imkakati
Ujumbe wa Gideon ulimfariji Joe, hakika aliona yupo na mshirika
mwaminifu na mwanamkakati wa dhati. Ujumbe aliousoma kwa Waziri
En ndio uliomtia wazimu kidogo.
“Comrade, what is the progress? We haven’t heard from you for some
days now. Is President Costa not happy with our agreement?”
(Kamaradi, maendeleo yakoje? Hatujasikia chochote kutoka kwako kwa
siku kadhaa sasa au Rais Costa hakuaϐikiana na makubaliano yetu?”
Ujumbe wa Waziri En uliuliza.
Ujumbe ule ulimchanganya kichwa Joe kwa sababu jibu atakalolitoa
hapo litaamua swali au hatua itakayofuata kwa Korea Kaskazini.
Alijua akisema mambo yapo sawa wakati hayapo sawa ingeleta shida.
Lakini akisema hayapo sawa ingezua maswali kwa En na hakuwa tayari
kwa hilo kujulikana kwa sasa. Aliwaza sana lakini mwisho alipata cha
kueleza. Aliwaza kuwa dawa ya moto ni kuumwagia maji na sio
kuwasha moto mwingine. Aliwaza, kama Pius aliamua kuwasaliti basi
acha ammalize kabisa kabisa kwenye sura ya Korea Kaskazini.
Alijua kwa vyovyote Rais Costa angemtumia Pius kuendelea na misheni
na yeye angekuwa hana maana tena hata kama akifa, wazungu
wanasema ‘He will be of no relevance’. Alijua hakuna kitu kibaya kwenye
maisha kama kupoteza thamani ya uwepo wako mahali fulani kwa
sababu utatemwa au wazungu wanasema ‘you will be rejected’.
Alifahamu hata ndoa huvunjika baada ya mwanandoa mmoja kupoteza
thamani mbele ya mwenzake, mtu hufukuzwa kazi baada ya kupoteza
thamani yake kwenye kampuni/shirika/oϐisi hiyo n.k
Joe hakukubali thamani yake kwenye serikali ya Stanza ipotezwe
kirahisi. Alijua ku ‘deal’ na matukio ya namna hiyo.
“Comrade, things are not ϐine. Pius has informed the president that I
have a secret mission with you that’s why we have agreed the
involvement of nucler weapons in our agreements. Now I am under the
extreme hunt together with Habibu to be terminated. This is the reason
why you don’t hear from me neither from the President”
(Kamaradi, mambo hayapo sawa. Pius amemtaarifu Rais kuwa nina
mpango wa siri na ninyi na ndio maana tumekubaliana nanyi juu ya
mpango wa silaha za kinyuklia. Sasa hivi nipo kwenye msako mkali ili
niuawe mimi na Habibu. Hii ndio sababu kwanini husikii lolote kutoka
kwangu wala kwa Rais). Joe alimjibu Waziri En.
“This is ridiculous, how could the soldier of the higher rank like Pius
behave like that? So you haven’t even arrived in Stanza?” (Hili jambo
linanishangaza sana, inawezekanaje askari wa cheo cha juu kama Pius
afanye mambo kama hayo? Kwa hiyo bado hujaϐika Stanza?) Waziri En
aliuliza kwa shangao.
“He has surprised all of us. Yes, We are still in Beijing” (Ametushangaza
wote. Ndio bado tupo Beijing) Joe alijibu.
“Africa has never stop to amaze us. So where are you and how can we
help you because you remember what we discussed?” (Africa haijawahi
kuacha kutushangaza. Kwa hiyo upo wapi na tukusaidieje kwa sababu
unakumbuka lile suala tulilojadili?) Waziri En alimuliza Joe.
Joe alianza kumwandikia Waziri En yote anayoona yanafaa ili
kuhakikisha yupo salama na misheni yake inaendelea. Mambo mengi En
alipingana nayo kwani kwa hakika yalikuwa yanaingilia uhuru na
utawala wa Stanza (Sovereignity interference). Waziri En alijua kwa
kufanya yale Joe aliyokuwa anamuomba angeibua hisia kubwa kwa
mataifa ya magharibi na ungekuwa ni uchokozi wa bayana kabisa
ambao ungekosa utetezi.
Waziri En alimwambia Joe asijali, kwanza atamtaarifu Rais Kim
kilichotokea na kisha atamrudia kumweleza nini wameϐikiria wanaweza
kusaidia. Waziri En alikuwa makini sana katika kila jambo alilopewa
kulisimamia na serikali yake ya Korea Kaskazini.
*******************************
“Mh. Rais umeona watu wanavyopiga kelele huko nje baada ya lile suala
la kodi kuanza kufanyiwa kazi?”, Gideon alikuwa akiongea na Rais Costa
asubuhi oϐisini kwake ambapo Rais Costa hupenda kupitia kila nyaraka
anayoikuta mezani kwake asubuhi, huo ukiwa ni utaratibu wake.
Gideon alikuwa akimkumbusha Rais juu ya ule mpango aliowahi
kumshauri wa kuhakikisha anaweka kodi koroϐi kwa wafanyabiashara
wa Stanza kwa kisingizio cha kuongeza mapato lakini hakika zikiwa
zinawatesa wananchi na kuua mitaji yao ya biashara. Agizo hilo lilikuwa
lipo katika utekelezaji na wananchi walikuwa wakilalamika na
kunyanyaswa sana na mamlaka ya makusanyo ya taifa wakishirikiana
na askari polisi pamoja na mgambo.
“Gideon, hizi kelele zimekuwa nyingi mpaka zinaanza kunipa hofu.
Ninataka bunge lipitishe muswada wa kutaka kubadili umri wa mtu
kugombea Urais ambapo tunauongeza, muswada huu utaleta kelele
nyingi kutoka kwa wapinzani sasa nahitaji wananchi wawe na amani na
mimi ili watu wangu watakapokuwa wanautetea wananchi waunge
mkono. Sasa, hili wazo lako naona linanichonganisha na wananchi tu
bila sababu”, Rais Costa alijibu huku akimalizia kusoma moja ya barua
alizozikuta pale mezani kwake ambayo aliiona haina maana akaiweka
kando.
“Mh. Rais, yani katika jambo litakupa ‘kiki’ ni hili, utakuja kunishukuru
baadaye. Wakati muswada ukiendelea kuandaliwa na huku tukisubiri
kipindi cha bunge kuanza ndio wakati huu wananchi watasumbuliwa
sana na watu wa Mamlaka ya Mapato na Makusanyo. Nimeona kila
halmashauri ya jimbo inawatumia mgambo kufanikisha makusanyo na
mgambo hawa wananyanyasa watu sana na kuzidisha chuki na hasira
kwa serikali na kwako.
Sasa hali hii iache iendelee na ikiwezekana kwenye mawasiliano yako
na wakuu wa mamlaka na wakuu wa mikoa na wilaya wasisitize kuwa
bado hujaona wakifanya jitihada vya kutosha ili wakazidi kutesa watu.
Sasa kipindi cha bunge kikianza tu ambapo muswada wako ndio
utajadiliwa wapinzani najua wataibuka na hoja nzito sana sasa wewe
ndio unatokea pale kuwavuruga kwa kusitisha kila aina ya manyanyaso
yanayoendelea kwa wafanya biashara juu ya ukusanyaji kodi. Tena ili
kuwamaliza kabisa toa tamko la kufuta mgambo wote kwenye miji yote.
Nakuhakikishia, ukifanya hivi utabadili upepo na muswada utapita bila
hata wananchi kuelewa na utapendwa kuliko ulivyowahi kupendwa.
Yani kwa ufupi ni kuwa, wakati wapinzani wakiwa na hoja ya muswada
wa umri wa kugombea uRais wewe unaibuka na suala la kutatua kero
za wananchi. Unakuwa ‘busy’ kupambana na hili suala la kodi koroϐi na
hivyo umakini wote wa wananchi unahamia kwako kama mkombozi
wao. Wakati wanagutuka tayari muswada umeshapita, na hapo
unakuwa umeua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza umeongeza
mapenzi kwa wananchi na pili muswada wako umepita bila kelele.
Wapinzani utakuwa umewapiga kile tunaita ‘Bao la kisigino” Gideon
aliendelea ‘kumjaza upepo’ Rais Costa
“Hujawahi kuacha kunishangaza Gidi. Ha ha ha! Leo ndiyo nimekuelewa
vizuri, hasa hiyo ‘timing’ ulivyoiweka”, Rais Costa alionekana
kufurahishwa sana.
“Ndiyo kazi yangu Mh. Rais, kukushauri”. Gideon alijibu kwa nidhamu.
“Kha! Huyu kijana ameipata wapi hii ‘issue’ ya mimi kununua kisiwa cha
kitalii huko Uϐilipino?”. Rais Costa alionekana kuuliza kwa kushangaa na
hasira mara baada ya kusoma gazeti la kiingereza la STANZA TODAY
lililomnukuu Julius Kibwe akisema amepata Ushahidi kuwa Rais
Sylvester Costa anamiliki moja ya visiwa vya kitalii huko nchini
Uϐilipino.
“Kwani ni kweli mkuu habari hizi?”, Gideon alihoji.
“Hilo ni swali gani Gideon? Kuna kosa gani mimi kuwapa maendeleo
wananchi na mimi kujipa maendeleo?”, Rais Costa alijibu kiutu uzima.
Gideon aligutuka kuwa kuzidi kuuliza ni kukoroϐishana na Mh. Rais na
hilo si jambo lililompeleka oϐisini asubuhi ile.
“Mh. Rais huyu kijana yafaa adhibitiwe mapema na ninakumbuka mara
ya mwisho ulisema ungeongea na Macha na Waziri wa Polisi walifanyie
kazi, waliϐikia wapi?”, Gideon alidodosa.
“Macha ndiye aliyesema angemdhibiti sasa ndiyo huyohuyo tena
mhaini. Hauwezi kuwaaamini binadamu, hata kama ni ndugu zako wa
damu. Nadhani nitamwambia Waziri wa Polisi aendelee na mpango
wake”, Rais Costa alijibu huku akikazana kuisoma ile habari.
Kwa kawaida kila siku Rais huwa na kikao kidogo asubuhi ili kuelezwa
kwa ufupi mambo yote yanayoendelea kwenye habari na mitandaoni,
wananchi wanazungumza nini na kadhalika. Akiwa hapo oϐisini wakati
ule alikuwa akisubiriwa ili apewe taarifa kwa kina juu ya ile habari
aliyoisoma kwenye gazeti.
“Mh. Rais ulipomtaja Macha umenikumbusha jambo, mahojiano naye
yameϐikia wapi, yamevuna taarifa gani muhimu?”, Gideon aliuliza.
“Macha hataki kuongea, anadai kuwa hakukuwa na jaribio lolote la
mapinduzi. Nimemwagiza Majita amtese hadi aseme mpango wote, na
kama kufa afe tu, sitaki upumbavu. Joe nae nimeshatoa amri popote
atakapoonekana auawe. Sitaki hata kuona sura yake katika maisha
yangu”. Rais Costa alionekana kutibuliwa hasira na Gideon mara baada
ya kuulizwa habari juu ya Macha.
Gideon aliposikia Macha yupo chini ya Inspekta Majita roho ilimruka.
Anamfahamu Majita kwa uhodari wake wa kuua watu katika mateso,
hana mzaha. Suala la Rais kutoa amri ya Joe kuuawa popote
atakapopatikana lilimshtua pia. Alifahamu kuwa makachero wa Stanza
walishawahi kutumwa katika misheni mbalimbali duniani na kuua
maadui wa Rais Costa tena kwa kutumia njia ambayo haiachi alama
yoyote kuwa ni tukio la mauaji.
Gideon aliona amefanikiwa suala moja la kuhakikisha familia za Joe na
Macha hazibughudhiwi, lakini taarifa aliyoisikia kwa Mh Rais kuwa
ameagiza wauawe ilimpa mshtuko mkubwa. Alijiona kabisa ana haki ya
kuwasaidia wenzake katika misheni. Isitoshe suala la Rais Costa
kumiliki kisiwa Uϐilipino nalo lilimuacha mdomo wazi.
Alianza kuunganisha nukta kwa kujiuliza kumbe ndio maana Rais huwa
ana fedha za holela tu bila hata kujua anazipata wapi na wala
kutokuwapo kwenye utaratibu wa kawaida wa bajeti. Kwa mara ya
kwanza alijua huko anapozipata hizo za kugawa ndio huko huko
huchota za kwenda kununulia visiwa vya kitalii nchi za ughaibuni.
Kwasababu yeye huambatana na Rais Costa katika ziara zake nchini
Stanza, pia alikumbuka kuwa Rais hugawa mamilioni ya fedha kila
anapojisikia akiwa kwenye mikutano ya hadhara.
Alikumbuka pia taarifa ya Mwanamahesabu wa Serikali zilizotolewa
miaka mitatu iliyopita na kuonesha kuwa kuna fedha nyingi zilitumika
katika miradi hewa na matumizi yake hayakufuata sheria wala
utaratibu. Aliϐikiria masuala mengi, lakini pia alijifunza kuwa ukiwa
kwenye nafasi ya mamlaka ya juu unaweza kufanya jambo lolote bila
yeyote kukuuliza.
“Mh. Rais, ninaϐikiri inawezekana nikasaidia katika kupata taarifa
kutoka kwa Macha. Kama hutojali na inawezekana, ningependa
kufahamu ni wapi Macha ameshikiliwa na mkaniruhusu nizungumze
nae katika njia Raϐiki, pengine anaweza akanipa ushirikiano Zaidi ya
hapa na kunieleza kiundani zaidi”, Gideon aliomba.
“Sijui wapi wamempeleka ila Sabinasi atakuja asubuhi hii nitamwambia
akupe ‘clearance’ ya kwenda kuongea nae”. Rais Costa alijibu huku
akisimama ili watoke aelekee kwenye kikao cha kupata taarifa za
habari, wao hukiita Media Brieϔing.
Wakiwa ndio wanataka kutoka mara aliingia Sabinasi Paulo, Mkuu mpya
wa Idara ya Usalama Wa Taifa Stanza aliepewa nafasi hiyo mara tu
baada ya Stanley Macha kuwekwa chini ya Ulinzi.
“Mkuu, nimeleta ile orodha ningeomba unisaidie kuidhinisha”, Sabinasi
aliongea kwa ufupi.
Haraka Rais Costa alipokea ile karatasi na kuiweka mezani na kupitisha
macho kwa haraka. Ilikuwa na majina kama ya watu watano hivi na
chini kuna Sehemu ya Rais kuweka sahihi na yeye Sabinasi.
Gideon alikuwa amesimama kwa mbali kidogo hivyo alishindwa
kuisoma vizuri lakini alifanikiwa kusoma maneno ya juu yaliyoandikwa
‘Order to kill’ yenye maana Amri Ya Kuua. Halafu kwa sababu Rais
aliweka mkono juu ya ile karatasi hakuweza kusoma majina yote lakini
alifanikiwa kusoma jina moja la mwisho lililosomeka Sylvanus Majura.
Rais Costa alimaliza kusaini na kumpa Sabinasi na kisha kumwagiza
Sabinus ampeleke Gideon kwenye nyumba walipomuhifadhi Macha.
Baada ya Rais Costa kutoka kwanza kama utaratibu ulivyo, Gideon na
Sabinasi nao walitoka. Sabinasi alimwambia Gideon asubiri palepale
Ikulu na kuwa gari maalumu lingekuja kumchukua na kumpeleka
kuonana na Macha. Gideon aliaϐiki.
**********************************
Sara, mke wa Rais Costa alikuwa kwenye sintofahamu kubwa
alipotaariϐiwa kuwa anatakiwa kurudi Stanza haraka. Alimuuliza
msaidizi wake ambaye ni Sehemu ya Usalama wa Taifa Stanza kama
kuna lolote analolijua lakini msaidizi yule alisema kwa hakika hana
taarifa zozote.
Wakiwa Safarini kutokea Canada alijawa na mawazo mengi sana kwa
sababu hata alipoongea na mume wake Rais Costa alimwambia tu
anamtaka arudi nyumbani haraka na hakumpa sababu.
Alidhani labda mtoto wao wa pekee Brian Sylvester Costa amepata
tatizo lakini alipompigia simu Brian anayesoma nchini Denmark
alimwambia mama yake kuwa yupo salama. Sara alipata wasiwasi lakini
alishindwa kutambua tatizo ni lipi linalomfanya kutakiwa kurudi nchini
kwake haraka.
Asubuhi ile alitua uwanja wa Kimataifa wa ndege Stanza na msafara
ulimpokea kama kawaida ili kumpeleka Ikulu.
***********************************
“Tumsifu Yesu Kristu Baba Askofu”, Julius Kibwe alimsalimia
Muhashamu Baba Askofu Damian Begere alipomtembelea kwenye
makazi yake kama walivyokubaliana siku ya Jumapili.
“Milele amina Kibwe. Unaendeleaje?” Askofu Begere alimjibu Julius
huku akimshika mkono kumwelekeza mahali wanapokwenda kukaa
kwa mazungumzo kwenye bustani maridadi zilizozunguka makazi yale.
Makazi ya Askofu Begere yalivutia sana. Kulikuwa na usaϐi na utulivu wa
hali ya juu. Bustani zilishamiri maua ya kila aina na ya kuvutia. Kukiwa
kumetengenezewa njia maalumu za kutembelea ili kujivinjari kwenye
bustani zile, kulijaa ndege kama Tausi, Kanga na Kasuku
walioning’inizwa kwenye vivuli vya miti kwenye vitenga vyao.
Mathalini, katikati ya njia na kwenye bustani zile kuliwekwa sanamu
nzuri za kuvutia za watakatifu na taa nzuri zilizowaka na kuzifanya
sanamu zile zivutie sana. Tena hapakukosa kile wakatoliki wanaita
Groto, yaani Sehemu iliyotengenezwa vizuri kama pango hivi ambapo
kuna sanamu nzuri ya Bikira Maria na ambapo watu kama watano
huweza kukaa na kufanya ibada.
Upande wa kulia kuliwekwa sehemu inayorusha maji na kutiririka
kwenye njia zake maalumu zilizotengenezwa na kufanya kama vijito
hivi. Miti mingi ya vivuli na matunda ilizunguka makazi yale. Ukiϐika
kwenye makazi ya Askofu Begere basi ilikuwa ni vigumu sana
kutofautisha msimu wa kiangazi na wa mvua ama msimu wa joto na
baridi. Muda wote palijawa na unyevunyevu na kiubaridi. Ilikuwa ni
pepo iliyopo Stanza.
“Julius umeibuka na hili la Rais Costa kumiliki kisiwa cha kitalii huko
Uϐilipino. Limekaaje hili” Askofu Begere alimuuliza Julius katika hali ya
ucheshi.
Alirejea taarifa aliyoisoma na yeye kwenye gazeti la STANZA TODAY
lililomnukuu Julius akisema ana ushahidi usio na shaka wa Rais Costa
kumiliki kisiwa cha kitalii nchini Uϐilipino.
“Baba Askofu ndiyo maana Jumapili iliyopita nilishangaa mahubiri yako,
hayakuwa katika hali uliyotufundisha na ya ukweli. Labda wewe ndiyo
uanze kunieleza mimi nini kimekupata maana ulinijibu tu kuwa wakati
mwingine mtu huhitajika kubwaga manyanga chini”, Julius ni kijana
mdogo kiumri lakini mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja katika
mijadala alimuuliza Askofu Begere kwa jicho la umakini.
“Hili lako ndilo la muhimu Julius. Ha ha ha!” Askofu Begere alisisitiza
huku akicheka.
“Baba Askofu, kwa kifupi tu ni kuwa kwa sasa tangu tuanze awamu hii
ya tatu ya Rais Costa, amekuwa akichukua pesa kwenye Kibubu Cha
Taifa kinyume na utaratibu. Amekuwa akitoa ‘Presidential Order’
kuidhinisha pesa kwa kisingizio kuwa anatekeleza miradi ya maendeleo
na kuwa taratibu za bunge ni ndefu na zinazorotesha kasi ya maendeleo
anayoitaka. Bahati mbaya bunge lina wabunge wengi wa chama chake
ambao hawataki kuhoji taarifa yoyote, ama kwa kuogopa au kwa
makusudi kwakuwa tu anayetenda hayo ni Mwenyekiti wa chama cha
Ukombozi Stanza.
Pesa hizi anazochota 25% anazichukua moja kwa moja ile 75%
inayobaki anaiingiza kwenye mradi lakini hao wanaotekeleza mradi
wanamwingizia asilimia 15% tena kwenye akaunti zake zilizopo Uswizi.
Kwa hiyo kwa mradi mmoja pesa zinazotoka kwa amri yake karibu 40%
humrudia yeye mwenyewe.
Isitoshe kila kampuni kubwa hapa nchini imekadiriwa kodi ya kihalali
kabisa na baada ya kujua ni kiasi gani kwa uhalali kampuni inatakiwa
kulipa basi kwa kutumia vyombo vyake hurekodi kwenye mamlaka ya
makusanyo ya taifa 25% pungufu ya uhalisia. Hii asilimia 25
huchukuliwa na kuingizwa kwenye akaunti zake.
Kwa maneno mengine kama kodi ya kampuni husika inatakiwa ilipwe
Milioni mia moja katika mwaka wa fedha huo basi italipa Milioni 75 na
ile Milioni 25 iliyobaki itaingizwa kwenye akaunti binafsi za Rais Costa.
Najua hayo watu wengi hawafahamu, ila nimepenyezewa na watu
ninaowaamini kutoka Idara za Makusanyo ya kodi na hata wandani wa
Rais.
Lakini pia, toka tulipoingia awamu hii ya tatu ya utawala wa Rais Costa
amejikusanyia ukwasi mkubwa kuliko aliokusanya awamu zote mbili
alizokaa madarakani. Sasa basi, ninazo taarifa za visiwa alivyonunua
huko Uϐilipino na Majengo na makazi aliyonunua huko Finland. Tena
hisa zake kwenye makampuni ya hisa ya nchi za Scandinavia pia tayari
taarifa ninazo”, Julius alimalizia.
Askofu Begere alikuwa amebaki mdomo wazi asiamini anachokisikia.
“Nimeshangaa sana Julius kama haya ni kweli. Lakini sasa huogopi
kuyatamka haya? Huogopi atakudhuru?”. Askofu Begere alihoji kwa
sauti ya chini sana.
“Ataua wangapi? Mimi nimeaga kwetu kuwatumikia wana Stanza. Kama
ni kufa sote tutakufa, hata yeye. Sintokuwa binadamu wa kwanza kufa.
Hakuna haja ya kuwa na hofu”, Julius Kibwe alijibu kijasiri.
“Kwa kweli kijana wangu kama una moyo wa kijasiri namna hiyo
nakupongeza. Si wengi wameumbwa na ujasiri huo. Mpo wachache
sana. Mimi nilisikitika sana kwa kitendo alichonifanyia Costa.
Aliamua kuzuia miradi yote mikubwa ya maendeleo ninayotaka
kuifanya. Ile yote niliyoitangaza kanisani aliizuia na imebidi nikubaliane
na matakwa yake ili iendelee.” Askofu Begere alimalizia na kutulia
kimya.
“Baba Askofu kuliko kuongea vile ni bora ungekaa kimya ama
kumsukumia msaidizi wako aongee. Kauli yako ina uzito sana na sasa si
vyema kuharibu uzito ule katika siku zako hizi za mwisho za utumishi”,
Julius aliongea kwa kumshauri Askofu Begere.
“Julius, sisi Wajesuiti tuna msemo unaosema kwa kilatini ‘dum in sua
non est super’ yaani ‘hatujamalizana mpaka tumalizane’. Askofu Begere
alimwambia Julius huku akimninia chai iliyokuwa imeletwa pale
bustanini na mmoja wa masista wa makazi yale.
“Sijakuelewa baba”, Julius alitaka ufafanuzi.
“Ha ha ha ha! The ϐight for justice is not over, not just yet. My son,
resistance to tyranny is obedience to God. What is going to unfold next
is bigger than he ever expected”. (Ha ha ha ha! Mapambano kwa ajili ya
haki hayajaisha, bado. Mwanangu, kukataa udhalimu ni kumtii Mungu.
Kinachofuata ni zaidi ya alichowahi kukitarajia maishani mwake’’),
Askofu Begere alijibu tena kimafumbo.
Alimkaribisha Chai na waliendelea na habari nyingine mchanganyiko
ikiwemo Askofu Begere kumwelezea kwa kina kisa kizima cha yeye na
Rais Sylvester Costa.
*******************************
Jesuiti, kwa kimombo wakiitwa Jesuits au kwa maneno mengine Society
of Jesus ni moja ya mashirika makongwe sana ya mapadri. Shirika hili
likiwa limeanzishwa huko Ufaransa na Mtakatifu Ignatus wa Loyola ni
moja ya mashirika yanayoheshimika sana na lenye nguvu kwenye
kanisa katoliki.
Mathalani, hata Baba Mtakatifu Francis ni zao la shirika hili akiwa ndiye
Papa wa kwanza ambaye ni Jesuiti. Wenyewe hujiita Jeshi la Mungu la
Askari wa Nchi kavu na kwenye Maji au kizungu hujiita ‘God’s Marines’.
Labda hii imetokana na asili ya mwanzilishi wao kuwa na historia ya
jeshi.
Moja ya sifa yao nyingine ni usomi wa hali ya juu. Ni wasomi wa
kiwango cha juu sana na ndio maana wana shule nyingi duniani na vyuo
vikuu zaidi ya 189 tena vyenye hadhi za juu. Chuo kama Georgetown
huko Marekani (Georgetown University), Boston (Boston Collage), Loyola
(Loyola University), Fordham (Fordham University) na vingine vingi ni
vyuo vinavyomilikiwa na shirika hili.
Inaaminika kuwa shirika hili ndilo humtii Papa kuliko mapadri wowote
wale. Wao husema kuwa wapo tayari kufa kwa ajili ya Papa na kufanya
chochote atakachowaagiza. Kiapo hiki wanachokiita Kiapo cha nne
(Forth Vow) hutakikuta kwenye shirika lolote la mapadre wa kanisa
katoliki isipokuwa kwa wana Jesuiti. Wana mengi hawa. Itoshe tu
kusema Jesuiti ni zaidi ya watawa.
*************************
Mishale ya saa tano hivi Gideoni alikuja kuchukuliwa oϐisini kwake pale
Ikulu ili akakutanishwe na Stanley Macha. Alitolewa na kuingizwa
kwenye gari siti za nyuma. Alishangaa kuona kuwa hawezi kuona nje
kwa namna yoyote ile, yaani ni kama mtu aliyeingia kwenye pipa halafu
likafunikwa kwa juu.
Ndani ya gari lile siti aliyokaa kwa juu kulining’inia kipaza sauti
ambacho aliweza kuongea na kujibiwa na waliokaa mbele. Aliuliza ni
kwanini wanamsaϐirisha katika hali ile na kujibiwa kuwa sehemu
anayopelekwa ni siri na alitakiwa asijue ni eneo au nyumba gani na
kwamba ni watu maalumu tu wanaotakiwa kujua nyumba hiyo ipo
wapi.
Gideon aliposikia hivyo akaona isiwe tabu akachukua simu yake ili
awashe Google Map na angeweza kujua anapoelekea. Alishangaa kuona
mtandao ndani ya gari lile haupatikani na hata sauti za nje hazisikii
ndani.
Gari lilianza safari na Gideon aliona ujanja ni kuanza kuhesabu kona.
Alijaribu akidhani atafanikiwa lakini kuna mahali alichanganywa hadi
biashara ile ikamshinda.
“Mkuu usihesabu kona hutaweza”, alisikika dereva akimwambia Gideon
huku akicheka. Walijua ujanja ambao Gideon angeufanya.
“Huku ndipo mnapopaita Red Square?”, Gideon alihoji.
“Ilipokuwa Red square ya zamani maana tangu juzi imetoka amri Red
square imeshabadilishwa eneo. Sabinasi kabadili na bado ni siri kubwa”,
dereva alijibu.
Gideon alihisi kuishiwa nguvu. Kwa miaka yake saba akiwa Ikulu
hakuwahi kujua Red square, moja ya nyumba za siri za Idara ya Usalama
Wa Taifa Stanza ipo eneo gani. Hata Raϐiki yake kipenzi Stanley Macha
hakuwahi kumwambia.
Walitembea kwa dakika 40 na kisha Gideon alihisi kama wanaingia
shimoni ama kwenye handaki maana gari iliinama chini kwa dakika
kama tatu hivi na kisha mlango ulifunguliwa akashuka.
Eneo lile lilikuwa na taa nyingi na madirisha lakini ambayo yalikuwa
ndani ya jengo yaani usingeweza kuona anga.
Kijana mmoja alimwongoza Gideon wakiwa wanapita milango kadhaa
iliyofunguliwa kwa alama za vidole (ϔinger prints) mpaka mlango wa
mwisho uliofunguliwa kwa kuweka lenzi ya mboni ya jicho ya mmoja
wa wale madereva.
Waliingia ndani na Gideon alistaajabu hali aliyomkuta nayo Macha.
Stanley Macha alikuwa amechoka na mwenye maumivu makali. Alikuwa
amelazwa kwenye kitanda cha chuma akiwa amefungwa mikono, kiuno
na miguu vyote vikiwa vimefungamanishwa na kitanda kile kama vile
maiti inayotaka kwenda kuzikwa.
Mbele ya nyayo zake kuliwashwa mishumaa iliyokuwa ikiunguza nyayo
zake tartiiibu hivyo kusababisha malenge lenge makubwa. Mdomoni
alifungwa riboni ya gundi iliyomfanya asiweze kutoa sauti za kilio cha
maumivu.
Inspekta Majita alikuwa akiendesha kile wazungu wanakiita ‘enhanced
interogation’ yaani mahojiano ya mateso. Mahojiano ya namna hii
hufanyika mara baada ya jitihada za kumfanya mlengwa aongee jambo
unalotaka aϐichue zinaposhindikana.
Lakini pia kwa siku za karibuni mahojiano ya namna hiyo yamekuwa
yakipigwa vita kwani humfanya mtu kudanganya au kukubali jambo
ama kukataa hata kama si kweli ili tu ajiepushe na mateso. Kwa nchi
zilizoendelea wametengeneza mifumo na teknolojia zinazoweza
kumfanya anaehojiwa kugundulika kama anadanganya ama la bila hata
kumtesa.
Mashirika mengi ya kijasusi na ya kiuchunguzi katika nchi zilizoendelea
hutumia teknolojia inayoitwa ‘Polygraph’, almaarufu kama ‘lie detector
test’ ambacho ni kifaa maalumu kinachopima na kurekodi viashiria
mbalimbali vya kimwili kama vile msukumo wa damu, mapigo ya moyo,
upumuaji, na mienendo ya ngozi wakati ambao mtuhumiwa anaulizwa
na kujibu maswali mfululizo.
Mathalani, kuna vifaa vinavyopima mapigo ya moyo ukiwa unaongea
ukweli au uongo, vifaa vinavyopima mpepeso wa macho na njia
nyingine kama zile wazungu wanazoita ‘Logical deduction’ ambazo
hazimuumizi muhojiwa lakini humpelekea anaehoji kuujua ukweli.
Pamoja na teknolojia hizi kuwepo, bado nchi nyingi duniani ikiwamo
Stanza ziliendelea kupendelea mfumo wa zamani wa mahojiano
uliohusisha mateso kwa mlengwa hadi aseme lile anayehoji anataka
kusikia. Hali hii ilimkumba Macha, aliyekuwa bosi wa wale wanaofanya
kazi hizo. Lakini Stanley Macha akiwa mtaalaamu wa yote hayo
ilishindikana kumpata kwa lolote.
Gideon alipoingia na kumkuta Macha akiwa kwenye mateso makubwa
huku akigugumia wakati Majita akivuta sigara bila hata kumtazama
Macha alipiga kelele….
“Kwa amri ya Rais simamisha zoezi hili Majita”, Gideon alifoka huku
machozi yakikaribia kumtoka.
Majita bila hata kujibu kitu alisogea na kufungua zile kamba kisha bila
kusema na mtu alitoka nje ya kile chumba. Majita alikuwa ni kama
shetani aliejivika ng’ozi ya mtu.
Gideon alimsogelea Macha na kukosa la kutamka. Alibaki akimwangalia
na Macha hakika alikuwa akigugumia kwa uchungu wa kilio alichojikaza
kisitoke nje.
“It’s ok. I have got your back”, Gideon alinong’ona.
“Familia yangu ipo salama? Joe amekamatwa?”. Macha aliuliza haraka.
“Familia zipo salama na Joe bado hajakamatwa ila Costa ametoa amri ya
Majita kukutesa hata kifo kama hutasema chochote kuhusu mpango ule.
Hivi ninapoongea na wewe amesema pia atawatuma watu China
wakamsake Joe na popote watakapoweza kumuua basi wamuue”,
Gideon aliongea kwa haraka na yeye. Hawakuwa na muda wa kupoteza.
“Umejitahidi mpaka kuϐika hapa kuniona, umejitahidi sana. Sasa
utawasiliana na Meja Kairuki Byabato wa pale makao makuu ya Jeshi,
ukiϐika mwambie ‘Sienta-Go’ ataelewa. Lakini pia Rais akikuuliza
nimekuambia nini kwa ujio wako huu mwambie ninahitaji kuongea nae.
Sio huku, Ikulu ama Idarani. Lakini niambie nani amekaimishwa
kuongoza Idara?” Macha alihoji kwa haraka.
“Sabinasi, na amepangua watu wote Ikulu. Hivi jengo hili lipo wapi
nimeshindwa kupafahamu.” Gideon alihoji.
“Majengo haya yanaitwa Red square huwa ni siri kubwa kati ya watu
wanne. Rais, Mkuu wa Idara na wale madereva wawili. Hata Inpekta
Majita hajui hapa ni wapi ameletwa kama ulivyoletwa wewe.
Sasa sidhani kama jengo hili mimi nitakuwa najua lipo wapi kwa sababu
lazima wamebadilisha na ndio utaratibu. La zamani lilikuwa mtaa wa
Khanama lakini najua mkuu mpya wa Idara akiingia cha kwanza ni
kutafuta Red square yake na madereva wake wa kuwaleta watu huku.
Huku ndiko watu huweza kutoweka na wasipatikane maisha yao yote
na watu wakadhani wamekufa kumbe wapo huku. Watu wenye taarifa
muhimu huwezi kuwaua, unawatunza lakini unawatoa kabisa kwenye
macho ya dunia na mara baada ya kujiridhisha kuwa hawana faida tena
na wewe ndio huwaua. Gideon nimekwambia kuliko uliyotakiwa
kusikiliza, muda sio Raϐiki, kaendelee na taratibu za misheni.
Ila hakikisha haukamatwi kwani mateso haya huwezi kuyastahimili
hata kwa sekunde moja”, Macha aliongea kama mzazi kwa mwanae.
“Sasa wakati nilipotaka kutoka niliona Rais Costa akisaini jalada fulani
limeandikwa Presidential Order: Order to Kill. Sikuweza soma vizuri
linahusu nini ila kulikuwa na majina na jina moja wapo ni Sylvanus
Majura, unalifahamu hili jina?”, Gideon alihoji.
“Loh, huyo ni ‘Special assassin’ wa Idara. Kwa vyovyote ni kati ya
waliotumwa kumuua Joe. Jina hilo llikuwa la kwanza ama la mwisho?”,
Macha aliuliza.
“La Mwisho”, Gideon alijibu kwa haraka.
“Basi huyo ndio kiongozi wa misheni. Sisi huandikaga kutokea chini
kwenda juu. Sasa mtaarifu Joe awe makini”, Macha alishauri.
Kabla Gideon hajaongea jambo lingine, mlango ulifunguliwa na Majita
kwa sauti ya kukoroma na yenye besi nzito alimtaka Gideon kuondoka
eneo lile.
Gideon alitoka kwa kasi akiongozwa na wale madereva na kuingia
kwenye gari lililomleta ili kuelekea Ikulu.
Aliϐika Ikulu na kukuta Rais yupo na ratiba yake ya vikao hivyo alienda
oϐisini kwake na kuingia kwenye game ya Clash Royale na kuanza
kumpa Joe taarifa zote alizokusanya siku ile.
******************************
“Habibu muda wetu kukaa hapa umekwisha kesho twapaswa
kuondoka” Joe alimwambia Habibu aliyekuwa amejilaza kitandani
kwenye kile chumba.
“Tunaeleke wapi?”, Habibu alihoji.
“Sijajua bado. Najua Korea wataanza kumsumbua Rais Costa kuanzia
kesho”, Joe alijibu.
Wakiwa wanajadiliana mara mlio wa simu wa Joe uliita kuonyesha
kuwa kwenye game yake ya Clash Royale kuna ujumbe umeingia.
Alichukua na kuanza kusoma.
Alikuwa Gideon amempa taarifa na mipango yote. Alihuzunika sana
aliposikia hali ya Macha.
“Subiri niwasiliane na Meshack kuhusu huyu Sylvanus”, Joe alimjibu
Gideon.
“Kuna taarifa gani?”, Habibu alihoji.
“Tuwe makini kuna watu wametumwa kuja kunitafuta ili waniue. Bahati
nzuri wewe sio tageti wa Rais Costa. Sasa subiri niwasiliane na
Meshack”, Joe alijibu.
Joe alianza kumpigia Meshack Simu kwa njia ya WhatsApp kwenye
namba ambayo Meshack huitumia kwa kazi maalumu. Kwa kawaida
simu za WhatsApp ni salama kwasababu maongezi yake hayawezi
kudukuliwa na serikali au mashushuhu kwasababu tu zina mfumo wa
usalama wa usimbaji ϔiche wa mpigaji au mtumaji ujumbe na mpokeaji,
yaani end-to-end encryption. Simu iliita na mwishowe akaipokea.
“Kaka”, Meshack aliita.
“Got an intel kuwa Sylvanus ametumwa kuja kunimaliza.
Unamfahamu?”, Joe alihoji.
“Ndiyo. He is the master of silent killing. One of the worst assasins in
Stanza, I can conϐidently argue”. Meshack alionekana kuongea kwa sauti
ya taratibu.
“Now, you need to deal with him before he boards to China”, Joe
alimwambia Meshack kifupi.
“Do you mean killing him? No, that I can’t guarantee you Joe. He is a
very intelligent agent, If I poke him, I may compromise everything here.”
Meshack alijibu
“Meshack, wewe ndio ulikuwa unamlinda Rais Costa, iliwezekanaje
awekwe mtu asiye hodari kumlinda Rais? Macha ameniagiza nikwambie
‘umhandle’ Sylvanus”, Joe alimwambia Meshack.
Meshack alikaa kimya kidogo. Alitafakari ni namna gani anaweza
kumuua Sylvanus, kwanza bila yeye kuwahiwa na pili bila kujulikana.
Aliona sasa hapo ametiwa majaribuni na suala hili litaweka Maisha yake
kwenye mstari wa mauti.
“Hii ni mbwa kula mbwa kaka”, Meshack alinong’ona akijua Joe
hamsikii.
“Vyovyote utakavyoiita. Just do it” Joe wakati huu alionekana kuongoea
kwa kutoa amri. Alikata simu.
Mara baada ya Joe kukata simu alipokea ujumbe mwingine kwenye
simu yake. Aliusoma kwa makini kama vile unampa maelekezo Fulani
aliyopaswa kuyafuata kwa makini. Wakati huo Habibu alikuwa
anamuangalia kila kitu, akishangazwa na sura ya Joe iliyoonekana kuwa
na hasira mara baada ya mazungumzo yake na Meshack.
Mara baada ya Joe kusoma ujumbe ule na kumaliza, alimwambia Habibu
kuwa asimame waondoke. Habibu alitaka kutouliza, lakini akajikuta
anashindwa kuvumilia.
‘’Joe, ni nini kinaendela? umeshajua tunakwenda wapi na hatua gani
inafuata’’? Habibu aliuliza maswali mfululizo.
‘’The transfer window has just opened. Expect some new powerful
signings soon. Stanza will be turned upside down soon enough. We are
going to reclaim our country, the country that the founding fathers and
mothers fought to liberate from the yokes of colonialism. We cannot
allow to be colonized by our fellow countrymen’’.
(Dirisha la Usajili limefunguliwa. Tarajia uhamisho wa wenye nguvu hivi
karibuni. Stanza itageuzwa juu chini hivi karibuni, ingawa bila kumwaga
damu ya mtu. Lazima tuichukue nchi yetu, nchi ambayo wazee wetu
waliipigania kuondoa minyororo ya ukoloni. Hatuwezi kuruhusu
kufanyiwa ukoloni na Wanastanza wenzetu’’, Joe alimjibu Habibu kwa
mafumbo.
‘’So be it’’, Habibu hakuongezea neno bali kujibu kwa ufupi.
*************************
Usiache Kufuatilia Sehemu Ya 14 Itakayokujia Siku Ya
Sent using
Jamii Forums mobile app