Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi: UKWELI WENYE KUUMA ( PAINFUL TRUTH )
Mwandishi: NYEMO CHILONGANI
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
Msichana Happy alikuwa akilalamikia uchungu ambao ulikuwa umemshika katika kipindi ambacho alikuwa shambani akilima. Damu zikaanza kumtoka katika sehemu zake za siri, akalitupa jembe lake pembeni na kuanza kulishika tumbo lake ambalo aliliona kuwa katika maumivu makali.
Mama yake ambaye alikuwa pembeni pamoja na wakulima wengine wakaanza kumsogelea, Happy alionekana kuhitaji msaada kwa wakati huo. Wakatandika kanga zao chini na kisha kuanza kumzalisha pale pale shambani. Mpaka wanafanikiwa kumtoa mtoto, Happy alikuwa amepoteza damu nyingi sana mwilini mwake.
Mtoto mchanga alikuwa akilia, walipomwangalia vizuri, waligundua kwamba alikuwa mtoto wa kiume. Walichokifanya ni kumuinua Happy na kisha kumpeleka katika kivuli cha mti wa mwembe ambao ulikuwa pembeni kidogo ya shamba hilo.
Happy bado alikuwa akiendelea kulia, maumivu makali bado yalikuwa yamelikamata tumbo lake. Kwa haraka haraka mzee Lyimo akachukua baiskeli yake aliyokuwa ameiegesha pembeni na kisha kumpakiza Happy na safari ya kuelekea katika zahanati ya Machame kuanza.
Njia nzima Happy alikuwa akilia, maumivu yalikuwa yakiongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele. Mpaka wanafika Zahanati, Happy alikuwa hoi, hakuwa akiweza hata kusogeza kiungo chake chochote cha mwili wake.
Manesi ambao walikuwa nje wakipiga stori, wakaanza kuwasogelea, wakamteremsha Happy kutoka katika baiskeli ile na kisha kuelekea ndani ya Zahanati hiyo. Mama yake Happy, Vanessa alikuwa amembeba mjukuu wake huku akijitahidi kumbembeleza aache kulia.
Happy akaingizwa ndani ya moja ya chumba cha zahanati ile na kisha kulazwa kitandani. Bado alikuwa akiendelea kulia kutokana na maumivu makali ambayo alikuwa akiyasikia yakizidi kadri muda ulivyozidi kwenda mbele. Manesi wakaanza kumhudumia Happy mpaka pale ambapo dokta wa zahanati ile alipofika.
Mzee Lyimo na mkewe, Bi Vanessa walikuwa nje wakisubiri kusikilizia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimeendelea ndani ya chumba kile.
Wala hazikupita dakika nyingi, dokta akatokea mahali pale. Akaanza kuwaangalia huku macho yake yakionyesha wasiwasi fulani, aliporidhika, akaiweka vizuri miwani yake.
“Mtoto wake yupo wapi?” Dokta aliuliza.
“Huyu hapa” Bi Vanessa alimwambia huku akimkabidhi dokta mtoto yule.
Dokta alibaki akishangaa, mtoto yule alikuwa mweupe kupita kawaida, kichwani hakuwa na nywele nyingi kama ambavyo watoto wengi wa kiafrika wanavyozaliwa. Dokta hakuonyesha mshangao wake waziwazi, alichokifanya ni kumchukua mtoto yule na kuingia nae ndani ya chumba kile.
Mzee Lyimo na Bi Vanessa waliendelea kukaa nje ya chumba kile kwa takribani dakika kumi, mlango ukafunguliwa na dokta kutoka.
Wote wakajikuta wakisimama kutoka katika viti vyao, dokta akawaomba wamfuate. Safari iliiishia ndani ya ofisi ya dokta yule.
“Kama msingemuwaisha binti yenu, hakika hali ingekuwa mbaya sana” Dokta aliwaambia.
“Kivipi?” Mzee Lyimo aliuliza.