SEHEMU YA 36
Kuwaona wazazi wake kwa mara nyingine lilionekana kuwa tukio kubwa na la kipekee katika maisha yake, furaha ikaonekana kumzidi, akajikuta akianza kutokwa na machozi. Wakakumbatiana kwa sekunde kadhaa na kisha kuachiana.
Hapo ndipo alipogundua kwamba wazazi wake walikuwa wamekuja na mtu mwingine mahali hapo, huyu alikuwa George. Annastazia akaonekana kushtuka, hakuamini kumuona George mahali hapo. Huku akionekana kushangaa, akayapeleka macho yake kwa wazazi wake, tabasamu pana yalikuwa yakionekana nyusoni mwao.
“Karibu Annastazia...” George alimkaribisha Annastazia.
“Asante” Annastazia alisema na kisha kulichukua begi lake.
Furaha yote ambayo alikuwa nayo katika kipindi kichache kilichopita ikatoweka moyoni mwake, uwepo wa George mahali pale ulionekana kumkasirisha. Kwa kipindi hicho alikuwa akikumbuka mbali sana toka katika kipindi ambacho George alikuwa akimfuatilia na kumkataa.
Wakaingia ndani ya gari, Annastazia hakutaka kuongea tena, muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia nje kupitia dirishani. Alionekana kukasirika, uwepo wa George mahali pale ulionekana kumkasirisha kupita kawaida.
Gari likafunga breki nje ya nyumba kubwa ya kifahari, geti likafunguliwa na gari kuingizwa ndani. Annastazia akateremka na moja kwa moja kuelekea chumbani kwake. Bado alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida, mama yake akaanza kupiga hatua kumfuata kule chumbani alipokuwa.
Annastazia alikuwa amelala kifudi fudi huku uso wake ukiangalia pembeni, mama yake akaingia na kukaa karibu nae pale kitandani. Bado ukimya ulikuwa umemtawala Annastazia, hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kumwangalia mama yake kana kwamba hakuwa akimfahamu.
“Mbona umebadilika hivyo?” Bi Sara aliuliza.
“Nahitaji muda wa kupumzika mama” Annastazia alimwambia mama yake.
Ingawa Bi Sara alionekana kufahamu kile ambacho kilikuwa kimememsababisha binti yake kuwa katika hali hiyo, akaamua kutoka ndani ya chumba kile na kuelekea sebuleni. Uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu pana, kwake aliona kwamba kazi wala haikuwa kubwa kama ambavyo walikuwa wakifikiria kabla.
“Kidogo uwepo wako umeonyesha mafanikio” Bi Sara alimwambia George.
“Mmh!”
“Mbona unaguna?”
“Inawezekana kweli? Hali yake haikuwa ya kawaida kabisa” George alisema.
“Hiyo niachie mimi. Unajua imekuwa kama suprise kwake, hata kama ningekuwa mimi ningekuwa katika hali kama yake” Bi Sara alimwambia George.
Siku hiyo Annastazia hakutoka chumbani kwake, alijifungia muda wote. Moyo wake bado haukuwa na furaha hata kidogo, kadri picha ya George ilivyokuwa ikimjia kichwani mwake ilionekana kumkasirisha. Moyo wake haukutokea kumpenda George wala kuvutiwa nae.
Wazazi wake hawakutaka kuvumilia kumuona akiwa kwenye hali hiyo, walichokifanya ni kumuita na kuongea nae sebuleni. Annastazia hakutaka kuwaambia ukweli wazazi wake japokuwa alikuwa akifahamu fika kwamba wazazi wake walikuwa wakifahamu kila kitu.
“Ni mchoko tu” Annastazia aliwaambia.
Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha yaliyokuwa na karaha, Annastazia hakuwa na raha tena, uwepo wa George ambaye alikuwa akifika nyumbani hapo mara kwa mara ulionekana kumkasirisha kupita kawaida. Hakumpenda kabisa George ingawa wazazi wake walikuwa wakiulazimisha ukaribu kuwepo miongoni mwao.
Kila alipokuwa akija George nyumbani hapo, Annastazia alikuwa akiitwa na kuachwa sebuleni pamoja na George. Muda wote wa kukaa hapo sebuleni Annastazia hakuwa akiongea kitu chochote kile zaidi ya kuangalia televisheni.
Mapaka kufikia hatua hiyo tayari akaona kulikuwa na kila dalili za pingamizi kutoka kwa wazazi wake kama tu angewaambia kuhusu Andy, alichoamua ni kukaa kimya. Kamwe George hakuchoka kuja nyumbani hapo, kila siku alikuwa akifikia nyumbani hapo.