SEHEMU YA 321.
Roma alishindwa kuelewa ni kipi ambacho mama yake alikuwa akipitia, ukweli tokea alivyorudi Japani hakukaa chini na kuongea na mama yake na Roma alielewa siku zote mama yake ni mwenye maswali mengi kuhusu yeye , lakini kutokana na sababu za kutotaka kukumbuka mambo yaliopita , hakutaka kabisa kuelezea historia iliokuwa nyuma ya Maisha yake , kwani aliona hakuna faida yoyote ya kuelezea.
Kitendo cha mama yake kusema asante , lakini wakati huo huo akiwa ni mwenye kutoa machozi ukweli ni kwamba hakukipenda kabisa , hakupenda kumuona mama yake anatoa machozi mbele yake kwani ilimfanya kujiona sio mwenye kumjali.
“Mama nilishasema sitaki kuona ukitoa machozi mbele yangu , unanifanya nijihisi mwenye hatia na sitimizi wajibu wangu kama mtoto”
“Hapana Roma Mwanangu usijihisi ni mwenye hatia kabisa , machozi haya ni kutokana na furaha niliokuwa nayo juu ya uwepo wako kwa mara nyingine kwenye Maisha yangu , umekuwa muujiza mkubwa sana ambao Mungu amenitendea”Aliongea Blandina na kumfanya Roma kutabasamu huku akimwangalia mama yake machoni.
“Mama niambie kama kuna kitu ambacho kinakusibu , sio mimi tu ambaye nakuona haupo sawa bali familia yote inakuona haupo sawa”Aliongea Roma na Blandina alifuta machozi kwa mkono wake wa kulia na kisha kuyaangalia maji ya bwawa la kuogelea , akiwa ni mtu ambaye anaonekana kufikiria.
Blandina alikuwa akijiuliza mara mbili mbili je amwambie Roma kwa kile kilichotokea jana yake kituoni au akae kimya , ukweli hata kuja kukaa hapo nje peke yake ilikuwa ni katika hali ya kutafakari , hakuwa tayari kukaa mbali tena na Roma , lakini pia hakuwa tayari kuona wale Watoto wanateseka tena kwasababu yake , aliamini kazi alioifanya katika ujenzi wa vituo vya kulelea Yatima ndani ya mataifa Zaidi ya ishirini, ndio sababu ambayo imemfanya hata Mungu kumuweka hai Roma na kumrudisha tena kwenye Maisha yake.
“Roma..!!!”
“Naam Mama nipo Hapa na kusikiliza”
“Ni kweli mwanangu kuna jambo ambalo linanisumbua , ila kwasasa siwezi kukuambia nahitaji muda wa kufikiria Zaidi”Aliongea Blandina.
“Mama kama unahitaji muda wa kufikiria mimi sina tatizo , lakini nataka uniahidi kitu kimoja mama yangu”Aliongea Roma na Blandina alitingisha kichwa.
“Niahidi utaniambia kwa kile kinachokusibu baada ya kufikiria”Aliongea Roma na Blandina alitabasamu kivivu na kumshika mkono Roma.
“Usiwe na wasiwasi nitakuelezea kila kitu”
“Sawa mama , lakini unavyokuwa hivi sisi wanafamilia ambao tunakujali tunakuwa na wasiwasi naomba upunguze mawazo.”.
“Nilitoka kwa ajili ya kupunga upepo nikipata muda wa kufikiria ,twende ndani chakula cha usiku kitakuwa tayari”Aliongea Blandina huku akinyanyuka wa kwanza , licha ya Roma kuona mama yake anakwepa kumwambia kile kinachomsibu lakini aliamini kuna tatizo ambalo linamfanya mama yake kuwa katika hali aliokuwa nayo.
“Mama kesho napanga kusafiri Kwenda mkoani”Aliongea Roma na kumfanya Blandina kumgeukia.
“Unaenda mkoa gani na kwenye shughuli gani?”Aliuliza na kumfanya Roma ashindwe hata kujua namna ya kujibu , kwani alijikuta akikosa ule ujasiri wa kutamka moja kwa moja kwamba alikuwa akimpeleka mchepuko wake nyumbani kwao.
“Nampeleka Nasra nyumbani kwao”
“Nasra…,! ,Ni mkwe wangu mwingine?”Roma aliitikia kwa kichwa akijibu ndio na Blandina alijikuta akivuta pumzi.
“Edna mkeo anafahamu hili?”
“Anajua mama nishamueleza ila sijamuaga kwa ajili ya safari”Aliongea Roma na Blandina alikosa usemi kwani alishindwa kumuelewa kabisa mtoto wake na kushindwa kuelewa mwisho wa hao wanawake ambao Roma anao ,kwanza kabisa aliweza kujua hata Japani alienda kwa ajili ya mwanamke, yaani Blandina mwanzoni alikuwa akijua Roma alikuwa akitoka nje ya ndoa na mwanamke mmoja , lakini kadri alivyokuwa hapo ndani aligundua Roma anao wanawake wengi Zaidi na kushindwa hata kuamua cha kufanya.
“Roma sitaki kukuingilia kwenye mahusiano yako kwani naamini unajua unachokifanya ,lakini ninachoweza kukushauri kama mama yako ni kuzingatia pia hisia za mke wako kwako , najua kuna kitu kati yako na Edna kinaendelea naamini utakifanyia kazi”Aliongea mama yake Roma na kisha aliongoza njia Kwenda ndani.
“Asubuhi nitaelekea HongKong”Aliongea Edna wakati wanafamilia wote wakiwa mezani wakipata chakula cha usiku na Roma ndio aliekuwa wa kwanza kumwangalia mke wake kama mtu mwenye swali la mbona ghafla sana.
“Safari ya kibiashara?”Aliuliza Roma na Edna alitingisha kichwa Roma alionekana kufikiria kidogo , lakini aliona aendeelee kula kwani alijua mke wake ni mfanyabiashara na safari za ghfla zaaina hio mara nyingi haziepukiki.
Asubuhi Roma alimsindikiza Edna mpaka uwanja wa ndege, kwenye gari hakukua na mazungumzo mengi ,kwani Edna alikuwa na ukauzu wa hali ya juu na ni kama hakuwa akitaka kuongea na Roma kabisa.
Ukweli ni kwamba Edna hakupendezwa kabisa na Roma Kwenda nyumbani kwa Nasra, alijihisi ni kama mtu ambaye alikosewa na ndio maana alianzisha vita baridi na Roma.
“Safari njema mke wangu kipenzi”
“Na wewe safari njema ya ukweni , nakuombea upokelewe”Aliongea Edna bila ya kuwa na tabasamu wala huzuni kwenye sura yake.
“Madam Boss!!!” Ilisika sauti upande wa nyuma baada ya Roma kumaliza kuagana na Edna, Roma ndio aliekuwa wa kwanza kugeuka mara baada ya kusikia sauti ya mwanaume.
Alikuwa ni mwanaume kijana rika lake ,alievalia vazi la suti ambalo limemkaa vyema sana mwilini , alionekana kupendeza kweli ukijumlisha pia na muonekano wake wa kihendsome.
Alikuwa ni Alhaji CEO ya kampuni ya Maple Group , kampuni inayomilikiwa na mwanamama Neema Luwazo.
“Alhaji kutana na Roma Ramoni Director wa kampuni yangu mpya ya Vexto Media, Roma huyu ni Alhaji Shekilindi ni CEO kampuni ya Maple Group”Aliongea Edna akimtambulisha Roma kwa Alhaji.
Roma hakuwahi kumuona Alhaji kwanza siku zote alikuwa akifahamu Neema Luwazo ndio aliekuwa CEO wa kampuni ya Maple ila imegeuka kumbe kuna CEO kijana mdogo kabisa ambaye anaongoza makampuni hayo makubwa nchini.
“Nimefurahi sana kukufahamu Mr Roma”Aliongea Alhaji kwa bashasha na kumpatia mkono Roma na hakuwa na sababu ya kuukataa mkono ule, ila Roma macho yake yote yalikuwa kwa mke wake.
Edna alikuwa amependeza haswa , licha ya kuvaa mavazi ya suti , lakini alionekana kuwa mrembo na hata Alhaji alipendezwa mno na uzuri wa CEO Edna, na sio kwake tu , kwa wanaume wote waliokuwa maeneo hayo walimwangalia Edna kwa uchu wa matamanio ya kufanya nae mapenzi.
“Alhaji utatangulia nakuja”Aliongea Edna mara baada ya kuona macho ya Roma yalivyokuwa yanamwangalia na Alhaji aliitikia kwa kichwa na aliondoka akiwaacha Roma na Edna.
“Roma wale wazungu wako si bado wapo , nina wasiwasi na ulinzi pale nyumbani licha ya kuingia mkataba na kampuni ya SinganoJr Security”
“Huna haja ya kuhofia kuhusu ulinzi nyumbani, wasiwasi wangu ni usalama wako Zaidi”
“Kama unahofia usalama wangu acha kumsindikiza Nasra na nisindikize Kwenda Hongkong”Aliongea Edna huku akimwangalia Roma usoni.
“Safari yako ni ya ghafla mke wangu na siwezi kuacha kutimiza ahadi niliowekeana na Nasra”
“Basi haina haja ya kuhofia usalama wangu , unaweza kuwazia usalama wa wanawake wako wengine , ninaweza kujilinda mwenyewe”Aliongea Edna na kugeuka kuondoka ila Roma alimpita kwa mbele na kusimama.
“Nieleze angalau unachoenda kufanya Hongkong”Aliongea Rpm ana Edna alivuta pumzi kidogo.
“Kampuni ya Aba Group kutoka Hongkong wanadai Yamakuza wameiba teknolojia(Intellectual Theft) inayohusiana na malighafi mpya ambazo tunatarajia kuzindua mwezi wa kumi na mbili na wamefungua madai kwenye ‘International Court of arbitration’ kuzuia uzinduzi wa hizo malighafi, kama umeangalia jana hisa za kampuni ya Vexto ziliporomoka thamani , chanzo ni hii kampuni ya Aba kufungua kesi , kampuni ya Luis Vuitton na kampuni nyingine ambazo wameweka oda za kuhitaji malighafi hizi wanataka kuvunja mkataba na sisi ndio maana napaswa Kwenda mwenyewe Hongkong kuangalia namna ya kutatua hili swala Pamoja na kampuni ya Maple , mwanasheria wetu Nadia alikwisha kutangulia tokea jana”.Aliongea Edna na kumfanya Roma kushangaa kidogo, ukweli swala hilo hakujua na hata hizo hisa za kampuni ya Vexto hakuwa na taarifa juu ya kushuka kwake, kitu kingine ambacho kilimfanya Roma kumkubali Edna ni kutokana na mwonekano wake , licha ya kwamba kampuni ilikuwa kwenye shida lakini alionekana kuwa na utulivu wa hali ya juu ni kama mtu mwenye uhakika wa kushinda.
“Mke wangu nimekukubali , licha ya kwamba kuna tatizo mbele yako lakini unaonekana kuwa sawa”
“Mambo kama haya yanatokea sana kwenye biashara na kama siku zote yakitokea utaanza kupatwa na mawazo utaishia kufa na magonjwa ya mshituko”Aliongea Edna.
“Kwahio utachukua siku ngapi HongKong?”
“Mpaka tufikie muafaka juu ya hili swala , kuna kitu nahisi kipo katikati na tunapaswa kukifahamu”Aliongea Edna na kisha aliangalia saa.
“Kwaheli muda wa kuwasili ushawadia , hakikisha nilichokuambia juu ya usalama pale nyumbani , sitaki Lanlan apatwe na shida yoyote”Aliongea Edna na Roma alitabasamu na kumsogelea Edna na kumkumbatia.
“Popote uendapo mke wangu upo salama , nadhani unakumbuka maneno ya Christine mumeo mimi ni mfalame hivyo na wewe ni Malkia, ukifika Hongkong Airport kuna mtu atakupokea”Aliongea Roma akiwa amemkumbatia Edna na kisha akamwachia, Edna baada ya kuachiwa macho yalianza kukagua eneo hilo na kuangalia usalama.
“Kulikuwa na ulazima wa kunikumbatia hadharani, si ungeniambia tu kwa mdomo”Aliongea Edna huku akishikilia mkoba wake vizuiri, lakini Roma hata hakujali aligeuka.
“Nenda mke wangu muda umewadia”Aliongea Roma na Edna aliangalia saa na kuona kweli muda umesogea , aligeuka na kuondoka.
Dakika kadhaa Roma alisimamisha gari yake aina ya Range Rover Sport kwenye makazi anayoishi Nasra , asubuhi hio hakutaka kabisa kurudi tena nyumbani kwani alishakwisha kuaga kabisa na alikuwa na mpango wa kuunganisha moja kwa moja kuanza safari kuelekea mkoani Tanga anakozaliwa mrembo Nasra.
Roma baada ya kusimamisha gari alitoa simu yake na kutafuta namba flani kwenye simu na kuipiga.
“Hades kama nilivyokuwa nikitegemea , hatimae umenipigia” ilisikika sauti upande wa pili kwa lugha ya kingereza.
“Kama unajua ninachokutafutia basi naamini pia unayo njia ya kutatua tatizo lililojitokeza”
“Unabahati kubwa san kwasababu nipo Hongkong mpaka sasa hivi Hades”
“Okey Edward mke wangu anakuja Hongkong kwa swala ambalo unalifahamu nataka umpatie msaada kwa kadri inavyowezekana ili swala lake liishe mapema”
“Hades kuhusu hilo ondoa shaka kama Madam Persephone atafikia makubaliano na sisi basi sina haja ya kuacha kumsaidia, nina hamu kubwa ya kukutana nae”
“Naelewa familia ya Rothchild kila sehemu mnataka kuweka mikono yenu, ushirikiano niliokuwa nao Pamoja na familia yenu kiungo natakiwa kuwa mimi na sio mke wangu , hivyo fanya juu chini kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa”Aliongea Roma na sauti upande wa pili ilikaa kimya kidogo.
“Okey! Hades nitaangalia namna ya kumsaidia Madam Persephone ili niwe upande mzuri na yeye”Aliongea na Roma alikata simu na alitafuta namba ya Tanya kiongozi wa kundi la Yamata Sect na kuandika ujumbe mfupi wa maandishi na baada ya kumaliza alifunga mlago wa gari na kuanza kupiga hatua kuingia ndani ya jengo hili la Apartment analoishi mrembo Nasra.
SEHEMU YA 322
Ni saa tatu asubuhi Roma na Nasra walionekana wakiwa kwenye barabara ya Bagamoyo Road wakipita Bagamoyo mjini kuelekea Msata.
Nasra alikuwa amevaa mavazi ya kidini kabisa siku hio alikuwa amependeza haswa na kuonekana mrembo Zaidi , kwa jinsi ambavyo alikuwa akionekana ilionyesha ni dhaihiri kabisa alikuwa akiendelea nyumbani.
Muda wote alionekana kucheka cheka , hakuamini kama alikuwa akielekea na mwanaume anaempenda nyumbani kwao , aliamini mama yake ambaye ana miaka mingi pasipo kuonana nae anakwenda kufurahi mno.
“Edna alishaondoka Kwenda Hongkong?”Aliuliza Nasra huku akionekana kutafuna karanga zilizokuwa kwenye kijimfuko.
“Babe Nasra unaonekana kuwa msahaulifu , umesahau nilikuwambia nimetoka Airport”Aliongea Roma na kumfanya Nasra kuachama.
“Ooh !, nilisahau”Aliongea Nasra na kumfanya Roma kutabasamu.
“Umefanya kazi ndani ya kampuni ya Edna kwa miaka mingapi ?”Aliuliza Roma.
“Toke animalize masomo, mwaka mmoja kabla ya Edna kuwa CEO”Aliongea Nasra na Roma kutingisha kichwa.
“Unaonekana unabahati sana , kufanya kazi kwenye kampuni kubwa kama Vexto ni bahati ambayo sio kila mtu anaweza kuwa nayo”
“Unachoongea ni sahihi , huenda nisingefahamiana na Mama yake Edna nisingefika nilipofikia mafanikio niliokuwa nayo leo hii yote ni kutokana na msaada mkubwa niliopata kutoka kwa familia ya Edna, nina deni kubwa sana kwao”
“Ulifahamiana vipi na mama yake Edna?”
“Ni Stori ndefu mno na ya kuumiza”Aliongea Nasra na kumfanya Roma kujawa na shauku ya kutaka kujua Zaidi.
******
Nasra Kihedu ndio jina kamili la Nasra , ni mzaliwa kutoka mkoani Tanga wilaya ya Lushoto halmashauri ya Bumbuli Kijiji cha Mponde.
Mama yake Nasra kabla ya kuolewa na Mzee Kihedu alikuwa tayari amekwisha kumzaa tayari Nasra na mwanaume ambaye inasemekana alimkimbia baada ya kupata ujauzito.
Mzee Kihedu licha ya kwmaba alimpenda sana mama yake Nasra , lakini hakumpenda kabisa mtoto wa Mwajuma(Mama Nasra) na hili lilipelekea Maisha ya Nasra na baba yake wa kambo kuwa magumu mno.
Kwani Nasra tokea akiwa mdogo aliishi kwa kunyanyasika sana , kwani mzee kihedu alikuwa akimpiga sana na kutomjali kabisa na hio ni kutokana na kwamba hakuwa mtoto wake wa damu , lakini jambo lingine ambalo lilimfanya mzee huyu kumnyanyasa Nasra ni kutokana na kutojaliwa mtoto na Mwajuma mke wake.
Sasa manyanyaso aliokuwa akipata Nasra ndio yalimpelekea kutoroka nyumbani kwao Tanga na kuja jijini Dara mara tu baada ya kumaliza darasa la saba, Nasra aliweza kuja Dar es salaam kwa msaada wa mtoto wa nyumba ya Jirani ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani jijini Dar es salaam.
Moja ya sababu kubwa abayo ilimfanya Nasra kutoroka ni mara baada ya Mzee Kihedu kumtafutia Nasra mchumba wa kuolewa nae mara baada tu ya kumaliza masomo yake ya darasa la saba , jambo ambalo Nasra hakulipenda kwani ndoto yake kubwa ilikuwa ni kusoma na kuwa mwanamke mwenye mafanikio.
Nasra alikuwa tofauti sana na mabinti wengi waliokuwa ndani ya kijiji chao, Kwani Nasra alikuwa amejaliwa akili nyingi sana , licha ya kwamba aliishi kwa manyanyaso mengi kutoka kwa baba yake wa kambo , lakini pia hali ya umasikini iliokithiri lakini changamoto hizo hazikumzuia kutokufanya vizuri kimasomo , wala kukata tamaa juu ya ndoto zake..
Nasra alikuwa na uwezo wa kutofika shule wiki nzima akishinda kwenye kibarua cha kuchuma majani ya chai yeye na mama yake kwenye mashamba ya watu , lakini atakaporudi kutoka kwenye kazi hio lazima aulizie kile wenzake walichofundishwa shuleni , kutokana na juhudi alizokuwa nazo Nasra katika masomo mama yake mwajuma alimsapoti mtoto wake kwa uwezo wake wote licha ya Maisha kuwa magumu.
Sasa Nasra aliona ndoto zake za Kwenda sekondari zinafifia mara baada ya baba yake Mzee Kihedu kupokea Kondoo wawili wa mahali kutoka kwa familia ya Mzee Shabani ,MzeeShabani licha ya kwamba umri wake ulikuwa umeenda lakini alitaka kumuona Nasra kama mke wake watatu , jambo ambalo mama yake Nasra Pamoja na Nasra walipinga vikali , lakini kelele zao zilikuwa kama za kuku Kwenda kwa mwewe, kwani Mzee kihedu hakutaka kabisa kusikiliza , kwanza kabisa alimpiga sana mke wake Mwajuma kwa kiwango kikubwa akimlazimisha akubaliane na matakwa yake ya kukubali Nasra aolewe , na Mwajuma baada ya kuona kipigo kutoka kwa mume wake ni kikali ndipo alipokubaliana na mume wake kumuozesha Nasra kwa Mzee Shabani , sasa kitendo cha mama Nasra kukubaliana na Baba yake, kilimfanya Nasra kutafuta namna ya kujiokoa kwenye adha ya kuolewa na Mzee Shabani , hapo ndipo alipokimbilia jijini Dar na rafiki yake mtoto wa Jirani yao anaefahamika kwa jina la Tabu.
Malengo ya Nasra ilikuwa ni kuja Dara kutafuta hela ili aende shule, lakini hali ilibadilika mara baada ya kufika Dara kwani yule Tabu aliekuja nae kwanza kabisa hakuwa akifanya kazi za ndani , alikuwa akifanya kazi za kujiuza maarufu kama uchangudoa, na alimshawishi Nasra kuja nae Dar kwa kumdanganya anakuja kufanya kazi za ndani , bali kwenye kichwa chake alikuwa akidhamiria kumuingiza Nasra kwenye biashara za kujiuza kama yeye na hio yote ni kutokana na uzuri aliojaliwa Nasra, aliamini Nasra ni rahisi kupata soko kuliko hata yeye.
Sasa baada ya wiki kama tatu kupita ya Nasra kuishi na Tabu maeneo ya Mbagala ,Tabu ndipo alipoanza kumlazmisha kujiunga na na kazi yake hio kuuza mwili, jambo ambalo N?asra alipinga vikali mno na kukataa kata kata, na hapo ndipo ulipotokea ugomvi kati ya Tabu na Nasra na kupelekea kufukuzwa kwenye chumba cha Tabu.
Nasra baada ya kufukuzwa usiku usiku ndipo alipokuja kupata msaada kutoka kwa mwanadada Najma na hapo ndipo urafiki kati ya Najma na Nasra ulivyoanza.Kipindi ambacho Nasra anakutana na Najma ni kipindi ambacho Najma alikuwa na mwaka mmoja tu tokea wazazi wake kufariki , kipindi hiko na Najma alikuwa amemaliza darasa la saba na alikuwa akisubiria matokeo.
“Nasra angalia hiki kipeperushi, tulipewaga siku ya mahafali yetu nimekikumbuka leo”Aliongea Najma siku moja usiku kabla ya kulala , hio ni siku kadhaa tokea Nasra kuanza kuishi na Najma.
Sasa Najma alikuwa amehifadhi kipeperushi hiko kwenye mkoba wake wa shule na alisahau kwa muda mpaka usiku huo alipokumbuka kwamba anakipeperushi hiko ambacho alipewa shuleni kwao Nzasa siku ya mahalafi yao ya kumaliza darasa la saba.
Nasra aliangalia kile kipeperushi kwa kukisoma na alijikuta akitabasamu na tumaini lake la kurudi shule kuchipua upya.
Kipeperushi kile kilikuwa kimegawiwa kwa wanafunzi wa Nzasa , kilikuwa ni kipeperushi ambacho kilikuwa kikihusiana na shule ya sekondari ya Son and Daughter iliokuwa Kiwangwa , shule hio ilikuwa ikitangaza ufadhili kwa baadhi ya wanafunzi , kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kwa wale wanaokidhi vigezo.
Licha ya kwamba kulikuwa na vigezo juu ya ufadhili hio , lakini Nasra aliamini hio ni fursa kwake ya kutimiza ndoto zake na wiki mbili mbele ndipo alipofanya safari ya Kwenda Kiwangwa.
Na bahati nzuri kwake ni mara baada ya kukutana na Mama Issa mkuu wa kituo cha Son And Daughter , mama Issa alimkubali Nasra mara baada ya kujua alikuwa akitokea sehemu moja , Mama Issa alikuw ani mwenyeweji pia wa mkoa wa Tanga wilaya ya Lushoto , hivyo ilikuwa rahishi kwa Nasra kuweza kupata ufadhili ndani ya shule hio baada ya kusikilizwa stori yake ambayo ilihuzunisha wengi , lakini pia **** Nasra sifa ya kuwa msichana jasiri.
Uwezo wa Nasra kimasomo ndio ulioweza kumkutanisha na Raheli mama yake Edna.
Nasra baada ya kumaliza kidato cha nne alifaulu kwa ufalu mkubwa na aliendelea na masomo ya kidato cha cha tano ndani ya shule hio hio iliokuwa ndani ya kituo hiko cha kulelea Watoto Yatima, Nasra kutokana na historia yake ya kimaisha alikuwa akiishi hapo hapo kituoni na hata kipindi cha likizo kama atatoka kusalimia basi mara nyingi alikuwa akienda kusalimiana na rafiki yake Najma na walikuja kuachana na rafiki yake huyo mara baada ya Najma Kwenda chuo cha ualimu Korogwe baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari.
Nasra baada ya kumaliza masomo ya kidato cha sita ndipo alipofadhiliwa na familia ya Edna na Kwenda kusomea Uhasibu nchini Marekani katika chuo cha Cambridge kilichokuwepo huko Boston.
Siku Nasra anapata ufadhili huo alijikuta akilia usiku mzima , hakua akiamini kama anakwenda kusomea kwenye nchi kubwa kama ya Marekani , shukrani zake zote zilienda kwa familia ya Raheli ambayo ndio walikuwa wafadhili wa masomo yake kuanzia kidato cha kwanza mpaka ngazi ya chuo, sharti pekee la mkataba wa ufadhili ni kufanya kazi ndani ya kampuni ya Vexto mara tu baada ya kumaliza masomo yake.Hivyo wakati Nasra akiwa masomoni Marekani upande wa Edna yeye alikuwa masomoni Uingereza.
Sasa tokea Nasra aanze masomo yake yote kuanzia kidato cha kwanza mpaka anafikia chuo kikuu hakuwahi kurudi tena kijijini kwao Zaidi ya kuwasiliana na mama yake mzazi kwa njia ya simu pekee.
Sasa hatimae siku ambayo Nasra kwa mara ya kwanza anarudi kijijini kwao baada ya miaka mingi tokea kuondoka anarudi na Roma Ramoni mwanaume anaempenda.
******
Roma alishangazwa na historia hio ya Nasra , lakini akimkubali Nasra kwa wakati mmoja kwani ujasili aliouonyesha wa kupigania ndoto zake , hatimae umemfanya kuwa mtu mkubwa sana ndani ya kampuni kubwa kama ya Vexto, kama agekubaliana na Maisha ya kukaa kijijini na kuolewa na Mzee Shabani asingefikia hatua aliofikia.
“Babe Nasra tukifika unaonaje tukamsalimie Mzee Shabani”Aliongea Roma na kumfanya Nasra kucheka.
Kwasababu usafiri ulikuwa ni wa binafsi , haikuwachukua muda mrefu kufika Soni wilayani Lushoto na kwa maelekezo ya Nasra , Roma aliichukua barabara nyingine inayoelekea kijijini wakiacha barabara kuu inayoenda Lushoto mjini.
Roma alipenda sana mazingira yalivyo kwani kulikua na ukijani usiokuwa wa kwaida, njia ambayo walikuwa wakiitumia ilikuwa ni ya msituni na haikuwa nzuri sana , hivyo Romma alijaribu kuendesha gari kwa umakini , na kilichosaidia tu ni kwamba walikuwa wakiendesha gari aina ya Range ambalo halipati shida sana kwenye kutembea kwenye barabara hio yenye mashimo mengi.
Sasa baada ya Roma kupita Kijiji kimoja kinachofamika kwa jina la Tonga , kwa maelezo ya Nasra ,waliingia msituni na hapo ndipo mvua ilipoanza kunyesha mfululizo , sasa Roma ile anakaribia katikati ya msitu mara alikanyaga breki na kusiimamisha gari mara baada ya kuona mwanamke aliekuwa amekaa barabarani katikati akiwa ananyeshewa na Mvua.Mwanamke ambaye alikuwa katikati ya barabarani alikuwa amekaa staili flani kama mwanamke ambaye anafanya meditation(Tahajudi).
Nasra alimwangalia Roma kwa wasiwasi na Roma yeye hakuwa na wasiwasi Zaidi ya kumwangalia mwanamke aliekuwa mbele ya barabara , Roma alipiga honi kwa Zaidi ya mara tatu , lakini mwanamke yule hakufumbua macho kwani alikuwa ameyafumba huku akiwa ameunganisha viganya vyake usawa wa kifua , alionekana kama alikuwa anasali.
SEHEMU YA 323
“Atakuwa ni nani?”Aliuliza Nasra kwa hofu mno.
“Ngoja nitajua”Aliongea Roma huku akifungua mkanda wa gari na kufungua mlango.
“Roma usiende inawezekana kuwa ni kiumbe kibaya na kinaweza kutuzuru”Aliongea Nasra akimshika mkono Roma.
“Babe Nasra usiwe na wasiwasi , hakuna kiumbe ambacho kinauwezo wa kunizuru”Aliongea Roma na kushuka , huku akiacha kujali mvua iliokuwa ikinyesha.
Roma bila ya wasiwasi alisogea mpaka alipoketi yule mwanamke na kuanza kumchunguza, na Roma alijikuta akihusudu uzuri wa mwanamke aliekuwa mbele yake .
“Hey!”Aliita Roma ,lakini mwanamke yule wala hakushituka kabisa alikaa vile vile huku midomo yake ikionekana kucheza cheza , alikuwa ni kama anasali.
“Hatimae umefika”Yule mwanamke alimaliza alichokuwa akikifanya na kumwangalia Roma aliekuwa akinyeshewa na mvua na aliongea kwa Kiswahili kizuri tu cha kueleweka , lakini alimshangaza Roma kwa maneno yake.
“Mbona unanishangaa Hades nilikuwa nikikusubiria licha ya kunyeshewa na mvua”Aliongea yule mwanamke huku akimwangalia Roma usoni na kuanza kumzunguka nyuma kama vile anamkagua Roma na hakujali kabisa mvua na alikuwa ameloa kiasi kwamba mpaka manyonyo yake yalionekana waziwazi.
Sasa kitendo cha Roma kuitwa jina la Hades alishangaa, kwani hakutegemea kukutana na mtu kwenye msitu mkubwa kama huu ambaye anamfahamu tena sio kwa jina la Roma bali kwa jina la Hades.
“Wewe ni nani?”
“Nipe Lift kama unataka kunifahamu”Aliongea yule mwanamke kwa namna ya kujiamini huku akipeleka mkono machoni na kufuta maji ya mvua yaliomloanisha, alikuwa amenyoa kipara huyu mwanamke.
“Nakupaje Lift wakati sikufahamu”Aliongea Roma
“Hahaha… Inashangaza mtu kama wewe unaetarajiwa kuokoa ulimwengu ukamuogopa mwanamke kama mim”Aliongea yule mwanamke na kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye gari na Roma alishangazwa na maneno ya mwanamke yule , kwakua Roma alikuwa akijiamini basi aliona haina haja ya kumkatalia anachotaka.
Nasra aliekuwa akishuhudia kila kilichokuwa kikiendelea aliishia kua katika mshangao na kushindwa kuelewa kinachoendelea.
“Roma ni nani?”Aliuliza Nasra akiwa na wasiwasi na Roma alitingisa mabega kwamba hamfahamu.
Kwakua mvua ilikuwa inanyesha Roma aliingia kwenye gari na kumfungulia yule mwanamke.
“Unaweza kuongea sasa , wewe ni nani na umenifahamu vipi”Aliongea Roma.
“Huna haja ya kunifahamu Hades , kukufahamu mimi inatosha, nimekusubiri kwa wiki nzima ndani ya huu msitu kwa ajili ya kukufikishia ujumbe niliokuwa nao kwa muda mrefu”Aliongea yule mwanamke.
“Roma unahakika ana akili nzuri”Aliongea Nasra akimwangalia Roma kabla hata ya kuendelea na safari.
“Hahaha...Nakiona kifo chako wewe mwanamke”Aliongea yule mwanamke na kumfanya Nasra kugeuza kichwa na kumwangalia.
“Usishangae I am from the Future”
“You are Light worker?”Aliuliza Roma kwa Kingereza baada ya yule mwanamke kuongea kwa lugha ya kingereza.
“Ooh !Hivyo ndio manavyotuita , ndio mimi ni Light Worker”Aliongea yule mwanamke akikubaliana na neno la Roma.
“Light Worker!! ni watu gani?”Aliuliza Roma.
Ni jamii ya watu ambao wamepewa uwezo usio wa kawaida tunaita ‘Special Gift’ wanaitwa ‘Light worker’ kwasababu kazi yao kubwa ni kuhakikisha dunia inakuwa sehemu salama , kwa maneno marahisi wanafanya kazi kwa ajili ya kusaidia jamii Zaidi”Aliongea Roma na kumfanya Nasra na kumgeukia yule mwanamke na kumuona akitabasamu.
“Sasa kwanini akawa huku msituni na kwanini anasema anaona kifo changu”Aliongea Nasra kwa wasiwasi.
“Naishi nikiwa mbele ya muda wa miaka mitatu Nasra Kihedu”Aliongea yule mwanamke kwa kutaja jina la Nasra na kumchanganya Zaidi.
“Unanifahamu mimi , umenijua vipi”
“Kwasababu mimi ni ‘Light worker’ na nilikuwa nikiwasubiria na ndio maana nikakaa katikati ya barabara licha ya mvua kunyesha”
“Nieleze ambacho unaona ndani ya miaka mitatu ijayo”Aliongea Roma kwa shauku kubwa , alijiambia kama kweli mwanamke huyu ni Lightworker na amekaa barabarani akitarajia ujio wao basi angalau anapaswa kumsikiliza.
“I see your death Hades , I see Snow mountains, I see Dark , I see the end of humanity”Aliongea yule mwanmke, na unachopaswa kuelewa mwanamke huyu alikuwa ni mwafrika kama kawaida , alikuwa na Ngozi nyeupe ya kibantu kabisa.
Sasa anamwambia Roma kwamba anaona kifo chake , anaona milima ya barafu na anaona giza na anaona mwisho wa binadamu.
“Sijawahi kuamini nabii yoyote kwenye Maisha yangu , unachoongea siwezi kuamini hata kidogo”Aliongea Roma huku akiwasha gari.
“Hauna haja ya kuniamini Hades ,mimi ni mjumbe na kazi yangu nikufikisha ujumbe mahali unapotakiwa kufika , kuhusu kuniamini hio sio kazi yangu , nimekwambia ninachoona ndani ya miaka mitatu ijayo”
“Niambie nakufa kwasababu gani?”
“Naona mwili wako usiokuwa na uhai , naona mwili wa mtu unaempenda sana usiokuwa na uhai, naona maangamizo ,naona mwanzo mpya wa ulimwengu, ”Aliongea yule mwanamke.
“Siwezi kukuamini, ungeniambia miaka mitatu ijayo , unaona Watoto niliozaa na mrembo wangu hapa , huenda ningekuamini”Aliongea Roma na yule mwanamke alitabasamu.
“Naomba kushuka , safari yangu inaishia hapa”Aliongea yule mwanamke baada ya kufika sehemu ambayo inaonekana ilikuwa ikichimbwa ili kupatikana kwa mchanga wa kusindilia barabara , mvua ilionekana kupungua kabisa na sasa ni kidogo sana iliokuwa inanyesha.
Roma alisimamisha gari na kuacha yule mwanamke kushuka na baada tu alivyoshuka alisogea mpaka upande wa dirishani.
“Kuna njia moja tu ya kuepuka kifo”Aliogea na kuangalia nyuma na mbele na kisha akaendelea
“You can’t win alone, unaweza usiamini maneno yangu , lakini wiki moja inayokuja kuna jambo litakaloumiza moyo wako litakalotokea, Naona Kifo”Aliongea na kisha akaanza kupiga hatua kurudi alikotoka na kumfanya Roma kutabasamu na kumwangalia Nasra.
“Atakuwa kichaaa”Aliongea Nasra
“Nakubaliana na wewe”Aliongea Roma na wote wakacheka na kuendelea na safari.
Kama nusu saa hivi nyuma kidogo na sehemu ambayo Roma waliweza kukutana na yule mwanamke , ilisimama gari aina ya Toyota Land Cruiser na walitoka wanaume wawili waliovalia mavazi ya suti na kufungua mlango na wakamruhusu mwanamke yule kuingia na gari ile ikaondoshwa.
Saa saba kamili hatimae Roma na Nasra waliweza kufika ndani ya Kijiji cha Mponde ,Kijiji ambacho kimezungukwa na mashamba ya chai kila kona , kilikuwa ni kijjiji ambacho kimechangamka.
Roma aliendesha gari kusonga mbele kwa maelekezo ya Nasra , kwa jinsi watu walivyokuwa wakishangaa gari yao , ilidhihirisha gari kama hio ni nadra sana kuonekana maeneo ya Kijiji kama hiki , kwani kila sehemu watu walikuwa wakiikodolea macho.
Nasra alishangazwa na namna ambavyo mazingira kutobadilika sana kama alivyoacha mazingira hayo miaka kadhaa iliopita, kila kitu kilikuwa vilevile kwake ilikuwa ni kama jana , kutokana na mazingira yalivyokuwa.
Baada ya kuendesha kwa muda wa kama dakika mbili hatimae Nasra alimwamrisha Roma kusimamisha gari pembeni , kwenye Kijiji kimoja kilichoahamika kwa jina la Mamoshi.
Wanawake kwa wanaume walionekana wakiwa wamesimama kando ya barabara , ni kama walikuwa wakiwasubiria wao.
“Nasraaa…!!!!”
“Sauti ya mwanamke aliejifunga vitenge vilivyofubaa alionekana akikimbilia upande wao m mara baada tu ya Nasra kushusha miguu yake chini.
“Mama…!” Aliita Nasra huku machozi yakimtoka , hakuamini aliekuwa mbele yake alikuwa ni mama yake mzazi.