The President And I(Mimi Na Rais)- Sehemu Ya Kumi Na Saba
Mambo Yazidi Kuwa Mazito
Ilikuwa ni asubuhi yenye utulivu katika Ikulu ya Stanza. Kila mtu akiwa anaendelea na shughuli zake kama kawaida Gideon alikuwa akikatiza kwenye korido za Ikulu huku akisalimiana na baadhi ya watendaji wa Ikulu kwenye ofisi zao.
Ni kawaida kwa Gideon kuingia kwenye ofisi za baadhi ya wafanyakazi pale Ikulu hasa ya Katibu Mkuu Kiongozi na kubadilishana nae mawazo mawili matatu. Kwa kufanya hivyo, ilimsaidia Gideon kujua mambo mengi yanayoendelea ndani ya Ikulu ya Stanza isiyoisha matukio.
“Ahaaa bwana Jabir, kwema kaka yangu?”, Gideon alimsalimia Jabir Salehe, Katibu Mkuu Kiongozi akiwa amesimama mlango wa ofisi yake alipopita kumsalimia.
“Gideon, salama mdogo wangu. Tena nilitaka kukufata ofisini kwako kwa sababu Mheshimiwa aliniambia amekupa kazi ya kuandaa majibu kwa Rais Chriss, umefikia wapi asee?”
“Ndiyo hii nilikuwa naelekea ofisini kwake sasa hivi akaipitie”, Gideon alimwonyesha Jabir karatasi aliyokuwa ameishikilia mkononi.
“Hata mimi nilikuwa na hii taarifa kwa vyombo vya habari aliyoandaa Alpha ya kumteua Ketina kuwa Mbunge. Ninaendelea kuihakiki ili akaitoe kwa umma”, Jabir alimwambia Gideon huku akiisoma ile barua ya majibu ya Rais Costa kwa Rais Chriss wa Marekani aliyokuwa ameishika Gideon.
Alpha Wauwau ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu.
“Amemteua Ketina kuwa Mbunge kwa zile nafasi zake tano za ubwerere? Ha ha ha!”, Gideon alimwambia Jabir kwa utani. Walipenda kutaniana sana.
“Ndiyo, na baada ya uteuzi huu atakuwa amezimaliza. Lakini sijui ni nani amemshauri hivi, maana yule binti ni kituko na usikute anataka kumpa nafasi nyeti”, Jabir alimwambia Gideon huku akimalizia kusoma ile barua.
“Washauri wa Rais ni wengi bwana. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuchagua ni ushauri upi auchukue upi auache”, Gideon aljibu kinafiki akijua fika ni yeye aliyemshauri Rais Costa afanye uteuzi huo.
“Haya majibu umeyapanga vyema Gideon” Jabir alimalizia na kumrudishia ile karatasi Gideon. Gideon alitoka na kuendelea na safari yake kuelekea ofisini kwa Rais.
Alifika ofisi ya Rais na kuambiwa yupo kwenye mkutano wa yaliyojiri (media briefing) na kuwa wamechelewa kumaliza. Alijua fika suala la yeye kumiliki kisiwa cha kitalii huko Ufilipino limemvuruga na sasa anataka kujua maendeleo ya habari hiyo na hatua gani vijana wake wamezichukua. Alitaka kugeuza ili arudi baadae lakini vile anataka tu kuondoka alimuona Rais Costa akija akisindikizwa na walinzi wake wawili.
“Gideon, what’s new?”, Rais Costa aliongea kwa sauti akitokea mbali alipomuona Gideon nje ya chumba cha ofisi yake.
“Mh. Rais”, Gideon alijibu kwa kuinamisha kichwa kidogo ishara ya utii kwa mkuu wa nchi.
Rais Costa alimfikia Gideon na kumshika begani na kuingia nae ofisini kwake. Akiwa ameingia tu aliichukua ile karatasi aliyokuwa ameishika Gideon na kuanza kuisoma.
Karatasi ile ilikuwa ni yale majibu ya Rais Costa kwa Rais Chriss wa Marekani juu ya shutuma dhidi ya Stanza kutokufuata misingi ya Kidemokrasia, Haki na Utawala Bora pamoja na uvunjwaji wa Katiba na Sheria.Rais Costa ndiye aliyemuomba Gideon aandae majibu yale.
Rais Costa aliipitia kwa umakini na kutabasamu kidogo. “Briliant reply, Gideon! Umeandika vizuri na kwa ustadi isipokuwa hapa ulipoandika ‘we kindly ask you to not intervene in our internal affairs as we are a sovereign country. You are not the police of the world, deal with your internal matters without jeopardizing peace and security of other countries’, mimi nadhani ni ‘understatement’ ya msimamo wetu kama nchi. Kwanini umeandika kama vile unamuomba?
Badilisha hiyo statement, mkumbushe kuwa according to the United Nations’ Charter, Chapter 1, Article 2, Section 4 inasema wazi ‘’all members shall refrain in their international relations from the threat or use of force against the ‘territorial integrity or political independence of any state, or in any other manner inconsistent with the purposes of the United Nations. Stanza ni taifa huru and so shall it remain.
Sasa sisi na wao wote ni wanachama wa Umoja huu, yeye anachofanya ni kukiuka kifungu hicho na kutumia mabavu dhidi ya nchi nyingine Gidi. Badilisha hapo halafu niletee nisome tena”, Rais Costa alimalizia kujibu kwa mchanganyiko wa Kingereza na Kiswahili na kumrudishia Gideon karatasi ile.
“Sawa Mheshimiwa! Halafu nimeona ni kama Katibu Mkuu Kiongozi anapitisha tangazo la uteuzi wako wa Ketina kuwa Mbunge, ndio ule mwendo wa kutaka kumteua kuwa Waziri nini?”. Gideon alipokea ile karatasi na kumuuliza Costa juu ya uteuzi wa Ketina.
“Oh! Yah yah Gideon! Nitafanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, Kinyamagoha atapisha wanaoweza kwendana na kasi yangu. Kama ulivyonishauri, Ketina nitampa hiyo Wizara nihakikishe muswada tunaokusudia kuufikisha bungeni unakwenda kwa kasi ninayoitaka”, Rais Costa alimjibu Gideon huku akianza kusoma kalabrasha pale mezani kwake.
“Ketina atalifanikisha. Nitamsaidia”, Gideon alijibu.
“Yes, infact utakuwa nae karibu maana ninakutegemea unisaidie kulifanikisha hili. Nitaongea na Spika wa Bunge na uongozi mzima wa Bunge wahakikishe muswada huu hauwekewi vikwazo hata kidogo. Ikiwezekana wale wabunge wote wenye kelele awapangie ziara nje ya nchi. Anyway, nitaona itakavyokuwa”, Rais Costa alionekana kuwa na mipango kichwani.
“Na vipi kuhusu suala la Julius kupeleka taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa unamiliki kisiwa cha kitalii Ufilipino mkuu?” Gideon alidodosa.
“Ndio kitu kilichonipotezea muda huko kwenye kikao. Hawa vijana ni wazembe, waliwezaje kuacha kitu kama kile kichapishwe? Angalau wamenihakikishia yule Muhariri wameshaelewana nae ile habari haitaendelea tena na Julius tutamshughulika tu. Mwanajeshi akisaliti, wenzake wanajua cha kumfanya. Hawezi kuendelea kuwepo, ipo siku”, Rais Costa alionekana kujibu kwa hasira.
Gideon hakutaka kuongeza neno, alimuaga Costa ili toke lakini ghafla mlango ulifunguliwa na aliingia Sabinas mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa la Stanza akiwa anaonekana kutokuwa sawa. Ni kama alikuwa amekuja kutoa habari fulani mpasuko.
“Mkuu nimepata taarifa kutoka kwa Sylvanus kuwa Meshack alikuwa amepanga kumuua. Jana usiku walikutana Casino na baadae aligundua kuwa Meshack alikwenda pale kumuua Sylvanus. Uthibitisho ni jinsi alivyovaa amenitumia na hizi picha. Na ninaamini ni kweli kwa sababu hakuna mwenye taarifa za Meshack kuwa hapa mjini kuanzia mimi wala kiongozi wake wa Kanda”.
Taarifa zile zilimshtua sana Gideon kiasi kwamba ilibaki kidogo ashindwe kujizuia kuonyesha hisia zake.
“Kwa hiyo nini kimetokea”, Rais Costa aliuliza huku akiangalia ile picha aliyoonyeshwa na Sabinas kwenye simu janja.
“Hii ina maana kuwa bado kuna mpango wa kukupindua unaendelea Mh. Rais na Joe bado ana watu wake ndani ya serikali anaowatumia kufanikisha mpango huo. Ni wazi huyu Meshack alitumwa kummaliza Sylvanus ili asiende China kummaliza Joe”, Sabinus aliongea kwa msisitizo.
“Ndio maana mimi nilishauri Mh. Rais ni vyema ukaongea na Macha yamkini akatufumbulia fumbo hili”, Gideon alidakia kwa kujikaza.
Machozi ya huzuni dhidi ya Meshack yalikuwa yakimlengalenga Gideon. Hakuamini kama ule ulikuwa ndiyo mwisho wa maisha ya kijana Meshack, alihuzunika sana lakini alijisemea kichwani kuwa ili mabadiliko ya kweli yatokee ni lazima baadhi ya wapambanaji wajitoe muhanga.
“Sabinas mwandae Macha, nitaonana nae leo jioni”. Rais Costa alionekana kuanza kupandisha munkari upya.
“Kwa hiyo Meshack ameuawa?”, Gideon alishindwa kuvumilia, alimuuliza Sabinas huku akiitazama ile picha iliyomwonyesha Meshack amelala pale chini.
“Swali la kujiuliza ni taarifa zilimfikiaje Meshack mpaka kuamua kumvizia Sylvanus. Alijuaje? Kwani wewe Sabinas yale majina uliyapanga na mtu? Ulimwonyesha mtu?”. Rais Costa aliuliza na kukatiza jibu alilotakiwa kupewa Gideon juu ya kifo cha Meshack.
“Hapana mkuu niliiandaa mwenyewe labda yule binti alieichapa pekee ndiye aliyeiona lakini tofauti na hapo hakuna”, Sabinas alijibu huku akiwaza sana kuwa kweli ni nani atakuwa amepenyeza zile taarifa.
“Yule binti asingeweza kuelewa Sylvanus anatumwa wapi maana tunamtuma kwingi. Hawezi akawa ni yule binti. This is serious”, Rais Costa alipata woga wa ukweli.
“Nitatazama kwenye kamera wakati yule binti anachapa orodha ile ni nani alikuwa karibu naye. Wanaweza wakawa hata wale walioko kwenye ‘control room’ za kamera wanatumiwa na Joe Mh. Rais”, Sabinas alijibu.
Wakati wote huo Gideon alikuwa kimya akiwa amejikaza maana aliona hakika muda wowote kibao kinaweza kumwangukia yeye. Lakini alijipa moyo kuwa siku ile alipoona lile jina alilitazama kwa ujanja na sio kuwa alishirikishwa kwa hiyo alikuwa na cha kujitetea.
“Sabinas haraka fanya uchunguzi taarifa hizi zimemfikiaje Meshack nataka nijue mzunguko mzima. Pia, kama nilivyokwambia, muandae Macha, nitazungumza nae leo jioni hukohuko idarani. Thank you, gentlemen”. Rais Costa alimwagiza Sabinas na kisha kuwaruhusu watoke.
Sabinas na Gideon wote walitoka kwa pamoja na haraka Gideon alimkimbilia Sabinas na kumuuliza kama Meshack alikufa ama la.
“Gideon does this have anything to do with you, kaka?”. Sabinas alimjibu Gideon. Kwa Kiswahili tungesema alimshushua.
‘’Ofcourse yes, Sabinas! I am a senior adviser to the president. I am also acting as his Special Councillor, do you truly believe that I should not be aware of anything that is going on, whatsoever?’’. Gideon alijibu kwa kuonekana na hasira kidogo kwa swali aliloulizwa na Sabinas.
Sabinas hakuwahi kuelewana na Gideon wala yeyote ndani ya Ikulu ya Stanza. Uhasama huo ulijengeka kutokana na ukweli kwamba Macha alikuwa mtu mzima kiumri na alipaswa kustaafu muda mrefu lakini hakuna mtu aliyewahi kumshauri Rais Costa amtoe Macha kwenye nafasi ile. Aliona ni kama wanamuwekea kile watoto wa mjini wanaita kauzibe. Hata nafasi ya Ukaimu wa Idara aliesababisha na kuweka msukumo sana yeye kuteuliwa alikuwa ni Katibu Mkuu Kiongozi aliyestaafu, ndugu Njano Manara.
Alijiona ni kama mtu anayejipambania mwenyewe mbele ya Rais Costa hivyo hakutaka kushiriki na mtu yeyote kwenye utawala wa wakati ule.
Gideon alipoona hakujibiwa aliachana nae na kuelekea ofisini kwake. Alikuwa akitembea huku akiwa na huzuni nyingi sana. Alijua tu kuwa kama Meshack atakuwaa amefikwa na umauti basi ni kwa sababu ya misheni yao. Alijua fika ni Joe ndiyo atakuwa amemtuma Meshack kumdhibiti Sylvanus.
Aliingia ofisini kwake na kujifungia. Aliingia kwenye game ya Clash Royale na kumtaarifu Joe kila alilosikia. Alimaliza na kuanza kulia.
****************************************
Meja Byabato aliingia ofisini kwake na kukaa huku akijishikashika Sehemu alizopigwa na wale vijana wake. Wale vijana nao walikaa kila mtu akigugumia kwa upande wake.
“What is the meaning of all this, young men?” (Maana ya haya yote ni nini nyie vijana?), Byabato aliwauliza wale vijana wake kwa kimombo.
“Hamna kitu mkuu tumeona tujipime tu ubavu na wewe. Unatunyanyasaga sana kwenye mazoezi tukasema leo tusherehekee siku yako ya kuzaliwa kwa kukupa kichapo. Ha ha ha!” Mmoja wapo alijibu.
“Kwa hiyo yale mazoezi mliyokuwa mnafanya wiki hii nzima ni kwa ajili mje mnipe kichapo?” Byabato aliuliza huku akitabasamu.
“Ndio, ila dah umetuweza, tutajipanga tena” Kijana mwingine alidakia.
“Mmejitahidi sana lakini. Ilikuwa nusura mniweke chini”. Byabato alikiri uwezo wa wale vijana wake.
Byabato alikuwa askari shupavu, mkomavu wa mbinu na mkorofi lakini alikuwa mtu wa utani na wale walio karibu nae. Aliwapenda na kuwajali, hivyo hata kuvamiwa kwake alishtuka ni kwanini. Alipogundua kuwa walimshughulikia kwasababu ya siku yake ya kuzaliwa, hata hakuwachukulia hatua za kinidhamu. Hii ilimsaidia kujenga ukaribu na upendo na wanajeshi wengi katika kikosi cha jeshi la anga la Stanza.
“Funga huo mlango vizuri”, Meja Byabato alimwambia mmoja wa wale vijana.
“Sasa sikieni mmetokea wakati mzuri sana. Actually, mliniona nilikuwa nakuja mbiombio kuna kazi inatakiwa kufanyika lakini nikawa nawaza sana nitampa nani au kwa maneno mengine nimuamini nani”, Meja Byabato alianza mazungumzo.
“Kivipi mkuu maana wewe ukitoa kazi kwetu ni amri, si ndo ujeda unavyosema mkuu?”, Mmoja wa wale vijana alijibu kihuni hivi.
Wao na Meja Byabato walikuwa na uhusiano zaidi ya kikazi kwani mbali ya kazi walikutana kila jioni kwenye sehemu yao wanapofanyia mazoezi hivyo walizoeana kutaniana japo waliheshimiana kama kaka na wadogo zake. Meja Byabato akiwa ni mkubwa kwao wote.
“Sio issue ya kazi Majengo, achana na kazi kabisa nataka tuongee kama watoto wa kiume hapa na kama kuna ambalo mtu hatakubaliana nalo basi liishie humu humu. Sawa?” Byabato aliongea.
Waliokuwa wamekaa ni vijana wawili na wawili walikuwa wamesimama upande wa mlangoni. Meja Byabato na yeye alisimama na kukunja mikono na kuzungukazunguka kama mtu aliyekuwa akiwaza jambo. Wale vijana walibaki kimya wakiwa wanamtazama wasijue mkuu wao anataka kuwaambia kitu gani.
Hakika Meja Byabato alijawa na mwazo mengi sana. Alikuwa akiwaza ikiwa awaamini hawa vijana ama la. Je, nini itakuwa madhara kama ikitokea mmoja wapo akakataa kukubaliana na akaenda kuropokwa nje. Alijilaumu ni kwanini hakuwa ameandaa vijana mapema kwa ajili ya jukumu lililo mbele yake mpaka umefika wakati anatakiwa kufanya na hajui nani wa kumsaidia.
Alifikiri mambo mengi kwa haraka na mwisho alijua nini cha kuwaambia na nini asiwaambie kwanza. Alijua awatume nini na nini atakifanya mwenyewe.
“Juma, Shafii sogeeni hapa mezani”, Byabato aliwaita wale waliokuwa wamesimama upande wa mlango wasogee karibu na meza waliyokuwa wamekaa wenzao. Alikuwa tayari kuwaambia kile alichofikiria kuwaambia.
************************************************
Gideon alikuwa katika majonzi makubwa pale aliposhtuliwa na simu yake ikiwa imeingia mlio wa game ya Clash Royale. Alijua lazima atakuwa ni Joe amesoma jumbe zake na kumjibu.
“Sadam, umeniumiza sana na taarifa hizo. Sina cha kusema zaidi ya kumsikitikia Meshack”, but sometimes sacrifices must be made. He did well’’, Joe aliandika.
“Nimeumia sana na hata nimeanza kuogopa. Woga wangu unazidishwa na huu utafutaji waliouanza wa nani kamtuma Meshack. Wataninasa tu!” Gideon aliandika.
“Ni ngumu. Hawakukushirikisha, huo ndio mlango wako wa kutokea. Sasa fuatilia Meshack issue yake imefikia wapi, mipango ya mazishi na kila kitu. He deserves our great respect. He lost his life in the line of duty for our great nation. History will honor him correctly”, Joe aliandika.
“Ni kweli maana watu wengi hujitoa sadaka na kupoteza hata maisha yao kwa ajili ya mambo makubwa ya Taifa lao lakini mwisho wa siku husahaulika na kutukuzwa wale wanaokuja kulifanikisha mwishoni. Lazima tulibadilishe hili…. kama tukifanikiwa lakini”, Gideon aliandika kwa majonzi makubwa.
“Tuyaache hayo, kwasasa fuatilia kwanza ujue kama ni kweli alikufa na mwili wake upo wapi. Lakini kuhusu suala la Ketina mtafute Sara, ukachochee kuni. Chochea kwa akili lakini. Kuhusu Costa kuonana na Macha hilo nalo ni la msingi sana”, Joe aliandika
“Sawa Che. Ila sasa kuwa makini Sylvanus atawasili huko usiku wa leo. He is a monster”. Gideon aliandika.
“Incase I don’t survive, you will tell the tale that I did this for the great good of our nation. If I die, please do pause the mission for now and find another way of starting afresh. But never abort. You can only retreat, but never surrender.” Joe aliandika. Gideon alisoma ujumbe wa Joe na kuona hali ya huzuni na uchungu. Aliendelea kuamini kuwa mtu huyu alitamani kuona mabadiliko ya kweli katika nchi yake.
“Sasa hivi mpo wapi kwani? Habibu anasemaje?”, Gideon aliandika.
“Habibu yupo kamili”, Joe alijibu swali la pili na kuacha la kwanza. Alitoka hewani.
Haraka Gideon alitoka ofisini kwake na kuanza kuelekea ofisi ya Sara, mke wa Rais Costa. Ofisi zake zilikuwa hatua chache kutoka kwenye jengo kuu la Ikulu ya Stanza na ndipo zilipokuwa ofisi za Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na vijana walioathirika na dawa za kulevya. Shirika linalosimamiwa na Sara.
Alifika kwenye ofisi zile na hakumkuta Sara. Aliuliza yupo wapi na walijibiwa kuwa ametoka ameelekea ofisini kwa Gideon. Gideon aligundua yeye alipitia njia ya nyuma hivyo Sara anaweza akawa alipita njia ya mbele. Alianza tena kurudi ofisini kwake.
*******************************************
Ilikuwa ni jioni iliyokuwa na joto kali siku ile. Rais Costa akiwa anasindikizwa na walinzi wake saba alikuwa akitoka nje ya Ikulu ya Stanza kuelekea ofisi za Idara ya Usalama wa Taifa Stanza.
Nje zilitangulia pikipiki mbili za ving’ora kisha likafuata gari la jeshi kisha likafuata gari la Usalama wa Taifa nyuma yake kulifuata gari la Rais na kisha yalifuata magari mawili ya Usalama wa Taifa na mwisho lilikaa gari la jeshi.
Kwake yeye hali hiyo ilikuwa ni kile wanausalama wa Stanza wanakiita Minor Presidential Convoy, yaani kamsafara kadogo tu kwa Rais kwasababu hakuwa anaenda mbali na eneo Ikulu ilipo.
Kwa kawaida misafara ya Rais Stanza imegawanywa katika makundi makuu matatu. Kundi la kwanza ndilo hilo Minor Presidential Convoy (MiPC), halafu wana Major Presidential Convoy (MaPC) ambapo hapa mbali ya magari mengine mengi ya usalama, polisi na jeshi ni lazima kuwe na magari matatu ya Rais yenye kufanana kabisa ambayo yatakuwa yakikimbia kwa kupishana.
Kundi la mwisho ni lile wanaliita Full Presidential Convoy (FPC). Katika msafara huu, huchukua kila kilichopo kwenye MaPC na kuongezea ulinzi wa anga kama ndege za kivita na Helikopta pamoja na vituo vya wanausalama kila baada ya kilometa 50 katika njia nzima ambayo Rais atakatiza katika safari yake.
Rais Costa aliwasili ofisi za Idara ya Usalama wa Taifa Stanza na kupokelewa kwa heshima kubwa na Sabinasi Paulo pamoja na viongozi wengine wa Idara ile. Bila kupoteza muda, Sabinas alimwelekeza Rais kwenye chumba walichokuwa wamekiandaa kwa ajili ya mazungumzo kati ya Rais Costa na Stanley Macha.
Mlango ulifunguliwa na Rais Costa aliingia.
“Mh. Rais”, Stanley Macha alinyanyuka kwa taabu na kunyoosha mkono ili kumsalimia Rais Costa. Jicho moja la Macha lilikuwa limevimba sana kwa sababu ya mateso aliyokuwa ameyapata kutoka kwa Inspekta Majita.
Rais Costa alimwangalia Macha kwa dakika kama moja hivi bila kupokea salamu wala mkono wa Macha.
“Keti”, Rais Costa alimwambia Macha na wote waliketi.
“Gentlemen, thank you.”, Rais Costa alisema kwa kifupi akiwa na maana ya kutoa amri watu wote waliopo pale waondoke na kuwapisha. Alimtoa nje kila mtu hadi Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Sabinasi.
“Thank you, Mr. President, for accepting my request to meet me”, Macha alianza kuongea.
“Macha, uniambie yote leo”, Rais Costa aliacha kumjibu Macha na kumtaka amwambie kila kitu.
Macha alivuta pumzi kwa nguvu na kusafisha koo lake, ishara ya kuwa tayari kuzungumza.
‘’Mh Rais, unachoona kuwa ni mpango wa mapinduzi, walioupanga ndo walitaka utokee kama ulivyotokea. Na uliowaweka karibu yako ndiyo watakaokuondoa madarakani’’, Macha alianza kwa kauli iliyomshtua Rais Costa.
**************************************
Nini Kitaendelea Katika Simulizi Hii Ya Kusisimua? Tukutane Wiki Ijayo.
the Legend☆