SHETANI RUDISHA AKILI ZETU
MTUNZI: SINGANOJR.
IMEHARIRIWA: ZERO’SLITERATURE.
SEHEMU YA 131
Kisasi chetu kimeanza rasmi
Hamza hakuchukulia eneo hilo kama chumba cha upasuaji wala hospitalini, ila kwake ilikuwa ni kama uwanja wa vita, na alijiambia kama anataka kufanikisha upasuaji huo, asiruhusu mazingira kumwathiri.
“Mgonjwa ana uvimbe upande wa kushoto kwenye mapafu yake, kwenye
lower lobe ulioshuka mpaka kwenye ateri kubwa. Nitafanya upasuaji wa kuondoa kipande chenye uvimbe na kuunganisha na arteri,” aliongea Hamza.
Mara baada ya Hamza kusema kauli hiyo, watoa huduma wa afya walijikuta wakishikwa na mshangao kama vile hawakuwa wamemsikia vizuri.
“Dokta, huo upasuaji haujawahi kufanyika kwenye hospitali yetu, hatuna uzoefu,” aliongea nesi aliyekuwa kiongozi. Maneno yake yalikuwa sahihi, upasuaji huo ulikuwa mkubwa sana kufanyika katika mazingira hayo na mara nyingi ulikuwa ukifanyika katika hospitali kubwa za rufaa.
“Uzoefu nilionao unatosha. Nyie mtafuata maelekezo pekee. Kumbuka mpo hapa kwa ajili ya kuokoa maisha ya mgonjwa na si vinginevyo,” aliongea Hamza akiwa siriasi.
“Dokta, unaonekana mdogo sana... utaweza kweli? Isije ikaleta matatizo?” aliuliza dokta wa usingizi, maana ndiye mtu pekee aliyekuwa na mamlaka ya kukataa au kuruhusu upasuaji huo kuendelea.
“Siwezi kuongea kitu ambacho sijawahi kufanya. Tusipomfanyia mgonjwa upasuaji sasa hivi, hatochukua muda mrefu atapoteza maisha. Najua una wasiwasi, lakini nakuhakikishia kama mtafuata maelekezo yangu vizuri, kila kitu kitaenda sawa. Hii ni operesheni ya dharura,” aliongea na kumfanya dokta yule kuangaliana na watu wengine, na wote walionekana kuwa na macho ya wasiwasi lakini yenye hali ya kutaka kumuacha Hamza ajaribu.
“Nitrous oxide...”
“Naam! Dokta, unataka kutumia nitrous oxide kama
supplemental anesthetic?” aliuliza, na Hamza alitingisha kichwa.
“Bahati na iwe juu yetu kumuokoa mgonjwa, anza na hiyo,” aliongea Hamza, na pale pale dokta alifanya kama alivyoambiwa.
“Scalpel.”
Ijapokuwa manesi walikuwa bado na wasiwasi, lakini kitendo cha Hamza kuwa na mwonekano wa utulivu na kujiamini, walijikuta wakitii maagizo na kuanza kumpatia kila alichokuwa akiagiza.
“Single pole lighting blade, sternum saw.”
Mikono ya Hamza ilianza kwenda spidi spidi. Muda ambao alianza kufungua kifua kwa ustadi wa hali ya juu, macho yao yalianza kumwangalia kwa namna ya kumkubali.
Hawakuwahi kuona mbinu ya upasuaji ambayo Hamza alikuwa akitumia.
Kutokana na hilo, kundi lote lilijikuta likipatwa na hali ya kujiamini na kuongeza umakini.
“Ni kama tulivyoona kwenye vipimo; uvimbe unazidi kusambaa na kutoa damu...” aliongea Hamza huku akichunguza kwa umakini.
“Dokta, nini kinafuata?” aliuliza msaidizi wake namba moja.
“Usiniambie hujawahi kuona upasuaji wa aina hii hata mara moja?” aliuliza Hamza na kumfanya msaidizi yule kushikwa na haya.
Licha ya kwamba hospitali yao ilikuwa na huduma ya upasuaji wa kifua na moyo, lakini ilikuwa ni hospitali ndogo na wagonjwa wengi hawakuwa wakiamini, hivyo kwenda kupatia matibabu katika hospitali kubwa jijini Dar es Salaam.
Hamza aliishia kutingisha kichwa na kumpa ishara ya kujifunza kile anachokifanya.
“Angalia ujifunze sasa. Naomba hemostatic pincer... Nipe scissors, ni muda wa kukata uvimbe,” aliongea Hamza huku akielekeza kila hatua aliyokuwa akifanya. Kwa haraka sana aliweza kuondoa uvimbe wote.
Muda nao ulikuwa ukienda kasi sana ndani ya chumba hicho cha upasuaji mpaka hatua ya kushona ikakaribia, ikionyesha Hamza amefanikiwa kumaliza upasuaji kabisa kwa asilimia mia moja bila kusababisha matatizo.
Asilimia kubwa ya manesi na mtaalamu wa usingizi walijikuta wakimwangalia Hamza kwa mshangao usio wa kawaida. Ilikuwa ngumu kuamini kuwa kuna daktari anayejiamini kwa namna hiyo na kufanya upasuaji katika mazingira hayo, na kutoa uvimbe mkubwa kiasi hicho. Zaidi sana, spidi yake ilikuwa ni kubwa mno.
“Asanteni kwa ushirikiano mkubwa. Msikose kujiamini tena baadaye mkikutana na kesi kama hii,” aliongea Hamza baada ya kuvua barakoa na kutoa tabasamu la kuwashukuru kwa msaada wao.
Kundi hilo la watoa huduma ya afya waliishia kurudisha tabasamu huku wakitingisha vichwa kumkubali.
Mama aliyekuwa na mume wake, mara baada ya kusikia habari za upasuaji kwenda vizuri, alijikuta akishukuru mno kiasi cha kutaka kupiga magoti kabisa, lakini Hamza alimuwahi na kumfariji ili asipige magoti.
Hamza aliangalia upande mwingine na mara baada ya kuona hakuna wagonjwa wengi wenye majeraha makubwa, aliamua kutoka kwenda kukutana na Regina sasa.
Baada ya kutoka nje, hakutegemea kumuona Fabi na Regina wamesimama pamoja, tena wote wakiwa wameshikilia juisi mikononi. Hamza aliishia kukunja ndita huku akiwa anawasogelea.
“Wife, bado tu huyu bwana yupo hapa?”
“Kwanini unaniuliza swali la namna hiyo, wakati alikuwa akiangalia maendeleo ya upasuaji wako?”
“Vipi kuhusu hiyo juisi yako, kama akikuwekea kitu kibaya je?”
“Hebu acha ukichaa na kumfanya Senior kuonekana mtu mbaya,” aliongea Regina huku akijiuliza Hamza anafikiria nini kila saa anapomuona na kaka yake Fabi.
Hamza alimpokonya Regina ile juisi na kisha aliinywa yote. Regina aliishia kumwangalia Hamza kwa hasira na mshangao kwa wakati mmoja. Ilikuwa mara yake ya kwanza kumwona Hamza akisumbuliwa na wivu namna hiyo.
“Unaonekana upo vizuri sana kwenye fani ya udaktari. Angalia hao manesi na madaktari wanavyokuangalia kwa macho ya kukushangaa. Unapaswa kujivunia,” aliongea Regina huku akiwaza ilikuwaje Hamza akawa na uwezo wa kufanya matibabu lakini bado ni mwanafunzi chuoni. Haikumwingilia akilini na alijiambia maisha ya Hamza hayakuwa yakieleweka kabisa. Lakini hata hivyo, alijihisi kujivunia kwa kuolewa na mwanaume mwenye uwezo.
“Kipi cha kujivunia sasa? Kama daktari, nikiwa katika chumba cha upasuaji, ninachowaza ni kumuokoa mgonjwa pekee. Kosa kidogo mgonjwa anakufa. Kwangu ni kitu cha kawaida, sioni cha kujivunia zaidi ya kushukuru kwamba nimeweza kumuokoa mgonjwa,” aliongea.
Regina mwanzoni alidhani Hamza akitoka hapo ataanza kujigamba, lakini hakutegemea angetoa jibu kama hilo. Aliishia kushangaa tu na hakujua namna gani anapaswa kujibu.
“Mr. Hamza, uwezo wako wa kufanya upasuaji ni wa viwango vya juu sana, nimetokea kukubali,” aliongea Afande Fabiani.
“Kwanini bado tu upo hapa? Makomandoo wa Malibu mpo
free kiasi hicho?” aliuliza Hamza kwa chuki.
“Usiwe na wasiwasi, ndio naondoka sasa maana muda wa kumpeleka Profesa Ndiswe umewadia,” aliongea na kisha akamgeukia Regina.
“Regina, kikosi changu kitakuwa jijini Dar kwa siku kadhaa tukiendelea kutoa ulinzi. Kama muda utakuwepo, unaonaje tukikutana na wenzetu tuliosoma nao na kupiga stori mbili tatu? Sijaonana nao kwa muda mrefu sana.”
Regina, mara baada ya kusikia kauli hiyo, alimwangalia kwanza Hamza na kisha akampa jibu:
“Kama nikipata muda tutaona itakavyokuwa,” aliongea Regina.
“Mke wangu yupo bize muda wote, sio lazima muonane,” aliongea Hamza akiwa hana furaha kabisa. Lakini hata hivyo, Fabiani hakuchukulia suala hilo moyoni. Badala yake alitingisha kichwa akiwa na tabasamu na kisha akaaga na kuondoka.
Hamza alishindwa kujizuia kumuuliza Regina maswali, hata baada ya Afande Fabiani kuondoka.
“Hamza, umepatwa na shida gani wewe leo? Nilivyokuwa nikikuangalia unafanya upasuaji ni adimu sana kukuona katika hali ya kupendeza macho, lakini kwanini unakuwa
petty mbele ya Fabiani?” aliuliza Regina, akiwa haelewi kwa nini Hamza alikuwa akionyesha wivu mbele ya kaka yake.
“Yule jamaa alikuwa akinichokoza kabisa kwa kukuchimba chimba, ningekaa kimya angeona kabisa namuogopa,” alijibu Hamza kwa sauti ya kujitetea.
Regina aliposikia maneno hayo, alipatwa na hasira, na kifua chake kilianza kupanda na kushuka kwa ghadhabu.
“Unaongea nini wewe, kunichimba chimba kivipi?”
“Kukumbushia yaliopita sio ndio kukuchimba? Kulikuwa na haja gani ya kukutania mbele yangu? Alipaswa kuniheshimu,” Hamza aliongeza, akijaribu kuelezea hisia zake.
“Kwahiyo ukadhania kukumbushia stori za nyuma ndio anaweza kunirudisha nyuma ya muda…?” Regina alikuwa na hasira sana na alishindwa hata kuongea vizuri. Hakupenda jinsi Hamza alivyokuwa akionyesha kutojiamini mbele ya kaka yake, Fabiani.
“Wife, usiwe na hasira… sitorudia kuwa na tabia ile tena,” aliongea Hamza, akijaribu kumtuliza Regina baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya.
Regina aliishia kumwangalia Hamza kwa sekunde kadhaa na kisha aligeuka na kutoka nje ya hospitali hiyo, Hamza akamkimbilia.
“Wife, usiwe na hasira, yule jamaa anaonekana kabisa sio mtu mzuri.”
“Usije ukamgusa, halafu mimi ni mtu mzima, nina mzunguko wangu wa watu ninaofahamiana nao katika jamii na huwezi kunizuia kusalimiana na marafiki wa kiume ninaofahamiana nao. Mbona mimi sikuzuii kuwa na ukaribu na wanawake nje, lakini mimi hutaki?” Regina aliongea kwa hasira.
Hamza alijikuta akikosa neno la kuongea. Alijua kuongea hivyo ilikuwa ni kwa faida yake mwenyewe lakini ilionekana nia yake imeeleweka vibaya.
“Okey sawa, Wife, nimekuelewa usiwe na hasira basi.”
Hamza alijiambia kama Fabiani atafanya hila ya kujaribu kumtega Regina, atamuua.
“Wife, huko unaenda wapi sasa, nisubiri,” aliongea.
“Unaulizaje wakati unaona tunaelekea stendi tupande basi kurudi, au unataka tulale hapa?”
“Ah!” Hamza aliishia kujiona mjinga, lakini ukweli hakujua kama Regina angekuwa na wazo la kupanda basi la kawaida kurudi Dar es Salaam. Wasingeweza kupanda treni tena kutokana na ajali ile iliyotokea.
Baada ya kutoka hospitalini hapo, walichukua taksi ambayo iliwapeleka moja kwa moja mpaka kituo cha mabasi na waliweza kufanikiwa kupanda basi la Luxury.
Wakati wakiwa njiani, walikuwa wakiangalia taarifa ya habari iliyokuwa ikionyesha tukio la treni kushambuliwa na magaidi. Lilikuwa tukio kubwa sana kwa nchi kutokana na kwamba ni mara chache sana matukio kama hayo hutokea. Katika taarifa hiyo, uchunguzi wa awali ulionyesha ni kundi la kigaidi lenye ushirikina na Alshabab ndio waliingia nchini kwa ajili ya kufanya shambulizi hilo la kigaidi.
Malengo yao hayakuwa kuua bali kumkamata mwanasayansi ambaye alikuwa akijua tafiti muhimu sana iliyokuwa ikiendelea kwa siri nchini Tanzania. Taarifa hiyo ilienda mbali kupongeza kikosi cha wanajeshi walioweza kuzima shambulizi hilo na kuzuia vifo vingi kutotokea.
Hamza wakati akisikiliza habari hiyo, muda uleule aliweza kumkumbuka Yulia na kujiambia au mwanasayansi yule alikuwa na uhusiano na utafiti wa Yulia. Hamza aliona uwezekano huo upo, maana kundi lile ni kati ya makundi ambayo yalikuwa na uwezo mkubwa na kupata msaada kutoka kwa watu wengi.
Kwa namna moja aliona pengine mtu aliyeajiri kundi hilo atakuwa ni yule yule aliyewaajiri wale maninja waliokuwa wanajaribu kumuua Yulia kule Bagamoyo-Msata. Kutokana na mlolongo huo wa matukio, Hamza alijikuta akizidi kushikwa na shauku ya kutaka kujua ni utafiti gani huo ambao Yulia anafanya mpaka watu wengi kuutolea macho namna hiyo, lakini bado hakupata jibu.
Waliweza kufika jijini Dar es Salaam saa mbili za usiku. Regina alikuwa hana uchovu sana kama ilivyokuwa mwanzo kutokana na kujifunza kuvuna nguvu za andiko la Lugha za malaika. Ijapokuwa alikuwa katika hatua ya kuelewa maana ya lugha ile, lakini nguvu yake ya kiroho ilikuwa imeimarika mno kiasi cha kupelekea hali yake ya furaha kuimarika.
Wakati wanashuka stendi ya Magufuli, sehemu hiyo ilikuwa imechangamka sana licha ya kwamba ilikuwa ni usiku. Madereva boda boda walianza kuwazonga kutaka kuwasafirisha lakini Regina hakuamini usalama kwenye kupanda usafiri huo, hivyo wakati akiwa kwenye basi alisha
request Uber kumchukua katika eneo hilo.
Sasa wakati gari ya Uber ikiwa imesimama kwa ajili ya wao kuingia, Hamza alijikuta akigeuza macho yake nyuma kama mtu anaeshangaa.
“Hamza, mbona unashangaa, ingia ndani tuondoke,” aliongea Regina.
Hamza alijikuta akiingia kwenye gari huku akijiambia pengine yalikuwa ni macho yake tu. Ukweli ni kwamba alihisi kuona mtu ambaye alimtambua lakini hakujua kama ni kweli au amemfananisha.
Kitendo cha taksi ile kuondoka, nyuma ya kituo cha kukatia tiketi za magari ya mwendokasi, walikuwa wamesimama mwanaume aliyekuwa amevalia tisheti ya mikono mirefu pamoja na kofia, lakini vilevile alikuwa ameambatana na mwanamke aliyekuwa amevalia vazi la Abaya na hijabu huku akiwa na miwani ya jua na ilionekana walikuwa wamejificha.
Kwani kitendo cha Hamza na Regina kuondoka, walitokeza na kwenda kuingia kwenye gari aina ya Ist iliyokuwa imeegeshwa karibu na eneo hilo, huku yule mwanaume aliyekuwa amevalia kofia akiwa ndio dereva.
“Kesi ilishafungwa muda mrefu na wanajua tumekwisha kufariki, lakini kwanini ni kama wanatufuatilia,” aliongea yule mwanaume.
“Nilikuwa sijawaona mwanzo ila ni wao, sijui wanafanya nini hapa, labda sio kama wanatufuatilia,” aliongea mwanamke.
“Kidogo tu wangetuona, ni bahati tu sisi sio kama wanajeshi wanaovuna nishati za mbingu na ardhi, vinginevyo ingekuwa rahisi kwa Hamza kutodharau hisia zake pale,” aliongea.
“Tunabahati kweli hajatuona, kwa namna tulivyopata tabu ya kurudi mpaka Dar kama angetuona ingetuletea shida kubwa,” aliongea yule mwanamke huku akishika kifua chake na upande wa yule mwanaume alitoa tabasamu la kejeli.
“Muda wowote tu tutaonana naye, ni kwamba tu muda huu sio sahihi, usidhani tumerudi hapa kwa ajili ya kuishi.”
“Hapana sifikirii hivyo. Hata hivyo, Saidi, unadhani tutaweza kweli kumuua Hamza?” Mwanaume yule mara baada ya kusikia kauli hiyo aliachia ile kofia na barakoa na palepale sura yake iliweza kuonekana. Alikuwa ni Saidi aliyekuwa na ndevu nyingi usoni.
“Lamla, kama huniamini ni kheri ukaacha kunifuata na ondoka zako,” aliongea kwa namna ya kufoka na palepale Lamla alitingisha kichwa kukataa.
“Hapana... hapana, nipo tayari kukufuata popote unapoenda, Adam nimekupa kila kitu changu, wewe ndio Master wangu kuanzia sasa, wewe ndio
my everything.”
Lamla alikuwa akielewa kwamba kama kweli atathubutu kuondoka, sio tu kwamba atagundulika kuwa ndani ya jiji la Dar, lakini Saidi anaweza kumuua kabla hata hajapiga hatua. Ukatili na uhuni wa Saidi alikuwa ameshaupitia na kufikia hatua ya kuelewa sheria zake na hakutaka kumchokoza kwa namna yoyote kama alikuwa akitaka kuendelea kuishi.
“Master wako! Kuniita hivyo sioni ni mbaya... Sawa kwanzia sasa na kuendelea wewe ni Mbwa wangu wa Kike, hivyo unatakiwa kutii kila ninachokuambia, nikisema bweka una bweka.”
“Yes Master,” alijibu Lamla . licha ya kuona anadhalilishishwa kwenye moyo wake laiini hakua na jinsi zaidi ya kumheshimu Master wake.
“Safi sana Mchumba haha.. hebu twende kwanza tukatafute namna ya kushiba na kisha turudi kwenye kambi yangu ya siri”Aliongea.
*****
Ikiwa ni saa nne usiku katika maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, kando ya bahari, kulikuwa na nyumba kubwa iliyojitenga, sehemu hiyo ilijulikana kama Kwa Mzee Mkulima. Kwa muda mrefu sana, nyumba hiyo haikuwa na mtu anayeishi baada ya Mzee Mkulima na familia yake yote kufariki. Mwanadiplomasia aliyekuwa mwanafamilia pekee aliyebakia alikuwa akiishi nje ya nchi, na mara chache sana alionekana nchini Tanzania.
Usiku huu wa saa nne, wakazi wa karibu katika eneo hilo walijikuta wakishangaa baada ya kuona taa za jumba hilo zikiwa zimewashwa ndani, ishara kwamba kulikuwa na mtu ndani yake. Lakini hata hivyo, wakazi hao waliamini pengine kijana wa Marehemu Mzee Mkulima alikuwa amerudi nchini, lakini kutokana na kutokuwa na mazoea naye, hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kwenda kusalimia.
Wakati huo ndani ya nyumba hiyo, chini ya ardhi, kulikuwa na chumba kikubwa sana ambacho kilikuwa cha siri, na kuingia kwake pia kulihitaji mlango wa siri. Ndani ya chumba hicho cha ardhini, taa zilikuwa zimewashwa na eneo kuwa angavu kama vile ni mchana. Alionekana Lamla, aliyekuwa amevalia mavazi yale yale aliyoyaonekana nayo akiwa katika steji ya Mbezi Luisi. Alikuwa amesimama katikati ya ukubwa wote wa chumba hicho chenye kila aina ya vifaa vya kisasa vya kimaabara, akihisi kama yupo mbele ya wakati.
Kulikuwa na kila aina ya kifaa cha kisayansi, tena vile vyenye teknolojia ya hali ya juu vilivyokuwa vimepangwa katika eneo hilo lenye mita za mraba mia nne. Kwenye baadhi ya glasi vilionekana aina nyingi za vimiminika, kwenye mafriji ya vioo vilionekana aina tofauti za viungo vya binadamu. Kulikuwa na kila aina ya kiungo, kuanzia viungo vya Kichina, Kizungu, Kiarabu, na kuendelea. Kulikuwepo hadi binadamu aliyekatwa kutoka juu mpaka chini na nusu yake kuhifadhiwa.
Lamla, mara baada ya kuangalia mwili wa mwanamke aliyekatwa nusu, alikuwa na uwezo wa kuona kila aina ya kiungo cha ndani katika mwili wake na alijikuta akikosa ujasiri na kuangalia upande mwingine. Saa moja na dakika kadhaa zilikuwa zimepita tangu waingie ndani ya maabara hiyo. Baada ya kuingia hapo ndani, Saidi alimwambia asubiri katika eneo hilo wakati yeye akiingia kwenye chumba kingine, na haikujulikana alikuwa akifanya nini kwa muda wote aliokuwa ndani huko.
Mmiliki wa maabara hiyo alikuwa ni Mzee Mkulima na alimrithisha mwanae aliyekuwa nje ya nchi, lakini mara baada ya Saidi kugundua kuhusu uwepo wa maabara hiyo kabla ya kurudi nchini, alimuua kwanza mtoto wa Mzee Mkulima na kujimilikisha eneo hilo ambalo rasmi likawa kambi yake ya siri ya kufanyia tafiti zake. Kwa sababu Saidi hakuwa na mahusiano yoyote na Mzee Mkulima, ingekuwa vigumu kwa mtu yeyote kugundua kama alikuwa akiishi hapo ndani. Ndio maana alijiamini kurudi nchini kuendeleza misheni zake kimyakimya ndani ya maficho hayo.
Lamla alipokuwa anatembea ndani ya eneo hilo, alishangaa mno na kuona Saidi au Adam alikuwa ni binadamu mkatili sana, ambaye muda wote alikuwa akipanga mitego yake.
Saa tano na nusu, hatimaye mlango wa kushoto ambao Saidi aliingia ulifunguliwa na mwanaume aliyekuwa hajavaa kitu chochote mwilini alitoka.
Lamla, mara baada ya kumwangalia mwanaume huyo, alijikuta akishituka palepale kiasi cha kutaka kudondoka chini maana ni kama alikuwa akiangalia mzimu.
"Wewe... wewe, Fra... Frank!?" Mwanaume aliyekuwa mbele yake alikuwa akifanana kila kitu na Frank, mtoto wake, lakini palepale Lamla alijua huyo siyo Frank mtoto wake, kwa sababu amekufa; ila huyo alikuwa ni Saidi katika sura ya Frank.
Saidi, aliyekuwa katika sura ya Frank, aliishia kutoa tabasamu la kikauzu, na muonekano wake ulizidi kuwa wa ajabu.
"Hmh, unafanana kwa kila kitu na marehemu mtoto wangu, unaogopesha sana," aliongea Lamla aliyekuwa akitetemeka huku akikumbuka namna mtoto wake alivyopoteza uhai.
"Master, kwa nini umejitengeneza kuwa hivyo?" Aliuliza na Saidi hakujali kama alikuwa uchi hata kidogo na alitembea kumsogelea Lamla.
"Ulidhani nilikupeleka Australia kuchukua hela zake? Kwangu mimi nilichoenda kuchukua ni wasifu wake kama mrithi wa makampuni ya Dosam."
"Mrithi wa makampuni ya Dosam!" Lamla palepale alijikuta akicheka kwa namna ya kusikitika huku akijiambia kwamba huo ndio ulikuwa mpango wa Saidi.
"Lakini Master, kumbuka Frank alikuwa ni mtoto wangu na Benjamini, hana damu kabisa ya familia ya Dosam? Na Wilson hakuwa baba yake."
"Haijalishi swala la damu, ili mradi Frank yupo hai ataendelea kutambulika kama mwanafamilia na Regina hawezi kumpotezea. Machafuko yatakayomtokea Regina na Hamza yatamtokea pia. Ninachotaka ni kumuona Hamza akiteseka ili na watu wanaomzunguka wateseke pia. Kisasi chetu kimeanza rasmi," aliongea Saidi kwa tabasamu.
Ijapokuwa Lamla hakuelewa kila kitu, aliishia kutingisha kichwa chake kwa haraka.
"Master, hakika una hekima sana. Yule kahaba sasa hivi anadhani ameniua na ameshakuwa mrithi halali wa kampuni. Awamu hii siwezi kumruhusu anishinde tena."
"Unamwita kahaba! Wewe ndiye kahaba uliezaaa mtoto nje ya ndoa," aliongea Saidi huku akitoa kicheko kikubwa. Ghafla tu alimsogelea Lamla na kumkaba shingo kwa nguvu, kisha akamwangusha chini na kurarua mavazi yake palepale.
"Master! Tafadhali!"
Lamla alishajua nini kinaenda kutokea. Licha ya kwamba alikuwa amezoea kufanyiwa hivyo, kitendo cha Saidi kuwa katika sura ya Frank kilimfanya ajihisi kama anafanya mapenzi na mtoto wake wa kumzaa. Hisia za huzuni na hatia zilimzidi sana moyoni mwake, lakini hakuwa na cha kufanya.
SEHEMU YA 132.
Muda ambao Hamza na Regina walifika nyumbani, shangazi alikuwa ameshaandaa chakula tayari mezani na alikuwa akiwasubiri. Baada ya kukaa kwenye meza, Regina alichukua jukumu la kumwelezea shangazi kila kitu kilichotokea wakati wakiwa njiani. Shangazi huyo alishangazwa na kusikia hayo na alimshukuru Hamza kwa kuendelea kuhakikisha usalama wa Regina. Pia, alimsifia bibi yake Regina kwa kutokukosea kumchagua Hamza kama mume wa Regina.
Kilichomfurahisha zaidi ni kuona kwamba wenza hao hawakuwa tu wamesameheana, bali pia walionekana kuwa na ukaribu mkubwa.
Siku iliyofuata ilikuwa ni Jumatatu. Wakiwa njiani kuelekea kazini, Regina alikuwa akiendelea na kazi kwenye laptop yake. Walipofika nusu safari, aliinua macho yake na kumwangalia Hamza kupitia kioo.
"Nisindikize kwenda London basi," aliongea Regina, akimfanya Hamza kushangaa na kumwangalia kupitia kioo cha nyuma.
"Unaenda Uingereza kufanya nini? Wife, usiniambie unataka twende kula fungate?" aliongea Hamza.
"Fungate ya kichwa chako! Nataka unisindikize kwa sababu nitapitia Ufaransa, na uwezo wako wa kuongea lugha hiyo ni mkubwa. Sitaki kuanza kutafuta mtafsiri nikifika. Matawi yetu ndani ya Ulaya tunayafungua rasmi, na nitaonana na wadau wengi kwa ajili ya kuandaa mpango wa kiuendeshaji," aliongea Regina, na Hamza alimgeukia na kumwongelesha kwa lugha ya Kiingereza.
"Wife, you are quite ambitious. This is very risky, and you might lose everything."
"High risk leads to high returns. My strength is in business. Nataka kuwa na uwezo wa kupambana na watu wa Bonde la Giza. Naona nimechelewa kuanza kujifunza yale mafunzo, na njia rahisi ya kuwa na nguvu ni kujiweka katika nafasi ya juu kwenye ulimwengu wa matajiri," aliongea Regina.
Hamza alitabasamu kidogo na alijiambia mawazo ya Regina yalikuwa rahisi sana. Ukweli ni kwamba haijalishi mtu ni tajiri kiasi gani, lakini mbele ya nguvu nyingine, pesa si chochote.
Sababu ya watu wengi kutotaka kustaafu ni kwa sababu walijua kwamba haijalishi ni matajiri kiasi gani; bila ya kuwa na ulinzi imara, pesa zao haziwezi kuwalinda.
Lakini Hamza hata hivyo aliamini kwamba ikiwa Regina atajitahidi na kujishikiza vizuri katika soko kubwa la mataifa ya Ulaya, basi biashara zake zingeweza kuongezeka na utajiri wake kukua. Hivyo, hakutaka kumkatisha tamaa.
“Mbona hutoi jibu, au unadhani nilichoongea ni upuuzi?” Regina aliuliza, akijisikia vibaya kutokana na Hamza kukaa kimya.
“Hapana, nilikuwa nikifikiria kwa kina, na nimeona maamuzi yako ni ya busara sana, mke wangu,” Hamza alijibu.
“Sikuamini wewe, lazima utakuwa unanicheka ndani kwa ndani,” Regina aliongea kwa mashaka.
“Hapana, naapia kwa Mungu,” Hamza alijibu, akijaribu kumtoa wasiwasi.
“Huna mshipa wa aibu kumhusisha Mungu kwenye uongo wako,” Regina aliongea kwa kukasirika.
“Sio…” Hamza alijikuta akishindwa kuendelea kuongea. Aliona pengine ni sahihi kutoongea chochote maana anaweza kuyaharibu mambo zaidi asubuhi hiyo.
Bila hata ya kujua, walikuwa tayari nje ya jengo la kampuni yao. Na wakati Hamza alipotaka kuliegesha gari ndani ya jengo, watu wawili, mwanaume na mwanamke waliovaa suti, walisimamisha gari lao mbele.
Hamza alikunja uso huku akisimamisha gari na kutoka nje.
“Wakubwa, mnajaribu kufanya nini kutusimamisha njiani?” aliuliza Hamza, akiwa amewajua watu hao. Walikuwa ni maafisa wa usalama na wanajeshi wa kitengo cha Malibu, Afande Barafu na Afande Mwiba.
“Mr. Hamza, umesahau leo ni ile siku ya makubaliano yetu?” aliuliza Afande Caro, maarufu kama Afande Barafu.
“Mpaka sasa maandalizi yote yamekwisha kufanyika na wafanyakazi wote wanaoenda kuhusika na majaribio hayo wapo tayari eneo husika. Natumaini utaungana na timu yetu ya ulinzi na usalama kwa ajili ya kufanikisha hili,” aliongea Afande Caro kwa heshima.
Hamza alijikuta karibu kujipiga kofi. Alikuwa amesahau kabisa kwamba leo ndiyo tarehe husika waliokubaliana. Aligeuka na kumwangalia Regina, ambaye pia alishuka kutoka kwenye gari. Alianza kuhisi kichwa kikimuuma asijue atamwambia vipi kuhusu suala hili ili amuelewe.
“Nini kinaendelea?” aliuliza Regina.
“Wife, niliwaahidi hawa marafiki zangu kwenda kuwasaidia kumlinda mtu. Nadhani nitaondoka kwa siku kadhaa,” Hamza aliongea, akihisi haya maana ni muda huo huo Regina alikuwa amemuomba kumsindikiza kwenda Ulaya.
“Unaenda kumlinda nani na hawa ni akina nani?” aliuliza Regina, akiwa ameshikwa na mshangao maana lilionekana kuwa suala la ghafla sana.
“Utuwie radhi, Madam, hili suala ni nyeti sana kukufahamisha,” aliongea Afande Caro. Palepale, alitoa nyaraka na kalamu na kumpatia Regina.
“Tunaomba pia ushirikiano wako kwa kusaini hii fomu ya makubaliano ya kutunza siri,” aliongeza.
Regina, licha ya kwamba alijua hata kama asiposainishwa hawezi kuongea chochote, aliishia kukubali na kusaini karatasi ile.
“Nawatakia kheri, Hamza, naomba uwe makini na usalama wako,” aliongea Regina.
Hamza, mara baada ya kusikia kauli hiyo, alijikuta akishikwa sana na furaha baada ya kuona Regina alikuwa akimjali sana. Aliishia kutikisa kichwa haraka haraka na kisha alimsogelea, akitaka kumkumbatia.
"Wife, unaonaje nikikuhug?" Hamza aliuliza kwa utani, akiwa na tabasamu usoni.
"Hebu nenda huko," Regina aliongea, akimzuia Hamza huku akirudi nyuma kidogo. Alikuwa na aibu na asingeweza kufanya hivyo mbele ya watu.
Hamza aliishia kumwangalia Regina kwa tamaa akiingia kwenye gari na kuliingiza maegeshoni.
"Tuondoke, Mr. Hamza," Afande Mwiba aliongea mara baada ya Regina kuondoka.
"Nisubirini kwanza, nakuja. Nina warembo wangu wawili napaswa kuwaaga kabla sijaondoka," Hamza aliongea, akimaanisha Yonesi na Eliza.
Siku hizi za karibuni, uhusiano wake na warembo hao ulikuwa umeimarika sana, na alijua hataonana nao kwa siku kadhaa. Hivyo, aliona si vyema kuondoka bila kuwaaga.
Afande Caro na Afande Mwiba waliishia kubakiwa na macho yasiyokuwa na viashiria vyovyote, hawakuwa na la kusema kuhusu maisha binafsi ya Hamza.
Ijapokuwa aliwaambia wasubiri kwa dakika chache, Hamza alikaa kwa zaidi ya nusu saa. Ndipo alipomaliza shughuli zake na kutoka kwenye jengo hilo la kifahari la kampuni ya Dosam, akaingia kwenye SUV ya kijeshi, na kuondoka.
Hamza alisafirishwa mpaka kwenye bandari ya jeshi, na hapo ndipo alipogundua kwamba wanasafiri kwa boti.
"Tunaelekea wapi?" aliuliza Hamza kwa wasiwasi kidogo.
"Chole Island," Afande Mwiba alijibu kwa kifupi.
Hamza alishangaa kwa dakika kadhaa. Ukweli ni kwamba alijua fika kuhusu kisiwa hiki kilichopatikana ndani ya Wilaya ya Mafia. Miaka kadhaa nyuma, ili kuinua uchumi wa Wilaya ya Mafia, Serikali ya Tanzania iliamua kuuza kisiwa hicho kwa kampuni ya Vexto Group kwa ajili ya kukigeuza kuwa eneo la kitalii la daraja la kwanza.
Kilikuwa mojawapo ya visiwa maarufu sana ndani ya Afrika Mashariki na Kati, na kilitembelewa na watalii wengi kila mwaka, hasa wale waliokuwa wakifika kwa ajili ya kupumzika na kufanya utalii wa kuangalia nyangumi (Whale Watching).
Ilikuwa ni hatua ya kishujaa sana ambayo serikali ilichukua kwa kushirikiana na wananchi wa kisiwa hicho. Licha ya kuendeleza kisiwa hicho na kukigeuza kuwa kisiwa cha kifahari kwa ajili ya matajiri, pia kisiwa kikuu cha Mafia kilipata maendeleo makubwa sana. Huduma za kijamii ziliboreshwa huku miundombinu yake ikikua kwa kiasi kikubwa, na kufanya wananchi wengi kupata ajira.
Sasa, Hamza, mara baada ya kusikia wanaenda kisiwa hicho, alishangaa kwa sababu alijua ni kisiwa kwa ajili ya utalii tu.
"Chole si kisiwa cha utalii pekee. Majaribio yanafanyikaje hapo?" Hamza aliuliza, akiwa na shauku ya kujua zaidi.
"Majaribio hayo ni hatari mno na ingekuwa hatari kama yangefanyika nchi kavu. Isitoshe, kisiwa hiki kinamilikiwa na kampuni ya Prima inayoongozwa na Madam Yulia. Mpango wa kuendeleza kisiwa hiki haukuwa kwa madhumuni ya kitalii tu; kuna maabara za siri zimejengwa chini yake," Afande Caro alieleza kwa utulivu.
Hamza, kadri alivyokuwa akisikiliza habari hizi, alijikuta akijawa na shauku zaidi ya kufika Chole. Kutokana na uzoefu wake, alianza kuhisi aina gani ya majaribio yanayoweza kufanyika katika kisiwa hicho.
"Nilijua tokea siku nyingi kisiwa hiki kipo chini ya kampuni ya Vexto?" Hamza aliuliza, akionyesha wasiwasi.
"Vexto ndiyo wawekezaji wakubwa ndani ya kampuni ya Prima. Unaweza kusema ni wamiliki wenza. Isitoshe, pia wamiliki wa Vexto ni sehemu ya familia ya Wanyika," Afande Caro aliongeza, akitabasamu.
"Nilidhani familia ya Wanyika ni ukoo?" Hamza aliendelea kuuliza, akionekana kuchanganyikiwa kidogo.
"Ni muunganiko wa koo nyingi zilizoungana na kutengeneza familia moja. Ila, kila koo ina biashara zake na inajitegemea kiuchumi," Afande Caro alifafanua, na Hamza alianza kupata picha kamili.
"Nakumbuka mlisema Yulia ni mfizikia, kwa maana hiyo utafiti wake unahusisha majaribio ya silaha?" Hamza aliuliza, na kumfanya Afande Caro na Afande Mwiba kuangaliana.
"Mr. Hamza, ukishafika huko utajua ni tafiti gani zinafanyika. Ukweli ni kwamba, kulingana na daraja letu la usalama, hatujui chochote kuhusu utafiti huo wala majaribio yake," Afande Caro alijibu kwa utulivu, na Hamza hakuhitaji kuuliza maswali mengi zaidi.
Baada ya kama dakika thelathini hivi, Hamza aliingia katika boti ya kijeshi kuelekea kisiwani Chole.
Baada ya dakika chache za kuondoka kwa Hamza na wenzake, kundi lingine la wanajeshi lilishuka kutoka kwenye gari katika bandari hiyo. Wanajeshi hao wote walikuwa na silaha za moto na walikuwa wamevalia kombati za kijeshi, wakiongozwa na Afande Fabiani, kiongozi wa kikosi maalum cha kuzuia mashambulizi.
Nyuma ya Afande Fabiani, alikuwepo Profesa Ndiswe ambaye alionekana ndio alikuwa amefikishwa hapo.
"Kapteni Fabiani, asante sana kwa uhodari wako. Profesa Ndiswe tutaondoka naye sasa," Kamanda Makwela, mkuu wa Divisheni Maalumu ya Usalama, aliongea kwa sauti yenye mamlaka.
"Kamanda Makwela, hutaki sisi kumsindikiza Profesa mpaka Chole?" Afande Fabiani aliuliza kwa mshangao, akimwangalia Kamanda Makwela kwa macho yaliyojaa maswali.
Kamanda Makwela alitoa tabasamu kidogo kabla ya kujibu, "Kulingana na maelekezo yaliyopewa, kitengo cha Malibu cha kupambana na ugaidi kitaachwa hapa jijini Dar es Salaam, na hakuna haja ya kwenda kisiwani kwa ajili ya ulinzi."
"Kwanini? Sisi si ndio kiini cha ulinzi katika hii misheni?" Afande Fabiani aliuliza tena, akionekana kuchanganyikiwa zaidi.
"Mwanzoni ilikuwa hivyo, lakini kwa maelekezo ya Mshauri Mkuu na Mkuu wa Majeshi, makubaliano yamehitimishwa na imekubalika kuwa ulinzi uliokuwepo kisiwani Chole ni mkubwa mno mpaka sasa, na hakuna uwezekano wa kutokea shida yoyote. Hivyo, hakuna haja ya watu wengi kuongezeka," Kamanda Makwela alijibu, akimfanya Afande Fabiani kubaki katika hali ya mshangao mkubwa.
"Afande, au na Nyakasura amehusishwa katika hii misheni?" Fabi aliuliza, akiamini kwamba kikosi chake ndicho chenye uwezo mkubwa zaidi ndani ya kitengo cha Malibu, ukiachana na wanajeshi wa kujitegemea wa kitengo hicho ambao, kutokana na uwezo wao, hawakuhitaji vikosi bali walijitegemea katika misheni. Mfano wa wanajeshi hao ni Nyakasura, Bumba, Nyame, Mawu, na Mamiwata.
Afande Makwela, baada ya kuona namna Fabi alivyofadhaika, aliishia kucheka.
"Afande Fabi, huna haja ya kuwaza sana kuhusu hilo. Nadhani unaelewa sheria zilivyo," Makwela aliongea kwa utulivu, kisha papo hapo akawapa ishara vijana wake kumchukua Profesa Ndiswe kwa ajili ya kuanza safari kuelekea kisiwani Chole.
Afande Fabi alijua licha ya kwamba Makwela hakutaka kuongea zaidi, lazima Nyakasura alikuwa ameitwa kwenye misheni hiyo. La sivyo, Mshauri Mkuu, Mkuu wa Majeshi, na Mheshimiwa Rais wasingekuwa na utulivu wa kuwaagiza wao wasijiunge na wengine kwenda Mafia kwa ajili ya ulinzi.
"Haha... Afande, hata hivyo nina mambo mengi ya kufanya hapa jijini kwa sasa. Ukirudi, naomba tukutane sehemu tupate mbili tatu. Kwa sasa napanga kukutana na wahitimu wenzangu kuongea nao mambo mawili matatu," Fabi aliongea, na Afande Makwela aliishia kutoa tabasamu kisha wakaagana na kuondoka.
"Profesa, nadhani safari yako imekuwa ngumu sana mpaka kufika hapa. Ukweli ni kwamba ulipaswa kufika kisiwani moja kwa moja, lakini kutokana na sababu za usalama na wewe kuishi nje ya nchi mara nyingi, ndio maana ndege yako ilielekezwa kutua Mwanza na kuja Dar es Salaam kwa treni. Ni itifaki za kiusalama tu ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa," Afande Makwela alieleza.
"Usiwe na wasiwasi kabisa, Afande. Najua umuhimu wa tafiti hii kwa taifa na nina ujuzi mkubwa wa kuhakikisha majaribio yanafanyika vizuri bila dosari. Mengine ni masuala ya kiusalama tu na naelewa," Profesa Ndiswe, akiwa na dalili za mvi, aliongea kwa utulivu.
"Shukrani zikuendee, Profesa, kwa uzalendo wako kwa taifa. Asilimia kubwa ya wanasayansi waliofanikiwa nje ya nchi wameomba kubadili uraia, lakini wewe pekee ndiye uliamua kuendelea kuwa Mtanzania licha ya kupata fursa za kubadili na kuwa raia wa Marekani," Afande Makwela aliongeza.
"Nashukuru, Afande, kwa kuona nia yangu ya dhati kwa taifa. Niseme tu kwamba Tanzania ni nchi ninayoipenda sana. Licha ya kuajiriwa kufundisha kwenye vyuo vikubwa nje ya nchi, matamanio yangu makubwa ni kuona Tanzania inazidi kukua katika nyanja ya sayansi na teknolojia, hususani katika masuala ya ulinzi. Shukrani pia zimwendee Yulia kwa uwezo wake. Yule mtoto ni hazina ya taifa kwa uwezo wake mkubwa wa akili. Napatwa na msisimko wa hali ya juu kukutana naye kwa mara ya kwanza katika haya majaribio," Profesa Ndiswe aliongea kwa furaha.
Wawili hao waliendelea kuzungumza wakati safari ya kuelekea kisiwani Chole ikianza rasmi.
*******
Hamza, mara baada ya kufika kisiwani Chole, alishangaa kugundua kuwa kisiwa kilikuwa hakina watalii kabisa.
Resorts zote zilikuwa zimefungwa huku ikisemekana kunafanyika maboresho katika nyumba hizo na kuongeza usalama.
Kitu kingine kilichomshangaza ni kuona eneo la kati ya kisiwa hicho kulikuwa na mionzi iliyokuwa ikitoka na kusambaa juu angani, na kulikuwa na ulinzi ambao haukuwa wa kawaida. Boti nyingi za ulinzi zilikuwa zikipiga doria kuzunguka eneo lote.
Katika kisiwa hicho, kulikuwa na rada ya kijeshi iliyofungwa na wanajeshi zaidi ya elfu moja waliokuwa katika kisiwa jirani cha Mafia, huku wanajeshi kadhaa wakiwa katika kisiwa hicho cha Chole. Hamza alijikuta akihema kama mtu ambaye hakuamini kile alichokuwa anakiona. Aliamini hata kama ni rais anayezuru kisiwa hicho, ulinzi usingekuwa mkali hivyo.
Ilikuwa wazi kwamba Yulia alikuwa ni hazina ya taifa, na sio mwanamke wa kuchukuliwa kawaida.
Baada ya kushuka, Afande Barafu na Afande Mwiba walipangiwa katika maeneo tofauti kwa ajili ya ulinzi, huku Hamza akichukuliwa na wafanyakazi wa hoteli ya CloudFeri.
"Mr. Hamza, tafadhali..." aliongea mwanamke ambaye alionekana kuwa kiongozi. Alikuwa na umri wa makadirio ya miaka thelathini hivi, akiwa amevalia miwani ya fremu nyeusi. Licha ya kuvalia mavazi ya kihudumu, alikuwa na sura ya ukali mno. Hamza aliishia kutabasamu kwa uchungu kwani, ukichana na mwanamke huyo, wafanyakazi wote aliokuwa nao hawakuonekana kuwa wafanyakazi wa hoteli, bali wanajeshi waliovaa sare za uhudumu wa hoteli.
"Haina haja ya kuninyenyekea, ongozeni njia," Hamza aliongea akiwa na tabasamu.
Moja ya kivutio kikubwa cha kisiwa cha Chole ni hoteli ya ghorofa ishirini na nne, iliyojengwa kwa usanifu wa hali ya juu katikati ya kisiwa hicho kwenye kimlima, na kuifanya ionekane katikati ya msitu wa minazi.
Ilikuwa ni hoteli ya nyota tano na ghali sana kwa Afrika nzima, ikiingia kwenye orodha ya hoteli mia moja ghali duniani, yenyewe ikishika nafasi ya ishirini na saba.
Hamza, mara baada ya kuchukuliwa kwenye kigari cha kitorori (trolley) kinachotumia umeme, kilichokuwa kikitembea juu ya reli, alifikishwa nje ya hoteli hiyo. Aliweza kuona wanausalama wengi waliokuwa wamevalia miwani za kijasusi na suti, wakihakikisha ulinzi mkali ndani ya eneo hilo kuimarika.
Hoteli hiyo ilikuwa kawaida ikijazwa na watalii wakizunguka maeneo ya nje, lakini siku hiyo ilijaa wanausalama pekee. Mara baada ya kushuka kutoka kwenye kile kijigari, yule mwanamke aliyemchukua kule kwenye gati alitoa mawasiliano kupitia simu ya upepo kwa lugha ya Kiingereza safi.
"Madam Yulia, Mr. Hamza amekwisha wasili. Nimpeleke chumbani kwake au...?"
"Mlete nilipo," sauti kutoka upande wa pili ilisikika.
Ijapokuwa Hamza alikuwa akimsikia vizuri, alikuwa na shauku ya kutaka kujua ni wapi Yulia alipo. Wahudumu wale walimwangalia Hamza kwa shauku kubwa, maana hawakuwa wakimjua, na isitoshe alionekana kawaida. Walimpa ishara ya heshima kufuata na kisha walikwenda kusimama nje ya lifti. Walitumia kadi maalum kuifungua. Lifti hiyo haikuwa na kitufe cha kubonyeza kama lifti za kawaida, bali ukishapewa kadi maalum mapokezi, kadi hiyo inakuwa na uwezo wa kufungua lifti na chumba chako tu. Kulikuwa na kitufe cha dharura (Manual override button) ambacho kilikuwa chini kabisa katika eneo hilo la mapokezi, na kilitumika wakati wa dharura.
Kwa ufupi, ni kwamba jengo hilo lilikuwa na teknolojia ya hali ya juu mno, na usalama wake haukuwa wa kawaida. Licha ya kwamba halikuwa jengo refu sana, gharama iliyotumika kulijenga ilikuwa kubwa sana, hususani upande wa vioo ambavyo havikupitisha risasi. Kwa habari ambazo hazikuwa na uhakika, ilisemekana ni jengo ambalo lingehitaji mabomu makubwa kubomoa kuta zake na vioo, na ndiyo maana ilikuwa maarufu sana Afrika.
Jambo lingine lililompa Hamza nafasi ya kuona ulinzi wa eneo hilo ni pale alipoingia kwenye lifti. Yule mwanamke kiongozi wa wahudumu aliishia kuchezesha vidole vyake hewani kama vile alikuwa akipangusa. Jambo hilo lilimfahamisha Hamza kuwa miwani yake haikuwa ya kawaida, na ndiyo maana asilimia kubwa ya wanausalama walikuwa wamevalia miwani hizo.
Hamza sio kwamba alikuwa mshamba. Ukweli ni kwamba alishafika kwenye hoteli nyingi ambazo hata kadi haitumiki, bali teknolojia ya akili mnemba ya mfumo wa utambuzi ndiyo ilikuwa ikifanya kazi. Kilichomshangaza ni kwamba Tanzania ilikuwa imepiga hatua sana kwenye suala zima la uwekezaji wa sayansi na teknolojia.
"Hili jengo zima linatumia hizo miwani?" Aliuliza Hamza.
"Sio lote. Miwani hizi ni maalum kwa wahudumu wa floor maalum pekee. Sakafu zingine kwenda juu zinatumia akili mnemba kwa njia ya kutamka unapotaka kufikishwa," aliongea mwanamke huyo, na palepale lifti ilianza kushuka chini badala ya kwenda juu.
Baada ya sekunde kumi tu, lifti ile ilifunguka katika eneo la chini, na Hamza aligundua karibu eneo lote lilikuwa ni maabara ya kijeshi. Kwa haraka haraka, alijua lazima ni karibu kisiwa chote.
Hamza aliweza kuona manowari mbili za kijeshi ambazo zilionekana kuwa katika hatua za ujenzi, na kwa kuangalia tu aliona teknolojia yake ni ile mpya kabisa katika matoleo yote ya manowari duniani.
Hamza aliishia kutabasamu kwa uchungu na kujiuliza yote hayo yamewezekana vipi kwa nchi ndogo kama Tanzania kuwa na maendeleo ya namna hii hadi kuanza kujenga kwa siri manowari za kijeshi.
“Mr. Hamza, kila kitu unachoona hapa ni siri za jeshi. Umeruhusiwa kuingia hapa kutokana na Dokta Yulia kukuruhusu; inaonekana anakwamini sana,” aliongea mwanamke mwingine mweusi aliyempokea Hamza. Baada ya hayo, wale wengine walirudi. Walipotembea kwa mita kadhaa, walisimama mbele ya mlango, na kisha mwanamke huyo alitoa kadi maalum na kuigusanisha na kifaa. Kadi ile ilikuwa na nembo ya Tanzania na chini yake kulikuwa na maandishi ya TIMISA (Tanzania Intelligence and Military Security Agency).
“Hasina, nilidhani wewe ni mhudumu tu; sikujua unatokea usalama wa Taifa?” aliuliza Hamza kwa kujifanya mjinga, alimfahamu mwanadada huyo kwani alijitambulisha baada ya kumpokea.
TISA ilikuwa idara kubwa zaidi nchini ya usalama wa Taifa. Ndani yake kulikuwa na vitengo vya Malibu na TIMISA, ambavyo kikatiba hujitegemea licha ya kuwa chini ya usimamizi wa TISA. Hata hivyo, ni vitengo vya jeshi ambavyo rais hana mamlaka navyo moja kwa moja. Kama ilivyo kwa Malibu, ndivyo ilivyo kwa TIMISA; wafanyakazi wake wote ni wanajeshi wa kiwango cha ukomandoo.
“Ukweli ni kwamba Prima ni jina la kibiashara tu katika upande wa huduma za hoteli, lakini kinachofanyika chini ya Prima ni utengenezaji wa silaha na utafiti, na Yulia ndiye injinia mkuu. Licha ya cheo chake, usalama wa tafiti zake na yeye mwenyewe upo chini ya jeshi. Kama si yeye mwenyewe kuomba wewe kuhusishwa katika ulinzi, usingeweza kupata nafasi ya kufika hapa. Hata sisi tunashangaa namna ambavyo anaonekana kukuamini,” aliongeza.
Ijapokuwa aliongea kwa sauti ya kirafiki, mwanausalama huyo alionyesha kila dalili ya kutofurahia uwepo wake ndani ya eneo hilo. Hamza aliishia kutingisha mabega yake. Alijua fika chini ya kitengo hicho cha TIMISA, haijalishi mwanajeshi ana uwezo kiasi gani, njia ambazo wanatumia kushughulika na adui ni tofauti na anavyopambana na adui.
Hivyo, Hamza aliishia kukubaliana kwa mkono na Afande Hasina.
Mara baada ya kuingia ndani, kitu cha kwanza kilichomkaribisha Hamza ni sauti ya mwanamke akiimba kwa sauti nyororo. Alipogeuza macho yake kushoto, alishtuka baada ya kugundua Yulia ndiye aliyekuwa akiimba. Alikuwa amevaa koti jeupe, sweta la beige, na suruali ya ngozi (leather) rangi nyeusi. Kama si kwa sababu ya urefu wake na umbo lake, mwanamke asiye na sifa hizo asingethubutu kuvaa aina hiyo ya mavazi.