STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 28:
Nchi nzima iliingia kwenye taharuki kubwa isivyokuwa kawaida kusikia kwamba mheshimiwa waziri wa ardhi ndiye aliyekuwa nyuma ya hiyo mipango yote. Kabla ya tukio hilo kuweza kutokea mwanaume huyo alikuwa ni miongoni mwa viongozi bora sana ambao nchi ilikuwa ikijivunia sana kuwa nao, sasa kivipi tena iwe ndiye yeye anayehusika na hayo mambo? Watu hawakuwa na namna kwa sababu walijua kwamba wanasiasa sio watu wa kuwaamini sana huwa wanabadilika kila sekunde moja iendayo wakijawa na maneno mengi sana mdomoni.
Hali ilikuwa hivyo pia hata kwa mrembo Sarafina, mtoto wa waziri mkuu. Alikumbuka vyema sana kwamba mwanaume huyo ndiye ambaye baba yake alimkutanisha naye na kuanza kufanya naye kazi yeye akiwa kama mkandarasi wa taifa, huyo ni miongoni mwa mawaziri ambao alikuwa akifanya nao kazi kwa ukaribu sana akiwepo pia na waziri wa ujenzi, hivyo alishangazwa sana na hizo habari ambazo aliweza kuzisikia. Aliamua kuifunga safari na kwenda mpaka nyumbani kwa waziri huyo ili kwenda kuzipata taarifa sahihi za nini kilitokea.
Alifanikiwa kufika nyumbani kwa waziri huyo lakini kitu cha ajabu ambacho alikutana nacho ni walinzi waliokuwa wengi sana ndani ya lile eneo, hakuamini baada ya kuambiwa kwamba familia hiyo imehamishwa kwa siri mpaka pale mambo yatakapo tulia ili isije kupata madhara ina maana kama baba wa familia alikuwa ni gaidi huenda kuna wengine ambao walikuwa naye wanaweza kuidhuru familia hiyo hivyo kwa usalama wao wameamua kuwahamisha ili mambo yakitulia iweze kurudishwa tena. Basi hakuwa na namna zaidi ya kuondoka.
Calvinjr, majira ya asubuhi na mapema baada ya kuisikiliza taarifa kutoka kwa mheshimiwa raisi aliwahi nyumbani kwa dada yake ambaye alikuwa bado anauguza kidonda chake tumboni baada ya kupigwa na kisu ndani ya jiji la DOGMA TULIPO. Mwanaume huyo alifika na kuingia mpaka ndani ambapo dada yake alikuwa amekaa sebuleni akionekana kuangalia runinga.
“Nilimshangaa sana huyo mwanaume ambaye alikuwa na jeuri ya kumgusa dada yangu na kufanikiwa kukizamisha kisu kwenye tumbo lake, kama ningefanikiwa kukutana naye basi huenda ningemfanyia kitu kibaya sana ambacho asingesahau kamwe kwenye maisha yake” aliongea akiwa anasogea kwenye friji na kuchukua maziwa kama ilivyokuwa kawaidea yake.
“Wewe ndo mwanaume kwenye familia na unakuwa goi goi namna hiyo utaweza kutulinda wewe kweli? Ilibaki kidogo tu ungempoteza dada yako?”
“Mhhhh dada hivi una uhakika kwamba mimi ni goi goi au wewe ndiye hunijui mimi vizuri?”
“Kwenda zako huko, unataka kuniambia kwamba mimi simjui mdogo wangu niliye muachia ziwa? Haya niambie ni kipi kimekuleta na asubuhi yote hii kwangu?”
“Hivi kinacho endelea wewe unakiamini sis?”
“Hapana kwanini unauliza?”
“Ukimwangalia vizuri Yule mke wa waziri wakati anaongea pale unajua kabisa kwamba ni mtu ambaye amelishwa maneno ya kuzungumza tena akiwa na hofu kubwa sana”
“Kwahiyo unataka kusemaje?”
“Inatakiwa nimtafute Yule mwanamke niongee naye”
“Calvinjr”
“Usijali sana mimi nitaongea naye mwenyewe”
“Hautakiwi kuongea naye kwa sasa?”
“Kwanini?”
“Muda huu zinahitajika akili zaidi kuliko haraka, inatakiwa kwanza tujue kama je waziri naye alikuwa ana uhusika kwenye haya matukio au kauziwa tu kesi, na kama anahusika kweli ni lazima basi tujue kwamba je yeye ndiye alikuwa kiongozi wa haya yote au katolewa tu sadaka?. Hapo ndipo tunaweza kujua kwamba tunatakiwa kuanzia wapi ila sio kwenda kwenda tu, tunaweza kuleta madhara ambayo siyo.”
“Una uhakika na unacho kisema?”
“Ndiyo, kwa sasa tunatakiwa tukae kwanza pembeni tuangalie ni kipi kinaendelea ili tujue kama kuna dalili za jambo lolote lile kutokea”
“Mhhhhh, sidhani kama hilo ni wazo zuri, adui ukimpa muda mrefu zaidi wa kujipanga, atakuwa na nguvu kubwa sana ya kuweza kukudhibiti wewe ila kama ukimtafuta akiwa naye anaendelea kujipanga inakuwa ni rahisi sana kukabiliana naye, tunavyo endelea kusubiri sana hili jambo litakuwa na madhara makubwa sana. Kama mambo yangekuwa kama unavyosema wewe hivyo ; haujiulizi inakuwaje mpaka kila mpango ambao tunaupanga wa siri watu hao wanakuwa wanajua hatua zetu? Wanajuaje? Unahisi ni waziri tu ndiye ambaye alikuwa anaweza kulifanya hili? Waziri hana hayo mamlaka ya kuweza kuzichuja taarifa za mamlaka za usalama angalau hata kama angekuwa waziri wa ulinzi ingeniingia akilini”
“Calvin kuna muda kumpa adui nafasi ya kuona ameshinda mchezo huwa ni njia rahisi sana ya kuweza kumshinda kwani atahisi kwamba amefanikiwa kuwafanya watu wote waonekane hawana akili hivyo anakuwa anajihisi yupo huru kila sehemu. Hiki walicho kifanya mimi sina imani nacho sana ila nahisi kama wanaigiza basi wamechukulia kwamba nchi nzima ina watu wapumbavu wasiokuwa waelewa hivyo wanaweza kuwafanya kila wanacho jisikia wao na muda wanao taka wao. Kama kuna chochote huu ndio utakuwa muda wetu mzuri zaidi wa kujua tunaanzia wapi”
“Okay” Calvin aliondoka kishingo upande kwa sababu maneno ya dada yake hayakumuingia sana ila hakuwa akipenda kubishana na dada yake huyo hivyo akaamua kuondoka.
Baada ya siku kadhaa kuweza kupita, mheshimiwa waziri aliweza kufikishwa mahakamani na kusomewa mashataka yake ambayo alikiri kuhusika na tukio hilo huku akimuomba msamaha mheshimiwa raisi kwa kuweza kumuangusha kwenye nafasi aliyoweza kumpa pamoja na kuwaomba wananchi wa Tanzania msamaha kwa kuweza kushindwa kukitimiza kile kiapo ambacho aliweza kukiapa. Waziri huyo alinyongwa mpaka kufa huku serikali ikiahidi kuwatafuta wale wote ambao alishirikiana nao kwa maana wengi walikuwa ni vijana wake na walikuwa wanajuliakana kwamba ni wapi wapo.
Kifo cha mheshimiwa huyo kilirejesha amani na furaha kwa wananchi kwa asilimia nyingi sana, watu walirejea kwenye majukumu yao ya kila siku huku wakiendelea kuyapambania maisha yao kama ilivyokuwa mwanzo kwani jambo hilo lilileta taharuki kubwa sana nchini. Ila kwa upande wa Calvinjr hakuwa tayari kuliacha hilo jambo lipite kwa maana kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa ni kikubwa sana na alishangaa mno baada ya kuona kinaisha kirahisi sana namna hiyo, hivyo aliandaa mpango wa pekeyake kuweza kuwatafuta watu wote ambao alihisi kwamba huenda ndio walikuwa ndani ya mpango huo pamoja na huyo waziri ambaye alikuwa amenyongwa.
Jioni moja baada yamiezi kadhaa kupita alienda kukutana na mkurugenzi wake wa shirika la kijasusi, alikuwa ana mazungumzo naye ya mhimu sana ambayo aliona yanaweza kuwa msaada mkubwa sana kwake.
“Kipi kimekufanya tukutane jioni hii ya leo?”
“Mkuu kuna jambo nataka nikuulize lakini pia nahitaji sana msaada wako”
“Lipi hilo?”
“Hivi haya mambo yote yaliyo tokea unayaamini na umeamua kuyaacha yapite?”
“Vipi kuna kitu umekihisi labda?”
“Hapana mkuu”
“Calvinjr nisikilize vizuri sana, hii nchi inaongozwa kwa miongozo maalumu, sio kwamba unaweza kujipangia namna ya kuyafanya mambo kwa sababu umeamua tu na kujisikia. Kila kitu ambacho kinafanyika kwenye nchi hii kinatoka kwenye kimywa cha mheshimiwa raisi kwa sababu yeye ndiye mtu mwenye kauli ya mwisho kabisa. Hata mimi nilikuwa nina mashaka sana na haya mambo, mimi nimeanza kufanya kazi kabla hata wewe haujazaliwa hivyo najua namna michezo ya siasa inavyokuwa inafanyika”
“Nina uhakika Yule waziri hana hatia ila kuna watu wapo pembeni wamejua tu kuzichanga karata zao vyema na kwa wakati huu wameshinda mchezo japo wametumia mbinu ya kitoto sana ila ndio washindi. Mimi nilimfuata mheshimiwa raisi ili kumweleza haya kwamba huenda kwa nyuma kuna michezo ambayo inaendelea lakini sijui hawa watu wamemuingiaje mheshimiwa raisi mpaka naye akawaamini, nahisi ni kwa sababu yeye alikuwa amechanganyikiwa na hajui atawaambia nini wananchi hivyo alivyopata wazo ambalo aliona litamtoa yeye kwenye lawama hakuwaza mara mbili akaamua kulipokea”
“Watu ambao wanaonekana wapo nyuma ya hili jambo wanaonekaan kuwa ni watu wenye nguvu mno, kumfanya waziri kama Yule akubaliane na wewe lazima nyuma yake kunakuwa kuna nguvu kubwa sana au kuna kitu kikubwa ambacho kinatumika kumfanya mtu akubali kila kitu ambacho anakuwa anakisiliza. Mheshimiwa raisi aliniambia kwamba niachane na haya mambo kwani yameisha salama tusije tukazusha mengine yakamharibia madaraka yake, kama mhusika kakubali kuhusika basi hakuna namna zaidi ya kuyateketeza magenge yake yote na hiyo ndiyo kazi ambayo inafanyika kwa sasa” mkurugenzi Gulamu Leopard alimweleza kijana wake yale ambayo hakuwa akiyajua kwamba hata yeye hakuwa na uhakika kabisa na hayo mambo ila hakuwa na cha kufanya.
“Kwahiyo mheshimiwa yeye anacho kiangalia ni nafasi yake tu?”
“Hivyo ndivyo siasa ilivyo bwana mdogo”
“Sasa kwanini ulikubaliana nae kirahisi sana hivyomkuu?”
“Mimi sijakubaliana naye kirahisi, ndani ya nchi hakuna mtu mwenye huo uwezo wa kukubaliana na raisi kwa sababu sisi tunaishi kwa kufuata amri yake hivyo anacho kiongea sio makubaliano bali ni amri ambayo utake usitake ni lazima uifuate na hii ni nchi yake, anafanya anacho kitaka yeye mpaka muda wake uishe”
“Kwahiyo hata kama anakosea mahali hatakiwi kurekebishwa?”
“Ngoja nikukumbushe kitu bwanamdogo, kwenye nchi hii wamewahi kutokea wazalendo ambao ulikuwa ukiikata miili yao tu inatoka damu yenye rangi ya bendera ya nchi hii. Wale watu ulikuwa ni mfano mzuri sana na kama alama nyingine ya ushindi wa taifa hili, walipigana pale ilipo wabidi, walipambana na kila namna ya udhalimu ili tu kuiweka nchi kwenye hali ya usalama ila walikosea sehemu moja tu pekee. Walikosea kuanza kuwagusa viongozi wakubwa, kwenye siasa tunaamini kwamba raisi hakosei bali huwa anapitiwa tu au kutingwa na majukumu ambayo yanamfanya achanganye baadhi ya mambo ambayo yanakuwa hayaendi sawa na hata mkitaka ayabadilishe mnatakiwa kwenda kumuomba na sio kufanya makubaliano”
“Kitu ambacho unatakiwa kukiweka akilini ni kwamba Yule ndiye amiri jeshi mkuu wan chi hii, yeye ndiye mtu anaye sikilizwa na kila mtu haijalishi wewe una cheo gani, yeye ndiye anaye toa amri kwa watu wote ndani ya nchi. Kwenda naye kinyume ni kwamba umeiasi nchi,anaweza kukufuta kazi muda huo huo na kukupatia kesi nzito na akatoa mwenyewe amri ya hukumu unayotakiwa kuipata, je unahisi bado unaweza kupingana na maamuzi yake? Raisi hata kama akiwa mtu wa hovyo, akiwa mtu ambaye anakurupuka kufanya maamuzi, akiwa ni mtu asiye na maono ya mbali, kitu pekee ambacho unatakiwa kukiweka akilini ni kwamba; Yule amechaguliwa na wananchi kukaa IKULU na hao hao wananchi ndio wana uwezo wa kumtoa IKULU na sio wewe pekeyako, nadhani sasa unanielewa vyema”
“Ndiyo mkuu, nimekuelewa ila mimi sikuhitaji tumhusishe raisi katika hili?”
“Whaaaat?”
“Hili jambo nahitaji nilifanye pekeyangu, hata dada yangu sijue kabisa”
“Una mpango gani?”
“Nina uhakika kwa asilimia miamoja kwamba huyu waziri hahusiki kwa lolote”
“Kipi kimekufanya uamini hivyo?”
“Nilimwangalia sana kwa makini mkewe akiwa anaongea mbele ya vyombo vya habari, alionekana kuongea kwa simanzi sana, inamaana hakupenda alichokuwa anakifanya, sasa kwanini asikipende? Huenda anajua anaongea uongo wa kumpeleka mumewe sehemu mbaya na hata yale maneno yake anaonekana kabisa kwamba amelishwa na mtu aweze kuyaongea. Jambo lingine nimekuja kugundua siku ile namuona mumewe akiwa anaongea mahakamani, ni mtu ambaye alikiri kuhusika lakini ukiangalia uso wake ulikuwa unaonyesha kabisa kwamba unapingana na yale maelezo ambayo alikuwa anayatoa hivyo naye alidanganya kama mkewe”
“Kwahiyo unataka kusemaje?”
“Yule mtu hahusiki kabisa na hili tukio”
“Kipi kimekufanya uhisi upo sahihi?”
“Unakumbuka uliwahi kunifundisha kwamba udhaifu wa mtu upo kwenye kile kitu ambacho anakipenda sana”
“Ndiyo, sasa hilo linahusikaje hapa”
“Familia ya waziri iko wapi?”
“Unataka kusema kwamba huenda wametumia familia yake kumfanya akubali kila kitu?”
“Ndiyo mkuu”
“Ooooh shiiit!” mkurugenzi aliongea akiwa anatabasamu na kumpiga piga Calvinjr mgongoni, alimtengeneza mtu ambaye alikuwa anawaza mbali sana.
“Kwahiyo unahitaji nini?”
“Najua wewe hakuna taarifa ambayo hauna ndani ya nchi hii, naomba unipe location ya sehemu ilipo hiyo familia”Calvinjr aliongea kwa kumaanisha sana akiwa ana imani kwamba huko angeenda kuupata ukweli wa kutosha ambao utawafanya wapate majibu ya maswali yao.
“Hakikisha haukamatwi huko unako enda na kama ikitokea umeamua kuua, usiache alama kabisa huko kwa maana mtu ambaye alikuwa ana uwezo wa kuua kama wewe aliwahi kuuawa miaka ya nyuma huko hivyo kama ukifanya hivyo utazua taharuki mpya na vyombo vingi vya usalama vitaanza kuweka jicho la umakini sana, fanya mauaji ya kawaida tu usiache alama yoyote ile” Mzee huyo alikubali kumpa location ya eneo ambalo ilikuwepo familia hiyo huku akimsisitiza kijana wake huyo asiende kufanya mauaji ya kikatili huko ambako alitakiwa kwenda kuichukua familia hiyo kwa maana ilikuwa chini ya ulinzi wa jeshi hivyo kuipata kwake ilitakiwa kutumia mabavu na kuondoka na familia hiyo ambapo wangeitumia kuweza kuupata ukweli.
“Asante sana bosi”
Kichaa kapewa rungu na kiongozi wake, nini anaenda kukifanya? Kumbuka huyu hajulikani kabisa, alikuwa ni jasusi wa siri sana hivyo eneo lolote ambalo angepatikana ingekuwa ni hatari sana kwake alitakiwa kujilinda mno.
Unahisi ni kwanini kiongozi wake alimsisitiza kutofanya mauaji ya kikatili, kuna nini nyuma ya huyu kijana? Na huyo anayesema kwamba aliwahi kufanya mauaji ya kikatili huko nyuma ni nani? Episode ya 28 inafika mwisho.
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app