maana walikuwa hawajui,
“Mama samahani, hatukuwaambia mwanzoni, ni hivi mtoto wenu Vaileth amezaa na kijana wetu”
“Oooh kumbe!! Ila kwanini hamkusema”
“Tuliogopa faini”
“Sasa faini tuwapige ya nini wakati mtoto mwenyewe alishazalia nyumbani tayari, tushindwe kumpiga faini aliyetuachia kuanzia mimba hapa kulea hadi mtoto halafu tuje kuwapiga faini nyie kweli!! Hilo ni jambo la kheri, tena tunashukuru sana mmetuambia, ni furaha sana kwetu kwani ni matunda mema”
Basi mama Angel alishukuru kwa yule mama kukubali tu bila ya tatizo lolote lile.
Siku ya sherehe, waliondoka familia nzima, mapema kabisa ili wawahi kule kijijini na pia waweze kuwahi kurudi, kwakweli ilikuwa ni furaha na shamra shamra nyingi tu.
Wakati sherehe ikiendelea, mama Angel alifatwa na mama Vaileth na kumwambia,
“Samahani mwanangu, kuna wazee pale wanahitaji maelezo pia uliyonipa mimi kuhusu Vaileth kuwa na mtoto”
Mama Angel hakuona tatizo, na moja kwa moja aliondoka na yule mama Vaileth ili kuwafuata wale wazee, ila kabla hajawafikia mama Angel alishikwa bega nyuma, alipogeuka alikutana macho kwa macho na dokta Jimmy.
Wakati sherehe ikiendelea, mama Angel alifatwa na mama Vaileth na kumwambia,
“Samahani mwanangu, kuna wazee pale wanahitaji maelezo pia uliyonipa mimi kuhusu Vaileth kuwa na mtoto”
Mama Angel hakuona tatizo, na moja kwa moja aliondoka na yule mama Vaileth ili kuwafuata wale wazee, ila kabla hajawafikia mama Angel alishikwa bega nyuma, alipogeuka alikutana macho kwa macho na dokta Jimmy.
Mama Angel alishtuka sana ila dokta Jimmy alimwambia kuwa asishtuke halafu akamuomba yule mama aliyekuwa ameongozana na mama Angel kuwa azungumze nae kidogo, yule mama hakukataa kwani yule dokta ni mtu ambaye aliheshimika sana pale kijijini.
Dokta Jimmy alisogea pembeni na mama Angel, kwakweli mama Angel alimfata tu na kujishangaa maana hakuwahi kufikiria kama siku akikutana na dokta Jimmy wazi kabisa atafanyaje nae.
Ila alivyozidi kusogea nae alimuuliza,
“Tatizo nini kwani?”
“Nisikilize Erica, kule na yule mama unaenda wapi?”
“Tatizo liko wapi? Unahisi naenda nae wapi?”
“Kijiji hiki unakifahamu vizuri Erica?”
“Hapana sikifahamu vizuri ila ninachojua ni kuwa hawa watu ni wakarimu sana”
“Mzee Mussa ndio ambaye alikuwa mshenga wenu, niliwahi kukutana nae na alinieleza kuhusu wewe, aliponiambia tu moja kwa moja nilitambua kuwa ni wewe. Swala la nyie kuja kuoa huku sio baya ila swala la nyie kuja kufanya sherehe huku ndio baya na msipokuwa makini litawagharimu sana”
“Sikuelewi”
“Kwani, muda huu yule mama kakuitia nini?”
Mama Angel aliamua tu kumwambia ukweli bila kujali kuwa huyu ni adui yao au la,
“Sasa hujawaambia kwani kuwa binti ana mtoto?”
“Nimeongea na mama yake kasema haina tatizo hilo ni swala la baraka ila sijajua kwanini leo kasema kuwa nikazungumze na wazee”
“Basi wale wazee watawaletea mlolongo usiotakiwa, na utajutia nakwambia, aiseee itawagharimu tena haswaaa, mimi nawajua wale wazee, yule mama hana tatizo ila wale wazee. Mimi ni kweli sio mtu mwema kwako, ila uliyopitia yanatosha, hakuna sababu ya kupitia mengine kwa wema wako ulioufanya kwa binti huyu. Mama wa huyu binti hana tatizo, hana tatizo kabisa, ni mtu mzuri, tatizo lipo kwa hao wazee waliokuita. Yani ukirudi nyumbani mwambie binti kuwa uliitwa na wazee, kwanza atatetemeka sana akisikia hivyo. Wale wazee wanaogopewa sana, na hivi hujaenda watafanya jambo”
“Kheee sasa nifanyeje?”
“Cha kufanya, nenda kakusanye familia yako hadi huyo binti na mtoto na mumewe, jifanye kama unaenda kuongea nae, zungukeni kwenye magari yenu muondoke hata msijisumbue kurudi wala nini kwa muda huu. Mimi nitaongea na yule mzee ambaye ni mshenga wenu ataenda kuwaombea ruhusa kuwa mmepatwa na dharula mmeondoka. Najua hata mlipokuja kutoa mahari hamkukutana na wale wazee”
“Hatukukutana nao ndio”
“Wale sio ndugu ila ni wazee wa kimila, wana mambo mabaya sana. Sio wa kuwaaga, nakuhurumia wewe na familia yako, ondoka muda huu na hivi umefanya sherehe wanajua wewe ni tajiri”
Kidogo mama Angel alishikwa na uoga, na hapo aliamua kufanya kamavile dokta Jimmy alivyomwambia, alivuta familia yake na kuondoka nayo huku akimwambia mumewe kuwa pale sio pazuri, wanatakiwa kuondoka halafu wanatakiwa wawahi ili wafike mjini mapema. Kwahiyo waliondoka bila wenyeji kujua maana hata Vaileth hakuaga, zaidi ya kuitwa kama kwa maongezi na kupandishwa kwenye gari, hapo ilikuwa ni safari tu ya kuondoka kurudi nyumbani.
Mama Angel alikuwa na mashaka sana ukizingatia alibeba familia yake yote na kwenda nayo huko, hakuelewa wala hakuwa na raha dhidi ya kile kitu kilichopo.
Walifika nyumbani wakiwa na uchovu kiasi, ila wote waliuliza ni kwanini wameondoka gafla vile ila mama Angel aliwaambia ni kwaajili waweze kuwahi, kwa upande mwingine alishukuru hawakwenda kule na wafanyakazi wa baba yake na Junior ambao walisema wataandaa tafrija fupi tu ya kumpongeza yule kijana, ila kule kijijini waliona kuwa ni mbali. Yani mama Angel hata kumuuliza Vaileth kwa siku hiyo alishindwa kabisa yani alikuwa hadi anatetemeka na kuamua tu kwenda kulala maana hata mumewe hakumwambia ukweli.
Kulipokucha, kitu cha kwanza kabisa, mama Angel alienda chumbani kwa Vaileth na kumtaka Vaileth kuongea nae,
“Samahani Vaileth, eti kwenu kuna mila gani?”
“Kivipi?”
“Mimi, niliongea na mama yako kuhusu wewe kupata mtoto, mamako hakuwa na tatizo lolote lile na alibariki tu lile swala. Ila toka tumefika jana kwenye ile sherehe nikashangaa tukiendelea na sherehe ila hakuna aliyeuliza mtoto wa Vaileth yuko wapi au mlete mtoto tumshike, hata wakati mtoto upo nae pale mbela, ila sikushangaa sana. Sema mama yako alikuja kuniita na kuniambia kuwa wazee wa kimila wanataka kuongea na mimi kuhusu swala la wewe kuwa na mtoto”
Vaileth alishtuka na kumuuliza mama Angel,
“Ulienda kuongea nao?”
“Hapana sikwenda, kuna mtu akanitonya kuwa niondoke na nisiende kuwasikiliza hao wazee wa kimila”
“Aaaarrrgh wale wazee wana mambo ya ajabu sana, sijui nani atakuwa kawaambia kuhusu shefrehe nyumbani kwetu. Ndiomana mimi wakati tumefika toka mwanzo nilimuachia mtoto akae na Erica tu hadi pale alipomleta ili anyonye, nawajua wale wazee yani lazima wamemsumbua mama ndiomana kakuita”
“Huwa wanataka nini?”
“Yani wale wazeee ungeenda kuwasikiliza, wangekutajia faini ya kulipa kwa kitendo cha mimi kuzaa kwanza kabla ya ndoa, halafu wana mtindo wa kuangalia uwezo wako kwahiyo wanakutajia faini kulingana na uwezo wako. Na hivi waliona tumeenda na magari basi hapo lazima wanajua ni matajiri kwahiyo wangetaja faini ndefu, ukikataa kulipa wanakwamisha safari yani unashangaa tu pale kijijini huwezi kuondoka, yani mnekuwepo pale na kuwaachia chochote mlichokuwa nacho, halafu wanawapa shida sana kwenye safari. Sikujua kama wale wazee wamerudi tena kijijini kwetu. Kuna kipindi waliondoka”
“Duh!! Kwahiyo ningewasikiliza ingekuwa balaa, kwahiyo wangenitajia ngapi?”
“Huwa wanataja wale, wakiona mtu ana gari wanaanza kutaja milioni ishirini”
Mama Angel alishtuka sana,
“Kheee jamani, hiyo hela ya mtaji kabisa wa biashara kubwa tu”
“Ndio hivyo, pole mama. Ashukuriwe huyo aliyekwambia mapema”
“Kwanini mama yako nae asiniambie?”
“Sijui ila najua pia hakupenda ila hakuwa na namna, ngoja nimpigie”
Muda huu Vaileth alimpigia simu mama yake na aliweka sauti kubwa na kuanza kumsalimia pale, ambapo mama yake alimuuliza,
“Mlifika salama jana?”
“Ndio mama tulifika salama, ila mama kulikuwa na tatizo gani?”
“Mmmmh si wale wazee jamani, mimi niliwaita wajomba zako na kuwaambia ukweli, sijui mjomba wako gani na kiherehere chake kaenda kuwaambia wale wazee wa mila, nikashindwa kufanya chochote kile. Nakumbuka hata mwanangu ulisema kuwa mahari tusipange kubwa ila wale wazee wa mila najua lengo lao lilikuwa ni kuwaumiza wageni wetu”
“Sasa mama, kwanini usingetutaarifu mapema”
“Jamani mwanangu, kwani siipendi familia yangu kuendelea kuishi huku!! Hii sehemu ni nzuri, ardhi inarutuba, tunakula na kuishi, nilivyoona vile niliamua kuongea na yule mshenga wao nikamueleza kuhusu wale wazee wa kimila, basi yule mshenga wao nae aliogopa jambo kulibeba yeye kama yeye, basi akasema kuna yule dokta mkubwa aliwahi kuongea nae na anaonekana kufahamiana na watu hao, akasema ataenda kumwambia, kwahiyo hata wakati naondoka na mama yako halafu dokta akamuita sikuwa na tatizo sana, ukizingatia karibia nilikuwa nafika nae kwa wazee wa kimila, kwahiyo wote waliona jinsi alivyoitwa na yule dokta. Si unajua yule dokta anavyooogopewa hapa kijijini, basi ndio ikawa rahisi, hata mlipoondoka na mshenga kuja kusema mmepata tatizo, na wenyewe walihisi mambo mbalimbali ila nani wa kumshikilia kasema? Watamshikilia yule dokta watamuweza yule? Nisamehe sana mwanangu, ila hawa wazee hata sikutaka wafike, ndiomana umeona hata sijafurahia ujio wenu, hata sijataka kumshika mjukuu wangu, yani hawa wazee hapana kwakweli. Nisamehe sana mwanangu”
Basi Vaileth alimaliza kuongea na mama yake na kukata ile simu huku akimuangalia mama Angel ambaye alipumua tu na kusema,
“Kweli duniani kuna mambo jamani, sikutegemea kama kuna sehemu kuna hayo mambo ya ajabu kama huko kijijini kwenu”
“Wenye mambo ya ajabu ni wale wazee ila wengine wapo salama tu”
“Au ndioama yule mwanaume wa mwanzo alikimbia kwa mambo kama haya?”
“Hapana, kipindi kile wale wazee wa kimila walikuwa vijiji vingine, wanazunguka wale sio kwamba wapo kijiji kimoja, wale ni watu wa kuzunguka. Sio watru wazuri”
“Duh!! Nimefahamu vitu vingi, mmmh sikutegemea kwakweli. Nilihisi mwili wote kusisimka”
Basi mama Angel alimaliza pale na kumuacha Vaileth huku akirudi chumbani kwake sasa ambapo mumewe alikuwepo tu amekaa kitandani huku akisoma gazeti, alianza kumwambia yale na kumfanya ashangae sana kwani ni kitu ambacho hata yeye hakukitegemea kabisa na aliona ni cha ajabu,
“Yani dokta Jimmy ambaye ndiye adui yetu namba moja halafu yeye ndio amekuwa msaada wetu!”
“Ndio hapo”
“Ila licha ya hayo, ila nahisi kuna mengi katikati hapo”
“Kama yapi mume wangu?”
“Nahisi dokta Jimmy hataki twende tena kule kijijini kumfatilia, kwahiyo ameshatutisha tayari na hatuwei kwenda tena maana tuna uoga”
“Ila mume wangu licha ya hivyo ametusaidia sana”
“Hata kama, bado sio mtu wa kumuamini dokta Jimmy, wala sio mtu wa kumshukuru kwani bado mabaya yake yanaendelea kucheza katika maisha yetu. Yeye na hao wazee wa kimila ni wako sawasawa, halafu hao wazee nadhani hawajawahi kukutana na watu wabishi, hivi nianze tu kutoa milioni ishirini mimi!! Labda sio mimi Erick”
Baba Angel alitabasamu tu, mama Angel alijua utata wa mumewe, alijua pale lazima lingezuka la kuzuka maana baba Angel asingekubali kutoa hiyo hela.