Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi : MIKONONI MWA NUNDA
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
UKEKE Maulana alikuwa mzee ambaye siku zote alipingana na uzee, mzee ambaye hakukubali uzee umtawale hata mara moja. Alikuwa vitani akiupinga na kuudhihaki hadi uzee ukaelekea kumpigia magoti. Kama si kwa ajili ya mvi chache ambazo zilikataa kuitii kanta, hata wewe ungemwondoa katika orodha ya wazee na kumwita kijana. Kumwita hivyo kungekufanya akupende, na watu wote wamjuao wasingekulaumu. Wangekulaumu vipi wakati hata chembe moja ya ndevu haikuthubutu kujitokeza katika kidevu chake?
Wakati mavazi yake yalikuwa yale ya vijana? Wakati mienendo yake yote ilikuwa katika kumbi na vipenyo vilevile ambavyo vijana walipenda kupita? Si hayo tu, zaidi ni jinsi alivyokuwa akienda sehemu hizo, dansini, baa, sinema na kokote; akiwa amefuatana na msichana mwenye umri ambao haukuwa mbali na wajukuu zake. Naam, Ukeke alikuwa Ukeke.
Sifa zake hizo zilitajwa na zilizosahauliwa, ziliwafanya watu watundu waanze kumwita majina kadha wa kadha. Mara “Mzee kijana,” mara “Kizito”, ama “Mwenyewe” pamoja na yote waliyodhani yangemfaa. Yote hayo yalimpendeza Ukeke. Lakini hakuna lililomfaa zaidi ya “Ukeke.” Hivyo, Ukeke akabaki Ukeke na kuendelea kuwa Ukeke.
Alichukia jinsi uzee ulivyotishia kumpokonya nafasi yake ya kustarehe. Na aliupenda na kuung’ang’ania ujana kwa ajili ya ile ahadi ya kuwa huru katika harakati za anasa na starehe, anasa ambazo zilimjaza furaha na hamu ya maisha. Hiyo ndiyo sababu iliyomfanya augande ujana akifurahi na kustarehe pamoja na vijana.
Starehe aliipata kama alivyopenda. Fedha haikuwa kipingamizi. Alikuwa na kazi yenye cheo katika moja ya kampuni za umma, kazi ambayo, licha ya kumlipa vizuri, ilikuwa nafasi nyingine iliyomwezesha kujipatia chochote nje ya mshahara, kwa njia moja au nyingine. Hivyo, starehe zake hazikupotoshwa na aina yoyote ya kipingamizi cha fedha au “watoto watakula nini.” Bali alistarehe alivyopenda; huku kaandamana na binti yeyote aliyempenda.
Hata hivyo, jioni hii aliiona “mbovu.” Kama kawaida, tatizo halikuwa pesa. Hizo alikuwa nazo. Tatizo lilikuwa ampate nani wa kula naye pesa hizo. Aliwapigia simu wasichana wote aliodhani wangestarehe naye jioni hii, hakufanikiwa. Kila mmoja alitoa udhuru ambao haukuweza kupingika.