Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi : SAFARI NDEFU KUELEKEA KABURINI
Mwandishi : NYEMO CHILONGANI
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
Muda ulikuwa ukizidi kwenda mbele huku dereva wa gari ndogo aina ya Prado akiwa amesimama nje ya gari hilo huku akimsubiri msichana mrembo, Patricia Thomson aweze kutoka ndani ya nyumba yao na hivyo kuanza safari ya kuelekea shuleni alipokuwa akisoma kidato tatu, Salma Kikwete Secondary School iliyokuwa Kijitonyama. Muda ulikuwa ukizidi kwenda lakini bado Patricia alikuwa ndani akiendelea kujiremba, bado alikuwa akiendelea kujipaka mafuta ya gharama pamoja na kujipulizia manukato ya bei kubwa.
Muda mwingi dereva wa gari lile, Sam alikuwa akipiga honi kama hatua moja ya kumfanya Patricia ndani alipokuwa afanye haraka lakini hiyo wala haikuweza kusaidia. Bado Patricia alikuwa akiendelea kujiremba kana kwamba honi zile ambazo zilikuwa zikiendelea kupigwa hakuwa akizisikia masikioni mwake.
“Mbona unamchelewesha mwenzio?” Bi Beatrice alimuuliza Patricia mara alipoufungua mlango wa chumba cha binti yake.
“Nakuja mama. Kuna kitu namalizia” Patricia alimwambia mama yake huku akiendelea kujiremba.
Zilipita dakika thelathini na ndipo Patricia alipomaliza kujiremba na hivyo kutoka ndani ya chumba kile. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kumfuata mama yake sebuleni alipokuwa na kisha kumbusu na kumuaga. Bi Beatrice alibaki akimwangalia Patricia huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, uzuri wa binti yake ulionekana kumvutia hata yeye mwenyewe.
Patricia akaingia garini bila ya kumsalimia Sam ambaye alionekana kukasirika. Akajifunga mkanda na kutulia kimya mpaka pale Sam alipoingia garini na kasha kuwasha gari na kuliondoa mahali hapo. Ukimya mkubwa ulikuwa umetawala garini, Patricia hakutaka kuongea kitu chochote kile kwani aliamini kwa kile alichokuwa amekifanya cha kuchelewa kutoka ndani ya chumba chake kilikuwa kimemkasirisha Sam.
“Naomba unisamehe kaka Sam” Patricia alimwambia Sam ambaye alionekana kuwa bize na usukani.
Patricia akaonekana kuumia, ni kweli alijua kwamba alikuwa amefanya kosa na ndio maana kwa wakati huo alikuwa radhi kuomba msamaha lakini ukimya wa Sam ukaonekana kumuumiza, hakupenda kumuomba msamaha mtu halafu asijibu kitu chochote kile, alipenda kusikia Sam akiongea neno lolote