Simulizi ya Kijasusi: Tutarudi Na Roho Zetu?

Simulizi ya Kijasusi: Tutarudi Na Roho Zetu?

SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 8



Hivyo, alijifanya mnyonge zaidi. Akajiweka kitini hapo katika hali iliyotosha kumsumbua mwanamume yeyote. Von alikwisha timiza Fula yake ya kimwili kwa Nuru. Hata hivyo, Nuru alijua fika kwamba, kutokana na tabia ya roho ya Fula ya mwanaume; dakika chache baadaye angerudiwa na Fula ileile kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Wewe ni mshenzi…” alimchokoza tena ili atazamwe wakati huohuo akiyalegeza macho yake na kuzidi kujiweka juu ya kochi kinamna fulani.

*********
Kitu hiki ambacho asili kiliwekwa baina ya mwanaume na mwanamke, kitu ambacho hakielezekai kikamilifu kwa maneno, kilitimiza wajibu wake. Nuru alibaini kuwa Von na ukatili wake, pamoja na kuamini kwake kuwa ametosheka na kukinai, alianza upya kutaabika. Macho yake hayakuweza tena kutulia, mikono yake ilikuwa haikai pamoja. Alihangaika, akienda hapa na pale na kushika hiki na kile. Tahamaki akawa ameketi kochi moja na Nuru, mkono wake mmoja ukikosa kochi na kuangukia juu ya paja nono la Nuru.
“Wewe ni mtu mbaya sana,” Nuru alisema, sauti ikiwa laini, huku akijitia kusogea kando kidogo.
“Sikiliza…”
Nuru alijitia kumsikiliza. Alichofanya hasa ilikuwa kuupima uwezekano wa kumzidi Von maarifa aikwapue bastola yake ambayo ilikuwa imara kama hirizi katika mkono wake wa pili.
Von hakuwa mgeni kwa silaha hii ambayo ilikuwa ikitumiwa na Nuru. Alifahamu fika kuwa msichana huyu alikuwa akitumia mbinu ili ayaokoe maisha yake. Lakini kufahamu huko hakukukata shauku yake ya kutamani tena. Alitamani tena, kwa mara ya mwisho. Nuru angefanya nini? Kama kuna kisu basi Nuru alikuwa ameshika makali yake yeye akiwa ameshikilia mpini. Hata hivyo, alijua kuwa anacheza mchezo hatari, anacheza na nyoka. Haikuwa busara kuchezea roho kando ya shimo la mauti lililowazi kiasi hicho. Ni hilo ambalo lilimfanya aendelee kuishikilia bastola kama roho yake.
Wakati huo Von alikwishaibonyeza mitambo yake ambayo alisema ingemwezesha kuiona setilaiti hiyo ikishuka taratibu toka angani na kuiendea anga ya Tanzania ambapo ingesubiri muda uliopangwa kabla ya kuanza kuachia dhoruba za hewa ambayo ingezusha moto wa kutisha. Katika kioo hicho waliweza kuyaona mawingu mazitomazito yakipita katika kioo. Kisha dude la ajabu likajitokeza. Lilikuwa kubwa, jeusi lenye muundo wa ndege aina ya kunguru. Lilikuwa likisafiri kwa mwendo mkali sana kama linaloifuata televisheni hiyo.
Von aliinuka ghafla huku ameshikwa na mshangao. Aliiendea meza iliyokuwa na chombo chenye vidude vingi alivyokuwa akivibonyeza na kuvikagua kwa makini. Alibonyezabonyeza na kutazama tena katika kioo. Alikuwa kama ambaye hakuyaamini macho yake kuliona dude hilo likizidi kusogea. Mara jiji la johanesburg likajitokeza katika kioo hicho, majumba fulanifulani makubwa yakitoa nuru nyekundu kama gari linaloonyesha linaelekea upande upi. Nuru hiyo ilipokelewa au kujibiwa na dalili hiyo ya moto kutoka katika domo la chombo hicho ambacho sasa kilikuwa kikielea juu ya mji..
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 7



Nuru aliyaelewa majumba yote hayo ambayo yalionyesha alama za moto. Ni yale ambayo yeye na Joram walifanikisha kutega vile vigololi walivyovipata kutoka kwa hayati Chonde. Akaitazama saa yake. Ilikuwa ikikaribia muda uleule ambao Joram alikuwa ameviandaa vidude vile kufanya kazi. Alitamani apige ukulele wa furaha. Tangu walipoanza harakati hizo hakuwa na hakika kama walikuwa wakifanya kitu chenye uhakika. Wala hakumwona Joram kuwa na hakika hiyo, pamoja na kufunua majitabu mengi ambayo yalikaribiua kumtia wazimu. Kumbe alijua anachokifanya! Ndoto yake imetukia kuwa kweli.
Wakati Nuru akifanya sherehe hiyo moyoni, Von alikuwa akitaabika kichwani. Hakuelewa kinachotokea. Dalili zilizojitokeza zilikuwa za kutisha kabisa, zisizokubalika. Ilionyesha kuwa wakati wowote mji wa Johanesburg ungekuwa ukiwaka moto, Johannesburg badala ya Dar es Salaam, aliwaza kwa hasira. Haikuwepo njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuamuru setilaiti hiyo iharibiwe na kuanguka. Si kitu ikiangukia mji na kuua watu kadhaa. Heri nusu shari kuliko shari kamili. Ni hilo alilokusudia kufanya, kuinua simu na kuwapa wahandisi amri hiyo.
Hilo pia hakuweza kulifanya. Alijikuta akitazamwa na bastola yake mwenyewe, ambayo alihisahau kando alipokuwa akihangaika na mitambo. Bastola ilikuwa imara mikononi mwa Nuru, macho yake yasiyo na mzaha yakitangaza shari. “Pokea chako, mwuaji mkubwa,” Nuru alinong’ona akifyatua bastola.
Kwanza Von hakusikia maumivu. Alihisi kitu kikipenya kifuani na kuupapasa moyo wake. Kisha alisikia moyo ukiwaka moto. Akahisi kifo. Alipiga ukelele wa nguvu akichupa kumwendea Nuru mikono yake ikiwa wazi, tayari kumkaba koo. Lakini Nuru alimwepuka kwa urahisi na kumwongezea risasi nyingine ambayo ilimfumua fuvu la kichwa chake. Akadondoka chini na kulala kwa utulivu kama nguruwe aliyechunwa kwa maji ya moto.
Nuru aliyatazama matokeo ya kazi yake harakaharaka. Akaibusu bastola hiyo. Kisha akafanya haraka kujivika mavazi yake. Baada ya hapo alikimbilia kabati la Von ambalo alilifunua na kuanza kupekuapekua harakaharaka. Alipata alichokitaka. Ilikuwa ramani ya jengo hilo, ikiwa tofauti na ile waliyoitumia awali. Aliisoma himahima, kwa makini, kisha akaiweka mfukoni na kuuendea ukuta ambao ulikuwa na funguo nyingi. Akazichukua na kuziweka katika mfuko wake. Kisha, bastola ikimtangulia, alitoka chumbani humo mbio kama miguu yake ilivyoweza kumruhusu.

*********
Kuanguka umbali wa zaidi ya mita ishirini kutoka angani hadi juu ya sakafu ngumu sio mchezo. Bila ya uhodari wake wa karate na sarakasi, kama Joram asingefikia kichwa basi angefikia mgongo na kuvunjikavunjika. Lakini alijitahidi kusahau uchovu na maumivu makali aliyokuwanayo, akaikusanya akili yake pamoja na kubingirika. Hata hivyo, fahamu zilimtoka kwa dakika kadhaa.
Uhai ulipomrudia alifungua macho yake kwa taabu na kutazama pande zote. Aligutuka kujikuta akiwa amelala katikati ya mizoga mingi ya binadamu, baadhi ikiwa mifupamifupa, baadhi ikiwa imevimbiana, mingine ikiwa imeoza kabisa. Mara akapatwa na harufu kali ya kutisha, harufu ambayo iliambatana na mainzi mengi manene ya kutisha, ambayo yalikuwa yakirukaruka katika hali ya kushangilia mawindo haya rahisi. Licha ya mainzi hayo Joram aliwaona panya wakubwa mithili ya paka waliokuwa wakifanya karamu katika miili ya binadamu hao. Panya mmoja alikuwa akipita kumzunguka Joram huku akimtazama kwa namna ambayo ilionyesha kuwa alitamani kuanza kumla akiwa hai bado.
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 6





Moyo ulimdunda Joram. Ingawa hakujua au kupata kuhisi hofu katika moyo wake lakini kitu fulani kilimpanda moyoni na kumtia hasira na kichefuchefu. Alihisi kama aliyeruka jivu na kukanyaga moto. Kama kufa kwa nini afe kifo kibaya kama hiki? Afe huku anaona? Huku analiwa na panya? Kwa nini asingeruhusu lile dude limwue?
Kisha alijikaza kiume na kujikongoja kusimama wima. Ilikuwa baada ya kujikumbusha ule usemi wake wa mara kwa mara kuwa “Binadamu hufa kwa uzee, hufa kwa ajali, hufa kwa maradhi. Lakini kuna binadamu ambao hufa kwa uvivu vilevile, hasa katika shughuli hizi za upelelezi.” Wazo hilo lilimtuma aanze kutembeatembea humo akitafuta mwanya ambao ungeweza kumtoa nje ya kaburi hilo.
Alizitazama kuta na kugundua kuwa zilijengwa kwa chuma cha pua, zikiwa kama chumba kirefu chenye upana wa mita kumi kwa ishirini. Akatazama juu, akiangalia uwezekano wa kupanda hadi huko alikoangukia. Ilikuwa ndoto nyingine. Ukuta ulikuwa laini mithili ya kioo ambacho kingemshinda hata paka.
Afanye nini? Aketi kukisubiri kifo? Alijiuliza. Hapana, lazima ajitahidi kutafuta mwanya. Lazima kuna mahala pengine penye mlango unaotumiwa kuwaleta watu hawa kusubiri kifo. Akaendelea kutembea akiiruka mizoga na wakati mwingine kulazimika kukanyaga mifupa. Mainzi na panya vilimwongezea msukosuko kwa kukimbia hapa na pale, bila ya shaka kwa mshangao wa kuona mlo wao ukitembea ovyoovyo kwenda huko na huku.
Joram alichunguza kila ukuta kwa makini. Hatimaye, aliufikia ukuta uliokuwa na mlango wa chuma uliofungwa kwa nje. Alijaribu kuutingisha mlango huo bila ya mafanikio. Ulikuwa mlango imara kama ukuta huo. Akautia mkono wake mfukoni na kuitoa bastola yake ambayo aliilenga mlangoni na kuifyatua. Risasi iliugonga na kuanguka ardhini kama gololi. Hata bomu lisingeubomoa mlango huo, jambo lililomfanya Joram aduwae kwa mara nyingine akifikiri la kufanya.
Mara macho yake yakavutwa na maiti moja iliyokuwa ikitikisika. Akaisogelea na kuitazama kwa makini. Naam, ilikuwa na uhai mdogo mwilini mwake. Miguu yake ilikuwa imekatwa na Joram aliona vilevile kuwa jicho lake moja lilikuwa limeng’olewa. Huyu alikuwa mtu mweupe, kinyume cha wengi ambao walikuwa weusi. Bila ya shaka alikuwa Mrusi.
“Pole,” Joram alimwambia.
“Wewe ni nani?” mtu huyo aliuliza kwa udhaifu.
“Itakusaidia nini kunifahamu?” Joram alimjibu. “Unakaribia kufa.”
Mtu huyo alicheka kidogo kabla ya kujikongoja kusema polepole, “Kweli. Haiwezi kunisaidia chochote. Hata hivyo, naona wewe utakufa kabla yangu. Mwenzio hii siku ya kumi na nne bado naishi.”
Joram hakuona kama kuna umuhimu wowote wa kuendelea kumsikiliza mtu huyo aliyekaribia kukata roho. Lakini hakukuwa na jambo muhimu la kufanya na akaendelea kumsikiliza.
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 5


Haikuchukua muda kabla hajafahamu kuwa Mrusi huyo alikuwa mmoja kati ya watu wengi waliokuwa wakiuawa kinyama baada ya kushukiwa kuwa walikuwa wakifanya upelelezi dhidi ya utawala wa makaburu.
Pango hili lilichimbwa maalumu kwa ajili ya kuwaangamiza watu hao kwa siri baada ya mateso mengi. Wengi waliachwa na kufa kwa majeraha waliyoyapata, lakini adhabu kubwa iliyowaangamiza ilikuwa njaa.
“Usishanagae,” aliambiwa. “Ni njia pekee ya kutuwezesha kuishi.” Alipomwona Joram akizidi kushangaa aliongeza, “Au unaogopa kula maiti? Sikia, unaweza kunila nikiwa hai. Sina dalili ya kupona. Na ninavyokuona unaonyesha kuwa tuko pamoja katika kupambana na utawala huo haramu. Unaweza kunila ukaishi kwa wiki moja zaidi, pengine mwujiza utatokea nawe ukapona na kuendelea na pambano. Usiogope wala usinishukuru. Wala sitaki kujua wewe ni nani. Haitanisaidia.”.
Joram aliona kama angerukwa na akili endapo angeendelea kuketi hapo akimsikiliza mtu huyo ambaye ilikuwa dhahiri kuwa uhai mdogo aliobakiwa nao ulikuwa mdomoni mwake tu. Akaondoka hapo taratibu na kuurudia mlango huo ambao alitulia tena akiutazama kwa makini.
Bado hakujua angeweza kufanya nini kuufungua. Ingehitaji mwujiza. Harufu ya maiti hizo, kelele za panya na mainzi yaliyokuwa yakishangilia bahati zao, vilizidi kumsumbua. Joram alijua kuwa harufu na usumbufu huo vingemwua kabla hajasikia njaa.
Aliutazama tena mlango kwa uchungu na hasira. Akatamani apige magoti na kumwomba Mungu ili afanye mwujiza mlango ufunguke. Hilo hakufanya. Ingekuwa unafiki kwani hakuwa amemwomba Mungu walao kwa kumshukuru kwa miaka mingi sasa. Vipi amkumbuke wakati wa shida? Na vipi ategemee mwujiza mkubwa kiasi hicho wakati enzi ya miujiza ilikwishapita? Hii ilikuwa enzi nyingine, enzi ya kutumia akili na nguvu.
Bado hakuona kama alikuwa na lolote ambalo angeweza kulifanya kujitoa katika gereza hilo kwani kwa kila hali alijiona kama aliyefikia mwisho wa msafara wake kimaisha. Kwa mara ya kwanza alilaani bahati yake.
Si kwa hofu wala uchungu aliyoipata katika gereza hilo ambalo halikutofautiana na kuzikwa hai. Hasa alijilaumu kwa kuikosa fursa ya kujionea kwa macho yake mwenyewe utawala wa makaburu na raia wake watakavyotaabika pindi mitego aliyoitega itakapofyatuka na silaha ambayo waliiandaa kuwateketeza watu wasio na hatia itakapowageukia. Joram, kama alivyo, hakuna ambacho kingemsisimua zaidi ya hilo. Aone macho ya mshangao yanavyowatoka wakubwa wa utawala na machozi yaliyochanganyika na kamasi yanavyowatiririka juu ya mashavu yao meupe. Aone majumba yao makubwa waliyoyajenga kwa jasho la wanyonge yakiteketea na kubomoka kama milima ya barafu. Na hatimaye, aone setilaiti yao ikianguka katikati ya mji wao baada ya mitambo inayoiweka angani kulipuliwa. Ndiyo.
Ni hayo tu aliyoyahitaji Joram. Ni hayo ambayo yalimfanya ayahatarishe maisha yake kwa muda wote huu na hata kumwaga damu isiyo na hatia, ili, afanikishe dhamira yake. Hayo, kuyashuhudia kwa macho yake kungempendeza zaidi ya pesa na kumsisimua zaidi ya starehe. Kwa nini amekuwa hana bahati hiyo? Alijiuliza.
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 4



Kisha alimkumbuka Nuru. Kiasi hofu ikamrudia alipojiuliza kama atafanikiwa kunusurika katika mapambano haya. Alikuwa amempa maelekezo yote muhimu na kusisitiza wakati gani aanze safari ya kutoroka zake endapo asingemwona.
Bila shaka hakuna hatakayehangaika kumtafuta msichana mmoja ambaye hana tofauti na wasichana wengine wakati mamia ya watu yakiungua, maelfu yakikimbia kwa fujo na mamilioni yakiwa yamepigwa na butwaa, wakati majumba na viwanda vitakuwa vikiteketea kwa moto mkali ambao mfano wake haujapata kutokea katika historia ya nchi hii na dunia kwa ujumla, wakati chombo kisichoonekana kwa macho ya nguvu ya kawaida kitakuwa kikielea angani; na baadaye kuanguka; nguvu yake inayokifanya kielee angani na za madini inayokifanya kutoonekana zikiwa zimekwisha.
Hapana, Joram hakuona kama Nuru angeshindwa kuitumia fursa hiyo. Bila shaka baada ya kumchanganya kwa hila alipokuwa akimfuata, atayafuata maelezo yote.
Joram asingejisamehe endapo lolote lingemtukia msichana yule na kumpotezea maisha. Licha ya kwamba uzuri wa Nuru haukustahili kuharibiwa kwa mkono wa Kaburu yeyote katili, ushujaa wake ulikuwa nguzo ambayo Joram aliitegemea sana. Yote aliyoyatenda, hekima na juhudi za Nuru zilimsaidia. Mungu msaidie arudi salama, alimwombea.

Utulivu aliokuwa nao pindi akiwaza hayo ulimfanya panya mmoja amrukie kifuani na kujaribu kumwuma. Joram alimkwepa na kuliachia teke dhaifu ambalo panya alilikwepa vilevile. Hata hivyo, panya huyo alimfanya ayatoe mawazo yake nje na kuyarudisha katika pango hilo la mauti. Harufu mbaya ya binadamu waliooza ikamrudia tena akilini na moyoni. Akajisikia kutapika lakini akajikaza kisabuni.
Kisha alikumbuka kumtupia jicho jingine yule Mrusi. Akashangaa kuona kundi dogo la panya likiwa juu ya uso wake, wakimla. Kwanza alishangaa, kisha akaelewa. Mrusi huyo alikuwa amekata roho! Kichefuchefu kikamrudia tena Joram. Alitamani afumbe macho asiendelee kuona ukatili wa panya hao kumla mtu ambaye dakika chache walikuwa wakizungumza naye, mtu ambaye bila shaka ni mwema sana. Vinginevyo angewezaje kujitolea aliwe akiwa hai? Joram aliuliza.
Ghafla mwujiza ulitokea.
Joram aliuona mlango ukitikisika na hatimaye kufunguka. Yeyote ambaye angeingia Joram alitegemea kumlazimisha ama amwue kwa risasi ama amtoe chumbani humo. Hivyo, alisubiri kwa hamu akitazama kwa makini tayari kwa lolote, heri au shari.
Bastola ilichungulia ikiwa katika mkono wa kike. Ilifuatwa na uso mzuri, wenye jasho na damu. Uso wa Nuru.
“Joram?” alipiga ukelele wa furaha mara alipomwona Joram kasimama kando akimtazama.
“Naweza kuyaamini macho yangu?” Joram alimwuliza akiwa bado amesimama palepale. “Wewe ni Nuru kweli au malaika?” aliongeza.
Hakupata muda wa kujibiwa. Tayari Nuru alikuwa kifuani mwake kamkumbatia kwa nguvu huku akilia kwa sauti ndogo. Wakati ikimpambazukia Joram kikamilifu kuwa haikuwa ndoto – huyu alikuwa Nuru halisi aliyekuja kumwokoa – alianza kuinua mikono yake ili naye amkumbatie. Lakini Nuru tayari alikuwa amejitoa mikononi mwake na kumvuta nje harakaharaka huku akisema, “Twende zetu. Wakati umewadia.”
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 3



Joram alimfuata kikondoo.
Wakiwa nje baada ya kupigwa na hewa safi, fahamu zilimrudia Joram kikamilifu. Saa yake ilikuwa imevunjwa katika mapambano na jitu lile, aliitazama ya Nuru na kuelewa kwa nini aliambiwa wakati umewadia. Uhai ukamrudia mara moja rohoni, ingawa kimwili alikuwa bado dhaifu. “Niambie Nuru tafadhali. Niambie, mitego tuliyoitega haijafyatuka tu? Mji haujaungua?”
Badala ya kumjibu Nuru alimwambia, “Sikiliza.”
Kwa mbali mjini kulikuwa na kelele nyingi za hofu. Vilio na milipuko ya kutisha ilisikika kutoka katika kila upande. Walisikiliza kwa nusu dakika, kisha Joram alitabasamu na kusema polepole, “Nadhani inatosha. Wanakufa wenye hatia na wasio na hatia. Sasa iliyobaki ni ile kazi moja ya mwisho. Kuulipua huu mtambo.”
Alimshika Nuru mkono na kuanza kukiendea tena chumba cha mitambo. Nuru, akiwa na ramani halisi ya jengo hilo, alimshauri Joram wapitie wapi. Dakika mbili baadaye tayari walikuwa wamewasili katika chumba hicho.
Wahandisi watatu walikuwa chumbani humo, jasho likiwatoka kwa mshughuliko wa kutoelewa kinachotokea, hawakuweza kuwaona Joram na Nuru walioingia ghafla. Walipotanabahi walikuwa wakitazamana na bastola mbili. Wakaduwaa. Mshangao wao ulikoma pale risasi za mfululizo zilipopenya katika miili yao na kuwafanya waangukiane, damu zikiwavuja..
Joram aliikimbilia mitambo hiyo na kuanza kuikoroga kama alivyokusudia. Alipotosheka aliyatoa mabomu yake ya mkono na kuyatega sehemu mbalimbali za mtambo huo. Mara tu alipomaliza alimshika Nuru mkono na kutoka naye mbio.
Nje ya jengo, kwa mbali, waliona moto mkali uliokuwa ukipaa angani kwa namna ya kutisha. Kisha waliona kitu kingine cha kutisha. Kundi la askari wenye silaha likija mbio kiwandani huko.
Joram aliduwaa kidogo, akijiuliza wafanye nini. Kurudi ndani isingewezekana kwani jumba hilo pia lingelipuka wakati wowote. Na kukimbia ingewachukua hatua chache kabla ya kukamatwa na risasi za askari hao. Lakini Nuru, alijua la kufanya. Alimwongoza Joram katika upenyo alioutumia na Von hadi nje ya uwa ambako walipiga mbio wakitegemea kumkuta rubani akiwemo, ili wamlazimishe kwa bastola kuendeshwa kutoka nchini humo. Hakuwemo. Bila shaka “miujiza” iliyokuwa ikitokea ilimtia kiwewe hata akaondoka zake, au alikimbilia familia yake kwa matumaini ya kuiokoa. Hivyo, kiasi Nuru alikata tamaa. Lakini Joram alimrejesha matumaini alipomwamuru kupanda mara moja. Wakaingia.
Joram alikuwa na ujuzi wa nadharia juu ya kuendesha helikopta. Alilazimika kujikumbusha ujuzi huo kwa vitendo, jambo ambalo liliwagharimu zaidi ya dakika mbili. Wakati huo askari walikwishawaona na kuanza kuwafuata kwa nguvu zaidi.
Askari mmoja aliamua kutokimbia, badala yake aliilenga bunduki yake na kuiandaa kupiga.
 
SEHEMU YA MWISHO

COUNT DOWN - 2



Wakati huohuo jambo jingine la kushangaza lilitokea. Jumba hilo, ambalo lilikuwa hifadhi ya mitambo haramu lililipuka kwa mshindo mkubwa. Moto wa kutisha ulipanda juu na kusambaa kote.
Wakati askari hao walipokuwa wakitazama hilo, pia kwa mshangao, helikopta ilikuwa angani. Walipokumbuka kupiga risasi ilikuwa ikigeuzwa kuelekea Botwasana.

SURA YA KUMI NA MBILI

“… NA kama anafanya mauaji hayo kulipiza kisasi dhidi ya maafa ambayo utawala huu utayafanya katika nchi hii saa chache zijazo, bado si kitendo cha kujivunia sana, kwani haitasaidia kitu,” Kombora alinong’ona. Alikuwa akisema peke yake, akiwa kimya katika ofisi yake.
Hayo yalimtoka mara baada ya kutazama televisheni na kusikia habari za kutatanisha kutoka BBC, bila shaka zikiwa zimekuja kutoka Afrika Kusini bila hiyari ya utawala huo, kwamba Joram alikuwa ametoweka kutoka katika jumba alilowekwa nchini humo. Kwamba mauaji ya ajabuajabu dhidi ya makaburu katika nchi hiyo yalitokea usiku huo. Na kwamba kulikuwa na mashaka kuwa mwuaji au wauaji hao hawakuwa wengine zaidi ya Joram na Kiango na yule msichana anayefuatana naye, Nuru.
Habari hizo, zikiwa zimewasili pindi vyombo vyote vya habari nzito zaidi ya hiyo zilipokelewa kama habari ndogo na kupuuzwa mara moja. Kwa wananchi wa Tanzania na nchi nyingine ambazo zilikuwa mashakani zikisubiri maafa makubwa kwa hofu na mashaka makubwa, walizipokea kwa shangwe na vigelegele kwa dakika mbili tatu, dakika zilizofuata ikawa imesahauliwa. Hofu ikachukua nafasi yake. Wakaendelea kusubiri, kusubiri kifo.
Waumini wa dini walikisubiri kifo katika makanisa na misikitini. Wakristo walichubuka magoti kwa sala ndefu zilizoambatana na vilio. Waislamu walivunjika migongo kwa kwenda rakaa huku wakimlilia Mola. Wasiomjua Mola walikisubiri kwa namana mbalimbali. Wako waliotulia kwa utulivu, wako waliopiga kelele na kuna wachache ambao waliamua kufa wakiwa wamelewa; hivyo, chochote walichokuwa nacho walikitumia kununulia pombe. Watoto ambao walipata hisia fulani kutokana na tofauti katika tabia za wazazi wao walitulia kimya, kwa mara ya kwanza maishani mwao wakionja ladha ya hofu. Hata wanyama wanaofugwa, kama kuku, mbwa, mbuzi na ng’ombe hawakuwa katika hali ya kawaida kwani ilikuwa siku yao ya kwanza ambayo hawakushuhudia binadamu akila mayai, kuchinja mbuzi wala kumkamua ng’ombe.
Jeshi liliwekwa katika hali ya hadhari, tayari kwa lolote ambalo lingeweza kutukia. Lakini kwa vile madhara hayo yalikuwa hayafahamiki yangetokea upande upi, na silaha ipi ingeweza kuyazuia, ilikuwa dhahiri kuwa jeshi hilo lisingeleta upinzani wowote. Ilikuwa kama waliowekwa tayari kusubiri kifo.
Rais na mawaziri wake, pamoja na viongozi wa ngazi za juu katika Chama walijiinamia juu ya viti vyao vya Ikulu. Mengi yalikuwa yamesemwa, mengi yalifanywa, lakini halikuwepo lolote lililoelekea kuwa kipingamizi kwa maafa yaliyokuwa yakiendelea dakika baada ya dakika. Wao pia ilikuwa kana kwamba waliamua kusubiri kifo kwa pamoja. Mara kwa mara walitazama saa zao kisha wakatazamana. Kisha kiongozi mmoja aliinuka baada ya kumnong’oneza jirani yake kuwa anakwenda haja. Hakurudi. Mwingine aliondoka taratibu kwa madai hayohayo. Yeye pia hakurudi. Yuko ambaye alikwenda moja kwa moja msikitini. Kuna aliyekwenda kanisani. Mwingine alikwenda nyumbani ambako aliungana na familia yake, kusubiri kifo.


Tahamaki Rais alijikuta kabaki na Waziri wake Mkuu. Walitazamana kwa muda, kisha mmoja aliyaepuka macho ya mwenziwe, wakizitazama saa zao. Zilisalia dakika tano tu. Wakatazamana tena. Wakazitazama tena saa zao. Dakika tatu… Dakika mbili… mmoja alimsika mwenziwe akiguna. Mwingine aliinuka akiwa kaloa jasho ambalo hakufahamu lilivyoishinda air conditioner ambayo ilikuwa ikifanya kazi kikamilifu. Kisha aliketi tena na kuyafumba macho yake.
Dakika moja…

******
Dakika yoyote kuanzia sasa! Kombora aliwaza akitoka dirishani alikokuwa akichungulia na kukirudia kiti chake. Alikuwa ameamua lolote ambalo lingetukia limkute katika ofisi yake. Hakuiona haja ya ya kutaabika wala kwenda kushuhudia maisha yanavyowatoka wanawe endapo nyumba yake ingetukia kuwa moja kati ya nyumba zisizo na bahati.
Mara mawazo ambayo hakutaka yamjie akilini yakamtoka. Mawazo ya upweke, unyonge na msiba mkubwa, mawazo ambayo yalikuwa yakimfunulia hali ambayo angekuwa nayo endapo ingetukia yeye kuwa mmoja kati ya wale watakaosalimika na familia yake nzima kuteketea. Angeishi vipi bila ya mama watoto wake, yule mwanamke mpole ambaye hajaacha kumwonea haya kwa kiwango kilekile walipokuwa wachumba hadi leo ambapo wamekuwa pamoja zaidi ya miaka thelathini. Angeishi vipi bila ya watoto wake wanne, mmoja akiwa mwanamume ambaye amehitimu Chuo Kikuu na kuajiriwa mwaka jana na wale wa kike ambao wote wameolewa na kumpatia wajukuu watano? Maisha yangekuwa vipi endapo yote hayo yangebadilika ghafla kwa ajili ya ukatili wa utawala dhalimu wa weupe wachache huko kusini?
Kisha alikumbuka saa yake. Dakika kumi zilikuwa zimepita! Hakuyaamini macho yake. Akayainua na kupiga hatua mbili tatu kuliendea dirisha. Akachungulia chini. Mitaa yote ya Dar es Salaam ilikuwa imetulia kabisa. Kelele ndogo zilisikika kwa mbali kutoka katika viwanda kadhaa ambavyo vilikuwa vikiendelea na kazi. Kombora aliirudia meza yake na kuketi. Masikio yake yalikuwa wazi yakisubiri kwa hofu kudaka mlio wowote wa mashaka ambao ungesikika. Macho pia yalikuwa wazi yakitazama angani kupitia dirishani.
Dakika ishirini!.
“Wakati wo…” alitaka kutamka. Sauti yake ilikatizwa na ukelele wa ghafla ambao ulivuma ghafla katika anga. Bila ya kutegemea aliyafumba macho yake kwa nguvu na kutamani kuweka vidole masikioni ili asisikie zaidi. Kelele ziliendelea kwa mvumo mkubwa zaidi. Hisia zilimfanya Kombora adhani kuwa zilikuwa kelele za kushangilia badala ya vilio na maombolezo kama alivyotarajia. Akasikiliza kwa makini zaidi. Naam. Watu walikuwa wakipiga vigelegele na kucheka kwa nguvu.
Watu wote!
 
Back
Top Bottom