KABURI LA MWANAMUZIKI EP 12
Mtunzi: Robert Heriel
0693322300
Nilifanikiwa kuingia ndani ya ile Boti pasipo kushtukiwa, nikazama upande wa ndani kimyakimya mithili ya chui awindaye. Nikajibanza kwenye moja ya kona mule ndani, nikipima utulivu wa eneo lile, palikuwa kimya taa ya rangi nyekundu ikitoa nuru hafifu katika kona ile, nikaifuata korido fupi ambayo mbele yake ulikuwepo mlango uliokuwa umefungwa, nikashika kitasa cha ule mlango kisha nikapeleka sikio mlangoni, bado kulikuwa tuli, nikaingiwa na wasiwasi isijekuwa ni mtego, nikafikiri huenda wameshaniona hivyo wameniwekea mtego, lakini nikajipa ujasiri na kupuuzia wazo hilo. Nikakitekenya kitasa cha mlango polepole, mlango ukafunguka pasipokutoa sauti, nikapokelewa na chumba kingine ambacho kilikuwa na samani kama masofa, meza ya kioo, luninga kubwa, Jokofu la milango miwili, chini palikuwa na vigae vya mbao, Luninga ilikuwa ikionyesha muziki uliokuwa ukiendelea. Nikapiga hatua kwa tahadhari huku nikiendelea kusahili chumba kile. Sikuona jambo la maana nikaufikia mlango mwingine ambao ulikuwa umefungwa, hapo nikachungulia Kupitia tundu lililokuwa usawa wa macho yangu kwenye ule mlango, nikashtuka kumuona Dora na wanaume watatu, mwanaume mmoja alikuwa anaasili ya Kiarabu, pamoja na vijana wawili, walikuwa wamekaa wakiwa wameizunguka meza fupi ya kioo Dora na yule mwanaume wa kiarabu walikuwa wamekaa upande mmoja, huku wale vijanaa wawili wakiwa wamekaa upande wa pili wa ile meza ambayo juu yake kulikuwa na begi mfano wa Briefcase,
Nilipokaza jicho langu vizuri, nikamtambua moja wa wale vijana alikuwa ni Stelini Kaboga, nilimkumbuka kwa sababu alikuwa miongoni mwa washindi wa shindano la Tanzania Got Talent tena ndiye aliyeshika nafasi ya pili, Nikawa najiuliza, Stelin anafanya nini kwenye hii Boti, anamahusiano gani na Dora, vipi huyu muarabu ni nani, sikutaka kumfahamu sana yule kijana mwingine, hata hivyo macho yangu yakatua katika lile begi, “ Kuna nini ndani ya lile begi” Nikawaza, nikaingiza mkono mfukoni nikatoa Kalamu maalumu yenye kamera kisha, nikaiweka kwenye kile kitundu na kuanza kurekodi matukio nikiwachukua wahusika bila ya wao kujua. Baada ya kuridhika kurekodi kilichokuwa kinaendelea, nikairudisha ile kalamu mfukoni. Nikachungulia tena, hapo nikawaona wakicheka, kisha yule muarabu akaweka simu sikioni wengine wakakaa kimya, akaongea kwa dakika moja kisha akakata simu. Sikuwa nawasikia walichokuwa wanazungumza.
Nikawa nakisahili kile chumba walichokuwamo, kilikuwa chumba kikubwa cha wastani, chenye dirisha moja, alafu mbele kabisa kulikuwa na mlango niliokuwa natazamana nao. Punde mlango wa kile chumba nikaona ukifunguka, alafu akatokea mwanaume ambaye nilimkumbuka ndiye aliyembeba Dora mgongoni kumpandisha kwenye Boti kule Bwejuu.. Wakanyanyuka wale vijana, Stelini akabeba lile Begi kisha wakamfuata yule Mwanaume, Mlango ukafungwa, akabaki Dora na yule mwanaume wa Kiarabu. Wakawa wanazungumza lakini sikuweza kusikia chochote. Punde nikahisi kama Boti imesimama, nikaangalia huku na huku kwenye kile chumba nilichokuwepo, nikaona dirisha lenye pazia, nikalisogelea dirisha na kuchungulia kwa nje, kulikuwa na giza, tayari usiku ulikuwa umeingia, nikaangalia saa yangu ya mkononi, ilikuwa saa nne kasoro ya usiku, eneo lile lilikuwa kama kuna kisiwa, nikatoa hadubini”binocular” mfano wa bomba la makapeni, nikaiweka kwenye jicho moja, natazama nikaona kwa mbali nyumba nzuri yenye mfano wa Hoteli hivi, ikiwa inawaka mataa yenye kupendeza, alafu kulikuwa na vijumba vizuri vya msonge visivyo na kuta vyenye mapaa ya makuti kama Uyoga, chini yake kulikuwa na vitanda vya fukweni ambavyo juu yake walikuwa wamelala watu jamii ya kizungu, wake kwa waume wakila raha na kustarehe. Nikahamisha macho yangu upande mwingine nikaona majiko ya nyama choma yakiwa na nyama zilizotengenezwa vizuri pamoja na mishikaki, wakiwepo wapishi watatu waliokuwa wamevaa Aproni nyeupe na makofia meupe ya upishi. “ Kisiwa hiki kitakuwa kinaitwaje?” Nikawa najiuliza, niliamini kuwa pale sio Zanzibar ila ni moja ya vijisiwa vilivyopo karibu na Zanzibar.
Punde nikashangaa kuona boti ndogo ikiwasili katika kile kisiwa, nikashtuka kumuona Stelini na yule kijana wakishuka kutoka kwenye ile Boti wakiwa na lile Begi, kabla sijafikiri zaidi, nikashtuka Boti niliyoipanda ikianza kuondoka. Nikajua kuwa ilisimama ili wale kina Stelini na yule kijana washuke. Nikarudi kwenye ule Mlango, nikashtuka nilipochungulia, Dora na Yule Mwarabu hawakuwepo, akili yangu ilikosa utulivu, nikafikiri huenda nao walishuka. “ Nimefanya uzembe” Nikawaaza. Nikafungua mlango kisha nikatokea kwenye kile chumba walichokuwepo Dora na Yule Muarabu, hapakuwa na jambo lolote la maana, nikasonga kwenye mlango uliokuwa ukinitazama, nikaufungua kwa tahadhari huku nikipima utulivu wa upande wa pili, kulikuwa kimya, nikafungua mlango na kupokelewa na chumba mfano wa chumba nilichotoka, lakini chumba hiki kilikuwa na milango miwili, Mlango wa kwanza ulikuwa mbele yangu ukinikabili, Mlango wa pili ulikuwa upande wa kushoto; huu ulikuwa karibu zaidi kama hatua moja kutoka pale nilipokuwa nimesimama, kabla sijaamua nini nifanye, nikasikia miguno ya mahaba ikitokea katika ule mlango wa kushoto, ilikuwa sauti ya yule muarabu pamoja na Dora, nikaufungua kwa tahadhari pasipo ya wao kujua, macho yangu yaliingiwa na haya yalipotuama kwenye miili iliyokuwa uchi ikiwa inafinyangana kwa mahaba mazito, walikuwa katika sayari nyingine, sikutaka kuangalia yasiyo nihusu, pale chini nikaona nguo zao walizokuwa wamezitelekeza ungedhani hawatozihitaji tena, Lilikuwa gauni, chupi na brazia ya Dora, pamoja na suruali, boxer na Tsheti ya yule muarabu. Akili yangu ikaniamuru nikaipekue ile Suruali, Nikainama na kuanza kutambaa kama nyoka kuzifuata zile nguo pale chini, nilipokaribia nikamsikia Dora akizidisha sauti ya miguno hali hiyo ikanifanya moyo wangu kupiga sana,nikaifikie ile Suruali, nikaishika lakini kabla sijaipekua, macho yangu yakauona mguu wa Dora ukishuka chini, nikajiviringisha upesiupesi pembeni kuelekea chini ya uvungu wa kitanda bado nikiwa na ile suruali ya Muarabu.
Nikiwa mwanzoni mwa uvungu wa kitanda, Nikauona mguu wa dora ukikanyaga chini, kisha mguu wake mwingine ukafuata, nikabinya pumzi yangu huku nikiituliza akili yangu. Dora alikuwa akilalamika kuwa amechoka, lakini yule muarabu akawa anambembeleza waendelee. Nikaipekua mifukoni, nikapata simujanja ya yule Muarabu, upesiupesi nikaipigia simu yangu iliyokuwepo nyumbani kwa kutumia namba ya muarabu, baada ya simu kuita nikakata, kisha nikaenda sehemu kwenye setting ya simu, nikachukua Imei namba ya ile simu ya muarabu, nikajitumia ujumbe wenye Imei namba, kisha nikafuta ile meseji, kisha nikafuta pia kumbukumbu ya nilivyojipigia, kabla sijairudisha simu kwenye suruali nikashangaa kuona suruali ikivutwa, upesi nikajisogeza zaidi chini ya uvungu, huku tayari nikiwa nimeshaitoa bastola yangu na kuishika mkononi.
“ Leo umenikatili sana Dora” Yule Muarabu akasema, akiwa anavaa nguo zake. Dora hakumjibu, naye alikuwa akivaa nguo.
“ Tumeshakaribia Kufika Dar, Hakikisha mipango yetu inaenda kama tulivyopanga, unafahamu tupo nje ya wakati?” Muarabu akasema,
“ Nitakujulisha kila kitu kitakachoendelea, mipango yetu inaenda sawasawa, sioni sababu ya wewe kuwa na hofu” Dora akajibu akiwa anamalizia kufunga brazia yake.
“ Simu yangu iko wapi?” Muarabu akasema, huku akijaribu kuhangaika huku na huku kuitafuta. Maneno hayo yaliamsha mapigo yangu ya moyo, nikaishika vizuri bastola tayari kwa kupambana, nilidhamiria kuwa yeyote atakayeinama kuchungulia chini ya uvungu wa kitanda; nitakipasua kichwa chake kwa risasi.
“ Labda umeiacha kwenye kile chumba cha kikao” Dora akasema akiwa tayari amevaa gauni lake. Muarabu akatoka akamuacha Dora mule chumbani, mimi nikiwa bado chini ya uvungu, nilijua kuwa endapo ataikosa simu kule kwenye chumba cha kikao kitakachofuata ni kuipigia, kwa upesi nikasogea polepole mpaka mwanzoni mwa uvungu nikamchungulia Dora, nikamuona akijitazama kwenye kioo akiwa anajiweka sawa, kabla sijafanya jambo lolote nilishtuliwa na sauti ya mlango ukifunguliwa na Muarabu akatokea huku akisema;
“ Hata kule haipo”
“ Haipo! Ngoja niipigie” Dora akasema huku akichukua simu yake kutoka kwenye Mkoba wake, akabonyeza bonyeza, kisha akaweka Louderspeaker, punde simu ya Muarabu ikawa inaita, macho yao kwa pamoja yakaangalia chini, wakaiona ikiwa karibu na nguzo ya kitanda ikiwa inaita. Nilikuwa nimeiweka pale kisha nikarudi mbali zaidi chini ya uvungu, Muarabu akaichukua simu yake pasipokujua kilichotokea.
Tayari Boti ilikuwa imefika Dar es Salaam kwenye bandari Bubu majira ya saa nane Usiku, wakatoka, nami nikatoka pasipo ya wao kuniona, nikajirusha baharini nikaanza kuogelea mpaka ufukweni. Nikayaona magari mawili meusi yakiwa yamepaki kwa mbali karibu na usawa wa ile boti, Dora akapanda gari ya mbele, huku Muarabu akipanda Gari lililokuwa nyuma, Yale magari yakaondoka yakiacha eneo lile likiwa kimya, hapo sikuwa na ujanja zaidi ya kuyasindikiza magari yale kwa macho mpaka yalipopotea katika macho yangu.
***********************************
Nikachukua Laptop yangu kisha moja kwa moja nikaingia upande wa Email, nikakuta ujumbe wa Dr. Miranda akitaka kujua nini kinaendelea na nimefikia hatua ipi katika kazi aliyokuwa amenipa, nikaijibu ile Mail, kisha nikaondoka upande wa mail, na kufungua Programu maalumu ya kudukua mawasiliano ya simu, nilipoiwasha program ile, nikachukua simu yangu ambayo ni simu ya ya kazi, nikakuta missed call moja na ujumbe wenye Imei namba, nikachukua namba ya muarabu na Imei namba yake kisha nikaiingiza kwenye ile programu maalumu ya udukuzi, alafu mfumo ukawa unajiseti, baada ya dakika tatu zilikuja taarifa za ile simu aliyokuwa anaitumia Muarabu, kisha chini yake kulikuwa na taarifa za mawasiliano yote yaliyofanyika kwa siku tisini, Simu alizopiga, simu alizopigiwa, jumbe alizotuma na alizotumiwa. Jambo moja lililonishangaza ni kuiona namba ya Osman Midevu katika mawasiliano ya yule Muarabu. Nikafungua meseji walizokuwa wametumiana. Hapo nikahisi mapigo yangu yamoyo yakiniacha, sikuamini nilichokuwa nakiona. Kwanza nilishangaa kuona kwenye zile meseji jina langu likiwepo, Niliona baadhi ya movements zangu zikiwa zinajulikana na watu hawa wabaya, mbaya zaidi Osman Midevu alikuwa anafahamu mimi ndiye niliyemtorosha Mr. Kibadeni lakini hawakujua wapi nilimpeleka,
“ Jukumu la kumtafuta Peter Mirambo linapaswa kushughulikiwa mapema zaidi kabla hajatuharibia Mipango yetu, Tumejaribu kutafuta Cv yake lakini mpaka sasa hatujaipata, hata hivyo tayari tumemuandaa Mtu maalumu wa kushughulika na Peter Mirambo, atuambie ni nani, Yupo wapi, na wapi alipompeleka Mr. Kibadeni” Ujumbe huo uliokuwa umetumwa na Osman midevu kwenda kwa Ashraf ulitingisha mishipa ya moyo wangu, akili yangu ikapoteza mhimili wake, sasa nikawa nafikiri; “ Watu hawa wanamipango gani ambayo hawataki niivuruge” Nikameza mate, “ Huyo mtu maalumu aliyepewa jukumu la kunishughulikia ni nani” Nikawaza. Jambo moja la kushukuru nimejua mambo haya mapema, “Hii kazi nilijua itakuwa ngumu sana, lakini naona mambo yanajiseti yenyewe bila kutumia nguvu kubwa”
“ Hapa kuna Osman Midevu” Nikasema, huku nikiichapisha picha ya Osman Midevu, picha ikawa inatoka kwenye Printer polepole, ilipomalizika, nikaichukua na kuitazama nikiwa nimeiweka mbele ya uso wangu. Ilikuwa picha inayomuonyesha Osman akiwa na ndevu nyingi nyeusi, kichwani akiwa na upaa, alafu mdomoni akiwa na sigara iliyokuwa inatoa moshi. Nikachukua Gundi alafu nikaigundisha kwenye Ubao uliokuwa mule chumbani kama ubao wa matangazo. Alafu nikaiseti tena Printer, ikawa inanguruma “kraa! Kraa! Kraa!” kisha ikawa inatoa picha nyingine iliyokuwa inamuonyesha Ashraf, ndiye yule muarabu, nikaitoa ile picha kwenye Printer baada ya kuchapishwa, nikaishika mkononi nikiiweka usawa wa uso. “ Kuna huyu Ashraf” Picha ilimuonnyesha Ashraf akiwa na bonge la kitambi akiwa kifuaa wazi, akiwa amevaa miwani, nywele zake zikiwa zimeanguka kwenye mabega, mashavuni akiwa na timberland, akiwa kanyoa ndevu. Alikuwa kashika mkononi Bilauri yenye Pombe. Lakini picha hii ilikuwa na mtu mwingine kwa nyuma, ambaye alikuwa msichana akiwa kavaa nguo za kuogelea akiwa kajilaza kifudifudi kwa mapozi, wote walikuwa juu ya Boti. Nikajikuta natamani kumjua binti huyu lakini ningemjuaje ikiwa ndio mara ya kwanza kumuona tena kwenye picha.
Picha ya Tatu ilikuwa inamuonyesha Dora akiwa kavaa gauni refu jekundu linaloburuzika akiwa kwenye bustani yenye maua yenye kuvutia, alikuwa naye kavaa miwani. Nikazichukua zile picha kisha nikazibandika kwa gundi kwenye ule ubao kwa kufuata picha ile ya kwanza ya Osman Midevu.
Nikatoka katika chumba cha siri ambacho ndicho nilikuwa nahifadhia vifaa na nyaraka zangu za kazi za kijasusi, chumba hiki kipo chini kabisa ya ardhi, hakuna ambaye anajua kilipochumba hiki zaidi yangu. Moja kwa moja nikaenda kuoga ili kuupa mwili nguvu mpya, na kuifanya akili yangu ipate mng’ao. Baada ya kutoka kuoga, niliamua kwenda kumtazama Mr. Kibadeni katika ile nyumba ya chini. Huko nilimkuta Mr. Kibadeni akiwa anasoma kitabu licha ya kuwa ilikuwa ni saa kumi na moja alfajiri.
“ Bwana Mkubwa, hujalala tuu” Nikasema, nikiwa nafungua mlango baada ya kubisha hodi na Mr. Kibadeni kuniruhusu kuingia ndani. Akanitazama, kisha akatoa miwani yake usoni.
“ Sikutegemea ningekukuta upo macho” Nikasema, hapo nikakaa kwenye kiti kilichokuwa mule ndani.
“ Ratiba yangu huanza alfajiri na mapema, ninaanza kwa kusali na kumshukuru Mungu kwa kuniamsha salama, kisha ninakunywa maji, alafu ratiba ya mazoezi ingefuata, lakini kutokana na hali yangu ya ugonjwa nimesitisha ratiba ya mazoezi, nimerukia ratiba ya kusoma kitabu… hii imenisaidia sana..” Mr. Kibadeni ambaye ni Wakili, na aliyewahi kuwa Jaji, lakini pia Jasusi wa kitaifa yaani ndani ya mipaka ya nchi yetu. Sumu aliyokuwa amenyweshwa ilikuwa imemchakaza vibaya mno, nywele na ngozi yake vilionekana kama vya mtu mzee lakini usingeamini kama umri wake ni miaka hamsini,
“ Nimeipenda Ratiba yako” Nikasema, huku nikijaribu kuangalia picha zilizopo katika jalada la kile kitabu.
“ Vipi kazi zinaendaje huko?” Akaniuliza,
“ Bado kugumu, ila tumepiga hatua Fulani, ingawaje ni hatua ndogo ukilinganisha na muda uliobakia” Nikasema, Hapo nikamuona Mr. Kibadeni akiingiwa na fadhaa, taarifa ile haikumfurahisha,
“ Itakuwa mimi ndiye nimekuwa sehemu ya kufeli kwa misheni hii” Akasema kwa masikitiko yaliyonifanya nimuonee huruma.
“ Hapana! Usiseme hivyo. Hatujashindwa bado, iweje useme kuwa wewe ndiye sehemu ya kufeli kwa misheni hii?” Nikazungumza kama mtu niliyekasirishwa na maneno yake.
“ Nisikie Kibadeni, tayari ninamajina mengine mawili yaliyoongezeka katika chain tunayotakiwa kuifuata mpaka kuukuta mzizi wa jambo hili, watu hawa ni muhimu na ninaamini wataifanya kazi yetu iwe rahisi” Nikasema, taarifa hiyo ikamfanya Mr. Kibadeni anitazame, nikaona angalau sura yake imepata faraja. Nikamuona kama kuna kitu anataka kukisema, lakini akasita,
“ Vipi mbona kama unataka kuzungumza jambo Fulani alafu unasita?” Nikasema nikimtazama,
“ Unakumbuka shindano la Tanzania Got Talent?” Akaniuliza, nikamtingishia kichwa kuwa ninakumbuka.
“ Unaweza kuniambia nini kilitokea mpaka Gstar hajashinda katika shindano Lile?” Akasema, nikajikuta namtazama Mr. Kibadeni kwa macho ya kutafakari, kitambo kidogo nikiwa natafakari swali lake nikamuuliza;
“ Unafikiri kuna uhusiano wowote na misheni yetu?”
“ Peter, Kwenye upelelezikitu chochote kinaweza kuhusika, mimi ni Jaji mbali na upelelezi, nimefanya kazi ya ujaji kwa miaka kadhaa, ninajua visa na mikasa mingi kuhusiana na matukio ya uhalifu. Uzoefu wangu katika fani ya Ujaji unanionyesha kuwa matukio mazuri yanayoendelea mchana yameficha ubaya, ukatili, ushenzi na mambo ya kutisha yanayoendelea usiku. Peter Mirambo najua wewe ni Kijana Msomi, tena jasusi wa kimataifa, uliyebobea katika fani ya ukachero. Fuatilia nini kilitokea mpaka Gstar akashindwa katika shindano la Tanzania Got Talent” Mr. Kibadeni akasema, maneno yake yalivuta kumbukumbu ya siku ya fainali ya Tanzania Got Talent ambapo nilimuona Gstar akiwa na mwanamke mmoja chobingo ambaye mwanamke yule nilimtambua kama Dora. Akili yangu ikanipeleka Zanzibar nilipokuwa namfukuzia Dora kule Bweju, kisha akili yangu ikasafiri miaka mingi nyuma nikikumbuka yule mwanamke ndiye Dora akimuambia Baba yangu kuwa aachane kufuatilia jambo Fulani ambalo sikufanikiwa kulijua moja kwa moja. Ni kama Mr. Kibadeni kuna kitu anakisema ambacho akili yangu inataka kukubaliana naye lakini bado sikuwa nauhakika.
“ Peter Mirambo, panga mipango yako vizuri, mchunguze Gstar mpaka ujue nini kilitokea, kwa bahati nzuri Neema Mdogo wako yupo karibu na Gstar. Unaweza anzia hapo, wakati ukiendelea na hao watu wengine waliojitokeza” Mr. Kibadeni Akasema, nikamkubalia kwa kutingisha kichwa. Kisha nikamuaga, ratiba yangu kwa siku hii ilikuwa ni kumfuatilia Dora. Akili yangu ilimuona Dora kuwa sehemu ya wale niliopewa kazi ya kuwafuatilia katika Mpango wa Operation Tonardo, uwepo wa jina la Osman Midevu kwenye simu ya Muarabu Ashraf Amur uliniongezea imani ya kuwa Dora ni miongoni mwa wahusika hatari wanaohitajika kukamatwa na kupewa adhabu kali.
ITAENDELEA
Lipia Tsh 15,000/= kupata kitabu cha Kaburi la mwanamuziki Namba ya muamala 0693322300 Airtelmoney