Simulizi: Nini maana ya mapenzi

Simulizi: Nini maana ya mapenzi

SEHEMU YA 41


Ilipita kama miezi miwili, Babuu alikosa mawasiliano na Erica kabisa na alipojaribu kwenda chuoni kwao hakuweza kuonana nae, ikabidi aende tena ili ajaribu kuonana hata na Yule Dora ambaye ni rafiki wa Erica. Na alikuwa akienda mara kwa mara ila mara zote hakumpata yeyote kati ya Erica wala Dora, mpaka siku hiyo ilikuwa kama bahati maana alimuona Dora na kumuita,
“Dora”
Dora aligeuka nyuma kuangalia ni nani anamuita na akamuona ni Babuu, akaitika na kusogea ili kumsikiliza kuwa ana ujumbe gani.
“Naomba kuzungumza na wewe Dora”
“Hakuna shida, twende tukakae pale kwenye kimbweta”
Basi wakaenda kukaa kisha Babuu akaanza kutoa maelezo yake.
“Nina matatizo Dora, naomba unisaidie niweze kuonana na Erica”
“Si umpigie simu”
“Mwanzoni alikuwa hapokei simu yangu ila kwasasa simpati kabisa hewani, yani huwezi amini kila siku nakuja hapa chuoni ili kuangalia kama nitamuona ila leo Mungu mkubwa nimekuona wewe. Tafadhari naomba nisaidie kuonana na Erica”
“Nikuulize swali Babuu?”
“Niulize”
“Hivi huwezi kuwa na msichana mwingine zaidi ya Erica?”
“Jamani dora! Natumai unajua kuhusu kupenda, nampenda kweli Erica ninampenda sana”
“Na kama yeye hakupendi tena je?”
“Kama yeye hanipendi tena sijui ila ninachojua nina mpenda sana”
“Hivi huwezi hata kujiongeza, mwanamke ulikuwa unampigia simu hapokei simu zako na siku hizi ukimpigia humpati hewani yani unashindwa kujiongeza tu kuwa umeachwa?”
“Jamani Dora usiniumize moyo wangu, unajua nampenda sana Erica yani nampenda sana”
Dora alimuangalia jinsi Babuu alivyokuwa akiongea kwa huruma, na mbele yake kidogo akawaona Erica pamoja na George wakiwa wameongozana huku wameshikana mikono, Dora alimuangalia Babuu na kumwambia,
“Angalia kule ujionee”
Babuu aligeuka na kuangalia, kwakweli hakuamini macho yake na kuyafikicha fikicha yani hakuamini kabisa kama Erica aliyemopenda kupita maelezo ya kawaida yupo kwa mtu mwingine,
“Hapana Dora, yani Erica kaniacha kweli?”
“Ndio umeachwa, wakati anakupigia simu wewe na hupokei ulikuwa unamaanisha nini? Kama kuwekwa rumande alikutuma wewe kwenda kuchokoza polisi?”
“Dah! Unaniumiza Dora ila nashukuru sana ingawa roho inaniuma. Mimi nilikamwatwa na polisi baada ya kutoka kuonana na Erica yani siku hiyo nilichelewa sana kurudi, ila kama Erica kaamua kunifanyia hivi sawa bhana Mungu atannilipia”
Dora alicheka sana na kumwambia,
“Akulipie kwa lipi? Usinichekeshe mie, haya ni mapenzi tu, ukitendwa sehemu moja tafuta sehemu nyingine ujiliwaze. Pole sana”
Babuu hakuweza kuendelea kukaa mahali pale na kuamua kuondoka kwani aliona akizidi kuumia tu kwahiyo hakutaka kuendelea kujiumiza moyo kwa kitu ambacho ameona kwa ushahidi kabisa kuwa Erica ameamua kuachana nae na kuwa na mwingine kabisa kabisa.

 
SEHEMU YA 42


Dora wala hakutaka kujisumbua kumwambia rafiki yake kuwa Babuu alifika akitia huruma badala yake kila alipokutana nae alimwambia kuwa George anampendeza sana, na siku zote alikuwa akimsifia George tu katika maongezi yake.
Baada ya siku nyingi kupita, Dora aliamua kumchunguza rafiki yake kuhusu George na kujua kuwa kuna mipango gani inaendelea baina ya rafiki yake nba George maana ilionyesha kuwa Erica siku hizi kuna mambo anamficha, kwahiyo aliamua kutumia mbinu ya kuongea nae kwa kumsifia George ili ajue kinachoendelea baina yao.
“Yani George anakupendeza rafiki yangu balaa”
“Mmh Dora, ya kweli hayo?”
“Ndio ni kweli kabisa, anakupendeza sana. Sipati picha siku ya harusi yenu”
“Amesema akimaliza tu chuo ataenda nyumbani kwetu kujitambulisha na atanivesha pete ya uchumba”
“Wow jamani, hongera sana rafiki yangu. Umepata bahati haswaa, kumpata mwanaume mwenye upendo kama George ni vigumu sana kwasasa, unatakiwa shoga yangu na wewe kuwa mjuzi usiwe mshamba”
“Mmh ushamba gani tena?”
“Kwani hujatembea nae tu?”
“Sijatembea nae, nimemwambia asubirie ndoa”
“Hahaha usinichekeshe ujue, hiyo ndoa ya lini? Hivi wanaume unawajua au unawasikia? Yani utaona akipendwa mwenzio halafu wewe ukiachwa yani itakuuma moyo? Hivi unajua kwanini wanaume wanaamua kuoa?”
“Kwanini?”
“Mwanaume sio kwamba anafata kupikiwa, kama kupika anajua, sio kufuliwa yani kufua anajua. Ila anataka hilo tunda la katikati, sasa wewe endelea kumbania utashangaa unakosa mwana na maji ya moto. Mpe mtoto wa watu afaidi na akupende zaidi”
“Mmmh unanishawishi”
“Sikushawishi ila nakwambia ukweli, mpe tunda mtoto wa mwenzio achanganyikiwe vizuri na hakika baada ya hapo yani atakupenda maradufu”
Maneno ya Dora yalimuingia kichwani Erica vilivyo ukizingatia ni mara nyingi tu George amemuomba kufanya nae mapenzi ila alimkatalia kwa kumwambia kuwa wasubirie ndoa ila maneno ya rafiki yake yalimfanya aseme kuwa George akimwambia tena basi amkubalie.

 
SEHEMU YA 43


Ilikuwa siku ya kuzaliwa ya George na aliamua kwenda kwenye matembezi na mpenzi wake Erica,
“Utanipa zawadi gani kwenye siku yangu hii muhimu?”
Erica alicheka tu,
“Tafadhali Erica usiishie kucheka ujue nakupenda, na ninatamani kuwa na wewe”
Erica alijikuta amemkubalia George kuwa yupo tayari kutembea naye kwa siku hiyo, kwakweli George alifurahi sana na kutafuta chumba maeneo yale haraka iwezekanavyo.
Wakiwa ndani baada ya tendo, George alionekana kuchukizwa sana kisha kuchukua nguo zake na kuvaa halafu alimuangalia kwa chuki sana Erica, mpaka Erica aliogopa na kumuuliza,
“Vipi George imekuwaje?”
“Vaa nguo twende”
“Imekuwaje tena George?”
Safari hii George aliongea kwa ukali,
“Nimesema vaa nguo twende”
Kisha George alitoka nje, ikabidi Erica nae achukue nguo zake na kuvaa upesi upesi huku akijiuliza kuwa ni kitu gani amefanya.


Kisha George alitoka nje, ikabidi Erica nae achukue nguo zake na kuvaa upesi upesi huku akijiuliza kuwa ni kitu gani amefanya.
Lakini alikosa jibu kabisa maana yeye aliona kuwa ni kawaida sasa swala la George kuchukia kiasi kile lilimshangaza sana, akatoka nje ila hakumkuta George kwa maana kwamba alishaondoka muda tu, akachukua simu na kumpigia ila George hakupokea simu ile. Akajiangalia mfukoni, hakubeba hela yoyote maana George alimfanyia safari ya kumshtukiza, akawaza sana kuwa atafanyaje. Akampigia simu rafiki yake Dora,
“Best nimekwama huku, una hela kidogo unitumie nirudi, nikifika nitakupa hela yako”
“Umekwama wapi na kipi kilichokukwamisha?”
“Nitakwambia nikifika ila kwasasa nahitaji msaada wa pesa kidogo niweze kufanya nauli”
“Sina sh kumi shoga yangu, pole weee. Mpigie George”
“Hadi nimekupigia wewe jua nimekosa msaada kote huko, naomba nisaidie rafiki yangu”
“Sina hela”
“Niazimie hata kwa mtu nikirudi nitampa”
Simu ikakatika maana salio liliisha na kumfanya Erica achanganyikiwe zaidi ukizingatia kosa alilolifanya kwa George mpaka muda huo hakulijua na pia hakujua kuwa anarudi vipi hosteli, yani hapo kichwa kilikosa uelekeo kabisa.
Alienda kukaa mahali akilia maana hakujua hata aanzie wapi na aishie wapi, kuna mmama wa makamo alimuona na kumsogelea karibu na kumuuliza,
“Mwanangu vipi una tatizo gani? Mbona umejiinamia hapo? Unajua ni usiku huu?”
Erica aliinuka na kumuangalia Yule mama kwa uchungu sana, kisha akamwambia,
“Nimeibiwa mkoba wangu ndio ulikuwa na nauli hata sijui narudi vipi nyumbani”
“Pole sana, inuka mwanangu twende nyumbani kwangu maana huku nilikuwa nafanya mazoezi tu. Twende nyumbani nikakupe nauli naamini itakusaidia na utafika kwenu”
Erica aliinuka na Yule mama kisha kuanza kuondoka nae taratibu kuelekea anapoelekea Yule mama, kumbe alikuwa haishi mbali na maeneo yale maana walifika kwenye nyumba moja na kumkaribisha Erica,
“Karibu, hapa ni nyumbani kwangu. Karibu ndani nikutolee nauli binti yangu”
“Usijali mama, nitasubiria hapa hapa”
Erica hakutaka kukaribia ndani maana mambo ya mjini hayaelewekagi, unaweza kujikuta umekaribia kumbe unaenda kuchinjwa ila Yule mama nae hakutaka kumlazimisha sana Erica, alienda ndani na kumtolea nauli.
Alirudi na noti ya elfu kumi na kumkabidhi, kisha kujitambulisha
“Naitwa Mrs.Peter unaweza tu kuniita mama. Sijui wewe binti yangu unaitwa nani?”
“naitwa Erica”
“Karibu sana nyumbani kwangu, hapa ni kwangu hata usiwe na mashaka yoyote yale yani wewe ujisikie upo nyumbani. Sinaga mtoto wa kike, nina watoto wawili tu wa kiume na wote wapo masomoni nje ya nchi, karibu sana mwanangu”
“Asante sana”
“Unaweza ukawa unakuja kunitembeleaga, na vizuri ukinipa na namba zako za simu”
Basi Erica alimpa Yule mama namba zake za simu na kumshukuru sana kwa ukarimu wake kisha akamuaga na kuondoka zake.



 
SEHEMU YA 44


Erica alifika hosteli muda ukiwa umeenda sana, hakuamua kufanya chochote zaidi ya kuoga na kwenda kulala ila alikuwa na mawazo mengi sana kwani George hakumtafuta hewani kabisa na kumfanya akose raha.
Kulipokucha alioga na kuanza tena kumtafuta George hewani ila hakupokea simu zake na kuamua kumtumia ujumbe,
“George mpenzi wangu nimekukosea nini kwani? Kwanini unanifanyia hivi jamani?”
Ila ujumbe wake haukujibiwa, alijaribu kutuma tena na tena ila hakujibiwa kabisa na kumfanya akose raha zaidi, hata chai siku hiyo hakuweza kunywa kwani alikuwa na mawazo mengi sana muda huo kiasi kwamba alitaka hata kwenda nyumbani kwao kwani anamtindo wa kwenda kila mwisho wa wiki ila alishindwa sababu ya mawazo na kutokuwa na raha.
Wakati anawaza sana chini ya mti alikuja rafiki yake Dora na kumsalimia,
“Hapana Dora wewe sio rafiki kabisa, yani wewe wa kushindwa kunisaidia mimi? Hata ulishindwa kuniombea hela kwa mtu?”
“Jamani rafiki yangu nisamehe bure, yani jana nilivurugwa usione vile. Yani kuna mwanamke kanipigia simu kuwa ana mahusiano na mpenzi wangu yani akili yangu yote ikaruka. Nisamehe rafiki yangu, na wewe yamekusibu yepi?”
Erica baada ya kuambiwa maneno hayo na rafiki yake na jinsi alivyoweza kuona kweli mapenzi yanachanganya, akamuamini na kuamua kumuelezea kilichotokea ila baada ya maelezo Dora alicheka sana na kumfanya Erica amuulize kilichomchekesha,
“Sasa unacheka nini?”
“Samahani rafiki yangu, usinifikirie vibaya kwa kucheka ila sijui kama nikifikiriacho ni cha kweli”
“Kipi hicho?”
“Hivi Erica unafikiri George miaka yote mitatu hii aliyokaa chuoni hakuona mwanamke kweli akaja kukuona wewe”
“Kwanini unasema hivyo Dora?”
“Siamini kama kweli George anakupenda maana kama angekuwa nakupenda hata kama umemfanyia kitu gani asingethubutu kuondoka na kukuacha mwenyewe”
“Ni kweli usemayo, sasa ndio kimekuchekesha hicho?”
“Hapana, ukiongea na George nitakwambia kilichonichekesha”
“Kivipi?”
“Twende nikupeleke anapokaa George uweze kuongea nae”
“Kumbe unapajua?”
“Sio kupajua anapokaa tu ila George namjua vizuri yani in and out ndiomana sikushtuka sana uliponitambulisha na ndiomana toka siku ya kwanza nilikwambia unanidanganya kusema kuwa ni kaka yako”
“Mbona unanitisha Dora, George unamjua vipi wewe?”
“Erica usijipe presha ya bure, twende anapokaa George uongee nae, swala la mimi kumjua utamuuliza mwenyewe vizuri”
Erica aliwaza sana ila alikubali kwamba Dora ampeleke akaongee na George maana aliamini ana mengi ya kuongea nae.

 
SEHEMU YA 45


Erica aliongozana na Dora hadi mahali alipoonyeshwa kuwa George anakaa hapo, basi Dora alimwambia Erica aende nae akafanya hivyo.
Alivyofika akagonga mlango, na George ndiye aliyemfungulia, Erica akashangaa nae George akashangaa,
“Nani amekuleta hapa?”
“Kumbe kweli unaishi hapa?”
“Sasa unashangaa nini? Ulijua naishi kwenye kiota cha ndege?”
“Hapana sio hivyo ila nimeshangaa sababu hujawahi kunionyesha unapoishi kumbe sio mbali na chuo”
“Sasa ulitaka nikuonyeshe ili iweje?”
“Khee yamekuwa hayo? George mbona umebadilika gafla, tatizo ni nini?”
George hakumjibu kitu na kuingia ndani, ilibidi Erica nae amfate ambapo alimkuta amekaa tu kwenye kochi kwani chumba kile kilikuwa na kochi moja na kitanda, kwahiyo Erica alisimama tu na kuendelea kumuuliza George kuwa kwanini anamfanyia vile,
“Hivi wewe si umeahidi kuwa mume wangu jamani? Sasa mbona unanifanyia hivi?”
“Usitake kunichekesha Erica, hivi una sifa za kuwa mke wewe? Mke gani anaongea na mtu huku amesimama?”
Erica akajiangalia pale aliposimama, hata hivyo hapakuwa na sehemu nyingine ya kukaa zaidi ya kitandani na chini kwahiyo ilibidi akae chini na kumuuliza tena,
“Kwahiyo hatma yangu ni nini?”
“Unadhani ukikaa chini ndio utaonekana mke mwema? Kwani kitanda hukukiona kuwa unaweza kukaa pale?”
“George jamani, si uniambie tu kuwa nimekufanyia nini kuliko kunifanyia hivi?”
“Sikia nikwambie Erica, wewe hufai kuwa mke wangu yani hufai kabisa. Nilipenda mke wangu, mimi ndiye niwe mwanaume wake wa kwanza, ila sio mwanamke ambaye ameshapitiwa na wanaume wengine. Erica nilikuuliza kuhusu mahusiano yako ya nyuma ili uniambie ukweli lakini ulisema kuwa mimi ni mwanaume wako wa kwanza, kumbe ushapitiwa. Kweli mtu ni mpaka umuone ndani ila nje haitoshi kuonyesha mtu anayefaa. Yani kwa nje unaonekana ni binti mpole, mlokole kumbe ni mchafu tu”
Erica alikaa kimya kwa muda na kumfanya George aendelee kuongea,
“Umeona unashindwa kujieleza? Ningekukuta ni msichana bikira basi hata leo ningeenda kwenu kujitambulisha ila ilimradi ushapitiwa siwezi hata kuendelea na mahusiano na wewe”
Erica aliumia sana, alijikuta akiinuka na kuondoka bila ya kuaga.
Muda huu alienda kupanda gari kwani hata hakutaka tena kuonana na mtu yeyote maeneo yale, moja kwa moja alienda ufukweni.

 
SEHEMU YA 46


Alifika ufukweni na kukaa mahali peke yake, kisha alilia sana yani alilia kama mtu aliyefiwa vile hadi macho yalimvimba, hakuwa na raha kabisa hapo ndio alipoona kuwa mapenzi yanaumiza kiasi kile maana hakufikiria kuwa mapenzi yangemuumiza kile kiasi.
Alilia sana, yani hata Dora alipompigia simu hakupokea, akakumbuka siku ya kwanza kukutana kimwili na Babuu ilionyesha Babuu kafurahi sana tofauti na alivyokutana na George,
“Ndiomana dada aliniambia nijitunze mimi, ni mjinga sana mimi sijui nilikubali vipi kutembea na Babuu na sijui nimekubali vipi kutembea na George kumbe ni mwanaume mpumbavu kabisa”
Alilia sana, kuna mtu alisogea na kumshika bega, Erica akanyanyua kichwa kumtazama alikuwa ni mkaka aliyemuuliza kwa upole,
“Vipi dada una matatizo gani?”
Erica alikaa kimya tu huku akiendelea kulia,
“Pole dada ila una tatizo gani?”
Alikuwa akilia sana na kadri huyu kaka alivyomuuliza maswali ndivyo alivyozidi kulia kwani alihisi kama yale maswali yakimuumiza kichwa zaidi.
Yule kijana hakukata tamaa kwani alikaa pale pale akisubiria Erica anyamaze kulia huku akijitahidi kumbembeleza.
Erica alisikiliza wosia wa Yule kaka na kuamua kunyamaza kwani muda nao ulikuwa umeenda sana,
“Naitwa Bahati, sijui wewe mwenzangu unaitwa nani?”
“Naitwa Erica”
“Jina zuri, je nini kimekupata Erica hadi unalia?”
“Ni historia ndefu sana”
“Huwezi kuniambia hata kwa kifupi?”
Machozi mengine yalimtoka Erica na kumfanya Bahati kumbembeleza tena huku akijaribu kumpa maneno ya kumshauri,
“Matatizo tumeumbiwa, sio siku zote mtu utaishi kwa raha tu. Kuna kipindi utajikuta ukipatwa na matatizo ila si vizuri kuyaacha matatizo yachukue nafasi katika maisha yetu. Erica pole sana ila muda umeenda na si vizuri kuendelea kukaa mahali hapa, nakuomba tuondoke”
Erica aliamua kukubali na kumwambia kuwa anahitaji kwenda nyumbani kwao, kwavile Bahati alijitolea kumsaidia alimuomba ampeleke nyumbani kwao.
“Usijali nitafika tu”
“Hapana ni usiku sana kwasasa, naomba nikupeleke. Mimi ni mtoto wa kiume tofauti na wewe mtoto wa kike”
Basi Erica akakubali kisha akaongozana na Bahati hadi nyumbani kwao kwani Erica aliamua kurudi kwao tu na sio kwenda tena hosteli.
Alivyofika tu kwao, Bahati aliamua kuaga na kumuomba namba ya simu ambapo Erica alifanya hivyo kisha akagonga mlango wao na mama yake kumfungulia.

 
SEHEMU YA 47


Alipoingia ndani, mama yake alifoka,
“Erica mwanangu mbona usiku huu? Unajua ni saa tano sasa hivi!”
“Nisamehe mama ila nilipakumbuka nyumbani halafu leo kipindi kilichelewa kuisha, na muda narudi kulikuwa na foleni sana njiani”
“Kipindi kimechelewa kuisha Jumamosi? Si unakujaga asubuhi wewe?”
“Mama leo tulikuwa na kipindi cha dharula na tulitangaziwa jana jioni halafu kikawekwa leo jioni ndiomana imekuwa hivi”
“Na hayo macho vipi mbona yamevimba?”
“Nadhani ni sababu ya kusoma sana”
“Kheee pole mwanangu, nenda kaoge ule halafu ukapumzike”
Erica alienda kuoga ila alikula kidogo sana kwani kiukweli hakuwa na raha kabisa, kisha akaenda chumbani kwake kwa lengo la kulala.
Siku hiyo hakutaka kurudi hosteli kwani hakupenda wajue kuwa alikuwa na mawazo kiasi kile, kwahiyo alipoingia chumbani kwake alikaa kitandani huku bado akiendelea na mawazo yake. Akakumbuka siku ya kwanza kuwasiliana na Babuu, akakumbuka jinsi alivyokutana na George alijikuta akijisemea,
“Hakuna mwanaume mwenye upendo duniani, Erick nilijua ananipenda ila alitaka wasichana wote shuleni. John nae alinitaka kimapenzi tu, hivi alishindwa hata kuja kunitafita kwenye shule yangu? Babuu nae niliamini ananipenda kumbe alikuja kuniharibia maisha yangu, nimeharibu usichana wangu mimi nani atanioa ikiwa hata George amenikataa?”
Machozi mfululizo yalimtoka, kidogo akapokea ujumbe kwenye simu yake,
“Mambo Erica, mimi nimefika nyumbani salama kabisa. Je unaendeleaje?”
Erica alisoma ule ujumbe na kutamani hata ungekuwa umetoka kwa George ila sio kwa mtu ambaye amekutana nae ufukweni tu, ila ujumbe mwingine ukaingia.
“Naweza kukupigia simu Erica japo tuongee kidogo tu?”
Huu ndio akaujibu,
“Hapana tutaongea kesho”
“Basi hakuna tatizo, usiku mwema Erica. Kumbuka kuwa Mungu anakupenda sana ndiomana upo hadi leo”
Kidogo hili neno la kusema Mungu anampenda sana lilimuingia kwenye moyo wake na akajihisi fiuraha kidogo kwani aliona japo kuna vitendo vingi alivyoviona kwake vya ajabu ila Mungu anampenda sana. Akaamua kulala sasa na kupumzisha mawazo yake.

 
SEHEMU YA 48


Kesho yake baada ya kutoka kanisani alifika dada yake Bite na kumkuta pale nyumbani, na baada ya kusalimiana nae tu dada yake alimuuliza,
“Hivi kwanini ulibadilisha namba Erica?”
“Nilipoteza laini dada”
“Ulipoteza laini? Ulipotezaje?”
“Kuna mtu aliomba kuweka laini yake kwenye simu yangu, basi yangu tuliitoa na kuja kuitafuta tena sikuiona”
“Sawa kwanini usiende kurenew laini ile upate mpya kama ile”
“Mmmh wazo hilo hata sikuwa nalo halafu niliona ni mbali sana ndiomana nikanunua laini mpya tu”
“Erica mdogo wangu laini niliyokupa ilikuwa na maana sana, siku zote sikupati hewani hadi leo nimeamua kuja nyumbani na nimebahatika kukukuta. Laini hiyo mpya kila nikikupigia inatumika, yani mdogo wangu umekuwa kama kibanda cha simu?”
“Nisamehe dada”
“Nataka uirudishe ile laini ya awali”
“Sawa dada nitairudisha”
Ila Bite alimuona mdogo wake kama hana furaha ila kila alipojaribu kumuuliza, Erica alikuwa anabadilisha mada ili asiendelee kuulizwa kuwa kwanini anaonekana ana mawazo sana.
“Mdogo wangu unanificha hadi mimi dada yako? Unajua mimi ndio msiri wako, unatakiwa kuniambia mimi vitu vinavyokutatiza, nakuona kabisa huna furaha lakini unanificha”
“Hapana dada sikufichi chochote”
“Nyumbani kwangu unapafahamu, ukiona mambo yanakutatiza uje nyumbani nikushauri”
“Sawa dada”
Basi dada yake akaongea ongea nae kisha akajiandaa kwaajili ya kuondoka kwahiyo ikabidi aondoke nae maana nay eye alitaka kuelekea hosteli.
 
SEHEMU YA 49


Alifika hosteli na baada ya muda kidogo tu Dora nae alifika, ikabidi atoke nae nje kuzungumza nae,
“Jamani Erica una tabia mbaya, yani jana umeondoka bila hata ya kuniaga?”
“Nilichanganyikiwa rafiki yangu”
“Ulichanganyikiwa na nini?”
“Acha tu rafiki yangu”
“Mmmh niache nini si uniambie tu ukweli kuwa George hakukukuta na bikra”
“Umejuaje?”
“Najua vizuri, George huwa anapenda mabinti bikra na ndiomana alikupenda wewe ila hivyo kakuta huna bikra hawezi kukutaka tena”
“Kumbe unajua, mbona hukuniambi?”
“Na mimi mwenyewe sikujua kama wewe ushatumika”
Kisha akaanza kucheka,
“Sasa unacheka nini?”
“Usichukie rafiki yangu, kwa muonekano wako unaonekana ni msichana aliyetulia sana. Hata mimi sikujua kama umetumika tayari, George huwa anapenda mabinti bikra ndiomana akakupenda wewe”
“Ila wewe sio rafiki mwema, hata kama hukujua chochote kuhusu mimi ulitakiwa kunitahadhalisha na sio kunishawishi ili mwenzio niumbuke ufurahi”
“Hapana sijafurahi Erica”
“Nimegundua, wewe si rafiki mwema. Kwaheri”
Erica aliinuka na kurudi ndani kwani maneno ya rafiki yake hayakumfurahisha hata kidogo imekuwa kama alimpangia mpango ili aumbuke.
Akakumbuka jinsi alivyokuwa akimshawishi kuwa alale na George na kumfanya azidi kumchukia maana alimfanyia kitu kibaya.
 
SEHEMU YA 50


Erica alitulia ila ujumbe pekee alioupata kwenye simu yake kwa siku hizo ulikuwa unatoka kwa Bahati na ilionyesha huyu mkaka amempenda pia Erica,
“Anitolee balaa na yeye hata sitaki tena mapenzi, wanaume ni waongo sana”
Ila Bahati alizidi kumtumia ujumbe mbalimbali na jumbe zingine zilikuwa za kumpa moyo na kumfanya asikate tamaa, kwa sehemu nyingine alimuona Bahati kama rafiki mwema kwani muda wote alikuwa akimtumia ujumbe wa maana tu na sio wa kumtongoza.
Erica alijikuta akimaliza mawazo yake kwa kusoma ujumbe ambao anatumiwa na Bahati, kwahiyo siku zote alijiliwaza kwa ujumbe tu aliotumiwa na Bahati na katika siku zote hizo hakuna siku ambayo alitumiwa ujumbe na George.
Ilitokea siku moja alitumiwa ujumbe na dadake Bite,
“Umefikiria nini kuhusu swala la kurudisha laini yako ya mwanzo?”
Ila kabla hajajibu ujumbe huo alishangaa kupokea ujumbe kutoka kwa George,
“Erica, njoo uchukue picha zako”
Kwahiyo alijikuta akipaniki na kujibu kwanza ujumbe huo,
“Hizo picha kaa nazo, mwanaume wa ajabu sana wewe. Ulikuwa na lengo la kutembea na mimi tu eti hunitaki tena sababu mimi sio bikra. Kama ungetaka mabikra si ungeenda kuoa kijijini kwenu. Baki nazo hizo picha sizitaki”
Akatuma, baada ya hapo akaona ujumbe umefika, alipoangalia vizuri alikuta ujumbe ule umefika kwa dada yake Bite na si kwa George kama alivyodhamilia.

 
SEHEMU YA 51



Ilitokea siku moja alitumiwa ujumbe na dadake Bite,
“Umefikiria nini kuhusu swala la kurudisha laini yako ya mwanzo?”
Ila kabla hajajibu ujumbe huo alishangaa kupokea ujumbe kutoka kwa George,
“Erica, njoo uchukue picha zako”
Kwahiyo alijikuta akipaniki na kujibu kwanza ujumbe huo,
“Hizo picha kaa nazo, mwanaume wa ajabu sana wewe. Ulikuwa na lengo la kutembea na mimi tu eti hunitaki tena sababu mimi sio bikra. Kama ungetaka mabikra si ungeenda kuoa kijijini kwenu. Baki nazo hizo picha sizitaki”
Akatuma, baada ya hapo akaona ujumbe umefika, alipoangalia vizuri alikuta ujumbe ule umefika kwa dada yake Bite na si kwa George kama alivyodhamilia.
Akatetemeka sana na kuogopa hadi akaamua kuzima simu, na kujilaza kwa uoga huku akiwaza sana kuwa dada yake atamfikiriaje.

Badae akawasha simu yake kwa uoga sana kwani alikuwa anawaza kuwa atamweleza nini dada yake, alipowasha tu alipigiwa simu na dada yake, akaipokea kwa uoga,
“Nipo hapa kwenye baa ya karibu na hosteli kwenu njoo”
Erica akainuka pale kitandani kwa uoga uoga kwani ingawa ni mchana ila alilala sababu hakudhamiria kumtumia ujumbe kama huo dada yake.
Alienda alipo dada yake na kumuangalia kwa aibu sana, kisha dada yake akamwambia twende, akainuka nae na kwenda kupanda gari la dada yake kisha safari ya kwenda kwa dada yake ikaanza.

 
SEHEMU YA 52


Walifika nyumbani kwa dada yake na kuingia ndani, Erica alikuwa amesimama kama mlingoti, dada yake akamuamuru akae,
“Hivi Erica wewe ni wa kunificha mimi? Umeanza lini mambo ya ajabu haya? Kuwa muwazi mimi ni dada yako na najua jinsi ya kukusaidia”
“Nisamehe dada”
“Kukusamehe ndio nini? Kumbuka umetoa mwili wako, nini maana ya msamaha kwenye mwili wako?”
“Sikudhamilia dada”
“Hukudhamilia? Au nikosomee tena ujumbe wako? Yani unamwambia mwanaume kama angekuwa anataka bikra angeenda kuuoa kwao, wewe ushatembea na wangapi hadi huyo kakukuta umetumika?”
“Dada itakuwa hukuielewa tu meseji yangu”
“Sikuielewa? Kwahiyo mimi nimepaniki bila kuelewa? Unajua mimi ni mtu mzima Erica, kumbuka dada zako wote tumeolewa tena kwa ndoa za heshima sasa wewe kwanini unataka kutuaibisha kiasi hiki jamani!”
“Dada umenifikiria vibaya”
“Kama nimekufikiria vibaya, niambie ni kweli wewe sio bikra?”
“Mimi bado ni bikra dada”
“Kuwa mkweli Erica”
“Ni kweli dada, mimi ni bikra.”
“Sasa ule ujumbe ulikuwa unamaanisha nini? Ngoja nikusomee tena labda huelewi ulichotuma “Hizo picha kaa nazo, mwanaume wa ajabu sana wewe. Ulikuwa na lengo la kutembea na mimi tu eti hunitaki tena sababu mimi sio bikra. Kama ungetaka mabikra si ungeenda kuoa kijijini kwenu. Baki nazo hizo picha sizitaki” Ujumbe wako huo ulikuwa unamaanisha nini?”
“Dada, huyo mkaka alikuwa ananitongoza na aliniuliza kama mimi ni bikra nikamjibu kuwa mimi si bikra ili nipime imani yake, sasa kugundua hivyo akadai hanitaki tena ndio akasema nikachukue picha zangu. Kuna picha zangu alijipendekeza kuzichukua kwa mpiga picha, ndio nikamjibu vile dada ila sina mahusiano na huyo kijana wala sijawahi kutembea na kijana yeyote”
“Erica, Erica mdogo wangu, hivi unajua kuwa uzinzi ni dhambi? Unakumbuka ulivyocheza na kufurahi kwenye harusi yangu? Je wewe hutaki tucheze na kufurahi kwenye harusi yako? Erica mdogo wangu nilikwambia jitunze, ukijitunza ndio utapata mwanaume wa maana wa kukuoa ila ukiwa unaruka ruka ni ngumu kuolewa. Hakuna mwanaume anayependa msichana aliyetumika”
“Sijatumika dada”
“Sitaki kutafuta ushahidi ila sitaki aibu kwenye ukoo wetu, kuanzia sasa utaishi hapa kwangu na chuo nitakuwa nakupeleka nikiwa naenda kazini, ila kurudi utarudi mwenyewe na ufikie hapa. Hatutaki aibu Erica”
“Kwahiyo leo sirudi hosteli?”
“Leo utalala hapa, kesho utaenda chuo”
“Jamani dada, vitabu vyangu vyote vipo kule. Nitajisomea nini sasa?”
“Ulikuwa unajisomea wewe au unawasiliana na wanaume kwenye simu? Utakaa hapa kwa mwezi mmoja nichunguze tabia yako halafu ndio utarudi tena kukaa hosteli, hivyo vitabu vyako utaenda kuvichukua kesho”
Erica hakutaka kubisha sana kwani kwa upande mwingine alimuogopa sana dada yake huyu ingawa ni dada waliyefatana ila alimzidi mbali sana kimiaka na kimaisha, kwahiyo ilibidi awe mpole tu.



 
SEHEMU YA 53


Kesho yake alienda chuo kama kawaida ila kwa kipindi hiko hakutaka kuwa karibu na rafiki yeyote maana aliona wanazidi kumpoteza kimalengo, akiwaza jinsi Dora alivyomdumbukiza kwa kijana George ndio anakosa hamu ya marafiki kabisa.
Siku hii alikutana na George njiani, kwakweli hakusalimiana nae kabisa kwani alimuona kama ni mwanaume asiyefaa, aliposogea mbele kidogo akageuka nyuma kumuangalia George alikuwa akielekea wapi, akashangaa kumuona George amesimama na Dora huku wakiongea na kucheka, ilimuuma sana na kuzidi kumlaumu Dora katika maisha yake, wakati anawashangaa alitokea kijana mmoja nyuma yake na kumuuliza,
“Mbona unawashangaa hivyo wale?’
“Aaah nawashangaa tu”
“Wazoee, yani wale wana mipango ya ajabu ajabu hapa chuoni”
“Kivipi?”
“Nitafute kwa muda wako nikueleze”
Yule kijana akaondoka, Erica akaanza kumfata nyuma kwani kwa hakika alitamani kujua kuwa wana mipango ya ajabu ajabu ipi, alipomfikia alimuomba tena amueleze,
“Saivi nipo busy, kama vipi niachie namba yako nitakucheki”
Erica akampa namba na kumwambia,
“Naitwa Erica, sijui wewe unaitwa nani?”
“Naitwa Adam”
Basi Yule Adam akaondoka na kumuacha Erica akiwa na hamu ya kujua kuwa ni kitu gani kinaendelea kati ya George na Dora.
Akamaliza mambo yake yote chuoni akisubiri dadake aende kumchukua ila dada yake hakufanya hivyo, ikabidi ampigie simu kumuuliza kuwa imekuwaje,
“Wewe njoo tu mwenyewe, shemeji yako anarudi leo naenda kumpokea”
Ni muda mrefu tangu shemeji yake huyo asafiri, kwahiyo ile kama siku ya kurudi huyo shemeji yake lazima dadake aandae mazingira ya kumpokea.
Bahati alimtumia ujumbe Erica mara baada tu ya kukata simu ya dada yake akimuomba waonane, Erica akaona vyema amtajie mitaa ya kuonana karibu na kwa dadake ili iwe rahisi kwa yeye kurudi nyumbani. Alimtajia mitaa hiyo nae Bahti aliafiki.

 
SEHEMU YA 54


Erica alifika mahali alikopanga kuonana na Bahati, na kweli Bahati nae alifika mitaa ile na kukaa chini kuanza kuzungumza nae.
“Sijui Erica nimekukosea kitu gani, hujibu meseji zangu. Kiukweli unaniumiza sana”
“Pole”
“Mmmh haya asante, ila Erica mie mwenzio kama jina langu lilivyo yani najiona ni mwenye bahati sana kukutana na wewe”
“Kheee na wewe unataka kunianzia hoja za kunitongoza eeh! Mwenzio nina maumivu moyoni hata sitaki wanaume”
“Kuwa na maumivu moyoni suluhisho lake sio kutokutaka wanaume, ukumbuke kila binadamu kaumbwa na vitu vyake na tabia yake. Tunaweza kufanana sura ila tusifanane tabia, si kila mwanaume ni muongo. Tupo wengine wa kweli”
“Yani ndio ulichotaka kukutana na mimi hiko Bahati? Nilijua huwezi kuniambia ujinga maana siku zote hunitumiagi meseji za ujinga, imekuwaje leo?”
“Erica, toka ile siku ya kwanza nakuona hubanduki kwenye akili yangu, kiukweli nakupenda Erica. Unaweza kuona mimi ni mjinga ila mimi si mjinga nakupenda kweli, na leo sikuwa na lengo la kukwambia haya ila nimeshindwa kujizuia, ni kwelki nakupenda”
“Haya, ngoja nikuulize maswali nione kama una vigezo vyangu”
“Niulize tu”
“Umesoma hadi wapi?”
“Nimeishia la saba”
Erica alicheka sana yani sana na kumuuliza kwa mshangao,
“La saba!!!”
“Ndio la saba”
“Halafu bila hata aibu unakuja kunitongoza mimi mdada wa chuo?”
“Mapenzi Erica hayaangalii elimu, kabila, dini wala umri”
“Usinichekeshe mie, sina ndoto ya kuolewa na mwanaume wa la saba. Samahani Bahati, huna bahati kwangu, siwezi kukukubali”
“Jamani Erica?”
“Ndio hivyo sikutaki, kwanza dini gani wewe?”
“Mimi ni Mwislamu”
“Kheee Mwislamu kumbe!! Mimi ni Mkristo, uliona wapi Mwislamu na Mkristo wakaendana?”
“Mapenzi Erica, hayaangalii dini”
“Kwanza unafanya kazi gani?”
“Mimi ni mvuvi”
“Usinichefue, kwaheri yani bora hata ungekuwa na kazi ya maana labda ningekufikiria kidogo, yani mvuvi ndio uwe na mimi loh!”
Erica akaondoka zake na kumuacha Bahati akiwa peke yake, ila Bahati alimfatilia Erica bila ya Erica kujua, ila alimfatilia hadi kwa dada yake, alipohakikisha anaingia ndani ndipo akaondoka.

 
SEHEMU YA 55


Bite alimkaribisha mdogo wake na kumuonyesha shemeji yake tena,
“Umemuona shemeji yako, baada ya miaka mingi”
“Kheee huyu ndio Erica, amekuwa mdada siku hizi”
“Ndio yupo chuo”
“Hongera sana Erica”
Alitabasamu pale na kuongea ongea kidogo na shemeji yake. Kisha akaenda kwenye chumba chake ambacho huwa analala.
Siku hiyo alitumiwa ujumbe mwingi mwingi na Bahati ila hakujibu hata ujumbe mmoja kwani alimuona Bahati sio hadhi yake,
“Natakiwa nipate mume kama wa dada, msomi na ana hela. Sio wakina Bahati, kuniekea gundu tu. Mwanaume kaishia la saba, halafu mvuvi loh nitamtambulishaje kwa rafiki zangu? Anitolee balaa mie”
Siku iliyofuata ilikuwa ni mwisho wa wiki kwahiyo Erica hakwenda chuoni na alibaki nyumbani, muda huo shemeji yake alikuwa ametoka kwenda kutembelea ndugu, jamaa na marafiki. Erica alimuuliza dada yake,
“Dada ulimpataje shemeji?”
“Ni mwanaume niliyempata kwa bahati sana halafu ananipenda balaa maana alinikuta bikra. Unajua mwanaume akikukuta bikra anakupenda sana, yani James ananipenda mdogo wangu jamani ananipenda balaa”
“Kwahiyo hawezi kukusaliti?”
“Umefikiria nini kuuliza hivyo?”
“Nasikia asilimia kubwa ya wanaume ni wasaliti, yani wanakuwa na nyumba ndogo”
“Mambo hayo si kwa James wangu, kumbuka kuwa kanikuta bikra na nimekamilika kila idara, ataanzaje kunisaliti yani kwa mwingine anafata nini labda”
“Hongera dada”
“Sio hongera tu, na wewe ujitunze. Hakuna kitu wanaume wanapenda kama kuoa mwanamke bikra”
“Sawa dada nitajitunza”
Aliinuka Erica na kwenda chumbani, kiukweli alikuwa akiumia sana moyoni na kujiona kuwa atakosa bahati kabisa,
“Hivi kwanini kwangu imetokea hivi? Kuna atakayenioa wakati mimi sio bikra kweli? Hivi wadada wote walioolewa wameolewa wakiwa bikra mmh jamani! Sijui nifanyeje?”
Aliumia sana kwenye moyo wake, mara ukaingia ujumbe kutoka kwa Bahati,
“Erica nakupenda sana, usijali kuhusu elimu yangu, kuhusu dini yangu, kuhusu kazi yangu au kabila langu angalia upendo wa kweli. Nakupenda sana Erica, haijalishi umepita na wanaume wangapi wakakuumiza moyo ila mimi nakuahidi nitakusahaulisha yote”
Erica akamuuliza kwa ujumbe,
“Je upo tayari kuoa mwanamke asiye bikra?”
“Kwani bikra ni kitu gani katika mapenzi? Watu wanaoa wanawake walioathirika sembuse kuoa mwanamke asiye na bikra! Erica haijalishi ni wanaume wangapi wamepita kwako ila mimi najiona kama ni mwanaume wa kwanza kwako, hao makapi wote siwapi nafasi uwakumbuke”
Kidogo haya maneno yakaanza kumuingia akilini, na kutaka kumkaribisha Bahati katika moyo wake, ila akawaza hoja ya elimu na kuona kuwa atachekwa na watu, ikabidi asijibu chochote hadi atakapojihoji kwenye akili yake.

 
SEHEMU YA 56


Ilikuwa ni siku ya Jumapili, Bite alienda kanisani ila Erica hakwenda na mume wa Bite nae alidai kuwa bado anauchovu na safari kwahiyo hawezi kwenda kanisani, kwahiyo nyumbani walibaki wawili.
Erica hakwenda sababu alikuwa yupo na simu tu akipeana ujumbe na Bahati kwani kwa kiasi Fulani ulikuwa unamfariji, akiwa chumbani shemeji yake akamuita.
“Erica, toka nimerudi hatujapata muda wa kuzungumza”
Erica alitabasamu tu, na James aliendelea kuongea,
“Unatumiaga kilevi?”
“Hapana situmii kilevi”
“Aaah upo kama dada yako?”
“Siye kwetu wote hatutumii kilevi”
“Hahaha walokole eeeh! Sawa, ila siku hizi umekuwa mtamu”
“Kivipi?”
“Umekuwa umependeza yani ulikuwa mzuri wakati upo mdogo ila saivi umezidi kuwa mzuri”
“Asante shemeji”
“Mume mwenzangu ni nani?”
“Kivipi?”
“Namaanisha mpenzi wako”
“Hapana sina mpenzi”
James akainuka na kwenda chumbani, baada ya muda kidogo alimuita Erica chumbani kwao,
“Mmmh nije kufanya nini huko shemeji?”
“Kuna kitu naomba uje kunisaidia”
Erica hakuwa na wazo baya juu ya shemeji yake, akaenda na kumkuta James akiwa amejifunga taulo tu, kabla Erica hajashangaa vizuri James alikuwa tayari ameshamvuta karibu yake.

 
SEHEMU YA 57


Erica hakuwa na wazo baya juu ya shemeji yake, akaenda na kumkuta James akiwa amejifunga taulo tu, kabla Erica hajashangaa vizuri James alikuwa tayari ameshamvuta karibu yake.
James alikuwa na lengo moja tu muda huo ni kumbaka Erica maana alijua hatotoa ushirikiano kwake, na katika purukushani hadi alichana blauzi ya Erica.
Hapo Erica akajiongeza kuwa hata akifanya fujo haitamsaidia kitu sababu mtu ameshadhamilia kumbaka, kwahiyo ilibidi awe mpole na kuongea nae taratibu.
“Shemeji unajua hiki kitendo hakinogi kama ukitaka kunifanya kwa nguvu?”
“Mimi sitafanya kwa nguvu, taratibu tu”
“Sina tatizo juu ya hilo shemeji hata nashangaa umejukua jukumu la haraka sana kutaka kunibaka wakati ingewezekana ungeongea kawaida tu na mimi. Tunatakiwa wote tufurahie na kama tunataka kufurahi basi tusifanye hapa nyumbani maana hatutakuwa huru, dada atarudi muda wowote”
“Kwahiyo unataka tukafanye wapi?”
“Twende mahali shemeji hata guest, huko tutafurahi pamoja”
James akatabasamu kwani maneno ya Erica yalikuwa matamu sana kwa upande wake ukizingatia alikuwa akiongea kwa sauti ya kuvutia sana,
“Tunaweza kwenda saizi?”
“Ndio, kwanini nikatae?”
“Na dadako akirudi bila kutukuta utamwambiaje?”
“Swala la dada ni dogo sana, wewe utasema ulienda safari zako, na mimi nitasema nilienda chuo wenzangu waliniita. Mbona sio shida hiyo”
Shemeji yake alifurahi sana na kumsogelea Erica halafu akambusu, Erica akamwambia,
“Basi jiandae na mimi nikajiandae tuondoke”
“Mtoto mtamu wewe dah! Yani nitamuacha hata dada yako kwaajili yako, unaonekana unavutia sana halafu mambo unayaweza. Nakupenda Erica”
“Nakupenda pia”
Basi Erica akatoka chumbani kwa shemeji yake, alienda chumbani kwake na kuchukua blauzi, akavaa haraka haraka na kutoka kimya kimya.
 
SEHEMU YA 58



Alivyofika nje alishangaa kumuona Bahati,
“Khee wewe umefata nini hapa?”
“Nimekufata wewe Erica”
“Basi, naomba tuondoke”
Akamvuta mkono na kuondoka nae, mbele kidogo walisimamisha bodaboda na kwenda nayo stendi. Kufika stendi Erica aligundua kuwa hakutoka na pochi yake yenye hela ila aliogopa kwenda kuifata tena nyumbani,
“Bahati unajua sijatembea na pochi yenye hela!”
“Hela ya nini Erica, huyo bodaboda nitamlipa mimi”
Kisha Bahati akamlipa Yule wa bodaboda na kupanda daladala kisha kuondoka pale, ila hakujua Erica anataka kwenda wapi kwa muda huo ilibidi amuulize na Erica akamjibu kuwa anataka kwenda ufukweni, kisha wakaelekea huko.
Walifika ufukweni ila Erica alionekana kuwa na mawazo sana, ikabidi Bahati amuulize,
“Mbona una mawazo sana Erica?”
“Wewe acha tu, ngoja nikuulize. Pale nje kwetu ulikuwa unafanya nini? Na kama ulinifata mimi, ulijuaje kama naishi pale?”
“Siku ile nilikufatilia hadi unapokaa, na leo nilikuja kwa lengo moja nilihitaji kukuona. Nilijua umeenda kanisani, kwahiyo nilikuja na kukaa pale nje kwenu ili ukirudi kanisani nikuone”
“Kheee huoni kama ni tatizo, mfano dada yangu angekukuta je?”
“Ningemwambia ukweli kuwa nahitaji kukuona wewe sababu ni kweli nakupenda”
“Mmmh ila nyie wanaume ni waongo sana”
“Sio wanaume wote ni waongo, uongo ni hulka ya mtu Erica”
“Unaweza ukaoa, na mkeo akakupa kila kitu unachohitaji ila bado unatamani wanawake wa nje”
“Hiyo ni tabia ya mtu Erica”
“Mmmh na nyie waislamu kuoa wake wengi siwawezi”
“Sikia nikwambie Erica, kuna mwanaume anaweza kuoa mke mmoja, wake wawili, watatu au wanne ila akawaheshimu wote na kuwatimizia mahitaji yao yote sawa kwa sawa halafu wanajuana wote. Na kuna mwingine anakuwa na mke mmoja ila nyumba ndogo kila mahali, Kwa hapo inakuwa bora hata aliyewaoa kuliko huyu anaoewachezea wanawake wengi halafu anajifanya kaoa mmoja. Na si kila mwanaume wa Kiislamu ni lazima aoe wake wengi”
“Kwahiyo wewe utaoa wangapi?”
“Mimi nataka kuoa mke mmoja tu, ninayempenda, nitamtunza na kumuheshimu siku zote. Na si mwingine zaidi yako Erica, na sitakuwa na nyumba ndogo yoyote ile”
“Mmmh kama kweli vile”
“Ni kweli Erica, sikudanganyi wala sitanii”
Erica alimuangalia Bahati na kutabasamu tu kwani kiukweli alikuwa anaongea nae tu ila mawazo yake yalikuwa mbali sana.

 
SEHEMU YA 59


James alivyotoka chumbani alikuwa ameshavaa na kukaa sebleni akimsubiria Erica ila alishangaa kuona Erica hatoki chumbani kwake, ikabidi aende akamuangalie Erica. Alishangaa sana kutokumkuta, akajaribu kumuita ila hakumuitikia, wakati akimuita ita Erica mule chumbani kwake, mkewe nae akawa amerudi na kumshangaa James akiwa ametoka chumbani kwa Erica,
“Kheee vipi tena, ulifata nini kwa dogo huyo?”
“Nimemuita nikaona kimya, ndio nikaenda kumuangalia maana siku hizi ya dunia mengi”
“Sasa yuko wapi?”
“Sijui, hata mimi mwenyewe sielewi maana hajaniaga. Sasa nilikuwa namuita ili nimuage ndio sijamkuta”
“Na wewe ulitaka kwenda wapi”
“Si kutembea tembea jamani mke wangu”
“Ndio ulishindwa kunisubiria nikitoka kanisani twende wote, jamani James!!”
“Basi yaishe mke wangu”
Kisha Bite akaanza kuulizia vizuri kuhusu mdogo wake kaenda wapi na kwanini kaondoka bila kuaga, alipokosa jibu la maana aliamua kumpigia simu mdogo wake,
“Wewe Erica uko wapi? Na kwanini umeondoka bila ya kuniaga?”
“Nisamehe dada, ila kuna kazi ya muhimu sana niliitiwa chuo”
“Kwahiyo upo chuo kwasasa?”
“Ndio dada”
“Ukitoka urudi huku nyumbani”
Kisha Bite akakata ile simu ila Erica alikuwa anawaza sana kurudi kwa dada yake na kuwaza endapo dada yake akaondoka tena kwa bahati mbaya si shemeji yake atambaka na hawezi kumdanganya tena maana atajulikana ni muongo ukizingatia alishamdanganya, ila tatizo hakuchukua vitabu vyake kwahiyo ilibidi akubaliane na swala kwamba anatakiwa arudi kwa dada yake ila alipanga kesho yake abebe vitabu vyake na kurudi hosteli tu kwani aliona pale kwa dada yake si salama tena kwake.

 
SEHEMU YA 60


Muda ulifika alimwambia bahati kuwa anataka kurudi nyumbani, ila kwakweli Bahati hakumuelewa Erica kuwa ana tatizo gani sema sababu alitokea kumpenda hakutaka kumuuliza uliza sana kwa kuhofia kuwa atamkera, kwahiyo alivyosema anataka kurudi nyumbani aliongozana nae hadi nyumbani kwa dadake.
“Mmmh si ushanifikisha ondoka basi”
“Naondoka ila nasubiri uingie ndani”
Mara shemeji yake akatokea, kumbe alikuwa mitaa ya nje ya nyumba kwahiyo akamkuta Erica amesimama na huyo Bahati, aliwaangalia kwa ukali kama mkaka anayemlinda mdogo wake,
“Vipi wewe kijana una shida gani?”
Aliuliza kwa ukali mno, ikabidi Erica ajibu kwa niaba ya Bahati,
“Ni rafiki yangu, alinisindikiza tu”
Mara dada yake nae akatoka ndani na kuwakuta pale nje, ilibidi aulize kuwa kuna nini, James alijibu,
“Hata mimi nashangaa maana nimekuta wamesimama tu hapa nje”
“Erica mdogo wangu jamani, umeanza kuongozana na wanaume?”
Bahati akaanza kujitetea,
“Msilaumu tu mimi nilimsindikiza”
James akamuangalia kwa ukali na kumwambia,
“Kelele wewe, utamsindikiza kama nani? Ndio nyie mnaoharibu watoto wa watu, ondoka hapa upesi”
Bahati alisimama tu ikabidi Erica ampe ishara kuwa aondoke tu, kisha Bahati akaondoka na wao kuingia ndani. Bite alienda moja kwa moja na Erica chumbani kwa Erica ili kuzungumza nae, muda huo kumbe James alimfata Bahati, ndani walijua James yupo ndani nao ila alimfata Bahati.
Bite kama kawaida alianza kumsema mdogo wake,
“Erica mdogo wangu lini utajifunza wewe jamani? Yani unaanza kuongozana na wanaume jamani, mbona unataka kututia aibu?”
“Ila dada, mimi ni msichana mkubwa tayari”
“Kuwa chuo haimaanishi kuwa wewe ni msichana mkubwa Erica, angalia maisha yako ya badae. Kijana kama Yule atakupa maisha gani eeh! Jitathmini, ana hadhi ya kuwa na wewe Yule? Nimekwambia wanaume wanapenda sana wasichana bikra ila usiuze bikra yako kwa mwanaume asiyekuwa na maana, mwanaume asiyekuwa na maisha. Yule si mwanaume wa kuwa na wewe, unasoma nae?”
“Hapana”
“Amesoma hadi wapi?”
“Kaishia la saba”
“Haya sasa, mwanaume wa la saba kweli ukampe maisha yako? Kwanini kujidhalilisha kiasi hiko wakati wewe ni binti msomi jamani, angalia dada yako, nimeolewa na mwanaume mwenye maisha na ananipenda kupindukia sababu alinikuta bikra”
“Mmmh!”
“Unaguna nini sasa? Usitutie aibu, sitaki kumuona tena Yule kijana umenisikia eeh! Sitaki tena kumuona, na ukirudi nitamueleza mama hadi ule ujumbe uliotuma kwangu”
“Basi yaishe dada”
Kisha Bite akatoka na kumuacha Erica mule chumbani.

 
Back
Top Bottom