Simulizi ya Kijasusi: Kiguu Na Njia

Simulizi ya Kijasusi: Kiguu Na Njia

SEHEMU YA MWISHO

COUNTDOWN - 5




“Nadhani, maana niliondoka nikiwa mdogo sana. Hata sifahamu nianzie wapi kuwatafuta wazee wangu,” niliropoka bila kutegemea.

Kwa wakazi wa mkoa ambao hauna ajira za kutosha, ambao mkoloni aliutumia kama shamba la kuchukulia manamba wakakate mkonge huko Tanga na Kilimanjaro maelezo yangu hayakumshangaza dereva huyo hata kidogo. Alihitaji maelezo mafupi tu; niliondoka lini. Tulikuwa tukiishi wapi, ukoo wangu ni upi na mengineyo. Nilipomweleza juu ya hofu yangu juu ya vijiji vya Ujamaa alinielewa mara moja. Akanishauri nishuke katika kijiji kinachofuata, kinachoitwa Mayange, ambacho ni kikubwa na kilikusanya familia mbalimbali toka maeneo mengi.

“Walisema kingekuwa kijiji cha mfano kwa maendeleo,” alisema akicheka kwa kebehi. “Hebu katazame hayo maendeleo halafu utatuambia.”

na ushauri wake. Tulipofika Mayenge nililipa nauli yangu, nikateremka na kuanza kazi ya kutafuta ‘kwetu’.

Kama nilivyotegemea kijiji cha Mayange kilikuwa kinyume kabisa na matarajio ya awali kama ilivyokuwa kwa vijiji vingine vyote tulivyovipita njiani, Mayange ilitoa taswira ileile, umasikini unaonuka. Karibu watoto wote walichakaa miili na mavazi, wakifanya kazi ndogondogo kama kubeba mizigo ya wasafiri kwa mikokoteni yao ya miti au kuomba tu kwa wapita njia. Baadhi walivaa sare za shule. Lakini sare nyingi kati ya hizo hazikufanana kabisa na malengo ya wizara







kwa kuchoka na kuchakaa.

Watu wazima nao walikuwa na yao. Wengi wao walikuwa taabani, suruali zikiwa zimejaa viraka, shati zikiwa zimepasukapasuka, miguu iliyokuwa peku ikiwa imebadilika rangi kutokana na vumbi jekundu lililowapiga pindi wakihangaikia mkono kwenda kinywani.

Waliahidiwa huduma muhimu kama barabara; hazikupata kujengwa au kukarabatiwa. Waliahidiwa maji ya bomba; hawakupata kuyaona. Waliahidiwa umeme; ilikuwa ndoto za mchana. Waliahidiwa huduma ya matibabu; sasa ilibidi kuyalipia kwa fedha ambazo huna. Kwa ujumla, ahadi zote zilizotumiwa ili kuwaondoa katika makazi ya baba na babu zao ziligeuka hewa. Jambo hilo lilifanya nyuso za kila mtu unayekutana naye zitangaze dalili zote za kukata tamaa.
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNTDOWN - 4




Kazi ya kuitafuta familia moja, kati ya familia zaidi ya mia saba zilizohamishiwa hapo toka maeneo tofauti haikuwa ndogo. Nilitumia zaidi ya saa mbili kabla ya kumpata mzee mmoja ambaye alimfahamu babu, “Familia ya Kionambali, sio? Wala usihangaike. Wako humuhumu. Mtoto wake Karimanzira huwa namwona mara kwa mara.”

Nikapata matumaini. “Ni babu? Kionambali mwenyewe?” niliuliza.

“Huyo sina habari zake. Sijui kama bado yuko hai au tayari ametangulia,” mzee alinijibu. Laiti angejua kauli yake ilivyonishtua.

Nikiwa na matumaini mapya nilianza awamu ya pili ya kuwatafuta wazazi wangu. Zikiwa safari za mguu, katika kijiji kikubwa kisicho walao na jina la mtaa ilinichukua saa moja na nusu kabla ya kuonyeshwa kwa mbali nyumba iliyoaminika kuwa ya baba.







Ilikuwa nyumba iliyofanana na nyingine nyingi kijijini hapo; tofali za tope ambazo zilichakaa kabla ya kupata lipu, achilia mbali rangi. Juu nusu iliezekwa bati kuu kuu nusu nyasi. Sakafu ilikuwa ardhi ileile waliyoikuta palepale.

Nje ya nyumba hiyo alikuwepo bibi mmoja mchovu kama wengine wote kijijini hapo, akisuka ukili. Nilisogelea na kumwamkia. Kisha niliuliza kama hapo palikuwa nyumbani pa mzee Karimanzira. Swali langu lilimfanya bi mkubwa huyo ainuke na kunitazama kwa makini. Mara nikamwona akianza kutetemeka. Machozi yakianza kumtoka.

“Wewe ni Mtukwao!... Mwanangu! Umerudi…” alisema akinijia na kunikumbatia kwa nguzu zake zote.

Alikuwa mama! Mama yangu kipenzi! Fuko nililokuwa nalo mkononi lilidondoka pwaa, mikono yangu pia ikamkumbatia kwa nguvu. Masikioni nilisikia sauti nzito ya kiume ikilia! Kilio cha kwikwi. Ilinichukua muda kubaini kuwa ilikuwa ni mimi niliyekuwa nikilia.

Mara mzee mmoja akatoka nje ya nyumba hiyo. Alikuwa mchovu vilevile. Umbile lake refu lilipinda kwa mbele, ndevu zenye mchanganyiko na mvi zilimeza kidevu na kichwa chake kizima. Akitetemeka miguu na mikono yeye pia alinijia na kunikumbatia, machozi yakimlengalenga.

Baba! Amezeeka kabla hajapata kuwa kijana!

Dakika mbili tatu baadaye nyumbani palifurika. Watu waliotoka huko na huko walijazana kushangilia ujio wangu. Kila mtu alisema lake, ingawa mada ilikuwa ileile; Mwana mpotevu karejea!

Niliingizwa ndani, nikapewa kiti cha kifalme; kigoda cha baba. Fumba fumbua togwa tamu ikaletwa. Nikapewa kata kubwa iliyojaa. Kabla haijaisha nililetewa mihogo mitamu,
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNTDOWN - 3






huko nje nikiwaona vijana wakikimbizana na jogoo.

Baba na mama hawakubanduka ubavuni mwangu. Walikuwa na mengi ya kuniuliza mengi ya kunisimulia. Kwa bahati mbaya, hali haikuruhusu. Watu walikuwa tele, wakinishangaa kana kwamba nimetoka mwezini. Kelele pia zilishamiri. Watoto ambao hata sikuwafahamu walijipenyeza na kukaa miguuni mwangu, wakijitahidi sana kunikumbatia, walao miguu.

Kwa kweli sikutarajia mapokezi makubwa kama haya. Nikiwa mtu aliyepotea kwa zaidi ya miaka thelathini, mtu aliyerudi akiwa mikono mitupu kama nilivyokuwa, nilitarajia kupokelewa kwa kejeli au dharau. Si vicheko na kushangiliwa kwa takribani kijiji kizima kama ilivyokuwa. Hata hivyo, nilijihisi kama mtu aliyeutua mzigo mzito uliomlemea. Nilijihisi kama ambaye nilifutiwa madhambi yangu yote hata kabla ya kuomba radhi.

Kitu kimoja tu kilikuwa kikinisumbua. Mtu niliyetamani kumwona pengine kabla ya wengine wote hakuwa katika kundi la watu waliojitokeza kunilaki. Mtu huyohuyo nilihitaji sana kumwomba radhi kwa kumwamgusha katika matarajio aliyokuwa nayo juu yangu na kumpotezea hirizi yake muhimu. Nilimtegemea awe katika mjumuiko huo, aniite kando ambako tungeketi peke yetu na kuteta kama mtu na baba yake. Sikumwona. Wala sikuthubutu kuuliza harakaharaka kwa kuchelea kupewa jibu ambalo lingeweza kunitia ugonjwa wa moyo; Babu yake! Mbona alikufa zamani?

Kuku alikwishachinjwa na kupikwa. Ugali mweusi wa nyangwe uliletwa mbele yangu kwa kitoweo cha kuku huyo. Bila kuambiwa wageni walianza kupungua ili kuniachia faragha ya kufaidi chakula changu. Nilishindwa kujizuia. Kabla







ya kumega tonge la kwanza nilimuuliza baba, “Babu yuko wapi?” nilisubiri jibu lake kwa hofu kubwa, moyo ukinidunda. Lakini nilipomwona baba akitabasamu kabla hajanijibu hofu ilitoweka moyoni mwangu.

“Babu yako kwani humjui?” baba alisema. “Aligoma katakata kuhama. Jeshi la polisi, jeshi la mgambo na hata sungusungu walishindwa kabisa kumtoa. Hivi sasa yuko peke yake ndani ya msitu mkubwa wa yaliyokuwa makazi yake. Kila wiki huwa nakwenda kumjulia hali.”
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNTDOWN - 2




Nikapumua. “Bibi?” niliuliza.

“Yeye hatuko naye tena. Alitutoka miaka mitatu iliyopita. Alipatwa na ugonjwa wa malale uliokataa kila aina ya dawa.”

Ladha ya kuku ikaniishia palepale.



***

“Nilijua utarudi salama… nilikuwa nikikusubiri… nisingeweza kufa kabla hujarudi, mjukuu wangu,” ilikuwa kauli ya kwanza ya babu mara aliponitia machoni na kunipapasa kichwani.

Sikuweza kuyastahimili machozi yaliyomiminika toka machoni mwangu. Babu alinikumbatia, huku mkono wake ukiendelea kunipapasa kichwani kwa namna ya kunibembeleza. Kitendo hicho kilizidisha uchungu moyoni mwangu na kunifanya nizidi kulia. Kwa mara ya kwanza, hakunishutumu kwa kitendo hicho. Niliinua uso na kumtazama kwa wizi. Yeye pia alilowa macho kwa machozi.

Babu analia, chuma cha pua!

Kwangu, alikuwa zaidi ya babu. Alikuwa kila kitu; baba, babu, rafiki, mwalimu na zaidi ya hayo. Hayo nilibaini na kuyahakikisha muda huo ambao mzee hataweza kustahimili







kabisa kuficha udhaifu wake kwangu! Nitamsimuliaje malaika huyu kuwa jitihada zake zote za kupita mabonde, milima na misitu yenye hatari zote za dunia, hadi kunifikisha nchi ya Wahaya ili nipate elimu zilikuwa kazi bure? Nitaanzaje kumwambia kuwa ile hirizi yake, urithi pekee alioniachia ilipotea kwa uzembe? Niliteseka vibaya sana akilini nilipowaza hayo.

Nilikuwa nimemlazimisha baba alfajiri tu ya siku iliyofuata aniongoze kuja kumwona babu. Yeye akisisitiza kuwa ningepumzika walao siku mbili kabla ya kufanya safari hiyo. Jambo ambalo sikuafikiana nalo.

Kwa kutokuwa na uhakika wa kuwapata wazazi wangu, wakiwa hai nilifika nyumbani mikono mitupu. Hivyo, nilipopata fursa ya faragha ya kumkabidhi baba shilingi 50,000 kati ya zile laki moja nilizobakiwa nazo nilionekana shujaa mkubwa. Baba alianza mipango ya ‘kumaliza bati’ mama aliongea juu ya kulimisha shamba. Ilikuwa kama nimetoa milioni hamsini. Tulimkuta babu akifunga mbuzi wake nje ya nyumba.
 
SEHEMU YA MWISHO





Alivaa nguo zake zile alizozipenda, kaptula na shati nyeupe. Ziling’ara kama nilivyoziacha! Miguuni alitilia buti zake ambazo nazo ziling’ara kwa kiwi, ingawa zilianza kuchoka. Alikuwa peke yake katikati ya pori, isipokuwa kwa mifugo mingi ya mbuzi, kuku na bata. Watu wa pwani wangeweza kuapa kuwa ni jini jeupe linalokaa peke yake msituni. Babu alikuwa ametusikia toka mbali. Hivyo, alimfunga mbuzi yule harakaharaka na kusimama akitukodolea macho. Alipotuona alitukimbilia na kunidaka juujuu. Angeweza kunibeba… angeweza kunitia mweleka…. Babu alikuwa na nguvu zake. Ilikuwa kama ni binadamu pekee aliyebishana na uzee. Binadamu ambaye hakukubali kusalimu amri kwa kifo.







Pamoja na baba tulikuwa na vijana wengine wawili ambao nilielekezwa kuwa ni ndugu zangu. Vijana hao walipewa amri ya kumkamata beberu mkubwa kuliko wote na kumchinja. Akachunwa. Moto ukawashwa. Muda mfupi baadaye, tulikuwa tukimla mbuzi yule, wa kuchoma. Babu, akiwa na meno yake yote alitafuna mguu mzima wakati wengine tukishika shika hapa na pale.

Baadaye babu aliwataka baba na wale wenzetu wengine kuondoka kwa maelezo kuwa alikuwa na mengi ya kuzungumza na mjuu wake faragha. Usiri wangu na babu halikuwa jambo geni kwa baba, toka utoto wangu. Hivyo, hakutia ubishi, walichukua nyama ya kula nyumbani wakaondoka zao kwa ahadi ya kunifuata kesho.

Nikapata wasaa wa kuchomoa zile elfu hamsini nilizobakiza na kumkabidhi babu. “Zawadi pekee niliyoweza kukuletea ni hii,” nilisema kwa masikitiko.

Babu hakuzipokea. Badala yake alicheka kabla ya kusema, “Sidhani kama nazihitaji. Za nini? Kaa nazo, zitakufaa wewe zaidi. Naamini bado unasafari nyingine ndefu, yenye mafanikio makubwa zaidi. Halafu, bado tuna mengi ya kuzungumza, mimi na wewe.”



“Bila shaka. Niliitikia.

“Miaka mingapi vile toka tumetengana?” Babu aliniuliza. “Mingi sana. Ni aibu kuitaja.” Nilimjibu.

“Aibu ya nini? Mwanaume anayeonea aibu masaibu yake hafai. Kwa nini ufanye jambo ambalo utalijutia maishani mwako?”

Nilijua darasa la babu limeanza. Sikuwa tayari kwa darasa lolote wala somo lolote kabla ya kumtaka radhi. Hivyo nikajikongoja na kumwambia, “Babu ningeomba nianze kwa kukutaka radhi.”







“Radhi ya nini?” “Hirizi.” “Ilifanyaje?” “Ilipotea!”

Nilitarajia babu abadilike, akasirike. Lakini kwa mshangao nilimwona akiachia tabasamu jembamba. “Nisubiri kidogo,” alisema akiinuka na kuingia ndani, aliporejea alikuwa na hirizi mkononi.

“Hirizi hii siyo?”

Niliitazama kwa makini. Nisingeweza kuisahau. Ilikuwa



ileile!





Sikuyaamini macho yangu. Nikamkodolea babu macho



ya mshangao.

“Hii ndiyo inayokusumbua?” babu aliongeza baada ya kicheko kingine. “Usiwe na wasiwasi. Ilipotea ikatafuta njia, ikarudi nyumbani kukusubiri.”

Bado sikuweza kuelewa. Hirizi hiyo ilipotea porini katika purukushani za kuikimbiza isianguke mikononi mwa padri. Yule kimbelembele, Byabato, alinihakikishia kuwa aliiokota tena na kumrudishia padri Backhove ambaye aliichoma, ikakataa kuungua. Kwamba baadaye ilitupwa baharini. “Ilifikaje kwako?” nikamuuliza.

“Ni hadithi ndefu. Ili kuifanya fupi pengine nikuambie tu kuwa ililetwa.”

“Na nani?” nilizidi kumbana babu. “Na mizimu ya babu zetu.”

Bado nilikuwa sijamwelewa. Nikamwambia hivyo. “Mizimu ina njia nyingi ya kuwalinda wahanga wake,”

alifafanua. “Chochote kilichokutokea hadi hirizi hii kutengana nawe wahanga walikuwa wakiona. Ama kwa kujigeuza ndege,







ama kwa kuwatuma ndege, hirizi hii ililetwa hadi katika mikono yangu.”

Babu alipoona kuwa bado sijaridhika na ufafanuzi huo aliamua kuwa wazi zaidi. Alisema kuwa jioni moja alikuwa akiwinda katika mwambao wa mto Malagalasi. Mara akaona kundi kubwa la ndege aina ya hondohondo wakitua hatua chache toka alipokuwa. “Walikuwa wengi. Kama elfu moja hivi. Waliponiona waliruka kunikimbia. Lakini mwenzao mmoja hakuweza kuruka. Alikuwa akipigapiga mabawa kwa nia ya kupaa lakini hakuweza. Nikamsogelea kuona kapatwa na nini. Nikabaini kuwa shingo yake ilikabwa na kamba nyeusi ambayo ilinasa kwenye kichaka cha mti. Nilipomshika ili kumkwamua ile kamba nilishangaa kuona kuwa ilikuwa hirizi ile niliyokupa. Nikaitoa na kumwacha ndege ambaye alipaa kuwaendea wenzake waliokuwa wakihangaika angani kumsubiri.”

Ilikuwa habari ya ajabu kwangu. Hirizi yangu, iliyopotea zaidi ya miaka thelathini iliyopita imerejea mikononi mwangu. Niliipokea, nikaipapasa. Ilikuwa ileile, kwa rangi na uzito. Kwamba imerudi mikononi mwangu halikuwa jambo la ajabu sana, ni namna iliyoifanya irudi ambayo kichwa changu hakikuweza kupokea.

Falsafa nyingi zilipita kichwani mwangu. Kama kweli ilitupwa ziwani bila shaka ingeweza kuoza. Kama hilo halikutokea ni wazi kuwa ilimezwa na samaki ambaye huenda alivuliwa na kuliwa. Kama ilikuwa hivyo hirizi itakuwa ilitupwa kama sehemu ya uchafu wa matumbo ya samaki wanayotayarishwa kwa ajili ya minofu kusafirishwa Ulaya na “mapanki” kuvamiwa na akina baba na mama ntilie. Inawezekana kuwa katika jitihada za kujitafutia chochote ndege yule alijikuta ameivaa hirizi ile na kuisafirisha bila







kujua? Kama ni kweli kwa nini ailete hadi miguuni mwa babu? Katika pitiapitia yangu vitabuni nilikuwa nimesoma mahala tabia za ndege. Moja ya tabia zao za ajabu ni ile ya kuhama au kusafiri safari za mbali kila ifikapo msimu fulani. Mara nyingi ndege hao wanaweza kusafiri safari za mbali toka Marekani au Ulaya hadi Afrika. Inaaminika kuwa wengi uhama katika vipindi vya hali fulani ya hewa na kurudi hali inapotengemaa. Inaaminika pia huko ambako huenda ndiko ambako ndege huzaliana na kurejea likiwa kundi kubwa zaidi. Inawezekana kabisa kuwa hondohondo aliyebeba hirizi yangu alikuwa katika msafara huo. Anaweza kuwa alikuwa akitoka

zake Ulaya au nchi za Kiarabu na kuelekea Afrika Kusini!

Babau alikuwa kama anayeyasoma mawazo yangu. Alikohoa kidogo kabla ya kusema, “Naona na wewe tayari umeambukizwa yale maradhi yenu.”

“Maradhi gani?

“Maradhi ya kisomi. Naona unavyoona shida kuamini kuwa mizimu ya babu wa babu zako imekurejeshea hirizi hii! shauri lako. La msingi ni kwamba hirizi yako imerejea na tangu leo utaivaa tena. safari hii milango yote uliyoshindwa kuifunguwa itafunguka,” alisema akinivisha hirizi hiyo na kisha kunitemea mate kichwani na kifuani.

“Kuna jambo la pili.” Alisema akiinuka tena na kurudi ndani. Aliporejea alikuwa na bahasha tatu mkononi. Alinikadhi. Ilikuwa barua. Juu ziliandikwa jina lake na anuani ya kiji chake. Ilielekea barua hizo zilitoka nje ya nchi, kwani stempu zote zilikuwa na picha ya malkia au wafalme wazungu, muhuri ukiosomeka waziwazi “Stockholm-sweden”. Tarehe kwenye mihuri hiyo zilionyesha kuwa zilitumwa zaidi ya miaka kumi na mitano iliyopita!







“Barua!” Niliropoka.

“Ndiyo,” babu alijibu “Mbona hazijafunguliwa? Ni za zamani sana,” nilisaili.

Babu naye akaonyesha mshangao wake kwangu, “Mjukuu wangu, zinalekea kuwa ni barua muhimu sana. Unadhani ningeweza kumpelekea mtu yeyote asome siri zangu na kuanza kunitangaza? Nilikuwa nakusubiri, nilijua ungerudi salama.”

“Ni wewe peke yako utakayekuwa wa kwanza kuelewa chochote kilichoandikwa humo.”

“Zilifikaje hapa?” Niliuliza nikianza kufungua moja

niliyoiona ya zamani zaidi.

“Zililetwa. DC alileta kwa mkono wakemwenyewe.

Alinishawishi kufungua lakini nilikataa katakata.”

Baada ya maelezo hayo babu alikunjua kiti chake cha uvivu, kilichotengenezwa kwa ngozi ya nyati na kujilaza kimya kwa namna ya kunipa wasaa wa kusoma barua hizo kwa tuo. Barua ya kwanza ilikua ndefu kidogo. Ilianza kwa salamu za siku nyingi, ikaendelea kwa taarifa ya kuipongeza kazi yake alipokuwa nchini humo, “Tumetengeneza filamu mbili za ile michezo uliyoshiriki kuicheza. Filamu hizo zimependwa sana Ulaya nzima zinanunuliwa kama peremende. Taarifa tuliyoichapisha hapa chini ni malipo yako ya mrabaha hadi sasa. Tunaomba ufanye kila uwezalo kuwasiliana nasi ili

upokee malipo yako,” ilieleza barua hiyo.

Sehemu ya pili ya barua hiyo ilikuwa na mahesabu ya idadi ya mikanda iliyouzwa na televisheni zilizonunua hakimiliki na hakishiriki. Kwa hesabu za harakaharaka asilimia ya babu ilionyesha kama dola 227,000. Sikuyaamini macho yangu. Nikainua macho kumtazama. Alikuwa amesinzia, tabasamu likiwa mdomoni.







Nikafungua barua ya pili. Hii iliandikwa mwaka mmoja baadaye. Ilisisitiza, umuhimu wa babu kwenda haraka au kumtuma mrithi wake yeyote anayeaminika. Iliongeza kuwa iwapo kuna tatizo lolote la vitambulisho mwakilishi huyo alichotakiwa ni kwenda na ile hirizi ambayo ilikuwa haibanduki shingoni mwake. “Benki yetu tayari imearifiwa juu ya hilo. Usiwe na wasiwasi,” iliongeza barua hiyo.

Barua ya tatu iliambatanishwa na hundi. Hesabu zilizoandikwa juu ya hundi hiyo zilinitatanisha dola 812,000! Barua ilisisitiza fedha hizo kuchukuliwa. Ikiongeza kuwa benki yao tayari imefungua matawi nchini katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza, haikuwepo haja ya kusafiri hadi Ulaya tena.

Mara nikaanza kupata njozi za mchana. Nilijiona nikiandika kitabu, ambacho kiliyahusu maisha yangu mwenyewe. Niliyaumba na kuyaumbua matukio, mikasa na visa vyote vilivyonikumba toka katika safari zangu kuu mbili safari ya kimaisha iliyonifikisha kila pembe ya nchi na ile ya kimaumbile ambayo ilinitoa utotoni na kuniingiza ukubwani. Nilihisi hata jina la kitabu likinijia akilini; Kiguu na Njia.

Zikanijia njozi nyingine. Katika njozi hizi nilijiona nikiwalekeza watu wa masuala ya filamu wapi pa kuelekeza kamera zao, katika filamu niliyokua nikiitengeneza. Niliwataka ihusishe maeneo yote muhimu ya nchi yetu, mbuga za wanyama, maziwa na mito yote ambayo haikupata kutangazwa vizuri. Kwa njozi niliona mikanda ya filamu hiyo ikigombewa na kuwafanya watazamaji waone hazina kubwa iliyosahauliwa ambayo walijaliwa na Muumba.

Nikaona jinsi nilivyokuwa nikiishi na mke wangu Nashifa kwa furaha. Watoto wetu wawili wenye afya njema







wakicheka na kufurahi…

Halafu nikamkumbuka mwenye fedha zake, ambazo zingeniwezesha kufanikisha ndoto hiyo. Nikageuka.

“Babu!” niliita tena nikimtazama.

Alikuwa bado amelala vilevile kwenye kiti chake cha uvivu. Tabasamu lake lilikuwa bado limesahauliwa palepale usoni kama mtu aliyekuwa katika dimbwi la starehe. Niliinuka na kumshika bega. Nikamtikisa taratibu, baadaye kwa nguvu kidogo, “Babu… babu… babu…!

Kimya! Kimya!

Nikashtuka. Alikuwa kama hapumui! Nikamshika kifua kusikiliza mapigo ya moyo. Hayakuwepo. Hata mwili wake tayari ulikuwa umepoa. Ndio kwanza nikabaini kuwa babu hatukuwa naye tena duniani! Tabasamu lake lililobakia palepale kama ishara ya ushindi kwa jambo zito lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.

Nilitetemeka mwili mzima. Nguvu zikaniishia, furaha, faraja na matumaini makubwa niliyoyapata mara baada ya kuisoma barua yake, ikatumbukia nyongo.

MWISHO






BURE SERIES
 
Daaa sina kumbukumbu kama nilishawah kuisoma riwaya tam kama hii!!

Yaan na"kielimu changu cha shule!!!!
Kwenye hichi kitabu!! Nimeongeza Elimu kubwa mnooo!!!

Na Nimezifaham tamadun nyingi mnooo!!!!! Na Mazingira yake!!!


BEN R MTOBWA......SALUTE.......
 
SHUKRANI ZA DHATI KWA WEWE TULIYEKUWA PAMOJA TOKA MWANZO HADI MWISHO

ENDELEA KUFURAHIA SIMULIZI NYINGE ZINAZORUSHWA NA

PSEUDEPIGRAPHAS
Lakin mkuu!! Nimetembelea kweny acc yake huyu jamaa!! Sijakiona hichi kitabu..

Kuanzia jukwaa zote kama za kijasusi /maisha/kusisimua ama ameiweka sehem gan!!??


Lakin Tunashukulu sana kwa ulivojitoa mkuu!!!![emoji120]
 
KONGOLE. KONGOLE.. KONGOLE... kwako mkuu. Nimekuwa nikiifuatilia riwaya hii kimyakimya tangu mwanzo.

Nikiri tu kuwa hakika BEN .R. MTOBWA ni jabali wa fasihi. Utafiti wa kina, ufundi na uhunzi wa maandishi uliotumika humu umenifanya niduwae. Kinywa wazi!

Sijapatapo kusoma maandishi adhwimu namna hii. Humu nimecheka, nikakasirika, nikahuzunika, nikafarijika na kupata hisia kadha wa kadha.

Basi itoshe kusema kuwa Fasihi ilizaliwa ndani ya BEN ikastawi ndani yake na kuchanua kila kona ya Tanzania kwa waraibu wa fasihi hasa andishi.

Huko uliko amani ya bwana ikuangazie BEN .R. MTOBWA[emoji120]
 
SHUKRANI ZA DHATI KWA WEWE TULIYEKUWA PAMOJA TOKA MWANZO HADI MWISHO

ENDELEA KUFURAHIA SIMULIZI NYINGE ZINAZORUSHWA NA

PSEUDEPIGRAPHAS
Shukrani kwako pia mkuu. Mungu akubariki kwa kujitoa kutuletea riwaya bora kutoka kwa mwandishi bora wa muda wote[emoji120]

Ukipata wasaa ningeomba utuletee riwaya ya msalaba wa shetani/dhahabu kutoka kwa kigongo mwengine wa fasihi andishi, Alwatan BEKA MFAUME.
 
Daaa sina kumbukumbu kama nilishawah kuisoma riwaya tam kama hii!!

Yaan na"kielimu changu cha shule!!!!
Kwenye hichi kitabu!! Nimeongeza Elimu kubwa mnooo!!!

Na Nimezifaham tamadun nyingi mnooo!!!!! Na Mazingira yake!!!


BEN R MTOBWA......SALUTE.......
Great appreciation 🙏🙏
 
Lakin mkuu!! Nimetembelea kweny acc yake huyu jamaa!! Sijakiona hichi kitabu..

Kuanzia jukwaa zote kama za kijasusi /maisha/kusisimua ama ameiweka sehem gan!!??


Lakin Tunashukulu sana kwa ulivojitoa mkuu!!!![emoji120]
Soon utakiona mkuu, katika ukurasa wa Kijasusi, kuna list ya vitabu tunakamilisha kuviweka sawa, kisha tutaanza kuupdate blog
 
KONGOLE. KONGOLE.. KONGOLE... kwako mkuu. Nimekuwa nikiifuatilia riwaya hii kimyakimya tangu mwanzo.

Nikiri tu kuwa hakika BEN .R. MTOBWA ni jabali wa fasihi. Utafiti wa kina, ufundi na uhunzi wa maandishi uliotumika humu umenifanya niduwae. Kinywa wazi!

Sijapatapo kusoma maandishi adhwimu namna hii. Humu nimecheka, nikakasirika, nikahuzunika, nikafarijika na kupata hisia kadha wa kadha.

Basi itoshe kusema kuwa Fasihi ilizaliwa ndani ya BEN ikastawi ndani yake na kuchanua kila kona ya Tanzania kwa waraibu wa fasihi hasa andishi.

Huko uliko amani ya bwana ikuangazie BEN .R. MTOBWA[emoji120]
Amina mkuu, asante kwa kuweka alama yako, asante kwa kuifuatilia riwaya hii
 
Shukrani kwako pia mkuu. Mungu akubariki kwa kujitoa kutuletea riwaya bora kutoka kwa mwandishi bora wa muda wote[emoji120]

Ukipata wasaa ningeomba utuletee riwaya ya msalaba wa shetani/dhahabu kutoka kwa kigongo mwengine wa fasihi andishi, Alwatan BEKA MFAUME.
AMEN..... Sawa mkuu !! Nitavitafuta
 
Duuuh toka nimeanza kuisoma hadithi hii haichoshi nitatoa maoni yangu nikiimaliza hongera sana kwa mtunzi
 
Back
Top Bottom